SAYYIDAT ZAINABUL-KUBRA (A.S).
BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM:
SAYYIDAT ZAINABUL-KUBRA (A.S)
SAYYIDAT ZAINAB NI NANI?
Sayyidat Zainab ni mmoja kati ya watoto wa Imam Ali (a.s) na Fatima Az-zahraa (a.s).Imam Ali (a.s) alikuwa na watoto ishirini na saba (27) wakiume na wakike.Watoto hao mama zao ni tofauti.Mke wa kwanza kabisa wa Imam Ali (a.s) ambaye kaozeshwa na Mtume (s.a.w) ni Fatima Az-zaharaa (a.s) ambaye baba yake ni Mtume Muhammad (s.a.w). Fatima (a.s) baada ya kuolewa na Imam Ali (a.s),Mwenyeezi Mungu (s.w) aliwaruzuku watoto wanne,wawili wa kiume na wawili wa kike,watoto hao ni hawa hapa wafuatao:
1-Hasan (a.s)
2-Husein (a.s)
3-Sayyidat Zaibul-Kubra
4-Sayyidat Zainabus-Sughra aliyekuwa akiitwa -kwa laqab ya- {Ummul-kulthuum}
Hawa wote wanne mama yao ni Fatimatul Batuul (a.s) Mbora wa wanawake wote wa ulimwengu mzima ambaye ni bint ya Mbora wa Mitume (s.a.w). Leo hii tunamzungumzia walau kwa ufupi Sayyidat Zainabul-Kubra (a.s) ambaye ni mtoto wa tatu kwa Imam Ali (a.s) na Fatima (a.s).
KUZALIWA KWAKE (A.S).
Kuzaliwa kwake ilikuwa ni mwaka wa tano,mwezi wa tano ambao ni(Jamaadil-Awwal) baada ya Hijra ya Mtume (s.a.w) kutoka Makka kwenda Madina ambapo aliishi katika mji huu aliohamia wenye nuru (Madina) miaka kumi akitangaza dini tukufu ya
Mwenyeezi Mungu (s.w) ambayo ni dini ya Kiislaam.
NASABA YAKE (A.S).
Hakuna Nasaba katika dunia ya Kiislaam na dunia nyingine yoyote bora zaidi na yenye utukufu wa daraja ya juu kama Nasaba ya Sayyidat Zainabul-Kubra (a.s).Hakika Zainab huyu amegawanyika kutoka katika mti mkubwa wa Unabii na Uimam.Na alikutana na utukufu wote na adhama kubwa kutoka katika mti huu wa Unabii na Uimam.Sayyidat Zainab (a.s) ni tawi safi na takatifu kutoka kwa Mtume Muhammad (s.a.w) na kutoka kwa Imam Ali (a.s).Na hawa wawili, yaani Mtume (s.a.w) na Imam Ali (a.s); ndio viumbe bora katika viumbe alivyoviumba Mwenyeezi Mungu (s.w) katika wanaadamu.
Hivyo Mwenyeezi Mungu (s.w) Alimbariki Sayyidat Zainab (a.s) ukoo huu (Nasaba hii) mzuri wenye kila aina ya sifa nzuri,famila ambayo imekuwa na utukufu na daraja ya juu kabisa ambapo Mwenyeezi Mungu (s.w) kupitia familia hiyo aliwapa nguvu na kuwaimarisha Waarabu na Uislaam na akaifanya (familia hiyo tukufu) kuwa asili au chimbuko au chemchem ya Maarifa,Elimu na ufunuo (IL-HAAM) kwa Waislaam katika kipindi chote cha kihistoria.Ni wazi kwamba Familia tukufu ya Ali bin Abi Twalib (a.s) ndio familia ya pekee ambayo historia imeitambua kwa Jihad yake na harakati yake,na jitihada yake,na bidii yake,na malezi yake,na fikra yake kuhusiana na haki za watu pamoja na hukumu,na ushujaa wake wa kupinga dhulma na Uovu.Hakuna katika familia zote za ulimwenguni popote pale ardhini kama familia ya Imam Ali (a.s) katika kupambana na kuwahami wenye kudhulumiwa na wenye kuteswa,kuadhibiwa na kusumbuliwa.Na wengi katika familia hii tukufu,wamekufa mashahidi kwa ajili ya kutetea uhuru wa Mwanaadamu na utukufu wake. Kwa ufupi huu ndio ukoo na nasaba tukufu ambayo ndio asili ya Sayyidat Zainabul-kubra (a.s).
