4
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA NANE
وَرَبُّكَ الْغَنِيُّ ذُو الرَّحْمَةِ ۚ إِن يَشَأْ يُذْهِبْكُمْ وَيَسْتَخْلِفْ مِن بَعْدِكُم مَّا يَشَاءُ كَمَا أَنشَأَكُم مِّن ذُرِّيَّةِ قَوْمٍ آخَرِينَ ﴿١٣٣﴾
133.Na Mola wako ndiye Mkwasi, mwenye rehema, Akipenda atawaaondoa, na kuweka wengine awapendao baada yenu. Kama alivyowaanzisha kutokana na uzao wa watu wengine.
إِنَّ مَا تُوعَدُونَ لَآتٍ ۖ وَمَا أَنتُم بِمُعْجِزِينَ ﴿١٣٤﴾
134.Hakika mnayoahidiwa yatafika tu. Wala hamtaweza (kuepuka)
قُلْ يَا قَوْمِ اعْمَلُوا عَلَىٰ مَكَانَتِكُمْ إِنِّي عَامِلٌ ۖ فَسَوْفَ تَعْلَمُونَ مَن تَكُونُ لَهُ عَاقِبَةُ الدَّارِ ۗ إِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الظَّالِمُونَ ﴿١٣٥﴾
135.Sema: Enyi watu wangu! Fanyeni vile muwezavyo; na mimi nafanya. Mtakujajua ni nani atakuwa na makazi mema mwishoni, Hakika madhalimu hawafaulu.
NA MOLA WAKO NDIYE MKWASI
Aya 133 – 135
MAANA
Na Mola wako ndiye mkwasi, mwenye rehema.
Baada ya Mwenyezi Mungu kutaja kwamba atawahisabu watu kulingana na matendo yao. Ameashiria kuwa yeye ni mkwasi (mwenye kujitosheleza), hawahitajii viumbe.
Haimnufaishi twaa ya mwenye kumtii, wala hayamdhuru maasi ya mwenye kuasi; na kwamba ulimwengu wote una haja ya rehema yake; Kwa sababu, yeye ndiye sababu ya kwanza ya kupatikana huo ulimwengu.
Akipenda atawaaondoa
kwa sababu ni Mkwasi, hawahitajii,na kuweka wengine awapendao baada yenu
awabadili wengine wawe watiifu zaidi kuliko nyinyi. Lakini amewaacha na kuwapa muda kutokana na fadhila na ukarimu kutoka kwake.
Kama alivyowaanzisha kutokana na uzao wa watu wengine.
Yaani kama ambavyo imekuwa wepesi kwake kuwaleta nyinyi kutokana na kizazi kilichopita, vilevile ni wepesi kwake kuleta kizazi kipya kutokana na nyinyi na wengineo.
Makusudio ya Aya hii ni kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu anawaonya makafiri, wenye inadi, na maangamivu, kama ilivyokuwa kwa kaumu ya Nuh
, A’d na Thamud.
Hakika mnayoahidiwa yatafika tu.
Baada ya Mwenyezi Mungu kuwahofisha na adhabu ya dunia, sasa anawahofisha na Kiyama na adhabu yake; kwamba Kiyama kitakuja bila ya shaka yoyote, wala hapana pa kukikimbia ila kwake yeye tu, peke yake.
Sema: Enyi watu wangu! Fanyeni vile muwezavyo; na mimi nafanya. Mtakujajua ni nani atakuwa na makazi mema mwishoni.
Baada ya Mtume(s.a.w.w)
kuwalingania kwenye Uislamu waarabu wa ujahiliya na wakaitikia mwito wake walioitikia na kupinga waliopinga, Mwenyezi Mungu Mtukufu alimwamrisha kuwaambia wenye inadi: Kuweni kama mlivyo na mimi ninafanya kulingana na uongozi wa Mola wangu.
Baada ya muda mtajua mwisho mwema utakuwa wa nani; sawa na kumwambia yule anayepinga nasaha zako: Haya endelea tu utaona!
Hakika madhalimu hawafaulu.
Wale wanaojidhulumu wenyewe au wengineo kwa uadui. Lau angefaulu dhalimu, basi mwadilifu angelikuwa na hali mbaya kuliko dhalimu. Na maneno ya msimamo wa usawa yangelikuwa ni misamiati ya unafiki na ria.
