12
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA NANE
وَبَيْنَهُمَا حِجَابٌ وَعَلَى الْأَعْرَافِ رِجَالٌ يَعْرِفُونَ كُلًّا بِسِيمَاهُمْ وَنَادَوْا أَصْحَابَ الْجَنَّةِ أَن سَلَامٌ عَلَيْكُمْ لَمْ يَدْخُلُوهَا وَهُمْ يَطْمَعُونَ ﴿٤٦﴾
46. Na Baina Yao Patakuwa Na Pazia, Na Juu Ya A’raf Watakuwako Watu Watakaowafahamu Wote Kwa Alama Zao, Na Watanadia Watu Wa Peponi: Salamun Alaykum. Hawajaingia Nao Wanatumai.
وَإِذَا صُرِفَتْ أَبْصَارُهُمْ تِلْقَاءَ أَصْحَابِ النَّارِ قَالُوا رَبَّنَا لَا تَجْعَلْنَا مَعَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴿٤٧﴾
47. Na Macho Yao Yanapogeuzwa Kuelekea Watu Wa Motoni, Husema: Mola Wetu Usituweke Pamoja Na Watu Waliodhulumu.
وَنَادَىٰ أَصْحَابُ الْأَعْرَافِ رِجَالًا يَعْرِفُونَهُم بِسِيمَاهُمْ قَالُوا مَا أَغْنَىٰ عَنكُمْ جَمْعُكُمْ وَمَا كُنتُمْ تَسْتَكْبِرُونَ ﴿٤٨﴾
48. Na Watu Wa A’raf Watawanadia Watu Wanaowafahamu Kwa Alama Zao, Waseme: Haukuwasaidia Mjumuiko Wenu Wala Mlivyokuwa Mkijivunia.
أَهَـٰؤُلَاءِ الَّذِينَ أَقْسَمْتُمْ لَا يَنَالُهُمُ اللَّـهُ بِرَحْمَةٍ ادْخُلُوا الْجَنَّةَ لَا خَوْفٌ عَلَيْكُمْ وَلَا أَنتُمْ تَحْزَنُونَ ﴿٤٩﴾
49. Je, Hawa Ndio Wale Mliokuwa Mkiwaapia Kwamba Mwenyezi Mungu Hatawafikishia Rehma? Ingieni Peponi, Hakuna Hofu Juu Yenu Wala Hamtahuzunika.
WATU WA A’RAF
Aya 46 – 49
A’RAF
Sisi tunaamini siku ya Kiyama, hisabu na malipo, kwa ujumla, ikiwa ni msingi katika misingi ya dini. Ama ufafanuzi na mafungu yake, hayo ni katika elimu ya ghaibu. Wala hakithibiti kitu chochote katika ulimwengu huo ila kwa Aya iliyo wazi au kwa Hadith wazi iliyothibiti kutoka kwa Ma’sum kwa khabar Mutawatir, na wala sio habari Ahad. Kwa sababu Habari Ahad ni hoja katika matawi tu, si katika misingi.
Khabar Mutawatir ni ile ambayo wanaipokea watu wengi bila ya kutokea mgongano wa uwongo. Kinyume chake ni Khabar Ahad.
Imethibiti kutokana na Wahyi kwamba huko Akhera kutakuwa na mahali, baina ya Pepo na moto, panaitwa A’raf. Hapo si mahali pa Pepo wala moto, lakini kwa undani ni rehema inayofuata Pepo; na kwa dhahiri ni adhabu inayofuatia Moto. Mwenyezi Mungu anasema:
فَضُرِبَ بَيْنَهُم بِسُورٍ لَّهُ بَابٌ بَاطِنُهُ فِيهِ الرَّحْمَةُ وَظَاهِرُهُ مِن قِبَلِهِ الْعَذَابُ ﴿١٣﴾
“… utiwe baina yao ukuta wenye mlango; ndani yake mna rehema na nje kwa upande wake wa mbele kuna adhabu.”
(57:13).
Katika mahali hapo paitwapo A’raf kutakuwa na watu wanaowajua watu wote wa Peponi na wa Motoni. Hawawajui kwa majina au hali yao; bali wanawajua kwa alama zinazowatofautisha.
Wao watawaangalia wa Peponi na kuwasalimia wakitumai kuwa pamoja nao wakati fulani. Na jicho lao likiwaangukia watu wa motoni tu, humwomba Mwenyezi Mungu asiwajaalie kuwa pamoja na watu madhalimu walioangamia. Kisha mwisho wa mambo watu wa A’raf wataingia Peponi. Kwa sababu wao ni katika watu wa Lailaha illa Ilah na Mwenyezi Mungu ana usaidizi maalum kwa watu wa aina hiyo.
