3
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI
يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ حَسْبُكَ اللَّـهُ وَمَنِ اتَّبَعَكَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿٦٤﴾
64. Ewe Mtume! Mwenyezi Mungu anakutosheleza wewe na wale waliokufuata katika waumini.
يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ حَرِّضِ الْمُؤْمِنِينَ عَلَى الْقِتَالِ إِن يَكُن مِّنكُمْ عِشْرُونَ صَابِرُونَ يَغْلِبُوا مِائَتَيْنِ وَإِن يَكُن مِّنكُم مِّائَةٌ يَغْلِبُوا أَلْفًا مِّنَ الَّذِينَ كَفَرُوا بِأَنَّهُمْ قَوْمٌ لَّا يَفْقَهُونَ ﴿٦٥﴾
65. Ewe Nabii! Wahimze waumini wende vitani; wakiwepo miongoni mwenu ishirini wenye subira, watashinda mia mbili; na kama wakiwa mia moja miongoni mwenu watawashinda elfu moja katika waliokufuru, maana hao ni watu wasiofahamu.
الْآنَ خَفَّفَ اللَّـهُ عَنكُمْ وَعَلِمَ أَنَّ فِيكُمْ ضَعْفًا فَإِن يَكُن مِّنكُم مِّائَةٌ صَابِرَةٌ يَغْلِبُوا مِائَتَيْنِ وَإِن يَكُن مِّنكُمْ أَلْفٌ يَغْلِبُوا أَلْفَيْنِ بِإِذْنِ اللَّـهِ وَاللَّـهُ مَعَ الصَّابِرِينَ ﴿٦٦﴾
66. Sasa Mwenyezi Mungu amewahafifishia na anajua kuwa kuna udhaifu miongoni mwenu. Kwa hiyo wakiwa mia moja miongoni mwenu wenye subira watawashinda mia mbili, na kama wakiwa elfu moja miongoni mwenu watawashinda elfu mbili kwa idhini ya Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wanaosubiri.
ANAKUTOSHELEZA MWENYEZI MUNGU
Aya 64 – 66
MAANA
Ewe Mtume! Mwenyezi Mungu anakutosheleza wewe na wale waliokufuata katika waumini.
Imesemekana kuwa maana yake ni kuwa Mwenyezi Mungu anakutosha wewe Muhammad na pia anawatoshea waumini waliokufuata. Ama sisi tunaelemea kwenye kauli ya aliyesema kuwa maana yake ni: Ewe Muhammad! Anakutosha Mwenyezi Mungu na waumini kwa Utume wako. Dalili yetu katika hilo ni Aya iliyotangulia (62): “Basi Mwenyezi Mungu atakutoshelezea.
Yeye ndiye aliyekupa nguvu kwa msaada wake na kwa waumini.” Aya hii inaeleza wazi kuwa Mwenyezi Mungu na waumini walimsaidia Muhammad, basi ni hivyo hivyo “Anakutoshelezea wewe Mwenyezi Mungu na wale waliokufuata katika waumini.”
Vyovyote iwavyo, makusudio ni kumtuliza Mtume kwamba vita vyake na makafiri vimedhaminiwa katika hali yoyote ile, Kwa sababu nguvu inayomsaidia haishindiki.
Ewe Nabii! Wahimze waumini wende vitani; wakiwepo miongoni mwenu ishirini wanaosubiri, watashinda mia mbili; na kama wakiwa mia moja miongoni mwenu watawashinda elfu moja katika waliokufuru, maana hao ni watu wasiofahamu.
Mwenyezi Mungu Mtukufu anamwambia Mtume wake washujaishe na vita Ewe Muhammad, watu wako, na uwape habari kwamba wao ni kufu ya maadui wa Mwenyezi Mungu na maadui zao, hata kama watazidi zaidi ya mara kumi. Hilo ni kwa kuwa waumini wanafahmu amri ya Mwenyezi Mungu na wanaitakidi siku ya mwisho; na kwamba heri itapatikana kwa jihadi na kufa shahidi. Kwa hiyo wanakwenda kwa nia njema, Ama makafiri hawafahmu amri ya Mwenyezi Mungu wala hawaitakidi ahadi. Kwa hali hii wao wanabania maisha yao.
Sasa Mwenyezi Mungu amewahafifishia na anajua kuwa kuna udhai- fu miongoni mwenu. Kwa hiyo wakiwa mia moja miongoni mwenu wenye subira watawashinda mia mbili, na kama wakiwa elfu moja miongoni mwenu watawashinda elfu mbili kwa idhini ya Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wanaosubiri.
