1
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI
Mwendelezo Wa Sura Ya Nane: Surat Al-Anfal
وَاعْلَمُوا أَنَّمَا غَنِمْتُم مِّن شَيْءٍ فَأَنَّ لِلَّـهِ خُمُسَهُ وَلِلرَّسُولِ وَلِذِي الْقُرْبَىٰ وَالْيَتَامَىٰ وَالْمَسَاكِينِ وَابْنِ السَّبِيلِ إِن كُنتُمْ آمَنتُم بِاللَّـهِ وَمَا أَنزَلْنَا عَلَىٰ عَبْدِنَا يَوْمَ الْفُرْقَانِ يَوْمَ الْتَقَى الْجَمْعَانِ وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿٤١﴾
41. Na jueni kwamba chochote mlichopata ghanima, basi khumsi yake ni ya Mwenyezi Mungu na Mtume na jamaa na mayatima na masikini na msafiri. Ikiwa nyinyi mmemwamini Mwenyezi Mungu na tuliyoteremsha kwa mja wetu siku ya upambanuzi, siku yalipokutana majeshi mawili. Na Mwenyezi Mungu ni muweza juu ya kila kitu.
KHUMS
Aya 41
LUGHA
Neno; Ghanima kwa lugha ya kiarabu lina maana ya kupata kitu. Wametofautiana kuhusu maana ya Fay-u kwa kauli mbili: kauli ya Kwanza kuwa ni ghanima, na kauli ya pili kuwa ni mali inayochukuliwa bila ya vita.
Ama kuhusu Nafal yametangulia maelezo yake mwanzo wa Sura hii. Makusudio ya jamaa ni jamaa za Mtume. Yatima ni yule aliyefiwa na baba yake kabla ya kubaleghe. Na Khums ni humusi (sehemu moja ya tano).
MAANA
Na jueni kwamba chochote mlichopata ghanima, basi khumsi yake ni ya Mwenyezi Mungu na Mtume na jamaa na mayatima na masikini na msafiri.
Wafasiri wamefanya utafiti katika pande nyingi kuhusu Aya hii, Ama sisi tutatosheka na pande mbili tu:
Kwanza: dhahiri ya Aya inafahamisha pande hizo mbili.
Pili: kwamba upande mwingine hautumiki. Katika pande hizo mbili tutakazozitaja ni kueleza maana ya neno ghanima na kubainisha wale wanaostahiki Khumsi.
Wametofautiana Sunni na Shia kuhusu makusudio ya neno ghanima katika Aya. Sunni wamesema ni ngawira wanayoiteka waislamu kutoka kwa makafiri kwa vita.
Kulingana na kauli yao hii, suala la Khums linakuwa kwao halipo siku hizi; sawa na suala la utumwa. Kwa vile hakuna dola ya kiislamu inayopigana jihadi na makafiri na washirikina hivi sasa.
Shia wamesema kuwa ghanima ni zaidi ya ngawira ya vita inayochukuliwa na Waislamu kutoka kwa makafiri, na kwamba inakusanya madini; kama vile mafuta ya petroli, dhahabu nk. Vile vile dafina ikiwa haijulikani mwenyewe na wanavyovitoa watu kutoka baharini kwa kuzamia; kama vile lulu.
Nyingine ni mali inayozidi gharama za mtu yeye na watoto wake katika chumo la mwaka, mali ya halali iliyochanganyika na ya haramu na haijulikani kiwango cha haramu.
Pia ghanima ni ardhi aliyoinunua kafir dhimmi kutoka kwa Mwislamu. Ufafanuzi uko kwenye vitabu vya Fiqh, kikiwemo Fiqh Imam Jaffer As Sadiq Juz.2. Kulingana na kauli ya Shia suala ya khums linakuwa bado lipo.
Kama walivyotofautiana katika maana ya ghanima, vile vile wametofau- tiana katika idadi ya mafungu ya khums na wanaostahiki.
Shia wamesema: khums hugawanywa mafungu mawili: La kwanza litagawanywa mafungu matatu: Fungu la Mwenyezi Mungu, la Mtume wake na la jamaa. Lile la Mweneyzi Mungu ni la Mtume na la Mtume ni la jamaa zake.
Na msimamizi wa jamaa baada ya Mtume ni Imam anayesimamia kazi za Mtume. Akiweko atapewa yeye; kama hayuko basi ni wajibu kulitoa fungu hilo katika maslahi ya kidini, ambayo muhimu zake ni kuutangaza Uislamu na kazi ya kuusambaza na kuutukuza.
Ama fungu la pili, nalo lina sehemu ya mayatima wa ukoo wa Muhammad(s.a.w.w)
, masikini wao na wasafiri wao. Wanaohusika katika fungu hilo ni ukoo wa Muhammad(s.a.w.w)
tu peke yao, Kwa sababu Mwenyezi Mungu anawaharamishia sadaka akawawekea Khums.
Tabari katika tafsir yake na Abu Hayan Al-Andalus katika Bahrul-Muhit wanasema: “Amesema Ali bin Abu Talib
:Mayatima na maskini ni mayatima wetu.
