4
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MOJA
مَا كَانَ لِأَهْلِ الْمَدِينَةِ وَمَنْ حَوْلَهُم مِّنَ الْأَعْرَابِ أَن يَتَخَلَّفُوا عَن رَّسُولِ اللَّـهِ وَلَا يَرْغَبُوا بِأَنفُسِهِمْ عَن نَّفْسِهِ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ لَا يُصِيبُهُمْ ظَمَأٌ وَلَا نَصَبٌ وَلَا مَخْمَصَةٌ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَلَا يَطَئُونَ مَوْطِئًا يَغِيظُ الْكُفَّارَ وَلَا يَنَالُونَ مِنْ عَدُوٍّ نَّيْلًا إِلَّا كُتِبَ لَهُم بِهِ عَمَلٌ صَالِحٌ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُضِيعُ أَجْرَ الْمُحْسِنِينَ ﴿١٢٠﴾
120. Haiwafalii watu wa Madina na Mabedui walio kandoni mwao kubaki nyuma ya Mtume wa Mwenyezi Mungu; wala kujipendelea nafsi zao kuliko nafsi yake. Hayo ni kwa sababu ya kuwa hakiwapati kiu wala taabu wala njaa katika njia ya Mwenyezi Mungu; wala hawakanyagi ardhi ichukizayo makafiri, wala hakiwapati chochote kutokana na adui, ila huandikiwa kuwa ni amali njema. Hakika Mwenyezi Mungu haupotezi ujira wa watendao mazuri.
وَلَا يُنفِقُونَ نَفَقَةً صَغِيرَةً وَلَا كَبِيرَةً وَلَا يَقْطَعُونَ وَادِيًا إِلَّا كُتِبَ لَهُمْ لِيَجْزِيَهُمُ اللَّـهُ أَحْسَنَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٢١﴾
121. Wala hawatoi chochote cha kutumiwa kidogo wala kikubwa wala hawalikati bonde ila wanaandikiwa kuwa Mwenyezi Mungu awalipe mema ya yale waliyokuwa wakiyatenda.
HAIFAI WATU WA MADINA KUBAKI NYUMA
Aya 120 – 121
MAANA
Haiwafalii watu wa Madina na Mabedui walio kandoni mwao kubaki nyuma ya Mtume wa Mwenyezi Mungu; wala kujipendelea nafsi zao kuliko nafsi yake.
Mtume wa Mwenyezi Mungu ni Muhammad(s.a.w.w)
. Makusudio yake hapa ni dini ya Mwenyezi Mungu na haki, Kwa sababu dini ya haki inaun- dika katika utu wake mtukufu.
Kuinusuru haki ni wajibu kwa kila Mwislamu, wala hakuhusiki na watu wa Madina na walio kandoni mwao; isipokuwa wametajwa hao kwa kuwa karibu kwao na kuwa jirani, na pia kwa kulingana na mazungumzo ya vita vya Tabuk. Maana ni kuwa ni juu ya kila Mwislamuu kuinusuru haki na kuizuia batili wala asiathirike na manufaa na masilahi kuliko dini ya Muhammad, kwa kutoa visababu vya uwongo, kama walivyofanya wanafiki.
Hayo ni kwa sababu ya kuwa hakiwapati kiu wala taabu wala njaa katika njia ya Mwenyezi Mungu; wala hawakanyagi ardhi ichukizayo makafiri, wala hakiwapati chochote kutokana na adui, ila huandikiwa kuwa ni amali njema.
Hayo ni ishara ya kukataza kubaki nyuma na kuacha kuwapiga jihadi wabatilifu.
Ni jambo la kutia uchungu kwa mtu yeyote, awe Mwislamuu au la, kumwacha akanyage mchanga wa mji wake na nchi yake; pengine awe kibaraka asiye na dini wala dhamiri. Uislamu haumruhusu yeyote, vyovyote alivyo, kukanyaga ardhi ya mwingine ila kwa sababu mbili; Kuzuia madhara ya watu; kama vile kuzima moto kukinga mali na mali ya jirani.