Wafasiri na mafakihi wamerefusha maneno kuhusu Aya hii. Kuna waliosema kuwa Aya hii ni Nasikh (inayofuta hukumu) ya Aya iliyotangulia ambayo imemlazimisha Mwislamu asiwakimbie watu kumi. Wengine wakasema ilikuwa uzito kwa Waislamu kukabili mmoja kwa kumi, ndipo ikaja tahfifu hiyo. Mafakihi nao kwa kutegemea Aya hi wamefutu kuwa ni haramu kukimbia vitani ila ikiwa idadi ya jeshi la adui ni maradufu ya idadi ya jeshi la Waislamu.
Katika kufasiri Aya 15 katika Sura hii, tumebainisha kuwa mafakihi hawana fatwa katika suala hili; na kwamba anachiwa suala hili, kamanda mkuu peke yake mwenye ujuzi na mwaminifu.
Kwa ajili hii tunatilia nguvu kuwa Aya mbili hizi na ile iliyo kabla yake, hazikuja kubainisha hukumu ya kukimbia, isipokuwa zinahusika na Mtume na sahaba zake tu; na Mwenyezi Mungu ndiye mjuzi zaidi wa makusudio yake.
مَا كَانَ لِنَبِيٍّ أَن يَكُونَ لَهُ أَسْرَىٰ حَتَّىٰ يُثْخِنَ فِي الْأَرْضِ تُرِيدُونَ عَرَضَ الدُّنْيَا وَاللَّـهُ يُرِيدُ الْآخِرَةَ وَاللَّـهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ ﴿٦٧﴾
67. Haimfalii Nabii yoyote kuwa na mateka mpaka awe ameshinda sawasawa katika ardhi, Mnataka vitu vya dunia Na hali Mwenyezi Mungu anataka Akhera. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu mwenye hekima.
لَّوْلَا كِتَابٌ مِّنَ اللَّـهِ سَبَقَ لَمَسَّكُمْ فِيمَا أَخَذْتُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ ﴿٦٨﴾
68. Lau isingelikuwa hukumu iliyotangulia kutoka kwa Mwenyezi Mungu, bila shaka ingeliwapata adhabu kubwa kwa yale mliyoyachukua.
فَكُلُوا مِمَّا غَنِمْتُمْ حَلَالًا طَيِّبًا وَاتَّقُوا اللَّـهَ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٦٩﴾
69. Basi kuleni katika vile mlivyoteka ni halali na vizuri, na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.
يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّمَن فِي أَيْدِيكُم مِّنَ الْأَسْرَىٰ إِن يَعْلَمِ اللَّـهُ فِي قُلُوبِكُمْ خَيْرًا يُؤْتِكُمْ خَيْرًا مِّمَّا أُخِذَ مِنكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٧٠﴾
70. Ewe Nabii! Waambie wale mateka waliomo mikononi mwenu: Kama Mwenyezi Mungu akijua heri yoyote nyoyoni mwenu, basi atawapa bora kuliko vilivyochukuliwa kwenu na atawasamehe. Na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.
وَإِن يُرِيدُوا خِيَانَتَكَ فَقَدْ خَانُوا اللَّـهَ مِن قَبْلُ فَأَمْكَنَ مِنْهُمْ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴿٧١﴾
71. Na kama wanataka kukufanyia hiyana, basi walikwishamfanyia hiyana Mwenyezi Mungu kabla, na akakupa ushindi juu yao. Na Mwenyezi Mungu ni mjuzi mwenye hekima.
KATEKA
Aya 67 – 71
MAANA
Haimfalii Nabii yoyote kuwa na mateka mpaka awe ameshinda sawa-sawa katika ardhi.
Wameafikiana wafasiri kwamba Aya hii imeshuka kuhusu mateka wa Badr, Dhahir ya mfumo inafahamisha hivyo. Wametofautiana katika tafsir yake, nasi tutaileta kwa njia ya swali na jawabu:
Ikiwa kuna vita baina ya Waislamu na waabudu masanamu. Na, Mwenyezi Mungu akampa ushindi Mwislamu kwa kafiri, je, ni wajibu kwa Mwislamu kumuua kafiri huyo? Au inajuzu kumchukua mateka? Na kama akimchukua mateka, je iko hiyari kwa Mtume baina ya kumuua na kumwacha kwa fidia? Na kumwacha bila ya fidia?.
Jibu
: ni lazima lifafanuliwe katika hali mbili: Kwanza, ni kutokea vita baada ya dini kuwa na nguvu katika ardhi na watu wake kuwa na nguvu kwa namna ambayo hila na vitimbi vya maadui haviwadhuru, kwa kuwa ipo nguvu ya kujikinga.