Hayo ndiyo ujumla wa yaliyoelezwa na Qur’an kuhusu A’raf na watu wake, lakini Wafasiri wengi wamepetuka mpaka katika ufafanuzi huu, sasa tunaingilia kufasiri yanayofahamishwa na Aya:
Na baina yao patakuwa na pazia.
Yaani baina ya Pepo na Moto au baina ya watu wa sehemu hizo mbili. Pazia ni hiyo A’raf iliyoashiriwa na kauli yake Mwenyezi Mungu:
Na juu ya A’raf watakuwako watu watakaowafahamu wote kwa alama zao.
Yaani watu wa A’raf watawajua wote watu wa Peponi, na watu wa motoni kwa alama zitakazowatambulisha sio mbali kuwa alama hizi ni zile zilizoashiriwa na Aya isemayo:
يَوْمَ تَبْيَضُّ وُجُوهٌ وَتَسْوَدُّ وُجُوهٌ ﴿١٠٦﴾
“Siku ambayo nyuso zitang’aa na nyuso (nyingine) zitasawijika.”
(3:106).
Na pia Aya isemayo:
وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ مُّسْفِرَةٌ ﴿٣٨﴾ ضَاحِكَةٌ مُّسْتَبْشِرَةٌ ﴿٣٩﴾ وَوُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ عَلَيْهَا غَبَرَةٌ ﴿٤٠﴾ تَرْهَقُهَا قَتَرَةٌ ﴿٤١﴾ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْكَفَرَةُ الْفَجَرَةُ ﴿٤٢﴾
“Nyuso siku hiyo zitanawiri. Zitacheka na kufurahika. Na nyuso nyingine siku hiyo zitakuwa na mavumbi. Zimefunikwa na weusi weusi, Hao ndio makafiri, watendao maovu”
(80:38-42)
Imesemekana kuwa alama hizo ni za ujumla watazijua watu wote; na dhahiri ya Aya inafahamisha kuwa alama hizo watazijua watu wa A’raf tu.
Kwa vyovyote itakavyokuwa, mambo ni mepesi sana hakuna taabu, maadamu sisi si wenye kukalifiwa wala hatutaulizwa kuhusu alama hizo zitakavyokuwa na hakika yake au sifa zake maalum au za ujumla.
Utauliza
: Ni nani hao watu wa A’raf?
Jibu
: Wafasiri wana kauli nyingi, yenye nguvu ni ile waliyoielezea wengi kwamba wao ni wale ambao uzani wao umekuwa sawa sawa; si mema yao yatakayozidi wala maovu yao. Lau mojawapo lingezidi jingine kwa uzani wa tonoradi, basi mwisho wao ungelijulikana, kuwa aidha Peponi au motoni.
Swali la pili
: watu wa Peponi watajulikana kwa kuingia humo; vilevile watu wa Motoni, Sasa kuna haja gani ya alama?
Jibu
: Huenda ikawa alama hizo ni za kupambanua baina ya makundi mawili kabla ya hisabu na adhabu; kama ambavyo mhalifu anavyotambulika kutokana na hali ya uso wake unavyokuwa anapopelekwa mahakamani.
Na watanadia watu wa Peponi: Salamun Alaykum.
Dhamir ya Watanadi ni ya watu wa A’raf. Maana ni kuwa wao watakapowaangalia watu wa Peponi watawasalimia kwa maamkuzi ya heshima.
Hawajaingia nao wanatumai
kuingia Peponi, Kwa sababu wao ni katika watu wa Lailaha illa llah. Na kila anayemwamini Mwenyezi Mungu anatumaini rehema yake na maghufira yake. Mwenyezi Mungu anasema:
إِنَّهُ لَا يَيْأَسُ مِن رَّوْحِ اللَّـهِ إِلَّا الْقَوْمُ الْكَافِرُونَ ﴿٨٧﴾
“Hakika hawakati tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu isipokuwa watu makafiri.”
(12:87).
Kuna Hadith isemayo kuwa mtu mmoja alisema: “Wallahi Mwenyezi Mungu hatamsamehe fulani.” Mwenyezi Mungu akasema: “Ni nani huyu anayeniapia mimi kuwa nisimsamehe fulani?” Hakika mimi nimekwisha msamehe fulani na nimezishusha amali za mwenye kuapa.”
Na macho yao yanapogeuzwa kuelekea watu wa Motoni, husema: Mola wetu usituweke pamoja na watu waliodhulumu.
Neno ‘Yanapogeuzwa’ linafahamisha kuwa kuangalia kwa watu wa A’raf kwa watu wa motoni si kwa kukusudia.
Makusudio ya dhulma hapa ni ushirikina na kufru. Maana ni kuwa wao wakisadifu kuyaona ya watu wa Motoni huogopa na kunyenyekea kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu asiwajaalie kuwa pamoja na watu makafiri walioangamia.
Na watu wa A’raf watawanadia watu wanaowafahamu kwa alama zao, waseme: Haukuwasaidia mjumuiko wenu wala mlivyokuwa mkijivuna.
