TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MOJA Juzuu 11

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MOJA0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MOJA Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MOJA

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 10603
Pakua: 2516

Maelezo zaidi:

Juzuu 11
Juzuu 1
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 15 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 10603 / Pakua: 2516
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MOJA

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MOJA Juzuu 11

Mwandishi:
Swahili

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MOJA

IMEANDIKWA NA: SHEIKH MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYA

IMETAFSIRIWA NA: SHEIKH HASAN MWALUPA

IMEHARIRIWA NA: USTADH ABDALLAH MOHAMED

IMEPANGWA KATIKA KOMPYUTA NA: UKHT PILI RAJABU

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu

UTANGULIZI WA MCHAPISHAJI

Kitabu hiki kilichoko mikononi mwako hivi sasa ni juhudi ya miaka mingi sana ya watu waliojitolea kuona kazi hii imefanikiwa bila ya kumsahau Marhum Abu Muhammad wa London.

Kama lilivyo jina la Tafsiri yenyewe ndivyo ilivyo Tafsiri yenyewe ambayo mwanachuoni huyu mahiri kabisa aliyeifafanua ni mtu aliyebobea katika fani zote ambazo mfasiri (Mfafanuzi) anatakiwa awe nazo. Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya ameonesha cheche zake katika vitabu vingi alivyoviandika katika maudhui mbali mbalimbali na hivyo kujipatia wasomaji wengi sana.

Msomi huyu, mwenye fikra huru na anayetetea kile anachokiamini, ni mtu mwenye mawazo mapana na kuyaangalia mambo kwa undani sana, kipaumbele chake ni katika maslahi ya umma huu na amejaribu sana kwenda na wakati.

Sifa kubwa pekee ya mwanachuoni huyu ni kuwa yeye hakujihusisha sana na kung'ang'ania madhehebu fulani tu, labda hii yatokana na wadhifa wake wa ukadhi aliokuwa nao katika nchi ya Lebanon ambayo ina madhehebu mengi, ambapo sula la madhehebu ni nyeti nchini humo, hata hivyo yeye aliweza kuamua matatizo ya watu kwenye ofisi yake kulingana na madhehebu yao pale walipomwendea, hiyo ilimsaidia sana hata kuweza kutoa kitabu kitwacho 'Al-Fiqh a'laa madhaahabil-khamsah' (Fikhi ya madhehebu matano) yaani ya Hanafi, Maaliki, Shafi, Hambali na Shia (ambacho twataraji kitatoka hivi karibuni Inshaallah).

Jambo lililotupa msukumo wa kukifasiri kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili ni zile faida nyingi atakazozipata msomaji na kujua mambo mengi na ya ajabu yaliyo mapya kwake ambayo si rahisi kuyapata kwa wafasiri wengine.

Msomaji atapata faida katika fani za Sayansi, Siasa, Historia, Mashairi, visa vizuri, na Saikolojia miongoni mwa mengine; ndiyo maana msomaji atashangaa kidogo anapoisoma Tafsiri hii atakapoona mwandishi amewataja na kuwanukuu watu kama kina Mfalme Edward, wanasyansi kama kina Enstein, Charlie Champlin (Mchekeshaji maarufu), na wengineo, hali inayoifanya tafsiri hii kuwa ni ya kipekee kabisa.

Mtindo alioutumia mwandishi ni sahali uliokusudiwa watu wa tabaka mbalimbali, wanavyuoni na watu wa kawaida.

Nia yetu ni kukigawanya kitabu hiki bure lakini tumelazimika kukiuza kwa bei nafuu ili kurudisha gharama za uchapishaji.

Mwisho: Shukrani kubwa iwaendee bila ya kuwataja watu waliojitolea usiku na mchana, jopo la wafasiri, wahariri, wachapaji, waliotupa moyo na kutoa maoni yao na walioisimamia ili kuhakikisha kwamba kitabu kimemfikia msomaji.

MAKOSA YA CHAPA

Sikumbuki kama nimewahi kusoma kitabu kilichotoka kupigwa chapa, cha zamani au cha sasa, bila ya kukuta makosa ya chapa, Nafikiri sitasoma kitabu kisichokuwa hivyo. Nimejaribu sana kuliepuka hilo katika tungo zangu, lakini sikufanikiwa.

