10
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MOJA
وَمَا تَكُونُ فِي شَأْنٍ وَمَا تَتْلُو مِنْهُ مِن قُرْآنٍ وَلَا تَعْمَلُونَ مِنْ عَمَلٍ إِلَّا كُنَّا عَلَيْكُمْ شُهُودًا إِذْ تُفِيضُونَ فِيهِ وَمَا يَعْزُبُ عَن رَّبِّكَ مِن مِّثْقَالِ ذَرَّةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي السَّمَاءِ وَلَا أَصْغَرَ مِن ذَٰلِكَ وَلَا أَكْبَرَ إِلَّا فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ ﴿٦١﴾
61. Na huwi katika jambo lolote, wala husomi sehemu yoyote katika Qur’ani, wala hamtendi kitendo chochote ila sisi huwa ni mashahidi juu yenu mnaposhughulika nacho. Na hakifichikani kwa Mola wako chenye uzito hata wa chembe katika ardhi na katika mbingu wala kidogo kuliko hicho wala kikubwa ila kimokatika kitabu kinachobainisha.
أَلَا إِنَّ أَوْلِيَاءَ اللَّـهِ لَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ ﴿٦٢﴾
62. Juweni kuwa mawalii wa Mwenyezi Mungu hawana hofu wala wao hawahuzuniki.
الَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ ﴿٦٣﴾
(Hao) ni ambao wameamini na wakawa na takua.
لَهُمُ الْبُشْرَىٰ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ لَا تَبْدِيلَ لِكَلِمَاتِ اللَّـهِ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ ﴿٦٤﴾
64. Wao wana bishara katika maisha ya dunia na katika Akhera. Hakuna mabadiliko katika maneno ya Mwenyezi Mungu, Huko ndiko kufuzu kukubwa.
HUWI KATIKA JAMBO LOLOTE
Aya 61 – 64
MAANA
Na huwi katika jambo lolote, wala husomi sehemu yoyote katika Qur’ani, wala hamtendi kitendo chochote ila sisi huwa ni mashahidi juu yenu mnaposhughulika nacho.
Msemo katika huwi unaelekezwa kwa Mtume Muhammad(s.a.w.
w
)
na katika hamtendi unaelekezwa kwa Mtume na uma wake. Maana kwa ujumla ni kuwa hakuna hali yoyote anayokuwa nayo Mtume na uma wake isipokuwa Mwenyezi Mungu anajua.
Na hakifichikani kwa Mola wako chenye uzito hata wa chembe katika ardhi na katika mbingu wala kidogo kuliko hicho wala kikubwa ila kimo katika Kitabu kinachobainisha.
Kitab kinachobainisha ni Lawhin Mahfudh. Kwa ufupi Aya inaeleza kuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye wasaa, Mjuzi, wa kila kitu. Na makusudio ya kujua kwake hapa ni malipo kwenye kauli za watu na vitendo vyao vya heri au vya shari, vikubwa au vidogo.
Juweni kuwa mawalii wa Mwenyezi Mungu hawana hofu wala wao hawahuzuniki.
Imam Ali
anasema katika wasifu wake kwa vipenzi (mawalii) wa Mwenyezi Mungu:“Hao ni wale ambao wameiangalia dunia kwa undani wakati watu wameiangalia kwa nje. Wamejishughulisha na wakati ujao wakati watu wamejishughulisha na wakati wa sasa. Wakaua yale wanayohofia kuwauwa – yaani hawa-na wakaacha katika dunia yale ambayo wanajua kuwa yatawaacha.”
Amesema tena: “Hakika bora wa watu kwa Mitume ni yale anayejua zaidi yale waliyokuja nayo; na kwamba mpenzi wa Muhammad ni yule anayemtii Mwenyezi Mungu, hata kama mwili wake utakuwa mbali naye na adui wa Muhammad ni yule mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu hata kama atakuwa karibu naye kiudugu.”
Maana ya yote hayo ni kuwa kuamini bila ya kumcha Mwenyezi Mungu na vitendo hakuna manufaa yoyote. Ndio Mwenyezi Mungu akaashiria kwa kusema:
Hao ni ambao wameamini na wakawa na takua.
Tumeyafafanua zaidi hayo katika Juz, 2 (2:212) na Juz.4 (3:200)
Wao wana bishara katika maisha ya dunia na katika Akhera.
Wao ni wacha Mungu, na bishara yao katika dunia inatoka kwa Mwenyezi Mungu na Mtume kwamba wao wako katika haki ya itikadi yao na matendo yao. Hapana mwenye shaka kwamba nafsi inatulia na kuona raha, ikiwa ina imani na dini yake na matendo yake.
Ama bishara ya wanaomcha Mwenyezi Mungu katika Akhera ni furaha yao kwa neema za Mwenyezi Mungu na fadhila zake.
يَسْتَبْشِرُونَ بِنِعْمَةٍ مِّنَ اللَّـهِ وَفَضْلٍ وَأَنَّ اللَّـهَ لَا يُضِيعُ أَجْرَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿١٧١﴾
“Wanashangilia neema na fadhila za Mwenyezi Mungu na kwamba Mwenyezi Mungu hapotezi ujira wa waumini” (3:171)
Hakuna mabadiliko katika maneno ya Mwenyezi Mungu,
kwa sababu Mwenyezi Mungu havunji ahadi yake, na anapotaka kitu hakuna wa kupinga matakwa yake.
وَإِن يَمْسَسْكَ اللَّـهُ بِضُرٍّ فَلَا كَاشِفَ لَهُ إِلَّا هُوَ وَإِن يُرِدْكَ بِخَيْرٍ فَلَا رَادَّ لِفَضْلِهِ ﴿١٠٧﴾
“Na kama Mwenyezi Mungu akikugusisha dhara hakuna wa kuiondoa isipokuwa yeye tu na kama akikutakia heri, basi hakuna mwenye kuirudisha fadhila zake.” (10:107)
Huko ndiko kufuzu kukubwa,
ambako hakuna kufuzu kwengine zaidi yake, Kila kufuzu kunakotokana na natija ya kuamini haki na jihadi katika njia yake, basi huko ni kufuzu kukubwa.
وَلَا يَحْزُنكَ قَوْلُهُمْ إِنَّ الْعِزَّةَ لِلَّـهِ جَمِيعًا هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴿٦٥﴾
65. Wala isikuhuzunishe kauli yao. Hakika enzi yote ni ya Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye
mwenye kusikia, Mjuzi,
أَلَا إِنَّ لِلَّـهِ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَمَن فِي الْأَرْضِ وَمَا يَتَّبِعُ الَّذِينَ يَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ شُرَكَاءَ إِن يَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ وَإِنْ هُمْ إِلَّا يَخْرُصُونَ ﴿٦٦﴾
66. Juweni kuwa ni wa Mwenyezi Mungu wote waliomo mbinguni na waliomo ardhini. Na wale wanaoomba asiyekuwa Mwenyezi Mungu hawawafuati kuwa ni washirika, hawafuati ila dhana tu, na hawasemi ila uwongo tu.
هُوَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ اللَّيْلَ لِتَسْكُنُوا فِيهِ وَالنَّهَارَ مُبْصِرًا إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَسْمَعُونَ ﴿٦٧﴾
67. Yeye ndiye aliyewafanyia usiku ili mtulie humo na mchana wa kuonea. Hakika katika haya kuna ishara kwa watu wanaosikia.
قَالُوا اتَّخَذَ اللَّـهُ وَلَدًا سُبْحَانَهُ هُوَ الْغَنِيُّ لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ إِنْ عِندَكُم مِّن سُلْطَانٍ بِهَـٰذَا أَتَقُولُونَ عَلَى اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ ﴿٦٨﴾
68. Wanasema: Mwenyezi Mungu amejifanyia mtoto! Ametakata na hayo! Yeye ni mkwasi. Ni vyake vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini. Nyinyi hamna dalili kwa haya, Je, mnasema juu ya Mwenyezi Mungu msiyoyajua?
قُلْ إِنَّ الَّذِينَ يَفْتَرُونَ عَلَى اللَّـهِ الْكَذِبَ لَا يُفْلِحُونَ ﴿٦٩﴾
69. Sema: Hakika wale ambao wanamzulia Mwenyezi Mungu uwongo hawatafaulu.
مَتَاعٌ فِي الدُّنْيَا ثُمَّ إِلَيْنَا مَرْجِعُهُمْ ثُمَّ نُذِيقُهُمُ الْعَذَابَ الشَّدِيدَ بِمَا كَانُوا يَكْفُرُونَ ﴿٧٠﴾
70. Ni starehe katika dunia. Kisha marejeo yao ni kwetu, tena tutawaonjesha adhabu kali, kwa sababu walikuwa wakikufuru Mungu.
ENZI YOTE NI YA MWENYEZI MUNGU
Aya 65 – 70
MAANA
Wala isikuhuzunishe kauli yao. Hakika enzi yote ni ya Mwenyezi Mungu.
Enzi hapa ina maana ya nguvu na ushindi.
Walipagawa wakubwa kutokana na mwito wa Mtume Muhammad(s.a.w.
w
)
kwenye uadilifu na usawa na kuharamisha dhulma na ukandamizaji. Walipagawa na mwito huu kwa sababu ulikuwa ukiingilia enzi yao na utajiri wao. Kwa hiyo wakajaribu kumzuia na kupambana naye.
Mwanzo wa mapambano yao ulikuwa ni uzushi na kueneza uvumi. Wakasema ni mwenda wazimu, lakini hakuna aliyewaamini, wakasema ni mchawi, lakini hali halisi ikawafanya waongo, Ndipo wakadhamiria kumuua, wakawa wanashauriana katika njia ya kummaliza.
Mwenyezi Mungu akamwambia Mtume wake usijali na yale wanayoyasema na wanayoyapanga kuhusu wewe, kwani nguvu na utukufu wote ni wa Mwenyezi Mungu, sio wa jaha wala mali. Yeye ndiye ambaye humtukuza amtakaye na humdhalilisha amtakaye. Na atawaadhibu wale waliokukadhibisha na kukuambia waliyokuambia na hawatapata msaidizi wala mlinzi atakayewakinga na adhabu na ghadhabu za Mwenyezi Mungu.
Yeye ndiye mwenye kusikia uzushi wao juu yako Mjuzi, wa njama wanazozipanga juu yako na yeye anawagonja.
Unaweza kuuliza
: kuwa Aya hii imefahamisha kuwa ushindi wote ni wa Mwenyezi Mungu peke yake, Kuna Aya isemayo:
وَلِلَّـهِ الْعِزَّةُ وَلِرَسُولِهِ وَلِلْمُؤْمِنِينَ ﴿٨﴾
“Na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye enzi na Mtume wake, na Waumini.” (63:8).
Jibu
: Enzi ya Mtume na ya Waumini inatokana na Mwenyezi Mungu; wana nguvu za ushindi kutokana na yeye na kwake wanategemea.
Juweni kuwa ni wa Mwenyezi Mungu wote waliomo mbinguni na waliomo ardhini.
Mwenye kuwa na yote hayo ana uwezo wa kumnusuru Mtume wake na kumpa nguvu mbele za maadui zake. Mwenyezi Mungu amesema: waliomo na wala hakusema vilivyomo, kwa sababu mazungumzo yanawahusu washirikina ambao wamemzulia uwongo Mwenyezi Mungu
Na wale wanaomba asiyekuwa Mwenyezi Mungu hawawafuati kuwa ni washirika, wa Mungu.
Ukiwa unamfuata mtu kwa kuitakidi kuwa yuko sawa na akawa amepotea, basi utakuwa hufuati usawa bali unafuata upotevu. Hivyo ndivyo ilivyo wanaoabudu masanamu kwa kuitakidi kuwa ni washiriki wa Mwenyezi Mungu. Kwa hakika hasa ilivyo, ni wao hawaabudu washirika wa Mwenyezi Mungu, kwa sababu sio washirika wa Mwenyezi Mungu kiuhakika.
Maana haya yanafafanuliwa na kauli yake Mwenyezi Mungu. Hawafuati ila dhana tu,
na hawasemi ila uwongo tu,
kauli ya hawasemi ila uwongo tu, inatia nguvu kauli ya hawafuati isipokuwa dhana tu. Umetangulia mfano wa Aya hii na maelezo yake katika Aya 28 ya Sura hii.
Yeye ndiye aliyewafanyia usiku ili mtulie humo na mchana wa kuonea. Hakika katika haya kuna ishara kwa watu wanaosikia.
Mchana ni wa kuona ili tujishughulishe kwa kazi na usiku ni giza ili tupumzike kutokana na mihangaiko ya mchana. Ufafanuzi zaidi wa Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu.
وَجَعَلْنَا اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ آيَتَيْنِ فَمَحَوْنَا آيَةَ اللَّيْلِ وَجَعَلْنَا آيَةَ النَّهَارِ مُبْصِرَةً لِّتَبْتَغُوا فَضْلًا مِّن رَّبِّكُمْ ﴿١٢﴾
“Na tumeufanya usiku na mchana ni ishara mbili, kisha tukaifuta ishara ya usiku na tukaifanya ishara ya mchana ya kuonea ili mtafute fadhla itokayo kwa Mwenyezi Mungu.” (17:12)
Wanasema: Mwenyezi Mungu amejifanyia mtoto! Ametakata na hayo! Yeye ni mkwasi. Ni vyake vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini. Nyinyi hamna dalili kwa hayo, Je, mnasema juu ya Mwenyezi Mungu msiyoyajua?
Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz.1 (2:117). Huko tumezungumzia utatu (mungu baba, mungu mwana na roho mtakatifu).
Sema: Hakika wale ambao wanamzulia Mwenyezi Mungu uwongo hawatafaulu
katika Akhera ambayo ni bora na yenye kubaki kulinganisha na maisha yetu haya.
Adhabu yao na maangamizi yao yatakuwa makubwa, ikiwa uzushi wao ni katika dhati yake Mwenyezi Mungu na sifa Zake na kumnasibishia washirika mke na mtoto
Ni starehe katika dunia.
Yaani neema waliyonayo washirikina ni starehe duni, hata kama mali yao ni nyingi na wakawa na jaha kubwa, kwa sababu yote hayo ni ya muda mfupi tena yanachanganyika na matatizo. Nayo si lolote yakilinganishwa na neema za Akhera.
Kisha marejeo ni kwetu tena tutawaonjesha adhabu kali, kwa sababu walikuwa wakikufuru Mungu na neema zake na kumkadhibisha Mtume wake.
وَاتْلُ عَلَيْهِمْ نَبَأَ نُوحٍ إِذْ قَالَ لِقَوْمِهِ يَا قَوْمِ إِن كَانَ كَبُرَ عَلَيْكُم مَّقَامِي وَتَذْكِيرِي بِآيَاتِ اللَّـهِ فَعَلَى اللَّـهِ تَوَكَّلْتُ فَأَجْمِعُوا أَمْرَكُمْ وَشُرَكَاءَكُمْ ثُمَّ لَا يَكُنْ أَمْرُكُمْ عَلَيْكُمْ غُمَّةً ثُمَّ اقْضُوا إِلَيَّ وَلَا تُنظِرُونِ ﴿٧١﴾
71. Na wasomee habari za Nuh alipowaambia watu wake: Enyi watu wangu! Ikiwa cheo changu na kukumbusha kwangu Ishara za Mwenyezi Mungu kunawachukiza, basi mimi namtegemea Mwenyezi Mungu, nanyi tengenezeni mambo yenu na washirika wenu, tena mambo yenu yasi- fichikane kwenu, kisha mlitekeleze kwangu wala msinipe nafasi.
فَإِن تَوَلَّيْتُمْ فَمَا سَأَلْتُكُم مِّنْ أَجْرٍ إِنْ أَجْرِيَ إِلَّا عَلَى اللَّـهِ وَأُمِرْتُ أَنْ أَكُونَ مِنَ الْمُسْلِمِينَ ﴿٧٢﴾
72. Lakini mkikengeuka, basi mimi siwaombi ujira. Ujira wangu hauko ila kwa Mwenyezi Mungu, Na nimeamrishwa niwe miongoni mwa waislamu.
فَكَذَّبُوهُ فَنَجَّيْنَاهُ وَمَن مَّعَهُ فِي الْفُلْكِ وَجَعَلْنَاهُمْ خَلَائِفَ وَأَغْرَقْنَا الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا فَانظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُنذَرِينَ ﴿٧٣﴾
73. Wakamkadhibisha, basi tukamwokoa na waliokuwa naye katika jahazi na tukawafanya ndio waliobakia, Tukawazamisha waliozikadhibisha Ishara zetu. Basi angalia vipi ulikuwa mwisho wa walioonywa.
HABARI ZA NUH
Aya 71 – 73
MAANA
Na wasomee habari za Nuh.
Anaambiwa Mtume Muhammad(s.a.w.
w
)
awasomee washirikina wa Makka.
Alipowaambia watu wake: Enyi watu wangu! Ikiwa cheo changu na kukumbusha kwangu Ishara za Mwenyezi Mungu kunawachukiza, basi mimi namtegemea Mwenyezi Mungu, nanyi tengenezeni mambo yenu na washirika wenu, tena mambo yenu yasifichikane kwenu, kisha mlitekeleze kwangu wala msinipe nafasi.
Mtume Muhammad(s.a.w.
w
)
aliwaonya watu wake katika washirikina wa Makka akawatahadharisha na adhabu kali, lakini wakachukia mawaidha yake na maonyo yake. Bado aliendelea kuwalingania, wakachukizwa na cheo chake na wakajaribu kumuua.
Ndipo Mwenyezi Mungu akamwamrisha awasomee habari za Nuh ambaye aliwaonya watu wake, wakachukia maonyo yake na cheo chake, sawa na ilivyo kwake yeye Muhammad na washirikina wa Makka.
Muhtasari habari za Nuh alizowasomea washirikina wa Makka ni kwamba Nuh alishaindana na waliomkadhibisha na akawaambia kuwa mimi ninamtegemea Mwenyezi Mungu na nitawashinda; hata kama nyinyi ni wengi na wenye nguvu, Kwa sababu Mwenyezi Mungu ameniahidi kunipa ushindi naye havunji ahadi yake. Ama vitisho vyenu kwangu haviwezi kunizuwiya kuendelea na mwito wa Mwenyezi Mungu.
Kwa hiyo lililobaki kwenu ni kupanga njama kwa kadiri mtakavyoweza, muwakusanye wale wasiokuwa Mwenyezi Mungu, uonyesheni uadui mnavyotaka, endeleeni kuniudhi na yafanyeni hayo.
Lakini mkikengeuka, basi mimi siwaombi ujira.
Yaani kama mtapinga mwito wangu, basi mimi sijali upinzani wenu, kwa sababu hakuna manufaa yoyote nitakayoyakosa wala madhara nitakayopata.
Ujira wangu hauko ila kwa Mwenyezi Mungu
sio kwenu nyinyi, kwani hakika mimi ninamfanyia yeye sio nyinyi.
Na nimeamrishwa niwe miongoni mwa waislamu.
Mimi nimetii na kutekeleza ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa njia zake.
Baada ya hapo nishauri yenu mkisilimu au mkikufuru.
Wakamkadhibisha, basi tukamwokoa na waliokuwa naye katika jahazi na tukawafanya ndio waliobakia, Tukawazamisha waliozikadhibisha Ishara zetu. Basi angalia vipi ulikuwa mwisho wa walioonywa.
Hivyo ndivyo unavyokuwa mwisho wa wanaopinga. Wanaangamia na Waumini wanaokoka na kuchukua mahali pa wanaokadhibisha walioangamia. Basi anagalia jinsi ulivyokuwa mwisho wa wale walioonywa. Anaambiwa Mtume Muhammad(s.a.w.
w
)
awaonye washirikina wa Makka yasije yakawapata yaliyowapata watu wa Nuh. Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz. 8 (7:72).