Anaongeza Tabari: “Ali bin Hussein (r.a) alimwambia mtu mmoja kutoka Sham: Je, hukusoma katika Sura Anfal:“Na jueni kwamba chochote mlichopata ghanima, basi hakika khums yake ni ya Mwenyezi Mungu na Mtume na jamaa na mayatima na masikini na msafiri.
Akasema yule mtu: “Naam! Kwani ndiyo nyinyi? Akasema: ndiyo” Ama wasemavyo Sunni, tuwaachie maulamaa wawili wakubwa, mmoja wao ni wa zamani, Razi, na mwingine ni wa hivi karibuni, Maraghi, mmoja wa Masheikh wa Az-har na rais wake wakati wake.
Razi anasema: “Kauli zilizo mashuhuri ni kwamba hiyo humusi ni sehemu tano:
1. Mtume wa Mwenyezi Mungu.
2. Jamaa zake katika Bani Hashim, na Bani Muttwalib, sio Bani Abdu Shams (Umayya) na Bani Naufal.
3. Mayatima.
4. Masikini.
5. Wasafiri.
“Hiyo ni katika uhai wa Mtume wa Mwenyezi Mungu. Ama baada ya kufa kwake(s.a.w.w)
, kwa upande wa Shafii sehemu ni tano.
Ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, inatolewa kwenye maslahi ya Waislamu, ya jamaa matajiri na makufara, ilyobaki ni ya mayatima, maskini na wasafiri.
Abu Hanifa anasema kuwa sehemu ya Mtume wa Mwenyezi Mungu inaondoka baada ya kufa kwake kwa saba Na hugawanywa Khums kwa mayatima, maskini na wasafiri. Malik naye anasema: “Mambo ya khums huachiwa rai ya Imam.”
Sheikh Maraghi anasema: “Amepokea Bukhari kutoka kwa Mut’im bin Jubair wa Bani Nawfal, kwamba yeye alikwenda na Uthman bin Affan wa Bani Abd Shams kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
akawaambia: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Umewapa Bani Muttalib na ukatuacha na hali sisi na wao ni daraja moja. Akasema Mtume(s.a.w.w)
: “Hakika Bani Muttalib na Bani Hashim ni kitu kimoja.”
Sheikh Maraghi anaongezea juu ya Hadith hii kwa kusema, na siri ya hilo ni kwamba Makuraish walipoandika maazimio yao ya kuwatoa Bani Hashim Makka na kuwazuia katika Shii’b waliingia humo pamoja na Bani Muttalib, na wala hawakuingia Bani Abu Shams wala Bani Nawfal kwa uadui waliokuwa nao na Bani Hashim wakati wa Jahaliyya na wakati wa Uislamu.
Akawa Abu Sufyan anapigana na Mtume(s.a.w.w)
na kuungana na washirikina na watu wa Kitab dhidi yake, mpaka Mwenyezi Mungu alipompa ushindi Mtume wake na Waarabu wakaingia kwenye dini kwa ushindi wa Makka. Vile vile baada ya Uislamu Muawiya alimtokea Ali na akapigana naye.
Nasi tunaungia maneno ya Sheikh Maraghi kuwa vile vile Yazid mjukuu wa Abu Sufyan alimuuwa Hussein Bin Ali, mjukuu wa Mtume(s.a.w.w)
. Mshairi anasema kuhusu uadui huu wa kurithiana baba na babu.
Bin Harb na Mustwafa, Aliy na mwana wa Hind, Husein hawakumfaa, alipambana na Yazid
Ikiwa nyinyi mmemwamini Mwenyezi Mungu na tuliyoteremsha kwa mja wetu siku ya upambanuzi, siku yalipokutana majeshi mawili. Na Mwenyezi Mungu ni muweza juu ya kila kitu.
Wafasiri wanasema kuwa makusudio ya siku ya upambanuzi na siku yalipokutana majeshi mawili ni siku ya Badr. Kwa sababu Mwenyezi Mungu alifarikisha baina ya ukafiri na imani kwa kuuweka Uislamu juu ya shirk. Vile vile ni siku yalipokutana majeshi mawili, la waumini na la washirikina ambapo jeshi la washirikina waliipata.
Maana ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakubali kumwamini yeye, vitabu vyake na Mitume yake kama nadharia tu, bila ya vitendo, isipokuwa anakubali imani ya anayehukumu na kufanya amali kwa anavyohukumu Mwenyezi Mungu.
Razi anasema: “Kauli yake Mwenyezi Mungu: Mkiwa mmemwamini Mwenyezi Mungu, inafahamisha kuwa ikiwa haukupatikana ugavi huu, kama alivyohukumu Mwenyezi Mungu, basi imani nayo haipo.”
Nasi tunaongezea juu ya kauli ya Razi kuwa vile vile ikiwa hukumu haikupatikana katika usiokuwa ugavi huu, kama alivyohukumu Mwenyezi Mungu, basi imani nayo haitapatikana. Kwa vile, sababu inayowajibisha ukafiri ni moja nayo ni kuhalifu hukumu ya Mwenyezi Mungu makusudi. Kimisingi ni kwamba sababu hii haikubali kufungwa wala kuhusishwa na jambo moja tu.