BABU YAKE
Babu yake na Sayyidat Zainabul-Kubra (a.s) ni Mbora wa viumbe, naye si mwingine bali ni:Mtume Muhammad (s.a.w) ambaye amemwaga chemchem za elimu na hekima katika ardhi,na akaasisi vibao vya kuonyesha njia (yaani aliweka utaratibu na kanuni ambazo ni njia ya) kuelekea katika ustaarabu,adabu,malezi,utamaduni,uungwana na elimu; na akajenga Jamii bora ambayo inaongozwa na uadilifu,kanuni na sheria;na akaondoa na kufutilia mbali itikadi mbovu za kijahiliyya pamoja na desturi na tabia za zama hizo.Pia akayavunjilia mbali na kuyasagasaga masanamu yalikuwa yakiabudiwa katika zama za Kijaahiliyya.Kwa ufupi huyu ndiye Babu yake na Sayyidat Zainabul-Kubra (a.s) ambaye Mwenyeezi (s.w) amesema katika suura ya 21 (Suuratul Anbiyaa), aya ya 107 kwamba:
*Nasi hatukukutuma ila uwe ni rehema kwa walimwengu wote* Kwa kauli hii tukufu ya Mwenyeezi Mungu (s.w), Babu yake na Zainabul-Kubra (s.a.w) ni rehema kwa watu wote ulimwenguni wenye kutofautiana lugha zao,na rangi zao.
BIBI YAKE
Bibi yake na Sayyidat Zaibaul-Kubra ni Ummul-muuminina,Mbora wa wanawake wa Mtume (s.a.w),naye si mwingine bali ni:Khadijatul-Kubra ambaye aliunusuru Uislaam pindi ulipokuwa katika siku za huzuni,majonzi,masikitiko na ukiwa.Na alifanya jihadi kubwa katika njia ya Mwenyeezi Mungu (s.w),na alitoa chochote kile alichokimiliki katika kuuhudumia na kuunusuru Uislaam.Na alikuwa ni Tajiri mkubwa kuliko Maqurayshi wote wa Makka.Lakini mpaka anakufa hakuwa akimiliki chochote katika hazina ya mali zake ispokuwa kirago (yaani mkeka au jamvi) kilichochakaa.!!Mali zake zote alizotoa ili kuuhudumia na kuunusuru Uislaam.Mtume (s.a.w) alikuwa akimkumbuka sana Khadija (a.s) muda wote wa maisha yake yote aliyoishi baada ya kufariki kwake (a.s) na alikuwa akimuombea rehema kwa Mwenyeezi Mungu (s.w) na alikuwa kila akichinja Mbuzi au Kondoo,anatuma ile sehemu ya nyama nzuri zaidi kwa marafiki zake na Khadija (a.s) ili kuhifadhi ada ya mkewe Khadija (a.s) ambaye pindi alipokuwa hai hivyo hivyo ndivyo alivyokuwa akifanya.Kwa ufupi huyu ndiye Bibi yake na Sayyidat Zainabul-Kubra (a.s).
MAMA YAKE
Mama yake na Sayyidat Zainabul-Kubra (a.s) ni Batuul, Atw-twaahira,Fatimatuz-Zahraa (a.s),Mbora wa wanawake wote wa ulimwenguni katika fadhila zake,utakatifu wake,na twahara yake kutokana na uchafu wa kimaada na kimaanawi kama vile kutenda dhambi,na Fatima huyu ni sehemu ya nyama ya Mtume (s.a.w) na ni kipenzi zaidi wa wanae wa kike na wa kiume kwake (s.a.w).Mtume (s.a.w) mapenzi yake kwa Fatima yalifikia daraja ya mwisho kabisa kiasi kwamba pindi alipokuwa akitaka kusafiri kwenda sehemu yoyote ile,mtu wa mwisho aliyekuwa akimuaga alikuwa ni Fatima (a.s) ili sura yake ibaki ikiwa ni yenye kujitokeza mbele yake popote pale atakapokuwa katika safari yake.
Na hivyo hivyo ndivyo ilivyokuwa pindi alipokuwa akirudi (s.a.w) kutoka katika safari yake,mtu wa kwanza ambaye Mtume (s.a.w) alikuwa akielekea kwake alikuwa ni Fatima(a.s).Hii ni kwa sababu ya sehemu yake aliyokuwa nayo mbele ya Mtume (s.a.w) na ubora wake kwa Mtume (s.a.w).Kwa kuonyesha mapenzi yake kwa mwanaye Fatima (a.s) Mtume (s.a.w) aliamua kumzawadia mwanae huyo Shamba kubwa lililokuwa likitoa mavuno kipindi chote bila kukatika,shamba ambalo huitwa katika vitabu vya historia ya Uislaam kwa jina la {FADAK}.
Fadak hii baada ya Mtume (s.a.w) kufariki,alidhulumiwa na kunyanganywa na aliyejiitwa kuwa ni Khalifa wa Kwanza wa Mtume (s.a.w).Na aliyejiita Khalifa wa pili baada ya kuhifa wa kwanza naye aliendelea kuhifadhi dhulma hii kwa kulishikilia shamba hili la Fatima (a.s) alilopewa na baba yake (s.a.w).Pia na yule aliyejiita kuwa ni Khalifa wa tatu wa Mtume (s.a.w) naye aliendelea kuhifadhi sunna hiyo iliyoanzishwa na makhalifa hao wawili waliomtangulia kwa kulibania shamba hilo na kamwe hakukubali kulirudisha mikononi mwa Ahlul bayt (a.s) wa Mtume (s.a.w).
Ama khalifa wa nne kwa hisabu isiyokuwa sahihi ambaye ni khalifa wa kwanza kwa hisabu sahihi aliyoitaja Mtume (s.a.w) pale aliposema kuwa: "Makhalifa baada yangu ni Kumi na wawili" huku akitaja majina yao mmoja baada ya mwingine, pindi aliposhika usukani,mara moja bila kuchelewa,FADAK hiyo au shamba hilo alilirudisha katika mikono ya Ahlul-bayt (a.s) hata kama mwenye nalo yule ambaye Mtume (s.a.w) kampatia shamba hilo alikuwa tiyari amesha kufa kishahidi.Shamba hilo lilibaki kuwa ni urithi wa Ahlul-bayt (a.s). Kwa ufupi huyu ndiye Mama mzazi wa Sayyidat Zainabul-Kubra (a.s) ambaye Mtume (s.a.w) amemwambia akisema: "Ewe Fatima,hakika Mwenyeezi Mungu (s.w) hughadhibika unapoghadhibika (wewe),na huridhia unaporidhia (wewe)"
BABA YAKE
Baba yake na Sayyidat Zainabul-Kubra (a.s) ni Amirul-Muuminina,Dalili na Imam wa Hekima na Uadilifu katika Uislaam, ndugu yake na Mtume (s.a.w) na Mlango wa Elimu yake (s.a.w) na ambaye daraja yake kwa Mtume (s.a.w) ilikuwa ni daraja sawa na aliyokuwa nayo Haruna kwa Musa (a.s) ispokuwa kwamba hakuna Nabii baada ya Mtume (s.a.w).Na ndiye yule ambaye wapokezi wa riwaya wameitifakia kwa kauli moja kuwa ndiye wa kwanza kumuamini Mtume (s.a.w) na aliyesimama katika ubavu wake (s.a.w) kwa nguvu zote ili kuhakikisha Uislaam unasonga mbele na kuenea katika kila kona ya dunia.Alikuwa ni Shujaa wa Mashujaa katika Jeshi la Uislaam,Ukafiri ulipata misukosuko,tabu na mashaka makubwa pindi ulipokuwa ukikutana na upanga wa Imam Ali (a.s) na lau isingelikuwa Jihad ya Imam Ali (a.s) pamoja na Mali ya Bibi Khadija (a.s),Uislaam huu,tunaojivunia hii leo,usingelisimama na kufika hapa ulipo.
Baba yake huyu wa Sayyidat Zainabul-Kubra pia ndiye yule ambaye alionyesha imani ya hali ya juu pindi alipojitolea kunusuru maisha ya Mtume (s.a.w) kwa kulala katika kitanda chake.Tukio hili lilitokea baada ya Maqurayshi waovu wa Makka kudhamiria kumuua Mtume (s.a.w) ambapo walipanga mipango yao ikaiva,wakaafikiana jinsi watakavyofanikisha mauaji hao kwamba wataizingira nyumba ya Mtume (s.a.w) kila sehemu,na kumvamia kitandani akiwa amelala,na kumuua pale pale.Baada ya Mtume kupata Taarifa hizo kutoka kwa Mwenyeezi Mungu (s.w) alimjulisha Imam Ali (a.s) kuhusiana na njama hizo,Imam Ali (a.s) akamwambia je mimi nikilala katika kitanda chako,utasalimika?Mtume akasema ndio.Basi Imam Ali (a.s) hakuona tabu kulala katika kitanda cha Mtume (s.a.w) ili wale waovu wakija wamuue yeye na Mtume (s.a.w) asalimike. Kwa ufupi huyu ndiye Imam Ali (a.s) ambaye ndiye Baba yake mzazi wa Sayyidat Zainabul Kubra (a.s) ambaye alikuwa siku zote akisema:
