TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NANE Juzuu 8

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NANE0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NANE Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NANE

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 12578
Pakua: 3188


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 17 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 12578 / Pakua: 3188
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NANE

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NANE Juzuu 8

Mwandishi:
Swahili

9

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA NANE

وَيَا آدَمُ اسْكُنْ أَنتَ وَزَوْجُكَ الْجَنَّةَ فَكُلَا مِنْ حَيْثُ شِئْتُمَا وَلَا تَقْرَبَا هَـٰذِهِ الشَّجَرَةَ فَتَكُونَا مِنَ الظَّالِمِينَ ﴿١٩﴾

19. Na Ewe Adam! Kaa wewe na mkeo katika Bustani (Pepo); na kuleni humo maridhawa popote mpendapo, wala msiukurubie mti huu msije mkawa miongoni mwa waliodhulumu (nafsi zao).

فَوَسْوَسَ لَهُمَا الشَّيْطَانُ لِيُبْدِيَ لَهُمَا مَا وُورِيَ عَنْهُمَا مِن سَوْآتِهِمَا وَقَالَ مَا نَهَاكُمَا رَبُّكُمَا عَنْ هَـٰذِهِ الشَّجَرَةِ إِلَّا أَن تَكُونَا مَلَكَيْنِ أَوْ تَكُونَا مِنَ الْخَالِدِينَ ﴿٢٠﴾

20. Basi shetani aliwatia wasiwasi ili kuwafichulia tupu zao walizofichiwa. Na akasema: Mola wenu hakuwakataza mti huu ila msije mkawa Malaika au kuwa miongoni mwa wakaao milele.

وَقَاسَمَهُمَا إِنِّي لَكُمَا لَمِنَ النَّاصِحِينَ ﴿٢١﴾

21. Na akawaapia: Kwa hakika mimi ni miongoni mwa watoa nasaha kwenu.

فَدَلَّاهُمَا بِغُرُورٍ فَلَمَّا ذَاقَا الشَّجَرَةَ بَدَتْ لَهُمَا سَوْآتُهُمَا وَطَفِقَا يَخْصِفَانِ عَلَيْهِمَا مِن وَرَقِ الْجَنَّةِ وَنَادَاهُمَا رَبُّهُمَا أَلَمْ أَنْهَكُمَا عَن تِلْكُمَا الشَّجَرَةِ وَأَقُل لَّكُمَا إِنَّ الشَّيْطَانَ لَكُمَا عَدُوٌّ مُّبِينٌ ﴿٢٢﴾

22. Basi akatelezesha kwa hadaa. Walipouonja mti ule, tupu zao ziliwadhihirikia, wakaanza kujibandika majani ya kwenye Bustani (Pepo), Na Mola wao akawaita: Je, sikuwakataza mti huo na kuwaambia kwamba shetani ni adui yenu wa dhahiri?

قَالَا رَبَّنَا ظَلَمْنَا أَنفُسَنَا وَإِن لَّمْ تَغْفِرْ لَنَا وَتَرْحَمْنَا لَنَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ ﴿٢٣﴾

23. Wakasema: Mola wetu! Tumedhulumu nafsi zetu; na kama hutatughufiria na kuturehemu tutakuwa miongoni mwa waliohasirika.

قَالَ اهْبِطُوا بَعْضُكُمْ لِبَعْضٍ عَدُوٌّ وَلَكُمْ فِي الْأَرْضِ مُسْتَقَرٌّ وَمَتَاعٌ إِلَىٰ حِينٍ ﴿٢٤﴾

24. Akasema: Shukeni, nyinyi kwa nyinyi ni maadui. Na makao yenu na starehe yatakuwa katika ardhi kwa muda.

قَالَ فِيهَا تَحْيَوْنَ وَفِيهَا تَمُوتُونَ وَمِنْهَا تُخْرَجُونَ ﴿٢٥﴾

25. Akasema: Mtaishi humo na mtafia humo na mtatolewa kutoka humo.

NA WEWE ADAM KAA PEPONI PAMOJA NA MKEO

Aya 19 – 25

MAANA

Na Ewe Adam! Kaa wewe na mkeo katika Bustani (Pepo); na kuleni humo maridhawa popote mpendapo, wala msiukurubie mti huu; msije mkawa miongoni mwa waliodhulumu (nafsi zao).

Imepita tafsir yake kwa ufafanuzi katika Juz.1 (2:35).

Basi shetani aliwatia wasiwasi ili kuwafichulia tupu zao walizofichiwa.

Maana ya walizofichiwa ni kuwa kila mmoja hakuweza kuona tupu yake wala ya mwenziwe. Hatujui wasiwasi wa shetani ulikuwaje, lakini tunaamini kuwa mawazo yoyote, kauli au kitendo chochote kinachokikingama katika njia ya uhai basi kinatokana na mawazo ya shetani.

Vyovyote iwavyo ni kwamba shetani alidhihirisha nasaha kwa Adam na Hawa na akaficha uwongo. Na dhahiri ya Aya inaonyesha kuwa Iblisi alikuwa akijua kwamba mwenye kula mti huu basi atakuwa uchi na kwamba mwenye kuwa uchi hufukuuzwa Peponi; na ndio akafanya hila hiyo ya kuwatoa Peponi na akasema:

Mola wenu hakuwakataza mti huu ila msije mkawa Malaika au kuwa miongoni mwa wakaao milele. Na akaawapia: Kwa hakika mimi ni miongoni mwa watoa nasaha kwenu.