وَجَعَلُوا لِلَّـهِ مِمَّا ذَرَأَ مِنَ الْحَرْثِ وَالْأَنْعَامِ نَصِيبًا فَقَالُوا هَـٰذَا لِلَّـهِ بِزَعْمِهِمْ وَهَـٰذَا لِشُرَكَائِنَا ۖ فَمَا كَانَ لِشُرَكَائِهِمْ فَلَا يَصِلُ إِلَى اللَّـهِ ۖ وَمَا كَانَ لِلَّـهِ فَهُوَ يَصِلُ إِلَىٰ شُرَكَائِهِمْ ۗ سَاءَ مَا يَحْكُمُونَ ﴿١٣٦﴾
136.Na wamemfanyia sehemu Mwenyezi Mungu katika mimea aliyoiumba na katika wanyama na kusema: hii ni ya Mwenyezi Mungu, kwa madai yao, na hii ni ya wale tunaowashirikisha. Basi vile walivyokusudia wale wanaowashirikisha, havifiki kwa Mwenyezi Mungu, na vilivyokuwa vya Mwenyezi Mungu huwafikia wanaowashirikisha, Ni mabaya kabisa wanayoyahukumu.
وَكَذَٰلِكَ زَيَّنَ لِكَثِيرٍ مِّنَ الْمُشْرِكِينَ قَتْلَ أَوْلَادِهِمْ شُرَكَاؤُهُمْ لِيُرْدُوهُمْ وَلِيَلْبِسُوا عَلَيْهِمْ دِينَهُمْ ۖ وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا فَعَلُوهُ ۖ فَذَرْهُمْ وَمَا يَفْتَرُونَ ﴿١٣٧﴾
137.Namna hivi wanaowashrik- isha wamewapambia wengi katika makafiri kuwaua watoto wao. Ili kuwaangamiza na kuwavu- rugia dini yao. Na kama Mwenyezi Mungu angependa wasingalifanya hayo. Basi waache na haya wanayoyazua.
وَقَالُوا هَـٰذِهِ أَنْعَامٌ وَحَرْثٌ حِجْرٌ لَّا يَطْعَمُهَا إِلَّا مَن نَّشَاءُ بِزَعْمِهِمْ وَأَنْعَامٌ حُرِّمَتْ ظُهُورُهَا وَأَنْعَامٌ لَّا يَذْكُرُونَ اسْمَ اللَّـهِ عَلَيْهَا افْتِرَاءً عَلَيْهِ ۚ سَيَجْزِيهِم بِمَا كَانُوا يَفْتَرُونَ ﴿١٣٨﴾
138.Na husema: Wanyama hawa na mimea hii ni mwiko, hawatokula ila wale tuwapendao - kwa madai yao (tu). Na wanyama wengine imeharamishwa migongo yao, Na wanyama wengine hawalitaji jina la Mwenyezi Mungu juu yao. Wanamzulia tu. Atawapa kwa hayo wanayomzulia.
وَقَالُوا مَا فِي بُطُونِ هَـٰذِهِ الْأَنْعَامِ خَالِصَةٌ لِّذُكُورِنَا وَمُحَرَّمٌ عَلَىٰ أَزْوَاجِنَا ۖ وَإِن يَكُن مَّيْتَةً فَهُمْ فِيهِ شُرَكَاءُ ۚ سَيَجْزِيهِمْ وَصْفَهُمْ ۚ إِنَّهُ حَكِيمٌ عَلِيمٌ ﴿١٣٩﴾
139.Na husema: waliomo matumboni mwa wanyama hawa ni kwa ajili ya wanaume wetu tu, na wameharamishwa kwa wake zetu. Lakini ikiwa ni nyamafu hushirikiana. Atawalipa kwa maelezo yao. Hakika Yeye ni mwenye hekima, Mjuzi
قَدْ خَسِرَ الَّذِينَ قَتَلُوا أَوْلَادَهُمْ سَفَهًا بِغَيْرِ عِلْمٍ وَحَرَّمُوا مَا رَزَقَهُمُ اللَّـهُ افْتِرَاءً عَلَى اللَّـهِ ۚ قَدْ ضَلُّوا وَمَا كَانُوا مُهْتَدِينَ ﴿١٤٠﴾
140.Hakika wamehasirika wale waliowaua watoto wao kwa upumbavu bila ya elimu, Na wakaharamisha alivyowaruzuku Mwenyezi Mungu Kwa kumzulia Mwenyezi Mungu, Hakika wamepotea wala hawakuwa wenye kuongoka.