"Niulizeni kuhusiana na njia za Mbinguni,hakika Mimi ninajua njia hizo sana kuliko ninavyozijua njia za Ardhini." Na alikuwa akisema: "Niulizeni kabla hamjanikosa". Kauli ambao haikuwahi kuzungumzwa na Swahaba yeyote yule wa Mtume (s.a.w) ispokuwa Imam Ali (a.s).Kauli hiyo inadhihirisha wazi elimu aliyokuwa nayo ya hali ya juu aliyoipata kutoka kwa Mtume (s.a.w).Pia kauli hiyo inathibitisha ile kauli ya Mtume (s.a.w) aliposema kwamba: "{Mimi} ni Mji wa Elimu na {Ali} ni Mlango wake (yaani Ali ni mlango wa Mji wa Elimu hiyo)"
BIBI YAKE KWA BABA YAKE
Bibi yake Sayyidat Zainabul-Kubra (a.s) kwa upande wa Baba yake alikiwa ni Sayyidat Az-zakiyya Fatima bint Asad bin Hashim bin Abdumanaafi,Mke wa Abi Twalib.Naye ni katika wanawake bora katika imani yake na Twabara yake.Mwanamke huyu alichukua jukumu zito la kumlea Mtume (s.a.w) na kumjali ambapo alikuwa akimhurumia Mtume (s.a.w) na kumpa malezi mazuri yenye upendo wa hali ya juu kuliko alivyowapenda wanae,na alikuwa akimpatia Mtume (s.a.w) huduma zote,na Mtume (s.a.w) katika moja ya sehemu ya maisha yake ameimaliza akiwa chini ya uangalizi wa Mwanamke huyu Mchamungu ambaye ni Bibi yake Sayyidat Zainabul-Kubra (a.s) ambaye hakuacha aina yoyote ile ya upendo na uagalizi ispokuwa kaitoa kwa Mtume (s.a.w).Kwa Mtume (s.a.w), Fatima bint Asad Bibi yake na Sayyidat Zainabul-Kubra (a.s),alikuwa ni mtu bora sana kuliko.
Kwa ufupi huyu ndiye Bibi yake na Sayyidat Zainabul-Kubra (a.s) ambaye Mtume (s.a.w) anasema kwamba: "Hakuna Mtu aliyenipenda sana na kunifanyia wema baada ya Abi Twalib kama yeye,na nimemvalisha kanzu yangu ili aweze kuvalishwa mavazi bora ya peponi,na nililala pembeni ya ubavu wake katika kaburi lake ili aweze kuwekewa wepesi."
NDUGU ZAKE
Baada ya kutaja kwa ufupi Familia tukufu ambayo ndio ainayotokana nayo Sayyidat Zainabul-Kubra (a.s), litakuwa ni jambo jema tukitaja walau kwa haraka haraka majina ya ndugu zake na Mwanamke huyu ambaye ni mfano bora kwa wanawake wote wa ulimwenguni katika kila nyanja ya maisha.Ndugu zake hawa na Sayyidat Zainabul-Kubra (a.s) ambao kaishi nao wote ni ndugu ambao walilijaza tundu la dunia kwa Fadhila zao na athari zao nzuri.Nao ni hawa hapa wafuatao:
1-Imam Hasan (a.s) Imam Hasan (a.s) ni Sayyid wa vijana wa peponi,na ndiye mjukuu wa kwanza wa Mtume (s.a.w) ni mtoto wa kwanza wa Imam Ali (a.s).Sayyidat Zainabukl-Kubra (a.s) kaishi na kaka yake huyu Hasan (a.s) mpaka alipokuwa shahidi kwa kuuliwa na sumu alipewa na Mke wake kwa kutumwa na Muawiya.
2-Imam husein (a.s)
Imam Husein (a.s) ni kaka wa pili wa Sayyidat Zainabul-Kubra (a.s).Na aliishi na kukua na kaka yake ayake huyu (a.s) na alichukua tabia zake zote,na kulikuwa baina yao mapenzi ya hali ya juu,walipendana sana kupita maelezo,alimuona na kumchukulia Imam Husein (a.s) kuwa ni mbora zaidi kuliko maisha.Na alikuwa kishirikiana na kaka yake huyu Husein (a.s) katika kila amali na kila maumivu aliyoyapata Husein (a.s) naye pia alionja maumivu hayo.Imam Husein (a.s) alimthamini sana dada yake huyu kipendi,na hii kwa sababu ya rai nzuri na muono wa mbali aliokuwa nao Sayyidat Zainabul-Kubra (a.s),na adabu za hali ya juu,na heshima isiyokuwa ya kawaida ambayo kairithi kutoka katika mti wa Unabii na Mti wa Uimam.Zainabul Kubra (a.s) pia alikuwa na sura ile ile sahihi ya mama yake ambaye ni sehemu ya nyama ya Mtume (s.a.w),na mbora wa wanawake wa ulimwengu mzima,Az-zakiyya,Fatimatuz-zahraa (a.s).