Mlaanifu alibadilisha mambo kichwa chini miguu juu, aliapa kwamba yeye anawanasihi, na hali yeye ni adui mhasimu. Akaapa kuwa wao wakila mti watakuwa katika watakaokaa milele, naye anajua wazi kuwa mwisho wa kula huko ni kufukuzwa na mauti. Hivi ndivyo wafanyavyo mashetani wa kibinadamu, huwatia mawazo wenye akili ndogo, wakaona mangati ni maji na maji ni mangati.

Basi akawatelezesha kwa hadaa.

Yaani, baada ya Shetani kuwapia Adam na Hawa kwamba yeye ni mtoaji nasaha aliye mwaminifu walimwitikia hadaa zake wakidhani kuwa hakuna yeyote anayeweza kuapa kwa Mungu uwongo. Kwa sababu mlaanifu huyu ndiye wa mwanzo kuthubutu kula kiapo cha uwongo; kama ambavyo yeye ndiye wa kwanza kujinaki kwa asili yake na ndiye wa kwanza kukisia kwa rai yake.

Walipouonja mti ule, tupu zao ziliwadhihirikia, wakaanza kujibandika majani ya kwenye Bustani (Pepo)

Yaani walipokula mti kila mmoja akaiona tupu ya mwenziwe, ambapo mwanzo zilikuwa zimesitiriwa, wakatahayari na wakaona iko haja ya kujisitiri. Wakaanza kukusanya majani ya mti wa Peponi na kuyaweka kwenye tupu zao.

Na Mola wao akawaita: Je, sikuwakataza mti huo na kuwaambia kwamba Shetani ni adui yenu wa dhahiri?

Hii ni lawama kwa Adam na mkewe kutoka kwa Mwenyezi Mungu kutokana na kughurika kwao na kauli ya Iblisi, na udhaifu wa kukabiliana na upotevu wake; wakati huo huo akitanabahisha wajibu wa kutubia na kurejea.

Kwa hiyo ndio wakaharakisha kukiri dhambi na kuomba maghufira, wakasema:

Mola wetu! Tumedhulumu nafsi zetu; na kama hutatughufiria na kuturehemu tutakuwa miongoni mwa waliohasirika.

Na Mwenyezi Mungu alighufiria na kurehemu, kwa dalili ya Aya isemayo:

فَتَلَقَّىٰ آدَمُ مِن رَّبِّهِ كَلِمَاتٍ فَتَابَ عَلَيْهِ إِنَّهُ هُوَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ ﴿٣٧﴾

“Akapokea Adam maneno kutoka kwa Mola wake na Mola wake akapokea toba yake; hakika Yeye ni Mwingi wa kukubali toba, Mwenye kurehemu.” Juz, 1 (2:37).

Akasema (Mwenyezi Mungu): Shukeni, nyinyi kwa nyinyi ni maadui.

Maneno haya anaambiwa Adam, mkewe na Iblisi. Makusudio ya nyinyi ya kwanza ni Iblis na kabila yake, na ya pili ni Adam na kizazi chake. Sababu ya uadui huu ni kuwa Iblisi alikusudia kumpoteza mtu na kumharibu kwa kuchukua kisasi cha maafa yake.

Ama mtu hamwoni Iblisi kuweza kumpa udhia, Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

إِنَّهُ يَرَاكُمْ هُوَ وَقَبِيلُهُ مِنْ حَيْثُ لَا تَرَوْنَهُمْ َ ﴿٢٧﴾

“Hakika yeye na kabila lake anawaona, na nyinyi hamuwaoni.” (7:27)

Na akasema tena:

إِنَّ الشَّيْطَانَ لَكُمْ عَدُوٌّ فَاتَّخِذُوهُ عَدُوًّا ﴿٦﴾

“Kwa hakika Shetani ni adui yenu, basi mfanyeni adui” (35:6)

Na makao yenu na starehe yatakuwa katika ardhi kwa muda. Akasema mtaishi humo na mtafia humo na mtatolewa kutoka humo.

Hivi ndivyo alivyotuandikia Mwenyezi Mungu, baada ya kutokea yaliyotokea kwa Adam, kwamba tuishi na tufe katika ardhi hii, kisha tutolewe humu kwa ajili ya hisabu na malipo baada ya kupata taabu na mashaka.

KISA CHA ADAM KAMA KILIVYO KATIKA QUR’AN

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja kisa cha Adam, Katika Juz.1 (2:33) na Aya zinazofuatia, Juz.8. (7:18) na Aya zinazofuatia, na katika Juz.16 (20: 116) na Aya zinazofoutia.

Muhtasari wa kisa chenyewe, kama kilivyoelezwa katika Aya hizo, ni huu ufuatao:

Mwenyezi Mungu Mtukufu aliwafahamisha Malaika wake kwamba yeye ataumba viumbe katika ardhi hii, watakaotembea katika pande zake zote na kula riziki yake. Na Malaika wakamwambia: Vipi unataka kuweka katika ardhi atakayefanya ufisadi na kumwaga damu kwa kushindania matunda yake; na sisi hapa tuko, tukikuabudu wewe milele? Mwenyezi Mungu akawapa jibu la kutuliza nyoyo zao na kuwataka wamsujudie Adam alipomkamilisha kuwa mtu.

