MDAHALO NA AHMAD DEEDAT
BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM
MDAHALO NA AHMAD DEEDAT
Ulimwengu wa Kiislamu ulipata taarifa nzito za kuondokewa na mmoja wa wanaharakati wake mashuhuri Sheikh Ahmed Deedat wa Afrika Kusini. Deedat ni mwanazuoni mashuhuri katika fani ya Mlingano wa dini, Compatarative Religion. Alisafiri huku na kule duniyani katika harakati za kutowa mihadhara na kushiriki katika midahalo baina yake na wawakilishi wa imani ya Kikristo. Katika mihadhara na midahalo hiyo aliweza kuwavutiya mno wasikilizaji kwa ule umahiri wake wa kujenga hoja pamoja na ufasaha wa lugha ya Kiingereza. Aidha sheikh Deedat ameandika vitabu vingi vyenye mada na maudhuwi mbalimbali.
Kwa pamoja mihadhara, midahalo na vitabu vyake vimeleta athari kubwa ulimwenguni. Mbali na watu wa imani nyingine kuuona ukweli wa imani ya Kiislamu, piya vimetowa changamoto kwa Waislamu wengi duniani ambao wamerithi kazi yake. Kwa hali hii, licha ya kufikwa na umauti, Deedat ataendeleya kuwa hai kutokana na kazi hizo muhimu alizozifanya. Sote lazima tutoweke duniani lakini wapo waja wa MwenyeziMungu ambao watabakizwa hai na yale waliyoyafanya. Sheikh Deedat ni mfano wa waja hao. Tunamuomba MwenyeziMungu aikubali juhudi yake, amghufiriye upungufu wake na amkutanishe na waja wema Peponi-Inna lillahi wainna ilaihi rajiuun. Katika makala haya tunarejeleya moja ya maandiko yake: Majibizano ya Waislamu na Wakristo:
Mdahalo katika televisheni-1983
(Na Ahmed Deedat)
Mwishoni mwa mdahalo- juu ya "Uislamu na Ukristo" ambao ulioneshwa katika Televisheni ya SABC wakati wa kipindi cha "CROSS (+) QUESTIONS siku ya Jumapili, Juni 5, 1983, Mwenyekiti, Bw. Bill Chalmers alisema hivi: "Nadhani kutokana na mjadala huu yaweza kusemwa kuwa, kwa kiyasi fulani, hivi sasa upande wa Uislamu ndio wenye nafasi kubwa zaidi kwa mwasisi wa Ukristo kuingiya huko kuliko nafasi ulionayo upande wa Ukristo kwa Mwasisi wa Uislamu kuingiya huko. Nini undani wa hilo, hiyo tunakuwachiya wewe mtazamaji kuamuwa, ila tu nadhani sote tunakubaliyana kuwa hili ni jambo jema kwani tunakaa pamoja kuzungumza".
"Bill" kama asifiwavyo na wazungumzaji wake wote, si mtu mwenye urasimu katika vipindi vyake, ni mcheshi mno na mwingi wa maungwana. Bwana Billy ni mfano wa Wakristo ambao Qur'an inawaelezeya hivi:
"....Na utawaona walio karibu kwa urafiki na Waislamu ni wale wanaosema: "Sisi ni Wakristo." (Hayo) ni kwa sababu wako miongoni mwao wanavyuoni na wachao Mungu, na kwa sababu wao (Wakristo) hawatakabari (wakijuwa haki huifuwata). (5:82)
HADHI YA YESU
Je wale Waislamu waliokuwa kwenye jopo la wazungumzaji, walikuwa wakijaribu kukonga nyoyo za watazamaji wa Televisheni kinyume na sera au kwa kutumiya uwongo au kwa kutumiya diplomasiya? La hasha! Hapakuwa na kitu cha namna hiyo. Waislamu hao walikuwa wakiyasema yale ambayo MwenyeziMungu, katika Qur'an, amewaamrisha kuyasema. Haikuwa hiyari yao bali walilazimika kusema kwa kutumiya maneno mengi tu kuwa- "Sisi Waislamu tunaamini kuwa Yesu alikuwa mmoja wa Mitume wakubwa wa MwenyeziMungu, kwamba yeye ndiye Masihi, kwamba alizaliwa kimiujiza-bila maingiliyano ya jinsiya ya kiume na ya kike ( jambo ambalo Wakristo wengi wa leo hawaliamini), kwamba aliwafufuwa wafu kwa idhini ya Mungu, na kwamba aliwaponya vipofu na wakoma kwa idhini ya Mungu. Kwa kweli Muislamu hawi Muislamu kama hamuwamini Yesu!"
