TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MOJA Juzuu 11

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MOJA0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MOJA Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MOJA

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 10613
Pakua: 2532

Maelezo zaidi:

Juzuu 11
Juzuu 1
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 15 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 10613 / Pakua: 2532
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MOJA

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MOJA Juzuu 11

Mwandishi:
Swahili

9

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MOJA

وَيَوْمَ يَحْشُرُهُمْ كَأَن لَّمْ يَلْبَثُوا إِلَّا سَاعَةً مِّنَ النَّهَارِ يَتَعَارَفُونَ بَيْنَهُمْ قَدْ خَسِرَ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِلِقَاءِ اللَّـهِ وَمَا كَانُوا مُهْتَدِينَ ﴿٤٥﴾

45. Na siku atakapowakusanya itakuwa kama kwamba wao hawakukaa isipokuwa saa moja tu ya mchana, Watatambuana. Hakika wamehasirika waliokanusha kukutana na Mwenyezi Mungu, wala hawakuwa wenye kuongoka.

وَإِمَّا نُرِيَنَّكَ بَعْضَ الَّذِي نَعِدُهُمْ أَوْ نَتَوَفَّيَنَّكَ فَإِلَيْنَا مَرْجِعُهُمْ ثُمَّ اللَّـهُ شَهِيدٌ عَلَىٰ مَا يَفْعَلُونَ ﴿٤٦﴾

46. Na vyovyote vile, tukikuonyesha baadhi ya tunayowaahidi au tukakufisha, basi marejeo yao ni kwetu. Kisha Mwenyezi Mungu ni shahidi wa wanayoyafanya.

وَلِكُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولٌ فَإِذَا جَاءَ رَسُولُهُمْ قُضِيَ بَيْنَهُم بِالْقِسْطِ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ ﴿٤٧﴾

47. Na kila Umma una Mtume Basi anapokuja Mtume wao inahukumiwa baina yao kwa uadilifu; nao hawatadhulumiwa.

SIKU ATAKAYOWAKUSANYA

Aya 45 – 47

MAANA

Na siku atakapowakusanya itakuwa kama kwamba wao hawakukaa isipokuwa saa moja tu ya mchana.

Kusema saa moja tu ya mchana ni fumbo la kuwa maisha ya dunia hata yakiwa marefu kiasi gani bado ni mafupi tu, kwa sababu yanaisha.

Maneno ya watu kuhusu kuikashifu dunia kimashairi na kinathari yamejaza kurasa za vitabu. Lakini jambo la kushangaza ni kuwa wanachanganya kuikashifu na kuisifu. Bali watu lau watarudishwa duniani baada ya kufa, wangelirudia yale yale waliyokatazwa. Hii inafahamisha kwamba watu hawatambuliki kwa maneno.

Watatambuana .

Dhahiri ya tamko inajulisha kuwa wenye makosa watatambuana siku ya mkusanyiko; vile vile watu wema.

Unaweza kuuliza : Hii haipingani na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

يَوْمَ تَرَوْنَهَا تَذْهَلُ كُلُّ مُرْضِعَةٍ عَمَّا أَرْضَعَتْ ﴿٢﴾

“Siku mtakapoiona kila mwenye kunyonyesha atamsahau amnyonyeshaye” (22:2)

Jibu : Kuna tofauti kati ya ufufuo na kukusanywa na vile vile siku ya Kiyama ambayo ni siku ya kuharibiwa ulimwengu. Na Aya ya (22:2) inazungumzia siku ya Kiyama, Na kauli yake Mwenyezi Mungu: “Watatambuana” inazungumzia siku ya kukusanywa. Zaidi ya hayo ni kwamba vituo vya mkusanyiko vitakuwa vingi. Watu wataweza kutambua na hasa siku ya hisabu na vingine hawatatambuana; kama vile wakipelekwa motoni.

Hakika wamehasirika waliokanusha kukutana na Mwenyezi Mungu, wala hawakuwa wenye kuongoka.