Nilikuwa sifikirii kama ninaweza kuona makosa haya katika maandishi ya msahafu mtukufu, kama yale yaliyo katika baadhi ya chapa; kwa mfano neno yabswutu kwa swad, badala ya yabsutu kwa sin, na katika chapa ya Tafsir Arrazi ya Misr ya mwaka 1935, Sura ya (2:146). Imeandikwa La Ya'alamuun, (hawajui) badala ya Ya'alamuun (wanajua), Mfano wa makosa haya hausameheki.

Katika Tafsir Al-Manar, chapa ya Pili, sura (5:212), imeandikwa "Fawqahum ila yawmil qiyama” badala ya “Fawqahum yawamal qiyama", Hatuwezi kusema kosa hili ni kubwa zaidi kuliko lile.

Lakini mkosaji atatuletea udhuru kwa msemo mashuhuri huko kwetu jabal amail 'Makosa ya chapa.'

Katika Tafsiri Majmau chapa ya Urfan, Sura (46:15), imeandikwa: " Hatta idha balagha arbai' na sanah badala ya: Hattaidha balagha ashuddahu arbai ' na sanah"

Kusema hivi sio kama ninajitetea kutokana na makosa ya chapa atakayoyakuta msomaji katika kitabu hiki, ijapokuwa naomba msamaha kama litatokea hili, lakini makusudio yangu hasa ni kumwambia yule atakayefungua macho yake kwenye makosa ya matamko na kuufungia macho uzuri wa maana.

Vilevile ninamwambia yule ambaye siku moja aliniambia: "Vitabu vyako vimejaa makosa ya chapa, kama kwamba hakuna kitu chochote katika vitabu hivyo isipokuwa makosa ya chapa tu. Wote hao ninawaambia: Mungu awasamehe na aniongoze mimi na nyinyi.

Vyovyote iwavyo, mimi ninaomba msamaha kutokana na makosa ya kifikra na ya chapa. Anasema Amirul Muminiin(a.s) :"Watu wote ni wapungufu wenye kuchanganyikiwa, isipokuwa yule aliyehifadhiwa na Mwenyezi Mungu."

Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye mwenye jukumu la kunikubali- ayale niliyoyapatia na kunisamehe niliyakosea, kwa jaha ya Mtume na kizazi chake, ziwashukie rehema na amani (Amin).

MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYAH

1

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MOJA

Mwendelezo Wa Sura Ya Tisa: Suart At – Tawba.

يَعْتَذِرُونَ إِلَيْكُمْ إِذَا رَجَعْتُمْ إِلَيْهِمْ قُل لَّا تَعْتَذِرُوا لَن نُّؤْمِنَ لَكُمْ قَدْ نَبَّأَنَا اللَّـهُ مِنْ أَخْبَارِكُمْ وَسَيَرَى اللَّـهُ عَمَلَكُمْ وَرَسُولُهُ ثُمَّ تُرَدُّونَ إِلَىٰ عَالِمِ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ فَيُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٩٤﴾

94. Watawatolea udhuru mtakaporudi kwao, Sema, msitoe udhuru; hatutawaamini, Mwenyezi Mungu amekwishatueleza habari zenu, Na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ataviangalia vitendo vyenu. Kisha mtarudishwa kwa Mjuzi, wa ghaibu na dhahiri awaambie mliyokuwa mkiyatenda.

سَيَحْلِفُونَ بِاللَّـهِ لَكُمْ إِذَا انقَلَبْتُمْ إِلَيْهِمْ لِتُعْرِضُوا عَنْهُمْ فَأَعْرِضُوا عَنْهُمْ إِنَّهُمْ رِجْسٌ وَمَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ جَزَاءً بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ ﴿٩٥﴾

95. Watawaapia Mwenyezi Mungu mtakaporudi kwao ili muachane nao. Basi achaneni nao, Hakika wao ni uchafu, na makazi yao ni Jahanamu; ni malipo ya yale waliyokuwa wakiyachuma.

يَحْلِفُونَ لَكُمْ لِتَرْضَوْا عَنْهُمْ فَإِن تَرْضَوْا عَنْهُمْ فَإِنَّ اللَّـهَ لَا يَرْضَىٰ عَنِ الْقَوْمِ الْفَاسِقِينَ ﴿٩٦﴾

96. Wanawaapia ili muwe radhi nao. Kama mkiwa radhi nao, basi hakika Mwenyezi Mungu hatakuwa radhi na watu mafasiki.

WATAWATOLEA UDHURU

Aya 94 – 96

MAANA

Watawatolea udhuru mtakaporudi kwao.