Katika hali hii, Mwislamu anayepigana, anahiyarishwa baina ya kuua na kuchukua mateka. Na akichukua mateka itakua hiyari kwa Mtume baina ya kuua mateka na kumwacha kwa fidia au bila ya fidia. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
فَإِذَا لَقِيتُمُ الَّذِينَ كَفَرُوا فَضَرْبَ الرِّقَابِ حَتَّىٰ إِذَا أَثْخَنتُمُوهُمْ فَشُدُّوا الْوَثَاقَ فَإِمَّا مَنًّا بَعْدُ وَإِمَّا فِدَاءً ﴿٤﴾
“Basi mnapokutana vitani na wale waliokufuru wapigeni shingo mpaka mkiwashinda sawa sawa, hapo wafungeni pingu, Baadae waacheni kwa ihsani au kwa kujikomboa” (47:4)
Siri katika hilo iko wazi, nayo ni kupatikana nguvu ya kujikinga.
Hali ya pili ni kutokea vita kabla dini haijamakinika vizuri na kuwa na nguvu katika ardhi. Hapo Mwislamu anayepigana, akimmudu kafiri anayepigana naye amuue sio kumchukua mateka. Siri ya hili ni kutia hofu moyo wa kila anayejaribu kutangaza vita dhidi ya waumini.
Haya yanafahamika kutokana na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Haimfalii Mtume kuwa na mateka mpaka ashinde sawasawa’ Yaani hakuna kuchukua mateka wa kikafiri mpaka dini iwe na nguvu kamili ya kujihami ambayo makafiri na mataghuti watakuwa chini yake.
Mnataka vitu vya dunia
Maneno haya yanaelekezwa kwa mwenye kuteka mateka kwa kukusudia ngawira na kuchukua fidia bila ya kujali kuharibika maisha yake katika ardhi.
Na hali Mwenyezi Mungu anataka Akhera.
Mwenyezi Mungu anawatakia waja wake malipo ya akhera kwa sababu ndiyo bora na yenye kubaki kuliko mapambo ya dunia.
Na Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu mwenye hekima.
Anawapa nguvu waumini hata kama hawana mateka; na ni mwenye hekima katika kupanga mambo yake na amri yake na makatazo yake.
Lau isingelikuwa hukumu iliyotangulia kutoka kwa Mwenyezi Mungu, bila shaka ingeliwapata adhabu kubwa kwa yale mliyoyachukua.
Ilitangulia hukumu ya Mwenyezi Mungu kuinusuru dini yake na Mtume wake pamoja na watu wachache aliokuwa nao Badr, na kuteswa makafiri, pamoja na wingi wao, kwa kuuliwa na kutekwa kwa mikono ya waumini.
Lau si kupitisha kwake huku Mwenyezi Mungu, wangeliadhibiwa waumini ambao waliwachukua mateka maadui wa Mwenyezi Mungu kwa tamaa ya kupata fidia. Kwa sababu Mwenyezi Mungu Mtukufu anataka jihadi na amali iwe ni kwa ajili yake yeye Mwenyezi Mungu tu.
Kuna hadith isemayo “… ambaye hijra (kuhama) yake ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi hijra yake ni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na ambaye hijra yake ni kwa ajili ya kupata dunia au kuoa mwanamke, basi hijra yake ni kwa lile alilolihajira.”
Ilivyo ni kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu hakubainisha aina ya adhabu ambayo angeliwapa wachukuaji mateka katika masahaba, lau si kupitisha alivyopitisha. Je, ilikuwa ni adhabu ya kidunia au ya kiakhera.
Utauliza
: Ikiwa kuchukua mateka kulikuwa ni haramu kabla ya kushamiri dini yake Mwenyezi Mungu juu ya dini zote, ilikuwaje kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
kuwaruhusu masahaba siku ya Badr na akakubali kuchukua fidia kabla ya ushindi kamili? Na vita vya Badr vilikuwa ndio vya kwanza na kukafuatiwa na vita vilivyoendelea hadi mwaka wa kuchukuliwa Makka?
Wafasiri na wengineo wamedangana katika kujibu swali hili au mushkeli huu; na yakagongana maneno yao. Wengine wakajiachia na kusema ‘Mtume sio maasum aweza kukosa. Lakini hapana, hayuko hivyo Mtume wa Mwenyezi Mungu ambaye hatamki kwa hawa yake
Tunalotilia nguvu ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) alivua uharamu wa kuchukua mateka kwa kila mateka aliyeachwa huru na Mtume(s.a.w.w)
siku ya Badr. Wengi wao walisilimu na kuwa watu wazuri; bali hata walikuwemo waliochukuliiwa vitani kwa kulazimishwa.
