14
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA NANE
لَقَدْ أَرْسَلْنَا نُوحًا إِلَىٰ قَوْمِهِ فَقَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ إِنِّي أَخَافُ عَلَيْكُمْ عَذَابَ يَوْمٍ عَظِيمٍ ﴿٥٩﴾
59. Hakika tulimtuma Nuh kwa watu wake. Akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenyezi Mungu, hamna Mungu mwingine zaidi yake. Hakika mimi ninawahofia na adhabu ya siku iliyo kuu.
قَالَ الْمَلَأُ مِن قَوْمِهِ إِنَّا لَنَرَاكَ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿٦٠﴾
60. Wakasema wakuu wa watu wake: Hakika sisi tunakuona umo katika upotofu ulio wazi.
قَالَ يَا قَوْمِ لَيْسَ بِي ضَلَالَةٌ وَلَـٰكِنِّي رَسُولٌ مِّن رَّبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٦١﴾
61. Akasema: Enyi watu wangu! Mimi simo katika upotevu, lakini mimi ni Mtume nitokaye kwa Mola wa walimwengu wote.
أُبَلِّغُكُمْ رِسَالَاتِ رَبِّي وَأَنصَحُ لَكُمْ وَأَعْلَمُ مِنَ اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ ﴿٦٢﴾
62. Nawafikishia ujumbe wa Mola wangu na nawanasihi; na ninajua kwa Mwenyezi Mungu msiyoyajua.
أَوَعَجِبْتُمْ أَن جَاءَكُمْ ذِكْرٌ مِّن رَّبِّكُمْ عَلَىٰ رَجُلٍ مِّنكُمْ لِيُنذِرَكُمْ وَلِتَتَّقُوا وَلَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴿٦٣﴾
63. Je, mnastaajabu kuwafikia mawaidha kutoka kwa Mola wenu kupitia mtu anayetokana na nyinyi ili awaonye na ili muwe na takua, na ili mpate kurehemiwa? ”
فَكَذَّبُوهُ فَأَنجَيْنَاهُ وَالَّذِينَ مَعَهُ فِي الْفُلْكِ وَأَغْرَقْنَا الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا إِنَّهُمْ كَانُوا قَوْمًا عَمِينَ ﴿٦٤﴾
64. Basi walimkadhibisha. Nasi tukamwokoa yeye na waliokuwa pamoja naye katika jahazi, na tukawazamisha waliozikadhibisha ishara zetu, Hakika wao walikuwa watu vipofu.
NUH
Aya 59 – 64
MAANA
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kusema, katika Aya 35 ya Sura hii:“Enyi Wanadamu! Watakapowafikia Mitume kutoka miongoni mwenu”
Anaashiria, katika Aya hii na zinazofuatia, kisa cha Mitume Nuh, Hud, Swaleh, Nabii Lut, na Shuaib
.
Mwenyezi Mungu amekifupisha sana hapa kisa cha Nuh, ambapo ametosheka tu na kutaja majibizano kati yake na jamaa zake na namna walivyoepuka mwito na jinsi walivyostaajabu kuchagua Mwenyezi Mungu Mtume kutokana na wao.
Na kwamba yeye (s.w.t) aliwagharikisha wakadhibishaji na kuwaokoa waumini.
Hakika tulimtuma Nuh kwa watu wake.
Tabrasi anasema katika Majamaul-Bayan: “Yeye ni Nuh bin Mulk bin Matoshalkh bin Ukhnun, Mtume Idris. Na Nuh ni Mtume wa kwanza baada ya Idris.”
Inasemekana kuwa yeye alikuwa ni seremala na kwamba alizaliwa mwaka aliokufia Adam, Ama sisi, hatujui chimbuko la kusemekana huku.
Akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenyezi Mungu, hamna Mungu mwingine zaidi yake. Hakika mimi ninawahofia na adhabu ya siku iliyo kuu.