Kila mwenye kufanya kwa ajili ya jambo ambalo haliko, au akapuuza na asifanye kwa ajili ya jambo liliopo ambalo linaambatana naye na mwelekeo wake, basi atakuwa ni katika wenye kupotea wenye kuhasirika. Na hivyo ndivyo ilivyo kwa yule anayefanya amali kwa ajili ya dunia bila ya akhera, ni sawa awe mkweli au mwogo.

Na vyovyote vile, tukikuonyesha baadhi ya tunayowaahidi au tukakukufisha, basi marejeo yao ni kwetu.

Maneno yanaelekezwa kwa Mtume(s.a.w.w ) . Maana nikuwa Mwenyezi Mungu anawashtua na kuwaahidi wale wanaowakadhibisha kuhusu hizaya hiyo kuwa hapana budi itawapata tu, iwe ni katika uhai wa Mtume au baada ya kufa kwake. Kwa vyovyote vile, marejeo yao ni kwa Mwenyezi Mungu na atawaadhibu adhabu kubwa.

Kisha Mwenyezi Mungu ni shahidi wa wanayoyafanya.

Yaani anayajua yote wayafanyao, hakifichiki kitu chochote kwake; na kisha atawalipa yale wanayostahiki.

Na kila Umma una Mtume anayewapa bishara na kuwaonya. Na baada ya maonyo itakuwa hisabu na adhabu, Kwani hakuna adhabu bila ya onyo.

Basi anapokuja Mtume wao na akawaeleza yale yaliyowajibu kuyajua katika dini; na kusibakie udhuru wa mwenye kutafatu udhuru,inahukumiwa baina yao kwa uadilifu. Yule aliyetikia mwito wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, atahukumiwa kufuzu na kupata Pepo. Na yule anayeukataa atahukumiwa adhabu

Nao hawatadhulumiwa.

Hakuna upungufu wa thawabu za mtiifu, bali huenda akazidishiwa. Wala hakuna kuzidishiwa aliyeasi, bali huenda ikamfikia rehema.

Hayo ndiyo maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu ‘kwa Uadilifu’ Ni desturi ya Qur’ani kusisitiza kila linaloambatana na akhera na malipo yake ya thawabu na adhabu.

وَيَقُولُونَ مَتَىٰ هَـٰذَا الْوَعْدُ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٤٨﴾

48. Na wanasema: Ni lini ahadi hii, ikiwa mnasema kweli?

قُل لَّا أَمْلِكُ لِنَفْسِي ضَرًّا وَلَا نَفْعًا إِلَّا مَا شَاءَ اللَّـهُ لِكُلِّ أُمَّةٍ أَجَلٌ إِذَا جَاءَ أَجَلُهُمْ فَلَا يَسْتَأْخِرُونَ سَاعَةً وَلَا يَسْتَقْدِمُونَ ﴿٤٩﴾

49. Sema: Similikii nafsi yangu dhara wala nafuu, isipokuwa apendavyo Mwenyezi Mungu, Kila umma una muda, Unapofikia muda wao hawakawii saa moja wala hawatangulii.

قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِنْ أَتَاكُمْ عَذَابُهُ بَيَاتًا أَوْ نَهَارًا مَّاذَا يَسْتَعْجِلُ مِنْهُ الْمُجْرِمُونَ ﴿٥٠﴾

50. Sema: Mwaonaje ikiwafikia adhabu yake usiku au mchana, Sehemu gani ya adhabu wanaihimiza wenye makosa?

أَثُمَّ إِذَا مَا وَقَعَ آمَنتُم بِهِ آلْآنَ وَقَدْ كُنتُم بِهِ تَسْتَعْجِلُونَ ﴿٥١﴾

51. Tena, Je, ikishatokea Mtaiamini? Sasa tena? Na hali mlikuwa mkiihimiza?

ثُمَّ قِيلَ لِلَّذِينَ ظَلَمُوا ذُوقُوا عَذَابَ الْخُلْدِ هَلْ تُجْزَوْنَ إِلَّا بِمَا كُنتُمْ تَكْسِبُونَ ﴿٥٢﴾