Ibn Athir katika Tarikh yake Juz: 2 katika kifungu; vita kuu ya Badr, anasema: “Mtume(s.a.w.w)
aliwaambia sahaba zake siku hiyo:“Ninajuwa watu katika Bani Hashim na wengineo wametolewa kwa kulazimishwa. Kwa hiyo atakayekutana na yeyote katika Bani Hashim asimwue”
Miongoni mwa mateka alikuwemo Suhail bin Amr. Umar bin Al-Khattab akasema. “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu: Acha nimwue asije akakuudhi.”
Mtume akasema:“Mwache atakuwa na jambo utakalomsifia.”
Mateka mwingine alikuwa Abul As bin Rabii mume wa Zainab binti ya Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
.
Zainab akapeleka fidia ya kumkombolea mumewe ukiwemo mkufu wa mama yake Khadija. Mtume alipouona aliingiwa na huruma nyingi sana, na kuwaambia Waislamu:“Kama mtaonelea ni vyema kumwachia na kumrudishia vitu vyake basi fanyeni”
Basi Waislamu walimwachia na kumrudishia mkufu, Abul As akasilimu baada ya hapo.
Mtume(s.a.w.w)
aliua, miongoni mwa mateka waovu ambao haitarajiwi heri kwao, na wala hakukubali fidia yao. Ibn Athir anasema: “Miongoni mwa mateka alikuwemo Nadhr bin Harith na Uqba bin Abi Muiti. Mtume akaamuru wauliwe akasema Uqba: “Je, mimi si kama mateka hawa?” Lakini Mtume hakujali kauli yake hiyo, kwa vile anajua uovu wake na uhaini wake, na kwamba maisha yake ni shari na ufisadi katika ardhi.
Kwa hiyo kuwaachia huru baadhi ya mateka na kuwaua wengine, kunafahamisha kuweko masilahi kwa Uislamu na Waislamu katika kuwaacha walioachwa; nayo yalidhihiri, baadae, kama tulivyoelezea. Kwa ajili hii ndipo ikasihi kuvua hukumu ya uharamu katika mateka wa Badr.
Basi kuleni katika vile mlivyoteka ni halali na vizuri, na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.
Maneno yanaelekezwa kwa waliopigana vita Badr pamoja na Mtume. Yana madhumuni ya kuidhinisha kula walivyochukua ngawira katika vita, iwe ni fidia au ngawira yenyewe. Hii ni dalili kwamba kuchukua mateka katika Badr kuliruhusiwa. Kwa sababu kuruhusu moja ya badali mbili (kitu na thamani yake) ni kuruhusu ya Pili; yaani ikiruhusiwa thamani ndio imeruhusiwa mali yenyewe. Kuna Hadith isemayo: “Mwenyezi Mungu akiharimsha kitu basi pia huharamisha thamani yake.”
Ewe Nabii! Waambie wale mateka waliomo mikononi mwenu: Kama Mwenyezi Mungu akijua heri yoyote nyoyoni mwenu, basi atawapa bora kuliko vilivyochukuliwa kwenu na atawasamehe. Na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.
Baada ya Mtume kuchukua fidia kutoka kwa mateka aliamrishwa kuwaambia hao mateka kuwa ikiwa mnamwamini Mwenyezi Mungu atawapa badali bora kuliko fidia, duniani na akhera.
Wafasiri wanasema kuwa baadhi ya mateka walidhihirisha Uislamu, ndipo Mwenyezi Mungu akamwaamrisha Mtume wake kuwaambia kuwa ikiwa mliyoyasema ni haki basi Mwenyezi Mungu anajua na atawapa badali bora kuliko vile vilivyochukuliwa kwenu na atawasamehe. Na ikiwa ni unafiki basi mmekwisha kufuru na mkafanya vitimbi kabla ya hapo na Mwenyezi Mungu akampa ushindi Mtume wake juu yenu.
Kisha wakaendelea kusema wafasiri, akiwemo Razi na Tabrasi, kwamba Mtume(s.a.w.w)
alimwambia ami yake, Abbas: Jikomboe wewe na watoto wawili wa nduguyo, Aqil na Naufal. Abbas, akasema: Nilikuwa Mwisilamu wakanilazimisha kutoka. Mtume akamwambia Ikiwa uyasemayo ni kweli, basi Mwenyezi Mungu atakulipa. Abbas akasema: Sina chochote. Mtume akasema: Iko wapi ile dhahabu uliyompa mkeo,
Ummul Fadhi na kumwambia: Nikitokewa na lolote basi ni yako na watoto wako?
