9
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA
أَيُشْرِكُونَ مَا لَا يَخْلُقُ شَيْئًا وَهُمْ يُخْلَقُونَ ﴿١٩١﴾
191. Je, wanawashirikisha wale ambao hawaumbi kitu, hali wao wameumbwa?
وَلَا يَسْتَطِيعُونَ لَهُمْ نَصْرًا وَلَا أَنفُسَهُمْ يَنصُرُونَ ﴿١٩٢﴾
192. Wala hawawezi kuwasaidia wala kujisaidia wenyewe.
وَإِن تَدْعُوهُمْ إِلَى الْهُدَىٰ لَا يَتَّبِعُوكُمْ سَوَاءٌ عَلَيْكُمْ أَدَعَوْتُمُوهُمْ أَمْ أَنتُمْ صَامِتُونَ ﴿١٩٣﴾
193. Na kama mkiwaita kwenye uwongofu hawatawafuata, Ni sawa ikiwa mtawaita au mtanyamaza.
إِنَّ الَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ عِبَادٌ أَمْثَالُكُمْ فَادْعُوهُمْ فَلْيَسْتَجِيبُوا لَكُمْ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿١٩٤﴾
194. Hakika hao mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni waja mfano wenu, Hebu waombeni nao wawaitikie ikiwa nyinyi mnasema kweli.
أَلَهُمْ أَرْجُلٌ يَمْشُونَ بِهَا أَمْ لَهُمْ أَيْدٍ يَبْطِشُونَ بِهَا أَمْ لَهُمْ أَعْيُنٌ يُبْصِرُونَ بِهَا أَمْ لَهُمْ آذَانٌ يَسْمَعُونَ بِهَا قُلِ ادْعُوا شُرَكَاءَكُمْ ثُمَّ كِيدُونِ فَلَا تُنظِرُونِ ﴿١٩٥﴾
195. Je, wao wanayo miguu ya kuendea? Au wanayo mikono ya kushika? Au wanayo macho ya kuonea? Au wanayo masikio ya kusikiliza? Sema: Waiteni hao mnaowashirikisha kisha nifanyieni vitimbi wala msinipe muda.
إِنَّ وَلِيِّيَ اللَّـهُ الَّذِي نَزَّلَ الْكِتَابَ وَهُوَ يَتَوَلَّى الصَّالِحِينَ ﴿١٩٦﴾
196. Hakika mlinzi wangu ni Mwenyezi Mungu aliyeteremsha Kitab naye ndiye awalindaye wafanyao mema.
وَالَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِهِ لَا يَسْتَطِيعُونَ نَصْرَكُمْ وَلَا أَنفُسَهُمْ يَنصُرُونَ ﴿١٩٧﴾
197. Na wale mnaowaabudu badala yake hawawezi kuwasaidia wala kujisaidia wenyewe.
وَإِن تَدْعُوهُمْ إِلَى الْهُدَىٰ لَا يَسْمَعُوا وَتَرَاهُمْ يَنظُرُونَ إِلَيْكَ وَهُمْ لَا يُبْصِرُونَ ﴿١٩٨﴾
198. Na kama mkiwaita kwenye uongofu hawatasikia, Na unawaona wanakutizama, nao hawaoni.
JE, WANAWASHIRIKISHA WASIOUMBA KITU?
Aya 191 – 198
MAANA
Je, wanawashirikisha wale ambao hawaumbi kitu, hali wao wameumbwa?
Kuumba na amri ni ya Mwenyezi Mungu tu ndiye ambaye kukiambia kitu kuwa kikawa. Yoyote asiyekuwa Yeye, yakiwemo masanamu, anamhitajia Yeye katika asili ya kupatikana kwake na katika kuendelea kuweko kwake.
Wala hawawezi kuwasaidia wala kujisaidia wenyewe.
Usaidizi, ushindi, utukuzaji na udhalilishaji, yote hayo yako chini ya uwezo wa Mwenyezi Mungu. Masanamu yanayokojolewa na paka na mbwa hayawezi kusaidia wala kujisaidia.