Tumeeleza mara nyingi kwamba makusudio ya ukafiri katika mfano huu ni ukafiri wa kimatendo, yaani ufasiki sio ukafiri wa kiitikadi.
إِذْ أَنتُم بِالْعُدْوَةِ الدُّنْيَا وَهُم بِالْعُدْوَةِ الْقُصْوَىٰ وَالرَّكْبُ أَسْفَلَ مِنكُمْ وَلَوْ تَوَاعَدتُّمْ لَاخْتَلَفْتُمْ فِي الْمِيعَادِ وَلَـٰكِن لِّيَقْضِيَ اللَّـهُ أَمْرًا كَانَ مَفْعُولًا لِّيَهْلِكَ مَنْ هَلَكَ عَن بَيِّنَةٍ وَيَحْيَىٰ مَنْ حَيَّ عَن بَيِّنَةٍ وَإِنَّ اللَّـهَ لَسَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴿٤٢﴾
42. Mlipokuwa kando ya bonde lililo karibu, nao wako kando ya bonde lililo mbali; na msafara upo chini yenu, Na lau mngeliagana mngelihitalifiana katika miadi. Lakini ili Mwenyezi Mungu alitimize jambo lililokuwa lifanyike Ili aangamie wa kuangamia kwa dalili dhahiri na awe hai wa kuwa hai kwa dalili dhahiri. Na hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kusikia mwenye kujua.
إِذْ يُرِيكَهُمُ اللَّـهُ فِي مَنَامِكَ قَلِيلًا وَلَوْ أَرَاكَهُمْ كَثِيرًا لَّفَشِلْتُمْ وَلَتَنَازَعْتُمْ فِي الْأَمْرِ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ سَلَّمَ إِنَّهُ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ ﴿٤٣﴾
43. Alipokuonyesha katika usingizi wako kuwa ni wachache. Na lau angelikuonyesha kuwa ni wengi mngelivunjika moyo na mngelizozana katika jambo hilo, lakini Mwenyezi Mungu alilinda. Hakika yeye ni mjuzi wa yalimo vifuani.
وَإِذْ يُرِيكُمُوهُمْ إِذِ الْتَقَيْتُمْ فِي أَعْيُنِكُمْ قَلِيلًا وَيُقَلِّلُكُمْ فِي أَعْيُنِهِمْ لِيَقْضِيَ اللَّـهُ أَمْرًا كَانَ مَفْعُولًا وَإِلَى اللَّـهِ تُرْجَعُ الْأُمُورُ ﴿٤٤﴾
44. Na alipowaonyesha machoni mwenu mlipokutana kuwa ni wachache Na akawafanya nyinyi kuwa wachache machoni mwao ili Mwenyezi Mungu alitimize jambo lililokuwa lifanyike.
MLIPOKUWA KANDO YA BONDE LILILOKARIBU
Aya 42 – 44
MAANA
Aya hizi zinaonyesha baadhi ya sababu ambazo aliziandaa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ushindi wa waislamu kwa washirikina katika vita vya Badr. Miongoni mwa sababu hizo ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwapa ilhamu waislam kujiweka mwenye bonde lililo karibu na Madina. Ama washirikina wao walikuwa upande ulio mbali zaidi na hapa; na kati ya pande mbili kulikuwa na kilima kinachotenganisha.
Kulingana na mfumo wa maneno, inaonyesha kuwa upande wa waislamu ulikuwa ndio mahali pa vita walipomkusudia adui yao, Ni katika mipango yake Mwenyezi Mungu kuliweka kila jeshi mahali pake bila ya kujuana. Kwani lau waislamu wangeliwaona maadui zao kwa macho, wangeliogopa na kukata tamaa ya kuwashinda.
Vile vile ni katika mipango yake Mwenyezi Mungu, kwamba yeye – imetukuka hekima yake – aliwafanya wachache washirikina kwenye macho ya waislam walipokutana. Yote hayo ni kwa ajili kuidhirisha dini yake juu ya dini zote, hata kama watachukia washirikina.
Pia ni katika hekima yake kuwa Abu Sufyan aupeleka msafara wa ngamia kwenye mwambao wa bahari, ili majeshi mawili, ya batili na haki, yakutane na wala waislamu wasifuate msafara tu wakaacha jeshi.
Baada ya utangulizi huu, sasa tunaingilia kufasiri Aya:
Mlipokuwa kando ya bonde lililo karibu, nao wako kando ya bonde lililo mbali.
Msemo unatoka kwa Mwenyezi Mungu kuelekezwa kwa waislamu, akiwakumbusha mahali walipokuwa - kando ya bonde lililo karibu ya Madina, na mahali walipokuwa washirikina nao ni upande wa mbali: Vile vile anawakumbusha kugeuza njia kwa msafara wa ngamia kuelekea mwambao wa bahari, ambako Mwenyezi Mungu (s.w.t) amekuashiria kwa kauli yake:
Na msafara upo chini yenu.
