8
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA NANE
Sura Ya Saba: Sura Al-A’raf
Imeteremshwa Makka, isipokuwa Aya 163, Mwenye Majmau anasema imeshuka Madina. Ina Aya 205.
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu
﴿١﴾ المص
1. Alif Lam Mim Swad
كِتَابٌ أُنزِلَ إِلَيْكَ فَلَا يَكُن فِي صَدْرِكَ حَرَجٌ مِّنْهُ لِتُنذِرَ بِهِ وَذِكْرَىٰ لِلْمُؤْمِنِينَ ﴿٢﴾
2. Kitab kimeteremshwa kwako, basi isiwe dhiki kifuani mwako kwacho ili upate kuonya kwacho na kiwe ni ukumbusho kwa wanaoamini.
اتَّبِعُوا مَا أُنزِلَ إِلَيْكُم مِّن رَّبِّكُمْ وَلَا تَتَّبِعُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ قَلِيلًا مَّا تَذَكَّرُونَ ﴿٣﴾
3. Fuateni mliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wenu, Wala msifuate wasimamizi badala yake, Ni machache mnayoyakumbuka.
KITABU KIMETEREMSHWA KWAKO
Aya 1 – 3
MAANA
Alif Lam Swad
Hizi huandikwa na kutamkwa kwa majina ya herufi zake kama zilivyo. Yamepita maelezo yake katika Juz.1 mwanzo wa Sura ya pili (Al- Baqara).
Kitab kimeteremshwa kwako, basi isiwe dhiki kifuani mwako kwacho, Ili upate kuonya kwacho na kiwe ni ukumbusho kwa wanaoamini.
Maneno anaambiwa Mtume Muhammad(s.a.w.w)
, Makusudio ya Kitab ni Qur’an, na waumini ni kila anayenufaika na Qur’an, ni sawa iwe ni sababu ya kuamini kwake au kuimarisha imani yao waendelee nayo.
Maana ni kuwa: Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameteremsha Qur’an kwa Mtume(s.a.w.w)
ili awaonye kwayo walahidi na washirikina na watu wa dini za ubatilifu; na ili wanufaike nayo watu wenye maumbile safi.
Kazi hii inampa uzito Mtume(s.a.w.w)
kutoka kwa makafiri ambao anawakabili kwa Qur’an. Kwa sababu, inalenga katika kubatilisha itikadi zao na hali zao ambazo wamezirithi kutoka kwa mababu zao wa jadi. Hapo Mtume alipata dhiki kutokana na inadi na upinzani wao.
Mwenyezi Mungu anasema:
وَلَقَدْ نَعْلَمُ أَنَّكَ يَضِيقُ صَدْرُكَ بِمَا يَقُولُونَ ﴿٩٧﴾
“Na kwa hakika sisi tunajua kwamba kifua chako kinadhikika kwa yale wayasemayo”
(15:97) .
Na akasema tena Mwenyezi Mungu:
إِنَّا سَنُلْقِي عَلَيْكَ قَوْلًا ثَقِيلًا ﴿٥﴾
“Hakika sisi tutakuteremshia kauli nzito”
(73:5)
Fuateni mliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wenu.
Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu amemwamrisha Mtume wake kufikisha na kutojali upinzani. Katika Aya hii anawaamrisha watu wamfu- ate Mtume na waitumie Qur’an.
Ali Al-Murtadha
anasema: “Hatawaadhibu Mwenyezi Mungu watu wajinga kwa kutojifundisha, mpaka awaadhibu wenye elimu kwa kutofundisha” Na kinyume chake pia.
Wala msifuate wasimamizi badala yake.
Kwa sababu hakuna badala ya Qur’an ila upotevu na matamanio.
Ni machache mnayoyakumbuka
na hali mnawaidhika na mawaidha ya Mwenyezi Mungu na nasaha zake. Kwa sababu nyinyi hamwogopi mwisho utakuwaje; na anayewaidhika ni yule anayeogopa.
Kauli yake ‘ni machache mnayokumbuka’ ni kuashiria uchache wa wale wanaowaidhika.
