12
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA
وَاتَّقُوا فِتْنَةً لَّا تُصِيبَنَّ الَّذِينَ ظَلَمُوا مِنكُمْ خَاصَّةً وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ ﴿٢٥﴾
25. Na jikingeni na fitna ambayo haitawasibu wale waliodhulumu miongoni mwenu peke yao, na jueni kuwa Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.
وَاذْكُرُوا إِذْ أَنتُمْ قَلِيلٌ مُّسْتَضْعَفُونَ فِي الْأَرْضِ تَخَافُونَ أَن يَتَخَطَّفَكُمُ النَّاسُ فَآوَاكُمْ وَأَيَّدَكُم بِنَصْرِهِ وَرَزَقَكُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴿٢٦﴾
26. Nakumbukeni mlipokuwa wachache, mkionekana wadhaifu katika nchi; mkawa mnaogopa watu wasiwanyakue; akawapa makao na akawatia nguvu kwa nusura yake na akawapa riziki njema ili mpate kushukuru.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَخُونُوا اللَّـهَ وَالرَّسُولَ وَتَخُونُوا أَمَانَاتِكُمْ وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿٢٧﴾
27. Enyi mlioamini! Msimfanyie hiyana Mwenyezi Mungu na Mtume na mkahini amana zenu na hali mnajua.
وَاعْلَمُوا أَنَّمَا أَمْوَالُكُمْ وَأَوْلَادُكُمْ فِتْنَةٌ وَأَنَّ اللَّـهَ عِندَهُ أَجْرٌ عَظِيمٌ ﴿٢٨﴾
28. Na jueni kwamba mali zenu na watoto wenu ni fitna. Na hakika kwa Mwenyezi Mungu yako malipo makubwa.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن تَتَّقُوا اللَّـهَ يَجْعَل لَّكُمْ فُرْقَانًا وَيُكَفِّرْ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ وَاللَّـهُ ذُو الْفَضْلِ الْعَظِيمِ ﴿٢٩﴾
29. Enyi mlioamini! Mkimcha Mwenyezi Mungu atawajaalia upaambanuzi, na atawafutia makosa yenu na atawasamehe; na Mwenyezi Mungu ni mwenye fadhila kuu.
OGOPENI ADHABU
Aya 25 – 29
LUGHA
Neno Fitna lina maana nyingi, miongoni mwa maana hizo ni adhabu ambayo ndiyo makusudio yake katika Aya hii ya 25. Ama katika Aya 28, makusudio yake ni mapenzi na hawaa zinazozuia haki. Makusudio ya upambanuzi ni mwongozo.
MAANA
Na jikingeni na fitna ambayo haitawasibu wale waliodhulumu mion- goni mwenu peke yao, na jueni kuwa Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.
Ni tahadhari inayotoka kwake Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kila mfitini anayeharibu nchi; hasa wale wanaoeneza farakano na kuvuruga amani na kuwachokoza wanyonge. Hadhari ni kwamba ubaya wa adhabu hautaishia kwa madhalimu tu, bali utaenea katika jamii yote na kumwenea mwema na mwovu.
Imeelezwa katika Tafsir Tabari akimnukuu Sadiy, ambaye ni mfasiri mkubwa, kwamba Aya hii inafungamana na watu wa (Vita vya Jamal) ngamia ambao walimpiga vita Ali bin Abu Talib.
Ametaja Razi katika kufasiri Aya hii: “Zubeir siku moja alikuwa akibarizi na Mtume(s.a.w.w)
mara akatokea Ali (r.a), Zubeir akamcheka. Mtume wa Mwenyezi Mungu akamwambia: “Vipi unavyompenda Ali?” Akajibu “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu ninapenda kama ninavyompenda mwanangu au zaidi. Mtume akamwambia:‘’Utakuwaje ukienda kupigana naye?