HUSEMA: HII NI SEHEMU YA MWENYEZI MUNGU
Aya 136 – 140
MAANA
Na wamemfanyia sehemu Mwenyezi Mungu katika mimea aliyoiumba na katika wanyama na kusema: hii ni ya Mwenyezi Mungu, kwa madai yao, na hii ni ya wale tunaowashirikisha. Basi vile walivyokusudia wale wanaowashirikisha, havifiki kwa Mwenyezi Mungu, na vilivyokuwa vya Mwenyezi Mungu huwafikia wanaowashirikisha, Ni mabaya kabisa wanayoyahukumu.
Dhamiri katika ‘wamemfanyia’ inawarudia washirikina wa kiarabu.
Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) baada ya kubatilisha itikadi ya washirikina, katika Aya zilizotangulia, kwa mantiki ya kiakili na kimaumbile, katika Aya hizi anaonyesha baadhi ya vile ambavyo washirikina walikuwa wakivitenga katika mali zao na watoto wao.
Aya hii tuliyonayo inaonyesha hali zao katika utajiri wao wa mali ambao ni kilimo na mifugo. Walikuwa, kama inavyoelezwa katika vitabu vya tafsiri, wakitenga sehemu katika mimea yao na mifugo kwa ajili ya Mungu na kuitoa kwa watoto na maskini. Na hutenga sehemu kwa ajili ya masana- mu yao, na kuitoa kwa watunzaji na walinzi wa masanamu.
Walikuwa wakijitahidi kuzidisha fungu la masanamu, kuliko la Mwenyezi Mungu, ili litosheleze. Kwa sababu Mwenyezi Mungu ni tajiri na masanamu ni mafakiri. Ikiwa kitu walichokifanya ni cha Mwenyezi Mungu kinachanganyika na kile walichokifanya cha masanamu, basi hukiachia masanamu. Na ikiwa kile walichokifanya ni cha masanamu kinachanganyika na kile walichokifanya ni cha Mwenyezi Mungu, hukirudisha kwa masanamu. Vilevile wakikumbwa na ukame walikuwa wakila fungu la Mwenyezi Mungu na kuacha fungu la masanamu.
Huu ni ufafanuzi wazi wa“Ni mabaya kabisa wanayoyahukumu”
katika kuyatanguliza masanamu yao kuliko Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Namna hivi wanaowashirikisha wamewapambia wengi katika makafiri kuwaua watoto wao.
Yametangulia maelezo kuwa maana ya wanaowashirikisha katika Aya iliyopita kuwa ni masanamu. Ama katika Aya hii inakusudia makuhani na walinzi wa masanamu kulingana na hali ilivyo. Kwa sababu masanamu hayatambui wala hayasemi, basi yatawezeje kuwapambia na kuwahadaa. Maana ni kuwa washirikina kama waliyopiga mafungu mali zao kwa Mwenyezi Mungu na masanamu, vilevile makuhani na watunzaji wamewapambia kuwaua watoto wao.
Unaweza kuuliza
: Matumizi ya washirikina katika mali zao na watoto wao, kwa namna iliyotangulia, yalikuwa ni kwa kutokana na desturi ya wakati wa ujahiliya. Inajulikana kuwa desturi huwekwa na watu. Mmoja wao alikuwa anaweza kuua mwanawe kwa kuogopa ufukara, au akimzika binti yake kwa kuogopa aibu; kama ilivyonasibishwa kwa Qais bin Asim aliyeigwa kwa ujinga. Sasa kuna wajihi gani katika kulinasibisha hilo kwa masanamu au wanaosimamia masanamu?
Jibu
: Ni kweli kuwa matumizi ya washirikina yalitokana na desturi, lakini Makuhani na viongozi wao walipendekeza na kuipamba desturi hii, nao ndio wasemaji rasmi wa masanamu, kwa hiyo ikafaa kunasibishwa kwenye masanamu.
Ili kuwaangamiza na kuwavurugia dini yao.
Yaani Makuhani waliwapambia washirikina amali zao, ikawa natija ya kupambia huku ni kuangamia washirikina na kupotea kwao na haki na dini iliyonyooka.
Na kama Mwenyezi Mungu angependa wasingalifanya hayo.
Yaani kama Mwenyezi Mungu angelitaka kuwazuia hilo kwa nguvu wasingelifanya ubaya huo kwa mali zao na watoto wao, lakini amewaacha kama walivoyo baada ya kuwabainishia njia ya kheri na shari.
Basi waache na haya wanayoyazua
ya kutegemeza kwa Mwenyezi Mungu yale wanayoyahalalisha na kuyaharamisha.