Baada ya kwisha kumuumba kutokana na mchanga na kumweka sura ya mwisho, Malaika walimuadhimisha na kumsujudia, isipokuwa Iblisi akadhihirisha uasi na akatangaza jeuri.

Mwenyezi Mungu alipomuuliza akasema: “Mimi ni bora kuliko yeye.” Mwenyezi Mungu akampa malipo ya kumfukuza na laana.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimfundisha Adam majina ya viumbe vyote, ambapo Malaika walikuwa hawayajui, Mwenyezi Mungu akaamwamuru Adam awaambie, ili kubainisha ubora wake na kudhihirishaa hekima yake Mungu, ya kumweka Adamu kuwa khalifa katika Ardhi.

Mwenyezi Mungu akamfanyia Adam mke kutokana jinsi yake, Akawakalisha kwenye Bustani (Pepo) ya neema zake, akawaruhusu kula matunda yote na akawakataza mti mmoja katika miti yake. Akawapa dhamana, kama wakifuata amri, hawatakuwa na njaa wala kiu au kuwa uchi. Kisha akawatahadharisha na Iblisi na hadaa zake.

Mlanifu Iblisi aliona uchungu yeye kuwa mwovu na kuneemeka yule aliyekuwa ni sababu ya uovu wake na kufukuuzwa kwake kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu. Akawafitini kwa kuwapambia maneno na kuwahadaa.

Walikuwa na kivazi cha kuwasitiri tupu zao, hawajioni wala hawaonani uchi, lakini walipomaliza kula tunda hilo tu, sitara iliwaondoka wakawa uchi. Ndipo wakaharakisha kujifunika kwa majani ya Peponi.

Mwenyezi Mungu, Mtukufu akawalingania huku akiwalaumu, kwa kughafilika na nasaha yake na kusahau hadhari aliyowapa juu ya Iblisi.

Hapo wakanyenyekea kwake kwa kukiri na kujuta huku wakitaka rehema na maghufira. Lakini aliwatoa kwenye neema waliyokuwa nayo na akawakalisha kwenye ardhi hii aliyowafanyia njia mbili: Uongofu na upotevu.

Na akamwahidi Pepo yule atakayefuata uongozi wake; na kumpa kiaga cha moto yule atakayepotea. Akamfahamisha Adam na kizazi chake kwamba uadui baina yao na Iblisi utaendelea mpaka siku ya mwisho na kuwatahadharisha na fitina yake.

Huu ndio muhtasari wa yaliyo katika Qur’an kuhusu kisa cha Adam na mkewe. Kuhusu kisa hiki, watu wana kauli mbili: wale wanaopinga Wahyi na wale wanaouamini. Na hawa nao wako makundi mawili: Kuna kundi lilipetuka dhahiri ya Qur’an, wakategemea ngano za Kiyahudi katika kufasiri Bustani (Pepo) ya Adam na mengineyo.

Kwamba bustani hiyo ilikuwa duniani ikiitwa Bustani ya Aden; na mti aliokula Adam na Hawa ni ngano, na wao walijisitiri na majani ya mti wa Tini; na kwamba Iblisi aliingia kwenye Bustani akiwa ndani ya nyoka na mengineyo yasiyokuwa na asili yoyote ya Hadith wala Qur’an.

Kundi jingine likakimbilia kwenye mambo yasiyohisiwa, Wakafasiri mti kuwa ni mtihani, shetani kuwa ni matamanio, uchi kuwa uchafu na mengineyo katika fahamu za kisufi.

Sisi tuko katikati, tunaamini kiujumla yale yaliyotolewa Wahyi na dhahir ya Qur’an kwamba mti, uchi na majani, yote hayo yalikuwa ni vitu hasa vya kuhisiwa. Kwa sababu ndio ufahamisho wa kihakika wa tamko, wala hakuna la kuwajibisha kuleta taawili, maadam akili inakubali maana ya dhahiri wala haikatai.

Hatuwezi kuzungumzia hakika ya Bustani ya Adam, kwamba ilikuwa hapa duniani au penginepo; wala aina ya majani aliyojisitiria Adam na Hawa, aina ya mti, wala jinsi alivyonyapa Iblisi na kujipenyeza Peponi. Kwa sababu ufafanuzi wa haya ni katika ilimu ya ghaibu wala haukuteremshiwa wahyi na akili inashindwa kufahamu.

Imepokewa kutoka kwa Imam Ahmad amesema: “Mambo matatu hayana asili: Tafsir, mapigano na vita.” Anakusudia Tafsir ya Maneno ya Mwenyezi Mungu kwa yasiyokuwa maana ya dhahiri. Kwa sababu yeye ni katika ambao wanatoa dalili kwa dhahiri hii katika msingi na matawi.

