UIMAM
BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM
UIMAM
Ndugu Waislaam, napenda kuwaamkieni kwa maamkizi safi na bora kabisa kuliko maakizi yoyote yale, nayo ni :Assalaam Alaikum Warahmatullah Wabarakaatuh. Leo hii nimeona ni bora zaidi tukiuzungumzia Uimam.lakini kwanza kabla ya yote tufaidike na utangulizi huu ili baadae utusaidie kuelewa maana ya uimam na faida zake.
Utangulizi:
Bila shaka kila mtu anatambua kuwa serikali iliyoundwa nchini kwa lengo la kuyashughulikia masuala ya wananchi haiwezi kujiongoza yenyewe. Iwapo watu wanaofaa na wenye ujuzi hawatajitokeza kutekeleza shughuli zake basi bila shaka serikali hiyo haitadumu wala kuwahudumia wananchi.
Hali yo pia inahusika na taasisi nyinginezo katika jamii ya Mwanadamu kama vile taasisi za kiutamaduni,za kiuchumi,za kielimu na kadhalika.Daima taasisi kama hizi huwategemea wakurugenzi wanaofaa na waaminifu,la sivyo zitaanguka au huanguka na kufungwa katika kipindi.Hii ni hakika iliyokuwa wazi ambayo inaweza kuonekana hata kwa mtazamo wa kaiwada tu.Uzoefu mwingi pia unaelezea ukweli na hakika hii.Hivyo si lazima na haihitaji mtu uwe na maelimu mengi sana ili kutambua hakika hii na ukweli huu!
Ikiwa hili litathibiti,basi kutakuwa hakuna shaka kwamba taasisi ya Dini ya Kiislaam ambayo naweza kusema ni taasisi kubwa sana duniani, nayo hufuata mfumo huu.Taasisi hii ya Dini ya Kiislaam huwategemea wasimamizi na viongozi ili iendelee kudumu.Daima huwatafuta watu wanaofaa kwa lengo la kuwapa mafundisho ya Kiislaam na kutekeleza sheria katika jamii ya Kiislaam na pia kutoacha nafasi au fursa yoyote ya uvunjaji sheria katika kuulinda Uislaam.
Usimamizi wa masuala ya Kidini katika Jamii ya Kiislaam unaitwa Uimam.Na Msimamizi au Kiongozi huitwa Imam. Washia (Wale ambao watu wakitofautiana kuhusu Mtume (s.a.w) huchukua kauli ya Imam Ali (a.s), na wakitofautiana kuhusu Imam Ali (a.s) huchukua kauli ya Imam Jaafar bin Muhammad -Al-swadiq- (a.s) ) huamini kuwa baada ya kifo cha Mtume (s.a.w) ni lazima Imam achaguliwe na Mwenyeezi Mungu (s.w) ili awe msimamizi na mlinzi wa mafundisho ya sheria za Kiislaam pamoja na kuwaongoza watu katika njia iliyonyooka.
Ikiwa mtu atafanya uchunguzi wa kina katika Mafundisho ya Kiislaam,na kutoa uamuzi wa kwa msingi wa uadilifu,akaweka taasubi na matamanio ya nafsi yake pembeni ili ahukumu kwa haki,basi ataona kuwa Uimam ni mojawapo ya misingi isiyokuwa na shaka katika dini ya Kiislaam na kuwa Mwenyeezi Mungu (s.w) anazungumzia suala hili katika aya za Qur'an Tukufu na kutambulisha Taasisi ya dini ya Kiislaam.
Mwisho.
Sehemu ya pili tutazungumzia dalili ya Uimam.
Usikose kufuatilia sehemu hii ili ujue ni dalili zipi
Zinazothibitisha Uimam.