Aliufupisha Nuh
ujumbe aliouchukua kwa watu wake kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa jumla moja tu: Mwabuduni Mwenyezi Mungu peke yake kwa sababu hakuna Mola mwingine isipokuwa yeye. Na kwam- ba mwito wake huo kwao ni kuwahurumia na adhabu ya siku ya Kiyama.
Wakasema wakuu wa watu wake: Hakika sisi tunakuona umo katika upotofu ulio wazi.
Wakamshutumu kwa upotevu na usafihi si kwa jingine ila tu kwa vile amewakataza walioyazoea na kuyarithi ya kuabudu mawe.
Hivi ndiyo alivyo kila safihi na kila mpotevu, humzulia ule ugonjwa wake kila anayekwenda kwenye njia ya uongofu.
Akasema: Enyi watu wangu! Mimi simo katika upotevu, lakini mimi ni Mtume nitokaye kwa Mola wa walimwengu wote. Nawafikishia ujumbe wa Mola wangu na ninawanasihi; na ninajua kwa Mwenyezi Mungu msiyoyajua.
Aliwajibu kwa kukanusha upotevu yeye mwenyewe na kujisifu kwa sifa tukufu kwamba yeye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, amempeleka ili awaokoe na upotevu na kuangamia, na kwamba yeye ni mtoaji nasaha mwaminifu, na anajua kutoka kwa Mwenyezi Mungu umoja na uadilifu wake. Na mwenye kuwa na sifa hizi hawezi kuwa mpotevu.
Je, mnastaajabu kuwafikia mawaidha kutoka kwa Mola wenu kupitia mtu anayetokana na nyinyi ili awaonye na ili muwe na takua na ili mpate kurehemiwa?
Watu wake walimwaambia wewe ni mtu tu kama sisi, Lau Mwenyezi Mungu angelitaka kutuma mjumbe angelimtuma Malaika. Akawajibu kwamba hakuna ajabu kutuma Mwenyezi Mungu mtu kwa watu wake akiwa hana masilahi yoyote au lengo lolote ila kuwaongoza kwenye lile lililo na kheri yao na utengenefu wao, isipokuwa ajabu ni kupuuzwa na kuachwa bila ya mwongozi.
Razi anasema huu ni utaratibu wa lengo zuri, kwani lengo la kutuma ujumbe ni kuonya, na lengo la kuonya ni takua, na lengo la takua ni kufuzu rehema ya Mwenyezi Mungu katika nyumba ya akhera.
Basi walimkadhibisha, Nasi tukamwokoa yeye na waliokuwa pamoja naye katika jahazi, na tukawazamisha waliozikadhibisha ishara zetu, Hakika wao walikuwa watu vipofu.
Milango ya mbinguni ilifunguka ikatoa maji na ardhi ikachimbuka chem-chemi. Hapo Mwenyezi Mungu akawaangamiza madhalimu wenye kukad- hibisha na akaokoka Nuh
na waumini aliokuwa pamoja nao. Yatakuja maelezo kwa ufafanuzi kuhusu Nuh
na watu wake katika Sura iliyoitwa kwa jina lake (71) inshaallah.
وَإِلَىٰ عَادٍ أَخَاهُمْ هُودًا قَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ أَفَلَا تَتَّقُونَ ﴿٦٥﴾
65. Na kwa Adi (tulimpeleka) ndugu yao Hud. Akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenyezi Mungu, nyinyi hamna Mungu mwingine zaidi yake, Basi hamwogopi?
قَالَ الْمَلَأُ الَّذِينَ كَفَرُوا مِن قَوْمِهِ إِنَّا لَنَرَاكَ فِي سَفَاهَةٍ وَإِنَّا لَنَظُنُّكَ مِنَ الْكَاذِبِينَ ﴿٦٦﴾
66. Wakasema wakuu waliokufuru katika watu wake: Hakika sisi tunakuona umo katika upumbavu na tunakudhania ni katika waongo.
