6
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّمَا الْمُشْرِكُونَ نَجَسٌ فَلَا يَقْرَبُوا الْمَسْجِدَ الْحَرَامَ بَعْدَ عَامِهِمْ هَـٰذَا وَإِنْ خِفْتُمْ عَيْلَةً فَسَوْفَ يُغْنِيكُمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ إِن شَاءَ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴿٢٨﴾
28. Enyi Mlioamini! Hakika washirikina ni najis, kwa hivyo wasiukaribie Msikiti Mtakitifu baada ya mwaka wao huu. Na kama mkihofia umasikini, basi hivi karibuni Mwenyezi Mungu atawatajirisha kwa fadhila yake akitaka. Hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi mwenye hekima.
WASHIRIKINA NI NAJISI
Aya 28
MAANA
Enyi Mlioamini! Hakika washirikina ni najis, kwa hivyo wasiukaribie Msikiti Mtakitifu baada ya mwaka wao huu.
Yaani mwaka wa tisa wa Hijra, mwaka ambao Ali
aliwasomea watu Aya za kujitoa katika dhima.
Aghlabu Qur’an hulitumia neno washirikina kwa wanaoabudu masanamu; hasa washirikina wakiarabu. Na hutumia neno ‘Watu wa Kitab’ kwa mayahudi na wanaswara (wakristo). Kuunganisha washirikina na watu wa Kitab katika Aya isemayo:
مَّا يَوَدُّ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ وَلَا الْمُشْرِكِينَ ﴿١٠٥﴾
“Hawapendi waliokufuru miongoni mwetu wa Kitab wala washirikina” (2:105)
na ile isemayo:
إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ وَالْمُشْرِكِينَ ﴿٦﴾
“Hakika waliokufuru katika watu wa Kitab na washrikina…”(98:6)
Kunafahamisha kuwa kinachounganishwa si sawa na kinachouganishiwa, ingawaje inawezekana kuunganisha maalum kwenye ujumla, lakini ni kulingana na jumla yenye ilivyo.
Mafakihi wametofautiana kuhusu kuwazuia makafiri kuingia msikitini, Shafii anasema wanazuiwa mskikiti mtukufu (Masjidul-haram) tu, Malik anasema watazuiwa misikiti yote, Abu Hanifa anasema hazuiwi msikiti wowote, Hayo yamo katika Tafsir ya Razi katika kufasri Aya hii.
Tuonavyo sisi ni kuwa ni wajibu kuzuia najisi kwenye msikiti wowote na ikiwemo ndani ni wajibu kuitoa, ni sawa iwe ni ya mtu, mnyama au kitu kingine chochote. Iwe ni najisi ya itakayochafua msikiti na kuivunjia heshima yake au la. Dalili ya hayo ni kwamba hukumu ya kuharamisha imeachwa bila ya kufungwa na kitu chochote.
Tukisema mtu aliye najisi tuna maanisha mkanushaji na mwabudu masana- mu na mizimu. Ama watu wa Kitab tumethibtisha utohara wao katika Juz. 6 (5:5)
Unaweza kuuliza kuwa
: kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘kwa hivyo wasiukaribie Msikiti Mtakitifu” inafahamisha kusihi kauli ya Shafii, kuwa kuzuia kunahusika na Msikiti Mtakatifu (Masjidul-haram) tu, sio mwengineo, Kwa sababu hakusema wasikaribie kila msikiti.
Jibu
: mkusanyiko wa Aya unafahamisha kuenea, sio mahsusi. Kwa sababu linalokuja haraka kwenye fahamu ni kuwa sababu ya kuzuiwa kuingia ni najisi na kuheshimu msikiti mbele ya Mwenyezi Mungu.
Hakuna mwenye shaka kwamba kila msikiti unaheshimiwa mbele ya Mwenyezi Mungu kwa sababu unanasibishiwa kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na hukumu inakwenda pamoja na sababu yake kwa kuthibitisha na kukanusha.
Ndio maana mafakihi wakakongamana kuwa wiski ni haramu, ingawaje hakuna kauli wazi juu yake, kwa kutosheka na sababu ya kuharimishwa ulevi.