يَا بَنِي آدَمَ قَدْ أَنزَلْنَا عَلَيْكُمْ لِبَاسًا يُوَارِي سَوْآتِكُمْ وَرِيشًا وَلِبَاسُ التَّقْوَىٰ ذَٰلِكَ خَيْرٌ ذَٰلِكَ مِنْ آيَاتِ اللَّـهِ لَعَلَّهُمْ يَذَّكَّرُونَ ﴿٢٦﴾

26. Enyi wanadamu! Hakika tumewateremshia vazi lifichalo tupu zenu na vazi la pambo, Na vazi la takua ndiyo bora. Hiyo ni katika Ishara za Mwenyezi Mungu ili wapate kukumbuka.

يَا بَنِي آدَمَ لَا يَفْتِنَنَّكُمُ الشَّيْطَانُ كَمَا أَخْرَجَ أَبَوَيْكُم مِّنَ الْجَنَّةِ يَنزِعُ عَنْهُمَا لِبَاسَهُمَا لِيُرِيَهُمَا سَوْآتِهِمَا إِنَّهُ يَرَاكُمْ هُوَ وَقَبِيلُهُ مِنْ حَيْثُ لَا تَرَوْنَهُمْ إِنَّا جَعَلْنَا الشَّيَاطِينَ أَوْلِيَاءَ لِلَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ ﴿٢٧﴾

27. Enyi wanaadamu! shetani asiwatie katika fitina, kama alivyowatoa wazazi wenu katika Bustani (Pepo) akiwavua nguo zao ili kuwaonyesha tupu zao. Hakika yeye na kabila lake anawaona, na nyinyi hamuwaoni. Hakika sisi tumewajaalia mashetani kuwa watawala wa wale ambao hawaamini.

KIVAZI CHA KUONEKANA NA KISICHOONEKANA

Aya 26 – 27

MAANA

Katika Sura 6:141, Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja fadhila ya chakula aliyowapa waja wake. Na katika Aya hii tuliyo nayo anataja neema ya kivazi.

Enyi wanadamu! Hakika tumewateremshia vazi lifichalo tupu zenu na vazi la pambo.

Maneno wanaambiwa wanadamu wote, Maana ya kuwateremshia ni kuwapa. Mwenyezi Mungu amewaneemesha waja wake, katika aliyowaneemesha, aina kwa aina za kivazi; kuanzia cha hali ya chini ambacho kinasitiri uchi mpaka cha hali ya juu cha kifahari.

Na vazi la takua ndiyo bora.

Nalo ni kumuogopa Mwenyezi Mungu na kufanya amali njema. Takua imetumiwa kuwa ni vazi kwa sababu imekinga mtu na adhabu ya Mwenyezi Mungu, kama vazi linavyomkinga mtu na joto na baridi, Mwenyezi Mungu anasema “Na amewafanyia nguo za kuwakinga na joto na za kuwakinga na vita vyenu” (16: 81).

Hiyo ni katika Ishara za Mwenyezi Mungu ili wapate kukumbuka.

Yaani Mwenyezi Mungu amewapa kivazi kwa fadhila zake, ili mjue twaa yake na muache kumwasi.

Enyi wanaadamu! Shetani asiwatie katika fitina, kama alivyowatoa wazazi wenu katika Bustani (Pepo) akiwavua nguo zao ili kuwaonyesha tupu zao.

Asiwatie katika fitina; yaani msighafilike na fitina yake na hadaa yake. Kuwavua nguo zao ni kuwa yeye alikuwa ni sababu ya kuvuliwa nguo.

Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameashiria uadui wa Shetani kwa Adam na jinsi alivyomfanyia vitimbi mpaka akamtoa yeye pamoja mkewe kwenye maisha ya raha kwenda kwenye maisha ya tabu na mashaka.

Katika Aya hii Mwenyezi Mungu anawahadharisha wanaadamu wasiingie katika mtego wa Shetani na fitina yake na kuwateka kwenye maasi ili kuwazuia kuingia Peponi; kama alivyowahadaa wazazi wao, na kuwa ni sababu ya kuwa uchi na kutolewa Peponi.

Ilivyo hasa ni kwamba kuzuia kuingia Peponi ni rahisi zaidi kuliko kutoa. Kwani kumtoa mlowezi ni kuzito sana kuliko kumzuia anayetaka kulowea na kukalia ardhi ya watu. Mmoja wa watoaji waadhi anasema:

“Kosa moja tu lilimtoa Adam Peponi baada ya kuingia akiwa mtulivu, je, watoto wake wataingia vipi na hali makosa yamewajaa?”

Hakika yeye na kabila lake anawaona, na nyinyi hamuwaoni.

Shetani na majeshi yake anatuona, na sisi hatumuoni hata mmoja, kwa mujibu wa habari hizi za Wahyi, nasi tunauamini.

Hakika sisi tumewajaalia mashetani kuwa watawala wa wale ambao hawaamini.

Kifungu hiki kinaashiria jibu la swali la kukadiriwa ambalo ni: Ikiwa Shetani anatuona na sisi hatumuoni, maana yake ni kuwa yeye anatumudu na sisi hatumuwezi na kwamba yeye anaweza kutumaliza wakati wowote akitaka bila kuweza kujikinga naye. Sasa imekuwaje tukaamrishwa kujikinga naye na kutomsikiliza?

Jibu kwa ufafanuzi zaidi, ni kweli kwamba sisi hatumuoni Shetani, lakini tunahisi athari yake ambayo ni wasiwasi wake ukituambia kuwa hakuna Pepo wala moto na mfano wa hayo.

Mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho huachana na wasiwasi huu wala hauitikii; na na anijlinda na yule mwenye kumtia wasiwasi. Kwa hiyo Shetani anarudi akiwa amehizika na kupata hasara.

Ama yule anayemkufuru Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho huingiwa na wasiwasi huu na hutawaliwa na Shetani, hivyo humwongoza vile atakavyo na wakati atakao. Ama waumini hawawezi kusimamiwa na Shetani; Kwa sababu wao wamempa uongozi Mwenyezi Mungu peke yake. Hayo ndio maana ya kauli ya Mwenyezi Mungu:

اللَّـهُ وَلِيُّ الَّذِينَ آمَنُوا يُخْرِجُهُم مِّنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ وَالَّذِينَ كَفَرُوا أَوْلِيَاؤُهُمُ الطَّاغُوتُ يُخْرِجُونَهُم مِّنَ النُّورِ إِلَى الظُّلُمَاتِ ﴿٢٥٧﴾

“Mwenyezi Mungu ni mtawala wa wale walioamini, huwatoa gizani na kuwaingiza katika mwangaza,lakini waliokufuru watawala wao ni mataghuti, Huwatoa kwenye mwangaza, na kuwaingiza katika giza.” Juz.3 (2:257).

Baadhi wafasiri wamesema kuwa mashetani tusiowaona ni viini na virusi vya magonjwa vinavyobebwa na nzi na mbu kumwambukiza mwanadamu. Huzalikana humo na kukua kwa haraka na kusababisha maradhi yasiyoponyeka. Hii ni kufasiri makusudio ya Mwenyezi Mungu kwa kukisia na kubahatisha; na hiyo sio njia yetu kabisa!

10

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA NANE

وَإِذَا فَعَلُوا فَاحِشَةً قَالُوا وَجَدْنَا عَلَيْهَا آبَاءَنَا وَاللَّـهُ أَمَرَنَا بِهَا قُلْ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَأْمُرُ بِالْفَحْشَاءِ أَتَقُولُونَ عَلَى اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ ﴿٢٨﴾

28. Na wanapofanya machafu husema: Tumewakuta nayo baba zetu na Mwenyezi Mungu ametuamrisha hayo. Sema: Hakika Mwenyezi Mungu haamrishi machafu Je, mnasema juu ya Mwenyezi Mungu msiyoyajua?

قُلْ أَمَرَ رَبِّي بِالْقِسْطِ وَأَقِيمُوا وُجُوهَكُمْ عِندَ كُلِّ مَسْجِدٍ وَادْعُوهُ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ كَمَا بَدَأَكُمْ تَعُودُونَ ﴿٢٩﴾

29. Sema: Mola wangu ameamrisha uadilifu. Na elekezeni nyuso zenu katika kila msikiti, na muombeni yeye tu kwa ikhlas kama alivyowaumba kwanza ndivyo mtarudi.

فَرِيقًا هَدَىٰ وَفَرِيقًا حَقَّ عَلَيْهِمُ الضَّلَالَةُ إِنَّهُمُ اتَّخَذُوا الشَّيَاطِينَ أَوْلِيَاءَ مِن دُونِ اللَّـهِ وَيَحْسَبُونَ أَنَّهُم مُّهْتَدُونَ ﴿٣٠﴾

30. Kundi moja ameliongoa. Na kundi jingine limethibitikiwa na upotofu, Hakika wao wamefanya mashetani kuwa watawala wao badala ya Mwenyezi Mungu, Na wanadhani kwamba wao wameongoka.

WANAPOFANYA UCHAFU

Aya 28-30

MAANA

Na wanapofanya machafu.

Dhamir inawarudia wale ambao hawaamini, waliotajwa mwisho wa Aya iliyotangulia. Kundi la wafasiri wamesema kuwa makusudio ya uchafu ni walivyokuwa wakifanya Waarabu wakati wa ujahilia kutufu Al-Kaaba wakiwa uchi, wake kwa waume. Lakini ilivyo hasa ni kuwa neno hilo linaenea yote ya haramu waliyokuwa wakifanya.

Wanapokatazwa husema:

Tumewakuta nayo baba zetu na Mwenyezi Mungu ametuamrisha hayo.

Kitendo cha mababa kimekuwa ni hoja ya washirikina na wengineo; hata kwa maulamaa wengi wa kidini, lakini hawatambui. Ama madai ya washirikina kuwa Mwenyezi Mungu amewaamrisha machafu yameetole- wa dalili na Aya isemayo:

“Watasema walioshirikisha: Lau angelitaka Mwenyezi Mungu tusingelimshirikisha sisi wala baba zetu;” Mwenyezi Mungu akawarudi kwa kuwaaambia:

قُلْ هَلْ عِندَكُم مِّنْ عِلْمٍ فَتُخْرِجُوهُ لَنَا إِن تَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ وَإِنْ أَنتُمْ إِلَّا تَخْرُصُونَ ﴿١٤٨﴾

“Je, mnayo elimu mtutolee? Nyinyi hamfuati ila dhana tu, na hamsemi ila uwongo tu.” (6:148).

Na hapa Mwenyezi Mungu akawarudi kwa kusema: Sema:

Hakika Mwenyezi Mungu haamrishi machafu.