Lengo la ukumbusho huu ni kwamba mambo yote yalikuwa kwa masilahi yao; kama ilivyobainika.
Na lau mngeliagana mngelihitalifiana katika miadi.
Waislamu walitoka pamoja na Mtume(s.a.w.w)
kufuatia msafara wa ngamia na mizigo yake, bila ya kukusudia kupigana, lakini Mwenyezi Mungu akaigeuza safari hii ya kufuatia mali kuwa ya kupigania jihadi katika njia yake.
Hilo likawa ni heri kubwa kwao. Lau kama tangu mwanzo wangelijua kuwa wanakwenda kupigana na washirikina; kisha wakajua wingi wao, basi baadhi ya waislamu wangeligeuka kwa hofu, na kutofautiana na wale watakaotaka kupigana, Matokeo yake ushindi usingelipatikana.
Lakini ili Mwenyezi Mungu alitimize jambo lililokuwa lifanyike.
Yaani lakini Mwenyezi Mungu alipanga kukutana huku bila ya ahadi, ili litimie alilokukusudia la kutukuka dini na kudhalilika washirikina.
Ili aangamie wa kuangamia kwa dalili dhahiri na awe hai wa kuwa hai kwa dalili dhahiri.
Makusudio ya mwenye kuangamia ni kafiri, na mwenye kuwa hai ni yule mwenye kuamini. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu aliwanusuru vipenzi vyake na kuwashinda nguvu maadui zake, siku ya Badr ili hilo liwe ni hoja mkataa kwa yule mwenye kupinga na hoja dhahiri kwa mwenye kuamini.
Utauliza
: Dhahiri ya Aya inaonyesha kuwa mwenye kushindana na haki atashindwa, lakini tujuavyo, wabatilifu mara nying si wanaishinda haki?
Jibu
: Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwaahidi ushindi waislamu kupitia kwa Mtume wake, kabla ya vita, ingawaje walikuwa wachache na wanyonge; kama alivyosema katika Aya ya 7 ya sura hii: “Na alipowaahidi moja ya makundi mawaili kuwa ni lenu.” Mwenyezi Mungu akatekeleza ahadi hiyo, ukathibiti muujiiza wa Muhammad(s.a.w.w)
aliyewapa habari ya ushin- di wakati ambapo dalili zote zilionyesha ni kinyume na hivyo.
Zaidi ya hayo walisaidiwa na malaika, kama inavyofahamisha Aya ya 9 na fumba la mchanga au changarawe alilowatupia mtume(s.a.w.w)
; kama ilivyo katika Aya ya 17. Yote haya na mengineyo yalikuwa ni muujiza wa wazi uliodhihiri mikononi mwa Muhammad, siku ya Badr. Na ndiyo makusudio ya dalili dhahiri kwa anayekufuru na dalili dhahiri kwa anayeamini; na wala sio ushindi tu.
Kwa maneno mengine ni kutoa habari ya ushindi kabla ya kutokea kwake pamoja na miujiza; na wala sio makusudio ya ushindi wenyewe.
Na hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kusikia mwenye kujua.
Hakifichuki chochote katika kauli na vitendo na yanayopita nyoyoni.
Alipokuonyesha katika usingizi wako kuwa ni wachache. Na lau angelikuonyesha kuwa ni wengi mngelivunjika moyo na mngelizozana katika jambo (hilo), lakini Mwenyezi Mungu alilinda.
Huu nao ni muujiza mwingine wa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
. Nao ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimwonyesha usingizini kwamba washirikina ni wachache tena madhaifu; na kushujaika. Lau Mwenyezi Mungu angelimuonyesha kuwa maadui wana nguvu, basi azma ya waislamu ingelidhoofika, wakawa wanyonge wa kupigana na kutofautiana. Hilo lingelifuatiwa na kushindwa. Lakini Mwenyezi Mungu alilinda tatizo hili na akawahurumia waja wake waumini.
Hakika yeye ni mjuzi wa yalimo vifuani.
Yaani anajua kuwa nyoyo za waislamu zitahisi hofu ya kupigana zikijua wingi wa adui; ndipo akiziweka mbali, Mwenyezi Mungu, hisia hizi kwa alivyoona Mtume uchache wa maadui usingizini.
Na alipowaonyesha machoni mwenu mlipokutana kuwa ni wachache ili muwe imara enyi waislamu, na muwe na ukakamavu na uthabiti katika kupigana na adui yenu. Na akawafanya nyinyi kuwa wachache machoni mwao ili wasijiandae sana kupigana nanyi na kuchukua hadhari.
Hivyo ndiyo ilivyokuwa; hata Abu Jahl akasema: “Watu wa Muhammad ni mboga tu.” Mwisho wa dharau hii ulikuwa ni balaa na udhalili.
Matukio yamethibitisha kuwa silaha kubwa iliyo mkononi mwa adui ni kudharau na kutojiandaa vizuri.
Ili Mwenyezi Mungu alitimize jambo lililokuwa lifanyike.