AJABU NA KWELI
Zaidi ya asilimiya tisini (90%) ya watu walioshuhudiya mdahalo huo kwa vyovyote watakuwa wameufurahiya lakini kwa mashaka- mashaka hivyo hivyo! Pengine labda hawakuamini masikio yao. Huwenda watakuwa wamedhani kuwa labda Waislamu walikuwa wanajaribu kuwakoga tu Wakristo- (they were playing to the gallery) Kwamba walikuwa wanajaribu kujipendekeza kwa wananchi wenzao Wakristo (they were trying to curry favour with their fellow Christian countrymen); kwamba kama wao Waislamu wangesema maneno mawili-matatu matamu kuhusu Yesu basi Wakristo nao, katika majibu yao, wangeweza kusema maneno mazuri kuhusu Muhammad (Amani na Rehema za Mungu ziwe juu ya Waja wake wote wema-Musa, Yesu, Muhammad na wengineo); sawa na kusema kwamba, "mimi nakukuna mgongo na wewe nikune mgongoni- I scratch your back and you scratch mine- huu ungekuwa ubazazi au unafiki kabisa!
CHUKI ILIVYOPANDIKIZWA
Hatuwezi kuwalaumu Wakristo kwa shaka waliyonayo. Kwani wamepandikizwa kasumba hiyo kwa karne nyingi. Wamepandikizwa fikra mbaya sana juu ya Muhammad (saw) na dini yake. Ona jinsi Thomas Carlyle alivyozungumza kwa maneno ya busara juu Wakristo wenziwe zaidi ya miyaka miya moja na hamsini iliyopita- "MANENO CHUNGU TELE YA URONGO AMBAYO USHABIKI WENYE NIYA NJEMA UMEMMIMINIYA MTU HUYU (Muhammad) YANATUFEDHEHESHA SISI WENYEWE TU." Na sisi Waislamu tunabeba nusu ya mzigo wa lawama kwa ujinga wa kushangaza walionao Wakristo 1,200,000,000 waliopo ulimwenguni. Hatujafanya jitihada kubwa kuondowa utando (uliowafunika macho wenzetu).
BAHARI YA UKRISTO
Afrika Kusini ni bahari ya Ukristo. Ikiwa Libya inajivuniya idadi kubwa ya Waislamu barani Afrika, basi Jamhuri ya Afrika Kusini nayo itakuwa na haki ya kujivuniya idadi kubwa ya Wakristo. Katika bahari hii ya ukristo (katika Jamhuri ya watu wa Afrika Kusini-R.S.A), Waislamu ni asilimiya mbili tu (2%) ya watu wote. Waislamu huku hatuna nguvu ya kura. Kitakwimu, hatuhesabiki kwa chochote; hatuhesabiki kisiyasa, hatuhesabiki kiuchumi, mzungu mmoja tu kama Oppenheimer, anaweza kununuwa vitu vyetu vyote kwa jumla (kwa mkupuo mmoja tu) na kumaliza maduka na akiba. Kwa hiyo kama tungejikumbata tu na kujipendekeza basi tungeweza kuachwa tu kama tulivyo. Lakini hapana! Lazima tuhubiri yale anayoyataka Mola wetu; Lazima tuutangaze ukweli hadharani, tupende, tusipende. Kwa maneno ya Yesu (as): "Tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru." (Yohana Mtakatifu 8:32).