Na kama mkiwaita kwenye uwongofu hawatawafuata, Ni sawa ikiwa mtawaita au mtanyamaza.
Haya masanamu hayaumbi, hayasaidii wala hayajisaidii, hayaongoki wala hayaongozi, hayamwiti yeyote wala hayaitikii mwito wa yeyote. Pamoja na yote haya yanaabudiwa!
Hakika hao mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni waja mfano wenu, Hebu waombeni nao wawaitikie ikiwa nyinyi mnasema kweli.
Mmedai nyinyi washirikina kwamba masanamu ni miungu; na Mungu hunufaisha na kudhuru, hutoa na kuzuia, basi waombeni ili tuone kuwa je, wataitikia maombi yenu?
Je, wao wanayo miguu ya kuendea? Au wanayo mikono ya kushika? Au wanayo macho ya kuonea? Au wanayo masikio ya kusikiliza?.
Huku ni kuamshwa na kuzinduliwa washirikina kwamba wao ni bora kuliko masanamu wanayoyaabudu. Kwa sababu wao wana akili za utambuzi, macho ya kuona, masikio ya kusikia, miguu ya kutembelea, mikono ya kushika na ndimi za kutamka.
Lakini masanamu hayana chochote katika hayo, Sasa imekuaje aliye duni ndiye anayeabudiwa badala ya aliye mkamilifu?
Sema: Waiteni hao mnaowashirikisha kisha nifanyieni vitimbi wala msinipe muda.
Anaambiwa Nabii Muhammad(s.a.w.w)
awaambie washirikina, ikiwa masanamu yenu yana kitu, kama mnavyodai, basi mimi ninayadharau pamoja na nyinyi, basi kama mnaweza shindaneni wala msingoje.
Hakika mtawala wangu ni Mwenyezi Mungu aliyeteremsha Kitab naye ndiye awalindaye wafanyao mema.
Baada ya Mtume(s.a.w.w)
kuwakana washirikina na miungu yao aliwaam- bia kuwa nyinyi mnawatawalisha masanamu na mimi ninatawalisha Mungu aliyeniteremshia Qur’an iliyo na ubainifu wa kila kitu yake, Yeye vilevile anasimamia hifadhi yangu nani mlinzi wangu.
Je, masananu yenu yana kitabu? Je,yanawalinda? Natija ikawa, kama wanavyojua wote, ni kudhalilika washirikina na kutukuka Uislam na waislamu.
Na wale mnaowaabudu badala yake hawawezi kuwasaidia wala kuji- saidia wenyewe.
Imetangulia punde katika Aya 192. Kumekuja kukaririka kwa sababu Mtume(s.a.w.w)
alishindana na masanamu, kuwa yampe madhara, ndipo ikanasibu kuishiria kwamba hayo hayawezi hata kujisaidia yenyewe.
Na kama mkiwaita kwenye uongofu hawatasikia.
Vilevile imetangulia katika Aya 193, kukiwa kukaririka ni kwa lengo hilo hilo.
Na unawaona wanakutizama,nao hawaoni.
Inafahamisha nasi hii kwamba masanamu yalikuwa sawa na masanamu haya yaliyomo makanisani. Na kwamba Waarabu walikuwa ni wasanii wa kuchonga. Kwani wao waliyafanya masanamu yao yaonekane kama yanaona ukiyatazama haraka haraka.
Utauliza
: Kwa nini Mwenyezi Mungu amerudiarudia katika Aya zinazo fanana kwamba masanamu hayadhuru wala hayanufaishi, hayasaidii wala hayajisaidii na kwamba hayana mikono wala miguu wala macho, mpaka kufikia Aya tisa ambapo ingeotosha tu kusema hayo ni mawe?
Jibu
: Fikra ya kuabudu mizimu na masanamu ilitawala sana katika akili za waarabu na ikachanganyika na roho zao na damu zao kwa vizazi na karne. Imani yao hii ilikuwa na nguvu kuliko kumwamini Mwenyezi Mungu waliyemfanya ni mshirika wa masanamu.
Kwa hiyo haikuwa rahisi kubadili itikadi yao hii. Wao walikuwa wakijitolea kwa pumzi zao zote, kama ikitajwa kwa ubaya imani yao hiyo.