Wafasiri wamesema: Jumla hii imekaririka kwa vile sababu yake katika Aya ya kwanza ni kukusanyika waislamu na washirikina katika vita bila ya miadi. Ama sababu katika Aya hii imekuja kwa kufanyisha uchache kila kundi machoni mwa mwenzake.
Nasi tumetangulia kusema kuwa kukaririka katika Qur’an ni aina ya utangazaji uliofaulu.
Na kwa Mwenyezi Mungu hurejeshwa mambo yote.
Hutokea kwake na huishia kwake. Yeye ndiye mwenye kuyapanga kwa uadilifu wake na hekima yake.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا لَقِيتُمْ فِئَةً فَاثْبُتُوا وَاذْكُرُوا اللَّـهَ كَثِيرًا لَّعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٤٥﴾
45. Enyi mlioamini! Mnapokutana na jeshi, basi kazaneni, na mumkumbuke Mwenyezi Mungu sana ili mpate kufaulu.
وَأَطِيعُوا اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَلَا تَنَازَعُوا فَتَفْشَلُوا وَتَذْهَبَ رِيحُكُمْ وَاصْبِرُوا إِنَّ اللَّـهَ مَعَ الصَّابِرِينَ ﴿٤٦﴾
46. Na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake wala msizozane, msije mkavunjika moyo na zikapotea nguvu zenu, na subirini. Hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wanaosubiri.
وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ خَرَجُوا مِن دِيَارِهِم بَطَرًا وَرِئَاءَ النَّاسِ وَيَصُدُّونَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ وَاللَّـهُ بِمَا يَعْمَلُونَ مُحِيطٌ ﴿٤٧﴾
47. Wala msiwe kama wale waliotoka majumbani mwao kwa fahari na kujionyesha kwa watu, na kuzuilia njia ya Mwenyezi Mungu: Na Mwenyezi Mungu ameyazunguka wanayoyafanya.
وَإِذْ زَيَّنَ لَهُمُ الشَّيْطَانُ أَعْمَالَهُمْ وَقَالَ لَا غَالِبَ لَكُمُ الْيَوْمَ مِنَ النَّاسِ وَإِنِّي جَارٌ لَّكُمْ فَلَمَّا تَرَاءَتِ الْفِئَتَانِ نَكَصَ عَلَىٰ عَقِبَيْهِ وَقَالَ إِنِّي بَرِيءٌ مِّنكُمْ إِنِّي أَرَىٰ مَا لَا تَرَوْنَ إِنِّي أَخَافُ اللَّـهَ وَاللَّـهُ شَدِيدُ الْعِقَابِ ﴿٤٨﴾
48. Na shetani alipowapambia vitendo vyao, na kusema: Leo hakuna wa kuwashinda na hali mimi ni mlinzi wenu. Yalipoonana majeshi mawili, alirudi nyuma na kusema: Mimi si pamoja nanyi, mimi naona msiyoyaona, mimi namwogopa, Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.
إِذْ يَقُولُ الْمُنَافِقُونَ وَالَّذِينَ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ غَرَّ هَـٰؤُلَاءِ دِينُهُمْ وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَإِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ ﴿٤٩﴾
49. Waliposema wanafiki na wale wenye maradhi nyoyoni mwao: Hawa imewadanganya dini yao, Na mwenye kumtegemea Mwenyezi Mungu, basi hakika Mwenyezi Mungu ndiye mwenye nguvu mwenye hekima.
MNAPOKUTANA NA JESHI KAZANENI
Aya 45 – 49
MAANA
YANAYOLETA USHINDI
Enyi mlioamini! Mnapokutana na jeshi, basi kazaneni, na mumkumbuke Mwenyezi Mungu sana ili mpate kufaulu.
Makusudio ya jeshi ni lile linalofanya ufisadi katika nchi. Kauli yake Mwenyezi Mungu ili mpate kufaulu yaani mlishinde.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja mambo mawili yanayoleta ushindi katika Aya hii:
La kwanza: ni uthabiti na ushupavu, aliposema; “Kazaneni.”
La pili: ni ikhlas, aliposema “Mkumbukeni Mwenyezi Mungu sana.” Makusudio ya kumkumbuka Mungu vitani sio dhikri ya takbira na tahalili tu; isipokuwa ni kuwe kupigana na ukakamavu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu tu; kwa maana ya kutoathirika vita na hali yoyote isipokuwa kwa ajili ya kuthibitika haki na kubatilika batili; kwa ajili ya kuhifadhi amani ya watu na usalama wao; na kuwapiga waovu wanaoeneza ufisadi katika nchi kwa kunyanganya na kupora huku wakileta vita na fitina ili watawale miji na riziki za waja.
Na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake wala msizozane, msije mkavunjika moyo na kupoteza nguvu zenu, na subirini. Hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wanaosubiri.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja katika Aya iliyotangulia mambo mawili ya kuleta ushindi; na katika Aya hii anataja matatu: Kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume, kujiepusha na mizozo na kusubiri (kuvumilia.) Lakini kuwa na subira ndiko kukazana. Kwa hiyo kauli yake Mwenyezi Mungu: Subirini ni ibara nyingine ya kazaneni; kama ambavyo kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake ndiyo ikhlasi. Ama kutofautiana kwingine ni kuzuri na kwengine ni kubaya, Ufafanuzi utafuatia.