ثُمَّ بَعَثْنَا مِن بَعْدِهِ رُسُلًا إِلَىٰ قَوْمِهِمْ فَجَاءُوهُم بِالْبَيِّنَاتِ فَمَا كَانُوا لِيُؤْمِنُوا بِمَا كَذَّبُوا بِهِ مِن قَبْلُ كَذَٰلِكَ نَطْبَعُ عَلَىٰ قُلُوبِ الْمُعْتَدِينَ ﴿٧٤﴾
74. Kisha baada yake tukatuma Mitume kwa watu wao. Nao wakawajia kwa Ishara zilizo wazi. Lakini hawakuwa ni wenye kuamini waliyokuwa wameyakadhibisha kabla, Hivyo ndivyo tunapopiga muhuri juu ya nyoyo za wapetukao mipaka.
ثُمَّ بَعَثْنَا مِن بَعْدِهِم مُّوسَىٰ وَهَارُونَ إِلَىٰ فِرْعَوْنَ وَمَلَئِهِ بِآيَاتِنَا فَاسْتَكْبَرُوا وَكَانُوا قَوْمًا مُّجْرِمِينَ ﴿٧٥﴾
75. Kisha tukapeleka baada ya hao Musa na Harun kwa Firauni na waheshimiwa wake kwa ishara zetu, Wakafanya kiburi nao walikuwa watu wenye makosa.
فَلَمَّا جَاءَهُمُ الْحَقُّ مِنْ عِندِنَا قَالُوا إِنَّ هَـٰذَا لَسِحْرٌ مُّبِينٌ ﴿٧٦﴾
76. Basi ilipowafikia haki kutoka kwetu walisema: Hakika huu ni uchawi ulio wazi.
قَالَ مُوسَىٰ أَتَقُولُونَ لِلْحَقِّ لَمَّا جَاءَكُمْ أَسِحْرٌ هَـٰذَا وَلَا يُفْلِحُ السَّاحِرُونَ ﴿٧٧﴾
77. Musa akasema: Mnasema juu ya haki ilipowafikia, je huu ni uchawi? na wachawi hawafanikiwi!
قَالُوا أَجِئْتَنَا لِتَلْفِتَنَا عَمَّا وَجَدْنَا عَلَيْهِ آبَاءَنَا وَتَكُونَ لَكُمَا الْكِبْرِيَاءُ فِي الْأَرْضِ وَمَا نَحْنُ لَكُمَا بِمُؤْمِنِينَ ﴿٧٨﴾
78. Wakasema: Je, umetujia ili utuondoe katika yale tuliyowakuta nayo baba zetu. Ili ukubwa uwe wenu nyinyi wawili katika nchi, na sisi hatuwaamini nyinyi.
وَقَالَ فِرْعَوْنُ ائْتُونِي بِكُلِّ سَاحِرٍ عَلِيمٍ ﴿٧٩﴾
79. Akasema Firauni: Nileteeni kila mchawi mjuzi.
فَلَمَّا جَاءَ السَّحَرَةُ قَالَ لَهُم مُّوسَىٰ أَلْقُوا مَا أَنتُم مُّلْقُونَ ﴿٨٠﴾
80. Basi walipokuja wachawi, Musa akawaambia: “Tupeni mnavyotupa
فَلَمَّا أَلْقَوْا قَالَ مُوسَىٰ مَا جِئْتُم بِهِ السِّحْرُ إِنَّ اللَّـهَ سَيُبْطِلُهُ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُصْلِحُ عَمَلَ الْمُفْسِدِينَ ﴿٨١﴾
81. Walipotupa, Musa akasema: Mlioleta ni uchawi, hakika Mwenyezi Mungu ataubatilisha, Hakika Mwenyezi Mungu hafanikishi vitendo vya wafisadi.
وَيُحِقُّ اللَّـهُ الْحَقَّ بِكَلِمَاتِهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُجْرِمُونَ ﴿٨٢﴾
82. Na Mwenyezi Mungu anaihakikisha haki kwa maneno yake, ingawa watachukia wenye makosa.
KISHA TUKAWAPELEKEA MITUME BAADA YAKE
Aya 74 – 82
MAANA
Kisha baada yake tukatuma Mitume kwa watu wao. Nao wakawajia kwa Ishara zilizowazi. Lakini hawakuwa ni wenye kuamini waliyokuwa wameyakadhibisha kabla.
Yaani baada ya Nuh tulipeleka Mitume kwa watu wao, kama Ibrahim, Hud, Swaleh na wenginio, wakiwa na dalili na miujiza, lakini miujiza hii haikuwatoa kwenye ushirikina, kuwageuza kwenye imani ya umoja wa Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho.
Wao waliyakadhibisha hayo kabla kuwajia Mitume na hoja zilizo wazi, kwa hivyo waliendelea na kukadhibisha kwao huku hata baada ya kuwajia Mitume na kuwaonya.Kwa maneno mengine ni kuwa hawakunufaika na elimu ya Mitume na mwongozo wao.
UONGOFU NA UPOTEVU
Hivyo ndivyo tunapopiga muhuri juu ya nyoyo za wapetukao mipaka.
Unaweza kuuliza
: ikiwa Mwenyezi Mungu ndiye aliyepiga muhuri juu ya nyoyo zao, basi vipi atawaadhibu?
Jibu
: Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaka uongofu uwe na njia yake maalum ambayo ni kufuata Mitume yake. Na upotevu nao uwe na njia yake ambayo ni kufuata matamanio. Kwa hiyo mwenye kufuata njia ya Mitume atafikia kwenye uongofu kwa vyovyote vile, na mwenye kufuata matamanio atafikia kwenye upotevu, sawa na alivyojaalia Mwenyezi Mungu kwamba mwenye kujitupa kutoka juu atakufa na mwenye kujitupa baharini akiwa hajui kuogelea atakufa maji tu.
Kwa kufangamanisha njia hizo mbili na matakwa ya Mwenyezi Mungu ndio ikawa Mwenyezi Mungu ndiye aliyepiga muhuri hizo njia mbili, Yamekwisha elezwa maelezo hayo mara nyingi, Kwa ibara mbali mbali.
Kisha tunapeleka baada ya hao Musa na Harun kwa Firauni na waheshimiwa wake kwa Ishara zetu.
Yaani baada ya Mitume waliokuja baada ya Nuh, tulimtuma Musa na Harun na miujiza, kama vile fimbo kugueka nyoka na mkono kuwa mweupe.
Kusema kwake Mwenyezi Mungu‘na tukawapelekea’
inafahamisha wazi kuwa Harun ni Mtume sawa na nduguye Musa. Inasemekana kuwa Harun ni mkubwa wa Musa kwa miaka mitatu.
Wakafanya kiburi
kukubali hakinao walikuwa watu wenye makosa.
Kila anayepinga kukubali haki basi ni mwenye makosa.
Basi ilipowafikia haki kutoka kwetu
ambayo ni miujiza aliyoidhihirisha Mwenyezi Mungu mikononi mwa Musa
,walisema
:
Hakika huu ni uchawi ulio wazi.
Kama hivyo walisema washirikina wa Kiquraish kuhusu Mtume Muhammad(s.a.w.
w
)
alipowajia na Qur’ani na muujiza wake. Ni muhali kabisa kupona muongozaji na uzushi wa wafisadi.
Na uzushi wenyewe unakwenda na wakati. Hapo mwanzo watu walikuwa wakiamini mchawi, kwa hiyo kiongozi mwema alikuwa akiitwa mchawi, ama leo ambapo hakuna imani ya uchawi wanamwita ni mvurugaji.
Musa akasema: Mnasema juu ya haki ilipowafikia, je huu ni uchawi?
Vipi iwe hivyo haki ina lengo la kuwaongoza watu ambapo uchawi unapotosha hali halisi na kuwapoteza watuna wachawi hawafanikiwi
! Je, anaweza kufanikiwa mwenye kiini macho.
Wakasema: Je, umetujia ili utuondoe katika yale tuliyowakuta nayo baba zetu.
Huu ni mchezo anaoucheza kila mwenye ufisadi ambao una maslahi kwake. Suala ni kuhofia maslahi tu, sio suala la mababa na masanamu. Dalili ya hilo ni kauli yao anayoisimulia Mwenyezi Mungu:Ili ukubwa uwe wenu nyinyi wawili katika nchi.
Hiyo ni kauli ya Firauni na wakuu wake wa nchi kumwambia Musa na ndugu yake Harun. Walikuwa na maana ya kuwa lengo ni kunyang’anywa ufalme wa Misr sio ujumbe wa Mwenyezi Mungu. Ndipo wakasema:Na sisi hatuwamini nyinyi.
Bali tutapigana kulinda manufaa yetu na vyeo vyetu.
Akasema Firauni: Nileteeni kila mchawi mjuzi,
naye hajui matekeo ya hayo.
Basi walipokuja wachawi, Musa akawaambia: Tupeni mnavyotupa.
Alisema hivi kwa kuwapuuza wao, uchawi wao na Firauni wao, Kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemwaahidi ushindi.
Walipotupa, Musa akasema: Mlioleta ni uchawi, hakika Mwenyezi Mungu ataubatilisha.
Huo wenyewe ni batili tangu mwanzo, lakini Mwenyezi Mungu atadhihirisha ubatilifu wake kwa watu. Ama fimbo ya Musa haipatwi na ubatil- ifu kwa sababu ni haki itokayo kwa Mwenyezi Mungu.
Hakika Mwenyezi Mungu hafanikishi vitendo vya wafisadi, Na Mwenyezi Mungu anaihakikisha haki kwa maneno yake
ambayo ni hoja mkataa. Ingawa watachukia wenye makosa, kwa sababu chuki yao haiwezi kusimamisha matakwa ya Mwenyezi Mungu.
11
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MOJA
فَمَا آمَنَ لِمُوسَىٰ إِلَّا ذُرِّيَّةٌ مِّن قَوْمِهِ عَلَىٰ خَوْفٍ مِّن فِرْعَوْنَ وَمَلَئِهِمْ أَن يَفْتِنَهُمْ وَإِنَّ فِرْعَوْنَ لَعَالٍ فِي الْأَرْضِ وَإِنَّهُ لَمِنَ الْمُسْرِفِينَ ﴿٨٣﴾
83. Basi hawakumwamini Musa, isipokuwa baadhi ya vijana katika watu wake, kwa sababu ya kumwogopa Firauni na wakubwa wao asiwatie msuko suko. Na hakika Firauni alikuwa jeuri katika nchi, na kwa hakika alikuwa miongoni mwa waliopita kiasi.
وَقَالَ مُوسَىٰ يَا قَوْمِ إِن كُنتُمْ آمَنتُم بِاللَّـهِ فَعَلَيْهِ تَوَكَّلُوا إِن كُنتُم مُّسْلِمِينَ ﴿٨٤﴾
84. Na Musa akasema: Enyi watu wangu! Ikiwa nyinyi mmemwamini Mwenyezi Mungu, basi mtegemeeni yeye, ikiwa nyinyi ni waislamu.
فَقَالُوا عَلَى اللَّـهِ تَوَكَّلْنَا رَبَّنَا لَا تَجْعَلْنَا فِتْنَةً لِّلْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴿٨٥﴾
85. Wakasema: Tumemtegemea Mwenyezi Mungu. Ewe Mola wetu! Usitufanye wenye kutiwa misukosuko na watu madhalimu.
وَنَجِّنَا بِرَحْمَتِكَ مِنَ الْقَوْمِ الْكَافِرِينَ ﴿٨٦﴾
86. Na utuokoe kwa rehema yako na watu makafiri.
وَأَوْحَيْنَا إِلَىٰ مُوسَىٰ وَأَخِيهِ أَن تَبَوَّآ لِقَوْمِكُمَا بِمِصْرَ بُيُوتًا وَاجْعَلُوا بُيُوتَكُمْ قِبْلَةً وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَبَشِّرِ الْمُؤْمِنِينَ ﴿٨٧﴾
87. Na tukampa wahyi Musa na Harun: watengezeeni watu wenu majumba Misr, Na mzifanye nyumba zenu zenye kuelekea upande mmoja, Na simamisheni swala Na wape bishara waumini.
وَقَالَ مُوسَىٰ رَبَّنَا إِنَّكَ آتَيْتَ فِرْعَوْنَ وَمَلَأَهُ زِينَةً وَأَمْوَالًا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا رَبَّنَا لِيُضِلُّوا عَن سَبِيلِكَ رَبَّنَا اطْمِسْ عَلَىٰ أَمْوَالِهِمْ وَاشْدُدْ عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ فَلَا يُؤْمِنُوا حَتَّىٰ يَرَوُا الْعَذَابَ الْأَلِيمَ ﴿٨٨﴾
88. Na Musa akasema: Mola wetu! Hakika wewe umempa Firauni na wakuu wake mapambo na mali nyingi katika maisha ya dunia. Mola wetu! Hivyo wanawapoteza watu na njia yako. Mola wetu! Ziangamize mali zao, Na zitie shida nyoyo zao, Na hawataamini mpaka waione adhabu yenye kuumiza.
قَالَ قَدْ أُجِيبَت دَّعْوَتُكُمَا فَاسْتَقِيمَا وَلَا تَتَّبِعَانِّ سَبِيلَ الَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٨٩﴾
89. Akasema Mwenyezi Mungu, maombi yenu yamekubaliwa. Basi muwe na msimamo wala msifuate njia ya wale wasiojua.
HAWAKUMUAMINI MUSA
Aya 83 – 89
MAANA
Basi hawakumwamini Musa, isipokuwa baadhi ya vijana katika watu wake, kwa sababu ya kumwogopa Firauni na wakubwa wao asiwatie msuko suko.
Baada ya Musa kutupa fimbo na Mwenyezi Mungu kudhihirisha haki mikononi mwake, waliamini wachawi na watu wengi. Lakini kabla ya tukio la fimbo, walioamini ni vijana tu, katika Waisrael. Kwa sababu vijana walikuwa na wanaendelea kuwa ni wenye hamasa kwa kila jipya.
Lakini walimwamini Musa huku wakimhofia Firauni na pia wakubwa wa Waisrael, wasiwatie msuko suko kwa kuwaadhibu ili waikatae dini yao. Baadhi ya wanaotafuta maslahi katika Mayahudi walikuwa wakila njama na Firauni dhidi ya watu wao; kama ilivyo watu wa dini kila wakati na kila mahali.
Na hakika Firauni alikuwa jeuri katika nchi, na kwa hakika alikuwa miongoni mwa walipita kiasi katika na utaghuti wake. Na Musa akasema: Enyi watu wangu! Ikiwa nyinyi mmemwamini Mwenyezi Mungu, basi mtegemeeni yeye, ikiwa nyinyi ni waislamu.
Musa hakuwa na chochote isipokuwa haki, na Firauni alikuwa na kila kitu, isipokuwa haki. Alikuwa akimkandamiza na kumtesa kila anayemwamini Musa. Musa akawa anawaambia watu wake, mimi sina nguvu wala nyinyi hamna nguvu za kumzuwiya Firauni na dhulma yake, isipokuwa kumtegemea Mwenyezi Mungu, na vilevile kutegemea ahadi yake kwamba mwisho ni wa wenye kumcha Mwenyezi Mungu, kwa hiyo tegemeeni mambo yenu kwake Mwenyezi Mungu, ikiwa kweli mnamtii yeye.
Aliwatajia sifa tatu: Imani ambayo ni kusadikisha moyoni. Ya pili ni Uislam ambao makusudio yake hapo ni kufuata na kusalim amri kwa Mwenyezi Mungu, ya tatu ni kumtegemea Mwenyezi Mungu, nako ni kufanya Ikhlasi na kutegemeza mambo yote kwa Mwenyezi Mungu peke yake. Mwenye kukusanya sifa hizi atakuwa pamoja na Mwenyezi Mungu.
Wakasema: Tumemtegemea Mwenyezi Mungu,
na mambo yote tumemwachia yeye. Ndiye anayejua hali yetu na maslahi yetu, na yeye ni mweza juu ya kila jambo.
Ewe Mola wetu! Usitufanye wenye kutiwa misukosuko na watu madhalimu.
Makusudio ya madhalimu hapa ni makafiri ambao ni Firauni na watu wake. Na misukosuko ni adhabu, kwa maana ya kuwa, usitujaalie ni mahali pa adhabu yao.
Na utuokoe kwa rehma yako na watu makafiri.
Makafiri hapa ni hao madhalimu ambao ni Firauni na watu wake ambao waliwakandamiza Waisrael. Makusudio ya kuokoka hapa ni kuokoka na dhulma yao na ukandamizaji wao. Kwa hiyo Aya hii ni tafsir ya Aya iliyo kabla yake.
Na tukampa wahyi Musa na Harun: watengezeeni watu wenu majumba Misr.
Yaani msiondoke hapo Misr na mfanye maskani kwa ajili ya Waisrael watakapokimbilia na kujilinda.
Na mzifanye nyumba zenu zenye kuelekea upande mmoja.
Yaani nyote mkae kwenye mtaa mmoja.
Imesemekana kuwa maana yake ni ‘mzifanye nyumba zenu ni mwahala mwa ibada,’ lakini tafsir ya kwanza ina nguvu kuliko kuwa majumba yawe miskiti kwa sababu majumba sio miskiti, miskiti ni ya ibada na majumba ni ya kukaa.
Na simamisheni Swala,
kwa sababu ndiyo mambo ya Ikhlas na inaziku- sanya nyoyo kwenye hisiya ya umoja.
Na wape bishara waumini
ya kuokoka na Firauni na wakubwa wake wa nchi katika dunia na kupata Pepo akhera.
Maneno yameelekezwa kwa Musa, kwa sababu yeye ndiye asili ya ujumbe, na kwa Harun kwa sababu yeye ni mfuasi wake.
Na Musa akasema: “Mola wetu! Hakika wewe umempa Firauni na wakuu wake mapambo na mali nyingi katika maisha ya dunia.
Aya hii ilishuka wakati ambao watu hawakuwa wakijua chochote kuhusu yaliyomo katika makaburi ya mafir’aun, Kisha wachimbaji wagunduzi wakagundua mali na vipambo vilivyoelezwa na Qur’ani. Huu ni ushahidi usiokuwa na shaka yeyote kwamba Qur’ani ni wahyi utokao kwa anayejua ghaibu.
Hivyo wanawapoteza watu na njia yako.
Yaani natija ya kuneemeshwa kwao na Mwenyezi Mungu kwa vipambo na mali, ni kumwasi badala ya kumtii.
Mola wetu! Ziangamize mali zao.
Mtu anaweza kudhani kuwa katika dua, Nabii Musa alimtaka Mwenyezi Mungu kuzuwiya utajiri wa wapotevu, ili wasizidi upotevu, lakini lililokatazwa ni ufisadi ambao ameukataza Mwenyezi Mungu. Tumelifafanua hilo katika Juz; 6 (5:66) kifungu cha ‘riziki na ufisadi.’
Na zitie shida nyoyo zao.
Imesemekana kuwa makusudio ni kuzifunga nyoyo zao wabaki katika miji yao ili waone kwa macho maangamizi ya mali zao. Pia ikasemekana ni kuzifunika nyoyo. Lakini tuonavyo sisi ni kuwa makusudio ni shida.
Yaani Musa
alimwomba Mwenyezi Mungu kuleta shida katika nyoyo zao.
Tafsiri hii inanasibiana na ombi lake Musa
la kuangamizwa mali zao.
Na hawataamini mpaka waione adhabu yenye kuumiza.
Jumla hii inaungana na ‘wawapoteze waja wako’. Yaani mwisho wa neema ya Mwenyezi Mungu kwa Firauni ni kuwapoteza watu na kutoamini mpaka waione adhabu, wakati ambao haitafaa imani. Hapana mwenye shaka kwamba Musa
hakuomba haya yote ila baada ya kukata tamaa na kuongoka kwao.
Akasema Mwenyezi Mungu
:
maombi yenu yamekubaliwa.
Yaani mambo ya kuangamizwa mali ya Firauni na wakubwa wake wa nchi na shida na masaibu kwenye nyoyo zao.
Basi muwe na msimamo
katika njia hiyo ya jihad ya kuilingania haki.wala msifuate njia ya wale wasiojua
ukubwa wa Mwenyezi Mungu na hekima yake.