Sayyidat Zainabul-Kubra (a.s) alikuwa ni sehemu ya siri ya Imam Husein (a.s),na alijua mambo yote ya Imam Husein (a.s) ya siri na yasiyokuwa ya siri.Imam Husein (a.s) alikuwa akimtaka ushauri dada yake Sayyidat Zainabul-Kubra (a.s) katika mambo yote alikuwa akithamini ushauri.Sayyidat Zainabul-Kubra (a.s) aliambatana na kaka yake Husein (a.s) katika Mapinduzi yake yenye kudumu vizazi hadi vizazi na ambayo ni mfano unaoigwa kwa kila mwenyekutaka kusimamisha mapinduzi kwa kuipinga dhulma na kusimamisha haki.
Na lau kama si Jihad yake ,na juhudi yake,na msimamo wake uliowayumbisha Watawala wa Bani Umayya,basi mapinduzi haya ya kaka yake Husein (a.s) yangelipotea,na kuondoka heshima ya mwanadamu katika uso wa ardhi ambayo kwa baraka ya mapinduzi ya kaka yake Husein (a.s) ilitanda uliwemgu mzima.
Sayyidat Zaibul-Kubra (a.s) urafiki wake,ukaribu wake na mapenzi yake kwa kaka yake Husein (a.s) yalifikia hatua ya juu kabisa kiasi kwamba Imam Husein (a.s) katika Uwanja wa mapambano huko Karbala,alienda kwa dada yake Sayyidat Zainabul-Kubra (a.s) na kumuaga kwa mara ya mwisho,kisha Imam Husein (a.s) akamuomba dada yake Zainabul-Kubra (a.s) asisahau kumuombea katika swala zake za usiku.
3-Abbas: Abbas (a.s) alikiitwa (Qamaru bani Haashim), fahari ya Uislaam, mwenye kuhuisha Uislaam, ambaye naye alikufa shahdi katika uwanja wa karbalaa akiwa na kaka yake Husein (a.s).Mama yake ni Ummul-Banina, naye ni mwanamke bora katika wanawake bora na wema wa kiislaam katika fadhila zake, na utukufu wake, na twahara yake.Imam Ali (a.s) alimuoa mwanamke huyu (Ummul-Banina) baada ya kufa mkewe kipenzi wa kwanza Fatimatuz-zahraa (a.s).
Ummul Banina mama yake na Abbas, alisimama kidete kuhakikishia anawalea vizuri wajukuu wawili ambao ni masayyid wa vijana wa peponi ambao ni Hasan na Husein (a.s) na dada yao Sayyidat Zainabul-Kubra (a.s).Alikuwa akiwatanguliza mbele katika kila kitu kuliko watoto wake, kwa sababu alijua kuwa hao ni kizazi kitukufu cha Mtume (s.a.w) ambao Mwenyeezi Mungu (s.w) kawataka (si kwa khiari yao bali ni laziama wafanye hivyo) waislaam wote kuwapenda.
Na Mtoto wa kwanza wa Ummul-Banina kwa Imam Ali (a.s) alikuwa ni Abul-Fadhul-Abbas ambaye alilelewa nakukua pamoja na ndugu zake, kaka zake Hasan na Husein (a.s) na dada yake Zainabul Kubra (a.s),Wakamnywesha fadhi na adabu na akhlaaq na elimu ya Uimam,na akapnda katika nafsi yake Kumcha Mwenyeezi Mungu (s.w) ambapo taqwa yake ilifikia kiwango cha juu kabisa mpaka alifikia kuwa mfano wa watu wenye iman,aliigwa na wengi matendo yake,alimpenda sana kaka yake Imam husein (a.s) nauhusiano wao ulikuwa wa kuaminika,Imam Husein (a.s) alijihisi mwenye nguvu kipindi chote alipomuonaAbbas kando yake,alijihisi unyonge kupita kiasi pindi ndugu yake huyu Abbas alipokufa shahidi kwa kukatwa mikono yake miwili huko katika uwanja wa karbala.
Abbas alikuwa akimpenda sana dada ayake Sayyidat Zainabul-Kubra (a.s) ambapo Sayyidat Zainab (a.s) alipata mambo mengi sana kutoka kwa Abbas akama vile upole,huruma,moyo wenye kuonyesha kujali na kuthamini kuliko alivyopata vitu hivyo kwa ndugu yake yeyote yule wa upande wa Baba yake.
Na pindi Sayyidat Zainabul-Kubra (a.s) aliposafiri pamoja na kaka yake Baba wa Mashahidi kutoka Madina kuelekea Makka kisha kutoka Makka kuelekea Karbala, Abbas ndiye aliyekuwa akimhudumia dada yake huyu Zainabul-Kubra (a.s) na hakukubali hata sekunde moja amhudumie asiyekuwa yeye katika watoto wa Imam Ali (a.s).Na pindi Abbas (a.s) alipokufa shahidi huko Karbala, Sayyidat Zainabul Kubra (a.s) alipata machungu mazito sana katika nafsi yake, akamlilia ndugu yake Abbas (a.s) na kwamwe alimkumbuka katika maisha yake yote aliyoishi baada ya tukio hilo la karbala.