Kwa ufupi mambo yanayoleta ushindi wa hakika yaliyoelezwa katika Aya mbili ni matatu:
1. Subira na kukazana, nako ni kujitolea mhanga kwa moyo wote ili kuinusuru haki ishinde batili; kama ambavyo haki inashinda kwa kuondoka batili, vile vile haki inashinda kwa kufichuka batili na kuidhihirisha kwa watu.
Subira ni lazima katika kufika lengo lolote. Hakuna mwanafunzi, mwalimu, mgunduzi, au mfanyi biashara yeyote anayeweza kupata kitu bila ya subira (uvuumilivu) na kukazana. Kiwango cha kuvumilia kwake mashaka na uchungu ndicho kiwango cha kufaulu kwake, Na hii ndiyo siri ya kauli yake Mwenyezi Mungu.
Hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wanaosubiri
وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ ﴿١٥٥﴾
“Wape habari njema wanaosubiri (2:155)
وَلَا يُلَقَّاهَا إِلَّا الصَّابِرُونَ ﴿٨٠﴾
Wala hawatapewa hayo isipokuwa wanaosubiri” (28:80)
وَلَئِن صَبَرْتُمْ لَهُوَ خَيْرٌ لِّلصَّابِرِينَ ﴿١٢٦﴾
“Na kama mkivumilia hiyo ni kheri kwa wanaosubiri” (16:126) na Aya nyinginezo.
Mimi nimejaribu kuwa na subira nilipokuwa mwanafunzi na mtunzi. Sikuona kitu chenye mwisho mtamu na manufaa kama hicho. Tumezungumzia kuhusu kuwa na subira na uvimilivu katika Juz.2 (Sura 2:155)
2. Ikhlasi: Kukusudia kitendo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kumtegemea yeye sio mwingine na kuamini kwa imani mkato kwamba yaliyoko mbele ya Mwenyezi Mungu ni bora na yatasalia kuliko jaha, mali na watoto, kisimwaathiri chochote katika hivi na kumtii Mwenyezi Mungu na radhi yake.
Mtu huweza kufikia malengo yake ya kishetani, lakini haya hayahisabiwi kuwa ni ushindi, ila kama tukizingatia batili ni fadhila, wizi ni ghanima na ufisadi ni takua na utengenevu.
3. Kujiepusha na aina yoyote ya kutofautiana. Inaweza kutokea kutofautiana katika maoni na mtazamo kwa ikhlasi. Kutofautiana huku hakupingani na kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wala hakuzuii kuafikiana lengo; kama vile kupigana jihadi na wafisadi. Mara nyingi huko kunakuwa ni njia ya kufunguka uhakika.
Vile vile inaweza kuwa sababu ya kutofautiana ni hawaa, na ubinafsi na kupupia dunia. Hayo ndiyo makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu: “Wala msizozane msije mkaharibikiwa na kupoteza nguvu zetu.”
Mifano ya madhara ya kuzozana na kushindana haina idadi, na katika Historia ni mamia. Hatuna haja ya kutoa mfano wa historia ya mbali, Historia yetu tu ya sasa hivi inatutosha kwa mifano yote. Hivi karibuni nimesoma makala ya mwandishi wa Kimarekani, Salz Bridge aliyoiandika katika gazeti la Herald Tribune. Ninamnukuu:
“Washington inapima tofauti ya idadi ya waarabu na Israil; na inasisitiza kwamba, hata kama si kwa masilahi ya Israil, lakini daima kipimo kitakuwa ni kugawanyika kunakoendelea baina ya dola za kiarabu. Kwa sababu kugawanyika huku kunaifanya idadi ya waarabu iwe ni nambari tu, isiyokuwa na thamani yoyote.”
Kabla ya mwandishi huyu viongozi wa Israil wametangaza mara nyingi kuwa wao walifaulu katika vita vya tarehe 5 Juni kwa msaada wa Marekani na kutofautiana kwa waarabu. Na ni kitu gani kilichowapendeza waisrail kuliko kushikiana silaha waarabu wenyewe kwa wenyewe, badala ya kuwashikia Israil? Kwa ajili hiyo wakoloni wa kizayuni wamefanya kila wawezalo kuwagombanisha waarabu. Jambo la kusikitisha ni kuwa wamepatikana waliowaitikia, bali wanaozungumza kwa niaba yao, Hata hivyo, mapambano bado yanaendelea. Ni lazima wakoloni na vibaraka wao watashindwa, sasa au baadaye.
Wala msiwe kama wale waliotoka majumbani mwao kwa fahari na kujionyesha kwa watu, na kuzuilia njia ya Mwenyezi Mungu, Na Mwenyezi Mungu ameyazunguka wanayoyafanya.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwaamrisha waislamu mambo matatu wakiwa wanawaelekea vitani, sasa anawakataza mambo matatu: fahari, kujionyesha, na kuzuilia njia ya Mwenyezi Mungu.