YESU NDANI YA QUR'AN
WAKRISTO HAWALIJUWI HILI
Mkristo hajuwi kuwa ile imani ya dhati ya wema ambayo Muislamu anaionesha kwa Yesu na mama yake inatokana na msingi mkuu wa imani yake-Qur'an Tukufu. Mkristo hajuwi kuwa Muislamu halitaji jina la Yesu-Isa bila kuongeza duwa ya amani juu yake-kwa Kiarabu, Isa alai-hiss-salaam- Kwa Kiingereza-Jesus, peace be upon him (Kwa Kiswahili-Yesu/Isa, amani iwe juu yake). Kila mara Muislamu anapolitaja jina Isa bila maneno haya ya kumtakiya amani, basi huonekana mtovu wa Akhlaq (Adabu). Mkristo hajuwi kuwa katika Qur'an Tukufu Yesu (as) anatajwa kwa jina mara nyingi zaidi kuliko jina (Muhammad). ( utajo wa jina Isa ndani ya Qur'an unauzidi mara tano (5x) utajo wa jina Muhammad) Kwa idadi halisi-Yesu anatajwa mara ishini na tano wakati Muhammad anatajwa mara tano. Kwa mfano: ...."na Tukampa ISA, mwana wa Mariyamu ( Yesu mtoto wa Maria) hoja zilizo wazi wazi, na Tukamtia nguvu kwa Roho mtakatifu".(Qur'an 2:87).
"Ewe Mariyamu! Mwenyezi Mungu anakupa khabari njema za neno litokalo kwake. Jina lake ni Masihi, ISA mwana wa Maryamu..." Qur'an (3:45) ...Masihi ISA bin Maryamu ni Mtume wa MwenyeziMungu....(Qur'an 4:171) ..."Na Tukawafuwatishia (Mitume hao) ISA bin Maryamu.." (Qur'an 5:46). "Na Zakaria na Yahya na ISA na Ilyas, Wote (walikuawa) ni miongoni mwa watu wema. (6:85).
YESU NA MAJINA YAKE
Ingawaje Yesu anatajwa kwa jina mara ishirini ndani ya Qur'an Tukufu, piya kiheshima anaitwa "Ibni Maryam"- Mwana wa Maryam; Masihi-Messiah (kwa Kiebrania)-ambalo hutafsiriwa kama Kristo "Abd-ullah"- mja wa Allah; "Rasul-ullah"-Mtume wa Allah. Anaelezewa kama "neno la Mungu" , "kama Roho wa Mungu" "ishara ya Mungu", na sifa nyingine kemkem za utukuzo zilizotolewa katika zaidi ya sura kumi na tano. Qur'an inampa heshima Mtume huyu mkubwa wa Mungu, na Waislamu hawajafanya kinyume na hivyo kwa miyaka elfu moja na miya nne. Hakuna hata neno moja la dharau katika Qur'an yote ambalo wale Wakristo wenye hiyana zaidi wanaweza kulitafutiya dosari.
"ISA" ALIVYOTIWA KATIKA KILATINI
Qur'an Tukufu inamtaja Yesu kama "Isa", na hili ndilo jina lililotumika mara nyingi zaidi kuliko jina lake jingine kwani hili ndilo jina lake la kuzaliwa. Kwa jina sahihi (la Kiarabu) ni Isa au (kwa Kiebrania) "Esau" ambalo Mataifa ya Kikristo ya Magharibi yakaligeuza kwa Kilatini kuwa Jesus. Si "J" wala "s" ya pili katika jina Jesus inayoonekana katika lugha ya asili.-herufi hizo hazimo katika lugha za Kisemiti. Neno jepesi tu E S A U-ndilo jina mashuhuri la Kiyahudi lililotumika zaidi ya mara sitini katika kitabu cha kwanza kabisa cha Biblia katika sura iitwayo 'Genesis-Mwanzo. ('Jesus' mbona wako wengi?)
Mwanahistoriya wa Kiyahudi Josephus anawataja'Jesus' ishirini na tano katika kitabu chake- "Book of Antiquities" Agano jipya linamzungumziya "Bar-Jesus" ( Bar-Yesu)- mchawi, nabii wa uwongo (Matendo: 13:6). Linamtaja piya "Jesus-Jestus"-Yesu-Yusto (Yesu aitwaye Yusto) (Wakolosai:4:11). Hawa ni AkinaJesus wengine kabisa tofauti na Yesu mwana wa Maryamu. Kugeuza Esau kuwa (J)esu(s)-Jesus-kunaliacha Esau liwe jina la mtu mmoja pekee. Jina hili la peke yake (?) liliyanza kuacha kutumika miongoni mwa Wayahudi na Wakristo kuanziya karne ya pili baada ya Kristo. Kwa wayahudi jina hili lilifutika kwa sababu lilikuja kuwa jina la kishenzi (jina la utovu wa heshima)-jina la mtu aliyekufuru katika uyahudi. Na kwa Wakristo jina hili lilifutika kwa sababu lilikuwa jina la mungu wao (?)-mungu aliyejitokeza kwa umbile la kibinadamu. Lakini Muislamu hasiti hata kidogo kumpa mwanawe jina hili-Eesa (Isa)-kwa sababu ni jina la heshima, jina la mja mwema wa Mola Muumba.
MAMA NA MWANA
MARIA ANAVYOHESHIMIWA KATIKA UISLAMU
Mada ya pili ya "uzawa wa Yesu"-inaelezewa katika sura mbili- Sura ya 3 na Sura ya 19 (za Qur'an). Tunapousoma uzawa wa Yesu kuanziya mwanzo kabisa tunakutana na kisa cha Mariamu (habari ya Mariya) na hadhi kubwa aliyonayo katika Uislamu: NA KUMBUKA MALAIKA WALIPOSEMA: "EWE MARIAM! KWA HAKIKA MWENYEZIMUNGU AMEKUCHAGUA NA KUKUTAKASA NA KUKUTUKUZA KULIKO WAMAWAKE WA ULIMWENGU (WOTE)." (3:42) "Amekuchagua, kukutakasa na kukutukuza kuliko wanawake wa ulimwengu wote" Heshima hii Maria hakupewa katika Biblia, kitabu cha Wakristo! Aya inaendeleya: "EWE MARYAM! MNYENYEKEE MOLA WAKO NA USUJUDU NA UINAME (USALI) PAMOJA NA WAINAMAO" (3:43).
UFUNUWO WA MUNGU
Ni nini asili ya ujumbe huu mzuri na wa utukuzo ambao, ukisomwa katika lugha yake ya asili ya Kiarabu, hugusa hisiya za mtu hata kumtowa machozi? Aya ya 44 inafafanuwa hapa chini:- HIZI NI KHABARI ZA GHAIBU TUNAZOKUFUNULIA; NAWE HUKUWA NAO WALIPOKUWA WAKITUPA KALAMU ZAO NDANI YA MAJI (KWA KURA, WAJUWE) NANI WAO ATAMLEA MARYAM, NA HUKUWA NAO WALIPOKUWA WANASHINDANA.
KUZALIWA KWA MARYAM
Kisa kinasema hivi, Bibi yake Yesu, Hanna hadi wakati huwo alikuwa mgumba. Akaweka nadhiri kwa Mungu: Kwamba kama atamjaliya kupata mtoto basi atamtowa mtoto huyo hekaluni kwa ajili ya kumtumikiya Yeye (Mungu).
KINYUME NA MATAZAMIYO
Mungu akaipokeya Duwa yake na Maryamu akazaliwa. Ikawa kinyume na matarajiyo yake. Yeye alikuwa anataka kupata mtoto wa kiume lakini badala yake akajifunguwa mtoto wa kike; na mwanamke si kama Mwanaume kwa yale aliyoyawaziya kichwani mwake. Alikuwa na nini basi cha kufanya? Maanake alikuwa ameweka nadhiri kwa Mungu. Akamsubiriya Maryam awe mkubwa kiyasi cha kuweza kujitunza mwenyewe. Alipotimiza makamo hayo, Hanna akampeleka binti yake mpendwa hekaluni kumkabidhisha huko kwa ajili ya utumishi katika hekalu. Kila Kuhani akagombeya awe Baba mlezi wa mtoto huyo wa kupendaza. Wakapiga kura kwa mishale kama vile kurusha Sarafu (kurusha shilingi) - Kichwa au samaki/ mzee au Mwenge? Hatimaye msichana Maryam akaangukiya kwa mzee Zakariya-lakini bila kuzozana.