4-Muhammad bin Al-hanafiyya. Pia ni mtoto wa Imam Ali (a.s) aliyekuwa akiitwa kwa laqab ya {Ibnil-Hanafiyya}.
ASILI YA JINA LA ZAINAB
Baada ya Fatimatuz-zahraa (a.s) kujifungua mwanae huyu kipenzi, alimchukua kwa Imam Ali (a.s), Imam Ali (a.s) akamchukua kisha akaanza kumbusu mwanae huyu kipenzi, kisha Fatima (a.s) akamtazama Imam Ali (a.s) na kumwambia: "Mpe jina Mtoto huyu mchanga". Imam Ali (a.s) akamjibu mkewe Fatima (a.s) kwa adabu na unyenyekevu: "Siwezi kumtangulia Mtume wa Mwenyeezi Mungu (s.w)"
{yaani siwezi kuwa mwenye kutangulia kumpa jina kabla ya Mtume -s.a.w-} Akamchukua mtoto huyu mchanga kwa Mtume (s.a.w) ili awe ndie mwenye kumpa jina, Mtume (s.a.w) naye akasema: "Siwezi kumtangulia Mwenyeezi Mungu (s.w)" {Yaani siwezi kuwa mwenye kutangulia kumpa jina kabla ya Mwenyeezi Mungu -s.w-}. Bai hapo ndipo aliposhuka Mjumbe wa Mbinguni (Jibrail a.s) kwa Mtume (s.a.w),na akamwambia Mtume (s.a.w):
"Muite Mtoto huyu mchanga {Zainab}; Mwenyeezi Mungu amemchagulia jina hili" Hivi ndivyo jina la Sayyidat Zainabul -Kubra (a.s) lilivyopatikana.Ni zawadi kutoka kwa Mwenyeezi Mungu (s.w) ambaye ndiye aliyemchagulia jina hili zuri.Zainabu inatokana naneno (Zainu) maana yake ni pambo, kitu kizuri chenye kupendeza (Graceful).Hivyo yeye ni pambo la wazazi wake.Uzuri ulioje wa jina hili!!
LAQABU ZA SAYYIDAT ZAINABUL-KUBRA (A.S).
Baada ya Shahada ya Imam Husein (a.s) bi Zainabul-Kubra (a.s) anidye aliyekuwa akiongoza na kupangilia mambo ya Ahlul-bayt (a.s),na si Ahlul bayt (a.s) tu peke yake bali ukoo wa mzima wa Baniy Haashim.Alikuwa na moyo wa kupenda kujituma kuhudumia na kuikirimu familia nzima ya watu wa Nyumba ya Mtume (s.a.w) na ukoo mzima wa Baniy Haashim. Alikuwa na Laqabu nyingi sana kulingana na tabia yake na utukufu wake ulivyokuwa.Na hizi hapa baadhi ya Laqabu zake:
1-UQAYLA BANI HASHIM
Na (Uqayla) maana yake:Ni Mwanamke Mkarimu kwa watu wake,na Mtukufu katika nyumba yake.Na Sayyidat Zainabul-Kubra ni Mwanamke mbora sana na Mtukufu katika Dunia ya Waarabu na Uislaam.Na Laqb hii ilikuwa ni alama kwa kizazi chake,wanae wote walikuwa wakiitwa kwa laqabu ya 'Baniy Uqayla'.
2-AL-AALIMA
Na mjuu huyu wa Mtume (s.a.w) alikuwa ni katika Wanawake watukufu Maulamaa wenye elimu nyingi na kubwa katika Familia ya Unabii. Alikuwa kama wanavyosema wanahistoria wakubwa:Marejeo ya wanawake watukufu,wachamungu na bora katika Uislaam,walikuwa wakirejea kwake ili kupata elimu katika mambo yao ya kidini.
3-A'BIDAT A'LI AL
Zainabu (a.s) alikuwa Mwanamke miongoni mwa Wanawake bora na waja wa Mwenyeezi Mungu (s.w) katika wanawake wa Kiislaam, alimuabudu Mwenyeezi Mungu (s.w) kiasi kwamba hakuna sala ya sunna katika sala za sunna za kiislaam aliyoiacha ispokuwa aliiswali.Baadhi ya wapokezi wa hadithi wanasema kwamba:
Sayyidat Zainabul Kubra (a.s) aliswali sunna zote katika usiku wa kumi na moja katika mwezi wa Muharram ambao ulikuwa ni usiku mzito sana na mgumu wenye kila aina ya mashaka na khofu na huzuni kwa kizazi cha Mtume (s.a.w) kutokana na hatari ya kuuliwa iliyokuwa ikiwakabili kutoka katika jeshi la Yazid mwana wa Muawiya ambaye ndiye aliyetekeleza shughuli nzima ya kuhakikishi anafyekelea mbali na kumaliza kizazi cha Mtume (s.a.w) kwa kuwachinja na kuwakata vichwa vyao na kuwatunduka juu ya mikuki na kuvizungusha vichwa hivyo vikiwa juu ya mikuki huku na huko katika mji wa Kufa na Shaam.