Kuingiza nguvu iliyoadilifu itakayowazuia watu wa hapo na dhuluma na uadui kwa mji mwingine; kama alivyofanya Mtume(s.a.w.w)
katika vita vya Tabuk, baada ya Waroma kuazimia kuipiga madina na kuumaliza Uislamu na Mtume wake.
Hakika Mwenyezi Mungu haupotezi ujira wa watendao mazuri.
Hakuna kitu rahisi kwa mtu kuliko kufanya wema, maadamu Mwenyezi Mungu anakuandikia wema kukaa kwake, kusimama kwake, na hata unyao mmoja tu anaoukanyaga kwa ajili ya kumtii Mwenyezi Mungu.
Wala hawatoi chochote cha kutumiwa kidogo wala kikubwa wala hawalikati bonde ila wanaandikiwa kuwa Mwenyezi Mungu awalipe mema ya yale waliyokuwa wakiyatenda.
Haya na yaliyo kabla yake yanafupilizwa na kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu:
فَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ خَيْرًا يَرَهُ ﴿٧﴾
“Na atakayefanya heri uzani wa sisimizi ataiona” (99:7).
Lengo la ufafanuzi huu ni kuhimiza mali ya heri na kuhimiza kumpiga jihadi anayeeneza ufisadi katika ardhi.
وَمَا كَانَ الْمُؤْمِنُونَ لِيَنفِرُوا كَافَّةً فَلَوْلَا نَفَرَ مِن كُلِّ فِرْقَةٍ مِّنْهُمْ طَائِفَةٌ لِّيَتَفَقَّهُوا فِي الدِّينِ وَلِيُنذِرُوا قَوْمَهُمْ إِذَا رَجَعُوا إِلَيْهِمْ لَعَلَّهُمْ يَحْذَرُونَ ﴿١٢٢﴾
122. Wala haiwafalii waumini kutoka wote, Kwa nini kisitoke kikundi katika kila kundi miongoni mwao kuji funza dini na kuwaonya watu wao watakapowarudia, Ili wapate kujihadhari.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قَاتِلُوا الَّذِينَ يَلُونَكُم مِّنَ الْكُفَّارِ وَلْيَجِدُوا فِيكُمْ غِلْظَةً وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ مَعَ الْمُتَّقِينَ ﴿١٢٣﴾
123. Enyi mlioamini! Piganeni na wale walio karibu yenu katika makafiri na wakute kwenu ugumu; na jueni kuwa Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wenye takua.
KWA NINI KISITOKE KIKUNDI
Aya 122 – 123
MAANA
Wala haiwafalii waumini kutoka wote.
Aya hii inaungana na Aya iliyotangulia kuwa haifai watu wa Madina kubaki nyuma. Njia ya kuungana ni kwamba iliposhuka Aya iliyotangulia Makabila ya Kiislam yalisema: Wallahi kuanzia leo hatutabaki nyuma ya Mtume katika vita. Wakamiminika kutoka madina kwa lengo hili.
Ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akateremsha Aya hii, tuliyonayo, kuwa hawatakiwi kutoka wote kwa jihadi, bali hali hiyo inatofautiana kwa kutofautiana vita. Mara nyingine jihadi inakuwa ni wajibu kwa kila mtu, mara nyingine inakuwa ni wajibu kifaya, wakitekeleza baadhi basi wajibu umewaondokea wote.
Ama atakayetofautisha kati ya wajib hizo mbili ni Mtume(s.a.w.w)
. Watatoka Waislamu wote kama akitaka watoke, na watatoka baadhi akitaka hivyo.
Kwa nini kisitoke kikundi katika kila kundi miongoni mwao kujifunza dini na kuwaonya watu wao watakapowarudia.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kubainisha kuwa si wajibu kwa kundi lote kutoka katika kila vita, sasa ana bainisha kuwa kuna wajibu mwingine usiokuwa jihadi ambao ni wajibu kuutekeleza, sawa na jihadi; kama vile kutoka kikundi katika kila mji au kabila kwenda Madina au mahali penginepo, kujifunza dini ya Mwenyezi Mungu – wajue halali na haramu; kisha warudi kwa watu wao wawongoze na kuwatahadharisha na adhabu ya Mwenyezi Mungu inayotokana na kumwasi na kuhalifu amri zake.