Abbas akashangaa na kumuuliza: Ni nani aliyekuambia?
Mtume akasema: Mwenyezi Mungu ndiye aliyeniambia. Abbas akasema: Nashuhudia kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu; Wallahi hakujua habari hii yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu. Baada ya hapo Abbas alisema: Amesema kweli Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hakika Mwenyezi Mungu alinibadilishia ziada nyingi baada ya kutoa fidia.
Na kama wanataka kukufanyia hiyana, basi walikwishamfanyia hiyana Mwenyezi Mungu kabla, na akakupa ushindi juu yao. Na Mwenyezi Mungu ni mjuzi mwenye hekima.
Dhamir katika kama wanataka, inawarudia mateka ambao aliwaacha huru Mtume(s.a.w.w)
. Maana ni kuwa usiogope hiyana ya mateka uliowaachia, kwani wananini wakitaka kufanya hiyana? Walikupiga vita kabla na haikuwa lolote:
وَمَنْ عَادَ فَيَنتَقِمُ اللَّـهُ مِنْهُ وَاللَّـهُ عَزِيزٌ ذُو انتِقَامٍ ﴿٩٥﴾
“Na atakayerudia, Mwenyezi Mungu atampa adhabu; na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye nguvu mwenye kuadhibu” Juz.7 (5:95)
Hii ni dalili nyingine kuwa Mwenyezi Mungu aliwahalilishia waislamu mateka katika vita vya Badr.
Kwa ufupi ni kuwa Mwenyezi Mungu amewajibisha kuwaua washirikina katika vita yao na waumini ikiwa vimetukia kabla ya dini kuwa na nguvu; isipokuwa katika vita vya Badr.
Kwani Mwenyezi Mungu alihalalisha kwa Mwislamu anayepigana kuchukua mateka kwa masilahi ya Uislamu na waislamu.
إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَهَاجَرُوا وَجَاهَدُوا بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَالَّذِينَ آوَوا وَّنَصَرُوا أُولَـٰئِكَ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ وَالَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يُهَاجِرُوا مَا لَكُم مِّن وَلَايَتِهِم مِّن شَيْءٍ حَتَّىٰ يُهَاجِرُوا وَإِنِ اسْتَنصَرُوكُمْ فِي الدِّينِ فَعَلَيْكُمُ النَّصْرُ إِلَّا عَلَىٰ قَوْمٍ بَيْنَكُمْ وَبَيْنَهُم مِّيثَاقٌ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ ﴿٧٢﴾
72. Hakika wale walioamini na wakahajiri na wakapigania dini ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao na nafsi zao; na wale waliokaribisha hao ndio wanaosimamiana wao kwa wao. Na wale walioamini na wasihame, hamna haki ya kuwasimamia hata kidogo mpaka wahame. Lakini wakiwaomba msaada katika dini, basi ni juu yenu kuwasaidia, isipokuwa juu ya watu ambao yapo mapatano baina yenu na wao, Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayoyatenda.
وَالَّذِينَ كَفَرُوا بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ إِلَّا تَفْعَلُوهُ تَكُن فِتْنَةٌ فِي الْأَرْضِ وَفَسَادٌ كَبِيرٌ ﴿٧٣﴾
73. Na wale waliokufuru wanasimamiana wao kwa wao; msipofanya hivyo itakuwa fitina katika ardhi na ufisadi mkubwa.
وَالَّذِينَ آمَنُوا وَهَاجَرُوا وَجَاهَدُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَالَّذِينَ آوَوا وَّنَصَرُوا أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقًّا لَّهُم مَّغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ ﴿٧٤﴾
74. Na wale walioamini waka- hajiri na wakafanya jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu na wale waliokaribisha na kusaidia, hao ndio waumini kweli, wana wao maghufira na riziki njema.
وَالَّذِينَ آمَنُوا مِن بَعْدُ وَهَاجَرُوا وَجَاهَدُوا مَعَكُمْ فَأُولَـٰئِكَ مِنكُمْ وَأُولُو الْأَرْحَامِ بَعْضُهُمْ أَوْلَىٰ بِبَعْضٍ فِي كِتَابِ اللَّـهِ إِنَّ اللَّـهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴿٧٥﴾
75. Na wale walioamini baadaye wakahajiri na wakapigania jihadi pamoja nanyi, basi hao ni katika nyinyi. Na ndugu wa tumbo wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe katika Kitab cha Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa kila kitu.