Vilevile imeelezwa katika Tafsiru Tabari: “Zubeir bin Al-a’wam alisema: “Tumesoma Aya hii zama zilizopita, lakini hatukuwaona wanaohusika nayo, mara sisi ndio tunahusika nayo”.
Na kumbukeni mlipokuwa wachache, mkionekana wadhaifu katika nchi; mkawa mnaogopa watu wasiwanyakue; akawapa makao na akawatia nguvu kwa nusura yake na akawapa riziki njema ili mpate kushukuru.
Maneno wanaambiwa Maswahaba wa Mtume(s.a.w.w)
. Mwenyezi Mungu mtukufu anawakumbusha udhaifu na hofu waliyokuwa nayo kabla ya Uislamu. Vilevile udhalili na ufukara, na jinsi alivyowapa amani utajiri na utukufu baada ya Uislamu, kwa vile wao wameitikia mwito wa maisha waliyopewa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake.
Lengo la ukumbusho huu ni kuwa waendelee na utiifu na kuitikia mwito wa uhai, ili waishi wakiwa wenye nguvu na heshima. Na kwamba wao pindi tu wakikengeuka na kuasi watarudia unyonge na udhalili waliokuwa nao wenzao, kama ilivyo hali ya waislamu leo, hasa waarabu.
Enyi mlioamini! Msimfanyie hiyana Mwenyezi Mungu na Mtume.
Kumfanyia hiyana Mwenyezi Mungu sio kuacha kufunga na kuswali tu; isipokuwa hiyana kubwa ni kuufanyia hiyana umma na nchi, kwa kuwatawalisha mataghuti kwenye sehemu za uongozi wakatawala nchi na huku tunawavumilia na kuwanyamazia bila ya kuwapiga vita.
Na mkahini amana zenu.
Yaani wala msihini amana zenu, Wafasiri wengi wamesema kuwa ukatazo huu ni wa hiyana ya amana ya mangiliano ya kimali baina ya watu. Hakuna mwenye shaka kwamba kurudisha amana ni wajibu na kuifanyia hiyana ni haramu, lakini hiyana kubwa ni kuacha kusaidiana na wanyonge kurudisha haki zao kutoka kwa wenye nguvu walio madhalimu.
Na hali mnajua.
Hakuna mjeuri zaidi kwa Mwenyezi Mungu kuliko yule anayemuasi Mwenyezi Mungu kwa makusudi hali anajua.
Jueni kwamba mali zenu na watoto wenu ni fitna.
Imekuja Aya hii baada ya makatazo ya hiyana ili kumzindua Mumini kwamba haitakikani mali na watoto wamzuie kutekeleza wajibu wake kwa umma na nchi mbele ya Mungu. Makusudio ya fitna hapa ni mapenzi yanayozuia haki na kheri.
Imepokewa Hadith kutoka kwa Mtume(s.a.w.w)
amesema: “Mtoto ni tunda la moyo. Na yeye ni mahali pa woga, ubahili na huzuni” Sawa na mali ambayo ni matunda ya jasho na mkono.
Ni woga kwa sababu, mwenye nayo huhofia kusema haki na kufanya kwa kuihofia; kama ambavyo anahofia juu ya mtoto wake.
Ni ubahili, kwa sababu mwenye kuimiliki anakuwa na pupa nayo na uchoyo; kama anavyokuwa na pupa na mtoto wake.
Nayo ni huzuni kwa sababu mwenye kuikusanya huhuzunika ikipatwa na jambo; kama anavyohuzunika likipatwa na jambo tunda la moyo wake.
Maneno mazuri niliyosoma kuhusu maudhui haya ni shairi la bedui mmoja akisema:
• Alikuwa fukara
• Akatajirika akapenda mali uchu ukamshika
• Akitaka kutumia huhuzunika
Na hakika kwa Mwenyezi Mungu yako malipo makubwa.
Mwenye akili hupendelea malipo haya na kuyahangaikia kwa juhudi na amali njema; wala haathiriki na mali inayokwisha na mtoto asiyebakia.