وَكَم مِّن قَرْيَةٍ أَهْلَكْنَاهَا فَجَاءَهَا بَأْسُنَا بَيَاتًا أَوْ هُمْ قَائِلُونَ ﴿٤﴾
4. Na vijiji vingapi tuliiangamiza; ikafikia adhabu yetu usiku au katika wakati wa kailula.
فَمَا كَانَ دَعْوَاهُمْ إِذْ جَاءَهُم بَأْسُنَا إِلَّا أَن قَالُوا إِنَّا كُنَّا ظَالِمِينَ ﴿٥﴾
5. Basi hakikuwa kilio chao, ilipowafikia adhabu yetu, ila kusema: Hakika sisi tulikuwa madhalimu.
فَلَنَسْأَلَنَّ الَّذِينَ أُرْسِلَ إِلَيْهِمْ وَلَنَسْأَلَنَّ الْمُرْسَلِينَ ﴿٦﴾
6. Kwa hakika tutawauliza wale waliopelekewa (Mitume) na pia kwa hakika tutawauliza (Mitume) waliopelekwa.
فَلَنَقُصَّنَّ عَلَيْهِم بِعِلْمٍ وَمَا كُنَّا غَائِبِينَ ﴿٧﴾
7. Tena kwa hakika tutawasimulia kwa ujuzi, wala hatukuwa mbali.
وَالْوَزْنُ يَوْمَئِذٍ الْحَقُّ فَمَن ثَقُلَتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ ﴿٨﴾
8. Na kipimo siku hiyo kitakuwa haki, Basi ambao uzani wao utakuwa mzito, hao ndio wenye kufaulu.
وَمَنْ خَفَّتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَـٰئِكَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُم بِمَا كَانُوا بِآيَاتِنَا يَظْلِمُونَ ﴿٩﴾
9. Na ambao uzani wao utakuwa hafifu, basi hao ndio waliozitia hasara nafsi zao kwa sababu ya kuzidhulumu Ishara zetu.
وَلَقَدْ مَكَّنَّاكُمْ فِي الْأَرْضِ وَجَعَلْنَا لَكُمْ فِيهَا مَعَايِشَ قَلِيلًا مَّا تَشْكُرُونَ ﴿١٠﴾
10. Na hakika tumewamakinisha katika ardhi na tukawawekea humo mahitaji ya maisha, Ni shukrani ndogo mnazotoa.
NA MIJI MINGAPI TULIIANGAMIZA
Aya 4-10
MAANA
Na miji mingapi tuliiangamiza; ikafikia adhabu yetu usiku au katika wakati wa kailula
.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kumwamrisha Mtume wake Mtukufu kuonya kwa Qur’an na kuamrisha watu kuifuata, katika Aya hii, anataja maangamizo ya waliopita ambao aliwaangamiza kwa sababu ya kupinga kwao Mwenyezi Mungu na kukadhibisha Mitume yake, na kwamba yeye Mwenyezi Mungu aliwateremshia adhabu usiku au wakati wa kailula, mchana, ambao ni wakati wa raha na amani, ili adhabu iwaumize zaidi.
Wafasiri wengi wanasema kuwa kaumu ya Nabii Lut walijiwa na adhabu usiku. Nami nashangaa sijui wameyatoa wapi haya, na Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema:
إِنَّ مَوْعِدَهُمُ الصُّبْحُ أَلَيْسَ الصُّبْحُ بِقَرِيبٍ ﴿٨١﴾ …
“Hakika miadi yao ni asubuhi, Je, asubuhi si karibu”
(11:81).
Kuna kikundi cha wafasiri waliosema kuwa kuna mageuzi ya kutanguliza maneo katika Aya hii tunayoifasiri; Kwa sababu kuangamia kunakuja baada adhabu, Kwamba isomeke hivi: Ni miji mingapi ilifikiwa na dhabu yetu tuliiangamiza? Razi ametaja njia tatu za kuawili Aya hii na Tabrasi akazidisha ya nne.