Wale waliokuwa wakijivuna katika ardhi walikuwa wakiwadharau waumini na wakijitukuza kwa yale waliyokuwa wakimiliki miongoni mwa mali na jaha; na wakiwaambia: Hamtapata kamwe rehema ya Mwenyezi Mungu, lakini kitakapofika kiyama na waovu kulipwa matendo yao, basi watu wa A’raf watawakumbusha mambo mawili:
Kwanza
: yale waliyokuwa wakiyakusanya na kujivunia nayo, mali na kadhalika. Hayo yanaashiriwa na kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Haukuwasaidia mjumiko wenu wala mlivyokuwa mkijivunia.’
Pili
: Yale waliyokuwa wakiwaambia waumini kuwa hamtaingia Peponi. Hayo yameashiriwa na kauli yake Mwenyezi Mungu:
Je,hawa ndio wale mliokuwa mkiwaapia kwamba Mwenyezi Mungu hatawafikishia rehma?
Kwa hiyo neno ‘Hawa’ ni waumini wadhaifu na neno mkiwaapia wanaam- biwa wajivuni.
Ingieni Peponi, hakuna hofu juu yenu wala hamtahuzunika.
Yaani waumini walioambiwa na wajivuni kuwa hawataingia Peponi, ndio sasa wanaambiwa ingieni Peponi.
وَنَادَىٰ أَصْحَابُ النَّارِ أَصْحَابَ الْجَنَّةِ أَنْ أَفِيضُوا عَلَيْنَا مِنَ الْمَاءِ أَوْ مِمَّا رَزَقَكُمُ اللَّـهُ قَالُوا إِنَّ اللَّـهَ حَرَّمَهُمَا عَلَى الْكَافِرِينَ ﴿٥٠﴾
50. Watu wa Motoni watawanadia watu wa Peponi: Tumiminieni maji au katika vile alivyowapa Mwenyezi Mungu. Watasema: Hakika Mwenyezi Mungu ameyaharamisha vyote viwili hivyo kwa makafiri.
الَّذِينَ اتَّخَذُوا دِينَهُمْ لَهْوًا وَلَعِبًا وَغَرَّتْهُمُ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا فَالْيَوْمَ نَنسَاهُمْ كَمَا نَسُوا لِقَاءَ يَوْمِهِمْ هَـٰذَا وَمَا كَانُوا بِآيَاتِنَا يَجْحَدُونَ ﴿٥١﴾
51. Ambao waliifanya dini yao kuwa upuuzi na mchezo na yakawahadaa maisha ya dunia. Basi leo sisi tunawasahau kama walivyosahau kukutana na siku yao hii na kwa sababu walikuwa wakizikataa ishara zetu.
وَلَقَدْ جِئْنَاهُم بِكِتَابٍ فَصَّلْنَاهُ عَلَىٰ عِلْمٍ هُدًى وَرَحْمَةً لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ ﴿٥٢﴾
52. Na hakika tumewaletea Kitab tulichokipambanua kwa ujuzi, ambacho ni mwongozo na rehema kwa watu wanaoamini.
هَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا تَأْوِيلَهُ يَوْمَ يَأْتِي تَأْوِيلُهُ يَقُولُ الَّذِينَ نَسُوهُ مِن قَبْلُ قَدْ جَاءَتْ رُسُلُ رَبِّنَا بِالْحَقِّ فَهَل لَّنَا مِن شُفَعَاءَ فَيَشْفَعُوا لَنَا أَوْ نُرَدُّ فَنَعْمَلَ غَيْرَ الَّذِي كُنَّا نَعْمَلُ قَدْ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ وَضَلَّ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَفْتَرُونَ ﴿٥٣﴾
53. Hawangojei ila matokeo yake siku yatakapotokea matokeo yake, watasema wale walioisahau hapo zamani: Hakika Mitume wa Mola wetu walileta haki, Je, tunao waombezi watuombee. Au turudishwe ili tufanye yasiyokuwa yale tuliyokuwa tukiyafanya? Hakika wamejitia hasarani nafsi zao na yamewapotea waliyokuwa wakiyazua.
WATU WA PEPONI NA WA MOTONI
Aya 50 – 53
MAANA
Imeelezwa katika Hadith kwamba furaha ya watu wa Peponi kwa kuokoka na Moto itawazidishia neema na kwamba masikitiko ya watu wa Motoni kwa kukosa neema yatawazidisha adhabu; nao watajua kuwa watu wa Peponi wako kwenye neema. Ndio maana:
watu wa Motoni watawanadia watu wa Peponi: Tumiminieni maji au katika vile alivyowapa Mwenyezi Mungu.
Nao watu wa Peponi watawajibu:
Hakika Mwenyezi Mungu ameyaharamisha vyote viwili hivyo kwa makafiri.
