2
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MOJA
خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا وَصَلِّ عَلَيْهِمْ إِنَّ صَلَاتَكَ سَكَنٌ لَّهُمْ وَاللَّـهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴿١٠٣﴾
103. Chukua sadaka katika mali zao uwasafishe na uwatakase kwayo. Na uwaombee rehema, Hakika maombi yako ni utulivu kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Msikizi, Mjuzi.
أَلَمْ يَعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ هُوَ يَقْبَلُ التَّوْبَةَ عَنْ عِبَادِهِ وَيَأْخُذُ الصَّدَقَاتِ وَأَنَّ اللَّـهَ هُوَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ ﴿١٠٤﴾
104. Je, hawajui kwamba Mwenyezi Mungu ndiye anayekubali tob aya waja wake na kuzipokea sadaka. Na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kukubali toba, Mwenye kurehemu?
وَقُلِ اعْمَلُوا فَسَيَرَى اللَّـهُ عَمَلَكُمْ وَرَسُولُهُ وَالْمُؤْمِنُونَ وَسَتُرَدُّونَ إِلَىٰ عَالِمِ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ فَيُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿١٠٥﴾
105. Na sema: Tendeni vitendo Mwenyezi Mungu na Mtume wake na waumini wataviona vitendo vyenu na mtarudishwa kwa Mjuzi wa ghaibu na dhahiri, naye awaambie mliyokuwa mkiyatenda.
وَآخَرُونَ مُرْجَوْنَ لِأَمْرِ اللَّـهِ إِمَّا يُعَذِّبُهُمْ وَإِمَّا يَتُوبُ عَلَيْهِمْ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴿١٠٦﴾
106. Nawengine wanangojea amri ya Mwenyezi Mungu, ama atawaadhibu au awakubalie toba, Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.
CHUKUA SADAKA KATIKA MALI ZAO
Aya 103 – 106
MAANA
Chukua sadaka katika mali zao uwasafishe na uwatakase kwayo.
Wameafikiana kuwa dhamir katika ‘kwayo’ ni ya sadaka, na wakahitalifiana katika dhamir ya mali zao. Ikasemwa kuwa inawarudia wale waliochanganya amali njema na mbaya Ikasemwa kuwa inawarudia matajiri wote kwa sababu Aya imeshuka katika zaka ya wajibu. Kauli hii iko karibu na maana.
Kwa hiyo maana yatakuwa ni chukua ewe Mtume! Zaka katika mali za matajiri, kwani zinawatakasa na ubakhili kwa haki ya Mwenyezi Mungu. Tumezungumzia zaka katika kufasiri Aya 60 ya Sura hii, na Juz. 3 (2: 274)
Na uwaombee rehema, Hakika maombi yako ni utulivu kwao.
Yaani muombee baraka na maghufira mwenye kutoa zaka, kwani hupata furaha na raha ya nafsi kwa dua yao.
Na Mwenyezi Mungu ni Msikizi, Mjuzi.
Anasikia na ataitikia maombi yako kwa watoaji zaka, na anajua nia ya anayetoa zaka kwa roho safi, kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu peke yake.
Je, hawajui kwamba Mwenyezi Mungu ndiye anayekubali toba ya waja wake na kuzipokea sadaka?
Mfumo unaashiria kwamba toba imetajwa hapa kwa kuashiria kuwa mwenye kuzuia zaka, kisha akatubia na akaitoa, basi Mwenyezi Mungu ataikubali toba yake na kupokea sadaka yake. Maana ya kukubali ni kwamba Mweneyezi Mungu, ambaye limetukuka neno lake atailipa thawabu. Kuna Hadith isemayo: “Hakika sadaka inaingia mkononi mwa Mwingi wa rehema kabla ya kuingia katika mkono wa mwombaji.” Mkono wa Mwingi wa rehema ni fumbo la kukubali.
Na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kukubali toba, Mwenye kurehemu?