52. Kisha waliodhulumu watambiwa: onjeni adhabu ya kudumu. Kwani hamtalipwa isipokuwa yale mliyokuwa mkiyachuma?

وَيَسْتَنبِئُونَكَ أَحَقٌّ هُوَ قُلْ إِي وَرَبِّي إِنَّهُ لَحَقٌّ وَمَا أَنتُم بِمُعْجِزِينَ ﴿٥٣﴾

53. Na wanakuuliza: Je, ni kweli hayo? Sema: Ehe! Naapa kwa Mola wangu hiyo ni kweli nanyi hamuwezi kushinda.

وَلَوْ أَنَّ لِكُلِّ نَفْسٍ ظَلَمَتْ مَا فِي الْأَرْضِ لَافْتَدَتْ بِهِ وَأَسَرُّوا النَّدَامَةَ لَمَّا رَأَوُا الْعَذَابَ وَقُضِيَ بَيْنَهُم بِالْقِسْطِ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ ﴿٥٤﴾

54. Na lau kama kila nafsi iliyod hulumu inamiliki kila kilichomo ardhini, ingelitoa vyote kujikombolea. Na watakapoiona adhabu wataficha majuto Na patahukumiwa baina yao kwa uadilifu; nao hawatadhulumiwa.

أَلَا إِنَّ لِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ أَلَا إِنَّ وَعْدَ اللَّـهِ حَقٌّ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٥٥﴾

55. Jueni kuwa hakika vyote vilivyomo katika mbingu na ardhi ni vya Mwenyezi Mungu. Jueni kuwa hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni haki Lakini wengi wao hawajui.

هُوَ يُحْيِي وَيُمِيتُ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴿٥٦﴾

56. Yeye ndiye anayefufua na anayefisha na kwake mtarudishwa.

NI LINI AHAD HII?

Aya 48 – 56

MAANA

Na wanasema: Ni lini ahadi hii, ikiwa mnasema kweli?

Katika Aya 45, Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewatishia wale wanaokad- hibisha kuwa watakutana naye, kwamba yeye atawafufua baada ya kufa na awaadhibu kutokana na kukadhibisha kwao. Katika Aya hii 48, Mwenyezi Mungu Mtukufu anaishiria kwamba wao wanajibu vitisho hivyo kwa dharau wakisema kuwa yatakuwa lini hayo?

Sema: Similikii nafsi yangu dhara wala nafuu, isipokuwa apendavyo Mwenyezi Mungu.

Yaani nyinyi mnaniuliza jambo ambalo sina uwezo nalo, bali sina uwezo hata wa nafsi yangu sembuse hayo mengine! Mfano wa Aya hii umetangulia katika Juz.9 (7:188).

Kila umma una muda, Unapofikia muda wao hawakawii saa moja wala hawatangulii.

Tumeeleza kwa ufafanuzi, kuhusu mfano wa Aya hiyo katika Juz.4 (3:145).

Sema: Mwaonaje ikiwafikia adhabu yake usiku au mchana, Sehemu gani ya adhabu wanaihimiza wenye makosa?

Washirikina walikadhibisha adhabu ya Akhera, kisha wakaihimiza kwa dharau; ndipo Mwenyezi Mungu akamwamrisha Mtume wake kuwaambia kuwa Hebu niambieni mtafanya nini ikiwashukia adhabu mkiwa mko macho au mmelala, tena ni adhabu gani hiyo mnayoihimiza enyi wapumbavu? Je, mnangoja adhabu ya dunia au adhabu ya akhera? Vyovyote iwavyo, je, mnaweza kuikinga? Kuna yeyote miongoni mwenu awezaye kumkimbia Mwenyezi Mungu?

Tena, Je, ikishatokea Mtaiamini?