Ili wapate kujihadhari.
Yaani wawasikilize wanowaongoza na wawatii.
Hivi ndivyo tulivyoona katika kufasiri Aya hii, tukiwa tumetofautiana na wafasiri wengi ambao wamefanya ‘kujifundisha’ ni sifa ya watakaobaki, sio watakaotoka; wakasema katika ufanuzi wao kuwa ni wajibu kwa Waislamu kugawanyika makundi mawili: Kundi liende kwenye Jihad na kundi jingine libaki Madina kujifunza sunna na faradhi.
Tafsiri tuliyokwenda nayo sisi ndiyo yenye asili katika riwaya za Ahlu Bait wa Mtume(s.a.w.w)
ambao ndio wajuzi zaidi wa Qur’ani na siri zake.
Miongoni mwa riwya hizo ni ile isemayo kuwa Mtu mmoja alimwuliza Imam Ja’far Asswadiq
kuhusu maana ya kauli ya Mtume(s.a.w.w)
: “Kutofautiana umati wangu ni rehema”. Akasema: Makusudio ya kutofautiana sio kuzozana, vinginevyo kuafikiana kwao ingelikuwa ni adhabu; isipokuwa makusudio ni kuhangaika duniani kutafuta elimu. Kisha Imam akaitolea dalili Aya hii kwa makusudio ya maana hayo.
Hakuna mwenye shaka kwamba dalili hiyo haikamliki ila ikiwa kujielimisha ni sifa ya kikundi kinachotoka sio kinachobaki.
Wanachuoni wa usul wameitolea dalili Aya hii kuwa ‘Habari Moja’ inayo nukuliwa kutoka kwa Masumu ni hoja inayopasa kutumiwa katika hukumu za kisharia Njia ya kutoa dalili ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ame- wajibisha kwa ulama kufundisha na kuonya. Na, ukishakuwa wajibu huu kwa ulama, basi imekuwa wajibu kwa asiyejua kukubali kauli ya ulama na kuitumia; vinginevyo itakuwa wajibu wa kujifundisha na kuonya; ni mchezo tu.
Vile vile ikiwa ni wajibu kwa asiyejua kujifundisha, basi imekuwa ni wajibu kwa ulama kufundisha; vinginevyo itakuwa wajibu wa asiyejua kujifundisha ni mchezo tu. Imam Ali
anasema:“Mwenyezi Mungu hatawaadhibu wajinga kwa kutojifundisha mpaka awaadhibu wenye elimu kwa kutofundisha”.
Enyi mlioamini! Piganeni na wale walio karibu yenu katika makafiri.
Aya hii inawahimiza Waislamu kulinda mipaka na maadui wa Mwenyezi Mungu na maadui zao. Katika Majmaul-bayan kuna maelezo kuhusu tafsiri ya walio karibu yenu katika makafiri kuwa ni walio karibu zaidi, isipokuwa kama kuna mapatano. Hii ni dalili kuwa ni wajibu kwa watu walio katika hali ya hatari kujilinda wakihofia kuchafuliwa Uislamu au mji wa Waislamu, hata kama hayuko Imam mwadilifu”.
Tumezungumizia kwa ufafanuzi kuhusu kupigana na makafiri katika Juz: (2:193) Kwa anuani ya ‘Uislamu unapiga vita dhulma na ufisadi’.
IMAM ZAINULABIDIN NA MSINGI WA VITA
Na wakute kwenu ugumu.
Ugumu hapa ni fumbo la nguvu na kuilinda vizuri mipaka.
Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wenye takua.
Ambao wameamini imani ya kweli; wakafanya ikhlasi katika kupigana na adui yao na adui wa Mwenyezi Mungu; wakajiandaa kwa nguvu zao zote, kama alivyo waamrisha Mwenyezi Mungu.