Imefaa hapa kukatazwa ambaye hafanyi dhambi (maasum); Kwa sababu makatazo yanatoka kwa Mwenyezi Mungu si kwa mwingine. Ni kawaida aliye mkubwa kumwamuru aliye chini yake kwa namna yoyote alivyo.
وَجَاوَزْنَا بِبَنِي إِسْرَائِيلَ الْبَحْرَ فَأَتْبَعَهُمْ فِرْعَوْنُ وَجُنُودُهُ بَغْيًا وَعَدْوًا حَتَّىٰ إِذَا أَدْرَكَهُ الْغَرَقُ قَالَ آمَنتُ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا الَّذِي آمَنَتْ بِهِ بَنُو إِسْرَائِيلَ وَأَنَا مِنَ الْمُسْلِمِينَ ﴿٩٠﴾
90. Na tukawavusha bahari wana wa Israel na Firauni na askari wake wakawafuatia kwa dhulma na uadui mpaka kulipomfikia kufa maji, akasema: Nimeamini kwamba hakuna Mola isipokuwa yule wanayemuamini wana wa Israel nami ni miongoni mwa waislam (walionyenyekea).
آلْآنَ وَقَدْ عَصَيْتَ قَبْلُ وَكُنتَ مِنَ الْمُفْسِدِينَ ﴿٩١﴾
91. Je, sasa! Na hali uliasi kabla yake na ukawa miongoni mwa wafisadi.
فَالْيَوْمَ نُنَجِّيكَ بِبَدَنِكَ لِتَكُونَ لِمَنْ خَلْفَكَ آيَةً وَإِنَّ كَثِيرًا مِّنَ النَّاسِ عَنْ آيَاتِنَا لَغَافِلُونَ ﴿٩٢﴾
92. Basi leo tutakuokoa kwa mwili wako ili uwe ishara kwa ajili wa nyuma yako. Na hakika watu wengi wameghafilika na Ishara zetu.
وَلَقَدْ بَوَّأْنَا بَنِي إِسْرَائِيلَ مُبَوَّأَ صِدْقٍ وَرَزَقْنَاهُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ فَمَا اخْتَلَفُوا حَتَّىٰ جَاءَهُمُ الْعِلْمُ إِنَّ رَبَّكَ يَقْضِي بَيْنَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فِيمَا كَانُوا فِيهِ يَخْتَلِفُونَ ﴿٩٣﴾
93. Nao hawakuhitalifiana mpaka ilipowafikia elimu. Hakika Mola wako atahukumu baina yao siku ya Kiyama katika yale waliyokuwa wakihitalifiana.
NA TUKAVUSHA BAHARI WAISRAEL
Aya 90 – 93
MAANA
Na tukawavusha bahari wana wa Israel na Firauni na askari wake wakawafuatia kwa dhulma na uadui.
Umetangulia mfano wake katika Juz.1 (2:50) na Juz.9 (7: 136).
MWISHO WA UTWAGHUTI
Mpaka kulipomfikia kufa maji, akasema nimeamini kwamba hakuna Mola isipokuwa yule wanayemuamini wana wa Israel nami ni miongoni mwa waislam (walionyenyekea).
Jana alikuwa Firauni akisema: Mimi ndiye Mola wenu mkubwa ,na leo anakana, Hali zote mbili hazimfai, si ile ya kwanza wala hii ya sasa. Mlango wa twaa ulipokuwa wazi yeye aliasi, na sasa hakuna nafasi tena ya utiifu wala uasi.
Hivi ndivyo alivyo mtu duni, hujifanya mkubwa wakati wa neema na kujifanya mdogo wakati wa dhiki. Historia huwa inajirudia; yaani desturi ya Mwenyezi Mungu katika viumbe vyake ambayo ameisharia kwa kusisitiza pale aliposema:
فَلَن تَجِدَ لِسُنَّتِ اللَّـهِ تَبْدِيلًا وَلَن تَجِدَ لِسُنَّتِ اللَّـهِ تَحْوِيلًا ﴿٤٣﴾
“Basi hutapata mabadiliko katika desturi ya Mwenyezi Mungu, wala huta pata mageuko katika desturi ya Mwenyezi Mungu” (35:43)
Israil ya leo, inayokwenda kwa msaada wa ukoloni, inakwenda sawa na desturi ya Firauni hasa.
Firauni alikuwa akiwachinja watoto wa kiume wa Israel na kuwacha watoto wa kike. Leo Israel inafanya hivyo hivyo kwa wapalestina tena zaidi kuliko Firauni.
Firauni alisema:
قَالَ يَا قَوْمِ أَلَيْسَ لِي مُلْكُ مِصْرَ وَهَـٰذِهِ الْأَنْهَارُ تَجْرِي مِن تَحْتِي ﴿٥١﴾
“Enyi watu wangu, je, ufalme wa Misr si ni wangu na hii mito ipitayo chini yangu?” (43:51).
Israel nayo inasema: Je, Palestina si ni yetu pamoja na mali zake zote, ikiwa ni pamoja na milima ya Golan na ukanda wa Gaza. Firauni alisema:
فَقَالَ أَنَا رَبُّكُمُ الْأَعْلَىٰ ﴿٢٤﴾
“Mimi ndiye Mola wenu mkuu.” (79:24).
Israel na wanaowasaidia wanasema hatuwezi kushindwa sisi
Hazikupita siku nyingi ila ilianza kudhihiri desturi ya Mwenyezi Mungu. Ambapo Elat iliangamia na kuharibiwa vituo vya mabomu na wanaojitoa mhanga, kumemlazimisha Dayan kusema: “Ni lazima Mayahudi wajiandae kupanua uwanja wa makaburi yao.”
Na atasema tu, kama sio leo ni kesho: Nimemwamini yule anayeaminiwa na Waarabu na Waislam; sawa na alivyosema Firauni. Kwa sababu yeye anafuata nyayo zake, basi mwisho wake utakuwa sawa na Firauni tu. Mtu anaweza kusema kuwa vita vya Israael vimekuwa virefu na vyenye kuumiza
Tunaweza kujibu kuwa ni kweli, lakini ushindi wa mwisho ni wa wenye haki, hata kama muda utarefuka kwa kiasi gani. Historia ya zamani na ya karibuni ni shahidi wa hakika hii, kuanzia kwa Firauni na Hamana hadi kwa Hitler na Mussolini.
Je, sasa!
Baada ya kukupata yaliyokupata ndio unasema nimeamini?
Na hali uliasi kabla yake
ulipokuwa na hiyari ya kutubia na kurudi kwenye haki, lakini ukafanya dhulmana ukawa miongoni mwa wafisadi.
Kwa hiyo onja malipo ya amali yako kwa kufa maji, na kuangamia.
Basi leo tutakuokoa kwa mwili wako
sio kwa roho yako; na mwili wako na tutautupa nchi kavu ili auone yule aliyekuwa akikutukuza.