Ndipo ikalazimika kukaririka huko na kusisitiza na kufananua. Hebu tufaradhie mtu mmoja wa kanisa ajaribu kuondoa picha na sanamu ndani ya kanisa. Je, itatosha aseme tu, hizi ni karatasi na mawe au itabidi atoe hotuba ndefu na pana?
خُذِ الْعَفْوَ وَأْمُرْ بِالْعُرْفِ وَأَعْرِضْ عَنِ الْجَاهِلِينَ ﴿١٩٩﴾
199. Shika usamehevu na amrisha mema na achana na wajinga.
وَإِمَّا يَنزَغَنَّكَ مِنَ الشَّيْطَانِ نَزْغٌ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ إِنَّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴿٢٠٠﴾
200. Na kama uchochezi wa shetani ukikuchochea, basi jikinge kwa Mwenyezi Mungu; hakika yeye ndiye asikiaye na ajuaye.
إِنَّ الَّذِينَ اتَّقَوْا إِذَا مَسَّهُمْ طَائِفٌ مِّنَ الشَّيْطَانِ تَذَكَّرُوا فَإِذَا هُم مُّبْصِرُونَ ﴿٢٠١﴾
201. Hakika wale wanye takuwa zinapowagusa pepesi za shetani huzinduka.
وَإِخْوَانُهُمْ يَمُدُّونَهُمْ فِي الْغَيِّ ثُمَّ لَا يُقْصِرُونَ ﴿٢٠٢﴾
202. Na ndugu zao wanawavutia katika upotofu kisha wao hawaachi.
وَإِذَا لَمْ تَأْتِهِم بِآيَةٍ قَالُوا لَوْلَا اجْتَبَيْتَهَا قُلْ إِنَّمَا أَتَّبِعُ مَا يُوحَىٰ إِلَيَّ مِن رَّبِّي هَـٰذَا بَصَائِرُ مِن رَّبِّكُمْ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ ﴿٢٠٣﴾
203. Na usipowaletea ishara, husema: "Kwa nini hukuibuni?" Sema: Hakika nafuata niliyopewa wahyi kutoka kwa Mola wangu tu. Hizi ni busara zitokazo kwa Mola wenu na ni uwongofu na rehema kwa watu wanaoamini.
SHIKA USAMEHEVU
Aya 199 – 203
MAANA
Shika usamehevu na amrisha mema na achana na wajinga.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimfunza tabia njema Mtume wake Nabii Muhammad(s.a.w.w)
, naye alikuwa akisema katika dua yake: “Ewe Mwenyezi mungu nifanye mzuri wa maumbile na tabia na niepushe na tabia mbaya.” Alimwitikia dua yake na akamtimizia tabia njema kisha akamtuma kutimiza tabia njema kwa watu wote.
Aya hii ni miongoni mwa mafunzo ya Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake mtukufu(s.a.w.w)
. nayo imekusanya misingi mitatu ya sharia na adabu.
USAMEHEVU
Nao ni kuchukulia upole bila uzito wala mashaka. Nako kunakua katika vitendo na hulka. Na katika mali ni ile iliyozidi haja.
Mwenyezi Mungu amemwamrisha Mtume wake kutowatia kwenye uzito na mashaka katika anayowaamrisha na kuwakataza. Na kuchukua Zaka ya mali yao katika kinachozidi haja zao. Huu ni msingi katika misingi ya sharia.
وَمَا جَعَلَ عَلَيْكُمْ فِي الدِّينِ مِنْ حَرَجٍ ﴿٧٨﴾
“Wala hakuweka juu yenu uzito katika dini” (22:78)
Na pia alimwamrisha kutowakalifisha hulka; kama kumwamrisha mmoja wao asamehe deni lake au asichukue kisasi.
KUAMRISHA MEMA
Ni kheri inayojulikana na iliyo wazi anayoijua mtu kwa umbile lake.
NA ACHANA NA WAJINGA
Wale ambao hakutarajiwi kuongoka kwao kwa hoja na dalili wala kwa mawaidha na uongozi. Huenda ikawa kuwapuuza na kuachana nao ni vizuri kuliko kuwaongoza.