Enyi mlioamini! Mkimcha Mwenyezi Mungu atawajalia upaambanuzi.
Mara nyingi sana mtu anakuwa mateka wa matamanio. Humgeuzia zuri likawa baya na baya likawa zuri. Mara nyingi hilo huwa katika mambo yanayohusiana na mali na watoto ambapo matamanio hufikia kilele chake.
Kwa ajili hii ameamrisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) takuwa baada ya kuhadharisha fitna ya mali na watoto. Ama upambanzi, yaani mwongozo, anaowapa Mwenyezi Mungu wenye kumcha ili wapambanue haki na batili, ni natija ya kujikomboa na hawa na matamanio.
Kwa sababu, matamanio hupofusha na hutia uziwi.
Kunasibisha mwongozo kwa Mwenyezi Mungu ni kuwa yeye ndiye aliyeuwekea dalili. Mwenye kuzichunguza vizuri, akiwa hana malengo mengine yoyote isipokuwa kutafuta mwongozo wa haki, basi ataifikia tu.
Na atawafutia makosa yenu na atawasamehe; na Mwenyezi Mungu ni mwenye fadhila kuu.
Wafasiri wanasema kuwa makusudio ya kufutiwa makosa ni kusitiriwa duniani; na kusamehewa ni kusamehewa akhera, Wamesema hivi kukimbia kukaririka.
Ama sisi hatukimbii kukarika Qur’an na tumebainisha njia yake katika Juz.1 Maana ya Aya yote ni kuwa mwenye kumcha Mwenyezi Mungu atampa mwongozo, msamaha na thawabu.
Hilo kwa Mwenyezi Mungu si kubwa. Kwa sababu ni mkuu wa fadhila na kutoa kwake ni sahali kunamfikia kila mwenye kutafuta na kutaka radhi zake.
وَإِذْ يَمْكُرُ بِكَ الَّذِينَ كَفَرُوا لِيُثْبِتُوكَ أَوْ يَقْتُلُوكَ أَوْ يُخْرِجُوكَ وَيَمْكُرُونَ وَيَمْكُرُ اللَّـهُ وَاللَّـهُ خَيْرُ الْمَاكِرِينَ ﴿٣٠﴾
30. Na walipokupangia njama wale waliokufuru ili wakufunge au wakuue au wakutoe. Na wakapanga njama na Mwenyezi Mungu akapanga njama. Na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa kupanga njama.
وَإِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ آيَاتُنَا قَالُوا قَدْ سَمِعْنَا لَوْ نَشَاءُ لَقُلْنَا مِثْلَ هَـٰذَا إِنْ هَـٰذَا إِلَّا أَسَاطِيرُ الْأَوَّلِينَ ﴿٣١﴾
31. Na wanaposomewa Aya zetu, husema: Tumekwishasikia, na lau tungependa tungelisema kama haya. Haya si chochote ila ni ngano tu za watu wa kale.
وَإِذْ قَالُوا اللَّـهُمَّ إِن كَانَ هَـٰذَا هُوَ الْحَقَّ مِنْ عِندِكَ فَأَمْطِرْ عَلَيْنَا حِجَارَةً مِّنَ السَّمَاءِ أَوِ ائْتِنَا بِعَذَابٍ أَلِيمٍ ﴿٣٢﴾
32. Na waliposema: Ewe Mwenyezi Mungu! Ikiwa haya ni haki itokayo kwako, basi tupige mvua ya mawe kutoka mbinguni au tuletee adhabu iumizayo.
وَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيُعَذِّبَهُمْ وَأَنتَ فِيهِمْ وَمَا كَانَ اللَّـهُ مُعَذِّبَهُمْ وَهُمْ يَسْتَغْفِرُونَ ﴿٣٣﴾
33. Na Mwenyezi Mungu hakuwa ni mwenye kuwaadhibu maadamu wewe umo pamoja nao. Wala hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwaadhibu hali wanaomba msamaha.