Yaani anakubali toba na kuwarehemu wenye kutubia.
Na sema: Tendeni vitendo Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Waumini wataviona vitendo vyenu.
Katika kitabu Futuhatul-Makkiyaa J4, ameitaja Muhyiddin bin Al-arabi, Aya hii na kuifafanua kuwa maana ya kuona yanatofautiana kulingana na mwonaji. Kwa hiyo maana ya kuona kwa Mwenyezi Mungu ni kukijua kitu kwa pande zake zote. Maana yake kwa Mtume(s.a.w.w)
ni kujua kitu kwa njia ya wahyi uliomshukia. Maana yake kwa na mumin mwenye maarifa, ni kujua kwa kadiri ya alivyojua na kufahamu kutokana na wahyi ulioteremshiwa Mtume(s.a.w.w)
.
Kwa hiyo basi, mwenye kufanya amali kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu anajua hakika ya amali yake na kuiridhia; Mtume naye anajua kuwa amali hii imeridhiwa kwa Mwenyezi Mungu, na mumin pia anajua kuwa ni mwenye kuridhiwa na Mtume. Natija ya mwisho ni kuwa mwenye kufanya amali njema anaridhiwa na Mwenyezi Mungu, Mtume na waumini.
Na wengine wanangojea amri ya Mwenyezi Mungu, ama atawaadhibu au awakubalie toba.
Katika Aya ya 100 na inayofuatia, Mwenyezi Mungu (s.w.t), ametaja aina nne ya watu: Waliotangulia kuhama na waliotangulia kusaidia, waliowa- fuatia hao kwa wema, wanafiki na wenye kukiri dhambi zao.
Katika Aya hii ameashiria watu ambao hakuwapa sifa maalum, kama alivyofanya kwa aina hizo nne, wala hakuweka wazi hukumu yao; isipokuwa amesema kuwa wao wanangojea adhabu ya Mwenyezi Mungu au msamaha wake; yaani jambo lao liko Kwake Yeye Peke Yake, amewaficha. Huenda hekima ya hivi ni kuwa wawe baina ya kuhofia na kutarajia, wasiwe na tamaa wala kukata tamaa.
Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.
Ni Mjuzi, wa yanayowafaa hawa na wengineo, na ni mwenye hekima kati- ka kufanya wangojee hukumu yao na katika kila analolifanya.
Wafasiri wengi wanasema kuwa Aya hii iliwashukia jamaa katika waislam waliobaki nyuma katika vita vya Tabuk, kisha wakajuta.
Lakini Aya 118, imeeleza kuwa masahaba watatu walibaki nyuma katika vita ya Tabuk, kisha wakatubia na kwamba Mwenyezi Mungu aliwatakabalia toba yao na akatangaza kukubali kwake, wala hakuwacha baina ya kuhofia na kukata tamaa.
Haya ndiyo yaliyotudhihirikia katiaka kufasiri Aya hii tuliyo nayo: hatujui tutapata maana gani tutakapofikia Aya hiyo ya 118, Tuonane huko.
وَالَّذِينَ اتَّخَذُوا مَسْجِدًا ضِرَارًا وَكُفْرًا وَتَفْرِيقًا بَيْنَ الْمُؤْمِنِينَ وَإِرْصَادًا لِّمَنْ حَارَبَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ مِن قَبْلُ وَلَيَحْلِفُنَّ إِنْ أَرَدْنَا إِلَّا الْحُسْنَىٰ وَاللَّـهُ يَشْهَدُ إِنَّهُمْ لَكَاذِبُونَ ﴿١٠٧﴾
107. Na wale waliotengeza msikiti kwa ajili ya kudhuru na ukafiri na kuwafarikisha waumini na mahali pa kuvizia kwa yule aliyempiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume hapo kabla. Na bila shaka wataapa kwamba hutakukusudia ila wema; na Mwenyezi Mungu anashuhudia kuwa wao ni waongo.