CHANZO CHA UJUMBE WAKE
Hiyo ndiyo habari ya Maryamu. Lakini huyu Muhammad (saw) alipata wapi yeye habari hii? Alikuwa hajuwi kusoma wala kuwandika (Ummi). Katika aya hapo juu Muhammad anakaririshwa na MwenyeziMungu kulijibu swali hili kwa kusema kuwa: "HIZI NI KHABARI ZA GHAIBU TUNAZOKUFUNULIYA" (HUKUWEPO WEWE WAKATI WALIPOKUWA WANAPIGA KURA!). Lakini bado mtu m-bishi anasema "Hapana!" "Haya kayatunga Muhammad mwenyewe. Alinakili aya zake kutoka kwa Wayahudi na Wakristo. Aliigiziya ( he plagiarised). Aligushi".
Sisi waislamu tunajuwa fika na tunaamini kama tunavyoamini kuwa Qur'an yote ni NENO halisi la Mungu. Lakini pamoja na hivyo, ngoja kidogo tutowe fursa ya mjadala na maaduwi wa Muhammad kwa kukubali kuwa; haya, sawa Muhammad aliandika Kitabu hiki! Labda hapo sasa twaweza kutarajiya kupata ushirikiyano fulani kutoka kwa yule asiyeamini. Muulize, "je una mashaka yoyote katika kukubaliyana kuwa Muhammad (saw) alikuwa Mwarabu?" Ni juha kalulu tu ( only an opinionated fool) atakayesita kukubali hivyo. Kwa hali hiyo hakuna maana ya kufanya mjadala naye. Katisha mazungumzo. Funga kitabu!
Akiwa ni mtu mwenye akili timamu tuendelee kujadiliyana naye hivi: Mwarabu huyu kwanza kabisa alikuwa akiwahubiriya Warabu wengine. Hakuwa akizungumza na Waislamu wa India, China au Nigeria. Alikuwa akizungumza na watu wa kwao- Waarabu. Ima walikubaliyana naye au la, yeye alikuwa akiwaambiya kwa maneno yenye utukuzo mkubwa ambayo yalikuwa na mchomo ndani ya nyoyo na vichwa vya wasikizaji wake kwamba MARIA MAMAKE YESU, MWANAMAMA WA KIYAHUDI ndiye aliyechaguliwa na kutukuzwa kuliko wanawake wote ulimwenguni.
Si mamake mzazi Muhammad, si Mkewe, si bintiye wala si mwanamke yoyote wa Kiarabu aliyepewa hadhi hiyo, bali mama huyo wa Kiyahudi tu. Nani anayeweza kusema hivi? Kwani, kwa kila mtu, mama yake mzazi au mke wake au binti yake ndiye anayepewa kipaumbele kabla ya wanawake wengine (watubaki).
Kwa nini basi Muhammad ambaye ni Mtume wa Waislamu aende akamtukuze mwanamke kutoka upande wa wapinzani wake! Tena basi Myahudi anayetokeya katika jamii ambayo ilikuwa ikiwadharau watu wake kwa maelfu ya miyaka ? Na bado mpaka leo jamii hiyo (ya Wayahudi) inawatazama kwa dharau Warabu wenziwe.
SARA NA HAJRA
Wayahudi wamepata siyasa ya ubaguzi wa kujiona wao bora kutokana na Biblia yao ambamo wanaambiwa kuwa baba yao Abraham alikuwa na wake wawili Sara na Hajra (soma kitabu Pros and Cons of Israel ambamo mwandishi anathibitisha kwa hoja kuwa Hajra alikuwa binti-mfalme (Princess) wa Misri na si kijakazi au mwanamke mtumwa). Wayahudi wanasema kuwa wao ni watoto wa Ibrahim kupitiya kwa Sara, mke wa halali; kwamba wenzao Warabu wametokana na Hajra, "Mjakazi" (Suriya, mwanamke aliyekuwa utumwani), hivyo Warabu ni kizazi dhalili (an inferior breed). Hivi yupo mtu yeyote atakayefafanuwa kioja hiki: kwamba kama Muhammad ndiye Mtunzi wa Qur'an, kwa vipi alihiyari kumpa Myahudi heshima kubwa namna hiyo? Jawabu ni jepesi tu-MUHAMMAD HAKUWA NA UHURU WA HIYARI KUAMUWA CHOCHOTE JUU YA QUR'AN- hakuwa na haki ya kusema kwa matakwa yake; WALA HASEMI KWA MATAMANIO (YA NAFSI YAKE). HAYAKUWA HAYA ANAYOYASEMA ILA NI WAHYI (UFUNUWO) ULIOFUNULIWA (KWAKE) (Qur'an 53:3-4).