وَمَا لَهُمْ أَلَّا يُعَذِّبَهُمُ اللَّـهُ وَهُمْ يَصُدُّونَ عَنِ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ وَمَا كَانُوا أَوْلِيَاءَهُ إِنْ أَوْلِيَاؤُهُ إِلَّا الْمُتَّقُونَ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٣٤﴾
34. Na wana jambo gani hata Mwenyezi Mungu asiwaadhibu; hali wao wanazuilia (watu) msikiti mtakatifu? Wala wao hawakuwa ndio walinzi wake. Hawakuwa walinzi wake isipokuwa wenye takuwa tu, lakini wengi wao hawajui.
وَمَا كَانَ صَلَاتُهُمْ عِندَ الْبَيْتِ إِلَّا مُكَاءً وَتَصْدِيَةً فَذُوقُوا الْعَذَابَ بِمَا كُنتُمْ تَكْفُرُونَ ﴿٣٥﴾
35. Na haikuwa Swala yao kwenye hiyo nyumba ila miluzi (kupiga mbinja) na makofi. Basi onjeni adhabu kwa sababu ya yale mliyokuwa mkikufuru.
WALIPOKUFANYIA VITIMBI
Aya 30 – 35
LUGHA
Njama ikinasibishwa kwa mtu maana yake ni hila na hadaa. Na ikinasibishwa kwa Mwenyezi Mungu maana yake ni kuvunja njama.
MAANA
Na walipokupangia njama wale waliokufuru ili wakufunge au wakuue au wakutoe.
Katika Aya iliyotangulia (26) Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewakumbusha Waislamu neema yake juu yao. Katika Aya hii anamkumbusha Mtume(s.a.w.w)
neema yake juu yake ambapo Washirikina wa Kiquraish walikubaliana kummaliza Nabii Muhammad(s.a.w.w)
, Wakatofautiana katika njia ya kummaliza, Mmoja akasema tumfunge, mwingine akasema tumtoe Makka.
Kisha wakaafikiana wachague mtu katika kila ukoo na waivamie nyumba yake akiwa amelala kitandani wampige kwa panga zao pigo moja. Hapo damu yake itakuwa kwa koo zote, na Bani Hashim watashindwa kupigana na waarabu wote.
Wafasiri wanasema, akiwemo Tabari, Razi, na Abul Hayaan Al-Andalusi, kwamba; Mwenyezi Mungu alimpa wahyi Mtume wake kumjulisha hilo. Akamwamrisha atoke kuelekea Madina na akamwamrisha Ali bin Abu Talib alale kitandani kwake. Ali akalala kitandani kwake na kujifinika shuka yake. Walipovamia kitanda chake walimwona Ali, wakapigwa na mshangao. Pia Mtume alimwusia Ali kurudisha amana za watu walizoziweka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu.
Na wakapanga njama na Mwenyezi Mungu akapanga njama na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa kupanga njama.
Njama ya Maquraish ni ile mipango yao ya kumuua Nabii Muhammad kwa namna ambayo ukoo wa Hashim utashindwa kulipizia kisasi. Ama njama ya Mwenyezi Mungu ni kupangua njama yao kwa kupanga Mwenyezi Mungu (s.w.t) Mtume atoke, na Ali alale kitandani kwake, Yametangulia maelezo kuhusu hayo katika kufasiri Juz.3 (3:54).
Na wanaposomewa Aya zetu, husema: Tumekwishasikia. Na lau tungependa tungelisema kama haya. Haya si chochote ila ni ngano tu za watu wa kale.
Maquraish walisema kuwa Qur’an ni ngano za watu wa kale, na kwamba wao wakitaka wanaweza kusema mfano wake. Walisema hivi wakiwa wanajua fika kwamba hiyo inatoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa sababu wao na watu wote walishindwa kuleta mfano wa hata Sura moja tu.
Maquraish wameshindwa ndio maana wanakimbilia uzushi, kuficha kushindwa kwao na upotevu wao; sawa na kila anayeshindwa kuikabili haki kwa hoja na mantiki.