Na kama mkihofia umasikini, basi hivi karibuni Mwenyezi Mungu atawatajirisha kwa fadhila yake akitaka. Hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi mwenye hekima.
Washirikina katika pembe zote za bara Arabu walikuwa wakielekea Makka kuhiji na kufanya biashara. Watu wa Makka walikuwa wakinufaika na hilo, wakiuza na kununua kutoka kwao, pia walikuwa wakiwakodisha majumba. Na Makka iko katika jangwa lisilokuwa na mmea.
Basi Mwenyezi Mungu alipowazuia washirikina baadhi ya watu wa Makka walihofia ufukara, ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawaambia hivyo; yaani mkihofia ufukara kwa sababu ya kukatika mawasiliano ya washirikina na Makka, basi Mwenyezi Mungu atawapa badali kwa njia nyingine.
Kwani sababu za riziki mbele yake ni idadi ya matone ya mvua; kama ilivyoelezwa katika Hadith.
Amesema kweli Mwenyezi Mungu na Mtume wake, aliwafungulia waislamu miji na ngawira, wakaingia watu kwa makundi katika dini yake, wakaelekea Makka kwa mamilioni pamoja na nyoyo zao na mali zao.
Watu wa Makka wakaona faida ambayo hata hawakuiota.
Utauliza
: nini lengo la kauli yake Mwenyezi Mungu ‘Akitaka’ pamoja na kuwa alikwishataka?
Jibu
: Yanaweza kuwa makusudio ni kudokeza kuwa visababishi vinapita kwa sababu zake na inaweza kuwa makusudio ni kuwafundisha waja wake wamtegemee Mwenyezi Mungu katika mambo yao yote na malengo yao wayaambatanishe na matakwa yake Mwenyezi Mungu pamoja na juhudi; kama ilivyo katika kauli yake Mwenyezi Mungu:
وَلَا تَقُولَنَّ لِشَيْءٍ إِنِّي فَاعِلٌ ذَٰلِكَ غَدًا ﴿٢٣﴾ إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ ﴿٢٤﴾
“Wala usiseme kamwe kwa jambo lolote lile: Hakika nitalifanya kesho ispokuwa Mwenyezi Mungu akitaka (inshaallah)” (18:23-24)
قَاتِلُوا الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَلَا بِالْيَوْمِ الْآخِرِ وَلَا يُحَرِّمُونَ مَا حَرَّمَ اللَّـهُ وَرَسُولُهُ وَلَا يَدِينُونَ دِينَ الْحَقِّ مِنَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ حَتَّىٰ يُعْطُوا الْجِزْيَةَ عَن يَدٍ وَهُمْ صَاغِرُونَ ﴿٢٩﴾
29. Piganeni na wale wasiomwamini Mwenyezi Mungu wala siku ya mwisho wala hawaharamishi aliyoharamisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala hawashiki dini ya haki, miongoni mwa waliopewa Kitab, mpaka watoe kodi kwa mkono hali wametii.
وَقَالَتِ الْيَهُودُ عُزَيْرٌ ابْنُ اللَّـهِ وَقَالَتِ النَّصَارَى الْمَسِيحُ ابْنُ اللَّـهِ ذَٰلِكَ قَوْلُهُم بِأَفْوَاهِهِمْ يُضَاهِئُونَ قَوْلَ الَّذِينَ كَفَرُوا مِن قَبْلُ قَاتَلَهُمُ اللَّـهُ أَنَّىٰ يُؤْفَكُونَ ﴿٣٠﴾
30. Na mayahudi wanasema, Uzair ni mwana wa Mwenyezi Mungu; na wanaswara wanasema Masihi ni mwana wa Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo kauli yao kwa vinywa vyao, wanayaiga maneno ya wale waliokufuru zamani. Mwenyezi Mungu awangamize! Wanageuzwa wapi?