Ilivyo hasa ni kuwa hakuna wajibu wowote wa kupangilia maneno kulingana na maana ya hali halisi, ikiwa utaratibu wa hali halisi uko wazi na unajulikana na wote; kama ilivyo katika Aya. Na herufi “Fa’, kama ambavyo inakuja kwa maana ya kufuatisha, vilevile inakuja ikiwa ni ya ziada na ya kufasiri, Hapa, herufi ‘Fa’ inafasiri aina ya maangamivu waliyoyapata washirikina.
Basi hakikuwa kilio chao, ilipowafikia adhabu yetu, ila kusema: Hakika sisi tulikuwa madhalimu.
Washirikina walikuwa wakitambika kwa majina ya masanamu wakiwa wameamini kabisa. Lakini walipoona adhabu walijitenga na waungu wao na wakaelekea kwa Mwenyezi Mungu wakikiri ukafiri na ushirikina wao, lakini ni baada ya kukatika taklifa zote na kufungwa mlango wa toba.
Kwa hakika tutawauliza wale waliopelekewa (Mitume) na pia kwa hakika tutawauliza (Mitume) waliopelekwa.
Baada ya Mwenyezi Mungu kuelezea maangamivu yao duniani anaelezea kuwa wao wataulizwa huko akhera na wataulizwa Mitume pia, wawatolee ushahidi.
Tena kwa hakika tutawasimulia kwa ujuzi, wala hatukuwa mbali.
Mwenyezi Mungu hatatosheka na kuwauliza tu na kuwauliza Mitume, bali yeye pia atawasomea kila kitu walichokisema na kukifanya:
يَوْمَ يَبْعَثُهُمُ اللَّـهُ جَمِيعًا فَيُنَبِّئُهُم بِمَا عَمِلُوا أَحْصَاهُ اللَّـهُ وَنَسُوهُ وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ﴿٦﴾
“Siku Mwenyezi Mungu atakapowafufua wote, awaambie yale waliyoya- tenda; Mwenyezi Mungu ameyadhibiti, na wao wameyasahau; na Mwenyezi Mungu ni shahidi wa kila kitu.”
(58:6)
Mkusudio yake ni kuwatia msukosuko watambue nakama ya Mwenyezi Mungu na ghadhabu yake kwao, yakiwa ni malipo ya uasi na ukaidi wao.
MIZANI YA MATENDO
Na kipimo siku hiyo kitakuwa haki.
Maneno yamekuwa mengi kuhusu hakika ya mizani ambayo atapimia Mwenyezi Mungu matendo ya watu; mpaka baadhi ya watu wakasema kuwa mizani hiyo itakuwa na mikono miwili.
Tunavyofahamu sisi kuhusu mizani hii – na Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi – ni kuwa ni kipimo ambacho kitampambanua mtiifu na mwasi na mwema na mwuovu. Kipimo chenyewe ni amri ya Mwenyezi Mungu na makatazo yake.
Ukifika wakati wa Hisabu, huangaliwa aliyoyafanya na aliyoyaacha mwanaadamu, na hulinganisha kati ya aliyoamrishwa na Mwenyezi Mungu kuyafanya na aliyoyaacha. Vitendo vyake vikifuatana na amri ya Mwenyezi Mungu na makatazo yake, basi atakuwa ni katika waliofaulu, na kama si hivyo atakuwa ni katika wale ambao uzani waao umekua hafifu na kuwa katika madhalimu waliojihasiri wenyewe na adhabu ya moto.
Kwa maneno mengine ni kwamba kila kitu katika maisha haya kina msingi na udhibiti wake, iwe ni sayansi, fasihi au fani yoyote nyingine. Na kwayo hutofautiana na kingine, bali uzuri wake na ubaya wake unajulikana kutokana na misingi hiyo.
Misingi hiyo na udhibiti huo inaitwa mizani, makisio, njia na mwamuzi. Basi hivyo hivyo hisabu katika akhera ina misingi na udhibiti ambao Qur’an imeipa jina la Mizan na Swirat.
Kwa hiyo misingi hii au Mizani hii ya matendo ya watu ni amri ya Mwenyezi Mungu na makatazo yake. Kazi yake katika kumhukumu mtu kesho, ni kama kazi ya fiqhi na kanuni katika kuhukumiwa mshitakiwa katika maisha ya hapa duniani.
