Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

HISTORIA YA UMMUL-BANIINA KWA UFUPI

0 Voti 00.0 / 5

HISTORIA YA UMMUL-BANIINA KWA UFUPI

BISMILLAH AR-RAHMANI AR-RAHIIM.

KWA JINS LS MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEM.

UTANGULIZI

ASALAMU ALAIKUM WASOMAJI WAPENZI
Sina budi kumshukuru Mola Mtukufu pamoja na kumtakia amani Mtume mtakatifu Yeye pamoja na kizazi chake, kwa mara nyengine tena Muumba Mtakatifu ameniwezesha kushika kalamu na kuyazungumzia maisha ya bibi Ummul-Banii katika Makala hii. Ninatarajia ndugu wasomaji mtafaidika kwa kiasi fulani kutokana na Makala hii. Hii ni makala maalumu ielezayo historia fupi juu ya mwanamke shupavu aliyejawa na fadhila, mwanamke ambaye alikuwa ni mke wa Imamu Ali (a.s) Baada ya kufiwa na mkewe wa mwanzo ajulikanaye kwa jina la Fatimatu Zahraa.

MWANZO WA MAKALA

Kipindi kirefu kilipita baada ya kufariki bibi Fatima Zahraa (a.s), huku Ali (a.s) akiwa katika hali ya ukiwa, na mwishowe Ali (a.s) alimuendea nduguye ajulikanaye kwa jina la Aqiil, na kumtaka amchunguzie mwanamke aliye shujaa katika makabila ya Kiarabu. Aqiil alikuwa ni mjuzi sana wa kuzitambua Nasabu za makabila Kiarabu, hapo basi Aqiil hakuchelewa kuyatekeleza maamrisho ya nduguye, na muda si mrefu akawa ameshakuja na habari nono mbele ya Imamu Ali (a.s). Jicho la Aqiil halikumuona mwanamke aliyekuwa na ubora pamoja na ushujaa zaidi kuliko Fatima Kilaabiyya (Ummul-Baniina), na hapo ndipo lilipo angukia chaguo la Aqiil. Imamu Ali (a.s) kwa kuwa alikuwa akimuwamini vizuri sana nduguye (Aqiil) katika utambuzi na ujuzi wake wa kuyatambua makabila mbali mbali ya Kiarabu pamoja na Nasabu zake, akawa ni mwenye kuridhika na chaguo la nduguye, muda si mrefu Ali (a.s) akatuma posa na hatimae ndoa ikafungwa.

Usemi wa Imamu Ali (a.s) uliyosema kuwambia watu kua: "yeyote ambaye anataka kuwa pamoja na sisi basi na ajiandae kwa misiba na matatizo" haukubaki bila ya kuchukuwa nasibu yake kutoka kwa bibi Fatima (Ummul-Baniina). Hivyo basi bibi Huyu akawa hana budi kujitolea muhanga katika hali mbali mbali zilizokuwa zikimsibu akiwa ni mmoja kati ya wapenzi Aali Muhammad (a.s.w.w).

KIZAZI CHA UMMUL-BANIINA
Ummul-Baniina ni mmoja kati ya wanawake waliyofanikiwa kupata kizazi kilichotakasika na kustawi katika utiifu wa Mola Mtukufu. Mwanamke huyu tokea mwanzo alikuwa ni mwenye mapenzi makubwa juu ya kizazi cha Mtume (s.sw.w), naye alizaliwa katika familia iliyojaa ushujaa, ushupavu na ukakamavu wa mwanamke huyu katika kuitetea haki ulidhihirika katika sura mbali mbali za misimamo aliyokuwa nayo bibi huyu mtukufu.

Ummul-Baniina (a.s) alifanikiwa kupata kizazi cha watoto wanne kutoka Imamu Ali (a.s), watoto ambao walijulikana kwa majina ya Abbas, Uthmaan, Jaafar na Abdulla, na hakukutokea hata mmoja miongoni mwa watoto hawa aliyepingana na Imamu Hussein (a.s) katika nyenendo zake za kimapinduzi. Mtoto wa kwanza wa bibi Fatima (Ummul-Baniina) alikuwa ni Abbas (a.s) mtoto ambaye alikua ni nyota na ni pambo la kizazi cha Mtume (s.a.w.w), naye alikuwa ndiye mshika bendera mkuu katika mapambano ya Karbala.

Ummul-Baniina aliweza kukilea kizazi chake kwa mafanikio ya hali ya juu kabisa, malezi ambayo natija yake ilikuwa ni kujitolea muhanga kwa watoto wake wote wanne katika vita vita haramu vilivyotayarishwa dhidi ya Uisalmu na kiongozi wa Kishetani ajulikanaye kwa jina la Yazidi bin Muaawia. Mapenzi ya Ummul-Baniina juu ya Imamu Husein (a.s) yalikuwa ni hali ya juu sana, kiasi ya kwamba pale alipopewa habari ya muhanga wa wanawe, alikua yuko katika fazaa ya kutaka kuelewa habari za Imamu Husein (a.s) kuliko hata habari za wanawe hao waliyojitolea muhanga kwa ajili ya ndugu yao, ambaye ni Husein (a.s), na pale walipokuja watu kumpa habari za kuuwawa kwa wanawe, yeye aliwakabili watu hao kwa kuwambia: "kwanza tafadhalini nielezeni Huseni bin Ali yuko katika hali gani".

HATIMA YA MAISHA YAKE
Baada ya Ummul-Banii kupata habari za kuuliwa kwa Imamu Huseini (a.s), alijawa na huzuni kiasi ya kwamba maisha ya dunia hii yalimbadilikia kuwa ni shubiri, na hatimae Tarehe 13 ya Jamadu Thani ikawa ndiyo hatima ya maisha ya bibi huyu mtukufu. MWISHO WA MAKALA

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini