6
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA NANE
قُلْ تَعَالَوْا أَتْلُ مَا حَرَّمَ رَبُّكُمْ عَلَيْكُمْ ۖ أَلَّا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا ۖ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا ۖ وَلَا تَقْتُلُوا أَوْلَادَكُم مِّنْ إِمْلَاقٍ ۖ نَّحْنُ نَرْزُقُكُمْ وَإِيَّاهُمْ ۖ وَلَا تَقْرَبُوا الْفَوَاحِشَ مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَمَا بَطَنَ ۖ وَلَا تَقْتُلُوا النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّـهُ إِلَّا بِالْحَقِّ ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ ﴿١٥١﴾
151.Sema: Njooni niwasomee aliyowaharamishia Mola wenu: Kwamba msimshirikishe na chohote, Na kuwafanyia wema wazazi wawili. Wala msiwaue watoto wenu kwa kuogopa kuishiwa sisi tutawaruzuku nyinyi na wao. Wala msikurubie mambo machafu, yaliyodhihirika na yaliyofichika; wala msiiue nafsi ambayo Mwenyezi Mungu ameharamisha (kuiua), ila kwa haki. Hayo amewausia Mwenyezi Mungu ili mpate kutia akili.
وَلَا تَقْرَبُوا مَالَ الْيَتِيمِ إِلَّا بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ حَتَّىٰ يَبْلُغَ أَشُدَّهُ ۖ وَأَوْفُوا الْكَيْلَ وَالْمِيزَانَ بِالْقِسْطِ ۖ لَا نُكَلِّفُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا ۖ وَإِذَا قُلْتُمْ فَاعْدِلُوا وَلَوْ كَانَ ذَا قُرْبَىٰ ۖ وَبِعَهْدِ اللَّـهِ أَوْفُوا ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ ﴿١٥٢﴾
152.Wala msiikurubie mali ya yatima isipokuwa kwa njia bora zaidi, Mpaka afikie kukomaa kwake. Na kamilisheni vipimo vya ujazo na uzani kwa uadilifu. Hatuikalifishi nafsi ila kwa uweza wake Na msemapo semeni kwa uadilifu hata kama ni jamaa, Na tekelezenim ahadi ya Mwenyezi Mungu. Haya ameusiwa ili mpate kukumbuka.
وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ ﴿١٥٣﴾
153.Na kwa hakika hii ndiyo njia yangu iliyonyooka, basi ifuateni wala msifuate njia nyingine zikawatenga mbali na njia yake (Mwenyezi Mungu). Hayo amewausia ili muwe na takua.
ALIYOWAHARAMISHA MOLA WENU
Aya 151 – 153
MAANA
Katika Aya zilizoatangulia, Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameonyesha kuwa washirikina walihalalisha na wakaharamisha kwa dhana na matamanio; na kwamba wao walimnasibishia Mwenyezi Mungu shirki kwa uzushi na bila ya ujuzi wowote. Akawajibu kwa mantiki ya kiakili na kimaumbile, na akataja katika vilivyo haramu: Mfu, damu ya kutirizika, nyama ya nguruwe na kilichochinjwa bila ya kutajwa jina la Mwenyezi Mungu.
Katika Aya hizi tatu (tulizo nazo) ametaja baadhi ya yaliyo haramu, Kwa upande mwingine ametaja baadhi ya mambo yaliyowajibu; kama vile kutopunja katika vipimo, kutekeleza ahadi na kufuata usawa.
Kimsingi ni kuwa kila ambalo ni wajib kulifanya, basi ni haramu kuliacha na kila lililoharamu kulifanya basi ni wajib kuliacha.
Baadhi ya wafasiri wameuita mkusanyiko wa Aya hizi tatu kuwa nasaha kumi.
NASAHA KUMI
Sema: Njooni niwasomee aliyowaharamishia Mola wenu: Kwamba msimshirikishe na chohote.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameanzia na msingi wa kwanza wa itikadi, ambao ni kukana shirki ambako mkabala wake ni kuthibitisha Tawhid. Haki zote na wajibu wote unategemea kwenye msingi huu, na kwa msingi huu hukubaliwa twaa na amali za kkheri. Maana ya Tawhid yanafupika katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ﴾
“Hakuna chochote kama mfano wake”
(42:11)
Si katika dhati wala sifa au vitendo.
