2
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA NANE
فَكُلُوا مِمَّا ذُكِرَ اسْمُ اللَّـهِ عَلَيْهِ إِن كُنتُم بِآيَاتِهِ مُؤْمِنِينَ ﴿١١٨﴾
118.Basi kuleni katika wale waliosomewa jina la Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi mnaziamini ishara zake.
وَمَا لَكُمْ أَلَّا تَأْكُلُوا مِمَّا ذُكِرَ اسْمُ اللَّـهِ عَلَيْهِ وَقَدْ فَصَّلَ لَكُم مَّا حَرَّمَ عَلَيْكُمْ إِلَّا مَا اضْطُرِرْتُمْ إِلَيْهِ ۗ وَإِنَّ كَثِيرًا لَّيُضِلُّونَ بِأَهْوَائِهِم بِغَيْرِ عِلْمٍ ۗ إِنَّ رَبَّكَ هُوَ أَعْلَمُ بِالْمُعْتَدِينَ ﴿١١٩﴾
119.Mna nini hamli katika wale waliosomewa jina la Mwenyezi Mungu? Na amewafafanulia aliyowaharamishia isipokuwa vile mnavyolazimika, Na hakika wengi wanapoteza kwa matamanio yao bila ya ilimu, Hakika Mola wako anawajua vyema wanaoru- ka mipaka.
وَذَرُوا ظَاهِرَ الْإِثْمِ وَبَاطِنَهُ ۚ إِنَّ الَّذِينَ يَكْسِبُونَ الْإِثْمَ سَيُجْزَوْنَ بِمَا كَانُوا يَقْتَرِفُونَ ﴿١٢٠﴾
120.Na acheni dhambi zilizo dhahiri na zilizofichikana. Hakika wale wanaochuma dhambi watalipwa yale waliyokuwa wakiyachuma.
وَلَا تَأْكُلُوا مِمَّا لَمْ يُذْكَرِ اسْمُ اللَّـهِ عَلَيْهِ وَإِنَّهُ لَفِسْقٌ ۗ وَإِنَّ الشَّيَاطِينَ لَيُوحُونَ إِلَىٰ أَوْلِيَائِهِمْ لِيُجَادِلُوكُمْ ۖ وَإِنْ أَطَعْتُمُوهُمْ إِنَّكُمْ لَمُشْرِكُونَ ﴿١٢١﴾
121.Wala msile wale wasiosomewa jina la Mwenyezi Mungu kwani huko ni ufasiki, Na hakika mashetani wanawafunza marafiki zao kubishana nanyi. Na kama mkiwatii, hakika mtakuwa washirikina.
BISMILLAH KWA KINACHOCHINJWA
Aya 118 – 121
MAANA
Basi kuleni katika wale waliosomewa jina la Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi mnaziamini ishara zake.
Waarabu wakati wa ujahiliya walikuwa wakila mfu, na wakitaja majina ya masanamu wanayoyaabudu wakati wa kuchinja. Mwenyezi Mungu akaharamisha hilo kwa Wailsamu; akahalalishia kula wanaochinjwa kwa sharti ya kutaja jina Lake na sio jina la mwengine.
Unaweza kuuliza
: kuwa kujuzu kula aliyechinjwa, aliyesomewa jina la Mwenyezi Mungu, hakuambatani na kumwamini Mwenyezi Mungu na ishara zake. Ambapo inajuzu kwa kafiri kumla huyo; kama ambavyo kumwamini Mwenyezi Mungu hakuambatani na kula aliyesomewa Jina la Mwenyezi Mungu. Ambapo Mumin anakuwa Mumin hata kama hakumla. Lakini dhahiri ya Aya inafahamisha kuwa kuamini ni sharti la uhalali wa kula chinjo hilo. Kwa sababu maana yake ni, kuleni ikiwa nyinyi ni waumini.
Jibu
: Kauli yake Mwenyezi Mungu, ‘Ikiwa nyinyi mnaziamini ishara zake,’ sio sharti la uhalali wa kula chinjo lililosomewa jina la Mwenyezi Mungu, isipokuwa hii ni kuonyesha kuwa anayemtaja asiyekuwa Mwenyezi Mungu kwa chinjo, basi amemfanyia Mwenyezi Mungu mshirika.