Amenasibisha sifa hizi tatu kwa makafiri wa kiquraish kwa sababu wao waliotoka kuelekea Badr kumpiga vita Mtume(s.a.w.w)
wakiwa wanajifaharisha, wanajionyesha na kuwazuilia waislamu na njia ya Mwenyezi Mungu.
Wafasiri wanasema: Abu Jahli alipokuwa akiwaongoza maquraish kumpiga vita Mtume huko Badr, njiani alijiwa na Ibn Al-Hiqaf Al-Kinaniy na zawadi kutoka kwa baba yake. Akamwambia Abu Jahli: “Baba yangu anakwambia, kama unataka atakuongozea watu, na kama unataka nitaungana nawe.” Abu Jahli akasema “Ikiwa tunapigana na Mwenyezi Mungu, kama anavyodai Muhammad, basi Wallahi hatumuwezi Mwenyezi Mungu na ikiwa tunapigana na watu, basi sisi ndio watu wenye nguvu zaidi, wala hatutarudi nyuma kupigana na Muhammad mpaka tufike Badr tunywe pombe na watuimbie watumwa na waarabu wasikie.”
Kujifaharisha kunadhihiri katika maana yake pana kwa kauli ya Abu Jahl: “Na sisi ni watu wenye nguvu zaidi.” Ama kujionyesha kuko katika kauli yake: “Na waarabu wasikie” Kwa ajili hii basi nasi tunaelemea kwenye kauli ya mwenye kusema kuwa Aya hii imemshukia Abu Jahli.
Ama mwisho wa fahari hiyo na ria ni kuuawa waliouawa, akiwemo Abu Jahli na kutekwa waliotekwa na kushindwa waliobakia.
Na shetani alipowapambia vitendo vyao, na kusema: Leo hakuna wa kuwashinda na hali mimi ni mlinzi wenu. Yalipoonana majeshi mawili, alirudi nyuma na kusema: Mimi si pamoja nanyi, mimi naona msiyoyaona, mimi namwogopa, Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.
Aya hii inasema waziwazi kuwa kuna kitu kinachoitwa Shetani kiliwachochea maquraish kumpiga vita Mtume huko Badr na kuwapa dhamana ya ushindi, na kwamba yeye alipoyakinisha mwisho wao alijitoa.
Tumekwishaelezea mara nyingi kwamba sisi tunaamini kila linaoelezwa na wahyi na lisilokataliwa na akili; na kwamba tunaiachia ghaibu ufafanuzi. Hakuna kitu katika hukumu ya akili kinachozuia kupatikana kitu kinachoonekana au kisichoonekana kinachowatia mshawasha watu kwenye batili na kuwahadaa. Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimwamrisha Mtume wake mtukufu ajilinde na shari ya mwenye kutia wasiwasi katika nyoyo za watu, awe jini au mtu.
Waliposema wanafiki na wale wenye maradhi nyoyoni mwao: Hawa imewadanganya dini yao. Na mwenye kutegemea kwa Mwenyezi Mungu, basi hakika Mwenyezi Mungu ndiye mwenye nguvu mwenye hekima.
Wanafiki ni wale wanaodhihirisha Uislamu na kuficha ukafiri. Ama wale ambao nyoyoni mwao mna maradhi, ni wanafiki, makafiri na mafasiki.
Kwa hiyo kuunganisha wenye maradhi nyoyonni juu ya wanafiki ni kati- ka kuunganisha jumla juu ya mahsusi.
Mwenyezi Mungu amesimulia, katika Aya hii, kuhusu wenye maradhi ya moyo, kwamba wao walishangaa walipoona kujitokeza kwa waislamu wachache wa kupigana vita na makafiri; wala hawakufahamu tafsir ya kujitokeza huku isipokuwa kujiangamzia kwa waislamu na kuhadaliwa na matumaini ya kufuzu pepo. Kwao hayo ni maneno yasiyo na maana. Kwa sababu kila kitu kwao ni biashara tu; hata dini.
JE WAKOMBOZI NI WAHARIBIFU?
Wakati huu ambapo nguvu za shari zimeungana kuwafanyia njama waarabu na waislamu na kuwafukuza wazalendo wa Palestina katika ardhi zao na kuwatupa ufuoni wanawake, wazee na watoto; wakati huu ambapo wakombozi wanawanyima usingizi waisrail na kuwakosesha raha; na kutamka neno, uhuru juu ya ukombozi wa ardhi iliyovamiwa, ndipo anaposema Sheikh mwenye kilemba kwenye mpaka wa Israil katika kijiji kimoja cha kaskazini, akinadi kwa kupaza sauti kadamnasi na kusema: “Wakombozi ni waharibifu” sawa na anavyosema Moshe Dayan.