Na waliposema: Ewe Mwenyezi Mungu! Ikiwa haya ni haki itokayo kwako, basi tupige mvua ya mawe kutoka mbinguni au tuletee adhabu iumizayo.
Baadhi ya watu wanaweza kung’angania dhambi kwa kiburi chao; sawa na wanavong’ang’ania dini au zaidi; mpaka wanafikia kuwa tayari kufa kuliko kukubali kushindwa, hata kama upande wa pili ni haki.
Wako tayari kuangamia na kuadhibiwa kuliko kuacha mafunzo yao na mila zao. Historia imetaja mifano mingi ya watu wa aina hiyo. Qur’an imetaja Firauni, watu wa Nuh, n.k.
Maquraish walipoitwa na Mtume kwenye Uislamu walisema: “Kama Muhammad ni mkweli basi itupige mvua ya mawe.” Yaani wanaona afadhali kuangamia kwa kupigwa mawe kuliko kumfuata Muhammad, hata kama ni Nabii.
Basi Mwenyezi Mungu akawajibu kwamba adhabu bado iko mbele yao na kwamba mlango bado uko wazi; na aliwapa muda kwa sababu moja aliy oiashiria kwa kauli yake:
Na Mwenyezi Mungu hakuwa ni mwenye kuwaadhibu maadamu wewe umo ndani yao.
Yaani Mwenyezi Mungu mtukufu hawaadhibu watu wa Makka maadamu Nabii Muhammad yuko. Hii ikiwa ni kumtukuza na kumwadhimisha.
Wala hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwaadhibu hali wanaomba msamaha.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kusema kuwa hatawaadhibu Maquraish maadam Nabii Muhammad yuko kwao, anasema kuwa, vilevile, hatawaadhibu wakiamini, ni sawa Nabii Muhammad awe nao au asiwe nao. Kauli yake hii Mwenyezi Mungu ni sawa na kauli yake nyingine:
مَّا يَفْعَلُ اللَّـهُ بِعَذَابِكُمْ إِن شَكَرْتُمْ وَآمَنتُمْ ﴿١٤٧﴾
“Mwenyezi Mungu ana haja gani ya kuwaadhibu kama mtashukuru na mtaamini” Juz.5 (4:147).
Makusudio ya maana haya yanafahamika kutokana na kusema kwake moja kwa moja.
Na wana jambo gani hata Mwenyezi Mungu asiwaadhibu?
Na pia kauli yake akiwaambia Maquraish:
Basi onjeni adhabu kwa sababu ya yale mliyokuwa mkikufuru.
Kwa ufasaha zaidi ni kuwa maana ya Aya ni kwamba, Yeye Mwenyezi Mungu hatawadhibu ikiwa Nabii Muhammad yuko kwao, Vilevile hatawaadhibu wakisilimu.
Ametumia neno msamaha kwa maana ya kusilimu, kwa sababu msamaha ni katika mambo yanayolazimiana na Uislamu, Kwa ufafanuzi huu, inatubainikia kuwa hakuna haja ya taawili walizozitaja wafasiri, tena zinamwacha msomaji gizani.
Na wana jambo gani hata Mwenyezi Mungu asiwaadhibu: hali wao wanazuilia (watu) msikiti mtakatifu?
Hilo ni swali lenye maana ya kukanusha; yaani hakuna chochote katika dini au tabia kitakachowazuia kuadhibiwa kwao. Kwani wao kwa upande wa ushirikina wao wanazuia waislamu kumwabudu Mwenyezi Mungu katika nyumba yake takatifu.
Mwislamu yeyote, hata Mtume(s.a.w.w)
alipokuwa Makka, hakuwa akiweza kuswali ndani ya Masjudil-Haram bila ya kupata udhia na mateso. Waliafikiana wamzuie Mtume kwa nguvu asifanye umra mwaka wa Hudaybiya.