Baada kukata tamaa na watu wa Peponi, watataka waokolewe na walinzi wa Motoni; kama anavyosema Mwenyezi Mungu:
وَقَالَ الَّذِينَ فِي النَّارِ لِخَزَنَةِ جَهَنَّمَ ادْعُوا رَبَّكُمْ يُخَفِّفْ عَنَّا يَوْمًا مِّنَ الْعَذَابِ ﴿٤٩﴾ قَالُوا أَوَلَمْ تَكُ تَأْتِيكُمْ رُسُلُكُم بِالْبَيِّنَاتِ قَالُوا بَلَىٰ قَالُوا فَادْعُوا وَمَا دُعَاءُ الْكَافِرِينَ إِلَّا فِي ضَلَالٍ ﴿٥٠﴾
Na wale waliomo Motoni watawaambia walinzi wa Jahanamu: “Muombeni Mola Wenu atupunguzie siku moja ya adhabu.” Na (walinzi) watasema: “Je, hawakuwawajia Mitume wenu kwa hoja zilizo wazi? Waseme: Kwa nini? Watasema: Basi ombeni, na dua ya makafiri haiwi ila ni ya kupotea bure.”
(40: 49-50).
Baada ya kukata tamaa na walinzi watataka kujiokoa kwa Mwenyezi Mungu Mola wa ulimwengu, jambo ambalo lilikuwa rahisi wakati wa raha.
قَالُوا رَبَّنَا غَلَبَتْ عَلَيْنَا شِقْوَتُنَا وَكُنَّا قَوْمًا ضَالِّينَ ﴿١٠٦﴾ رَبَّنَا أَخْرِجْنَا مِنْهَا فَإِنْ عُدْنَا فَإِنَّا ظَالِمُونَ ﴿١٠٧﴾ قَالَ اخْسَئُوا فِيهَا وَلَا تُكَلِّمُونِ ﴿١٠٨﴾
Watasema: “Mola wetu tulizidiwa na ubaya wetu na tukawa watu wenye kupotea. Mola wetu, tutuoe humu na tukirudia tena hakika tutakuwa wenye kudhulumu. Na (Mwenyezi Mungu) atasema: Hizikieni humo wala msinisemeshe.”
(23: 106 - 108).
Ambao waliifanya dini yao kuwa upuuzi na mchezo na yakawahadaa maisha ya dunia.
Imepita tafsir yake katika Juz.7 (6: 70).
Basi leo sisi tunawasahau kama walivyosahau kukutana na siku yao hii na kwa sababu walikuwa wakizikataa ishara zetu.
Makusudio ya kusahau hapa ni kupuuza, kwani:
وَمَا كَانَ رَبُّكَ نَسِيًّا ﴿٦٤﴾
“Mola wako si Mwenye kusahau”
(19: 64)
Na hakika tumewaletea Kitab tulichokipambanua kwa ujuzi, ambacho ni mwongozo na rehema kwa watu wanaoamini.
Katika Aya zilizotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja watu wa Peponi, wa Motoni na wa A’raf Na Aya hii na inayofuatia zinahusika na watu wa motoni tu, ambao wameghurika na maisha ya dunia.
Mwenyezi Mungu anasema kuwa tumewaletea hawa Qur’an inayoongoza kwenye uongofu na inayobainisha kwa ujuzi yake wanayoyahitajia watu katika maisha yao na marejeo yao na imemdhaminia – yule anayeamini na akayatumia mafunzo yake – uongofu wa kheri katika dunia na rehema ya Mwenyezi Mungu na thawabu katika Akhera. Ama mwenye kuachana nayo akafuata matamanio yake, basi marejeo yake ni Jahanamu.
Hawangojei ila matokeo yake.
Dhamir ya ‘yake’ inarudia Kitab; yaani kila linalotamkwa na Qur’an litatokea tu hapana budi.
Siku yatakapofika matokeo yake.
Kwa kutokea yale iliyoyatolea habari na uwabainikie makafiri kwa macho ukweli wake.
Watasema wale walioisahau hapo zamani: Hakika Mitume wa Mola wetu walileta haki.
Watayasema haya baada ya kuona adhabu, Na kabla yake waliwaambia Mitume kuwa ni wachawi na wazushi. Vilevile wataendelea kusema baada ya kuona adhabu:
Je, tunao waombezi watuombee
kwa Mwenyezi Mungu atusamehe makosa yetu na asitufanyie hizaya na adhabu kama tunayvostahiki?
Au turudishwe ili tufanye yasiyokuwa yale tuliyokuwa tukiyafanya?
Lau Mwenyezi Mungu ataitikia maombi yao haya, misimamo yote ingelibatilika, na mwovu, ambaye haamini mpaka awekewe upanga kichwani mwake, asingekuwa ana tofuati na mwema ambaye anaamini haki bila kulazimishwa na kujitolea mhanga katika njia ya haki kwa pumzi zake zote.