اتَّخَذُوا أَحْبَارَهُمْ وَرُهْبَانَهُمْ أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّـهِ وَالْمَسِيحَ ابْنَ مَرْيَمَ وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا إِلَـٰهًا وَاحِدًا لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ سُبْحَانَهُ عَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿٣١﴾
31. Wamefanya makuhani wao na watawa wao kuwa ni miungu badala ya Mwenyezi Mungu na Masih mwana wa Maryam. Wala hawakuamrishwa isipokuwa wamwambudu Mungu mmoja hakuna Mungu ila yeye Ametakata na wanayomshirikisha nayo.
يُرِيدُونَ أَن يُطْفِئُوا نُورَ اللَّـهِ بِأَفْوَاهِهِمْ وَيَأْبَى اللَّـهُ إِلَّا أَن يُتِمَّ نُورَهُ وَلَوْ كَرِهَ الْكَافِرُونَ ﴿٣٢﴾
32. Wanataka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao, Na Mwenyezi Mungu amekataa isipokuwa kuitimiza nuru yake, ijapokuwa makafiri wamechukia.
هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ ﴿٣٣﴾
33. Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uongofu na dini ya haki ili ipate kushinda dini zote, ijapokwa washirikina wamechukia.
PIGANENI NA WASIOMWAMNI MWENYEZI MUNGU
Aya 29 – 33
MAANA
Piganeni na wale wasiomwamini Mwenyezi Mungu wala siku ya mwisho wala hawaharamishi aliyoharamisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala hawashiki dini ya haki, miongoni mwa waliopewa Kitab, mpaka watoe kodi kwa mkono hali wametii.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuamrisha kupigana na washirikina ikiwa hawakusilimu wala hawakutoka, katika Aya hii ameamrisha kupigana na watu wa Kitab ikiwa hawakutoa kodi na kunyenyekea hukumu ya Kiislam.
Mwenyezi Mungu amewasifu kuwa hawamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho wala hawaharamishi haramu ya Mwenyezi Mungu au kufuata dini ya haki.
Ilivyo ni kwamba neno ‘miongoni’ katika kauli yake Mwenyezi Mungu ‘miongoni mwa wale walopewa Kitab’ ni la kubainisha jinsi. Na imesemekana ni la kufanya baadhi.
Hapa kuna maswali mawili:
Swali la Kwanza
: Aya imeawakanushia watu wa Kitab kumwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho pamoja na kwamba wao wanaamini kuweko Mwenyezi Mungu. Kwa sababu neno watu wa Kitab hilo lenyewe linafahamisha kumwamini kwao Mwenyezi Mungu ambaye ameteremsha Tawrat na Injil.
Vile vile wanaamini siku ya mwisho kwa nukuu ya Aya isemayo:“Na wanasema: hautatugusa moto isipokuwa kwa siku chache tu”
Juz. 1 (2:80) Ingawaje ni kweli kuwa wao hawafuati dini ya haki. Mayahudi wanaabudu mali na kanisa linauza cheki za msamaha?
Jawabu la swali hilo
tunalipata katika Aya iliyo baada yake, bila ya kuweko kati kitu kingine:
Na mayahudi wanasema, Uzeir ni mwana wa Mwenyezi Mungu; na wanaswara wanasema Masihi ni mwana wa Mwenyezi Mungu.
Njia ya jawabu ni kuwa Mayahudi na Wakristo wamemfanya Mwenyezi Mungu kuwa na mtoto. Maana yake ni kuwa wanamwamini Mwenyezi Mungu asiyekuwepo ila katika mawazo yao tu, Ama Mungu aliyeko kweli, wao hawamwamini. Wameleta picha ya kua ni Mungu mwenye watoto. Ama Mola wa uhakika ambaye hakuzaa wala hakuzaliwa wao hawamwamini wala hafungamani nao kwa mbali au karibu.
Kwa ufupi ni kuwa Mungu aliyeko hawamwamini na wanamwamini mungu asiyeko. Natija ya yote hayo ni kuwa wao hawamwamini Mwenyezi Mungu.