Bali “Shetani anawatisha na ufukara na anawaamrisha ubakhili”Juz.3 (2:257)

Je, mnasema juu ya Mwenyezi Mungu msiyoyajua?

Na kila anayesema, bila ya ujuzi wowote, basi ni mzushi mwongo, na ameruka patupu.

Sema: Mola wangu ameamrisha uadilifu.

Nao ni usawa na msimamo. Amesema Tabrasi: “Uadilifu ni neno linaloku- sanya kheri zote.” Maana yoyote yatakayokuwa ni kuwa kuamrisha uadilifu ni kupinga madai yao kuwa Mwenyezi Mungu amewaamrisha uovu.

Na elekezeni nyuso zenu katika kila msikiti, na muombeni yeye tu kwa ikhlas.

Makusudio ya elekezeni nyuso zenu ni kumwabudu Mwenyezi Mungu. Neno ‘Masjid’ ni mahali pa kusujudia na pia wakati wa kusujudu.

Lakini limetumika sana kwa maana ya jengo maalum la ibada (msikiti) mpaka likawa ni jina lake mahsusi. Makusudio ya kila msikiti sio misikiti yote bali ni msikiti wowote.

Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu anawaamrisha kufanya ibada kwenye msikiti, kwa kumwabudu yeye tu kwa ikhlas katika dini yenu na ibada yenu.

Kama alivyowaumba kwanza ndivyo mtarudi kwake siku ya Kiyama kwa ajili ya hisabu na malipo. Hili ni kemeo na onyo kwa yule anayekhalifu aliyoamrishwa na Mwenyezi Mungu. Miongoni mwa uadilifu, kufanya ibada na ikhlasi.

Kundi moja ameliongoa nao ni wale waliomfanya Mwenyezi Mungu ndiye mtawala wao na wakafuata amri yake na kujizuia makatazo yake, na wala wasihadaike na mambo ya shetani na ubatilifu wake.

Na kundi jingine limethibitukiwa na upotofu .

Nao katika akhera wana adhabu kubwa, Hilo ni kuwa Hakika wao wamefanya mashetani kuwa watawala wao badala ya Mwenyezi Mungu, Na anayemfanya shetani kuwa msimamizi badala ya Mwenyezi Mungu basi amepata hasara kubwa.

Na wanadhani kwamba wao wameongoka katika kufanya machafu, kuwafuata mababa na kumzulia Mwenyezi Mungu uwongo. Mwenyezi Mungu anasema:

قُلْ هَلْ نُنَبِّئُكُم بِالْأَخْسَرِينَ أَعْمَالًا ﴿١٠٣﴾ الَّذِينَ ضَلَّ سَعْيُهُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَهُمْ يَحْسَبُونَ أَنَّهُمْ يُحْسِنُونَ صُنْعًا ﴿١٠٤﴾

Sema: Je, tuwaambie wenye hasara zaidi kwa vitendo, ni ambao bidii yao imepotea katika maisha ya dunia, nao wanafikiri kuwa wanafanya vyema.” (18: 103-104).

يَا بَنِي آدَمَ خُذُوا زِينَتَكُمْ عِندَ كُلِّ مَسْجِدٍ وَكُلُوا وَاشْرَبُوا وَلَا تُسْرِفُوا إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُسْرِفِينَ ﴿٣١﴾

31. Enyi Wanadamu! Chukueni mapambo yenu katika kila msikiti, na kuleni na kunyweni wala msifanye ufujaji (israf), hakika Yeye hawapendi wafanyao ufujaji (israf).

قُلْ مَنْ حَرَّمَ زِينَةَ اللَّـهِ الَّتِي أَخْرَجَ لِعِبَادِهِ وَالطَّيِّبَاتِ مِنَ الرِّزْقِ قُلْ هِيَ لِلَّذِينَ آمَنُوا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا خَالِصَةً يَوْمَ الْقِيَامَةِ كَذَٰلِكَ نُفَصِّلُ الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَعْلَمُونَ ﴿٣٢﴾

32. Sema: Ni nani aliyeharamisha pambo la Mwenyezi Mungu ambalo amewatolea waja wake, na vilivyo vizuri katika riziki? Sema: Hivyo ni kwa wale walioamini katika maisha ya dunia, ni vyao tu siku ya Kiyama. Namna hii tunazieleza ishara kwa watu wajuao.

قُلْ إِنَّمَا حَرَّمَ رَبِّيَ الْفَوَاحِشَ مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَمَا بَطَنَ وَالْإِثْمَ وَالْبَغْيَ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَأَن تُشْرِكُوا بِاللَّـهِ مَا لَمْ يُنَزِّلْ بِهِ سُلْطَانًا وَأَن تَقُولُوا عَلَى اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ ﴿٣٣﴾

33. Hakika Mola wangu ameharamisha mambo machafu yaliyodhihirika na yaliyofichika. Na dhambi,na dhulma bila ya haki. Na kumshirikisha Mwenyezi Mungu na ambacho hakukiteremshia dalili, Na kusema juu ya Mwenyezi Mungu msiyoyajua.