Amri ya kuwaacha na uzushi wao, imekuja kwa kuwakemea na kuwapa kiaga washirikina na sio kwa njia yake na uhakika wake; kama vile ilivyo amri katika kauli yake Mwenyezi Mungu:
﴿ اعْمَلُوا مَا شِئْتُمْ إِنَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ﴾
“Fanyeni mpendavyo, hakika yeye anayaona myafanyayo.”
(41:40)
Baada ya hapo Mwenyezi Mungu anataja katika Aya inayofuatia kwamba washirikina waligawanya mavuno yao na mifugo yao mafungu matatu:
1. Fungu la kwanza:Na husema: Wanyama hawa na mimea hii ni mwiko, hawatokula ila wale tuwapendao - kwa madai yao (tu)
. Yaani washirikina walikuwa wakigawa sehemu ya mazao na mifugo na kukataza kutumiwa ila kwa wanaowachagua. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakubainisha hao waliochaguliwa na washirikina. Lakini baadhi ya wafasiri wamesema, ni makuhani na watumishi wa masanamu. Wengine wakasema ni wanaume tu, sio wanawake.
2. Fungu la pili:Na wanyama wengine imeharamishwa migongo yao,
hawapandwi wala kubebeshwa mizigo. Rejea maelezo katika Juz.7 (5:103).
3. Fungu la tatu:Na wanyama wengine hawalitaji jina la Mwenyezi Mungu juu yao
wakati wa kuchinja, bali wanataja majina ya waungu wao.
Umetangulia ufafanuzi katika kusafiri Sura hii, Aya ya 121, kuwa wao wamemnasibishia Mwenyezi Mungu kugawanya huku kwa uwongo na uzushi na Mwenyezi Mungu atawaadhibu.
Na husema: waliomo matumboni mwa wanyama hawa ni kwa ajili ya wanaume wetu tu, na wameharamishwa kwa wake zetu. Lakini ikiwa ni nyamafu hushirikiana. Atawalipa kwa maelezo yao. Hakika yeye ni mwenye hekima, Mjuzi.
Razi amesema: “Hii ni aina ya nne katika mambo yao maovu. Walikuwa wakisema katika mimba za Bahira na Saiba: “atakayezaliwa hai basi atahusu wanaume tu, hawali wanawake, na atakayezaliwa maiti basi watashirkiana kumla wanaume na wanawake.”Watalipwa maelezo yao.
Na makusudio ya kiaga cha kuwa.Hakika yeye ni mwenye hekima, Mjuzi,
ni makemeo yawe kwenye hekima na kwa mujibu wa inavyostahiki.”
Hakika wamehasirika wale waliowaua watoto wao kwa upumbavu bila ya elimu.
Kuna upumbavu gani zaidi ya mzazi kumchinja mwanawe kwa mkono wake au kumzika mzima. Kauli yake Mwenyezi Mungu bila ya elimu ni kusisitiza upumbavu wao. Ama hasara yao katika dunia ni kule kuua watoto wao na ufisadi wa maisha yao ya kijamii. Na hasara yao katika akhera ndiyo nzito na chungu.
Na wakaharamisha alivyowaruzuku Mwenyezi Mungu
katika wanyama na mazao ambayo wamedai kuwa ni mwiko.
Kwa kumzulia Mwenyezi Mungu
.
Kwa sababu kuharamisha kunatokana na wao na wala sio kutoka kwake Mwenyezi Mungu.
Hakika wamepotea wala hawakuwa wenye kuongoka
kwenye kheri yoyote na uwongofu.
Razi anasema: “Mwenyezi Mungu ametaja mambo saba na kila moja kati hayo ni sababu tosha ya kupatikana shutuma. Nayo ni: Kupata hasara, upumbavu, ujinga, kuharamisha aliyoyahalalisha Mwenyezi Mungu, kumzulia Mungu, upotevu na kuacha kuongoka.”
Kisha akaendelea kusema Razi: “Imethibiti kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu amewashutumu wanaowaua watoto na kuharamisha aliyohalalisha Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa sifa hizi saba zenye kuwajibisha aina kubwa na ya mwisho ya shutuma, na huo ni ufasaha wa hali ya juu.”
Nasi tunamwambia Razi: Ikiwa Mwenyezi Mungu amewashutumu kwa upotevu kuwa ndiyo aina kubwa na ya mwisho ya shutuma, sasa vipi wewe unadai kuwa Mwenyezi Mungu ndiye aliyewapoteza? Ni mantiki gani yanayosema kuwa inafaa asiye na hatia kuadhibiwa na kushutumiwa kwa kitendo ambacho amekifanya yule anayeshutumu na kuadhibu?