Hakika wamejitia hasarani na yamewapotea waliyokuwa wakiyazua.
Hivi ndivyo zinavyokwenda bure amali za wabatilifu na hupotelewa na waombezi na wasimamizi waliokuwa wakiwafanyia amali.
13
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA NANE
إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ يُغْشِي اللَّيْلَ النَّهَارَ يَطْلُبُهُ حَثِيثًا وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ وَالنُّجُومَ مُسَخَّرَاتٍ بِأَمْرِهِ أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ تَبَارَكَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ ﴿٥٤﴾
54. Hakika Mola wenu ni Mwenyezi Mungu aliyeziumba mbingu na ardhi katika siku sita, Kisha akatawala juu ya Arshi. Huufunika usiku kwa mchana, ufuatiao upesi upesi, Na jua na mwezi na nyota zinatumika kwa amri yake. Fahamuni! Kuumba na amri ni yake. Ametukuka Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu wote.
ادْعُوا رَبَّكُمْ تَضَرُّعًا وَخُفْيَةً إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُعْتَدِينَ ﴿٥٥﴾
55. Mwombieni Mola wenu kwa unyenyekevu na kwa uficho, Hakika yeye hawapendi wapetukao mipaka.
وَلَا تُفْسِدُوا فِي الْأَرْضِ بَعْدَ إِصْلَاحِهَا وَادْعُوهُ خَوْفًا وَطَمَعًا إِنَّ رَحْمَتَ اللَّـهِ قَرِيبٌ مِّنَ الْمُحْسِنِينَ ﴿٥٦﴾
57. Wala msifanye ufisadi katika ardhi baada ya kutengenea kwake. Na mwombeni kwa kuogopa na kwa kutumai. Hakika rehema ya Mwenyezi Mungu iko karibu na wanaofanya mema.
KATIKA SIKU SITA
Aya 54 – 56
MAANA
Hakika Mola wenu ni Mwenyezi Mungu aliyeziumba mbingu na ardhi katika siku sita.
Wafasiri wana kauli zenye kugongana katika Aya hii, Sababu yake ni mambo mawili:
Kwanza
: kwamba vitendo vya Mwenyezi Mungu havipimwi kwa wakati. Mwenyezi Mungu anasema:“Na amri yetu haikuwa ila ni moja tu kama kupepesa jicho.”
(54:50).
Yaani neno moja tu, “Kuwa, ikawa”
Pili
: kwamba wakati unahisabiwa baada ya kumbwa mbingu na ardhi na matukio yanayotokea ndani yake. Kwa hiyo kabla ya ulimwengu hakukuwa na wakati wala siku.
Sasa Je, hiyo si ni sawa na kusema: Nimejenga nyumba kutokana na paa?
Kwa hiyo basi hakuna budi kuleta taawili ya siku kwa maana inayokubalika na inayoingia akilini, Wametofautiana katika kuainisha maana hayo ya majazi, Kuna waliosema kuwa kuna maneno yaliyokadiriwa; yaani katika kipimo cha siku sita.
Wengine wakasema kuwa siku hapo ni fumbo la awamu, na kwamba Mwenyezi Mungu hakuumba huu ulimwengu kwa mkupuo mmoja bali ni kwa awamu sita ili kila kitu kiwe na kiwango na wakati wenye kukadiriwa.
Pia wako waliosema kwamba siku ni fumbo la vipindi na mabadiliko; kwamba yeye Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakuumba ulimwengu mwanzo kama ulivyo sasa, bali uligeuka umbo mpaka umbo jingine, sawa na nad- haria ya kukua mpaka kufikia umbo la sita na la mwisho, ambalo tunaliona hivi sasa.
Njia zote hizi ni za kufikiri, wala hatuna cha kutuwezesha kuipendekeza zaidi kauli mojawapo; ingawaje tumefuatilia tafsir za zamani na za sasa.
Kwa hiyo tunasema pamoja na yule anayesema: “Siku inawezekana kuwa ni awamu sita; au mambo sita; au siku sita katika siku za Mwenyezi Mungu ambazo hazipimwi kwa kiasi cha kipimo cha wakati wetu. Na inawezekana kuwa ni kitu kingine.
Hivyo basi, haifai kukata kabisa maana yoyote ya idadi hii, Na dhana ni jaribio la suluhu na kushindwa mbele ya kile kinachoitwa elimu – nayo si zaidi ya kudhani na kukadiria.”
Kisha akatawala juu ya Arshi.
Jumla hii inafasiriwa na ile inayofuatia -Fahamuni Kuumba na amri ni yake.
Yaani yeye anamilki dunia na kupanga mambo yake. Mfano wake ni Aya isemayo:
إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ﴿٣﴾
Hakika Mola wenu ni Mwenyezi Mungu aliyeziumba mbingu na ardhi katika siku sita, kisha akatawala juu arshi anapangilia (kila) jambo…”
(10:3).