Basi ambao uzani wao utakuwa mzito.
Nao ni wale ambao matendo yao yamelingana na misingi ya amri za Qur’an na makatazo yake yakawa makamilifu.
Hao ndio wenye kufaulu.
Kwa sababu hawakuanguka mtihani.
Na ambao uzani wao utakuwa hafifu.
Nao ni wale ambao umedhihirika umbali baina ya matendo yao na hukumu za Mwenyezi Mungu na mafunzo yake.
Basi hao ndio waliozitia hasara nafsi zao kwa sababu ya kuzidhulumu Aya zetu.
Wafasiri wengi wamesema kuwa makusudio ya kuzidhulimu hapa ni kuzikufuru, lakini sawa ni kukadhibisha Aya za Mwenyezi Mungu kwa hali yoyote, kama inavyoonyesha Aya yenyewe, ni sawa Aya hizo ziwe zinafahamisha umoja wa Mwenyezi Mungu, ujumbe wa Mitume yake, ufufuo au halali yake na haramu yake.
Na hakika tumewamakinisha katika ardhi na tukawawekea humo mahitaji ya maisha, Ni shukrani ndogo mnazotoa.
Baada ya Mwenyezi Mungu kuwamrisha washirikina kufuata waliyoteremshiwa, na kuwahofisha na adhabu ya dunia na akhera, sasa anawakumbusha neema yake kwao; na kwamba yeye ndiye aliyewaweka katika ardhi hii akawapa uwezo wa kuitumia kwa maslahi yao.
Mmoja wa wafasiri wa kisasa anasema: “Lau si Mwenyezi Mungu kumakinisha mtu katika ardhi hii, asingeliweza kiumbe huyu dhaifu kuyamudu maumbile”.
وَلَقَدْ خَلَقْنَاكُمْ ثُمَّ صَوَّرْنَاكُمْ ثُمَّ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ لَمْ يَكُن مِّنَ السَّاجِدِينَ ﴿١١﴾
11. Na hakika tuliwaumba, kisha tukawatia sura, Kisha tukawaambia Malaika: Msujudieni Adam; Basi waka- sujudu wote isipokuwa Iblisi hakuwa miongoni mwa walio- sujudu.
قَالَ مَا مَنَعَكَ أَلَّا تَسْجُدَ إِذْ أَمَرْتُكَ قَالَ أَنَا خَيْرٌ مِّنْهُ خَلَقْتَنِي مِن نَّارٍ وَخَلَقْتَهُ مِن طِينٍ ﴿١٢﴾
12. Akasema (Mwenyezi mungu): Nini kilichokuzuia kumsujudia nilipokuamrisha? Akasema: Mimi ni bora kuliko yeye, umeniumba kwa moto naye umemuumba kwa udongo.
قَالَ فَاهْبِطْ مِنْهَا فَمَا يَكُونُ لَكَ أَن تَتَكَبَّرَ فِيهَا فَاخْرُجْ إِنَّكَ مِنَ الصَّاغِرِينَ ﴿١٣﴾
13. Akasema: Basi shuka kutoka huko, haikufalii kufanya kiburi humo. Basi toka, hakika wewe ni miongoni mwa walio duni.
قَالَ أَنظِرْنِي إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ ﴿١٤﴾
14. Akasema: Nipe muda mpaka siku watakapofufuliwa.
قَالَ إِنَّكَ مِنَ الْمُنظَرِينَ ﴿١٥﴾
15. Akasema (Mwenyezi mungu): Utakuwa katika waliopewa muda.
قَالَ فَبِمَا أَغْوَيْتَنِي لَأَقْعُدَنَّ لَهُمْ صِرَاطَكَ الْمُسْتَقِيمَ ﴿١٦﴾
16. Akasema: Kwa kuwa umenipoteza, basi hakika nitawakalia katika njia yako.
ثُمَّ لَآتِيَنَّهُم مِّن بَيْنِ أَيْدِيهِمْ وَمِنْ خَلْفِهِمْ وَعَنْ أَيْمَانِهِمْ وَعَن شَمَائِلِهِمْ وَلَا تَجِدُ أَكْثَرَهُمْ شَاكِرِينَ ﴿١٧﴾
17. Kisha hakika nitawaendea kwa mbele yao na nyuma yao na kuumeni kwao na kushotoni kwao; wengi katika wao hutawakuta wenye kushukuru.