WAHAJIRI NA ANSAR
Aya 72 – 75
MAANA
Aya hizi zimewagawanya waumini kwenye mafungu; na zikaonyesha muungano wa kusaidiana ulioko baina yao kwa sababu ya imani na Hijra. Pia Aya zimeonyesha muungano wa makafiri na mirathi ya wenye udugu.
Ufafanuzi ni kama huu ufuatao:
1.Hakika wale waliaomini na wakahajiri na wakafanya juhudi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao na nafsi zao.
Hao ni wale wahajiri (wahamiaji) wa kwanza. Mwenyezi Mungu amewasifu kwa imani, kuhama mji na kufanya juhudi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa hali na mali.
Ni kwa kujitolea huku, sio imani tu, ndipo Qur’an ikawasifu na kuzungumza mengi ya kumwitikia kwao Mwenyezi Mungu na Mtume wake.
Utauliza
: Ilivyo ni kuwa wahajiri waliingia Madina wakiwa hawana kitu ndio maana Ansar waliwakaribisha majumbani mwao wakawapa chakula na mavazi, wakiwatanguliza wao kuliko wenyewe; kama asemavyo Mwenyezi Mungu: ‘Na wale waliokaribisha,’ sasa walitoa wapi mali waliyoijitolea katika njia ya Mwenyezi Mungu?
Jibu
: Kwanza: wahajiri walikuwa wakiwasaidia mafukara waislamu kabla ya Hijra.
Pili: wao waliacha majumba yao na mashamba yao yaporwe na washirikina, kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu. Hakuna kitu kikubwa kama mtu kuacha nyumba yake, na ardhi yake na yote aliyoyachuma kwa ajili ya maisha yake na watoto wake.
2.Na wale waliokaribisha na kusaidia hao ndio wanaosimamiana wao kwa wao.
Hao ni Ansar. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewasifu kuwa wao walimkaribisha Mtume na walioahama naye katika majumba yao, wakawapendelea kuliko nafsi zao na watoto wao.
Na kwamba wao walimpa amani aliyewapa amani wahajiri na kuwa hasimu waliowafanyia uhasimu. Kwa hali hiyo ndipo, Mwenyezi Mungu akawapa sifa hii mpaka likawa neno ‘Answar’ (wasaidizi) ndio nembo yao siku zote.
Kauli yake Mwenyezi Mungu hao ndio wanosimamiana ni kuashiria Wahajiri na Answar kwa pamoja; na kwamba kila mmoja anamsimamia mwenzake kama anavyojisimamia kimsaada na kiulinzi. Kuna Hadith isemayo: “Mfano wa waumini katika kuhurumiana na kupendana; ni kama mfano wa mwili, kiungo kimoja kikiwa na tatizo, basi huacha mwili mzima ukeshe na kuwa na homa.”
Baadhi ya wafasiri wamewatofautisha Wahajiri na Answar, wakawafanya bora hawa kuliko hao. Ama sisi tuko katika upande wa kuwa wote wako sawa. Hilo lafahamishwa na Aya tuliyo nayo, vile vile Aya isemayo:
وَالسَّابِقُونَ السَّابِقُونَ ﴿١٠﴾
“Na waolitangulia wametangulia” (56:10)
Hawa waliwatangulia wenzao kwa imani na kuhama na wale wakawatangulia wenzao kwa kukaribisha na kusaidia. Yakawa makundi yote ni katika waliotangulia. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewasifu hivyo katika Aya isemayo: “Na waliotangulia wa kwanza katika wahajiri na Answar”
Na wale walioamini na wasihame.
Hawa ni wale walioamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, lakini walikataa kutoka mji wa shirki na kuhamia mji wa Uislamu, pamoja na kuwa Qur’an imewaamrisha na kuwahimiza, lakini wao walishikamana na mali zao na kuhofia masilahi yao.
Yametangulia maelezo ya hawa na hukumu ya Hijra katika Juz.5 (4:97)
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amebainisha hukumu ya hawa ambao hawakuhama kwa kusema:
Hamna haki ya kuwasimamia hata kidogo mpaka wahame, Lakini wakiwaomba msaada katika dini, basi ni juu yenu kuwasaidia.
Yaani hawa hawazingatiwi kuwa ni sehemu ya jamii ya Kiislamu; wala haiwathibitikii haki yoyote ya waislamu wanaokaa katika mji wa Kiislam. Kwa sababu wao wamechagua hukumu ya shirk na washirikina kuliko hukumu ya Uislamu na waislamu.
