MUUNDO WA QUR'AN
MUUNDO WA QUR'AN
BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM
KUANDIKWA KWA QUR'AN (MUUNDO WA QUR'AN).
Assalaam Alaikum Warahmatullah Wabarakaatuh.
Kwa Muhtasari ningependa kuanza kwa kuashiria katika nukta hii kwamba kuandikwa kwa Qur'an Tukufu(Msahafu) na kuiweka katika mfumo huu ilivyo leo hii,yaani kupangilia aya zake na kupangilia suura zake katika utaratibu huu kuanzia Suuratul Faatiha na kuishia na Suuratun-Naas,na pia kuweka nukta katika herufu kuipanga iwe katika juzuu (mfano juzu ya kwanza (1) mpaka ya Juzu ya Thelathini (30) ) haikuwa ni kazi rahisi nyepesi nyepesi na haikuwa kama hivi mara moja tu ghafla ghafla,na pia mfumo huu haukakamila na kuwa na hivi katika kipindi cha WAHYI cha kwanza,bali shughuli hii imetimia kupitia muda kadhaa na vipindi tofauti tofauti na zama tofauti mpaka kuwa kama hivi tunavyoiona leo hii.
Kazi hii ya kuweka aya za Qur'an kwa kuzikusanya katika sehemu moja na hatimaye kuwa kitabu kimoja kilichokusanya aya zote zilizoshuka kwa Mtume wetu Muhammad (s.a.w) ili afikishe ujumbe wa aya hizo kwa wanadamu wote,ilianza katika kipindi cha RISALA na kuishia katika zama ambazo ndani yake zilifanyika harakati mbali mbali (Za Kuiunganisha misahafu yote iliyokuwa imeandikwa na Maswahaba wa Mtume (s.a.w) ili uwe msahafu mmoja unaowaunganisha waislaam wote ), ambazo ni zama za Uthman,Kisha katika kipindi au zama za Khaliyli bin Ahmad An-nahwiy ambaye ndiye aliyetimiza Muonekano wa msahafu au Qur'an hii kwa kuiweka katika hali hii ilivyo kwa sasa.
Jambo muhimu na la msingi ambalo ni muhimu tuliashirie katika bahthi hii ni kuhusiana na kutilia umuhimu wa kuisoma Qur'an Tukufu katika upande wa Kukusanywa kwake na kuandikwa kwake na kuwa Msahafu ulio baina ya majarida au magamba mawili.Na kwa kufanya uchunguzi kunako kipindi kile ambacho ndani yake ilikusanywa Qur'an na kuandikwa,na pia tusome mambo yote yaliyojiri katika tukio hili lililoonekana kuwa hatari sana la ukusanyaji na uandikwaji wa Qur'an Tukufu.
Ama Bahthi yetu kwa leo itakuwa katika sehemu tatu muhimu sana:
{1}-Kupangilia maneno yake na kuwa katika sura ya sentensi zenye kuleta maana na kukusanya au kukutanisha au kuunganisha maneno ndani ya Aya za Qur'an
{2}-Kupangilia au kuunda aya zake ndani ya Suura
{3}-Upangiliaji wa Suura za Qur'an Tukufu (baina ya magamba mawili) na kuwa msahafu kamili.
{1}-KUPANGILIA MANENO YAKE.
Hakuna shaka kwamba Maneno,sentensi, na Maelezo yote pamoja na Masimulizi yote ndani ya Qur'an Tukufu, vyote hivyo vilitendwa na asiyekuwa mwanadamu bali ilikuwa ni kazi ya Mwenyeezi Mungu (s.w), haikutokea na wala haijatokea mabadiliko yoyote katika kazi hii ya Mola wa Viumbe Mwenye Elimu isiyokluwa na mipaka (s.w).Sio kwa kuongeza wala kwa kupunguza na wala sio kwa kubadilika kwa sehemu hata siku moja. Na hili limethibitika ndani ya Qur'an yenyewe Pale Mwenyeezi Mungu (s.w) aliposema:
*لا يأتيه الباطل من بينِ يديهِ ولا من خلفِهِ تنزيلً من حکيمٍ حميدٍ*
Hautakifikia upotofu mbele yake wala nyuma yake,kimeteremshwa na Mwenye Hekima,Mwenye kuhimidiwa.