لَا تَقُمْ فِيهِ أَبَدًا لَّمَسْجِدٌ أُسِّسَ عَلَى التَّقْوَىٰ مِنْ أَوَّلِ يَوْمٍ أَحَقُّ أَن تَقُومَ فِيهِ فِيهِ رِجَالٌ يُحِبُّونَ أَن يَتَطَهَّرُوا وَاللَّـهُ يُحِبُّ الْمُطَّهِّرِينَ ﴿١٠٨﴾
108. Usisimame humo kabisa, Msikiti uliojengwa juu ya msingi wa takua tangu siku ya mwanzo, unastahiki zaidi wewe usimame humo. Humo mna watu wanopenda kuji takasa; na Mwenyezi Mungu anawapenda wanaojitakasa.
أَفَمَنْ أَسَّسَ بُنْيَانَهُ عَلَىٰ تَقْوَىٰ مِنَ اللَّـهِ وَرِضْوَانٍ خَيْرٌ أَم مَّنْ أَسَّسَ بُنْيَانَهُ عَلَىٰ شَفَا جُرُفٍ هَارٍ فَانْهَارَ بِهِ فِي نَارِ جَهَنَّمَ وَاللَّـهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ ﴿١٠٩﴾
109. Je, aliyeweka msingi wa jengo lake juu ya kumcha Mwenyezi Mungu na radhi (zake) ni bora au aliyeweka msingi jingo lake juu ukingo wa shimo linalomomonyoka, na likamomonyoka likaanguka pamoja naye katika moto wa Jahannamu na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu madhalimu.
لَا يَزَالُ بُنْيَانُهُمُ الَّذِي بَنَوْا رِيبَةً فِي قُلُوبِهِمْ إِلَّا أَن تَقَطَّعَ قُلُوبُهُمْ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴿١١٠﴾
110. Jengo lao hilo walilolijenga litaendelea kuwa ni sababu ya kutiwa wasiwasi nyoyoni mwao, isipokuwa nyoyo zao zikikatikakatika. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.
MSIKITI WA MADHARA
Aya 107 –110
MAANA
Aya zilizotangulia zimeonyesha aina mbali mbali za unafiki wa wanafiki. Aya hii inaonyesha aina nyingine ya unafiki wao na hila yao.
Jamaa fulani katika wanafiki wa Madina waliona njia nzuri ya kuufanyia vitimbi Uislam na Mtume wake Muhammad(s.a.w.w)
ni kujenga msikiti chini ya sitara ya kujumuika kumwabudu Mwenyezi Mungu na kunadi kuwa Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Nyuma ya nembo hii watakuwa wamemkufuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kuudhuru Uislamu na waislam na kuwagawanya.
Naam walijenga msikiti huu vizuri sana na kuutolea mapesa. Baada ya kuukamilisha walimwendea Mtume wa Mwenyezi Mungu wakamwambia: Nyumba zetu ziko mbali na msikiti wako inakuwa vigumu kwetu kuhudhuria na tunachukia kuswali swala isiyokuwa ya Jamaa; nasi tumejenga msikiti kwa lengo hili na kwa ajili ya wanyonge na vilema. Kama utaswali humo basi itakuwa ni vizuri na tutabaruku kuswali mahali utakaposwali.
Hivi ndivyo walivyo wanafiki na wahaini kila wakati, wanabeba nembo za kutengeneza kumbe wanataka kubomoa. Lakini mara moja inafichuka aibu yao na kufedheheka mbele ya watu wote; kama walivyofedheheka wenye msikiti wa madhara, pale Mwenyezi Mungu alipomfahamisha Mtume wake hakika yao, kwa kusema:
Na wapo waliotengeza msikiti kwa ajili ya kudhuru na ukafiri na kuwafarikisha waumini na mahali pa kuvizia kwa yule aliyempiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume hapo kabla.