قَالَ يَا قَوْمِ لَيْسَ بِي سَفَاهَةٌ وَلَـٰكِنِّي رَسُولٌ مِّن رَّبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٦٧﴾
67. Akasema: Enyi watu wangu! Mimi sina upumbavu, lakini mimi ni Mtume nitokaye kwa Mola wa walimwengu.
أُبَلِّغُكُمْ رِسَالَاتِ رَبِّي وَأَنَا لَكُمْ نَاصِحٌ أَمِينٌ ﴿٦٨﴾
68. Nawafikishia ujumbe wa Mola wangu na mimi kwenu nimtoa nasaha, mwaminifu.
أَوَعَجِبْتُمْ أَن جَاءَكُمْ ذِكْرٌ مِّن رَّبِّكُمْ عَلَىٰ رَجُلٍ مِّنكُمْ لِيُنذِرَكُمْ وَاذْكُرُوا إِذْ جَعَلَكُمْ خُلَفَاءَ مِن بَعْدِ قَوْمِ نُوحٍ وَزَادَكُمْ فِي الْخَلْقِ بَسْطَةً فَاذْكُرُوا آلَاءَ اللَّـهِ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٦٩﴾
69. Je, mnastaajabu kuwafikia ukumbusho kutoka kwa Mola wenu kupitia mtu anayetokana na nyinyi ili awaonye. Na kumbukeni alivyowafanya makhalifa baada ya watu wa Nuh, Na akawazidisha nguvu katika umbo. Basi kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu ili mpate kufaulu.
قَالُوا أَجِئْتَنَا لِنَعْبُدَ اللَّـهَ وَحْدَهُ وَنَذَرَ مَا كَانَ يَعْبُدُ آبَاؤُنَا فَأْتِنَا بِمَا تَعِدُنَا إِن كُنتَ مِنَ الصَّادِقِينَ﴿٧٠﴾
70. Wakasema: Je, umetujia ili tumwabudu Mwenyezi Mungu peke yake na tuyaache waliyokuwa wakiyaabudu baba zetu? Basi tuletee unayotuahidi ukiwa ni miongoni mwa wasemao kweli.
قَالَ قَدْ وَقَعَ عَلَيْكُم مِّن رَّبِّكُمْ رِجْسٌ وَغَضَبٌ أَتُجَادِلُونَنِي فِي أَسْمَاءٍ سَمَّيْتُمُوهَا أَنتُمْ وَآبَاؤُكُم مَّا نَزَّلَ اللَّـهُ بِهَا مِن سُلْطَانٍ فَانتَظِرُوا إِنِّي مَعَكُم مِّنَ الْمُنتَظِرِينَ ﴿٧١﴾
71. Akasema: Hakika adhabu na ghadhabu zimekwishawaangukia kutoka kwa Mola wenu. Je, mnanijadili katika majina mliyoyaita nyinyi na baba zenu ambayo Mwenyezi Mungu hakuyateremshia dalili yoyote? Basi ngojeni; mimi pia ni pamoja nanyi katika wangojao.
فَأَنجَيْنَاهُ وَالَّذِينَ مَعَهُ بِرَحْمَةٍ مِّنَّا وَقَطَعْنَا دَابِرَ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَمَا كَانُوا مُؤْمِنِينَ ﴿٧٢﴾
72. Basi tukamwokoa yeye na waliokuwa pamoja naye kwa rehema zetu na tukakata mizizi ya wale waliokadhibisha ishara zetu, na hawakuwa wenye kuamini.
HUD
Aya 65 – 72
MAANA
Imesemwa katika Tafsir Al-Manar kwa kunukuliwa kutoka kwa Is-haq bin Bashar na Ibn Asakir: “Nabii Hud
ndiye wa kwanza kuzungumza Kiarabu, alikuwa na watoto wane: Qahtan, Muq-hit, Qahit na Faligh ambaye ni baba wa Mudhar. (Abu Mudhar) Na Qahtan ni baba wa Yemen (Abul-Yaman), Ama Qahit na Muqhit hawana kizazi.”
Wafasiri wamesema: Watu wa Hud
walikuwa ni katika kizazi cha Nuh
na walikuwa kwenye dini yake. Baada ya muda kuwa mrefu, shetani aliwachezea, wakaabudu masanamu na wakafanya ufisadi katika ardhi.