Amesema Sheikh Maraghi katika tafsir ya Aya hii: “Imepokewa kutoka kwa Jafar As-Sadiq (r.a) kwamba yeye amesema: “Hakuna katika Qur’an Aya inayokusanya maadili mema kama hii.”
Na kama uchochezi wa shetani ukikuchochea, basi jikinge kwa Mwenyezi Mungu; hakika yeye ndiye asikiaye na ajuaye.
Mtume hukasirika, hilo halina shaka, lakini yeye anakasirika kwa ajili ya Mwenyezi Mungu; hata kukasirika kwa nafsi yake ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Huenda akakasirikia ujinga wa mjinga katika alioamrishwa kuachana nao na kutaka kumkabili kwa neno litakalomstahiki.
Ndipo Mwenyezi Mungu mtukufu akamwambia kwa kumfundisha: Ikisadifu kukutokea mfano wa hali hii, basi ghadhabu isiondoe upole wako, vumilia na mtake hifadhi Mwenyezi Mungu, kwani yeye anakusikia na kukuitikia na anajua yanayokupata kutoka kwa wajinga.
Hapana budi kuishiria kuwa kauli yake hii Mwenyezi Mungu ni kiasi cha kukadiria tu, kutokana na neno ‘kama’ sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu:
لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ ﴿٦٥﴾
”Kama ukishirikisha, hakika amali zako zitapomoka na utakuwa miongoni mwa wenye hasara. (39:65).
Kimsingi ni kwamba kukadiri muhali sio muhali. Katika Juz.3 (3:60) kifungu ‘Mtume na Isma’, tumebainisha kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) anaweza kuwakataza maasi Mitume wake walio maasum; Kwa sababu kukataza kwake kunatoka juu kuja chini; na wala haijuzu kwa yeyote, asiyekuwa Mwenyezi Mungu, kuwaamrisha au kuwakataza.
Hakika wale wenye takuwa zinapowagusa pepesi za shetani huzinduka.
Hakuna mtu asiyeshindana na misukumo ya kibinafsi, baadhi yake ni ya tamaa ya moyo, mingine ni ya akili na pia ya kidini.
Mara nyingi dini na akili hushindwa na msukumo wa moyo. Kwa sababu unachimbuka katika dhati ya mtu, na unakuwa naye tangu yuko tumboni mwa mama yake.
Na akili inakuja baadae, nayo hukua kwa mafunzo na majaribio. Ama dini imeletwa kuuzoeza msukumo wa moyo na kuufunga hatamu.
Nayo utendaji kazi wake ni dhaifu, isipokuwa tu kwa mtu aliyekinai kwa nafsi yake na dhati yake, kwa namna ambayo haoni wema, isipokuwa wa dini na kufanya amali kulingana na hukumu zake.
Aina hii ya wanadini ndio wale ambao dini yao inashinda mapondokeo yao. Ndio wanokusudiwa na kauli yake Mwenyezi Mungu: “Zinapowagusa pepesi za shetani huzinduka” Yaani shetani akiwahadaa kwa maasia ya Mwenyezi Mungu au akiwapa wasiwasi wa nafsi inayoamrisha uovu, basi hukumbuka aliyowaamrisha Mwenyezi Mungu na aliyowakataza. Mara wao hutambua vitimbi vya shetani na wasiwasi wa nafsi, basi hujizuia na maasi na dini yao hushinda hawa zao.
Na ndugu zao wanawavutia katika upotofu kisha wao hawaachi.
Makusudio ya ndugu hapa ni mashetani. Dhamir ya ndugu zao inarudia kwa washirikina ambao wametajwa. Makusudio ya hawaachi, ni kuwa shetani haachi kuwapoteza washirikina na kuwaharibu. Kwa ufupi ni kwamba mashetani ndio ndugu wa washirikina hawaachi kuwapoteza.
Na usipowaletea ishara, husema: Kwa nini hukuibuni?
Washirikina walikuwa wamemtaka Mtume miujiza maalum kwa njia ya inadi. Kama hakuwaletea muujiza huo husema: Kwani huwezi kuufanya mwenyewe, kwani wewe si ni Mtume?
