SWALA ZA WAJIBU
BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM
SWALA ZA WAJIBU
ASSALAAM ALAIKUM
Katika sehemu iliyopita kwa ufupi tumezungumzia umuhimu wa Swala, tukasema kwamba mtu mwenye kuswali ni lazima ajue anapokuwa anaswali anazungumza na nani?,kitendo cha kutambua anazungumza na nani kitamfanya kuzingatia swala hiyo anayoiswali au anayotaka kuiswali,ama yule anayeswali pasina kuzingatia swala yake ni kama mtu asiye swali kabisa bali anakuwa miongoni mwa wale ambao Allah (s.w) kawazungumzia katika Qur'an Tukufu akisema:
"Basi ole wao wanao swali, ambao wanapuuza (maamrisho ya) Swala zao." Ama somo letu la leo tutazungumzia kuhusu swala za wajibu.
Swala za wajibu ni sita.
1-Swala tano za kila siku
2-Swala ya Ayaat
3-Swala Maiti
4-Swala ya Twawafu (ya wajibu)
5-Swala ya Qadhaa ya baba na mama.
Ikiwa baba au mama amekufa na alikuwa na swala ambayo ilikuwa wajibu kwake aiswali na hakuiswali kwa sababu kadhaa wa kadhaa,basi itabidi amhusie mtoto wake wa kwanza wa kiume alipe swala hiyo au swala hizo,na ikiwa hakuacha usia,ikiwa motto atajua kuwa baba au mama alikuwa na swala kadhaa hakuziswali na niza wajibu,basi itatakiwa ni wajibu kwake kuswali swala hizo.Hivyo swala hii/hizi huitwa swala ya/za Qadha ya/za baba au mama {yaani swala ya/za kulipa zile swala ambazo zilikuwa katika dhimma ya baba au mama au zilikuwa ni wajibu kwa baba au mama kuziswali}.Swala hii ya Qadha ni wajibu kwa motto wa kwanza wa kiume kuziswali.
6-Swala ambayo inakuwa kwa mtu kutokana na sababu kadhaa. Hivyo swala hii inakuwepo na kuwa wajibu moja kwa moja pindi sababu hizi zitakapokuwepo. Mfano: Kuajiliwa kuswali(huitwa swala ya ijara):Yaani ikiwa fulani atakuajili uswali Swala kumi au mia au idadi yoyote ile,na wewe ukakubali kuajiliwa (yaani ukaridhika kufanya hivyo),na kwamba uko tiyari kutekeleza ajira hiyo ya kuswali Swala hizo,basi swala hizo moja kwa moja zinakuwa ni wajibu kwako kuziswali zote. Mfano mwingine,ni swala ya Nadhiri.
Ikiwa mtu ataweka nadhiri,akasema mfano: Nikifanikiwa katika jambo langu fulani,nitaswali rakaa (mfano) nane kwa ajili ya kumshukuru Mwenyeezi Mungu (s.w) au ikiwa nitaruzukiwa mtoto wa kiume au wa kike nitaswali rakaa idadi fulani kumshukuru Allah (s.w).Ikiwa utaweka nadhiri namna hiyo,basi hizo swala zitakuwa ni wajibu kwako kuziswali na huna khiyari ya kutoziswali. Vile swala nyingine zinazotokana na ahadi,nazo ni wajibu kwa mtu aliyeweka ahadi kuziswali,bila kusahau zile swala ambazo zinatokana na kiapo,ikiwa mtu ataapa kuswali swala kadhaa,swala hizo zitakuwa ni wajibu.
UTANGULIZI WA SWALA.
Tunaposema swala,tunamaanisha kusimama mbele ya Mwenyeezi Mungu (s.w) na kuonyesha uja wako kwake na kumwabudu yeye tu.Hivyo swala hii huhitaji utangulizi fulani kwani swala haiwezi kukubaliwa mpaka uwepo utangulizi huo na si kuwepo bali utekelezwe.Na utangulizi huo ni huu hapa ufuatao:
1-Tohara
2-Wakati
3-Nguo
4-Sehemu (ya kuswalia) na
5-Qibla.
Litakuwa ni jambo la msingi tukiubainisha utangulizi huu moja baada ya mwingine.
1-TOHARA.
Mtu anayetaka kuswali ni lazima awe na tohara,yaani awe mtoharifu.Ili awe mtoharifu ni lazima achukue udhu kabla ya swala au kuoga josho la lazima ikiwa ana janaba mfano,au ni lazima afanye Tayammum.Pia ni lazima nguo zake ziwe tohara (yaani ziwe safi) kutokana na najisi.