Aya tukufu inasema kuwa waliojenga msikit wa madhara wana malengo manne:
1. Kuwadhuru waislamu.
2. Kumkufuru Mwenyezi Mungu na kumtia ila Mtume wake.
3. Kuwagawanya waislamu na kuwaweka mbali na Mtume wa Mwenyezi Mungu.
4. Kuufanya msikiti ni maficho ya yule aliyempiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume wake zamani.
Wameafikiana wafasiri na waandishi wa sera ya Mtume kwamba makusudio ya adui aliyempiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume wake ni mtu mmoja katika Khazraji anyeitwa Abu Amir Arrahib
.
Alikuwa ameingia ukiristo, mwenye cheo katika watu wake, Mtume(s.a.w.w)
alipofika Madina alipambana kiuadui na mlanifu huyu ambaye Mtume alikuwa akimwita fasiki.
Alipoona Mtume anazidi kupata nguvu, alikimbilia Makka kuwachochea Maquraish dhidi ya Mtume, Baada ya ushindi wa Makka alikimbilia Taif.
Watu wa Taif waliposilimu alikimbilia Sham. Huko aliwaandikia wafuasi wake wamjengee msikiti kwa sababu yeye atakuja na jeshi la Kaizari kumpiga vita Muhammad(s.a.w.w)
.
Iliposhuka Aya hii, Mtume(s.a.w.w)
akiwambia baadhi ya masahaba zake: “Nendeni kwenye msikiti huu wa watu madhalimu muuvunje.”
Wakafanya hivyo na Mtume(s.a.w.w)
akaamrisha pale mahali pawe ni jaa. Baadhi ya mapokezi yameelezea kufananishwa msikiti wa madhara na ndama aliyeabudiwa na Waisrail na Musa akiwa hai. Kama ambavyo Nabii Musa aliamrishwa na Mwenyezi Mungu (s.w.t) kumvunjavunja ndama, vile vile Mtume aliamrishwa auvunje mskiti wa madhara.
Na, msikiti wowote, taasisi au klabu yoyote inayoundwa kwa sababu ya njama dhidi ya waumini basi hiyo ni ndama wa waisrail na ni msiki wa madhara, ni wajibu kuuvunja na kuufanya jaa.
Tangu yalipopatikana mafuta katika miji ya Kiarabu, mashirika ya nje ya kusimamia mafuta yalikuja na maamia ya misikiti ya madhara kwa sura mbali mbali. Miongoni mwa sura hizo ni kama hizi zifuatazo: Ile iliyobandikwa jina la sehemu ya kuabudia au vyuo, yenye jina la ofisi kuu au taasisi za kidini na yenye majina ya maendeleo ya kijamii au vilabu vya michezo.
Mingine ni ile iliyojitokeza kwa sura ya kitab, gazeti au mhadhara unao tangazwa kwenye idhaa kwa jina la dini au la nchi na mengineyo mengi ambayo dhahiri yake ni rehema na ndani yake ni adhabu. Yote hayo lengo lake ni kuharibu dini na nchi.
Tumezungumzia kuhusu nembo za kidini katika Juz 4 (3:142)
Na bila shaka wataapa kwamba hutakukusudia ila wema; na Mwenyezi Mungu anashuhudia kuwa wao ni waongo.
Yaani hawa wanafiki waliapa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
kwamba lengo la kujenga msikiti huu ni ibada tu na manufaa kwa waislamu; na Mwenyezi Mungu anajua kuwa wao hawakujenga msikiti ila kwa kutaka kuwadhuru waislamu, kumkufuru Mwenyezi Mungu, kuwatenganisha Waumini na maficho ya anayempiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume wake.
Usisimame humo kabisa.