SURA MARYAMU
Ndani ya Qur'an kuna Sura inayoitwa Surat Maryam (Sura Maria), hii ni Sura ya 19, imeitwa hivi kwa heshima ya Maryam, MAMAKE YESU (as). Hapa piya tena heshima hii huikuti katika Kitabu cha Wakristo, Biblia. KATIKA VITABU 66 VYA WAPROTESTANTI NA 73 VYA WAROMA (WAKATOLIKI) HAKUNA HATA KITABU KIMOJA KINACHOITWA MARIA AU YESU.
Utavikuta tu vitabu vyenye majina ya akina Mathayo, Marko, Luka, Yohana, Petro, Paulo lakini hakuna hata kimoja chenye jina la Yesu au Maria! Kama kweli Muhammad angelikuwa Mtunzi wa Qur'an basi, pamoja na MARYAMU, na yeye asingeshindwa kutiya jina la mamake mzazi AMINA, Mkewe aliyempenda (na aliyesaidiya dini yake) KHADIJA au binti yake mpendwa FATIMA. Lakini Hapana! Hapana! Hilo halikuwezekana. Qur'an haikuwa kazi ya Muhammad!
HABARI NJEMA
(KUMBUKENI) WALIPOSEMA MALAIKA: "EWE MARYAMU MWENYEZIMUNGU ANAKUPA HABARI NJEMA ZA NENO LITOKALO KWAKE. JINA LAKE NI MASIH, ISA MWANA WA MARYAMU, MWENYE HESHIMA KATIKA DUNIYA NA AKHERA, NA NI MIONGONI MWA WALIOPELEKWA MBELE (WALIOKARIBU ZAIDI) NA MWENYEZIMUNGU" (Qur'an 3:45).
Hii siyo Kuwa karibu zaidi na Mungu kimwili au kijiografiya bali kiroho. Hebu ilinganishe na- "Basi Bwana Yesu akaketi mkono wa Kuume wa Mungu". (marko 16:19). Umati mkubwa wa Wakristo umeilewa visivyo aya hii na aya nyinginezo za Biblia. Wao wanachukuliya kuwa Baba (Mungu) kakaa juu ya kiti cha Enzi na "Mwanawe"- Yesu kakaa upande wa kuliya. Unawezaje kuijenga akilini picha hii?
Kama ukiweza kuijenga picha hiyo akilini basi wewe umekosa elimu elimu sahihi juu ya Mungu. Mungu hayuko kama Fadha Krismasi (babu madevu). Yeye ni Dhati ya roho, yuko nje ya upeo wa akili ya binadamu, yutofauti kabisa na taswira yoyote inayojengwa kichwani mwa mtu. Ni kweli yupo, na yupo katika uhalisiya lakini hafanani na chochote tunachokifikiriya au kukihisi. Katika lugha za mashariki "mkono wa kuume" maana yake ni mahala pa heshima ambapo Qur'an inapaelezeya kwa uzuri zaidi kama ni upande wa wale waliokaribu zaidi na MwenyeziMungu.
Aya hapo juu inathibitisha kuwa Yesu ndiye MASIHI, kwamba yeye ni NENO ambalo Mungu alilitowa kwa Maryamu. Bado tena Mkristo anayapa maneno haya maana isiyoendana nayo. Ati wao wanaliowanisha neno Kristo (Masihi) na dhana ya Mungu aliyejitokeza kwa umbile la kibinadamu; na neno la Mungu kuwa ndio Mungu mwenyewe.