Tumewashuhudia watu wengi wapumbavu wakijaribu kuikabili hatari au wakiacha mambo ambayo yana manufaa kwao. Wanapopewa nasaha na wenye akili na kuwahadharisha na mwisho mbaya, wao wanaziba masikio yao na kuwa na inadi ya kufanya uovu au kuacha kufanya heri wakidharau matokeo yake na yule anayewahadharisha. Inapofikia huanza kusema: ole wetu tulikuwa tukiambiwa sisi.

Hivyo ndivyo itakavyokuwa kwa wale wanaokadhibisha siku ya mwisho. Waliikadhibisha wakati ambao kuiamini kulifaa na wataiamini siku ambayo kuiamini hakuna manufaa yoyote, wamekwisha chelewa.

Sasa tena? Na hali mlikuwa mkiihimiza?

Je, mnaikubali na kuiamini hivi sasa ambapo hakuna manufaa yoyote ya kuiamini, wakati ambao mlitakiwa kuiamini, hamkufanya hivyo. Hakika kumwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho ni kumwamini ikiwa ghaibu, lakini kuamini kiaga chake na siku ya mwisho baada ya kuiona, sivyo inavyotakiwa.

Kisha waliodhulumu watambiwa: onjeni adhabu ya kudumu.

Kifungo cha maisha, katika dunia, kinaishia kwa mauti. Ama kifungo katika Jahannam hakina mwisho, kwa sababu hakuna kufa wala adhabu yake haipunguwi.

Kwani hamtalipwa isipokuwa yale mliyokuwa mkiyachuma?

Lau wangeliadhibiwa kwa yale wasiyoyachuma, Mwenyezi Mungu angelikuwa dhalimu, Ametakata ambaye ghadhabu zake hazimfanyi kuacha uadilifu wake.

WALLAHI WEWE MUHAMMAD NI MTUME

Na wanakuuliza, Je, ni kweli hayo? Ya adhabu tuliyoahidiwa?

Sema: Ehe! Naapa kwa Mola wangu hiyo ni kweli nanyi hamuwezi kushinda.

Qur’ani mara nyingi imetaja ishara na ubainifu juu ya utume wa Mohammad na ukweli wake wa kauli na vitendo. Miongoni mwa Aya hizo ni Juz, 1 (2:23), Juz. 3 (3:61), Juz,11(10:16) n.k.

Inajulikana kwamba Mtume alikuwa mkweli na mwaminifu kabla ya kutangazwa kuwa Mtume. Kwa hiyo mtu ambaye watu wamemjua kuwa ni mkweli na mwaminifu kwa muda wa miaka arobaini, basi ni juu yao kumwamini katika kauli zake zote mpaka uthibitike uongo wake.

Mwenye kumjua kwa sifa hizi anapaswa amwamini katika madai yake ya utume kwa kuchukulia kuwa Mohammad ni mwaminifu. Lakini tamaa manufaa na hawa za nafsi zinaingia kati ya mtu na akili yake na moyo wake.

Ama wale ambao wameepukana na matamanio ya nafsi na wakaitafuta haki kwa njia ya haki, basi waliamini kuanzia mwanzo. Miongoni mwao wako waliotosheka, kwa kusema tu: mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, bila ya kutaka ubainifu wala kiapo; kama vile Aliy bin Abu Talib. Wengine wakataka ubainifu na wengine wakatosheka kwa kuapa, kama vile Dhamam bin Tha’laba.

Wamesema wapokezi, akiwemo Imam ibn Hambal, Bukhari na Muslim: “Wakati Mtume alipokuwa msikitini, mara aliingia mtu, akaanza kusaili: Ninani Mohammad katika nyinyi? Akaelekezwa, wakaanza mahojiano. Yule mtu akanza kwa kusema: Mimi nitakuuliza maswali mengi kwa hiyo usinichoke.

Mtume: Uliza upendavyo.

Mtu: Ninakuuliza kwa jina la Mola wako na Mola wa aliyekuwa kabla yako, Je, Mwenyezi Mungu amekutuma kwa watu wote:

Mtume: Ndio, kwa jina la Mola wangu.

Mtu: Nakuuliza kwa jina la Mwenyezi Mungu: Je, amekuamrisha kuswali swala tano, katika usiku na mchana?