قَالَ اخْرُجْ مِنْهَا مَذْءُومًا مَّدْحُورًا لَّمَن تَبِعَكَ مِنْهُمْ لَأَمْلَأَنَّ جَهَنَّمَ مِنكُمْ أَجْمَعِينَ ﴿١٨﴾
18. Akasema: Toka humo, hali ya kuwa ni mwenye kufedheheka na mwenye kufukuzwa. Atakayekufuata miongoni mwao, basi hakika nitaijaza Jahannam kwa nyinyi nyote.
NA HAKIKA TULIWAUMBA
Aya 11-18
ASILI YA MTU
MAANA
Na hakika tuliwaumba, kisha tukawatia sura.
Maneno haya wanaambiwa wanaadamu, Maana ya ‘tuliwaumba’ ni kuwa yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu aliianzisha asili yetu ya kwanza kutokana na mchanga na sisi akatutoa kutokana na tone la manii ambalo linaishia kwenye mchanga. Makusudio ya tuliwatia sura ni kwamba yeye amejaalia mada ya kwanza aliyotuumba kwayo kuwa ni mtu kamili; kama alivyosema:
أَكَفَرْتَ بِالَّذِي خَلَقَكَ مِن تُرَابٍ ثُمَّ مِن نُّطْفَةٍ ثُمَّ سَوَّاكَ رَجُلًا ﴿٣٧﴾ …
“Je, unamkufuru yule aliyekuumba kwa udongo, tena kwa tone la manii, kisha akakufanya mtu kamili?.
(18:37).
Kwa hiyo tofauti baina ya kuumba na kutia sura ni kwamba kuumba maana yake ni kukipatisha kitu na kukianzisha. Ama kukitia sura ni kukipa kitu sura hasa baada ya kukianzisha.
Unaweza kuuliza kuwa
: wafuasi wa Darwin wanasema kwamba mtu kwanza alipatikana katika sura isiyokuwa hii aliyo nayo sasa; kisha ikageukageuka mpaka kufikia ilivyo sasa.
Jibu
: sisi tuko pamoja na dalili za kielimu zisizokubali shaka na dhana za kupinga; Kwa sababu pale tu inapozuka dhana, basi dalili hubatilika. Hii ni hakika ya ubainifu iliyo wazi hawaipingi hata wenye nadharia ya majaribio ambao wamesema chimbuko la maarifa ni lazima litokane na majaribio ya kuhisi.
Dalili kubwa waliyoitegemea wenye nadharia ya mageuzi ni ufukuaji wa vitu vya kale; kuwa wamegundua aina za wanyama, wengine ni bora zaidi. Na kwamba muda wa wale waliokuwa bora zaidi umechelewa kuliko wa wale walio duni na kwamba kuna kushabihiana na binadamu katika mambo mengi.
Sisi hatupingi ugunduzi huu lakini, hauthibitishi nadharia ya Darwin, Kwa sababu hauleti uhakika usio na shaka kuwa aliye bora amekuwa kutokana na aliye duni, bali hilo haliwezekani na inawezekana kuwa kila mmoja kati ya aliye bora na duni ni aina nyingine iliyopatikana kutokana na hali inayo afikiana nayo, kisha ikatoweka wakati ilipobadilika hali yake, kama zilivyotoweka aina nyinginezo za wanyama na mimea.
Ikiwa mambo mawili yanawezekana, basi kuchukua moja tu, na kuacha jingine ni kujichukulia madaraka.
Katika niliyoyasoma ni kwamba wataalamu wengi, wakiwemo walahidi, walikuwa wakiamini nadharia ya Darwin, lakini walipoingia katika nyanja za elimu wakabadilika kutokana na yale tuliyoyataja; na kwamba mtu ana aina pekee za kiakili na kiroho zinzohusiana naye, zinazomfanya awe tofauti na viumbe vingine.