Najisi
Kuna vitu ambavyo ni najisi na inatakiwa kuondolewa najisi hiyo kabla ya swala. Najisi hizo ziko katika aina kadhaa zifuatazo:
Moja Mkojo na Mavi. Ile sehemu ya kutokea mkojo inaweza kutoharishwa kwa kumia maji,lakini ile Ile sehemu ya kutokea mavi,inaweza kutoharishwa kwa kutumia maji,mawe matatu au vitu kama hivyo ili mradi mavi yale yasiwe yenye kuenea au (kusambaa) sehemu kubwa kuliko ile sehemu ya kawaida yanakotokea,ama ikiwa sio hivyo,au kwa ibara nyingine tunaweza kusema:ikiwa mavi yale yamesambaa sehemu kubwa kuliko ile sehemu ya kawaida yanakotokea,basi sehemu hiyo itakuwa haiwezi kutwaharishwa kwa mawe matatu wala kitu kingine chochote kile ispokuwa maji tu ndiyo yatakayotakiwa kutumika.
Hapa ni lazima tuweke wazi kwamba,ikiwa Mtu umetumia mawe matatu ili kutwaharisha au sehemu kunakotokea mavi,lakini mawe hayo matatu hayakuweza kutosha au hayakufanikiwa kuondoa au kutwaharisha sehemu hiyo,basi mawe zaidi yatahitajika kwa lengo la kusafisha vizuri sehemu hiyo ili kuhakikisha sehemu inatwaharika kisawa sawa.
Pili
Mkojo na mavi ya wanyama ambao nyama yao hailiwi na damu yao (wakichinjwa) hutoka kwa kuruka. Hawa ni wanyama ambao damu yao zinapokatwa mishipa zao hutoka kwa Kuruka kama vile pake,mbweha,sungura,samba,na wengine.Na hapa tuna- gundua kwamba mkojo au mavi au nyama ya wanyama kama vile kuku ndege na wanyama wengine wenye kuliwa sio najisi,ispokuwa ikiwa wanyama hao watakula mavi ya mwanadamu ,basi mkojo na damu,na mavi pamoja na nyama ya wanyama hao itakuwa ni najisi (kama nasiji ya wanyama wengine).
Tatu
Mzoga wa mnyama ambaye damu yake ni yenye kuruka anapochinjwa sawa sawa nyama yake ni halali kuliwa (kama Ngo'mbe) au si halali kuliwa bali (ni haramu kuliwa) kama (mbweha) atakuwa ni najisi. Lakini sehemu zingine za mzoga huo ambazo hazina uhai ,sio "Najisi" bali ni sehemu toharifu kama vile nywele,kucha,manyoya.
Nne
Damu ya mnyama ambaye damu yake huruka anapochinjwa vile vile ni najisi,sawa sawa nyama iwe ni halali kuliwa au haramu kuliwa. Tano
Sehemu zote za mbwa mwitu ni najisi,sawa sawa ziwe ni sehemu zenye kuwa na uhai au zile zisizokuwa na uhai kama vile kucha na nywele na manyoya yake,mwili mzima kwa ujumla ni najisi. Sita
Sehemu zote za Kitimoto au Nguruwe ni najisi,sawa sawa ziwe ni sehemu zenye kuwa na uhai au zile zisizokuwa na uhai kama vile kucha na nywele na manyoya yake,mwili mzima kwa ujumla ni najisi. Saba
Pombe na kitu chochote kile kinachomlevya mwanadamu lakini kikiwa katika hali ya maji maji (liquid) ni najisi. Nane
Bia.
Hivyo kabla ya swala,ni lazima mwenye kuswali kuhakikisha hana aina moja wapo ya najisi tulizozitaja hapo juu au ni lazima aondoe najisi hizo na kuwa mtwaharifu ili aweze kuiswali swala yake akiwa katika hali ya twahara na akifanya hivyo basi swala yake itakuwa sahihi lakini ikiwa pia atatekeleza utangulizi mwingine uliobaki kama tuliyoutaja katika somo hili. Na ili aweze kuondoa au kujitoharisha kutokana na najisi hizo (nane) kama tulivyojitaza,itatakiwa kutumia vitu ambavyo vinaondoa najisi.na kitu chochote kile kinachondoa najisi huitwa kwa lugha ya Kiarabu:Mutwahhir.
VITU VINAVYOTOHARISHA
VITU VINAVYOTOHARISHA (AU VINAVYOONDOA NAJISI) "Mutwahhiraat"
Somo hili litaendelea:
Somo lijalo tutataja vitu vinavyondoa najisi na kutoharisha. Usikose kufuatilia somo hilo ili ujue ukiwa na najisi yoyote kati ya tulizozitaja unaweza kuiondoa vipi,mfano ikiwa sehemu (Ardhi mfano) ni najsi ,ufanyeje ili kuitwaharisha? Au mbwa au mzoga ambavyo ni najisi,ikiwa unataka kuitwaharisha au kuutwaharisha mzoga huo ufanye au utumie kitu gani ili mbwa huyo au mzoga huo ubadilike kutoka najisi na kuwa toharifu/ yote hayo utayajua katika somo lijalo inshaallah.
Suuratul Maau'un:Aya 4-5.
MWISHO