Kimsingi ni kwamba asiyemwamini Mwenyezi Mungu haamini akhera kwa imani sawa, wala hafuati dini ya haki, hata kama itafikiriwa kuwa yeye ni katika wanaoamini akhera na wenye kufuata dini ya haki. Kwa sababu kumwamini Mwenyezi Mungu ndio asili (shina) mengineyo ni matawi, yaani yeye anaamini akhera na dini ambayo haina athari yoyote isipokuwa katika mawazo yao tu; kama kusema kwao: Hautatugusa moto isipokuwa kwa siku chache tu. Dini hiyo ndiyo ile iliyotajwa na yule aliye- sema: “Dini inatengenezwa na mawazo na njozi.”
Swali la pili
: Uislamu haumlazimishi yeyote kuukubali kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu:
لَا إِكْرَاهَ فِي الدِّينِ ﴿٢٥٦﴾
“Hakuna kulazimishwa katika dini….”Juz: 3(2:256).
Na pia kauli yake Mwenyezi Mungu:
أَفَأَنتَ تُكْرِهُ النَّاسَ حَتَّىٰ يَكُونُوا مُؤْمِنِينَ ﴿٩٩﴾
Basi je, wewe unawalazimisha watu hata wawe waumini? (10: 99).
Sasa imekuwaje kuamrishwa kupigana na watu wa Kitab mpaka waamini au watoe kodi?
Swali hili tumelitaja
katika kufasiri Aya ya pili katika Sura hii, ambayo imeamrisha kupigana na washirikina.Tukajibu kwamba
: amri ya kupigana nao ilikuwa ni hukumu maalum ya wakati huo, kwa sababu mahsusi, kwamba jamii ya Kiislam ndio ilikuwa inaanza na washirikina walikuwa ni kikosi cha tano
walifanyia vitimbi Uislamu na watu wake.
Masilahi yakawa ni kuwatoa bara arabu au kuwaua. Na amri ya kupigana hapa ni mahsusi kwa watu wa Kitab ambao walikuwa wakiungana na washirikina kuwapiga vita waislamu kama walivyofanya Mayahudi wa Madina na walio pembeni baada ya kuwekeana mkataba wa amani na mtume na kufanya muungano nao.
Zaidi ya hayo, kiini cha Sura hii ni vita vya Tabuk, kama itakavyoelezwa katika Aya 38 na zinazofuatia. Na, Mtume(s.a.w.w)
alipata habari kwamba Warumi wakiwa Sham wanaanda majeshi kwa ajili ya kuumaliza Uislamu na watu wake. Na dalili zilionyesha wazi kuwa watu wa Kitab walikuwa ni wasaidizi na mawakala wa wakristo wa Roma; na kwamba wao walikuwa wakila njama nao dhidi ya Mtume na wafuasi wake waumini.
Kwa ajili hiyo ndipo ikawa hukumu ni kupigana nao au waweke silaha chini na wawe chini ya hukumu ya Kiislamu, pamoja na kutoa kodi ambayo itaonyesha usalama wao na kutekeleza kwao ahadi yao. Wakitoa kodi basi ni wajibu kuwapa amani kuwahami na kuwapa uhuru katika dini yao. Wakisilimu watapata waliyonayo waislamu, Vinginevyo basi ni kuwaua kujikinga na shari yao.
Wafasiri na mafakihi wamerefusha maneno kuhusu kodi, kiasi chake na sharti zake. Maneno yao wakati huo yalikuwa na faida ambapo uislamu ulikuwa na dola yake na nguvu zake. Ama leo mazungumzo kuhusu kodi ni kuongeza maneno tu.
Na mayahudi wanasema: Uzair ni mwana wa Mwenyezi Mungu; na wanaswara wanasema, Masihi ni mwana wa Mwenyezi Mungu.
Kauli ya Wakristo kuwa Masih ni mwana wa Mwenyezi Mungu ni maarufu na tumeizungumzia katika Juz.6 (5:18)
Ama kauli ya Mayahudi kuhusu Uzair, mwenye Tafsir Al-Manar amenukuu kuwa jina la Uzair liko katika vitabu vitakatifu vya mayahudi,Vile vile amenukuu kutoka Daira tul-Maarifil-Yahudiyya kwamba zama za Uzair ndizo zama nzuri za Historia ya mayahudi. Katika Tafsir ya Tabari, Razi na Tabrasi imeelezwa kwamba kikundi cha Mayahudi walimwambia Mtume(s.a.w.w)
: Tutakufuata vipi nawe umeacha Qibla chetu na wala hudai kuwa Uzair ni mwana wa Mwenyezi Mungu, ndipo ikashuka Aya.