Maelezo ya kupendeza kuhusu maudhui haya ni dua ya Imam Zainul Abidin, Ali Bin Hussein
, akimlingania Mola wake na kuwaombea watu walio katika hatari ya kushambuliwa na walinzi wa miji ya Kiislamu. Alisema katika aliyoyasema:
“Ewe Mola Wangu! Mrehemu Muhammad na Ali wa Muhammad. Na uifanye nyingi idadi yao, uzinoe silaha zao, uzilinde nchi zao, uzuie kushambuliwa kwao, ushikamanishe mjumuiko wao, uyaaangalie vizuri mambo yao, uwatoshelezee mahitaji yao, uwasaidie kwa kuwapa subra (uvumilivu), uwahurumie kwa kuwakinga na hadaa, uwafahamishe wasiyoyajua, uwaelimishe wasiyokuwa na ujuzi nayo.
Wanapokutana na adui wasahaulishe kukumbuka dunia yao iliyo na hadaa na ghururi, ufute katika nyoyo zao mawazo ya mali yenye fitna na uijalie pepo machoni mwao.”
Hiyo ndiyo misingi ya ushindi wa kuweza kulizuwiya jeshi lolote kadiri litakavyokuwa na silaha za kisasa; hata tonoradi, mizinga, mapesa ya kuwalipa wapiganaji, elimu ya vita na kutumia silaha pamoja na mbinu zote za kupigana.
Silaha kubwa zaidi ni kuunganisha majeshi na kuzifanya nyoyo ziwe na ikhlasi ya kupigana na kuwa na uvumilivu hadi kufa, kuisahau dunia na kuamini kuwa mtu kufa shahidi, katika kupigania dini yake na nchi yake ndio faida na kufuzu kukubwa.
Je, si Waarabu na Waislamu, wa zamani na wasasa, wamekuwa ni chakula kwa sababu tu ya mali yenye fitina? Dalili ya hayo ni janga la tarehe 5 June,1967.
Maneno haya ya Imam Zainul Abidin yamepitiwa na zaidi ya karne 13, lakini pamoja na hayo lau, hivi sasa, kamanda mkuu angetaka kusoma sababu za ushindi, basi hatahitajia ila kufafanua matamko haya mafupi aliyoyatamka Imam.
وَإِذَا مَا أُنزِلَتْ سُورَةٌ فَمِنْهُم مَّن يَقُولُ أَيُّكُمْ زَادَتْهُ هَـٰذِهِ إِيمَانًا فَأَمَّا الَّذِينَ آمَنُوا فَزَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَهُمْ يَسْتَبْشِرُونَ ﴿١٢٤﴾
124. Na inapoteremshwa Sura yoyote, basi miongoni mwao kuna wanaosema: Ni nani miongoni mwenu Sura hii imemzidishia imani? Basi wale walioamini inawazidishia imani, nao wanafurahi.
وَأَمَّا الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ فَزَادَتْهُمْ رِجْسًا إِلَىٰ رِجْسِهِمْ وَمَاتُوا وَهُمْ كَافِرُونَ ﴿١٢٥﴾
125. Ama wale wenye maradhi katika nyoyo zao, basi inawazidshia uovu juu ya uovu wao, Na wanakufa hali ni makafiri.
أَوَلَا يَرَوْنَ أَنَّهُمْ يُفْتَنُونَ فِي كُلِّ عَامٍ مَّرَّةً أَوْ مَرَّتَيْنِ ثُمَّ لَا يَتُوبُونَ وَلَا هُمْ يَذَّكَّرُونَ ﴿١٢٦﴾
126. Je, hawaoni kwamba wao wanajaribiwa kila mwaka mara moja au mara mbili? Kisha hawatubu wala hawakumbuki.
وَإِذَا مَا أُنزِلَتْ سُورَةٌ نَّظَرَ بَعْضُهُمْ إِلَىٰ بَعْضٍ هَلْ يَرَاكُم مِّنْ أَحَدٍ ثُمَّ انصَرَفُوا صَرَفَ اللَّـهُ قُلُوبَهُم بِأَنَّهُمْ قَوْمٌ لَّا يَفْقَهُونَ ﴿١٢٧﴾
127. Na inapoteremshwa Sura wanatazamana: Je, kuna yeyote anyewaona? Kisha hugeuka, Mwenyezi Mungu amezigeuza nyoyo zao kwa kuwa wao ni watu wasiofahamu.