Maneno anaambiwa Mtume, lakini makatazo ni kwa wote; sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu:
أَقِمِ الصَّلَاةَ لِدُلُوكِ الشَّمْسِ ﴿٧٨﴾
“Simamisha Swala jua linapopenduka” (17:78)
Wafasiri wamesema kuwa makusudio ya usisimame, hapa, ni usiswali. Lakini kwa dhahiri hapa, kusimama ni ujumla, kunachanganya swala na mengineyo.
Kwa vyovyote ilivyo, kauli yake Mwenyezi Mungu usisimame humo kabisa ni dalili mkataa ya kutosihi swala katika msikiti uliojengwa kuwadhuru waislamu na kuwatenganisha na kwamba mwenye kuswali humo, basi swala yake ni batil, ni lazima airudie mahali pengine, Kwa sababu ukatazo katika ibada unafahamisha kuharibika.
Msikiti uliojengwa juu ya msingi wa takua tangu siku ya mwanzo, unastahiki zaidi wewe usimame humo.
Imesemekana kuwa makusudio ni msikiti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w)
kwa sababu ndio uliojengwa siku ya kwanza Madina. Na ikasemekana kuwa ni Msikiti Quba ambao waliujenga Bani Amr bin Auf. Kwa dhahiri ni kwamba makusudio ni kila msikiti uliojengwa kwa ajili ya kumcha mungu, Kwa sababu neno Msikiti limekuja kiujumla (nak`ra).
Na kauli yake:‘Tangu siku ya mwanzo,
’ maana yake ni kuwa umejengwa kwa lengo la uislamu tangu siku ya kuanza kujengwa kwake. Kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Unastahiki zaidi,’ maana yake ni kwa uhakika, na wala sio kuwa huu ni bora zaidi kuliko wa madhara. Kwa sababu msikiti wa Madhara sio bora hata kidogo na haifai kuswali ndani yake kwa vyovyote vile.
Humo mna watu wanopenda kujitakasa; na Mwenyezi Mungu anawapenda wanaojitakasa.
Yaani, msikiti huu ambao umeasisiwa kwa msingi wa takua, wenye ikhlasi wanaukusudia kwa swala na ibada ya Mwenyezi Mungu tu, si kwa unafiki na njama dhidi ya uislamu na Mtume; kama walivyofanya wenye msikiti wa madhara.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameleta ibara ya swala hapa kwa neno kuji- takasa, kwa sababu swala inamtakasa mtu na madhambi. Kuna Hadith isemayo: “Hakika swala ni kama mto unaopita, mwenye kuoga humo mara tano kila siku hatabakiwa na uchafu; vile vile mwenye kuswali mara tano kila siku hatabakiwa na dhambi.
Haya ndiyo tuliyoyafahamu katika Aya hii, pamoja na kukiri kuwa hakuna mfasiri yeyote aliyefasiri kutakata kwa maana ya swala, kama tunavyojua; na kwamba wengi wao wamefasiri kwa maana ya kutakasa uchafu kwa maji.
Je, aliyeweka msingi wa jengo lake juu ya kumcha Mwenyezi Mungu na radhi (zake) ni bora au aliyeweka msingi jengo lake juu ya ukingo wa shimo linalomomonyoka, na likamomonyoka likaanguka pamoja naye katika moto wa Jahannamu na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu madhalimu.
Makusudio ya Aya ni kutofautisha baina ya msikiti wa Takua na msikiti wa madhara. Kwani wa madhara hauna uthabiti na unaweza ukaanguka kwenye moto mara moja; sawa na ambaye amejenga ukingoni mwa mto au kwenye mto. Ama jengo la msikiti wa takua ni thabiti lenye msingi imara usiotingishwa na chochote; na watu wake wako katika amani. Aya hii ni mfano wa Aya isemayo:
لَا يَسْتَوِي أَصْحَابُ النَّارِ وَأَصْحَابُ الْجَنَّةِ أَصْحَابُ الْجَنَّةِ هُمُ الْفَائِزُونَ ﴿٢٠﴾
“Hawalingani sawa watu wa motoni na watu wa peponi. Watu wa peponi ndio wenye kufuzu” (59:20).