Na kuwafanyia wema wazazi wawili.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amekutanisha nasaha kwa wazazi wawili pamoja na uungu wake, kutambulisha kuwa kuwafanyiwa wema wazazi wawili kunapasa kuwe kwa aina yake. Ni kama kwamba amesema: Msimshirikishe Mwenyezi Mungu na kitu wala msishirikishe kuwafanyia wema wazazi wawili na wema wowote. Tumeyafafanua hayo katika kufasiri Juz.1 (2:83)
Wala msiwaue watoto wenu kwa kuogopa kuishiwa, sisi tutawaruzuku nyinyi na wao pia.
Baada ya kuwausia watoto kwa mababa, sasa anawausia mababa kwa watoto, Yametangulia maelezo yake katika kufasiri Aya 137 ya Sura hii.
Wala msikurubie mambo machafu, yaliyodhihirika na yaliyofichika.
Kila linalopetuka mpaka katika ubaya ni ovu; kama vile zina, ulawiti, dhuluma na kuvunja heshima. Vilevile uwongo, kusengenya, fitina, na husuda. Uovu mkubwa zaidi ni ulahidi, kumshirikisha Mwenyezi Mungu, kuwaudhi wazazi wawili, kuua nafsi isiyo na hatia na kula mali ya yatima.
Mwenyezi Mungu amehusisha kuyataja haya pamoja na kuwa yanaingia katika uwovu, kwa kufahamisha kuwa yamefikilia ukomo wa ubaya na uovu; ni sawa yawe yamefanywa kisiri au kidhahiri.
Imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas kwamba watu wa wakati wa ujahiliya walikuwa wakichukia zinaa kufanywa dhahiri na walikuwa wakiifanya kisiri, ndipo akawakataza Mwenyezi Mungu katika hali zote mbili. Na imepokewa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.w.t), amesema: “Je, niwafahamishe yule aliye mbali na mimi?” Wakajibu: “Ndio Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu!” Akasema: “Ni mwovu mno, mwenye kuchukiza, bahili, mwenye kiburi, hasidi, aliyesusuwaa moyo, aliye mbali na kila kheri inayotarajiwa na asiyeaminiwa na kila shari inayoogopwa.”
Wala msiiue nafsi ambayo Mwenyezi Mungu ameharamisha (kuiua), ila kwa haki.
Kimsingi, kuua nafsi ni haramu, wala hakuwi halali ila kwa sababu moja kati ya nne ambazo tatu katika hizo zimeelezwa na Hadith ya Mtume(s.a.w.w)
: “Haiwi halali damu ya Mwislamu (kuuawa) ila kwa moja ya mambo matatu: Kukufuru baada ya kuamini, kuzini baada ya kuoa na kuua nafsi bila ya haki.” Qur’an nayo imeelezea sababu ya nne iliposema:
﴿ إِنَّمَا جَزَاءُ الَّذِينَ يُحَارِبُونَ اللَّهَ وَرَسُولَهُ وَيَسْعَوْنَ فِي الْأَرْضِ فَسَادًا أَنْ يُقَتَّلُوا أَوْ يُصَلَّبُوا﴾
“Hakika malipo ya wale wanaopigana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kufanya ufisadi katika ardhi, ni kuuawa au kusulubiwa”
(5:33).
Hayo amewausia Mwenyezi Mungu ili mpate kufahamu.
Yaani mjue ubaya wa ushirikina, kuua nafsi, kufanya uovu na mjue uzuri wa kuwafanyia wema wazazi wawili.
Wala msiikurubie mali ya yatima isipokuwa kwa njia bora zaidi.
Kuzuia kukurubia ndio ufasaha zaidi wa kukataza kuliko kukataza tendo lenyewe, na kunahusu njia zote za matumizi; kama ambavyo bora zaidi ni nzuri kuliko bora tu.
Maana yaliyokusudiwa ni kutilia mkazo katika kutunza mali ya kila asiyeweza kutumia mali yake; awe yatima, mwendawazimu, safihi, aliyepotea au mtoto mdogo anayesimamiwa mali zake na baba yake. Kwa hiyo ni juu ya wasimamizi kuzichunga mali za wanaowasimamia na kuangalia vizuri mambo yao.