Kwa vyovyote ilivyo ni kwamba Mtume aliwakabili Mayahudi wa zama zake kwa Aya hii, na haikunukuliwa kutoka kwa yeyote katika wao kumkosoa au kumpinga pamoja na kumkadhibisha kwao sana Mtume, Kwa hiyo inafahamisha kuwa wao waliamini hivyo wakati huo.
Hiyo ndiyo kauli yao kwa vinywa vyao, wanayaiga maneno ya wale waliokufuru zamani. Mwenyezi Mungu awangamize! Wanageuzwa wapi?.
Yaani kauli ya mayahudi inafanana na kauli ya washirikina waarabu ambao walisema: Malaika ni mabinti wa Mwenyezi Mungu, vile vile kauli ya waabudu mizimu wa zamani, waroma, wayunani, wabudha na wengineo.
Wamefanya makuhani wao na watawa wao kuwa ni miungu badala ya Mwenyezi Mungu na Masih mwana wa Maryam.
Hii ni dalili nyingine kwamba wao hawamwamini Mwenyezi Mungu bali wanaamini wanayoyasema watu wa dini yao na itikadi yao. Imam Jaffer As-sadiq
anasema:“Wao hawakuwafungia swaum au kuwaswalia, lakini waliwhalalishia haramu na wakawaharamishia halali, wakawafuata na kuwaabudu bila ya kutambua.”
Haya ni sawa na yaliyo katika Hadith kwamba Udey bin Hatim alimwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
: Sisi hatuwaabudu wao.
Mtume akamwambia: Je, hawaharimishi aliyohalalisha Mwenyezi Mungu mkayaharamisha; na kuhalalisha aliyoharamisha Mwenyezi Mungu mkayahalalisha? Udey akasema: Ndio, Mtume akasema: huko ndiko kuwaabudu.
Voltare anasema: Makasisi wetu hawajui chochote isipokuwa sisi ni wepe-si wa kusadiki wayasemayo.
Wala hawakuamrishwa isipokuwa wamwambudu Mungu mmoja hakuna Mungu ila yeye Ametakata na wanayomshirikisha nayo.
Razi katika Tafsir yake anasema: Maana yako dhahiri. Lakini mfasiri mwingine ambaye alitaka asema tu: “Yaani wamwabudu Mola Mkuu”.
Wanataka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao.
Makusuido ya nuru ya Mwenyezi Mungu hapa ni Uislamu. Maana ni kuwa watu wa Kitab walijaribu kuumaliza Uislamu kwa kila njama na uwongo; ikawa ni kama mtu anayejaribu kuzima nuru, ambayo imeenea ulimwenguni, kwa pumzi yake.
Na Mwenyezi Mungu amekataaa isipokuwa kuitimiza nuru yake, ijapokuwa makafiri wanachukia.
Hii ni ahadi ya Mwenyezi Mungu, kupitia mdomoni mwa Mtume wake, kuunusuru Uislamu na kuudhihirisha mashariki ya ardhi na magharibi. Amesema kweli Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na ahadi ambayo inafahamisha utume wa Mohammad(s.a.w.w)
ikathibiti na ukweli wake katika kila alilolitolea habari.
Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uongofu na dini ya haki ili ipate kushinda dini zote, ijapokwa washirikina wanachukia.
Aya hii ni ubainifu na ufafanuzi wa Aya iliyo kabla yake. Mwenyezi Mungu aliwajalia waislamu kuwashinda washirikina katika miji ya Kiarabu, Mayahudi walipowatoa huko, wakristo katika Sham na Majusi katika Fursi. Imam Ali anasema: “Hakika huu Uislamu umedhalilisha dini (nyingine) kwa utukufu wake, ukaziondoa mila kwa utukufu wake na ukawatweza maadui zake kwa utukufu wake.”