Sema: Hakika nafuata niliyopewa wahyi kutoka kwa Mola wangu tu.
Yaani sema ewe Muhammad kuwaambia hawa wenye inadi: Ndio mimi ni Mtume, lakini Mtume hatengenezi muujiza wala haonyeshi ishara yoyote au kuipendekeza kwa Mwenyezi Mungu; bali anangoja wahyi na kuufik- isha kwa waja wake.
Hii ni busara zitokazo kwa Mola wenu na ni uwongofu na rehema kwa watu wanaoamini.
Hii ni ishara ya Qur’an na busara ni hoja na dalili ambazo mwenye akili anapata busara kwazo.
Baada ya Mtume(s.a.w.w)
kuwaambia washirikina kuwa nafuata niliyope- wa wahyi kutoka kwa Mola wangu, aliwaambia, na Mwenyezi Mungu amenipa wahyi hii Qur’an ambayo ina dalili wazi za utume wangu. Nayo ni uwongofu na rehema kwa anayetaka kuamini haki kwa njia ya haki.
Mkiwa mwaitafuta haki, kama mnavyodai, basi acheni shirk na msilimu. Vinginevyo basi nyinyi ni watafutaji manufaa na watu wa malengo yenu tu.
وَإِذَا قُرِئَ الْقُرْآنُ فَاسْتَمِعُوا لَهُ وَأَنصِتُوا لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴿٢٠٤﴾
204. Na isomwapo Qur’an isikilizeni na mnyamaze ili mpate kurehemiwa.
وَاذْكُر رَّبَّكَ فِي نَفْسِكَ تَضَرُّعًا وَخِيفَةً وَدُونَ الْجَهْرِ مِنَ الْقَوْلِ بِالْغُدُوِّ وَالْآصَالِ وَلَا تَكُن مِّنَ الْغَافِلِينَ ﴿٢٠٥﴾
205. Na mtaje Mola wako nafsini mwako kwa unyenyekevu na hofu na bila ya kupiga kelele kwa kauli, asubuhi na jioni, Wala usiwe miongoni mwa walioghafilika.
إِنَّ الَّذِينَ عِندَ رَبِّكَ لَا يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِهِ وَيُسَبِّحُونَهُ وَلَهُ يَسْجُدُونَ
۩﴿٢٠٦﴾
Hakika wale walioko kwa Mola wako hawajivuni wakaacha kumwabudu na wanamtakasa na wanaumsujudia.
ISOMWAPO QUR’AN ISIKILIZENI
Aya 204 – 206
MAANA
Na isomwapo Quar’an isikilizeni na mnyamaze ili mpate kurehemiwa.
Alipotaja Mwenyezi Mungu (s.w.t) katika Aya iliyotangulia kwamba hii Qur’an ni busara na uwongofu na rehema, anaamrisha katika, Aya hii, kuisikiliza na kunyamaza ili kuzingatia uwongofu na dalili zilizomo. Hapana shaka kwamba mwenye kuizingatia vyema Qur’an na akawaidhika nayo, basi yeye anastahiki rehema ya Mwenyezi Mungu na radhi zake.
Wameafikiana mafakihi, isipokuwa wa madhebu ya Dhahiriya, kwamba kuinyamazia Qur’an ni sunna na wala sio wajibu kwa asiyekuwa Maamuma anayeswali nyuma ya Imam.
Wamehitalifiana kuhusu Maamuma, kuwa je, ni wajibu asikilize na amnyamazie Imam akiwa anasoma Qur’an? Kuna kundi lililosema kuwa ni wajibu na wengine wakasema si wajibu.
Kwa hali yoyote iwavyo, ni kwamba amri katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
‘Isikilizeni’ na nyamazeni’ ni ya kupendekeza sio ya wajibu. Kwa sababu amri hii hukumu yake ni kama hukumu ya Aya inyofuatia (Na mtaje Mola wako moyoni mwako…) Kwa sababu, zote mbili zimekuja katika mfumo mmoja. Na amri ya kutaja ni ya sunna, kwa hiyo pia amri ya kusikiliza na kunyamaza.