Ewe mheshimiwa! Wakombozi ni waharibifu! Je, wewe na Israil ndio watengenezaji? Kwa nini wakombozi wawe waharibifu? Je, ni kwa kuwa wanapigania haki zao, katika njia ya kuuawa na kuua; au ni kwa vile wao wamebadilisha jina la wakimbizi na kuwa wakombozi? Na, je, wewe katika kauli yako hii unamtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kupigana jihadi kutekeleza wajibu wa kidini na wa kiuzalendo?
Ni dini gani hiyo inayokataza kujitolea mhanga kwa ajili ya kulinda mtu nchi yake na kutaka kuishi huru na kuheshimiwa; hata kwa thamani ya namna gani?
Mimi nimeelewa mantiki yako ewe Sheikh, Wewe unasema kuwa Israil inajibu mashambulizi ya wakombozi kwa kuwatesa wanyonge, nasi twakuuliiza: Walikuwa wapi wakombozi mnamo tarehe 29 Juni 1897, wakati Uzayuni ulipofanya mkutano mkuu huko Uswisi, na kupitisha azimio la kuwafukuza waarabu Palestina na waikalie Mayahudi? Je, azimio hilo lilitokana na wakombozi wakati huo?
Kisha utasema nini kuhusu mauaji ya Diryasin na uchinjaji ulofanywa na Mayahudi kwa wakazi wasio na hatia, kabla ya jeshi kuingia Palestina?
Inakupasa ujue ewe mwenye kilemba cha usheikh na kila Mwarabu kwamba waisrail hawatosheki tu na Palestina, Jordan, Lebanon, Syria na Iraq; isipokuwa lengo lake ni kuwadhalilisha waarabu wote wanyenyekee Uzayuni na ukoloni kisiasa na kiuchumi. Israil inatamani mafuta ya Kuwait, Qatar, Abu Dhabi na Saudia.
Tamaa yao hii wameipanga na kuiwekea mkakati kwa kula njama pamoja na dola za kikoloni, Harakati za wakombozi ndizo zilizoharibu mikakati hii ya waisrail kiasi cha kufikiria kuwa Israil haitakuwako.
Ni bora mara elfu tuvumilie maumivu yanayosababishwa na vitendo vya wakombozi, kuliko kuwacha yatimie malengo ya Israil ambayo haiatoshe- ki na chochote; hata mto Nail na Furat.
Zaidi ya hayo, hivi sasa inatulazimu kumkabili adui kwa kupatikana wakombozi wa kujitolea mhanga; kama hatua ya kwanza na tuvumilie taabu zote zitakazosababishwa nao ili kukinga ambalo ni baya na kubwa zaidi.
Baada ya hayo, ewe Sheikh! Unasemaje kuhusu vikosi vilivyokuwa vikitumwa na Muhammad(s.a.w.w)
kukata njia ya maadui zake washirikina na kuchukua mali zao, kuua na kuchukua mateka na kuwakosesha amani majumbani akiwa yeyey mwenye binafsiakiongoza baadhi ya mashmbulizi hayo; kama alivyowapiga Mayahudi wa Bani Quraidha baada ya kuvunja ahadi na kujiiunga na Abu Sufyan, adui wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake katika vita vya Ahzab.
Mtume(s.a.w.w)
aliliamrisha jeshi lake alilokuwa akiliongoza yeye mwenyewe lichome mimea ya mayahudi, na kukata miti yao na kuvunja majumba yao, Je, kitendo chake hicho Mtume kilikuwa cha utengezaji au uharibifu?
Imepokewa Hadith Mutawatir aliposema Mtume(s.a.w.w)
: “Mwenye kufa akilinda mali yake amekufa Shahid” Je vipi kwa yule atakayokufa katika hali ya kumzuia Mwisrail adui wa Mwenyezi Mungu, wa nchi na wa binadamu wote?
Mwenyezi Mungu anasema:
إِنَّ اللَّـهَ اشْتَرَىٰ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ أَنفُسَهُمْ وَأَمْوَالَهُم بِأَنَّ لَهُمُ الْجَنَّةَ يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَيَقْتُلُونَ وَيُقْتَلُونَ وَعْدًا عَلَيْهِ حَقًّا فِي التَّوْرَاةِ وَالْإِنجِيلِ وَالْقُرْآنِ وَمَنْ أَوْفَىٰ بِعَهْدِهِ مِنَ اللَّـهِ فَاسْتَبْشِرُوا بِبَيْعِكُمُ الَّذِي بَايَعْتُم بِهِ وَذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ ﴿١١١﴾
‘Hakika Mwenyezi Mungu amenunua kwa waumini nafsi zao na mali zao kuwa wao watapata pepo. Wanapigana katika njia ya Mwenyezi Mungu, wanaua na wanuawa. Hii ni ahadi aliyojilazimisha kwa haki katika Tawrat na Injili na Qur’an, Na ninani atimiziaye ahadi kuliko Mwenyezi Mungu? Basi furahini kwa biashara yenu mliyofanya naye, Na huko ndiko kufuzu kukubwa” (9:111)
Wala hakuna anayeitumia Aya hii katika umma wa Kiarabu isipokuwa wapiganaji ukombozi; na kujitolea kwao ndio jiwe la msingi la mapinduzi ya mataifa yote ya kiarabu.