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ كَثِيرًا مِّنَ الْأَحْبَارِ وَالرُّهْبَانِ لَيَأْكُلُونَ أَمْوَالَ النَّاسِ بِالْبَاطِلِ وَيَصُدُّونَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلَا يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ ﴿٣٤﴾
34. Enyi mlioamini! Hakika wengi katika watawa na makuhani wanakula mali za watu kwa batili na kuwazuilia njia ya Mwenyezi Mungu. Na wale walimbikizao dhahabu na fedha na hawazitumii katika njia ya Mwenyezi Mungu, basi wabashirie adhabu iumizayo.
يَوْمَ يُحْمَىٰ عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَىٰ بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنُوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ هَـٰذَا مَا كَنَزْتُمْ لِأَنفُسِكُمْ فَذُوقُوا مَا كُنتُمْ تَكْنِزُونَ ﴿٣٥﴾
35. Siku zitakapotiwa moto kati- ka moto wa Jahannam, na kwazo vitachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao; Haya ndiyo mliyojilimbikizia, basi onjeni yale mliyokuwa mkiyalimbikiza.
WALE WANAOKUSANYA DHAHABU NA FEDHA
Aya 34 – 35
MAANA
Enyi mlioamini! Hakika wengi katika watawa na makuhani wanakula mali za watu kwa batili na kuwazuilia njia ya Mwenyezi Mungu.
Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewataja mayahudi na wakristo kwamba wao wanawafanya viongozi wao wa kidini ni waungu badala ya Mwenyezi Mungu. Katika Aya hii amewataja hao viongozi kwa kula mali ya batili na kuzuia watu na njia ya Mwenyezi Mungu.
Makusudio ya kula mali kwa batili ni kuchukua bila ya njia ya sharia; kama vile rushwa na riba ambayo ilienea sana kwa mayahudi. Pia uuzaji wa cheki ya msamaha kwa wakatoliki nk. Wanahistoria wanasema watu wa kanisa waliwahi kuwa ndio matajiri zaidi.
Makusudio ya kuzuia watu na njia ya Mwenyezi Mungu ni kuwazuilia akili zao na kuzuia watu kukubali Uislam, bali na kuwafanya wautuhumu na Mtume wake.
Voltaire alilichagiza kanisa na kuwalaumu wakubwa wake kwa ulafi wao wa mali; akaituhumu Tawrat kutokana na mgongano. Akazuiliwa na kanisa na baadhi ya kubwa wake wakataka afungwe maisha. Akaogopa sana mwanafalsafa huyu wa kifaransa
. Hakupata njia yoyote ya kuokoka isipokuwa kutetewa na baba mtakatifu Bendedict xiv kwa kutunga Kitab cha kumtukana Muhammad. Akafanya hivyo na akasamehewa na kanisa; kikabarikiwa kitabu na mwandishi wake.
ABU DHAR NA UJAMAA
Na wale walimbikizao dhahabu na fedha na hawazitumii katika njia ya Mwenyezi Mungu, basi wabashirie adhabu iumizayo.
Kuna maneno mengi kuhusu Aya hii, Baadhi wakaitolea dalili juu ya kuweko ujamaa (usoshalist) katika Uislamu, Wengine wamediriki hata kusema kuwa Abu dharr alikuwa mjamaa kwa vile yeye alikuwa akiwatisha, kwa Aya hii, wale walioathirika na mali ya Mwenyezi Mungu kuliko watu wa Mwenyezi Mungu.
Tutaonyesha maana ya Aya na kila linalofugamana nayo kwa karibu au mbali, na kwayo tutaihukumu kauli ya anayeutolea dalili ujamaa wa Abu dhar kwa Aya hii:
1. Muawiya bin Abu Sufyan alisema kuwa Aya hii ilishuka kwa watu wa Kitab tu na wala haiwahusu Waislamu. Yaani, kwa mtazamo wake, Waislamu wanaweza kurundika mali wanavyotaka na wala wasitoe chochote katika njia ya Mwenyezi Mungu. Alinukuu kauli hii kutoka kwa Uthman bin Affan.