La kushangaza ni kauli ya baadhi ya wafasiri kwamba kauli ya ‘moto wa Jahanamu’ ni ishara ya yaliyotukia duniani kuwa moto ulitoka kwenye mskiti wa madhara na moshi wake ukabakia hadi zama za Abu jafar Al-Mansuru.
Jengo lao hilo walilolijenga litaendelea kuwa ni sababu ya kutiwa wasiwasi nyoyoni mwao, isipokuwa nyoyo zao zikikatikakatika. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.
Makusudio ya wasiwasi hapa, ni kwamba wanafiki hawakuamini utume wa Muhammad(s.a.w.w)
. Kukatika nyoyo ni fumbo la kufa. Maana ni kuwa wao walijenga msikiti wakiwa na shaka bila ya kumwamini Muhammad(s.a.w.w)
, watabaki na shaka hiyo hadi kufa.
إِنَّ اللَّـهَ اشْتَرَىٰ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ أَنفُسَهُمْ وَأَمْوَالَهُم بِأَنَّ لَهُمُ الْجَنَّةَ يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَيَقْتُلُونَ وَيُقْتَلُونَ وَعْدًا عَلَيْهِ حَقًّا فِي التَّوْرَاةِ وَالْإِنجِيلِ وَالْقُرْآنِ وَمَنْ أَوْفَىٰ بِعَهْدِهِ مِنَ اللَّـهِ فَاسْتَبْشِرُوا بِبَيْعِكُمُ الَّذِي بَايَعْتُم بِهِ وَذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ ﴿١١١﴾
111. Hakika Mwenyezi Mungu amenunua kwa Waumini nafsi zao na mali zao kwamba wao wapate Pepo, wanapi gana katika njia ya Mwenyezi Mungu, kwa hiyo wanaua na kuuawa. Ni ahadi aliyojilazimisha kwa haki katika Tawrat na Injil na Qur’ani. Na ni nani atekelezaye zaidi ahadi kuliko Mwenyezi Mungu? Basi furahini kwa biashara yenu mliofanya naye, Na huko ndiko kufuzu kukubwa.
التَّائِبُونَ الْعَابِدُونَ الْحَامِدُونَ السَّائِحُونَ الرَّاكِعُونَ السَّاجِدُونَ الْآمِرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَالنَّاهُونَ عَنِ الْمُنكَرِ وَالْحَافِظُونَ لِحُدُودِ اللَّـهِ وَبَشِّرِ الْمُؤْمِنِينَ ﴿١١٢﴾
112. Wanaotubia, wanaoabudu wanaohangaika, wanaorukuu, wanaosujudu, wanaoamrisha mema na wanaokataza maovu na wanaohifadhi mipaka ya Mwenyezi Mungu, Na wape bishara Waumini.
MUNGU HUUZA NA KUNUNUA
Aya 111 – 112
MAANA
Hakika Mwenyezi Mungu amenunua kwa Waumini nafsi zao na mali zao kwamba wao wapate Pepo, wanapigana katika njia ya Mwenyezi Mungu, kwa hiyo wanaua na kuuawa.
Mnunuzi ni Mwenyezi Mungu (s.w.t) muuzaji ni mumin, bidhaa ni nafsi na mali, cha kununuliwa ni pepo, na madalali ni Mitume. Bei yenyewe ni ya mkopo; kwamba muuzaji akabidhi bidhaa kwa mnunuzi atakapoitaka, lakini thamani yake atalipwa baadaye; na Mwenyezi Mungu ndiye mdhamini; na hakuna mwenye kutekeleza ahadi na tajiri zaidi ya Yeye.
Utauliza
: Mungu ni muumbaji wa nafsi na Mwenye kuruzuku mali, sasa vipi mwenye kumiliki kitu akinunue.