Kuanzia hapa ndio wamesema kundi la mafakihi wakubwa, kwamba haiwezekani kwa msimamzi kutumia mali ya anayemsimamia ila kwa masilahi ya mwenye mali. Na sisi tuko pamoja na rai hii; hata kama msimamizi ni baba au babu. Dalili yetu ni neno ‘njia bora zaidi’ Ama Hadith isemayo: “Wewe na mali yako ni (milki) ya baba yako”, ni hukumu ya kimaadili tu, si ya kisharia; kwa dalili ya neno ‘Wewe’, kwa sababu, mtoto si bidhaa anayomiliki baba.
Utauliza kuwa
: neno yatima linahusika na yule aliyefiwa na baba yake akiwa mdogo, sasa imekuaje kulihusisha na kila asiyeweza kutumia?
Sisi tunajua kabisa kwamba sababu ya kutumia kwa njia iliyo bora zaidi ni kule kushindwa kutumia yule mwenye mali na wala sio uyatima; na kushindwa kutumia kumethibitika kwa wote waliotajwa bila ya tofauti.
Mpaka afikie kukomaa kwake
. Utaipata tafsiri yake katika Juz.5 (4:6)
Na kamilisheni vipimo vya ujazo na uzani kwa uadilifu
mkiuza au mkininua.
Hatuikalifishi nafsi ila kwa uweza wake. Jumla hii imeingia katikati ikiwa na makusudio ya kufahamisha kuwa ukamilishaji wa vipimo uliotajwa ni ule uliozoelekea kwa watu; husamehewa kiasi kichache kilichozidi au kupungua. Kwa sababu kutekeleza kipimo cha sawaswa kabisa ni aina ya uzito:
﴿ وَمَا جَعَلَ عَلَيْكُمْ فِي الدِّينِ مِنْ حَرَجٍ﴾
“Wala hakuwawekea mambo mazito katika dini”
(22:78)
Kwa hali yoyote ni kuwa msingi katika aina zote za biashara ni kuridhia pande zote mbili, iwe ni bidhaa inayopimwa kwa kilo, kwa kuhesabiwa kwa mita, kukadiriwa kwa kifikra, kama kuandika, au kwa kuangalia tu, kama sanaa iliyoundwa kwa mkono.
Na msemapo semeni kwa uadilifu hata kama ni jamaa.
Huu ndio ushupavu wa yule anayemwogopa Mwenyezi Mungu na kumfanyia ikhalsi na kutambua kuwa mbele yake kuna majukumu, sio kuwa mbele yake kuna mke, baba, mama, mtoto au mkwe. Hakuna chochote isipokuwa haki na uadilifu tu. Ama mwenye kutumia jina la dini, kisha afuate matamanio yake kwa ndugu au rafiki, basi huyo hana dini kitu.
Na tekelezeni ahadi ya Mwenyezi Mungu.
Kila aliloharamisha Mwenyezi Mungu na alilolikataza ni ahadi yake. Utekelezaji wake ni kufuata amri na kutii. Hayo amewausia ili mpate kukumbuka, Msimsahau kumtii yule asiyewasahau.
Na kwa hakika hii ndiyo njia yangu iliyonyooka.
Hii ni ishara ya yote yaliyotajwa; ndiyo njia ya Mwenyezi Mungu iliyonyooka, vinginevyo ni upotevu.
Basi ifuateni wala msifuate njia nyingine
; kama vile shirki, ulahidi, vikundi na dini za ubatilifu.Zikawatenga mbali na njia yake (Mwenyezi Mungu).
Njia yoyote isiyokuwa Qur’an na Uislam basi hiyo ni njia ya matamanio tu, Na matamanio hayana udhibiti wala mpaka wowote. Watu wakiyafuata ndipo hugawanyika vikundi na vyama mbalimbali. Lakini kama wote wakifuata dini ya Mwenyezi Mungu basi itikadi ya kweli na imani ya sawa itawaweka pamoja.
Kuna Hadith isemayo kuwa Mtume(s.a.w.w)
alipiga msitari kwa mkono wake kisha akasema: “Hii ndiyo njia ya Mwenyezi Mungu iliyonyooka:” Kisha akapiga msitari kuumeni na kushotoni mwa msitari ule, akasema: “Hii siyo njia ispokuwa shetani ndiyo anayoilingania; kisha akasoma: “Na kwa hakika hii ndiyo njia yangu iliyonyooka, basi ifuatie wala msifuate njia nyingine zikawatenga mbali na njia yake (Mwenyezi Mungu).”