Kwenye Durrul Manthur ya Suyuti imeelezwa kuwa Uthman alipoandika msahafu walitaka kuondoa herufi wau (na) katika kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na wale walimbikizao dhahabu na fedha…” ili iwe ‘Walimbikizao ni sifa ya makasisi na watawa. Sahaba mmoja akapinga na kusema: Mtaiweka wau au ni uweke upanga wangu begani kwangu, ndipo wakaiweka.
Ilivyo hasa ni kuwa Aya inamhusu kila mwenye kukusanya mali na asitoe katika njia ya Mwenyezi Mungu, awe Mwislamu au si Mwislamu, kwa kuchukulia kuwa tamko ni la kuenea.
Imepokewa kutoka kwa Zaid bin Wahab kwamba alipita Rabdha, akamuona Abu dharr huko, akamuuliza: Kitu gani kilichokufikisha hapa? Akasema: Nilikuwa Sham nikasoma: ‘Na wale walimbikizao dhababu ….’ Muawiya akasema Aya hiyo haituhusu sisi ni ya watu wa Kitab. Nikasema: Hakika hiyo inatuhusu sisi na wao. Basi akanishtaki kwa Uthman ndipo wakanifukuza hadi hapa unaponiona.
2. Neno dhahabu na fedha ni Mahsus, lakini hukumu ni ya ujumla kwa aina zote za mali, hata ardhi madini miti majengo mifugo, magari na viwanda. Kwa sababu waliotishiwa adhabu iumizyao na Mwenyezi Mungu ni matajiri bahili na wala sio wanaomiliki dhahabu na fedha tu. Vingenevyo ingekuwa matajiri wa mafuta na wengineo ndio watu wema na watukufu zaidi kwa Mwenyezi Mungu duniani na akhera.
Linalotufahamisha kuwa, makusudio ni ya ujumla ni kuwa Aya hii iliposhuka iliwashughulisha waislamu kwa sababu wao walifahamu mali zote. Walipomuuliza Mtume(s.a.w.w)
aliwathibitshia walivyo fahamu na kuwambia: “Hakika Mola hakufaradhisha zaka ila kwa kuifanya njema iliyobakia katika mali zenu; na hakika amefaradhishia warithi mali zinazobakia baada yenu.”
3. Kutumia katika njia ya Mwenyezi Mungu ni pamoja na jihadi ya kupigania dini na nchi, kujenga madrasa, mahospitali na nyumba za mayaitma. Vile vile kuwapa sadaka mafukara kumtunza mke na watoto. Sehemu nzuri ya kutumia ni ile inayoienzi na haki na watu wake.
4. Madhehebu mane yamekongamana kuwa katika mali hakuna haki yoyote isiyokuwa zaka; kama ilivyoelezwa katika Ahkamul Qur’an cha Abu Bakr Al-Muafirir Al-andalusi.
Mafakihi wengi wa Kishia wamesema katika mali hakuna haki zaidi ya khumsi na zaka. Sheikh Tusi anasema “Iko haki nyingine nayo ni ile aliyoiaishiria Imam Saffer As-Sadiq kwa kauli yake: “Hakika Mwenyezi Mungu amefaradhisha katika mali za matajiri haki nyingine zisizokuwa zaka.
Kwa sababu yeye amesema:
وَفِي أَمْوَالِهِمْ حَقٌّ لِّلسَّائِلِ وَالْمَحْرُومِ ﴿١٩﴾
“Na ambao katika mali zao iko haki maalum kwa ajili ya aombaye au ajizuiaye” (51:19)
Haki maalum ni kitu chochote anachojilazimisha mtu kwa kadiri ya uwezo wake, atatoa kila siku akipenda, kila Ijuma au kila mwezi; kiwe kichache au kingi, mradi tu kiwe ni cha kudumu. Lakini kauli ya Imam, atajifaradhishia yeye mwenyewe, inatambulisha suna sio wajibu, kwa sababu wajibu unatokana na Mwenyezi Mungu si mwenginewe.