Mtume: Ndio, kwa jina la Mola wangu.

Mtu: Nakuuliza kwa jina la Mwenyezi Mungu: Je amekuamrisha kufunga mwezi mmoja katika mwaka?

Mtume: Ndio, kwa jina la Mola wangu.

Mtu: Nakuuliza kwa jina la Mwenyezi Mungu: Je, amekuamrisha kuchukua sadaka kutoka kwa matajiri na kuigawanya kwa mafukara. Mtume: Ndio, kwa jina la Mola wangu.

Mtu: Nimeamini uliyokuja nayo, nami nitakuwa mjumbe kwa watu wangu. Mimi ni Dhamam bin Tha’laba ndugu wa Bani Sa’d bin Bakr.

Yule mtu akatoka Msikitini na alikuwa na nywele zenye misokoti miwili, Mtume akasema yule mtu akisadikisha, ataingia peponi.

Alipofika kwa watu wake maneno yake ya kwanza yalikuwa: Lata na Uza hawana maana. Watu wakasema: We! Dhamam nyamaza, usije ukapatwa na mbalanga na ukoma! Akasema: ole wenu! Hao hawadhuru wala kunufaisha, Hakika Mwenyezi Mungu amewaletea Mtume na amemteremshia Kitabu kitakachowaokoa na haya mliyokuwa nayo.

Na mimi Ninushahadia kuwa hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu pekee hana mshirika; na ninashuhudia kuwa Muhammad ni mja wake na Mtume wake. Nimewaletea kutoka kwake yale mnayoamrishwa na mnayokatazwa.

Kama alivyosilimu yeye kirahisi, vilevile watu wake, waume kwa wake, walisilimu kirahisi.

Hivyo ndivyo alivyo kila ambaye matakwa yake na matamanio yake ni haki, anaiamini pale tu dalili yake inapomweka, kwa namna yoyote ile; sawa na apendaye kuwa kipofu. Ilikwishasemwa zamani: Hekima imempotea mumin, popote aipatapo huichukua. Makusudio ya mumin ni kila anayeiamini haki mara inapomdhihirikia bila ya taklifu yoyote wala mashaka.

Mwenyezi Mungu anasema:

وَالْبَلَدُ الطَّيِّبُ يَخْرُجُ نَبَاتُهُ بِإِذْنِ رَبِّهِ وَالَّذِي خَبُثَ لَا يَخْرُجُ إِلَّا نَكِدًا ﴿٥٨﴾

Na mji mzuri hutoa mimea yake kwa idhini ya Mola wake. Na ule ulio mbaya hautoi ila kwa taabu tu. Juz.8 (7:58)

Na lau kama kila nafsi iliyodhulumu inamiliki kila kilichomo ardhini ingelitoa vyote kujikombolea kutokana na adhabu na ukali wake, lakini hakuna fidia yoyote itakayofaa isipokuwa imani na amali njema. Mwenyezi Mungu anasema:

وَاتَّقُوا يَوْمًا لَّا تَجْزِي نَفْسٌ عَن نَّفْسٍ شَيْئًا وَلَا يُقْبَلُ مِنْهَا عَدْلٌ وَلَا تَنفَعُهَا شَفَاعَةٌ وَلَا هُمْ يُنصَرُونَ ﴿١٢٣﴾

“Na ogopeni siku ambayo nafsi haitafaa kitu nafsi nyingine, wala hakitakubaliwa kwake kikomboleo; wala maombezi (shufaa) hayatafaa, wala hawatanusuriwa” (2:123)

Na watakapoiona adhabu wataficha majuto lakini majuto, ya siri au dhahiri, hayafai kitu.

Na patahukumiwa baina yao kwa uadilifu; nao hawatadhulumiwa.

Aya hii, kama ilivyo, imetangulia katika Aya ya 47 ya Sura hii, Kule imetajwa kuwahadharisha wale wanaokadhibisha. Na hapa imerudiwa kuelezea kuwa hakuna faida ya fidia wala kikomboleo; hata kama ingeliwezekana kufanya hivyo.