Mfumo wa Aya unafahamisha kwamba Aya ilishuka wakati wa kurudi jeshi la Kiislamu kutoka vita ya Tabuk pale Mwenyezi Mungu alipowafahamisha kuwa watakapofika Madina, wanafiki watawakabili na nyudhuru kwa kukaa kwao nyuma, Watatoa nyudhuru za uwongo. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akamwambia Mtume wake:

Sema: msitoe udhuru; hatutawaamini, Mwenyezi Mungu amekwishatueleza habari zenu.

Huu ni ukatazo kutoka kwake Mwenyezi Mungu mtukufu kutokubali udhuru kutoka kwa wanafiki, na ni amri kwa Mtume(s.a.w.w) awaambie kuwa sisadiki chochote katika mnayonitolea udhuru.

Kwa sababu Mwenyezi Mungu amenipa wahyi yale yanayofichwa na nyoyo zenu miongoni mwa shari na unafiki.

Na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ataviangalia vitendo vyenu.

Yaani hatukubali nyudhuru zenu mpaka mthibitishe kwa vitendo sio kwa maneno kwamba nyinyi ni wa kweli katika nia zenu na malengo yenu, na wenye ikhlasi katika kumwamini Mwenyezi Mungu kama mnavyodai.

Kisha mtarudishwa Mjuzi, wa ghaibu na dhahiri awaambie mliyokuwa mkiyatenda.

Ghaibu ni yale tusiyoyajua, yanajuliwa na Mwenyezi Mungu.

Maana ni kuwa nyinyi kesho mtasimama mbele ya Mwenyezi Mungu, ambaye halijifichi kwake la kujificha, awape habari ya matendo yenu na awalipe. Ikiwa ni heri basi ni heri na ikiwa ni shari basi ni shari.

Watawaapia Mwenyezi Mungu mtakaporudi kwao ili muachane nao.

Yaani mtakaporudi kutoka katika vita vya Tabuk, Ili muachane nao; yaani mnyamazie unafiki wao ni msiwatahayarize.

Basi achaneni nao.

Yaani wapuuzeni na muwadharau. Baadhi ya wapokezi wanasema kwamba Mtume(s.a.w.w) aliwaamuru waislamu wasiwe na mawasiliano nao. Kisha Mwenyezi Mungu akabainisha sababu ya kuwapuuza na kuwadh rau kwa kauli yake:

Hakika wao ni uchafu, na makazi yao ni Jahanamu; ni malipo ya yale waliyokuwa wakiyachuma.

Kuna Hadith isemayo: “Tahadharini na kukaa na mauti.” Akaulizwa ni nani hao ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu. Akasema: Kila mwenye kupotewa na imani mjeuri wa hukumu.” Hadith nyingine inasema: “Mwenye hekima zaidi katika watu ni yule anayemkimbia mjinga zaidi katika watu.”

Wanawaapia ili muwe radhi nao. Kama mkiwa radhi nao, basi hakika Mwenyezi Mungu hatakuwa radhi na watu mafasiki.

Aina hii ya kukataza kwa upole ni mfumo fasaha zaidi. Kuwa radhi Waumini kunatokana na radhi ya Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu hawi radhi na watu mafasiki.

Sasa vipi Waumini wawe radhi nao? Yeyote anayedai kumwamini Mwenyezi Mungu huku akiwa radhi na yule aliyeghadhabikiwa na Mwenyezi Mungu basi yeye ni mnafiki, hilo halina shaka.

الْأَعْرَابُ أَشَدُّ كُفْرًا وَنِفَاقًا وَأَجْدَرُ أَلَّا يَعْلَمُوا حُدُودَ مَا أَنزَلَ اللَّـهُ عَلَىٰ رَسُولِهِ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴿٩٧﴾

97. Mabedui wamezidi sana katika kufuru na unafiki na wameelekea zaidi kutojua mipaka ya yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu juu ya Mtume. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.