INAPOTEREMSHWA SURA
Aya 124 – 127
MAANA
Na inapoteremshwa Sura yoyote, basi miongoni mwao kuna wanaosema: Ninani miongoni mwenu Sura hii imemzidishia imani?
Yaani baadhi ya wanafiki walikuwa wakidharau Qur’ani na kuulizana kuwa kuna ajabu gani ya hii?
Kwa hiyo wanazifanya nafsi zao, zilizochafuliwa na tamaa na dhambi, kuwa ni kipimo cha haki na ukweli.
La kushangaza ni kuwa washirikina walikuwa wakiukubali ukuu wa Qur’ani na athari zake zinazoingia nyoyoni, wakuwa wanausiana kuwa wasisikilize, kwa kuhofia kuvutwa kwenye Uislamu bila ya kujitambua. Mwenyezi Mungu anasema:
وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لَا تَسْمَعُوا لِهَـٰذَا الْقُرْآنِ وَالْغَوْا فِيهِ لَعَلَّكُمْ تَغْلِبُونَ ﴿٢٦﴾
“Na Walisema waliokufuru: Msisikilize Qur’ani hii na fanyeni zogo, huenda mkashinda” (41:26)
Hii inafahamisha, moja kwa moja, kuwa wanafiki wana athari mbaya zaidi kuliko washirikina.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewajibu wanafiki kwa kuwaaambia:
Basi wale walioamini inawazidishia imani.
Yaani, ikiwa katika nafsi zenu enyi wanafiki, haina athari yoyote nzuri, baada ya kupigwa chapa ya matamanio, basi waumini inawazidishia uongofu na yakini. Kwa sababu nafsi zao ni safi hazina taka ya uchafu kama nafsi zenu.
Nao wanafurahi
kila inapoteremshwa Sura au Aya katika Qur’ani, kwa sababu inawapa bishara ya Pepo na kuwaongoza kwenye njia iliyo sawa.
Ama wale wenye maradhi katika nyoyo zao, basi inawazidshia uovu juu ya uovu wao.
Kila mwenye kuwa mbali na haki na hali halisi, na imani yake na rai yake ikavutwa kwenye dhati yake na mawazo yake, basi yeye ni mgonjwa wa moyo na akili. Na anapotakiwa kuwa kwenye hukumu halisi na akakataa huzidi maradhi yake.
Unafiki ni maradhi kwa sababu ni upotevu. Wanafiki wa sasa jinsi wanavyopupia dunia ni kama mfano wa funza; kila anavyozidi kujikunja ndio anakuwa mbali zaidi na kutoka mpaka anakufa.
Na wanakufa hali ni makafiri
kwa uchaguzi wao mbaya; kama anavyok- ufa funza kwa sababu yake mwenyewe.
Je, hawaoni kwamba wao wanajaribiwa kila mwaka mara moja au mara mbili?
Makusudio ya kujaribiwa hapa ni kufedheheshwa na kufichuka njama zao kwa wote. Aya hii inaambatana na Aya iliyo tangulia: “Na inapoteremshwa Sura …”
Njia ya kuungana ni kuwa wanafiki walikuwa wakimlia njama Mtume(s.a.w.w)
na wakimshutumu; kama vile kusema kuwa ni sikio, lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t) alikuwa akimfahamisha Mtume wake njama zao, na Mtume akiwafedhei. Mara nyingine hilo hukaririka zaidi ya mara moja katika mwaka.
Katika hilo kuna dalili mkataa juu ya ukweli wa Mtume na kwamba Qur’ani inatoka mbele ya Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo ilikuwa ni wajibu kwao wapate mawaidha na wamwamini badala ya kudharau na kucheza chere kwa kusema: Ni nani miongoni mwenu amezidishiwa imani hii na hii?
Kisha hawatubu wala hawakumbuki.
Na hawakumbuki ila wenye akili; na hawa wamepofushwa akili zao na nyoyo zao kwa matamanio.
Na inapoteremshwa Sura hutazamana.