KRISTO SIYO JINA LA MTU
Neno KRISTO linatokana na neno Messiah la Kiebrania. Kwa Kiarabu ni Masih. Shina la neno ni m-a-s-a-h-a, maana yake ni kuchuwa, kusinga, kupaka. Makuhani na wafalme walisingwa (walipakwa mafuta) kabla ya kusimikwa katika katika nyadhifa zao. Lakini kwa haiba yake ya tafsiri ya Kigiriki, neno hili linaonekana kuwa mahususi, likiswihi kwa Yesu tu. Mkristo ana mazoweya ya kubadilisha metali kuwa dhahabu ing'arayo. Alichoweza kukifanya ni kuyabadili kabisa maneno katika lugha yake kama vile "cephus" kuwa Peter, "messiah" kuwa Christ. Anawezaje kufanya hivyo? Rahisi sana. Neno MASSIAH la Kiebrania, kwa Kiingereza, maana yake ni Anointed (aliyepakwa, aliyetiwa au aliyesingwa mafuta). Neno la Kigiriki la kutafsiri neno hilo ni "christos". Inyofowe 'os' katika neno christos, hapo unabakiwa na christ. Sasa geuza "c" ndogo kuwa "C" kubwa, yebo! Hapo sasa keshaunda jina jingine (?)!
Christos maana yake ni ALIYETIWA (ALIYEPAKWA) MAFUTA, na mpakwa mafuta, kwa maana yake ya kidini ni MTEULE (ALIYETEULIWA). Yesu (as), baada ya ubatizo wake kwa Yohana, aliteuliwa kuwa nabii wa Mungu. Kila nabii wa Mungu huteuliwa hivyo (anointed or appointed). Biblia imejaa "wapakwa mafuta" kibao. Yaani kwa lugha asiliya ya Kiebrania-waliofanywa kuwa "messiah". Hebu tubakiye na tafsiri hiyo ya Kiingereza- "anointed."
Siyo tu manabii makuhani na wafalme waliotiwa mafuta (christos-ed- waliofanywa kristo) bali pembe, kerubi na nguzo nazo piya zilitiwa mafuta (zilifanywa kristo) Kama Kuhani aliyetiwa mafuta akifanya dhambi... (mambo ya walawi 4:3 Kisha Musa akatwaa hayo mafuta matakatifu ya kutiya, akatiya maskani na vyote vilivyokuwamo...(mambo ya walawi 8:10) Bwana...........Na kuitukuza pembe ya masihi wake (1Samweli 2:10) Haya ndiyo Bwana amwambiayo Koreshi, masihi wake...(Isaya 45:1) Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta.... (Ezekieli 28:14) Kuna zaidi ya mifano miya kama hiyo katika Biblia. Kila ukutanapo na neno anointed katika lugha ya Kiingereza (iliyotumika kutafsiri Biblia kwa Kiswahili), uchukuliye kuwa neno hilo ni christos kwa tafsiri ya Kigiriki. Na ukilichukuwa neno christ ambalo wakristo wameliunda, utakuwa na Christ Cherub (Kerubi Kristo), Christ Cyrus (Koreshi Kristo), Christ Priest (Kuhani Kristo), Christ Pillar (Nguzo Kristo) n.k.
BAADHI YA MAJINASIFA YA KIPEKEE
Ingawaje lila Nabii ni Masihi wa Mungu, jina HILI Masihi au Messiah au Kristo kwa tafsiri yake, ni jinasifa linalotumika kwa Yesu mwana wa Maryamu peke yake katika Uislamu na Ukristo. Hili si jambo geni katika dini Kuna majina ya sifa makubwa ambayo yanaweza kutumika kwa zaidi ya nabii mmoja lakini bado katika matumizi yakawa mahususi zaidi kwa mmoja: kama vile "Rasul-lullah" maana yake ni Mtume wa Mungu, jina hili la cheo piya limetumika kwa Musa (19:51) na Isa (61:6) katika Qur'an. Lakini bado kwa Waislamu, jina hili la sifa ni mashuhuri zaidi kwa Muhammad (saw) Kwa kweli kila nabii ni RAFIKI WA MUNGU, lakini neno la kiarabu lilosawa na hilo :"Khalil-lullah" hunasibishwa na Ibrahim tu. Hii haina maana kuwa wengine si marafiki wa Mungu.