وَمِنَ الْأَعْرَابِ مَن يَتَّخِذُ مَا يُنفِقُ مَغْرَمًا وَيَتَرَبَّصُ بِكُمُ الدَّوَائِرَ عَلَيْهِمْ دَائِرَةُ السَّوْءِ وَاللَّـهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴿٩٨﴾

98. Miongoni mwa mabedui wako wanaochukulia kuwa wanayoyatoa ni gharama ya bure, Na wanawangojeleamisiba. Misiba mibaya itakuwa juu yao. Na Mwenyezi Mungu ni Msikizi, Mjuzi.

وَمِنَ الْأَعْرَابِ مَن يُؤْمِنُ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَيَتَّخِذُ مَا يُنفِقُ قُرُبَاتٍ عِندَ اللَّـهِ وَصَلَوَاتِ الرَّسُولِ أَلَا إِنَّهَا قُرْبَةٌ لَّهُمْ سَيُدْخِلُهُمُ اللَّـهُ فِي رَحْمَتِهِ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٩٩﴾

99. Miongoni mwa mabedui wako wanaomwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, na wanachukulia wanayoyatoa ndiyo ya kuwasogeza kwa Mwenyezi Mungu na dua za Mtume. Sikilizeni! Hakika hayo ni mambo ya kuwasogeza, Mwenyezi Mungu atawaingiza katika rehema yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha, Mwenye kurehemu.

MABEDUI WAMEZIDI SANA

Aya 97 – 99

USHAMBA NA KUENDELEA

Mabedui wamezidi sana katika kufuru na unafiki na wameelekea zaidi kutojua mipaka ya yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu juu ya Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.

Hii haina maana ya kuwagawanya watu kwenye ushamba na kuendelea kuwafanya bora watu wa mjini kuliko mabedui. Vipi? Iwe hivyo na hali Mwenyezi Mungu, katika Aya inayofuatia, anaelezea kuwa kuna watu katika mabedui wenye ikhlasi katika imani yao na matendo yao.

Kama ingelikuwa ubedui ni dhambi basi angeliuharamisha, sawa na alivyoharamisha dhulma. Na Qur’ani huwagawanya watu kwa misingi ya takua, yaani kumwamini Mwenyezi Mungu na amali njema, na imebainisha hakika hii na kuisisitiza kwa mifumo mbali mbali, bali hakika hiyo ndiyo lengo la kwanza na la mwisho la kuteremsha Qur’ani, mwito wake, mafunzo yake na sharia yake.

Aya hii tuliyo nayo inaashiria hilo kwani kauli yake hiyo Mwenyezi Mungu:

“Mabedui wamezidi sana katika kufuru na unafiki” inafahamisha kuwa sababu ya kutukanwa ni ukafiri na unafiki na kutojua hukumu za Mwenyezi Mungu alizoteremsha kwa Mtume wake, na wala ubedui sio sababu ya kutusiwa.

Ni kweli kuwa maisha ya ubedui (ushamba) na kuwa kwake mbali na maendeleo na maarifa, yanasababisha tabia ngumu na ya ovyo na kukeuka mipaka, lakini hilo ni kosa la mazingara sio kosa la ubedui, Kuna hadith isemavyo ifahamuni halali na haramu, vinginevyo basi nyinyi ni mabedui.” Yaani mtakuwa kama wao katika ujinga na kuwa mbali na maendeleo.

Baada ya utangulizi huu, sasa turudie kwenye Aya, Maana yaliyo kusudiwa katika Aya ni kuwa katika mabedui kuna makafiri na wanafiki sawa na wakazi wa mjini, isipokuwa makafiri wa kibedui na wanafiki wao ni zaidi kuliko wengine katika wakazi wa mjini.

Hayo ndio maana yanayopatikana katika dhahiri ya Aya, nasi tunaongezea kwamba ikiwa sababu inayowajibisha hilo ni ugumu wa tabia basi vile vile watakuwa ni wenye imani zaidi wakiamini na wenye ikhlasi zaidi watakapokuwa na ikhlasi, kwa vile sababu ni moja.

Kwa mnasaba huu tunadokeza maelezo yaliyokuja katika Kitabu Mizan Sha’rani, mlango wa Shahada, ninamnukuu: “Hambali hawakubali ushahidi wa bedui dhidi ya mtu wa mjini na Malik anaukubali katika kujeruhi na kuua tu, lakini sio katika haki nyingine”.