Ndio! wakiacha nchi ya washirikina kuelekea nchi ya Uislamu, basi wanayo haki ya kulindwa na kusaidiwa. Vile vile kama akiwachokoza mchokozi kwa ajili ya dini na itikadi yao na kujaribu kuwafitini na Uislamu.Lakini si wajibu kuwasaidia katika yasiyokuwa hayo. Kwa sababu, mfungamano wa dini unamlazimisha kila mmoja kulinda dini ya ndugu yake, hata kama ni fasiki. Kwa maneno mengine ni kuwa kuilinda itikadi ya fasiki ni kulinda dini hasa sio kumlinda fasiki mwenyewe.
Kama kwamba muuliizaji aliuliza: Ikiwa kafiri amemchokoza Mumin ambaye hakuhama: na baina ya kafiri mchokozi na Mumin aliye katika nchi ya Kiislam kuna mkataba, na Mumin aliyechokozwa akataka msaada kwa Mumin aliye katika nchi ya Kiislamu, Je, hapo ni wajibu kumsaidia aliyechokozwa?
Mwenyezi Mungu (s.w.t) akajibu kwa kusema:
Isipokuwa juu ya watu ambao yapo mapatano baina yenu na wao, Na Mweneyzi Mungu anayaona mnayoyatenda.
Yaani usaidizi haupasi katika hali ya namna hii kwa kulinda mkataba. Kwani Uislamu hauruhusu kwa hali yoyote kufanya hiyana, hata na kafiri.
JINA LA DINI HALINA ATHARI
Na wale waliokufuru wanasimamiana wao kwa wao.
Dhahiri ya Aya inaweza kutoa dhana kwamba kushirikiana katika ukafiri kunapelekea kusaidiana, Lakini hali haiko hivyo, Historia ya makafiri wao kwa wao ni historia ya vita na umwagikaji wa damu, Vile vile historia ya waislamu.
Majarabio yamefahamisha kuwa masilahi ndiyo yanayowaweka watu pamoja, Ama matamko tu na majina ya kidini, kama vile Mwislamu na Mkristo, yanaweza kuwa na athari, lakini haifikii kiwango cha kusimami- ana kwa kusaidiana.
Yaani huyu amsimamie mwenzake; kama anavyojisimamia kiasi cha kutoa mhanga masilahi yake yote, hata nafsi yake na watu wake na mali yake! Hapana, ila ikiwa ni kwa ajili ya dini.
Hayo ndiyo yanayokusudiwa na kauli yake Mwenyezi Mungu. ‘Hao ndio wanaosimamiana’ na pia kauli yake:
وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ﴿٧١﴾
Waumini wanaume na waumin wanawake ni mawalii wao kwa wao. Huamrishana mema na kukatazana maovu (9:71).
Yaani mema kwao ndio masilahi Ama makusudio ya kauli yake: ‘Na wale waliokufuru wanasimamiana wao kwa wao” na kauli yake:
وَإِنَّ الظَّالِمِينَ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ﴿١٩﴾
Na hakika madhalimu wanasimamiana (45: 19).
Pia kauli yake:
الْمُنَافِقُونَ وَالْمُنَافِقَاتُ بَعْضُهُم مِّن بَعْضٍ يَأْمُرُونَ بِالْمُنكَرِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمَعْرُوفِ ﴿٦٧﴾
“Wanafiki wanaume na wanafiki wanawake ni hali moja, Wanaamrisha maovu na kukataza mema” (9:67)
Makusudio ya Aya hizo tatu ni kuwa makafiri, wanafiki na madhalimu wanakuwa kitu kimoja dhidi ya haki, pamoja na uadui na kupigana baina yao. Kwa sababu masilahi yanawakusanya na kuwaweka safu moja, masi- lahi yenyewe ni kulinda manufaa na faida.
Hilo limekwishafanyika mara nyingi zamani na saa. Katika historia ya saa ni muungano wa wakoloni na wanyonyaji dhidi ya wazalendo na wanamapinduzi; na jinsi mashirika ya kilanguzi yanavyoshindania faida.
Na historia ya zamani ni kuafikiana washirikina wa kiarabu na mayahudi wa Hijaz na wanafiki kwa kauli moja kuupiga vita Uislamu na waislamu. Hakuna lililowapa msukumo huo isipokuwa masilahi ya pamoja; kwani uadui baina ya washirikina na mayhudi, kabla ya Uislamu, ulikuwa umepita kiasi.
Kwa maelezo hayo ndio tunafasiri kauli yakeMwenyezi Mungu: “Na wale waliokufuru wanasimamiana wao kwa wao.” Ama walioyoyaeleza wafasiri wengi kuwa makusudio ni kuwa makafiri wanarithiana, tafsiri hii iko mbali na dhahiri ya tamko.