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amekuita kumiliki kwake na kupanga kwake mambo, kuwa ni kutawala juu ya kiti cha enzi (arshi). Kwa sababu mfalme hutawala mambo na kuyaendesha akiwa yuko kwenye kiti chake cha enzi (arshi).
Makusudio ya kusema hivyo ni kukurubisha maana, na sio tashbihi, (ukamfananisha Mungu na Mfalme wa duniani). Amesema: “Hakuna chochote kama mfano wake.”
Huufunika usiku kwa mchana, uufuatiao upesi upesi.
Hii ni katika mipango yake Mungu ya mambo ya ulimwengu. Maana yake ni kwamba usiku unafuata mchana na huufuatia haraka haraka na kuushinda ulivyokuwa kwa kufanya giza baada ya kuwa ni mwangaza. Mfano wa hayo ni kauli yake Mwenyezi Mungu:
وَاللَّيْلِ إِذَا يَغْشَىٰ ﴿١﴾
“Naapa kwa usiku unapofunika”
(92:1)
Na vilevile kauli yake:
وَاللَّيْلِ إِذَا يَغْشَاهَا ﴿٤﴾
“Na (kwa) usiku unapolifunika”
(91:4)
Yaani unaushinda mwanga wa jua.
Na jua na mwezi na nyota zinatumika kwa amri yake.
Yaani na ameumba sayari hizi zinazo kwenda kwa matakwa yake na kwen- da kwa mujibu wa hekima na masilahi, Mazungumzo kuhusu sayari hizi yanahitajia elimu ya falaki, Nasi hatujui chochote katika elimu hiyo.
Fahamuni! Kuumba na amri ni yake.
Huu ni ubainifu na tafsir ya kauli yake: Kisha akatawala juu ya arshi; kama tulivyotangulia kusema. Kuna Hadith isemayo: “Mwenye kudai kwamba Mwenyezi Mungu amewajaalia waja kuwa na amri, basi amekufuru yaliyoteremshiwa Mitume yake, kutokana na kauli yake: “Fahamuni! Kuumba na amri ni yake”
Ametukuka Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu wote
kwa umoja wake, ufalme wake na upangaji wake.
Muombeni Mola wenu kwa unyenyekevu na kwa uficho.
Maana ya mja kumwomba Mola wake sio kusema ‘Ewe Mwenyezi Mungu naomba rehema zako na maghufira yako’ Hapana! Isipokuwa kuomba kwa haki ni kumwogopa, kumcha na kushikamana na amri zake na kujiepusha na makatazo yake. Na pia sio makusudio ya kunyenyekea kusema: ‘Ewe Mwenyezi Mungu nanyenyekea kwako natubia, na najilinda kwako,’ bali mtu awe mkweli, mwenye ikhlasi katika anayoyasema na anayoyafanya.
Ama maana ya kwa uficho ni kutojifaharisha na kutangaza kwa watu kheri anayoifanya. Kwani hiyo ni aina ya kupetuka mipaka, na Mwenyezi Mungu anasema:
Hakika yeye hawapendi wapetukao mipaka.
Na Mwenyezi Mungu amekataza kujifaharisha kwa ibada na kufanya kheri.
MWENYEZI MUNGU AMEITENGENEZA VIZURI ARDHI NA BINADAMU AKAIHARIBU
Wala msifanye ufisadi katika ardhi baada ya kutengenea kwake.
Mwenyezi Mungu aliitengeza vizuri ardhi hii kwa kuweka hazina zisizo na idadi za vitu vizuri na starehe za kiroho na kimaada. Kuanzia maumbile asili ya kupendeza hadi kwenye uzuri wa mwanamke, na kwenye utekelezaji urafiki hadi wema wa watoto; na kuanzia kukua maarifa na utalii hadi sauti za minong’ono na nyimbo mpaka yasiyo na mwisho.
Vitu vizuri vya kimaada katika vyakula ni pamoja na nafaka, mboga, nyama na matunda. Kila jamii katika hivyo ziko aina, rangi na maumbo mbali mbali.
Katika mavazi ni pamoja na sufu, pamba, ngozi na hariri. Kisha binadamu akagundua Nailoni na ataendelea kugundua ambayo tunadhani ni katika mambo yasiyowezekana kama alivyogundua namna ya kupunguza masafa ya ardhini na mbinguni kwa mtu kuweza kusafiri kwa madakika tu.
Ama katika nishati ni kuanzia miti hadi makaa ya mawe, na petroli hadi umeme, nguvu za jua (Solar) na Tonoradi. Miongoni mwa niliyosoma ni kwamba sayansi imevumbua katika petroli vioo visivyovunjika, mabomu ya Napalm, Nailoni, Samadi ya kemikali, sahani na mabomba ya kunyunyizia maji.