Tunajua wajihi wa anayesema kuwa haukubaliwi ushahidi wa asiyekuwa Mwislamuu dhidi ya Mwislamuu. Lakini kumlinganisha Bedui mwislamu na asiye kuwa mwislamu katika ushahidi, hatujui kumepitiwa njia gani. Mwenyezi Mungu anasema:

وَأَشْهِدُوا ذَوَيْ عَدْلٍ مِّنكُمْ ﴿٢﴾

“Na mshuhudishe mashahidi wawili waadiilifu miongoni mwenu” (65:2)

na wala hakusema katika wakazi wa mjini. Linalozingatiwa katika kukubaliwa ushahidi ni uadilifu sio ushamba wala kuendelea.

Miongoni mwa mabedui wako wanaochukulia kuwa wanayoyatoa ni gharama ya bure.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja kuwa miongoni mwa mabedui wako wanafiki, hapa anataja kuwa wao wanatoa mali zao, lakini wanaona kutoa huku ni gharama za bure sizizokuwa na faida, na kwamba thawabu na malipo yake siku ya Kiyama ni mambo ya kubandikwa tu.

Na wanawangojelea misiba.

Wanangonjea maadui wawashinde waislamu na wanatamani wamalizwe ili wapumzike na gharama hii ya hasara, kama wanavyoitakidi.

Misiba mibaya itakuwa juu yao.

Kuna kundi katika wafasiri wanaosema kuwa hii ni dua kwa wanafiki kuwa yawapate yale wanayowatamania Waumini. Pia inawezekana kuwa ni kutolea habari hali ya adhabu watakayokuwa nayo wanafiki siku ya Kiyama.

Na Mwenyezi Mungu ni Msikizi Mjuzi,

Anasikia wanayoyasema na anajua wanayoyaficha.

Miongoni mwa mabedui wako wanaomwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, na wanachukulia wanayoyatoa ndiyo ya kuwasogeza kwa Mwenyezi Mungu na dua za Mtume.

Mabedui ni kama watu wengine wako wanafiki wanaonyesha yasiyokuwa katika nyoyo na kuona wanayoyatoa ni gharama za bure sio wajibu; kama ilivyodokeza Aya iliyotangulia.

Na miongoni mwao wako Waumini wenye ikhlasi wanaotoa kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu na thawabu zake na kutaka dua ya Mtume ya kupata baraka na maghufira, kama ilivyoashiria Aya hii.

Sikilizeni! Hakika hayo ni mambo ya kuwasogeza, Mwenyezi Mungu atawaingiza katika rehema yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha, Mwenye kurehemu.

Dhamiri ya hayo ni yale wanayoyatoa; yaani kutoa huko kunakurubisha kwa Mwenyezi Mungu.

Maana ni kuwa wale walioamini wakatoa kwa kutaka kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu atakubali kutoa kwao; atawaingiza katika pepo yake na atawasamehe makosa waliyotekeleza na kuyakosa.

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ ﴿١٠٠﴾

100. Na waliotangulia wa kwanza katika wahajiri na Ansari. Na wale waliowafuata kwa wema. Mwenyezi Mungu yuko radhi nao na wao wako radhi naye; na amewaandalia Bustani zipitazo mito chini yake, watadumu humo milele, Huko ndiko kufuzu kukubwa.

وَمِمَّنْ حَوْلَكُم مِّنَ الْأَعْرَابِ مُنَافِقُونَ وَمِنْ أَهْلِ الْمَدِينَةِ مَرَدُوا عَلَى النِّفَاقِ لَا تَعْلَمُهُمْ نَحْنُ نَعْلَمُهُمْ سَنُعَذِّبُهُم مَّرَّتَيْنِ ثُمَّ يُرَدُّونَ إِلَىٰ عَذَابٍ عَظِيمٍ ﴿١٠١﴾

101. Na miongoni mwa mabedui walio pambizoni mwenu wamo wanafiki na katika wenyeji wa Madina wako waliobobea katika unafiki, Huwajui, sisi tunawajua, Tutawaadhibu mara mbili, kisha watarudishwa kwenye adhabu kubwa.

وَآخَرُونَ اعْتَرَفُوا بِذُنُوبِهِمْ خَلَطُوا عَمَلًا صَالِحًا وَآخَرَ سَيِّئًا عَسَى اللَّـهُ أَن يَتُوبَ عَلَيْهِمْ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿١٠٢﴾

102. Na wengine wamekiri dhambi zao; wakachanganya vitendo vyeman vingine viovu, Huenda Mwenyezi Mungu akapokea toba zao, Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wamsamaha, Mwenye kurehemu.