"Kalimul-lah" (aliyesemezwa na Mungu) halitumiki kwa mwingine ila Musa. Lakini sisi tunaamini kuwa Mungu alizungumza na Mitume wake wote wakiwemo Yesu na Muhammad (Amani na Rehema za Mungu ziwe juu yao). Hivyo basi kunasibisha sifa fulani na watu fulani hakuwafanyi wao kuwa watu tofauti. Tunawapa heshima kwa maneno tu tofauti. Kwa habari njema zilitolewa (kwa mujibu wa aya ya 45 iliyonukuliwa hapo juu), Maryamu aliambiwa kuwa mtoto wake atakayezaliwa ataitwa Isa, kwamba yeye ni Masihi, 'Neno' kutoka kwa Mungu na kwamba..
ATAZUNGUMZA NA WATU KATIKA UTOTO NA KATIKA UTUUZIMA NA (ATAKUWA) KATIKA WATU WEMA" (Qur'an 3:46). Bishara inatimiya baada ya muda mfupi sana kama tunavyoona katika Sura Maryamu: AKENDA NAYE KWA JAMAA ZAKE AMEM-BEBA. WAKASEMA: "EWE MARYAMU! HAKIKA UMELETA KITU CHA AJABU! UMEZAA (UMEZAA BILA YA KUOLEWA NDOA YA SHARIA!). EWE DADA YAKE HARUNI! BABA YAKO HAKUWA MTU M-BAYA WALA MAMA YAKO HAKUWA HASHARATI" (Qur'an 19:27-28)
WAYAHUDI WAPIGWA NA MSHANGAO
Hapo hakuna Yusufu, fundi seremala. Katika mazingira ya upweke, Maryamu alijitenga na alikwenda mbali upande wa Mashariki (Qur'an 19:16). Baada ya kujifunguwa mtoto akarejeya. "Mshangao wa watu ulikuwa mkubwa kupindukiya. Kwa vyovyote vile walikuwa walikuwa tayari wakimfikiriya vibaya sana kwani alipoteyana na nduguze kwa kitambo. Lakini sasa anajitokeza bila kuona haya akiwa amebeba kichanga mikononi! Ikaonekana ameiyaibisha nyumba ya Haruni iliyokuwa chemchem ya ukuhani!
DADA YAKE HARUNI:
hapa Mryamu anakumbushwa jinsi ukoo wao ulivyokuwa bora na maadili bora ya aina yake waliyokuwa nayo wazazi wake. Waksema imekuwaje tena yeye kaanguka na kuchafuwa jina la wazazi wake! Je hapo Maryamu angeweza kufanya nini? Angejieleza vipi aeleweke? Je watu hao wakiwa katika hali ya kumzonga kwa maneno ya lawama, wangeweza kweli kuyakubali maelezo yake? Alichoweza kukifanya ni kumuashiriya mtoto ambaye, yeye alijuwa, si mtoto wa kawaida. Hapo ndipo mtoto alipomtowa yeye lawamani. Kimiujiza mtoto huyo akamteteya mama yake na akaihubiriya kadamnasi ya makafiri. Hii ni sherehe ya A. Yusuf Ali, tanbihi 2480-2482 ukurasa 773 wa Tafsiri yake ya Qur'an.
(MARYAMU) AKAWAASHIRIYA KWAKE (YULE MTOTO WAMUULIZE). WAKASEMA: "TUZUNGUMZEJE NA ALIYE BADO KITANDANI?" (YULE MTOTO) AKASEMA: HAKIKA MIMI NI MJA WA MWENYEZIMUNGU, AMENIPA KITABU NA AMENIFANYA NABII, NA AMENIFANYA MBARIKIWA POPOTE NILIPO. NA AMENIUSIA SALA NA ZAKA MAADAM NI HAI. NA (AMENIUSIA) KUMFANYIA MEMA MAMA YANGU: WALA HAKUNIFANYA NIWE JEURI MUOVU. NA AMANI IKO JUU YANGU SIKU NILIYOZALIWA NA SIKU NITAKAYOKUFA NA SIKU NITAKAYOFUFULIWA KUWA HAI (Qur'an 19:29-33).
MWISHO