*إنَّ نحن نزَّلنا الذکر وإنَّ لهُ لحافظونَ*
Hakika sisi tumeiteremsha Qur'an,na hakika sisi ndio wenye kuilinda. Na kwa kubainisha zaidi tunasema:
Kwanza:
Kunasibisha maneno kwa mzungumzaji wa maneno hayo hupelekea mzungumzaji huyu kuwa ndiye mtendaji katika kupangilia maneno yake na kupangilia maana yake na njia zake za kipekee za kufikisha misemo yake,na kwa kuwa Qur'an Tukufu ni Maneno ya Mwenyeezi Mungu (s.w) Mwenye kuhimidiwa,basi ni lazima WAHYI uwe ndio Mtendaji wa pekee katika kupangilia maneno yake kisentensi na kuunganisha maneno katika utaalamu wa hali ya juu wenye kushangaza.! Pili:
Sehemu kubwa katika Qur'an Tukufu isiyo na kifani,au isiyoigika (Inimitability) ilikuwa nyuma ya mpangilio huu wenye utaalamu wa hali ya juu na wa kushangaza.! Na Qur'an hii Tukufu iliwachallenge (Ilitoa changa moto) au ilitoa mwito kwa waarabu waliokuwa wataalam wa kubainisha mambo na waliokuwa (ma-fluency) wafasaha na wanatamba zama hizo kuwa wamezama kwa ndani zaidi katika Lugha ya Kiarabu ili kuja kushinda na Qur'an Tukufu -Kwa ujumla-ambapo walitakiwa katika changamoto hiyo kuleta mfano wa Qur'an Tukufu na wakishindwa kuleta mfano wake (Yaani Qur',an Mzima) basi walau aya moja ili wathibitishe ujuzi wao wa kilugha! Na hawataweza kuleta mfano wake hata kama watasaidiana wao kwa wao kwani Mwenyeezi Mungu kaisha sema kwamba:
*ولا يأتون بمثله ولو کان بعضهم لبعض ظهيراً*
"Na hawataweza kuleta mfano wake hata kama watasaidiana wao kwa wao" Na changamoto hii kuhusiana na kuleta mpangilio wa maneno kama ya Qur'an Tukugu yenye maana ya hali ya juu na Balagha isiyoigika, ilikuwa na lengo kubatilisha changamoto hii kwamba hakuna kiumbe yeyote anaweza kujikakamua ili kufanya kushindana na Qur'an iwe Qur'an mzima au hata Aya moja ndani ya Qur'an Tukufu. Na mpaka leo hii hakuna anayemiliki fikra kama hii ya kwamba anaweza kuichalenge Qur'an hii! Hili liko wazi.
Tatu:
Umma katika vipindi vyote vya kihistoria umeafikiana kwa neno moja kwamba mpangilio huu uliopo katika Aya zote Tukufu za Qur'an umezalishwa au asili yake ni WAHYI WA MBINGUNI.Jambo ambalo Waislaam wote wanalizingatia pamoja na kutofautiana kwa rai zao katika sehemu nyinginezo. Na ndio maana hakuna A'alimu yeyote yule katika Maulamaa au wasomi wa kanuni za Lugha na Ufasaha aliyeonekana kuwa na wasi wasi katika Aya yoyote ile ya Qur'an kwamba imekuja kinyume na kanuni walizoziweka na kuzizoea ,bali waliichukua aya kuwa ni hoja ya kanuni zao na kuzibadilisha kanuzi zao baada ya kuona kanuni mpya katika aya waliyokuwa hawaijui ili kukutanisha kanuni zao na mpangilio wa Aya Tukufu za Qur'an Tukufu .Na hii ni kwa sababu walijua kwa yakini kwamba mfumo huu au mpangilio huu uliopo katika aya ni WAHYI ambao halipenyezi kosa la aina yoyote ile ndani yake.
Mfano wa hilo ni kauli ya Mwenyeezi Mungu (s.w):
*وَمَا أرسَلناکَ إلا کافة للناسِ*
"Na hatukukutuma ila kwa watu wote" Wasomi wa kanuni za Lugha na ufasaha walikidhani kwamba Haali (yaani neno Kaafatan katika aya hiyo juu) haimtangulii Mwenye nayo ambaye amekuwa majruur kwa herufi ya Laam (yaani neno Lin-Naas katika aya hiyo hapo juu),hii ndiyo iliyo kuwa kanuni yao.Lakini ikaja aya hii ikapangua na kufuta kanuni hii iliyokuwa katika vichwa vyao. Mfano mzuri ndugu msomaji ni Ibn Maalik ambaye tunamuona anakimbilia katika kubeza na kutupilia mbali kanuni hii kwa hoja kwamba inakwenda kinyume na Aya tukufu,ambapo alisema:
"وسبق حال ٍ ما بحرفٍ جرَّ قد أبَوا وَلا أمنعهُ قد َورَدَ"
Na Haali kumtangulia aliyekuwa Majruur kwa herufi Wamekataa lakini mimi sikatazi kwa sababu (kanuni hii) imethibiti (katika Qur'an)
{2}-KUPANGILIA AU KUUNDA AYA ZAKE KATIKA KILA SUURA.
Tutarudi ili kuendelea na sehemu hii ya pili hivi punde Inshaallah. Jitahidi kufuatilia sehemu hii ya pili ijayo ili ujue aya zilivyokuwa zikipangika katika kila suura na ujue ni alama ipi ambayo ilikuwa inajulisha kuwa aya hii ni mwisho wa suura hii na hii inayofuatia ni mwanzo wa suura nyingine.
MWISHO
Suurat Fusw-swila (Au Haa Mym): Aya ya 42.
Suuratul Hijr: Aya ya 9.
Suura Bani Israail;Aya ya 88.
Suura Sabaa:Aya ya 28.