Jueni kuwa hakika vyote vilivyomo katika mbingu na ardhi ni vya Mwenyezi Mungu. Anahukumu na kufanya atakavyo wala hapana mwenye kuzuia matakwa yake.

Jueni kuwa hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni haki katika kuweko siku ya mwisho, thawabu zake, adhabu zake na kila kilichoahidiwa.

Lakini wengi wao hawajui kwamba Kiyama kitakuja, hakina shaka na kwamba Mwenyezi Mungu, atawafufua walio katika makaburi, Wengi wenye imani hii ya ufufuo hawaifanyii kazi. Ikiwa, kwa ujumla, wengi hawajui na wale wachache wajuao hawayatumii wanayoyajua, basi itakuwa wajuzi wanaoufanyia kazi ujuzi wao ni nadra kuliko dhahabu nyekundu.

Yeye ndiye anayefufua na anayefisha na kwake mtarudishwa ili aadhibiwe aliyejua, na asiutumie ujuzi wake, adhabu kubwa na kali kuliko ya yule aliyezembea kutafuta ujuzi. Ni kweli kuwa mzembe anajukumu, laki- ni jukumu la anayejua na asiutumie ujuzi ni kubwa zaidi.

Kuhangaika kutafuta mali kwa ajili ya kulipa deni ni wajib na mwenye kuacha atapata dhambi. Lakini dhambi ya mwenye kuacha na hali anayo mali ya kulipa ni kubwa na kali sana.

يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءَتْكُم مَّوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَشِفَاءٌ لِّمَا فِي الصُّدُورِ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ ﴿٥٧﴾

57. Enyi watu! Hakika yamewafikia mawaidha kutoka kwa Mola wenu, na ponyo la yale yaliyomo vifuani mwenu na mwongozo na rehema kwa waumini.

قُلْ بِفَضْلِ اللَّـهِ وَبِرَحْمَتِهِ فَبِذَٰلِكَ فَلْيَفْرَحُوا هُوَ خَيْرٌ مِّمَّا يَجْمَعُونَ ﴿٥٨﴾

58. Sema: Kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema yake, basi nawafurahi. Hayo ni bora kuliko yale wanayoyakusanya.

قُلْ أَرَأَيْتُم مَّا أَنزَلَ اللَّـهُ لَكُم مِّن رِّزْقٍ فَجَعَلْتُم مِّنْهُ حَرَامًا وَحَلَالًا قُلْ آللَّـهُ أَذِنَ لَكُمْ أَمْ عَلَى اللَّـهِ تَفْتَرُونَ ﴿٥٩﴾

59. Sema: Je, mwaonaje zile riziki alizowateremshia Mwenyezi Mungu, kisha mkafanya katika hizo nyingine haramu na nyingine halali? Sema: Je, Mwenyezi Mungu amewaruhusu au mnamzulia Mwenyezi Mungu uwongo?

وَمَا ظَنُّ الَّذِينَ يَفْتَرُونَ عَلَى اللَّـهِ الْكَذِبَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِنَّ اللَّـهَ لَذُو فَضْلٍ عَلَى النَّاسِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَشْكُرُونَ ﴿٦٠﴾

60. Nini dhana ya wale wanaomzulia uwongo Mwenyezi Mungu juu ya siku ya Kiyama? Hakika Mwenyezi Mungu ana fadhila juu ya watu Lakini wengi wao hawashukuru.

YAMEWAJIA MAWAIDHA

Aya 57 – 60

MAANA

Enyi watu! Hakika yamewafikia mawaidha kutoka kwa Mola wenu, na ponyo la yale yaliyomo vifuani mwenu na mwongozo na rehema kwa waumini.

Sifa hizi mawaidha, ponyo, mwongozo, na rehema ni sifa za Qur’ani Tukufu, na lengo la kuzitaja ni kuwajibu washirikina na kila mwenye kukitilia shaka Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kukikataa.