ثُمَّ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ تَمَامًا عَلَى الَّذِي أَحْسَنَ وَتَفْصِيلًا لِّكُلِّ شَيْءٍ وَهُدًى وَرَحْمَةً لَّعَلَّهُم بِلِقَاءِ رَبِّهِمْ يُؤْمِنُونَ ﴿١٥٤﴾
154.Kisha tulimpa Musa Kitab, kwa kumtimizia yule aliyefanya wema. Na kuwa ni ufafanuzi wa kila kitu na mwongozo na rehema ili wapate kuamini kukutana na Mola wao.
وَهَـٰذَا كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ مُبَارَكٌ فَاتَّبِعُوهُ وَاتَّقُوا لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴿١٥٥﴾
155.Na hii ni Kitab tulichokiteremsha kilicho barikiwa. Basi kifuateni na muwe na takua ili mrehemiwe.
أَن تَقُولُوا إِنَّمَا أُنزِلَ الْكِتَابُ عَلَىٰ طَائِفَتَيْنِ مِن قَبْلِنَا وَإِن كُنَّا عَن دِرَاسَتِهِمْ لَغَافِلِينَ ﴿١٥٦﴾
156.Msije mkasema kuwa vitabu viliteremshiwa makundi mawili tu, yaliyokuwa kabla yetu nasi tulikuwa hatuna habari ya yale waliyoyasoma.
أَوْ تَقُولُوا لَوْ أَنَّا أُنزِلَ عَلَيْنَا الْكِتَابُ لَكُنَّا أَهْدَىٰ مِنْهُمْ ۚ فَقَدْ جَاءَكُم بَيِّنَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ ۚ فَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّن كَذَّبَ بِآيَاتِ اللَّـهِ وَصَدَفَ عَنْهَا ۗ سَنَجْزِي الَّذِينَ يَصْدِفُونَ عَنْ آيَاتِنَا سُوءَ الْعَذَابِ بِمَا كَانُوا يَصْدِفُونَ ﴿١٥٧﴾
157.Au mkasema: Lau tungeliteremshiwa Kitab bila shaka tungelikuwa waongofu zaidi kuliko wao. Basi imewafikia hoja kutoka kwa Mola wenu, uwongofu na rehema. Basi ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule anayezikadhibisha ishara za Mwenyezi Mungu na akajitenga nazo? Tutawalipa wale wanaojitenga na ishara zetu, adhabu mbaya kwa sababu ya kule kujitenga kwao.
KISHA TULIMPA MUSA KITAB
Aya 154 – 157
MAANA
Kisha tulimpa Musa Kitab.
Wameduwaa wafasiri kuhusu neno ‘Kisha’ Kwa sababu mazungumzo ni ya Qur’an katika Aya zilizotangulia. Na Aya hii inazungumzia Tawrat iliyoshuka kabla ya Qur’an; na ‘Kisha’ inafahamisha kuja nyuma ya kilicho kabla yake kwa wakati. Sasa imekuwaje itajwe Qur’an kisha Tawrat na iliyoanza ni Tawrat?
Razi ametaja njia tatu, na Tabrasi akazidisha ya nne, Sisi hatuoni jambo lolote la kurefusha maneno hapo. Kwa sababu mpangilio hapa ni wa maneno sio wa wakati, na uunganisho ni wa habari kuungana na habari nyingine sio maana kuungana na maana nyingine.
Kumtimizia yule aliyefanya wema.
Yaani tumempa Musa Kitab nacho kinatimiza upungufu wa aliyefanya wema, kunafaika nacho; kama kusema kwake Mwenyezi Mungu:
﴿الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا﴾
“Leo nimewakamilishia dini yenu na kuwatimizia neema yangu na nimewapendelea Uislamu kuwa dini”
(5:3)
Na kuwa ni ufafanuzi wa kila kitu.
Hii ni sifa ya pili ya Kitab cha Musa
kwamba kimekusanya hukumu zote walizozitaja watu wa wakati ule. Mwenyezi Mungu mtukufu anasema:
﴿وَكَتَبْنَا لَهُ فِي الْأَلْوَاحِ مِن كُلِّ شَيْءٍ مَّوْعِظَةً وَتَفْصِيلًا لِّكُلِّ شَيْءٍ﴾
“Na tukamwandikia katika mbao mawaidha ya kila kitu na ufafanuzi wa kila kitu”
(7:144).