Kwa sababu, ameelekeza tendo lake hili kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, kama walivyokuwa wakifanya washirikina wa Kiarabu; na kwamba mwenye kutaja jina la Mwenyezi Mungu kwa chinjo basi atakuwa amemwamini Mwenyezi Mungu na amemkanushia mshirika, Kwa vile atakuwa amemwelekea yeye tu peke yake.
Mna nini hamli katika wale waliosomewa jina la Mwenyezi Mungu?
Inaonyesha, kutokana na Aya hii, kwamba baadhi ya Waislamu walijizuilia kula chinjo ambalo limesomewa jina la Mwenyezi Mungu kwa kujitatiza; kwamba inakuwaje mtu achinje mnyama kwa mkono wake na ataje jina la Mwenyezi Mungu kisha ale na isijuzu kula mnyama aliyeuliwa na Mwenyezi Mungu ambaye amekufa mwenyewe!
Ndipo Mwenyezi Mungu akalipingia hilo kwa kusema: Mna nini hamli katika wale waliosomewa jina la Mwenyezi Mungu
Na amewafafanulia aliyowaharamishia isipokuwa vile mnavyolazimika.
Kuhusu aliyowafafanulia anakusudia wale aliowaishiria katika Aya 145, katika Sura hii, ambayo itakuja tafsir yake Inshaalah. Pia anaashiria wale waliotajwa katika Juz.2 (2:173).
Tumezungumzia kwa ufafanuzi kuhusu walioharamishwa na hukumu ya aliyelazimika katika Juz.2 (2:173).
Na hakika wengi wanapoteza kwa matamanio yao bila ya ilimu.
Yaani wanahalalisha na kuharamisha kulingana na matamanio yao bila ya dalili. Miongoni mwa hayo ni kuwa washirikina wa Kiarabu walihalalisha kula nyamafu na kuharamisha kula bahira, saiba, wasila na hami. Umetangulia ufafanuzi wa hayo katika Juz.6 (5:3).
Hakika Mola wako anawajua vyema wanaoruka mipaka.
Ambao wanahalalisha na kuharamisha kwa hawaa zao na matamanio yao, Na kwamba atawaadhibu inavyostahiki.
Na acheni dhambi zilizo dhahiri na zilizofichikana.
Makusudio ya dhambi ni kitendo cha haramu kinacholeta dhambi; na dhahiri yake ni kufanya maasi dhahiri; na kufichikana ni kuyafanya kisiri. Mwenyezi Mungu amekataza kufanya maasi yote ya dhahiri na ya batini.
Hakika wale wanaochuma dhambi watalipwa yale waliyokuwa wakiyachuma,
katika kufuata matamanio bila ya elimu; wala hawataachwa bure bure bila ya hisabu na adhabu.
Wala msile wale wasiosemowa jina la Mwenyezi Mungu kwani huko ni ufasiki.
Dhamiri ya huko inarudia kula, Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuhalalishia waliochinjwa kwa jina lake, anaharamisha ambao hawakutajiwa.
Kwa kutegemea hilo, ndipo mafakihi wote, isipokuwa Shafii, wamekonga- mana kuwa mchinjaji akiacha kutaja jina la Mwenyezi Mungu kwa makusudi, basi ni haramu; sawa na nyamafu. Inatosha jina la Mwenyezi Mungu tu, mfano: Allah, Allahu Akbar, Al-Hamdulillah, Bismillah, Lailaha illa Ilah na mfano wake.
Wametofautiana kuacha kusoma jina la Mwenyezi Mungu kwa kusahau. Hanafi, Jaafariya (Shia) na Hanbal wamesema si haramu nyama hiyo. Malik akasema ni haramu na Shafii amesema kuwa akiwacha kusoma jina la Mwenyezi Mungu kwa makusudi pia si haramu, sikwambii tena kusahau.
Na hakika mashetani wanawafunza marafiki zao kubishana nanyi.
Makusudio ya mashetani hapa ni maiblis–watu ambao wanauviringa ukweli na kutunga maneno wanayowahadalia wale wenye akili za juu juu. Kwa mafano, baadhi ya washirikana na maiblis wao walikuwa wakiwaambia wafuasi wao.
Waulizeni Masahaba wa Muhammad, vipi mnakula mnyama mliyemuua nyinyi wenyewe, kumchinja kwa mikono yenu; na wala hamli mnyama aliyeuawa na Mwenyezi Mungu, aliyekufa mwenyewe ambapo aliyeuawa na Mwenyezi Mungu ni bora kuliko mliyemuua nyinyi?