4-AL-KAAMILA
Sayyidat Zainab (a.s) ni mwanamke mkamilifu zaidi katika Uislaam kutokana na fadhila zake zilizofikia kiwango cha juu na utukufu wake na twahara yake kutokana na uchafu wa kimaada na uchafu wa dhambi.
5- AL-FAADHILA
Sayyidat Zainab (a.s) ni Mbora wa wanawake wa Kiislaam katika Jihad yake na huduma yake kwa ajili ya Uislaam, na kujitolea katika njia ya Mwenyeezi Mungu (s.w). Hizi ndizo baadhi ya Laqab zake (a.s) zinazoonyesha adhama ya dhati yake, cheo pamoja na heshima yake.
MUME WAKE NA SAYYIDAT ZAINABUL KUBRA
Baada ya sayyidat Zainabul Kubra kukua na kufikisha umri wa kuolewa, walikuwa watu mbali mbali wenye vyeo vyao na wenye majina makubwa kumchumbia Zainab (a.s), ili waweze kumuoa na kujenga majina yao.Na hii ni kutokana na ule utukufu na heshima na adabu na sifa nyingine nzuri walizokuwa wakiziona kwa Sayyidat Zainabul Kubra (a.s).Imam (a.s) hakuwajibu watu hao; hapo ndipo alipokuja mtoto wa ndugu yake aliyekuwa akiitwa: Abdullah bin Jaafar, ambaye ni katika masharifu na malodi na wakarimu wa dunia ya Waarabu na Uislaam, kumchumbia Bi Zainab (a.s) na Imam Ali (a.s) akamjibu katika hilo na kumkaribisha.
Kwa ufupi Abdullah:
" Baba yake alikuwa ni Jaafar bin Abi Twalib (a.s) ndugu yake na Imam Ali (a.s).
" Mama yake alikuwa ni Asmaau Bint Amiysi
(أسماء بنت عميس).
Abdullah alikuwa na sifa ambazo sehemu hii haitoshi kuweza kuzitaja zote na kuzimaliza,alikuwa akiitwa {Bahrul-juud}, na inasemekana kwamba:Hakukuwa na Mtu katika Uislaam aliyekuwa ni mkarimu,mwingi wa kutoa kama Abdullah bin Jaafar bin Abi Twali (a.s). Huyu ndiye aliyekuwa Mume wa pekee wa Sayyidat Zainabul-Kubra (a.s).
WATOTO WA SAYYIDAT ZAINABUL-KUBRA (A.S).
Zianabul-Kubra (a.s) ambaye tumeseme kuwa mume wake alikuwa ni Abdullah bin Jaafar bin Abi Twalib (a.s), alimzalia Abdullah bin Jaafar watoto ambao nao walichukua tabi nzuri ambazo chimbuko lake ni mti wa Unabii na Uimam.Alizaa watoto hawa wafuatao: 1-Aun ((عون: Alikuwa ni kijana mkarimu na mchamungu katika vijana wa Bani Haashim, alikuwa mchamungu sana mwenye kumcha Mungu na kutekeleza maamrisho yote ya Mwenyeezi mungu (s.w) na kujizuia na yale makatazo yote aliyoyakataza Mwenyeezi Mungu (s.w). 2-ALIYYU AZ-ZAINABIYYU.
3-MUHAMMAD
4-ABBAS
5-ASSAYYIDAT UMMU KUL-THUUM.
SUBIRA YA SAYYIDAT ZAINABUL-KUBRA (A.S).
Jambo kubwa sana ambalo Sayyidat Zainab (a.s) na kuwa mfano bora wa kuigwa na kila mwanadamu ni kuwa na Subira kwa majanga,shida,mashaka na manyanyaso ya dunia na matukio mengine mabaya aliyoyashuhudia na kuyapata katika uso huu wa ardhi. Sayyidat Zainabul Kubra (a.s) kaishi na maisha yake yote yalijaa matukio ya kusikitisha yaliyowakumba: Mama yake, Baba yake, kaka Mkubwa wa kwanza Hasan na Husein (a.s).