Na mwongozo na rehema.
Sifa mbili nyingine za Kitab cha Musa, Kwa mwongozo, watu watajua haki na kheri, na kwa rehema, watu wataishi maisha ya utulivu.
Ili wapate kuamini kukutana na Mola wao.
Dhamiri inawarudia waisrael, kwa maana tumempa Musa Kitab kilichokusanya sifa zilizotajwa, ili watu wake wamwamini Mwenyezi Mungu na thawabu zake na adhabu yake. Lakini wao waling’ang’ania inadi yao, na wakasema miongoni mwa waliloyasema:
﴿ يَا مُوسَىٰ لَنْ نُؤْمِنَ لَكَ حَتَّىٰ نَرَى اللَّهَ جَهْرَةً﴾
“Ewe Musa! Hatutakuamini mpaka tumwone Mungu waziwazi”
Juz.1 (2:55)
Tukadrie kama wangemwona Mwenyezi Mungu waziwazi - na kukadiria muhali si muhali - basi wao wangesema kuwa huyu si Mola, kwa vile yeye si pauni wala dola.
Na hii ni Kitab tulichokiteremsha kilichobarikiwa na baraka.
Hii ni Qur’an tukufu, nayo ni yenye baraka kwa sababu ina kheri na manufaa mengi.
Basi kifuateni na muwe na takua ili mrehemiwe.
Fuateni aliyowaamrisha na muache aliyowakataza ili iwaenee rehma yake duniani na akhera.
Msije mkasema kuwa vitabu viliteremshiwa makundi mawili tu, yaliyokuwa kabla yetu nasi tulikuwa hatuna habari ya yale waliyoyasoma.
Wanaambiwa washirikina wa Kiarabu. Makusudio ya vitabu ni Tawrat na Injil; na makundi mawili ni watu wa Kitab: Mayahudi na Manaswara (Wakristo).
Maana ni kuwa enyi Waarabu, tumewateremshia Qur’an kwa lugha yenu na kwa mtu wenu anayetokana nanyi ili msiwe na udhuru wa shirki yenu, kwamba hakikuteremshwa Kitab kwa lugha yenu na kuwa hamkujua kuk- isoma na kujifundisha mafunzo yake.
Au mkasema: Lau tungeliteremshiwa Kitab bila shaka tungelikuwa woaongofu zaidi kuliko wao.
Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu anawaondolea udhuru wa lugha, na katika Aya hii anawaondolea udhuru wa kufikiwa na Kitabu chenyewe. Kwa ufupi ni kuwa Aya hii na iliyo kabla yake inafanana na kauli ya asemaye: “Fulani ni tajiri na mimi sina chochote, lau ningekuwa na kitu basi ningelifanya mengi.” Ndipo Mwenyezi Mungu akawajibu kwa jawabu mkataa:
Basi imewafikia hoja kutoka kwa Mola wenu, na uwongofu na rehema.
Makusudio ya hoja ni Qur’an, ndani yake mna dalili na ubainifu wa kumsadikisha Muhammad(s.a.w.w)
. Vilevile mna hukumu na mafunzo yenye kuwatoa watu kwenye giza kwenda kwenye mwanga.
Basi ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule anayezikadhibisha ishara za Mwenyezi Mungu na akajitenga nazo?
Hakuna kabisa dhalimu mkubwa wa nafsi yake na watu kuliko yule anayekana haki na kheri, akahangaika katika dunia kufanya ufisadi na kupinga njia ya Mwenyezi Mungu.
Tutawalipa wale wanaojitenga na ishara zetu adhabu mbaya kwa sababu ya kule kujitenga kwao.
Ishara za Mwenyezi Mungu ni hoja zake na dalili zake. Maana ni kuwa yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu amesimamisha dalili na hoja mkataa juu ya umoja wake na juu ya utume wa Muhammad na ukweli wa aliyokuja nayo kutoka kwa Mola wake, lakini washirikina walipinga wakakataa kuzingatia vizuri hoja hizo kwa kuifanyia inadi haki na watu wa haki. Kwa hiyo wakastahiki hizaya na adhabu kali.