Katika Tafsir Tabari imeelezwa kuwa Imam Ali alimwambia mtu mmoja kutoka Yemen: “Je, umeona katika ardhi ya Hadharamauti chungu ya tifu-tifu jekundu iliyochanganyika na madongo mekundu, ina mipilipili na mikunazi mingi sehemu kadha wa kadha?” Akasema: “Ndio Ewe Amirul Muminin, wallah unapasifu sifa ya mtu aliyepaona.” Akasema Amirul-Muminina: “Hapana, nimehadithiwa”. Yule mtu akasema: “Kwani pana nini Ewe Amirul-Muminin?” Akasema: “Pana kaburi ya Nabii Hud
”
Ikiwa ni sahih Riwaya hii, basi itabidi iondolewe sehemu iliyoandikwa kwenye kaburi ya Imam Ali, isemayo: Amani ishuke juu yako na juu ya jirani zako Hud na Swaleh, ila ikiwa ujirani wenyewe ni katika akhera sio hapa duniani, au iwe mwili wa Hud ulihamishwa baada ya kufa Imam.
Aya hizi zilizoshuka kuhusu kisa cha Hud
zinaafikiana na Aya zilizotangulia, ambazo zimeshuka kuhusu kisa cha Nuh
kimaneno na kimaana isipokuwa katika mambo yafuatavyo:-
Nuh
aliwaambia watu wake: “Hakika mimi nawahofia na adhabu ya siku iliyo kuu”. Na Hud
akawaambia watu wake:Basi hamwogopi
? Hiyo ni kwa sababu kabla ya Nuh
hakukuwahi kutokea mfano wa adhabu hiyo, ambayo ni tufani. Na watu wa Hud
walikuwa wakijua, ndipo akawahadharisha na akawaamrisha kumwogopa Mwenyezi Mungu, kwa kuacha kumshirikisha na kumthibitishia umoja.
Nuh
aliambiwa na watu wake: ‘Hakika sisi tunakuona umo katika upotofu ulio dhahiri.’ Na watu wa Hud
walimwambia:
Hakika sisi tunakuona umo katika upumbavu, na hakika sisi tunakudhania ni katika waongo.
Kwa sababu Nuh
alikuwa akitengeneza safina mahali pasipo na bahari wala mito. Na kazi hii ukitazama kwa dhahiri ni ujinga na upotevu.
Ama Hud
hakufanya namna hii, isipokuwa aliwafanya wapumbavu watu wake kwa kuabudu masanamu. Kwa hiyo nao wakamrudishia na kumnasibishia upumbavu.
Nuh
aliwaambia watu wake: ‘Ili mpate kurehemiwa.’ Na Hud
aliwaambia watu wake:
Ili mpate kufaulu.
Nuh
alikusudia rehema, na kuondolewa adhabu na Hud
naye akakusudia kufaulu na kuongoka kwenye njia iliyo sawa, Maana zote mbili zinaungana, haziachani.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja katika Aya hizi mambo ambayo watu wa Hud
walimwambia mtume wao, lakini hakutaja kama watu wa Nuh
walimwambia Mtume wao nayo ni:
Wakasema: Je, Umetujia ili tumwabudu Mwenyezi Mungu peke yake na tuyaache waliyokuwa wakiyaabudu baba zetu?
Ibara inayotumiwa na kila jahili na mwenye kufuata. Basi tuletee unayotuahidi ukiwa ni miongoni mwa wasemao kweli”
Likaja jawabu la mkato na la haraka kutoka kwa Mtume akasema: Hakika adhabu na ghadhabu zimekwishwaangukia kutoka kwa Mola Wenu. Maana ya kuwaangukia hapa ni kuwawajibikia, na makusudio ya adhabu ni sababu yenye kuwajibisha adhabu.
Je, Mnanijadili katika majina mliyoyaita nyinyi na baba zenu ambayo Mwenyezi Mungu hakuyateremshia dalili yoyote?