Huo ndio mjadala wao ambao mashetani waliwashauri marafiki zao kwa makusudio ya kuingiza shaka katika nyoyo dhaifu za baadhi ya Waislamu na kuwafitini na dini yao.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) akasema kuwaambia hawa wadhaifu:
Na kama mkiwatii, hakika mtakuwa washirikina.
Yaani mwenye kuwasikiliza washirikina na akahalalisha kula nyamafu, kama walivyohalalisha, basi yeye ni mshirikina kama wao, na hukumu hii haihusiki na kula nyamafu peke yake, bali kila anayepinga hukumu ya sharia akijua kuwa imethibiti, basi huyo ni kafiri.
أَوَمَن كَانَ مَيْتًا فَأَحْيَيْنَاهُ وَجَعَلْنَا لَهُ نُورًا يَمْشِي بِهِ فِي النَّاسِ كَمَن مَّثَلُهُ فِي الظُّلُمَاتِ لَيْسَ بِخَارِجٍ مِّنْهَا ۚ كَذَٰلِكَ زُيِّنَ لِلْكَافِرِينَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٢٢﴾
122.Je, aliyekuwa maiti kisha tukamhuisha na tukamjaalia nuru, hutembea mbele za watu kwayo, mfano wake ni kama yule aliyegizani asiyeweza kutoka humo? Namna hiyo wamepambiwa makafiri waliyokuwa wakiyafanya.
وَكَذَٰلِكَ جَعَلْنَا فِي كُلِّ قَرْيَةٍ أَكَابِرَ مُجْرِمِيهَا لِيَمْكُرُوا فِيهَا ۖ وَمَا يَمْكُرُونَ إِلَّا بِأَنفُسِهِمْ وَمَا يَشْعُرُونَ ﴿١٢٣﴾
123.Na kama hivyo tumejaalia katika kila mji wakubwa wa wakosefu wake ili wafanye vitimbi humo; wala hawafanyii vitimbi isipokuwa wanajifanyia wenyewe, lakini hawatambui.
وَإِذَا جَاءَتْهُمْ آيَةٌ قَالُوا لَن نُّؤْمِنَ حَتَّىٰ نُؤْتَىٰ مِثْلَ مَا أُوتِيَ رُسُلُ اللَّـهِ ۘ اللَّـهُ أَعْلَمُ حَيْثُ يَجْعَلُ رِسَالَتَهُ ۗ سَيُصِيبُ الَّذِينَ أَجْرَمُوا صَغَارٌ عِندَ اللَّـهِ وَعَذَابٌ شَدِيدٌ بِمَا كَانُوا يَمْكُرُونَ ﴿١٢٤﴾
124.Na zinapowafikia ishara husema: Hatutaaamini mpaka tupewe sawa na yale waliyopewa Mitume wa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi wa kujua mahali anapoweka ujumbe wake. Itawafika wale waliokosea dhila inayotoka kwa Mwenyezi Mungu na adhabu kali kwa sababu ya vitimbi walivyokuwa wakivifanya.
KUMHUISHA MAITI
Aya 122 – 124
MAANA
Je, aliyekuwa maiti kisha tukamhuisha na tukamjaalia nuru, hutem- bea mbele za watu kwayo, mfano wake ni kama yule gizani asiyeweza kutoka humo?
Huu ni mfano alioupiga Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kulinganisha baina ya mumin na kafiri. Ufafanuzi wake ni kuwa, kuwalinganisha wawili hao ni sawa na kulinganisha mauti na uhai. Na mwanga na giza. Kafiri ni maiti akiamini hufufuliwa upya na kurudiwa na uhai na imani yake ni nuru anayokwenda nayo katika uhai wake.
Anayebakia kwenye ukafiri na shirki ni kama anajikokota gizani, anakwenda bila ya uongozi na haimfikii kheri yoyote katika maisha yake yote.
MWENYE KUULIZWA NA MUULIZAJI MKUU
Mtu anaweza kusema kuwa
: Aya imefananisha imani na uhai; na ukafiri na mauti; ingawaje makafiri na walahidi, katika zama hizi, wanaishi maisha ya anasa na wenye utajiri zaidi kuliko waumini na wenye kuabudu?