Kisha tukawaambia Malaika: Msujudieni Adam, Basi wakasujudu wote isipokuwa Iblisi hakuwa miongoni mwa waliosujudu.
Umetangulia mfano wake katika Juz.1 (2:82)
Akasema: Nini kilichokuzuia kumsujudia nilipoamrisha?
Makusudio ya kusujudu hapa ni kusujudu kwa kimaamkuzi, sio kwa kiibada, nako ni kumtii Mwenyezi Mungu, kwa sababu ni amri yake.
Akasema: Mimi ni bora kuliko yeye, umeniumba kwa moto naye umemuumba kwa udongo.
Chochote akifanyacho Iblisi, lazima atakitafutie visibabu; na sharti la msingi la kila kisababu katika mantiki yake ni kukhalifu matakwa ya Mwenyezi Mungu na radhi yake. Hiyo ndiyo asili ya kwanza anayoitege- mea Iblis katika kauli zake na vitendo vyake.
Fakihi anajitahidi kufanya utafiti ili aongoke kwenye hukumu alizoziwekea sharia Mwenyezi Mungu, lakini Iblisi kwake yeye sharia za hukumu ni zile zenye msingi wa “Mwenyezi Mungu anasema hivyo nami nasema hivi.”
Mwenyezi Mungu alimwamuru Iblisi amsujudie Adam, lakini akakataa wala asiombe msamaha, bali alijigamba kwa kusema: “Vipi nimsujudie ambaye mimi ni mbora wake.” Kama kwamba anamwambia Mwenyezi Mungu Mtukufu: Ilikuwa wafaa wewe umwamuru Adam anisujudie mimi, sio mimi nimsujudie yeye.
Kwa hivyo utukufu, kwa mantiki ya Iblis ni kwa kuangalia asili, sio kwa kumcha Mwenyezi Mungu; na kwa Mwenyezi Mungu ni vitendo na takua si kwa asili. Na elimu kwa Iblis ni kukisia (Qiyasi) na matamanio; na kwa Mwenyezi Mungu ni Wahyi na hukmu ya kiakili ambayo uwazi wake haufanyi kutofautiana watu wawili.
Kwa hiyo, mwenye kuangalia asili yake au akaifanyia kiasi dini kwa rai yake, basi atakuwa amemfuata Iblis atake asitake.
Mwenye Tafsir Al-Manar anasema: “Imepokewa Hadith kutoka kwa Jafar As-sadiq, kutoka kwa baba yake, naye kutoka kwa babu yake kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
amesema: “Wa kwanza aliyeifanyia makisio (qiyas) dini ni Iblis, Mwenyezi Mungu alimwambia amsujidie Adam, yeye akasema ni bora kuliko huyo”
Kisha akaendelea kusema Jafar: “Mwenye kulifanyia makisio (qiyas) jambo la dini, Mwenyezi Mungu atamkutanisha na Iblis siku ya kiyama.”
Utauliza
: Aya hii inafahamisha kuwa uhai unapatikana kutokana na moto kama vile Aya nyingine isemayo:
وَخَلَقَ الْجَانَّ مِن مَّارِجٍ مِّن نَّارٍ ﴿١٥﴾
“Na akaumba majini kwa ulimi wa moto”
(55:15)
Na Aya nyingine inasema:
وَجَعَلْنَا مِنَ الْمَاءِ كُلَّ شَيْءٍ حَيٍّ ﴿٣٠﴾
“Na tukafanya kwa maji kila kitu kilicho hai”
(21:30)
Jibu
: Vitu hai vilivyotajwa katika Qur’an tukufu viko aina nyingi: Kuna ulimwengu wa Malaika, wa majini na vile vilivyomo katika ardhi hii. Aina hii ya tatu ndiyo ambayo uhai wake uko katika maji, kama vile wanyama, mimea na watu. Hiyo ndiyo iliyokusudiwa kiujumla katika kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Na tukafanya kwa maji kila kitu kilicho hai.’