WALIOTANGULIA WA KWANZA

Aya 100 – 102

MAANA

Katika Aya hizi tatu Mwenyezi ametaja aina nne katika uma, kisha akaongezea aina ya tano katika Aya 106, tutaizungumzia tutakapofika huko. Ama aina nne ni hizi:

Na waliotangulia wa kwanza katika wahajiri na Ansari.

Wote (Wahajiri na Ansari) wamefanywa ni aina mbili zilizotangulia. Hakuna mwenye shaka kuwa makasudio ya kutangulia ni katika Hijra na Nusra (kuhama na kuwasaidia waliohama).

Sifa inatambulisha hivyo, lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakuelezea wakati wa huko kutangulia. Ndio maana wakatofautiana wafasiri: Kuna wenye kusema kuwa makusudio ni kuhama na usaidizi kabla ya siku ya Badr. Wengine wanasema kuwa ni kabla ya Baia ya Ridhwani iliyokuwa chini ya mti siku ya Hudaibia. Mwingine anasema ni wale walioswali Qibla mbili.

Tuonavyo sisi ni kwamba waliotangulia kuhama na kusadia (Muhajirin na Ansari) ni kabla ya waislamu kuwa na nguvu ya kuwazuia wanaowa- chokoza na kufitini dini yao; kama walivyofanya washirikiana mwanzo wa dawa.

Kwa hiyo basi kauli ya kwanza ndiyo yenye nguvu, kwa sababu nguvu ya waislamu ilidhihiri siku ya Badr walipohisi washirikina ukakamavu na nguvu ya Uislamu.

Na wale waliowafuata kwa wema.

Nao ni kila mwenye kwenda njia ya waliotangulia wenye ikhlasi. Anasema Tabrasi: Anaingia katika hao kila atakayekuja baada yao hadi Kiyama”.

Yamekuja maelezo ya waliowafuata kwa wema katika Aya isemayo:

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ ﴿١٠﴾

“Na wale waliokuja baada yao wanasema: Mola wetu! Tughufurie sisi na ndugu zetu waliotutangulia katika imani wala usijaalie katika nyoyo zetu mfundo kwa walioamini. Mola wetu! Hakika wewe ni Mpole sana Mwenye kurehemu” (59:10).

Tunataraji watapata funzo kwa Aya hii wale wanaotoa mwito wa imani na huku wenyewe wamejawa na mifundo ya hasadi.

Aina mbili hizi – waliotangulia na waliowafuatia – ndio ambaoMwenyezi Mungu yuko radhi nao na wao wako radhi naye na amewaandalia Bustani zipitazo mito chini yake, watadumu humo milele.

Mwenyezi Mungu yuko radhi nao kwa twaa yao na ikhlasi yao, na wao wako radhi naye kwa neema alizowamiminia.

Huko ndiko kufuzu kukubwa.

Yaani hakuna kufuzu kwa maana yake sahihi ila kwa radhi ya Mwenyezi Mungu.

Utauliza : Dhahiri ya Aya inaonyesha kule tu kutangulila kwa kuhama na kusaidia, kunatosheleza kupata radhi za Mwenyezi Mungu, na kwamba huo ni wema usiodhuriwa na uovu. Sasa je, dhahiri hii, ni hoja kiasi ambacho ni wajibu kwetu kumtukuza kila aliyetangulia kwa Hijra na Nusra, hata kama yamethibiti kwake maasi?

Jibu : Makusudio ya waliotangulia wa kwanza ni wale waliomtii Mwenyezi Mungu na wakafa juu ya sunna ya Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) .

Ama wale waliomwasi na wakafanya uovu baada ya kutangulia hawachanganywi na walio na radhi ya Mwenyezi Mungu; vipi iwe hivyo na hali yeye Mwenyezi Mungu anasema:

مَن يَعْمَلْ سُوءًا يُجْزَ بِهِ وَلَا يَجِدْ لَهُ مِن دُونِ اللَّـهِ وَلِيًّا وَلَا نَصِيرًا ﴿١٢٣﴾

“Mwenye kutenda uovu atalipwa kwa ovu huo, Wala hatajipatia mlinzi wala msaidizi zaidi ya Mwenyezi Mungu.” Juz.5 (4:123)

لِيَجْزِيَ اللَّـهُ كُلَّ نَفْسٍ مَّا كَسَبَتْ إِنَّ اللَّـهَ سَرِيعُ الْحِسَابِ ﴿٥١﴾

“Ili Mwenyezi Mungu ailipe kila nafsi kwa yale iliyoyachuma, Hakika Mwenyezi Mungu ni mwepesi wa kuhisabu” (14:51).