لِكُلِّ أُمَّةٍ أَجَلٌ فَإِذَا جَاءَ أَجَلُهُمْ لَا يَسْتَأْخِرُونَ سَاعَةً وَلَا يَسْتَقْدِمُونَ ﴿٣٤﴾

34. Kila umma una muda, utakapofika muda wao hawatakawia (hata) saa moja wala hawatatangulia.

CHUKUENI MAPAMBO YENU

Aya 31-34

MAANA

Enyi Wanadamu! Chukueni mapambo yenu katika kila msikiti

Wafasiri wanasema watu wa wakati wa ujahiliya walikuwa wakitufu Al- Kaaba wakiwa uchi, wake kwa waume: Na walikuwa hawali mafuta wakati wa Hijja; wala hawali chakula ila kiasi tu cha kuzuia tumbo, kwa ajili ya kuadhimisha Hijja, ndipo ikashuka Aya hii.

Na kwamba Mtume(s.a.w.w) alisema: “Baada ya mwaka huu pasihijiwe na mshirikina yeyote wala Al-kaaba haitazungukwa uchi”, basi kauli yake hiyo ikatangazwa kwenye msimu. Miongoni mwa visa vinavavyoingia katika maudhui haya ni kile cha mwanamke mmoja mzuri wa Kiarabu aliyevua nguo na kuweka mkono kwenye tupu yake na akatufu. Macho ya watu yalipompata sana alitunga shairi hili:

Kuona yote au sehemu sihalali kitachoonekana

Kivuli kikubwa adhimu hata akali hamtavuna

Hata mwenye fahamu naye pia hudangana

Akimaanisha kuwa tupu yake ni adhimu pale ilipo, ina haiba na hifadhi, wala hakuna yeyote anayeweza kuifikia; na kwamba yeye anamkemea na kumchukiua anayemwangalia.

Kwa vyovyote itakayokuwa sababu ya kushuka Aya ni kwamba Mwenyezi Mungu ameharamisha kwa mtu kando kuangalia uchi wa mwingine awe mwanamume au mwanamke.

Na amewajibisha kusitiri tupu mbili katika Swala na tawafu.

Makusudio ya kila msikiti ni kama yale tuliyoyaeleza katika Aya iliyotangulia. Maana ni kuhimiza usafi na utwahara kutokana na uchafu na hadath na vilevile kujipamba nguo nzuri katika Swala ya Ijumaa, ya Jamaa, ya Idd au kutufu, ambapo sehemu hizo wanakusanyika watu, ili watu wasimkimbie kwa harufu yake mbaya na mandhari yake. Kujipamba ni vizuri, hata kwa fukara pia ajipambe kwa kiasi cha hali yake. Kuna Hadith isemayo: “Hakika Mwenyezi Mungu ni mzuri na hupenda uzuri.”

Na kuleni na kunyweni.

Hii ni kupinga mwenye kuharamisha baadhi ya vyakula na vinywaji.

Wala msifanye ufujaji (israf) katika kula na kunywa na katika kujipamba kwa mavazi.

Hakika yeye hawapendi wafanyao ufujaji (israf)

Katika Aya nyingine anasema Mwenyezi Mungu:

﴿ إِنَّ الْمُبَذِّرِينَ كَانُوا إِخْوَانَ الشَّيَاطِينِ ﴾

“Hakika wabadhirifu ni ndugu wa mashetani” (17:27)

Na kuna Hadith isemayo: “Tumbo ni nyumba ya kila ugonjwa, na kula kwa makadirio ni msingi wa kila dawa, na uzoesheni kila mwili vile ulivyozoea.” Na Ali Al-Murtadha(a.s) anasema: “Ni mara ngapi tonge moja imezuia matonge mengi?”

Sema: Ni nani aliyeharamisha pambo la Mwenyezi Mungu ambalo amewatolea waja wake, na vilivyo vizuri katika riziki?

Dhahiri ya maneno ni swali na maana yake ni kukana sana uharamu wa kujipamba na vilivyo vizuri katika riziki. Na kwamba ni katika wasiwasi wa Shetani na si katika Wahyi wa Mwenyezi Mungu.

Kutegemeza neno mapambo kwa Mwenyezi Mungu kunafahamisha uhalali, na neno vitu vizuri linajifahamisha hilo lenyewe. Kwa sababu kila lililo haramu ni baya na wala si zuri.

Neno pambo linakusanya aina zake zote, ikiwa na pamoja na nyumba, na neno vitu vizuri linakusanya vyakula, vinywaji, kustarehe kwa mambo mazuri na wanawake, sauti nzuri, mandhari nzuri na kila starehe iliyo nzuri ambayo, sharia haikukataza.

Maulamaa wa Kiislam wameafikiana kwa kauli moja kwamba kila kitu ni halali mpaka uje ukatazo. Wakatoa dalili kwa hukumu ya akili, kwamba hakuna adhabu bila ya ubainifu, na kwa kauli ya Mtume Mtukufu(s.a.w.w) :

“Watu wako katika wasaa wa wasiyoyajua.” na kauli yake: “Yale ambayo Mwenyezi Mungu amewafunikia waja kuyajua basi yameondolewa kwao.” Amesema tena: “Kila kitu kimeachiwa mpaka uje ukatazo kwenye kitu hicho.”

Sema: Hivyo ni kwa wale walioamini katika maisha ya dunia, ni vyao tu siku ya Kiyama.