Waungu mnaowaabudu hawako, na kila kisichokuweko hakina athari wala dalili. Kwa hali hii majina waliyopewa yanakuwa ni maneno matupu yasiyokuwa na maana.
Basi ngojeni, mimi pia ni pamoja nanyi katika wangojao.
Hili ni jibu la kauli yao: “Basi tuletee unayotuahidi ukiwa miongoni mwa wasemao kweli.”
Basi tukamwokoa na waliokuwa pamoja naye kwa rehema zetu na tukakata mizizi ya wale waliokadhibisha ishara zetu, na hawakuwa wenye kuamini.
Kukatwa mizizi, ni kuangamizwa mpaka wa mwisho wao. Amebainisha Mwenyezi Mungu mahali pengine aina ya adhabu aliyowaangamizia watu wa Hud
, aliposema:
وَأَمَّا عَادٌ فَأُهْلِكُوا بِرِيحٍ صَرْصَرٍ عَاتِيَةٍ ﴿٦﴾ سَخَّرَهَا عَلَيْهِمْ سَبْعَ لَيَالٍ وَثَمَانِيَةَ أَيَّامٍ حُسُومًا فَتَرَى الْقَوْمَ فِيهَا صَرْعَىٰ كَأَنَّهُمْ أَعْجَازُ نَخْلٍ خَاوِيَةٍ ﴿٧﴾ فَهَلْ تَرَىٰ لَهُم مِّن بَاقِيَةٍ ﴿٨﴾
“Na ama Adi waliangamizwa kwa upepo mkali usiozuilika, Aliwapelekea masiku saba na siku nane mfululizo. Utawaona watu wameanguka kama kwamba ni magogo ya mitende yaliyo wazi, Basi je, unamwona mmoja wao aliyebaki?”
(69: 6 – 8).
Inshallah yatakuja maelezo zaidi kuhusu Hud
na watu wake katika Sura (11) iliyoitwa kwa jina lake.
وَإِلَىٰ ثَمُودَ أَخَاهُمْ صَالِحًا قَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ قَدْ جَاءَتْكُم بَيِّنَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ هَـٰذِهِ نَاقَةُ اللَّـهِ لَكُمْ آيَةً فَذَرُوهَا تَأْكُلْ فِي أَرْضِ اللَّـهِ وَلَا تَمَسُّوهَا بِسُوءٍ فَيَأْخُذَكُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٧٣﴾
73. Na kwa Thamud (tulimpeleka) ndugu yao Swaleh. Akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenyezi Mungu, nyinyi hamna Mungu mwingine zaidi yake. Hakika umekwishawafikia ubainifu kutoka kwa Mola wenu. Huyu ni ngamia wa Mwenyezi Mungu aliye ishara kwenu, Basi mwacheni ale katika ardhi ya Mwenyezi Mungu, wala msimtie dhara, isije ikawashika adhabu ya Mwenyezi Mungu iumizayo.
وَاذْكُرُوا إِذْ جَعَلَكُمْ خُلَفَاءَ مِن بَعْدِ عَادٍ وَبَوَّأَكُمْ فِي الْأَرْضِ تَتَّخِذُونَ مِن سُهُولِهَا قُصُورًا وَتَنْحِتُونَ الْجِبَالَ بُيُوتًا فَاذْكُرُوا آلَاءَ اللَّـهِ وَلَا تَعْثَوْا فِي الْأَرْضِ مُفْسِدِينَ ﴿٧٤﴾
74. Na kumbukeni alipowafanya makhalifa baada ya Ad na kuwakalisha katika ardhi mkajenga makasri katika nyanda zake na mkachonga majumba katika majabali, Basi zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu, wala msifanye ufisadi katika ardhi.
قَالَ الْمَلَأُ الَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا مِن قَوْمِهِ لِلَّذِينَ اسْتُضْعِفُوا لِمَنْ آمَنَ مِنْهُمْ أَتَعْلَمُونَ أَنَّ صَالِحًا مُّرْسَلٌ مِّن رَّبِّهِ قَالُوا إِنَّا بِمَا أُرْسِلَ بِهِ مُؤْمِنُونَ ﴿٧٥﴾
75. Wakasema wakuu wa watu wake waliotakabari kuwaambia walio wanyonge walioamini miongoni mwao: Je, mwajua kuwa Swaleh ametumwa na Mola wake? Wakasema: Hakika tunayaamini yale aliyotumwa.