Hayo Razi ameyasema mara kadhaa katika tafsir yake Al-Kabir, miongoni mwayo ni yale aliyoyasema karibuni katika kufasiri Aya 125 ya Sura hii.
وَهُوَ الَّذِي أَنشَأَ جَنَّاتٍ مَّعْرُوشَاتٍ وَغَيْرَ مَعْرُوشَاتٍ وَالنَّخْلَ وَالزَّرْعَ مُخْتَلِفًا أُكُلُهُ وَالزَّيْتُونَ وَالرُّمَّانَ مُتَشَابِهًا وَغَيْرَ مُتَشَابِهٍ ۚ كُلُوا مِن ثَمَرِهِ إِذَا أَثْمَرَ وَآتُوا حَقَّهُ يَوْمَ حَصَادِهِ ۖ وَلَا تُسْرِفُوا ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُسْرِفِينَ ﴿١٤١﴾
141.Naye ndiye aliyeumba bustani zenye kutambaa na zisizotambaa na mitende na mimea yenye kutofautiana uliwaji wake. Na mizaituni na mikomamanga. Inayofanana na isiyofanana, Kuleni matunda yake inapozaa, Na toeni haki yake siku ya kuvunwa kwake, Wala msifanye ufujaji, hakika Yeye hawapendi wafujaji.
وَمِنَ الْأَنْعَامِ حَمُولَةً وَفَرْشًا ۚ كُلُوا مِمَّا رَزَقَكُمُ اللَّـهُ وَلَا تَتَّبِعُوا خُطُوَاتِ الشَّيْطَانِ ۚ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُّبِينٌ ﴿١٤٢﴾
142.Na katika wanyama wale wabebao na wa kutoa matandiko. Kuleni katika alivyowaruzuku Mwenyezi Mungu, wala msifuate nyayo za Shetani; hakika yeye ni adui yenu dhahiri.
ثَمَانِيَةَ أَزْوَاجٍ ۖ مِّنَ الضَّأْنِ اثْنَيْنِ وَمِنَ الْمَعْزِ اثْنَيْنِ ۗ قُلْ آلذَّكَرَيْنِ حَرَّمَ أَمِ الْأُنثَيَيْنِ أَمَّا اشْتَمَلَتْ عَلَيْهِ أَرْحَامُ الْأُنثَيَيْنِ ۖ نَبِّئُونِي بِعِلْمٍ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿١٤٣﴾
143.Namna nane za madume na majike: wawili katika kondoo dume na jike na wawili katika mbuzi dume na jike. Sema je, ameharamisha madume mawili au majike mawili, au waliomo matumboni mwa majike mawili, niambieni kwa ilimu ikiwa nyinyi mnasema kweli.
وَمِنَ الْإِبِلِ اثْنَيْنِ وَمِنَ الْبَقَرِ اثْنَيْنِ ۗ قُلْ آلذَّكَرَيْنِ حَرَّمَ أَمِ الْأُنثَيَيْنِ أَمَّا اشْتَمَلَتْ عَلَيْهِ أَرْحَامُ الْأُنثَيَيْنِ ۖ أَمْ كُنتُمْ شُهَدَاءَ إِذْ وَصَّاكُمُ اللَّـهُ بِهَـٰذَا ۚ فَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا لِّيُضِلَّ النَّاسَ بِغَيْرِ عِلْمٍ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ ﴿١٤٤﴾
144.Na wawili katika ngamia na wawili katika ng’ombe, Sema je, ameharamisha madume mawili au majike mawili, au waliomo matumboni mwa majike mawili? Au nyinyi mlikuweko Mwenyezi Mungu alipowausieni haya? Basi ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule anayemzulia Mwenyezi Mungu uwongo ili kuwapoteza watu bila ya ilimu? Hakika Mwenyezi Mungu hawaongozi watu madhalimu.
KULENI MATUNDA YAKE
Aya 141 – 144
MAANA
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kubainisha katika Aya zilizotangulia, waliyoharamisha katika kilimo na mifugo kwa uzushi, amebainisha katika Aya hizi kwamba yeye ameumba mimea na wanyama binadmau anufaike nayo.
Anasema Mtukufu wa Wasemaji:
Naye ndiye aliyeumba bustani zenye kutambaa
inayowekwa matawi yake katika chanjana zisizotambaa na mitende na mimea
inaungana na Bustani katika upande wa kuunganisha mahsus kutoka ujumla.