Vilevile imetoa vipodozi, kama vile poda, rangi za mdomo, wanja na rangi za kucha. Pia imetoa maua ya bandia, vifunikia meza, dawa za meno, wino na filamu. Na vingine vingi hadi kufikia aina elfu tatu walizozihisabu Wataalamu, bali ni mpaka kufikia isiyo na idadi ila kwa yule ambaye anajua kila kitu:
وَإِن تَعُدُّوا نِعْمَتَ اللَّـهِ لَا تُحْصُوهَا إِنَّ الْإِنسَانَ لَظَلُومٌ كَفَّارٌ ﴿٣٤﴾
“Na mkizihesabu neema za Mwenyezi Mungu, hamtaweza kuzidhibiti, Hakika binadamu ni dhalimu mkubwa mwenye kukufuru sana”
(14: 34)
Aya hio ina matamko ya sana na kubwa pamoja na kutilia mkazo usisitizo huo, kwa neno hakika. Ni udhalimu gani mkubwa na utovu mkubwa wa shukran na ufisadi mkubwa kuliko kugeuza riziki njema kuwa mabomu ya Napalm, ya kuua watoto na kuwalemaza wakubwa, na hewa ya sumu inayochoma nyasi mbichi na kavu. Ama hayo mabomu ya Nuklia na Haidrojeni, ndiyo hayabakishi wala hayasazi!
Binadamu ameibadilisha neema kuwa kufuru na kuigeuza neema ya ardhi yake kuwa Jahanamu. Mwisho wa binadamu umefungamanishwa na manuklia. Mwenyezi Mungu ameweka katika ardhi hii starehe na riziki njema kwa waja wake.
Na yule dhalimu mkubwa asiye na shukrani ameweka mabomu ya Nuklia katika maghala yake na kwenye ndege zake zikizunguka angani, anangoja fursa tu aigeuze ardhi na vilivyomo kuwa majivu na mavumbi.
Hiyo ndiyo tafsir ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Wala msifanye ufisadi katika ardhi baada ya kutengenea kwake.” Kwa hiyo ni wajibu tumjue yule aliyeharibu ardhi baada ya Mwenyezi Mungu kututengenezea, na tumkatie njia kwa nyenzo zote tulizo nazo; angalau tumtangaze ajulikane na tumwite kwa jina lile alilopewa ‘Adui wa Mwenyezi Mungu na wa ubinadamu’ ili watu wote wawe na hadhari naye kutokana na vitimbi na hadaa zake.
Na mwombeni kwa kuogopa na kwa kutumai.
Kuwa na roho ya kukata tamaa ni hiyana. Kwa sababu hakuna maisha pamoja na kukata tamaa na kuacha kujihadhari pia ni hiyana kwa sababu ni kughurika. Njia ya kuokoka ni ile ya katika kati. Mwenyezi Mungu anasema:
وَيَرْجُونَ رَحْمَتَهُ وَيَخَافُونَ عَذَابَهُ ﴿٥٧﴾
“Na wanatumai rehema zake na wanaogopa adhabu yake”
(17:57)
Na amesema tena:
نَبِّئْ عِبَادِي أَنِّي أَنَا الْغَفُورُ الرَّحِيمُ ﴿٤٩﴾ وَأَنَّ عَذَابِي هُوَ الْعَذَابُ الْأَلِيمُ ﴿٥٠﴾
“Waambie waja wangu kwamba mimi ni mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu, Na kwamba adhabu yangu ndiyo adhabu iliyo chungu”
(15: 49 – 50).
Mumin mwenye akili anafanya amali hali ya kuwa anamcha Mwenyezi Mungu asijeikataa amali yake kwa makosa katika amali hiyo, na wakati huo huo anataraji kuokoka na kukubaliwa. Na yote hayo mawili, kuhofia na kutarajia yanaleta kujichunga na kufanya amali kwa uzuri.
Hakika rehema ya Mwenyezi Mungu iko karibu na wanaofanya mema.
Hapo kuna kuashiria kwamba mwenye kumwogopa Mwenyezi Mungu na akamtarajia, basi huyo ni katika watu wafanyao wema na kwamba Mwenyezi Mungu anawalipa wema kwa mfano wake.
وَهُوَ الَّذِي يُرْسِلُ الرِّيَاحَ بُشْرًا بَيْنَ يَدَيْ رَحْمَتِهِ حَتَّىٰ إِذَا أَقَلَّتْ سَحَابًا ثِقَالًا سُقْنَاهُ لِبَلَدٍ مَّيِّتٍ فَأَنزَلْنَا بِهِ الْمَاءَ فَأَخْرَجْنَا بِهِ مِن كُلِّ الثَّمَرَاتِ كَذَٰلِكَ نُخْرِجُ الْمَوْتَىٰ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ ﴿٥٧﴾
57. Na yeye ndiye azipelekaye pepo kuwa ni bishara kabla ya kufika rehema yake. Hata zinapobeba mawingu mazito tunayasukuma kwa ajili ya mji uliokufa, Kisha tunateremsha hapo maji, Kwa hayo tukaotesha kila matunda. Kama hivi tutawafufua wafu ili mpate kukumbuka.