قَالَ الَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا إِنَّا بِالَّذِي آمَنتُم بِهِ كَافِرُونَ ﴿٧٦﴾
76. Wakasema wale waliotakabari: Hakika Sisi tunayakataa yale mnayoyaamini.
فَعَقَرُوا النَّاقَةَ وَعَتَوْا عَنْ أَمْرِ رَبِّهِمْ وَقَالُوا يَا صَالِحُ ائْتِنَا بِمَا تَعِدُنَا إِن كُنتَ مِنَ الْمُرْسَلِينَ ﴿٧٧﴾
77. Wakamchinja ngamia na wakaasi amri ya Mola wao na Wakasema: Ee Swaleh! Tuletee unayotuahidi ikiwa wewe ni miongoni mwa Mitume.
فَأَخَذَتْهُمُ الرَّجْفَةُ فَأَصْبَحُوا فِي دَارِهِمْ جَاثِمِينَ ﴿٧٨﴾
Ukawanyakua mtetemeko wakawa wameanguka hawajimudu majumbani mwao.
فَتَوَلَّىٰ عَنْهُمْ وَقَالَ يَا قَوْمِ لَقَدْ أَبْلَغْتُكُمْ رِسَالَةَ رَبِّي وَنَصَحْتُ لَكُمْ وَلَـٰكِن لَّا تُحِبُّونَ النَّاصِحِينَ ﴿٧٩﴾
79. Basi Swaleh akawaacha na kusema: Enyi watu wangu! Kwa hakika nimewafikishia ujumbe wa Mola wangu na nikawanasihi, lakini hampendi wenye nasaha.
SWALEH
Aya Ya 73 – 79
MAANA
Na kwa Thamud (tulimpeleka) ndugu yao Swaleh. Akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenyezi Mungu, nyinyi hamna Mungu mwingine zaidi yake.
Thamud ni kabila katika Waarabu. Waliitwa kwa jina la babu yao Thamud bin Amir. Makazi yao yalikuwa Hijr, baina ya Hijaz na Sham mpaka Wadil-qura. Mwenyezi Mungu anasema:
وَلَقَدْ كَذَّبَ أَصْحَابُ الْحِجْرِ الْمُرْسَلِينَ ﴿٨٠﴾
“Na hakika watu wa Hijr walikadhibisha Mitume
(15:80).
Huyu ni ngamia wa Mwenyezi Mungu aliye ishara kwenu.
Kikundi cha Wafasiri wamesema kuwa watu wa Nabii Swaleh
walimwomba awatolee ngamia kutoka kwenye jiwe; na yeye alimwomba Mola wake hilo. Basi jiwe likashikwa na uchungu wa kuzaa kama mwanamke, likazaa ngamia wa kike mchangamfu mwenye manyoya.
Sisi tunaamini kiujumla kwamba ngamia alikuwa ni ubainifu na ishara kutoka kwa Mwenyezi Mungu; na kwamba hakuja kwa njia ya kawaida; na Mwenyezi Mungu alimtegemeza kwake kwa kumwadhimisha. Tunaamini hivi, bila ya kuongeza chochote ambacho hakikuelezwa na Wahyi au Hadith Mutawatir iliyotoka kwa Maasum.
Basi mwacheni ale katika ardhi ya Mwenyezi Mungu, wala msimtie dhara, isije ikawashika adhabu ya Mwenyezi Mungu iumizayo.
Swaleh
aliwaamrisha watu wake wamuache ngamia akae katika ardhi ya Mwenyezi Mungu, na akawahadharisha na mwisho mbaya ikiwa watamtaaradhi kwa udhia. Kisha akawaambia:
Na kumbukeni alipowafanya makhalifa baada ya Ad.