Hao wote wamedhulumiwa, kuteswa, mpaka kuuliwa hali ya kuwa Sayyidat Zainab (a.s) akiwa ni mwenye kushuhudia yote hayo, na mbaya zaidi kuliko yote ni kile kifo kibaya alichokufa kaka yake Imam Husein (a.s) katika ardhi ya Karbala ambapo alizingirwa na majeshi ya Yazid Mtoto wa Muawiya katika ardhi hiyo na hatimaye kumuua kikatili baada ya mapambano makali, majeshi hayo ya waovu, hayakutosheka na kumuua Imam Husein (a.s) bali waliona hiyo haitoshi wakaamua kumkata kichwa Imam Husein (a.s) nakukitundika juu ya mkuki na kukitembeza usiku na mchana kutokana Kuufa kukipeleka Syria ili kukikabidhi kwa Yazid mtoto wa Muawiya aliyekuwa huko na ambaye ndiye aliyetoa amri ya kufanya mauaji hayo yasiyosahaurika kizazi hadi kizazi.
Yote hayo yalifanyika mbele ya Sayyidat Zainabul-Kubra (a.s) ambapo aliona ndugu zake wote aliokuwa ishi nao na kukua nao, aliowapenda, waliompenda, wakiuliwa mmoja baada ya mwingine, lakini mwanamke huyu alikuwa na subira ya hali ya juu.Alivumilia maumivu hayo yagongayo moyo nahakuacha kumtegemea Mwenyeezi Mungu (s.w) ambaye hupenda subira, daima aliamini kuwa ipo siku huzuri hizo alizokuwa nazo katika motyo zitakuja kuondolewa na furaha ambayo Mwenyeezi Mungu (s.w) kawabashiria wenye kusubiri kwa kauli yake katika Suuratul-Baqarah aya ya 155 mpaka 157 aliposema:
*Na kwa hakika tutawajaribuni kwa jambo la khofu na njaa na upungufub wa mali na nafsi na matunda.Nawe wape (wabashirie) khabari ya furaha wenye kusubiri* Nakauli yake (s.w) katika Suuaratuz-zumar aya ya 10 anasema: *Bila shaka wanaofanya subira watapewa malipo yao pasipo hesabu* Na kauli yake (s.w) katika Suuratun-nahl; aya ya 97 anasema:
*Na bila shaka sisi tutawalipa waliosubiri malipo yao sawa na matendo mazuri waliyokuwa wakiyatenda*
Sayyidat Zainabul Kubra (a.s) amesubiri na kuvumilia matukio yote mabaya yaliyotokea na aliyoyashuhudia kwa macho yake mawili, akaonyesha msimamo na nguvu mble ya Maadui wa Mwenyeezi Mungu (s.w),na hayo ni sehemu ya matendo mazuri ya Sayyidat Zainabul Kubra (a.s) ambayo Mwenyeezi Mungu (s.w) anasema: *Na bila shaka sisi tutawalipa waliosubiri malipo yao sawa na matendo yao mazuri waliyokuwa wakiyatenda* Huyu kwa ufupi ndiye Sayyidat Zainabul Kubra ambaye amekuwa mfano bora wa kuigwa katika maisha kwa wanawake na wanaume katika Ulimwengu wa Waarabu na Uislaam.Kila ukisoma historia ya maisha yake basi utapata kujua mengi na kujifunza mengi kutoka kwa Sayyidat Zainabul-Kubra (a.s).Uislaam unajifakhilisha kuwa na mwanamke bora kama Huyu Zainabu (a.s) ambaye alizaliwa Mwezi wa tano wa Jamaadul Awwar, katika mwaka wa tano Hijria baada ya Mtume (s.a.w) kuhama kutoka Makka na kuelekea Madina.
Mwisho:
Tunawapongeza Waislaam wote Ulimwenguni kwa kuzaliwa Bibi Huyu Zainabul Kubra, Mtukufu, Mchamungu, Mkarimu, Mwenye Heshima, Adabu na kila aina ya sifa nzuri.Tunamuomba Mwenyeezi Mungu (s.w) atujaaliye na kutuwekea wepesi katika mambo yetu ,tuweze kumzuru na kumtembela Bibi Zainabul Kubra katika Haramu yake Tukufu iliyopokatika nchi ya Syria.Pia Tunamuomba Mwenyeezi Mungu (s.w) atufufua siku ya Kiyama pamoja na Kizazi Kitukufu cha Mtume (s.a.w) na atuweke mbali na maadui wa kizazi cha Mtume (s.a.w) walioshiriki kukiangamiza kizazi chake (s.a.w) na pia atuweke mbali siku hiyo ya kiyama na wale wote waliowaunga mkono au wanaowaunga mkono na kuwapenda na kuwatetea wale watu wenye chuki na Ahlul-bayt (a.s) ,waliowadhulumu,kuwatesa,kuwaadhibu na kuhatarisha amani ya kizazi cha Mtume (s.a.w).