Ndivyo walivyo wanafiki kila wakati na kila mahali – wanaposhindwa kuikabili haki kwa hoja basi wanakonyezana, kuonyesha kuzama kwao kwenye ukafiri na upotevu.
Je kuna yeyote anayewaona.
Yaani wanayasema haya kwa mdomo au kwa vitendo:
يَسْتَخْفُونَ مِنَ النَّاسِ وَلَا يَسْتَخْفُونَ مِنَ اللَّـهِ وَهُوَ مَعَهُمْ إِذْ يُبَيِّتُونَ مَا لَا يَرْضَىٰ مِنَ الْقَوْلِ ﴿١٠٨﴾
“Wanajificha kwa watu wala hawajifichi kwa Mwenyezi Mungu, na yeye yu pamoja nao walipokula njama usiku kwa maneno asiyoyapenda” Juz.5 (4:108)
Kisha hugeuka.
Yaani wanafanya wanayoyafanya kisha hugeukia kwenye shughuli zao; kama vile hawakufanya kitu.
Mwenyezi Mungu amezigeuza nyoyo zao kwa kuwa wao ni watu wasiofahamu.
Mwenyezi Mungu amezigeuza nyoyo zao na haki baada ya kuwasimamishia hoja na ubainifu, na baada ya kuwafanyia inadi na kukataa kusalimu amri. Kwa hiyo wao ndio sababu ya moja kwa moja ya kugeuka na ikategemzwa kwa Mwenyezi Mungu kupita kwao.
Ni desturi ya Qur’ani Tukufu kutegemeza mambo mengi ya waja kwa Mwenyezi Mungu, kwa kuangalia kuwa yeye ni muumbaji wao na mwenye kuutengeneze ulimwengu na vitu vyake.
لَقَدْ جَاءَكُمْ رَسُولٌ مِّنْ أَنفُسِكُمْ عَزِيزٌ عَلَيْهِ مَا عَنِتُّمْ حَرِيصٌ عَلَيْكُم بِالْمُؤْمِنِينَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ ﴿١٢٨﴾
128. Hakika amewajia Mtume kutokanana nyinyi wenyewe, Yanamhuzunisha yanayo-wataabisha, anawahangaikieni sana, kwa waumini nimpole, mwenye huruma.
فَإِن تَوَلَّوْا فَقُلْ حَسْبِيَ اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ وَهُوَ رَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ ﴿١٢٩﴾
129. Basi wakikengeuka, sema: Anitoshelezeaye ni Mwenyezi Mungu, hakuna Mola (apasaye kuabudiwa) ila yeye tu; kwake ninategemea; naye ndio bwana wa Arshi.
KWA WAUMINI NI MPOLE
Aya 128 – 129
MAANA
Hakika amewajia Mtume kutokana na nyinyi wenyewe.
Msemo huu anaambiwa kila mwanadamu anayetafuta uhakika na kutaka kuongozwa kwake. Mtume ni Muhammad bin Abudullah(s.a.w.w)
, aliyetumwa na Mwenyezi Mungu kwa watu wote kuwaokoa na ujinga na upotevu na kuwaongoza kwenye njia ya haki na heri.
Analotakiwa kufanya mwenye kutaka njia ya heri na haki ni kuangalia kwa ufahamu tu sera ya Muhammad(s.a.w.w)
na desturi yake na Kitabu alichokuja nacho kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Walimwamini mamilioni tangu zamani na sasa, wakiwemo maulama na wanafalsafa walioacha dini ya mababa na mababu, wakakubali Uislamu baada ya kutulia akili zao na nyoyo zao na kumuona Mtume wake mtukufu, kama alivyomsifu Mwenyezi Mungu kwa kauli yake:
Yanamhuzunisha yanayowataabisha, anawahangaikieni sana, kwa Waumini ni mpole, mwenye huruma.
Anahuzunika kwa kila baya linalomfika yeyote aliye ardhini; hata kama ni mnyama; mwenye kuhangaikia uwongofu na wema wa watu wote. Ama upole wake na rehema yake imewaenea watu wote:
وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِّلْعَالَمِينَ ﴿١٠٧﴾
“Nasi hatukukutuma ila uwe rehema kwa walimwengu wote” (21:107)
Na miongoni mwa Hadith zake ni: “Mimi ni rehema niliyetolewa zawadi”
“Wenye huruma huwarehemu Mwenyezi Mungu.” “Wahurumieni walio katika ardhi watawahurumia walio katika mbingu”.