Yaani katika maisha haya ya dunia wataneemeka wote waumini na makafiri, lakini kesho watakaoneemeka kwa mapambo ya Mwenyezi Mungu na vitu vizuri katika riziki, ni wale walioamini tu, peke yao bila ya kushirikiana na wale waliokufuru na kumshirikisha Mwenyezi Mungu.

Namna hii tunazieleza ishara kwa watu wajuao.

Mwenye kuifuatilia Qur’an ataona kuwa Mwenyezi Mungu anatumia neno Wajuzi (Ulama) kwa yule anayejua hukumu za Mwenyezi Mungu na akazitumia. Vilevile hulitumia kwa yule anayetarajiwa kuzijua na kuzitumia akifafanuliwa.

Kwa hiyo, makusudio ya watu wanaojua hapa ni aina ya pili ambao wanan- ufaika na ubainifu wa hukumu ya mapambo na vitu vizuri na vinginevyo na wanaowarejea maulama wa dini katika kujua hukumu za Mwenyezi Mungu (s.w.t) na kutoa dalili kwa Aya za Mwenyezi Mungu kwa halali yake na haramu yake.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kumkana anayeharamisha mapambo na vitu vizuri, sasa anabainisha misingi ya vilivyo haramu kama ifuatavyo:

Sema: Hakika Mola wangu ameharamisha mambo machafu, yaliyodhihirika na yaliyofichika.

Umetangulia ubainifu wake katika kufasiri Sura 6:151 kifungu cha wasia.

Na dhambi ni kila jambo ambalo anaasiwa kwalo Mwenyezi Mungu, iwe kauli au kitendo. Kuunganisha machafu kwenye dhambi ni katika hali ya kuunganisha mahsus kwenye ujumla; kama ilivyo katika kauli yake Mwenyezi Mungu:

﴿ كَمَا أَوْحَيْنَا إِلَىٰ نُوحٍ وَالنَّبِيِّينَ ﴾

“Kama tulivyompa Wahyi Nuh (a.s) na Mitume…” (4:163).

Na dhulma bila ya haki.

Kuna hadith inayosema “Lau jabali lingedhulu- mu jabali jingine, basi Mwenyezi Mungu angelifanya lile lililodhulumu lipondekepondeke” Na Amirul-Muminin anasema: “Mwenye kuchomoa upanga wa dhuluma atauwawa nao.”

Na kumshirikisha Mwenyezi Mungu na ambacho hakukiteremshia dalili.

Hakuna dhambi nyingine baada ya ukafiri na shirk. Shirk ni kinyume cha Tawhid ambayo muhtasari wake ni:

﴿ لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ﴾

“Hakuna chochote kama mfano wake” (42:11).

Umetangulia ufafanuzi katika kufasiri Sura 6:153, kifungu cha ‘Wasia kumi.’

Na kusema juu ya Mwenyezi Mungu msiyoyajua.

Miongoni mwa hayo ni yale yaliyoashiriwa katika Aya 28 ya Sura hii:“Na wanapofanya machafu husema tumewakuta nayo baba zetu na Mwenyezi Mungu ametuamrisha .” Hakuna uchafu mbaya kama kusema bila ya kujua; na hakuna tofauti katika hukumu baina ya kumzulia Mungu na kumshirikisha. Imam Ali amesema: “Mwenye kuliacha neno ‘sijui’ atakuwa hana salama.”

Kila umma una muda makusudio ya umma hapa ni kundi, kama lilivyotumika neno hilo katika Aya isemayo:

﴿ وَلَمَّا وَرَدَ مَاءَ مَدْيَنَ وَجَدَ عَلَيْهِ أُمَّةً مِنَ النَّاسِ يَسْقُونَ ﴾

“Alipofikia maji ya Madian alikuta umma wa watu wakinywesha.” (28:23)

Baada ya Mwenyezi Mungu kutaja uovu wa washirikina katika Aya 28; na yale aliyohalalisha katika Aya 31: na aliyoyaharamisha katika Aya 33. Baada ya haya yote anasema kila kundi, ikiwa ni pamoja na washirikina waliomzulia Mwenyezi Mungu, lina muda maalum katika maisha haya; kisha watarudishwa kwa Mwenyezi Mungu waambiwe yale waliyokuwa wakiyafanya.

Katika haya mna makemeo na kiaga kwa washirikina na wenye kufanya uovu na watu wa dhulma na kila anayesema juu ya Mwenyezi Mungu bila ya ujuzi.

Utakapofika muda wao, hawatakawia (hata) saa moja wala hawatatangulia.

Imepita tafsir yake katika kufasiri Juz. 4 (3:145).

﴿ يَا بَنِي آدَمَ إِمَّا يَأْتِيَنَّكُمْ رُسُلٌ مِنْكُمْ يَقُصُّونَ عَلَيْكُمْ آيَاتِي فَمَنِ اتَّقَىٰ وَأَصْلَحَ فَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ ﴾

Enyi: Wanadamu! Watakapowafikia Mitume kutoka miongoni mwenu, wakawaeleza ishara zangu, basi watakaoogopa na kufanya mema, haitakuwa hofu juu yao wala hawatahuzunika.

﴿ وَالَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَاسْتَكْبَرُوا عَنْهَا أُولَٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴾

Na wale watakaokadhibisha ishara zetu na kuzifanyia kiburi, hao ndio watu wa motoni, watadumu humo.