Tuonavyo sisi, baada ya kufuatilia Aya za Qur’an Tukufu, ni kwamba matajiri wanao wajibu, sio suna, kujitolea mali zao zaidi ya zaka na khums; kwa ajili ya kuipigania dini na nchi ihitajika; na ni juu ya mkuu wa waislamu kuwalazimisha hilo. Bali pia ni wajibu wajitolee kwa nafsi ikihitajika, Aya za namna hii ziko chungu nzima.
5.Siku zitakapotiwa moto katika moto wa Jahannam, na kwazo vitachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao; Haya ndiyo mliyojilimbikizia, basi onjeni yale mliyokuwa mkiyalimbikiza.
Hili ni fumbo la adhabu kali na vituko vyake. Aya hiyo ni mfano wa Aya isemayo: “Watatiwa mandakozi ya hivyo walivyofanyia ubakhili siku ya kiyama” Juz.4 (3: 180).
6. Kutokana na yaliyotangulia imetubainikia kuwa Aya inafahamisha kwa kinukuu na kimaana kwamba ni wajibu juu yao matajiri kutoa sehemu ya mali zao katika njia ya Mwenyezi Mungu, na kama wataifanyia uchoyo, basi Mwenyezi Mungu atawadhibu kwa adhabu kali. Ama kiwango cha fungu hili, na kwamba je, ni khumsi au ushuri, zaidi au chini na kwamba je, ni zaka au zaidi, Aya haifahamishi kwa Ibara wala kwa ishara.
Sasa basi ni wapi panapofahamisha ujamaa. Ujamaa ni siasa ya kiuchumi ambayo, kabla ya chochote, huangalia nyenzo za uzalishaji, kama ardhi nk, na kuweko viwango vya kumiliki; kisha huangalia uzalishaji wenyewe na njia za kukua kwake na mgawanyo wake. Hili ni jambo jingine na kuhimiza matajiri kutoa ni jambo jingine.
Kwa hiyo inatubainikia kuwa kauli ya mwenye kusema kuwa Abu Dhar alikuwa mjamaa kwa vile aliwakaripia matajiri kwa Aya hii, kuwa ni makosa na kuchanganyikiwa. Abu Dhar hana habari na ujamaa wala kitu chochote isipokuwa Uislamu. Mfano wake katika hilo ni mfano wa Mwislamu yeyote. Lakini yeye alikuwa mwenye Ikhlasi na dini yake, aliufanyia ikhlasi Uislamu na kutupilia mbali tamaa na malengo mengine.
Ikhlasi yake hii ndiyo iliyomfanya awapinge Maquraish na kuwatusi waungu wao siku aliposilimu, pale aliposimama kwenye Al-Kaaba akinadi kwa sauti kubwa: Hapana Mola mwingine ispokuwa Mwenyezi Mungu. Akikinadi tamko la Uislamu juu ya vichwa vya Maquraish siku waislamu walipokuwa hawana nguvu wala uwezo na hakuna aliye kuwa akithubutu kutamka jina la Mwenyezi Mungu na Mohammad isipokuwa kwa kujificha.
Aliendelea kuwa na msimamo huu hata mbele ya Uthman na Muawiya. Kama ambavyo alipata mapigo ya kuumiza kutoka kwa washirikina, pia kwa Uthman alipata pigo la kufukuzwa na kuwekwa mbali na watu, lakini halikumkasirisha kwa sababu yeye hakukasirikia katika maisha yake yote isipokuwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu peke yake.
Kwa ufupi alilofanya Abu Dhar ni kuwataka viongozi watawale kwa uadilifu na kuchunga haki pia aliwahofisha na adhabu kali na kuwahimiza wanaodhulumiwa kuwapinga madhalimu na kurudisha haki zao kutoka kwa madhalimu hao.
Sasa wapi na wapi hayo na Ujamaa? Tumezungumzia kuhusu kunasibish- wa ujamaa kwa Abudhar katika Kitab Maashiah Al-Imamia kwenye kifungu ‘Je Abudhar ni mjamaa?’ Na katika Kitabu Ma’ulamainnajaf Al-Ashraf kwenye kifungu ‘Abudharr’.