وَالْبَلَدُ الطَّيِّبُ يَخْرُجُ نَبَاتُهُ بِإِذْنِ رَبِّهِ وَالَّذِي خَبُثَ لَا يَخْرُجُ إِلَّا نَكِدًا كَذَٰلِكَ نُصَرِّفُ الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَشْكُرُونَ ﴿٥٨﴾
58. Na mji mzuri hutoa mimea yake kwa idhini ya Mola wake. Na ule ulio mbaya hau- toi ila kwa taabu tu. Namna hii tunazipambanua ishara kwa watu wanaoshukuru.
APELEKAYE PEPO KUWA BISHARA
Aya 57 – 58
MAANA
Na yeye ndiye azipelekaye pepo kuwa ni bishara kabla ya kufika rehema yake. Hata zinapobeba mawingu mazito tunayasukuma kwa ajili ya mji uliokufa, Kisha tunateremsha hapo maji, Kwa hayo tukaotesha kila matunda.
Makusudio ya rehema hapa ni mvua. Makusudio ya mawingu mazito ni yaliyotiwa uzito na mvuke wa maji. Na mji uliokufa ni ule usio na mimea.
Na kila matunda, makusudio yake ni ujumla wa kidesturi, sio wa kihalisi. Kwa ajili ya mji uliokufa ni kwa kukadiria, yaani kwa ajili ya uhai wa mji uliokufa.
Upepo huvuma, jua huyatia mvuke maji ya bahari na pepo hupandisha mvuke huu hadi juu; kisha ardhi huuvuta na kuanguka juu yake matone yenye kufuatana, yote haya na mfano wa hayo huja kwa mujibu wa desturi ya maumbile, Hilo halina shaka.
Lakini ni nani huyo aliyeweka maumbile haya na kuyapa utaratibu unaok- wenda nayo kwa jinsi moja katika mamilioni ya karne bila kugeuka au kubadilika? Je, maumbile yamepatikana kibahati tu. Je, kanuni, na desturi zimesimamiwa na sadfa tangu mwanzo hadi mwisho bila ya sababu yoyote? Vipi kisicho na nidhamu kizalishe nidhamu? Na kisicho na utambuzi kizalishe utambuzi?
Isitoshe je, maswali haya yana majibu ya kuingilika akilini na kukubalika zaidi ya kuwako muumbaji mwenye hekima, Aliyeyaleta maumbile na akayapa utaratibu na kanuni. Na kwake yeye kinaishia kila kitu na kuhitajia kila kitu, wala yeye hahitaji chochote?
Kwa hiyo upepo, mvua na kuhuyishwa mji uliokufa hunasibishwa kwenye desturi ya maumbile moja kwa moja na kupitia kwa muumbaji wa maumbile.
Kama hivi tutawafufua wafu, ili mpate kukumbuka.
Wakanushaji husema: Vipi tutaamini ufufuo na hatujaona yeyote aliyerudiwa na uhai baada ya kufa kwake? Wanasema hivi na wao wanaona kwa macho ardhi baada ya kufa inavyopata uhai, lakini wao wamesahau kuwa sababu ni moja na kwamba hakuna tofauti ila katika sura tu, ndipo Mwenyezi Mungu akawakumbusha hilo ili wao wanufaike kwa ukumbusho au iwalazimu hoja.
Na mji mzuri hutoa mimea yake kwa idhini ya Mola wake. Na ule ulio mbaya hautoi ila kwa taabu tu.
Kwa idhini ya Mola wake ni fumbo la kutoa kingi kutokana na uchache na kwa wepesi, na kidogo ni fumbo la kutoa kichache kwa uzito na ugumu.
Wafasiri wengi wanafananisha moyo wa mumin na kafiri, na mwema na mwovu na ardhi ambayo wote wameumbwa kutokana nayo. Wajihi wa kufananisha ni kwamba ardhi yote ingawaje ni jinsi moja, lakini kuna ile iliyo nzuri ambayo ikinywa maji husisimka na kututumka na kumea kila namna ya mimea mizuri.
Na kuna nyingine iliyosusuwaa imefungika inapinga kheri na utengenefu, inapojiwa na kheri yoyote ni kama kwamba inapelekwa kufa.
Namna hii tunazipambanua ishara kwa watu wanaoshukuru.
Mwenyezi Mungu hupiga mifano hii na mengineyo kwa wote kwa mwovu na mwema, lakini wema ndio wanufaikao nayo na kumshukuru Mwenyezi Mungu. Ama kwa mnasaba wa waovu. Basi ni hoja juu yao inayokata nyudhuru na sababu zao.