Tumezungumzia mfano wa Aya hii na masilahi ya pamoja baina ya mayahudi na wakristo wengi hivi sasa, katika Juz.6 (5:51) kifungu cha mayahudi petroli na wakristo.
Msipofanya hivyo itakuwa fitina katika ardhi na ufisadi mkubwa.
Yaani: Enyi Waislamu! Mlioamini msipowasaidia waislamu wenye kuwataka msaada dhidi ya makafiri ambao wanajaribu kuwafitini na dini yao na kuwarudisha kwenye shirki, basi itakuwa chokochoko na ufisadi kwa sababu ya shirki kutawala imani na batili kutawala haki.
Hakika wale waliaomini na wakahajiri na wakafanya Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao na nafsi zao. Na wale waliokaribisha na kusaidia hao ndio waumini wa kweli. Wana wao maghufira na riziki njema.
Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewataja wahajiri na Ansari kwa tamko hili hili kubainisha wajibu wa hilo kwa kila mmoja juu ya mwenzake katika kumlinda na kumsaidia. Kisha hapo amerudia kwa ajili ya kuwasifu kuwa wao ndio waumini wa kweli na kubainisha alivyowaandalia keshomsamaha na thawabu ambazo amezielezea kwa ibara ya ‘riziki njema.’
Sijasoma ibara fasihi zaidi kushinda wasifu wa Imam Zainul-Abidin
kwa wahajiri na Ansari huku akimlingani Mola wake na kuwatakia rehema na radhi, kwa kusema:“Ewe Mola! Hasa maswahaba wa Muhammad ambao walikuwa na usuhuba mzuri, wakawa na majaribu mema katika kumsaidia kwake.
Wakamwitikia alipowaaeleza hoja ya ujumbe wake.
Wakapigana na mababa zao na watoto wao ili kuithibisha unabii wake na wakashinda kupitia kwake.
Waliozingirwa na mapenzi wakitarajia biashara isiyo na hasara kwa ajili ya kumpenda kwake.
Wakatengwa na jamaa zao waliposhikamana na kamba yake, Udugu ulikwisha walipotulia chini ya kivuli cha udugu wake.
Basi ewe Mola usiwasahu kwa yale waliyoyawacha kwa ajili yako. Na uwaridhie kwa radhi zako.
Na walikuwa wakilingania kwako pamoja na mjumbe wako”
Hii ni sehmu ya kwanza ya dua namba nne inayopatikana katika kitabu cha dua kinachoitwa Asswahifatussajjadiyya ambacho Shia wanakiadhimisha na kuitukuza kila herufi yake.
Hili ni jawabu tosha la yule anayesema kuwa Shia wanawavunjia heshima maswahaba.
Na wale walioamini baadaye na wakahajiri wakapigana jihadi pamoja nanyi, basi hao ni katika nyinyi.
Hawa ni wale waliomwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wakahamia Madina na kupigania dini ya Mwenyezi Mungu kwa nafsi zao na mali zao, baada ya wale waliotangulia kwanza. Wote hukumu yao ni moja tu katika wajibu wa kuwasaida na kuwalinda.
Na ndugu wa tumbo wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe katika kitabu cha Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa kila kitu.
Wafasiri wanasema baada ya Mtume kuwafanyisha ndugu masahaba zake, na yeye akawa nduguye ni Ali; walikuwa wanasaidiana na kustahikiana katika mirathi; yaani warithiane kwa udugu huu sio kwa nasabu na akraba.
Kisha ikafutwa hukumu ya kurithiana huku, kukarudi kurithiana kwa udugu wa tumbo na akraba.
Aya hii wameitolea dalili Shia kwamba aliye karibu na marehemu kinasabu ndiye anayestahiki zaidi mirathi yake kuliko aliye mbali, ni sawa awe na fungu au la; au awe na nasaba au la, Kwa hiyo Binti wa marehemu anamzuia ndugu wa marehemu kurithi kwa vile yuko karibu naye zaidi; na dada wa marehemu anamzuia ami wa marehemu, Kwa sababu hiyo hiyo. Namna hii wa karibu zaidi humzuia wa mbali katika daraja zote.
Tumeyazungumzia hayo na kauli za Sunni na Shia kuhusu jambo hilo; kama tulivyoonyesha kurithiana kwa udugu na sabababu za kurithi wakati wa Jahilia, Yote hayo tumeyazungia katika Juz.4 (4:11).
MWISHO WA SURA YA NANE