Jibu
: Makusudio ya uhai katika Aya hii sio kuishi mtu katika neema na anasa, akawa anakula vizuri, kuvaa nguo za thamani na kunywa vinywaji vitamu. Hakika anasa hazihusiani na ukafiri wala imani. Kama ni hivyo waumini wa Mashariki na Magharibi wangelikuwa sawa katika maendeleo na uchumi mzuri, vilevile walahidi na makafiri.
Hali nzuri ya maisha ina sababu na mambo yanayoambatana nayo ambayo hayafungamani na chochote katika imani au ukafiri. Isipokuwa makusudio ya uhai, katika Aya hii, ni imani na hisia za kidini zinazompa mtu msukumo wa kutekeleza wajibu, akiwa ni mtu atakayeulizwa kuhusu mwenendo wake, atahisabiwa na kulipwa thawabu kwa wema wake, na adhabu kwa uovu wake.
Lau mtu angelikuwa si mwenye kuulizwa chochote, ingelikuwa sharia na kanuni ni maneno tu, yasiyokuwa na maana yoyote. Na tukipitisha kuwa mtu ataulizwa wala hataachwa bure bure, basi itatulazimu tupitishe kwam- ba yeye ataulizwa mbele ya yule ambaye
﴿ لَا يُسْأَلُ عَمَّا يَفْعَلُ وَهُمْ يُسْأَلُونَ﴾
“Haulizwi anayoyafanya, na wao ndio wanaoulizwa”
(21:23)
Lau muulizaji huyu anaulizwa, basi ingelipaswa kupatikana atakayemuuliza, na kuendelea hivyo hivyo bila mwisho.
Mwenye kukanusha kuweko muulizaji mkuu kabisa ambaye huuliza na haulizwi, basi atakuwa amekanusha maulizo; Kwa sababu hakuna maulizo bila ya muulizaji, Na mwenye kukanusha maulizo amekanusha maisha ya kijamii.
Unaweza kusema
: Ndio mtu ataulizwa, lakini si lazima muulizaji awe Mwenyezi Mungu; watu wanaweza kuchagua kundi (kamati) ambalo litauliza watu.
Nasi tutauliza je kundi hilo likikosea, liulizwe na lihukumiwe na nani? Ikijibwa ni dhamir.
Tutasema
:Kwanza
, dhamir ni jambo la kimaana si la kidhati.
Pili
, dhamiri anayo kila mtu, kwanini huyu aache dhamiri yake afuate ya mwingine?
Kwa hiyo, basi hakuna muulizaji asiyeulizwa ila Mwenyezi Mungu peke yake. Mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu akailazimisha nafsi yake kufuata sharia za Mwenyezi Mungu na hukumu zake, basi atakuwa na busara ya mambo yake, itikadi yake na tabia zake. Vinginevyo atakuwa kama aliye gizani asiyeweza kutoka.
Namna hiyo wamepambiwa makafiri waliyokuwa wakiyafanya.
Yaani kama waliyvopambiwa waumini amali zao, vilevile washirikina wamepambiwa amali zao. Tofauti ni kuwa wao wamepambiwa kinyume na hali halisi, wamepambiwa, kimawazo na kinjozi tu.
Na kama hivyo tumeajaalia katika kila mji wakubwa wa wakosefu wake.
Makusudio ya mji ni kila jamii (mkusanyiko) wa watu, wachache au wengi. Maana ni kuwa: Ewe Muhammad kama ambavyo wanapatikana katika jamii yako viongozi wa waovu wanaofanya vitimbi na kuifanyia uadui dini ya Mwenyezi Mungu, vilevile katika jamii zilizotangulia walikuwapo; na hivi sasa pia wako viongozi wanaowafanyia vitimbi watu wao na kuwa katika msimamo wa kuifanyia uadui haki na wenye haki.
Unaweza kuuliza
: Dhahiri ya Aya hii inafahamisha kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye aliyewafanya wakubwa kuwa waovu kwa watu wa haki, na tunajua kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu hukataza vitimbi na uovu; je, kuna taawili gani hapa?
Jibu
: Makusudio ya kunasibishwa kwake huku Mwenyezi Mungu Mtukufu, ni kuashiria kwamba matakwa ya Mwenyezi Mungu yamepitisha kuwa desturi ya jamii iwe kwenye misingi ya kupingana baina ya wenye haki na wenye batili, baina ya viongozi wenye kufanya uadui na wenye kufanyiwa uadui.