Ili uwe ishara kwa ajili wa nyuma yako
apate mawaidha yule atakayeiweka nafsi yake kwenye ufisadi. Lakini wapi! Ibra ni nyingi lakini mazingatio ni machache, ndio Mwenyezi Mungu akasema:
Na hakika watu wengi wameghafilika na ishara zetu, Nao hawakuhitalifiana mpaka ilipowafikia elimu.
Yaani baada ya kuangamia Firauni, tuliwapa makazi mazuri na ardhi yenye rutuba.
Wafasiri wametofautiana kuhusu mji waliokuwa, wengine wamesema ni Palestina na wengine wakasema ni Misr. Kauli ya Misr ndiyo yenye nguvu kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu. “Basi tukawatoa katika mabustani na chemchem, na mahazina na mahali pazuri. Kama hivyo, na tukawarithisha hayo wana wa Israel.” (26: 57-59).
Aya hii inaonyesha wazi kuwa Mwenyezi Mungu aliwakalisha wana wa Israel nyumba ya Firauni na wakubwa wake.
Nao hawakuhitalifiana mpaka ilipowafikia elimu.
Makusudio ya elimu hapa nia Tawrat, kama ilivyo teremshwa kwa Musa
. Ndani yake mlikuwa na habari ya Mtume Muhammad(s.a.w.
w
)
. Wana wa Israel walikuwa wamoja katika ukafiri na upotevu wao, kabla ya kuteremshwa Tawrat.
Baada ya kuwajia Tawrat wakatofautiana wakati wa Musa na baadae, wengine waliasi zaidi, wakaabudu ndama na wakamwambia Musa tuonyeshe Mwenyezi Mungu wazi wazi, na nenda wewe na Mola wako na mengineyo yaliyosajiliwa na Qur’ani.
Hakika Mola wako atahukumu baina yao siku ya Kiyama katika yale waliyokuwa wakihitalifiana.
Ambapo siku hiyo hakutakuwa na uwongo wala riya au kitu chochote, isipokuwa haki itakayowadhihrikia wote wazi wazi.
فَإِن كُنتَ فِي شَكٍّ مِّمَّا أَنزَلْنَا إِلَيْكَ فَاسْأَلِ الَّذِينَ يَقْرَءُونَ الْكِتَابَ مِن قَبْلِكَ لَقَدْ جَاءَكَ الْحَقُّ مِن رَّبِّكَ فَلَا تَكُونَنَّ مِنَ الْمُمْتَرِينَ ﴿٩٤﴾
94. Ukiwa na shaka juu ya tuliyokuteremshia, basi waulize wale wasomao Kitabu kabla yako. Haki imekwishafikia kutoka kwa Mola wako, kwa hivyo kabisa usiwe miongoni mwa wafanyao shaka.
وَلَا تَكُونَنَّ مِنَ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِ اللَّـهِ فَتَكُونَ مِنَ الْخَاسِرِينَ ﴿٩٥﴾
95. Na kabisa usiwe miongoni mwa wanaokadhibisha Ishara za Mwenyezi Mungu, usije ukawa miongoni mwa wenye hasara.
إِنَّ الَّذِينَ حَقَّتْ عَلَيْهِمْ كَلِمَتُ رَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ ﴿٩٦﴾
96. Hakika wale ambao neno la Mola wako limekwishawathibitikia hawataamini.
وَلَوْ جَاءَتْهُمْ كُلُّ آيَةٍ حَتَّىٰ يَرَوُا الْعَذَابَ الْأَلِيمَ ﴿٩٧﴾
97. Ijapokuwa itawajia Ishara, mpaka waione adhabu iumizayo.
IKIWA UNA SHAKA
Aya 94 –97
MAANA
Ukiwa na shaka juu ya tuliyokuteremshia, basi waulize wale wasomao kitabu kabla yako.
Makusudioya wale wasomao Kitabu ni maulama wa Injil na Tawrat na kinachoulizwa ni kisa cha Musa na Mitume wengine kulingana na Qur’ani. Hiyo ni kwa kuangalia mfumo wa maneno.
Kwa sababu Aya zilishuka kuhusu kisa cha Musa na Firauni.
Unaweza kuuliza
: kuna wajihi gani katika kauli yake Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake.“Ukiwa na Shaka” pamoja na kujua kuwa Mtume hana shaka katika hilo, vipi iwe hivyo na hali yeye amevumilia adha nyingi katika kufikisha ujumbe wake kiasi ambacho hakuwahi kuna nacho Mtume mwingine au kiongozi yoyote.
Jibu
: wajihi ni kumwambia Mtume Muhammad(s.a.w.
w
)
yule anayetia shaka yale yaliyotajwa na Qur’ani kuhusu kisa cha Musa na Mitume wengine, aulize Ulamaa wa watu wa Kitab wasio na upendeleo. Kwani hilo ni lenye kuthibiti katika Tawrat na Injil kama ilivyoeloezwa katika Qur’ani.
Haki imekwishafikia kutoka kwa Mola wako, kwa hivyo kabisa usiwe miongoni mwa wafanyao shaka, Na kabisa usiwe miongoni mwa wanaokadhibisha Ishara za Mwenyezi Mungu, usije ukawa miongoni mwa wenye hasara.
Yaani fikisha ujumbe ewe Muhammad kwa yule mwenye kutia shaka au kuikanusha haki iliyoteremshwa kwako, basi yeye ni miongoni mwa wenye kuadhibiwa siku ya Kiyama, hali ya kupata hasara.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameyatolea ibara makatazo haya kwa kumkataza Mtume kutokana na shaka na uongo, ili Mtume Muhammad(s.a.w.
w
)
aseme kwa watu: Mimi ni mtu mfano wenu na ni mmoja miongoni mwenu, kama nitatia shaka au kukanusha, basi nitahisabiwa na nitaadhibiwa; kama vile mtu yeyote yule atakayetia shaka au kukadhibisha Ishara za Mwenyezi Mungu.
Mfumo huu ni fasaha na wenye kufaulu zaidi katika kuilingania haki ambayo mbele yake inakuwa sawa kwa watu wote
Hakika wale ambao neno la Mola wako limekwishawathibitikia hawataamini, Ijapokuwa itawajia Ishara, mpaka waione adhabu iumizayo.
Makusudio ya neno la Mola wako hapa ni adhabu; yaani hakika wale ambao Mwenyezi Mungu atawaadhibu ni wale wasioiamini haki kwa hali yoyote hata kama ataletewa hoja elfu; isipokuwa kama ataiona adhabu. Na ilivyo ni kwamba imani ya namna hii haifai kitu kwa sababu ni sawa na imani ya Firauni wakati alipoangamia majini; kama iliyoelezwa hivi punde katika kufasiri Aya 90 ya Sura hii.