Yenye kutofautiana uliwaji wake.
Nafaka ziko aina nyingi na kila moja ina aina yake, na kila aina ina ladha yake. Matunda nayo yako aina kwa aina; yenye rangi tofauti, ladha na hata harufu, vilevile mboga.
Na mizaituni na mikomamanga.
Hiyo pia inaungana na bustani.
Inayofanana na isiyofanana.
Matunda ya mikomamanga yanafanana, lakini kuna yaliyo tamu na yaliyo ugwadu. Vilevile matunda ya jamii ya malimau na mizaituni; kuna mazuri na mabaya.
Kuleni matunda yake inapozaa.
Kwa sababu imeumbwa kwa ajili yenu.
Na toeni haki yake siku ya kuvunwa kwake.
Imesemekana kuwa makusudio ya haki yake ni Zaka. Wengine wakasema kuwa ni sadaka ya Sunna. Lakini, kauli zote mbili ni kinyume na dhahiri.
Linalokuja haraka kwenye akili ni kukusanywa na wala yasiachwe yakaharibika na kupotea.
Wala msifanye ufujaji, hakika Yeye hawapendi wafujaji.
Ufujaji (Israf) ni kupetuka kiwango, na Mwenyezi Mungu amelikataza hilo: ni sawa iwe ni kutumia mtu mwenyewe, au kumpa mwingine.
Na katika wanyama wale wabebao na wa kutoa matandiko.
Yaani ameumba katika wanyama wanaowabeba nyinyi na kubeba mizigo yenu; kama vile ngamia. Na wale mnaowachinja na kunufaika kwa nyama yake manyoya na sufi zake.
Kuleni katika alivyowaruzuku Mwenyezi Mungu,
kama vile wanyama hawa na wengineo na mshukuru neema zake.
Wala msifuate nyayo za Shetani
, kwa kuhalalisha aliyoyaharamisha Mwenyezi Mungu, na kuharamisha aliyoyahalalisha, na pia kufanya ubadhirifu.
Hakika yeye ni adui yenu dhahiri
.
Anawaamrisha uovu na kusema kwa Mwenyezi Mungu msiyoyajua.
Namna nane za madume na majike: wawili katika kondoo dume na jike na wawili katika mbuzi dume na jike. Sema je, ameharamisha madume mawili
ya kondoo na mbuziau majike mawili
, ya kondoo na mbuzi?Au waliomo matumboni mwa majike mawili
ya kondoo na mbuzi?
Niambieni kwa ilimu ikiwa nyinyi mnasema kweli
sio kwa hawa za nafsi na kufuata mnavyoambiwa tu, kwa sababu kuharamisha kunahitajia dalili mkato; sasa je, iko wapi?
Na wawili katika ngamia na wawili katika ng’ombe, Sema je, ameharamisha madume mawili au majike mawili, au waliomo matumboni mwa majike mawili? Au nyinyi mlikuweko Mwenyezi Mungu alipowausieni haya?
Walidai kwamba Mwenyezi Mungu ndiye aliyewaharamishia waliowa- haramisha katika wanyama na mimea. Ndipo akawaambia kuwa jambo halithibitiki ila kwa mojawapo ya hali mbili. Ama kwa kuona au kwa kushuhudia shahidi mkweli. Na nyinyi hamkupata hukumu ya uharamu kutoka kwa Mwenyezi Mungu moja kwa moja au kupitia kwa Mtume wake; basi mmezitoa wapi hukumu hizi?
Basi ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule anayemzulia Mwenyezi Mungu uwongo?
Ikiwa hamkuona, wala hakuna ushahidi wowote, basi nyinyi mtakuwa wazushi. Na mzushi ni dhalimu mwenye dhambi. Bali nyinyi ni madhalimu kuliko dhalimu yeyote, kwa sababu mnamzulia Mwenyezi Mungu uwongo.
Ili kuwapoteza watu bila ya ilimu.
Akiwazuia kufuata njia ya Mwenyezi Mungu na wakati huo huo anadai kuwa yeye ni kiongozi wa dini ya Mwenyezi Mungu; kama walivyo masheikh wengi siku hizi.
Hakika Mwenyezi Mungu hawaongozi watu madhalimu.
Kwa sababu wao wamekata uhusiano na Mwenyezi Mungu. Isitoshe wameharamisha aliyoyahalalisha na kuhalalisha aliyoyaharamisha.