Na amepokea Bukhari, katika sahih yake Juz.9 Kitabu Alfitan mlango wa kwanza, Hadith isemayo:

“Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) atasema siku ya Kiyama: Hao ni swahaba zangu. Naye ataambiwa: Hujui walifanya nini baada yako. Hapo nitasema: Ole wake! Ole wake, mwenye kuibadilisha (dini yake) baada yangu” [1]

Hakuna mwenye shaka kwamba waliotangulia katika kuhama na kusaidia wahamiaji wana ubora, lakini hili ni jambo jingine na kusamehewa maasi au kuwa wasihisabiwe ni jambo jingine.

3.Na miongoni mwa mabedui walio pambizoni mwenu wamo wanafiki na katika wenyeji wa Madina wako waliobobea katika unafiki, Huwajui, sisi tunawajua.

Amekwisha taja Mwenyezi Mungu (s.w.t) wanafiki katika Aya kadhaa, Hapa anawataja kwa mnasaba wa kuwataja waumini waliotangulia; na ili kumpa habari Mtume wake mtukufu sehemu walikokwamba wao wamemzunguka kila upande.

Wako Madina anapokaa yeye na vitongojini mwake, sehemu za jangwani. Na kwamba wanafiki wa Madina ni mahodari katika fani ya unafiki kiasi cha kuweza kuuficha kwa Mtume pamoja na kuwa nao wakati mwingi. Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) anabainisha malipo ya wanafiki kwa kauli yake:

Tutawaadhibu mara mbili, kisha watarudishwa kwenye adhabu kubwa.

Adhabu hii ya mwisho ambayo watarudishwa ni maarufu, Jahanamu. Ama aina na wakati wa adhabu ya mara ya kwanza na ya pili kabla ya adhabu ya Jahanamu, haikuashariwa na Aya.

Sio mbali kuwa adhabu ya mara ya kwanza ni wakati wa kufa kwa sababu ya kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu:

وَلَوْ تَرَىٰ إِذْ يَتَوَفَّى الَّذِينَ كَفَرُوا الْمَلَائِكَةُ يَضْرِبُونَ وُجُوهَهُمْ وَأَدْبَارَهُمْ وَذُوقُوا عَذَابَ الْحَرِيقِ ﴿٥٠﴾

“Na lau ungeliwaona Malaika wanapowafisha wale waliokufuru wakipiga nyuso zao na migongo yao na (kuwaambia) ionjeni adhabu iunguzayo” Juz.10 (8:50).

Ama adhabu ya mara ya pili ni adhabu ya kaburi kutokana na Hadith nyingi kuwa kaburi ya kafiri ni shimo miongoni mwa mashimo ya Jahanamu, na kaburi ya mumin ni bustani katika bustani za peponi.

4.Na wengine wamekiri dhambi zao; wakachanganya vitendo vyema na vingine viovu.

Hawa ni wale waumini ambao mara kwa mara wanafanya mema kwa msukumo wa imani yao na mara nyingine hawaa hushinda imani yao wakafanya uovu, nao ni wengi. “Ni nani ambaye hulka zake zote zinaridhisha” isipokuwa wale waliohifadhiwa na Mola wako. Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) akabainisha hukumu ya hawa kwa kauli yake:

Huenda Mwenyezi Mungu akapokea toba zao kwa vile wao wametambua makosa na kuyakiri kwa hiyo wamekuwa, kwa hilo, ni mahali pa kutarajia rehema ya Mwenyezi Mungu na maghufira yake.

Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

Katika Majmaul-Bayan imeelezwa: “Wafasiri wanasema: ‘Huenda’ ikitoka kwa Mwenyezi Mungu inakuwa ni hakika; isipokuwa amesema ‘huenda’, ili wawe baina ya tamaa na wasibwete wakupuuza toba.