Njia ya majibu hayo ni kwamba Qur’ani inaonya watu kwa mawaidha mazuri, inaponya nyoyo kutokana na hawaa na uchafu, inaogoza watu kwenye lile lililo sawa nayo ni rehma inayomuokoa na mangamizi na adhabu, yule atakayeitumia. Kwa hivyo basi atakayeikataa, atakuwa amekataa misingi hii ambayo ndiyo mihimili ya haki na heri na njia ya uwokovu.

Sema: Kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema yake, basi nawafurahi. Hayo ni bora kuliko yale wanayoyakusanya.

Yaani mwenye akili hafurahi kwa mali na starehe za maisha haya ya dunia, isipokuwa anastarehe kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema yake. Wafasiri wamerefusha maneno sana kuhusu maana ya fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema yake na wakabainisha tofauti kati ya maneno mawili hayo.

Mfumo wa Aya unafahamisha kuwa makusudio yake hapa ni kuongoza kwenye njia ya heri na kuokoa; sawa na ilivyo fadhila na rehema katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na lau si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yako na rehema yake, lingedhamiria kundi katika wao kukupoteza” Juz.5 (4:113).

Kwa hiyo kauli yake ‘kukupoteza’ inafahamisha kuwa makusudio ya fadhila yake na rehema yake Mwenyezi Mungu Mtukufu ni uwongofu au kuthibitisha kwenye huo uwongofu, kwa sababu ndio kinyume cha upotevu. Mfano mwingine ni Aya isemayo: Kisha mligeuka baada ya haya,“Na lau kuwa si fadhila za Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema Zake, mngelikuwa miongoni mwa wenye kuhasirika.” Juz.1 (2:64)

Sema: Je, mwaonaje zile riziki alizowateremshia Mwenyezi Mungu, kisha mkafanya katika hizo nyingine haramu na nyingine halali?

Maana ya Aya hii yako karibu na maana ya Aya iliyo Juz.7 (5:103) ambayo Tafsiri yake imekwishaelezwa.

Maana yanayopatikana ni kwamba Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume wake kuwaambia washirikina wa Makka ambao walifanya katika wanyama Bahira na Saiba (ngamia aliyezaa mimba kumi na ngamia wa nadhiri), kuwa hebu niambieni.

Ni jambo gani liliwafanya kufanya halali na haramu katika zile riziki alizowapa Mwenyezi Mungu; mpaka mkagawa mafungu haya?

Swali hapo ni la kukanusha; yaani Mwenyezi Mungu hakujalia hivyo kabisa, bali hayo yanatokana na nyinyi wenyewe peke yenu ndio mmeharamisha mliyo yaharamisha.

Sema: Je, Mwenyezi Mungu amewaruhusu au mnamzulia Mwenyezi Mungu uwongo?

Haiwezekani kudai kuwa Mwenyezi Mungu amewaruhusu hivyo, kwa hiyo nyinyi mnamzulia tu.

Nini dhana ya wale wanaomzulia uwongo Mwenyezi Mungu juu ya siku ya Kiyama?

Yaani je, wanafikiria wale wanaojihalalishia na kujiharamishia kuwa Mwenyezi Mungu atawaacha kesho bila ya kuwaadhibu kutokana na uwongo na uzushi wao? Kama ni hivyo basi itakuwa hakuna tofauti kati ya mwenye kumcha Mwenyezi Mungu na mwenye kuasi.

Itakuwaje hivyo na hali Mwenyezi Mungu amesema: “Je, tuwafanye walioamini na kutenda mema kuwa sawa na wafisadi ardhini? Au tuwafanye wenye takua kuwa sawa na waovu?” (38:28). Kusuta huku ni katika ufasaha zaidi wa kushtua na kutoa kiaga.

Hakika Mwenyezi Mungu ana fadhila juu ya watu kwa yale aliyowaneemesha katika akili na sharia inayowaamrisha heri na kuwakataza shari.

Lakini wengi wao hawashukuru.

Yaani hawajui kwa kutumia akili wala kwa hukumu ya sharia.