Mwenyezi Mungu aliangamiza kabila la Ad kwa dhambi zao, akawakumbusha neema hii ya kuwa makhalifa. Vilevile aliendelea kuwakumbusha kwa kuwaambia:
Na kuwakalisha katika ardhi mkajenga makasri kati- ka nyanda zake na mkachonga majumba katika majabali.
Kauli hii inafahamisha kuwa Thamud waliishi katika majengo yaliyoendelea na kwamba walikuwa katika neema na starehe.
Basi zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu, wala msifanye ufisadi katika ardhi.
Baada ya kuwakumbusha neema alizowamiminia Mwenyezi Mungu aliwaamrisha wakumbuke na washukuru neema hizo na kuwakataza wasifanye ufisadi. Hilo ni kuwahadharisha na uovu wa Mwenyezi Mungu na adhabu yake.
Wakasema wakuu wa watu wake waliotakabari kuwaambia wale walio wanyonge walioamini miongoni mwao.
Wale wapenda anasa katika watu wa Swaleh
waliendelea na utaghuti na kung’ang’ania kuabudu masanamu. Ama wale wanyonge kuna walioamini katika wao na waliobakia kwenye shirki kwa kuwafuata wapenda anasa. Basi hawa wakawaambia wale walioamini katika mafukara na wanyonge:
Je, mnajua kuwa Swaleh ametumwa na Mola wake?
Waliwauliza wanyonge swali hili kwa kupinga na kutishia au kwa dharau na stihzai.
Wakasema
– wale wanyonge –Hakika tunayaamini yale aliyotumwa.
Waliyasema haya bila ya kujali vitisho na stizai. Kwa sababu wao wana yakini na dini yao.
Wakasema wale waliotakabari kuwaambia wale wanyonge: Sisi tunayakataa yale mliyoyaamini.
Pamoja na dalili na ubainifu mkataa juu ya utume wa Swaleh. Kwa sababu masilahi yao ni zaidi kuliko dini za Mwenyezi Mungu na dalili ya kiakili. Razi anasema Aya hii ni miongoni mwa hoja kubwa kuwa kiburi kinatokana na wingi wa mali na jaha. Kwa sababu wingi huo ndio uliowafanya waendele kuasi na kukufuru.
Wakamchinja ngamia na wakaasi amri ya Mola wao.
Hakika yao inadhihirisha uasi huu, na kwamba wao hawajali isipokuwa masilahi yao tu. Wakamchochea Nabii Swaleh
kuleta adhabu haraka na wakasema:
Ee Swaleh!: Tuletee unayotuahidi ikiwa wewe ni miongoni mwa Mitume.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakuwachelewesha kuwalipa inadi hiiUkawanyakua mtetemeko wakawa wameanguka hawajimudu majumbani mwao
[3]
.
Mwenyezi Mungu anasema katika Aya nyingine:
وَفِي ثَمُودَ إِذْ قِيلَ لَهُمْ تَمَتَّعُوا حَتَّىٰ حِينٍ ﴿٤٣﴾ فَعَتَوْا عَنْ أَمْرِ رَبِّهِمْ فَأَخَذَتْهُمُ الصَّاعِقَةُ وَهُمْ يَنظُرُونَ ﴿٤٤﴾
Na katika Thamud walipoambiwa jifurahisheni kwa muda mdogo tu. Wakaasi amri ya Mola wao ikawanyakua rindimo na huku wanaona.”
(51:43-44)
Basi Swaleh akawaacha na akasema: Enyi watu! Kwa hakika nimewafikishia ujumbe wa Mola wangu na nikawanasihi, lakini hampendi wenye nasaha.
Nabii Swaleh
alipoona adhabu iliyowapata watu wake aliachana nao na akijiepusha na mwisho wao huu walioutaka wenyewe kwa uasi na jeuri.
Razi anasema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
: “Ewe Ali! Mwovu zaidi wa kwanza ni mchinja ngamia wa Swaleh, na mwovu zaidi wa mwisho ni muuaji wako”.
Tutarudia habari ya Nabii Swaleh
mara nyingine inshallah.