Jibu
: Huku siko kununua kunakojulikana; isipokuwa ni kuhimiza twaa. Mwenyezi Mungu ameleta ibara ya kununua kwa mambo mawili:
Kwanza
: mtiifu ategemee malipo na thawabu ya twaa yake; sawa na anavyotegemea muuzaji thamani badala ya bidhaa yake.
Pili
: kuzindua kuwa imani sio tu maneno ya mdomoni, picha za akilini au matamanio yanayohisiwa katika nyoyo; isipokuwa ni kujitolea mhanga kwa nafsi na mali, kutafuta thawabu za Mwenyezi Mungu ambazo ni ghali zisizokwisha; sawa na anavyotoa mnunuzi milki yake katika bidhaa ambayo anaiona ina manufaa na yenye kufaa.
Kitu kikubwa kwa binadamu ni uhai wake na nafsi yake. Ama kupenda kwake mali ni kwa kuwa hiyo ni nyenzo ya kuhifadhi uhai na kutekeleza matakwa yake na hawaa zake.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawatahini wanaodai wana imani kwa vitu wanavyovipenda ili ampabanue mkweli wa imani na mwongo; wala hataweza kutoa hoja kesho kwa saumu yake na swali yake akiwa amefanya ubakhili na kujizuia kujitolea kwa nafsi yake na mali yake.
Ni ahadi aliyojilazimisha kwa haki.
Hii ni sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu:
كَتَبَ عَلَىٰ نَفْسِهِ الرَّحْمَةَ ﴿١٢﴾
Amejilazimisha rehema Juz.7 (6:12)
Yaani yeye mwenyewe ndiye aliyejiwajibshia, Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewaahidi wapigania jihadi Pepo ikawa ni haki yao kutokana na ahadi hii;
hasa baada ya kuisajilikatika Tawrat na Injil na Qur’ani. Na ni nani atekelezaye zaidi ahadi kuliko Mwenyezi Mungu?
Lengo la usisitizo huu ni kuwa wapigania jihadi wawe na uhakika wa malipo na thawabu adhimu; mpaka wawe kama walioyaona kwa macho, wafurahi na wapate bishara.
Basi furahini kwa biashara yenu mliyofanya naye, Na huko ndiko kufuzu kukubwa.
Huu ni usisitizo mwingine wa ahadi ya malipo mema. Watalamu wa elimu ya Tawhidi wanasema kuwa Mwenyezi Mungu akiahidi thawabu, basi atatekeleza aliyoahidi, na akiahidi adhabu basi ana hiyari, akiadhhibu ni kwa uadilifu wake na akasamehe ni kwa fadhila zake; na Mwenyezi Mungu si mwenye kuwadhulumu waja.
Tumeizungumzia thamani ya Pepo katika kufasiri Juz. 2 (2:155).
Kisha Mwenyezi Mungu akawasifu wale waliouza nafsi zao na mali zao kwa Pepo yake, kwa sifa hizi zifuatazo:
•Wanaotubia
kwa kila wanalolikosea; hata kama ni la makruh.
•Wanaoabudu
. Yaani wenye ikhlasi katika matendo yao yote.
•Wanaohimidi
Mwenyezi Mungu katika raha na dhiki.
•Wanaohangaika
katika ardhi kutafuta elimu au riziki ya halali.
•Wanaorukuu, wanaosujudu,
Yaani wanaoswali.
•Wanaoamrisha mema na wanaokataza maovu.
yaani wanaoneza mwito wa Mwenyezi Mungu na twaa yake na kupamba na kila anayechezea haki yoyote miongoni mwa haki za Mungu na haki za waja wake.
•Na wanaohifadhi mipaka ya Mwenyezi Mungu
. Mipaka yake ni halali yake na haramu yake
•Na wape bishara Waumini
walio na sifa hizi, kuwa wao wana fadhila kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.