Utauliza
: Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema kwa Waumini ni Mpole mwenye huruma. Na katika Aya nyingine anasema: Nasi hatukukutuma ila uwe rehema kwa walimwengu wote; yaani waumini na wasiokuwa waumini, Sasa zinaungana vipi Aya mbili?
Jibu
: Makusudio ya kauli yake “Nasi hatukutuma ila uwe rehema kwa walimwengu wote,” ni kuwa dini ya Muhammad ni dini ya ubinadamu na sharia yake ni rehema kwa watu wote. Lau kama watu wangelifuata na wakaitumia ardhi ingelijaa heri na uadilifu.
Ama kauli yake Mwenyezi Mungu: “Kwa waumini ni Mpole,” maana yake ni kwamba yeye ni Mpole sana na mwenye huruma kwa anayeamini haki na akajizuia kuwaudhi watu.
Ama anayewafanyia uadui na kuichezea haki yeye anamchukulia ugumu wala hamfanyii upole.
Hii nidyo dini ya utu na rehema. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amekataza upole katika kutekeleza hadi (adhabu) kwa wakosaji. Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema:
الزَّانِيَةُ وَالزَّانِي فَاجْلِدُوا كُلَّ وَاحِدٍ مِّنْهُمَا مِائَةَ جَلْدَةٍ وَلَا تَأْخُذْكُم بِهِمَا رَأْفَةٌ فِي دِينِ اللَّـهِ ﴿٢﴾
“Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mpigeni, kila mmoja katika wao, mijeledi mia wala isiwashike huruma kwa ajili yao katika hukumu ya Mwenyezi Mungu” (24:2)
Anasema Ibin Al-Arabi katika Kitabu Futahahtuli-Makkiyya J2 “Makusudio ya waumini ni wenye kuamini haki na batili, sio wenye kuamini haki tu.” Lakini haya ni katika mambo ya kisufi.
Basi wakikengeuka, sema: Anitoshelezeaye ni Mwenyezi Mungu, hakuna Mola (apasaye kuabudiwa) ila yeye tu; kwake ninategemea; naye ndio bwana wa Arshi tukufu.
Hio ndiyo kazi ya Mtume – kufikisha tu. Mwenye kuongoka ni faida yake na mwenye kupotea ni hasara yake mwenyewe.
Mtume(s.a.w.w)
alikuwa na yakini kabisa kwamba Mwenyezi Mungu anamtosha, na ndiye anayempa nguvu za ushindi wake, kwa sababu anamtegemea yeye peke yake.
Tutamalizia Sura hii kwa alivyomalizia Mwenye Tafsir Al-Manar, aliposema:
“Ama uteuzi wake Mwenyezi Mungu mtukufu kwa Bani Hashim, ni kwa kuwa walikuwa wanatofautiana na Maquraishi wote kwa fadhila na ukarimu. Hashim ndiye aliyekuwa mwenye msafara wa Maquraish ambao aliuchukulia ahadi kuuwahami kutoka kwa Kizair wa Roma katika msafara wa kaskazi; na kutoka serikali ya Yemen katika msafara wa kusi.
Yeye ndiye wa mwanzo kuwalisha mafukara na mahujaji wote mkate na mchuzi, Na alimpa malezi ya ukarimu mtoto wake, Abdul-Muttwalib. Kwa ujumla ni kuwa Bani Hashim walikuwa ni wenye tabia njema kuliko Maquraish wote, walikuwa hawana kiburi wala ubinafsi.
Baadhi ya mapokezi yanasema kuwa Aya ya mwisho kushuka ni hii: “Anitoshelezeaye ni Mwenyezi Mungu, hakuna Mola (apasaye kuabudiwa) ila yeye tu; kwake ninategemea; naye ndio bwana wa Arshi tukufu”
MWISHO WA SURA YA TISA: SUART AT – TAWBA