Na kuna viumbe vingine ambavyo uhai wake uko katika moto. Kwa maneno mengine ni kwamba maji ni lazima kwa maisha ya mwanaadamu kulingana na maumbile yake, pia wanyama na mimea. Lakini hii haikanushi kuwa kuna viumbe vingine ambavyo moto ni lazima katika maisha yao. Wataalamu wa elimu ya wadudu wanasema: Kuna aina ya wadudu ambao maisha yao yanategemea hewa ya sumu na visima vya mafuta (Petroli)!
Akasema: Basi shuka kutoka huko, haikufalii kufanya kiburi humo. Basi toka, hakika wewe ni miongoni mwa walio duni.
Imesemeka kuwa dhamir ya ‘huko’ inarudia Pepo, Wengine wakasema ni mbinguni. Sisi hatujishughulishi na ufafanuzi ikiwa haukutajwa katika Qur’an wala Hadith, tunatosheka na ujumla.
Mfumo wa maneno unaonyesha kwamba dhamir inarudia kwenye daraja ya juu mbele ya Mwenyezi Mungu; maana yakiwa kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimfukuza Iblis kutoka katika rehema yake hadi kwenye laana yake, ikiwa ni malipo ya kiburi chake na kujizuilia kwake kumtii Mwenyezi Mungu. Kwani kumsujudia Adam ni amri ya Mwenyezi Mungu na ni kumtii Mwenyezi Mungu na sio Adam. Kila anayejiona kuwa sawa ni kukataa hukumu ya Mwenyezi Mungu, basi anastahiki laana mpaka siku ya malipo.
Akasema: Nipe muda mpaka siku watakapofufuliwa.
Iblis alikuwa na haja nafsini mwake - atakayoifafanua - ya kutaka kupewa muda.
Akasema
- Mwenyezi Mungu Mtukufu -:Utakuwa katika waliopewa muda
. Inasemekana Iblis alitaka muda mpaka siku ambayo watafufuliwa wafu wote kwa ajili ya hisabu na malipo, Mwenyezi Mungu akakataa maombi haya, akampa muda mpaka siku ya kufa wote walio hai, ambao umeashiriwa na Aya isemayo:
قَالَ فَإِنَّكَ مِنَ الْمُنظَرِينَ ﴿٣٧﴾ إِلَىٰ يَوْمِ الْوَقْتِ الْمَعْلُومِ ﴿٣٨﴾
“Akasema: Hakika wewe ni katika waliopewa muda mpaka siku ya wakati maalum”
(15: 37 – 38).
Na siku hiyo ni ile saa ya kupuziwa Parapanda ambayo imeelezwa na Aya isemayo:
وَنُفِخَ فِي الصُّورِ فَصَعِقَ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَمَن فِي الْأَرْضِ ﴿٦٨﴾
“Na itapulizwa parapanda watoke roho waliomo ardhini na waliomo mbinguni …”
(39: 68)
Akasema: Kwa kuwa umenipoteza, basi hakika nitawakalia katika njia yako iliyonyooka.
Iblis alijiwekea mkakati kuwa atalipizia kisasi kwa kiumbe huyu aliyekuwa ni sababu ya kufukuzwa kwake kutoka katika rehema ya Mwenyezi Mungu kwenda kwenye laana. Akabainisha aina hii ya kujilipiza kwamba yeye ataikalia na kuziba njia, kwa Adam na kizazi chake, ile ielekeayo kwa Mwenyezi Mungu na kwenye twaa yake.
Kisha hakika nitawaendea kwa mbele yao na nyuma yao na kuumeni kwao na kushotoni kwao; wengi katika wao hutawakuta wenye kushukuru.
Kuwaendea kwake kwa pande hizi nne ni fumbo la ushawishi wake na jitihada yake katika kuwapoteza, kiasi ambacho hataacha maasi yoyote ila huwahada kwayo, wala twaa yoyote ila huwazuia.
Mwenyezi Mungu akiwaamrisha jihadi na kujitolea mhanga, basi Iblisi huwapendekezea uhai. Na kama Mwenyezi Mungu (s.w.t) akiwahimiza kujitolea mali katika njia yake Mwenyezi Mungu, basi mlaanifu huyu huwahofisha na ufukara.