Wala wao hawakuwa ndio walinzi wake.
Yaani washirikina si walinzi wa Masjidul Haram wala si watu wa nyumba hiyo, bali ni maadui wa Mwenyezi Mungu na maadui wa nyumba yake. Kwa hiyo ni wajibu kuwafukuza na kuwazuia, kwa vile wanauchafua kwa najisi zao na uchafu wao. Kwa ajili hii, Uislamu ulipopata nguvu, walizuiliwa kuukurubia:
إِنَّمَا الْمُشْرِكُونَ نَجَسٌ فَلَا يَقْرَبُوا الْمَسْجِدَ الْحَرَامَ بَعْدَ عَامِهِمْ هَـٰذَا ﴿٢٨﴾
“Hakika washirikina ni najisi, kwa hiyo wasiukaribie Msikiti mtakatifu baada ya mwaka wao huu” (9:28).
Hawakuwa walinzi wake isipokuwa wenye takuwa tu.
Yaani hatastahiki yeyote, vyovyote alivyo; kuusimamia Msikiti mtakatifu (Masjidul Haram) ila akiwa ni mwema mwenye kumcha Mungu akiwa Mwislamu aliyepiga shahada, Je, itakuwaje mshirikina na mwenye kupinga?
Ingawaje maudhui ya Aya yanahusika na msikiti mtakatifu, lakini takuwa ni sharti ya kila anayesimamia misikiti au sehemu za kidini. Kwa vile sababu ya hilo ni utwahara wa mahali na utakatifu wake. La kushangaza ni kwamba wengi wanaosimamia mambo haya ni wale viumbe waovu ambao ni mabingwa wa fani ya hila na wizi.
Lakini wengi wao hawajui
kwamba mwenye kusimamia msikiti na sehemu takatifu ni lazima awe mwema, mcha Mungu; na kwamba hakuna usimamizi kwa fasiki.
Utauliza
: kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na wana jambo gani hata Mwenyezi Mungu asiwaadhibu” inafahamisha kuwa Mwenyezi Mungu aliwaadhibu Maquraish, ambapo inajulikana kuwa hayakuwapitia kama yaliyowapitia watu wa Mitume waliotangulia, kama vile Ad, Thamud, watu wa Nuh, wa Lut n.k.?
Jibu
: Wale waliomuudhi Mtume na waislamu, Mwenyezi Mungu aliwaua siku ya Badr kwa mikono ya waislamu wenyewe. Miongoni mwa waliouwawa ni Abu Jahl, Uqba bin Abu Mui’t, Nadhr bin Al-Harith, Umayya bin Khalaf na wengineo katika vigogo vya Maquraish ambao walikuwa wamezidi mno kuwaudhi waislamu.
Kwa mfano Umayya bin Khalaf alikuwa akimmiliki Bilal mwadhini wa Mtume(s.a.w.w)
. Alikuwa akimwadhibu kwenye mchanga ulio moto sana na kumpa adhabu za kila aina. Siku ya Badr Umayya alitoka pamoja na washirikina, na Bilal naye akatoka pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu.
Mara tu, Bilal alipomwona Umayya alipiga ukelele: “Huyu kiongozi wa ukafiri, ama zake ama zangu.” Wakakusanyika baadhi ya wanyonge waliokuwa wakiteswa na huyu Umayya wakamshika; Bilal naye akampiga Umayya kwa upanga mpaka akamuua.
Akakichukua kichwa chake akakitungika kwenye upanga wake na huku akicheza kwa furaha.
Na haikuwa swala yao kwenye hiyo nyumba ila miluzi (kupiga mbinja) na makofi.
Kama kwamba mwulizaji anauliza: Maquraish walikuwa wakiswali katika msikiti mtukufu, sasa vipi wamestahiki adhabu? Akajibu Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwa swala yao ilikuwa ni vurugu tu, haina unyenyekevu.
Kwa sababu ilikuwa ni miluzi (mbinja) ya mdomoni na makofi ya mikononi.