Zaidi ya hayo ni kwamba kumnyamazia kila msomaji ni jambo zito na lenye mashaka; hasa hivi sasa ambapo kusomwa Qur’an katika vipaza sauti ni kama mchezo na nyimbo; watu hupaaza sauti kukiwa na tukio na hata kama hakuna.
Na mtaje Mola wako nafsini mwako kwa unyenyekevu na hofu na bila ya kupiga kelele kwa kauli, asubuhi na jioni.
Msemo katika ‘Mtaje’ unaelekezwa kwa Nabii Muhammad na makusudio ni kwa wote. ‘Bila ya kupiga kelele’ maana yake ni mtaje Mola wako kwa sauti ya katikati baina ya sauti kubwa na ndogo. Na asubuhi na jioni ni fumbo la kudumu kumtaja na kumkumbuka.
Kauli yake Mwenyezi Mungu ‘Bila ya kupiga kelele’ inafahamisha wazi kwamba mtu anayeinua sauti yake kwa kusoma Qur’an basi ameacha mapendekezo na kufanya kinyume; hasa ikiwa ni kwa kuwasumbua wali- olala.
Wala usiwe miongoni mwa walioghafilika na kumtaja Mwenyezi Mungu katika nafsi yako.
Kwa sababu kumtaja kwa ulimi tu, kunafanana na maneno matupu yasiyo kuwa na maana. Maana ya kumtaja Mwenyezi Mungu mtukufu katika nafsi ni kujua kwamba Mwenyezi Mungu peke yake ndiye muumba mwenye kuruzuku mwenye kutoa uhai na mwenye kufisha na mwenye kuanzisha na kurud- isha.
Kumtaja kuliko bora ni kuogopa mtu kumfanyia ubaya ndugu yake binadamu kwa kuhofia mateso ya Mwenyezi Mungu; na bora zaidi kwake ni kumfanyia wema kwa kutaraji thawabu za Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Tunasema bila ya kusita kuwa; haya ndiyo makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu:
وَلَذِكْرُ اللَّـهِ أَكْبَرُ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ مَا تَصْنَعُونَ ﴿٤٥﴾
“Na kwa hakika kumbuko la Mwenyezi Mungu ni (jambo) kubwa kabisa, Na Mwenyezi Mungu anajua mnayoyatenda”
(29:45)
Kauli yake: “anajua mnayoyatenda” baada ya kusema “na kumbuko la Mwenyezi Mungu ni kubwa”, kunatilia nguvu kuwa kumtaja na kumkumbuka Mwenyezi Mungu ni kuwafanyia wema waja wa Mwenyezi Mungu.
Na mwenye hasara zaidi katika watu mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule anayefanya Tahlili na takbira, na huku anafanya ufisadi katika nchi kwa kudanganya na hadaa na kuwasaidia mataghuti na wakoloni dhidi ya waja wanyonge wa Mwenyezi Mungu wasio na hatia.
Hakika wale walioko kwa Mola wako hawajivuni wakaacha kumwabudu na wanamtakasa na wanamsujudia.
Wafasiri wanasema kuwa Mwenyezi Mungu amewakusudia Malaika,Wametoa dalili ya neno walioko kwa Mola wako. Kwa sababu walioko kwa Mwenyezi Mungu ni Malaika.
Lakini inawezekana kwamba makusudio ni kila mwenye nafasi na jaha mbele ya Mwenyezi Mungu; ni sawa awe ni Malaika au mwanadamu.
Wametofautiana mafakihi, kuwa je ni wajibu, kusujudu wakati wa kusomwa Aya iliyo na neno
‘Wanasujudi’, kama hii?
Amenukuu Tabrasi kauli kutoka kwa Hanafi kuwa ni wajib na kutoka kwa Shafii na Shia Imamiya kuwa ni sunna yenye kutiliwa mkazo.
Ikumbukwe kuwa Shia Imamia wamewajibisha kusujudi msomaji na msikilizaji zinaposomwa Aya zilizo katika Sura nne: 32, 41, 53 na 96.
MWISHO WA SURA YA SABA