Hakuna kimbilio la kuepuka mgongano huu ila kumalizwa waovu; na hapana budi kutimia hilo na kutukuka neno la haki mikononi mwa wanaolingania uadilifu na utengenevu; hata kama batili itakuwa kubwa kiasi gani. Hilo amelisajili Mwenyezi Mungu (s.w.t) katika Kitabu chake, aliposema:
﴿اسْتِكْبَارًا فِي الْأَرْضِ وَمَكْرَ السَّيِّئِ وَلَا يَحِيقُ الْمَكْرُ السَّيِّئُ إِلَّا بِأَهْلِهِ فَهَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا سُنَّتَ الْأَوَّلِينَ فَلَن تَجِدَ لِسُنَّتِ اللَّـهِ تَبْدِيلًا وَلَن تَجِدَ لِسُنَّتِ اللَّـهِ تَحْوِيلًا﴾
“Na vitimbi vibaya havimpati ila yule aliyevifanya, Basi hawangoji ila desturi iliyokuwa kwa watu wa zamani, wala hutakuta mabadiiko katika desturi ya Mwenyezi Mungu, wala hutakuta mageuko katika desturi ya Mwenyezi Mungu.”
(35:43)
Kukaririka huku ni kutilia mkazo kwamba mwisho ni wa wanaomcha Mwenyezi Mungu; kadiri zitakavyorefuka zama. Hivi ndivyo tunapata tafsir ya kauli yake Mwenyezi Mungu:
Ili wafanye vitimbi humo; wala hawafanyii vitimbi isipokuwa wanajifanyia wenyewe, lakini hawatambui.
Na zinapowafikia ishara husema: Hatutaaamini mpaka tupewe sawa na yale waliyopewa Mitume wa Mwenyezi Mungu.
Wametofautiana wafasiri katika maana ya Aya hii kwa kauli mbili: Kwanza, kwamba wakubwa waovu katika Waarabu walimtaka Muhammad(s.a.w.w)
awaletee muujiza kama aliopewa Musa, wa kupasua bahari; na wa Isa, wa kufufua wafu.
Kauli ya pili, ni kuwa wao walimwambia hatutakuamini mpaka utushushie wahyi kama ulivyowashukia Mitume. Razi akasema: “Hii ndio kauli mashuhuri baina ya wafasiri.”
Nasi tunaipa uzito kuliko ya kwanza; Kwa sababu mfumo wa Aya unafahamisha hivyo, ambapo Mwenyezi Mungu anawajibu wakubwa waovu kwa kauli yake:
Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi wa kujua mahali anapoweka ujumbe wake.
Kuongezea kuwa kutaka kwao Mwenyezi Mungu awateremshie Wahyi kunaafikiana na hasadi yao kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu amesema:
﴿ أَمْ يَحْسُدُونَ النَّاسَ عَلَىٰ مَا آتَاهُمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ﴾
“Au wanawahusudu watu kwa alichowapa Mwenyezi Mungu katika fadhila yake?.”
Juz.5 (4:54)
Katika Majmaul-bayan na kwengine, imeelezwa kuwa Walid bin Mughira alimwambia Mtume(s.a.w.w)
:“Lau Utume ungelikuwa ni kweli mimi ningelistahiki zaidi kuliko wewe, kwa sababu mimi ni mkubwa kuliko wewe, na nina mali nyingi kushinda wewe.”
Maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi wa kujua mahali anapoweka ujumbe wake’, ni kuwa yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu anauchagulia ujumbe wake mtu atakayefaa katika viumbe vyake, na Muhammad ni Mtukufu zaidi wa viumbe vya Mwenyezi Mungu na aheshimiwaye zaidi kwao.
Itawafika wale waliokosea dhila inayotoka kwa Mwenyezi Mungu.
Kwa sababu walijifanya wakubwa wakajiadhimisha, Ndipo wakastahiki malipo ya udhalilifu na fedheha. Kuna Hadith isemayo kuwa wenye kutakabari watafufuliwa katika Sura ya chembe (kama sisimizi) watakanyagwa na watu kwa nyayo zao, ikiwa ni malipo ya kujifanya kwao wakubwa katika dunia.
Na adhabu kali kwa sababu ya vitimbi walivyokuwa wakivifanya.
Udhalili ni malipo ya kiburi, na adhabu ni malipo ya vitimbi na hadaa. Kwa maneno mengine ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawafanyia wale wenye nia mbaya na malengo ya ufisadi kinyume cha wanavyokusudia na wanavyolenga.