Basi onjeni adhabu iliyowafikia siku ya Badr.
Na adhabu ya akhera ni kali zaidi.
Kwa sababu ya yale mliyokuwa mkikufuru.
Lau mngesilimu mngelisalimika na adhabu ya duniani na akhera.
إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا يُنفِقُونَ أَمْوَالَهُمْ لِيَصُدُّوا عَن سَبِيلِ اللَّـهِ فَسَيُنفِقُونَهَا ثُمَّ تَكُونُ عَلَيْهِمْ حَسْرَةً ثُمَّ يُغْلَبُونَ وَالَّذِينَ كَفَرُوا إِلَىٰ جَهَنَّمَ يُحْشَرُونَ ﴿٣٦﴾
36. Hakika wale waliokufuru hutoa mali zao ili kuzuilia njia ya Mwenyezi Mungu. Basi watazitoa, kisha zitakuwa majuto juu yao, kisha watashindwa. Na wale waliokufuru watakusanywa kwenye Jahanamu.
لِيَمِيزَ اللَّـهُ الْخَبِيثَ مِنَ الطَّيِّبِ وَيَجْعَلَ الْخَبِيثَ بَعْضَهُ عَلَىٰ بَعْضٍ فَيَرْكُمَهُ جَمِيعًا فَيَجْعَلَهُ فِي جَهَنَّمَ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ ﴿٣٧﴾
37. Ili Mwenyezi Mungu apate kuwapambanua walio wabaya na walio wazuri na kuwaweka wabaya juu ya wabaya wengine na kuwarundika wote pamoja na kuwatupa katika Jahanamu, Hao ndio waliohasirika.
قُل لِّلَّذِينَ كَفَرُوا إِن يَنتَهُوا يُغْفَرْ لَهُم مَّا قَدْ سَلَفَ وَإِن يَعُودُوا فَقَدْ مَضَتْ سُنَّتُ الْأَوَّلِينَ ﴿٣٨﴾
38. Waambie wale waliokufuru, kama watakoma, watasamehewa yaliyopita. Na wakirudia basi imekwishapita desturi ya watu wa zamani.
وَقَاتِلُوهُمْ حَتَّىٰ لَا تَكُونَ فِتْنَةٌ وَيَكُونَ الدِّينُ كُلُّهُ لِلَّـهِ فَإِنِ انتَهَوْا فَإِنَّ اللَّـهَ بِمَا يَعْمَلُونَ بَصِيرٌ ﴿٣٩﴾
39. Na piganeni nao mpaka kusiwe na fitna na dini yote iwe kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Wakikoma, basi hakika Mwenyezi Mungu anayaona wanayotenda.
وَإِن تَوَلَّوْا فَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ مَوْلَاكُمْ نِعْمَ الْمَوْلَىٰ وَنِعْمَ النَّصِيرُ ﴿٤٠﴾
40. Na wakigeuka, basi jueni kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mola wenu, ni Mola mwema na msaidizi mwema.
WALIOKUFURU HUTOA MALI ZAO
Aya 36 – 40
MAANA
Hakika wale waliokufuru hutoa mali zao ili kuzuilia njia ya Mwenyezi Mungu. Basi watazitoa, kisha zitakuwa majuto juu yao, kisha watashindwa. Na wale waliokufuru watakusanywa kwenye Jahanamu.
Washirikina walikuwa wakitoa mali zao katika kupigana na waislamu na kuzuilia watu Uslamu.
Ndipo Mwenyezi Mungu akabainisha, katika Aya hii, kwamba mali hizo zitawarudishia majuto, udhalili duniani na adhabu kali huko akhera. Kwa sababu mwisho ushindi utakuwa wa dini ya Mwenyezi Mungu na watu wake.
Ili Mwenyezi Mungu apate kuwapambanua walio wabaya na walio wazuri.