Ikiwa Mwenyezi Mungu Mtukufu anawakataza pombe, zinaa na kamari, yeye huwavutia huko kwenye anasa na matamanio. Mungu akiwapa kiaga cha moto na kuwaahidi Pepo, basi adui huyu wa Mwenyezi Mungu huwaambia, hakuna Pepo wala moto.
Basi namna hii huhisabu kila haki kuwa ni batil na kila msimamo kuwa ni kombo. Hii inafanana kabisa na wale waliouza dini yao kwa shetani wak- iboresha vitendo vya wakoloni, wakiua wanawake na kuwafukuza wasio na hatia nchini mwao.
Akasema: Toka humo, hali ya kuwa ni mwenye kufedheheka na mwenye kufukuzwa.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemhusisha Iblisi na kufedheheka na kufukuzwa kwa kuwa yeye Mwenyezi Mungu alimteremsha cheo alichokuwa nacho.
Atakayekufuata miongoni mwao, basi hakika nitaijaza Jahannam kwa nyinyi nyote.
Yaani Jahannam itakuwa yake na wanachama wake waliomfuata. Aya hii ni kama ile isemayo:
لَأَمْلَأَنَّ جَهَنَّمَ مِنكَ وَمِمَّن تَبِعَكَ مِنْهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٨٥﴾
“Kwa hakika nitaijaza Jahannam kwa wewe na wale wanaokufuata miongoni mwao wote”
(38:85)
Hapa kuna maswali yanayotaka kujibiwa:
1.Kwanza
, Je, maneno yalikuwa ni moja kwa moja au ni kwa kupitia hali fulani?
2.Pili
, kauli ya Iblis: “Umenipoteza” inafahamisha kwamba kupotea kwake kulitokana na Mwenyezi Mungu, vipi atamwadhibu?
3.Tatu
, kwa nini Mwenyezi Mungu amempa muda Iblis naye anajua ufisadi wake na kuwaharibu wengine?
Tutajibu maswali haya matatu kwa ufupi sana:
Jibu
la kwanza, ni kuwa sisi tunaamini kuweko kwa majibizano hayo, kwa vile Wahyi umefahamisha hilo na akili hailipingi hilo, na si juu yetu kufanya utafiti wa aina ya majibizano hayo yalivyokuwa, maadamu Wahyi haukufafanua.
Kuhusu jibu la pili, upotevu unatokana na Iblis, na wala hautokani na Mwenyezi Mungu Mtukufu. Iblis mwenyewe amekiri kuwa yeye ni mpotezaji katika Aya isemayo:
وَلَأُغْوِيَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٣٩﴾ إِلَّا عِبَادَكَ مِنْهُمُ الْمُخْلَصِينَ ﴿٤٠﴾
“Na nitawapoteza wote isipokuwa waja wako waliosafishwa”
(15:39 –40)
Na vipi Mwenyezi Mungu ampoteze mja kisha amwadhibu kwa upotevu? Mwenyezi Mungu ametakata kabisa na hayo.
Ama kauli ya Iblis “Umenipoteza” Maana yake ni kwa kuwa umenifanyia mtihani wa kuniamrisha kumsujudia Adam, mtihani ambao umeniingiza katika uovu na uasi, basi nami nitafanya hivi na vile. Kwa maneno mengine ni kuwa Iblis anasema kwa kuwa umeniamrisha na nikaasi amri yako, basi sitamwacha yeyote atii amri yako.
Jibu
la swali la tatu ni kuwa: matakwa ya Mwenyezi Mungu yamehukumia kumpa mtu akili, ukumbusho kupita utume, uwezo wa kufanya kheri na shari na kumwachia hiyari na kumjaribu kwa matamanio na hadaa ana- zoshawishiwa na Iblis na majeshi yake; ili kumpambanua mwema na mwovu na mwenye ikhlas na mwenye khiyana.
Kwa maelezo zaidi angalia Juz.7 (5:94) kifungu ‘Maana ya mtihani wa Mwenyezi Mungu.’