Hii ni sababu na kubainisha sababu yenye kuwajibisha majuto ya Washirikina na udhalili wao. Nayo ni kuwa Mwenyezi Mungu ni Mwadilifu na mwenye hekima.
Miongoni mwa uadilifu wake ni kutokuwa sawa mbele yake mwema na mwovu na Mu’min na kafiri, bali atampambanua kila mmoja na kumfanyia anayostahiki.
Kwa ajili hii, atampa thawabu mwema na kumwinua huko akhera. Na pengine humchanganyia malipo ya dunia na akhera. Na atamdhalilisha mwovu na kumwadhibu huko akhera kwenye nyumba ya hisabu na malipo. Pengine humpa aina fulani ya adhabu katika dunia kwa kadiri hekima yake inavyotaka.
Na kuwaweka wabaya juu ya wabaya wengine na kuwarundika wote pamoja na kuwatupa katika Jahanamu.
Makusudio ni jinsi ya wabaya; yaani wanaofungamana na jina hilo. Kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu.
Hao ndio waliohasirika.
Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu kesho atawakusanya wabaya wakiwa mrundo kisha awatupe katika Jahanamu, kama anavyofanya mtafuta kuni akizikusanya pamoja na kuzitia motoni. Mwenyezi Mungu anasema:
وَأَمَّا الْقَاسِطُونَ فَكَانُوا لِجَهَنَّمَ حَطَبًا ﴿١٥﴾
“Na ama wanaokengeuka (kuiacha haki) watakuwa kuni za Jahanamu.” (72:15).
Hao ndio waliohasirika.
Kuna hasara gani kubwa zaidi ya kuwa mtu na nyama zake na damu yake ni kuni za moto alioukoka Mwenyezi Mungu kwa ghadhabu yake juu ya aliyemfanyia hiyana Mola wake na dhamir yake!
“Ewe Mwenyezi Mungu! Hakika sisi tunaihofia adhabu yako, Na tunakimbilia kwako, Wewe ni mkarimu humfukuzi mwenye kutaka hifadhi ya ukarimu wako na kukimbilia rehema yako.”
Waambie wale waliokufuru, kama watakoma, watasamehewa yaliyopita.
Maneno haya anaambiwa Mtume(s.a.w.w)
. Mwenyezi Mungu anamwamrisha kuwapa mawaidha makafiri na kuwaambia mlango wa toba uko wazi mbele yao, na kwamba wamepewa fursa ya kuacha ukafiri na uadui kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, wakitubia basi Mwenyezi Mungu atawakubalia toba.
Kwa sababu Uislamu unakata yaliyokuwa kabla yake; kama ilivyoelezwa katika Hadith.
Na wakirudia basi imekwishapita desturi ya watu wa zamani.
Mfano wale waliokadhibisha Mitume na kuwapiga vita. Makusudio ya desturi ya Mwenyezi Mungu kwa waliopita – ni kuangamizwa makafiri, na Mitume kuwa washindi.
Mwenyezi Mungu amekwishandika: Hakika nitashinda mimi na Mitume wangu.
إِنَّ اللَّـهَ قَوِيٌّ عَزِيزٌ ﴿٢١﴾
“Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu, mwenye kushinda.” (58:21).
Na piganeni nao mpaka kusiwe na fitna na dini yote iwe kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Wakikoma, basi hakika Mwenyezi Mungu anayaona wanayotenda.
Makusudio ya Fitna hapa ni ukafiri. Aya imetangulia na tafsiri yake katika Juz.2 (2:193).
Na wakigeuka, basi jueni kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mola wenu, ni Mola mwema na msaidizi mwema.
Yaani kama washirikina wakipingana na ubainifu wa Mtume na amani yake, basi mjiizatiti enyi Waislamu wala msiwaogope. Kwani Mwenyezi Mungu atawasaidia na atawalinda; naye ni mbora wa walinzi na wasaidizi.
SHARTI YA KUCHAPA
Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein
Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini
ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.
MWISHO WA JUZUU YA TISA