Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

UHUSIANO ULIOPO BAINA YA HAKI NA DINI

0 Voti 00.0 / 5

UHUSIANO ULIOPO BAINA YA HAKI NA DINI
SEHEMU YA PILI

UTANGULIZI

Katika sehemu ya kwanza ya Makala hii tulizungumzia uhusiano uliopo baina ya Dini na Haki, pamoja na kutoa ufafanuzi wa kiasi fulani kuhusiana na uhakika wa vitu viwili hivyo, leo tena katika sehemu ya pili ya Makala hii tumeamua kuingia ndani zaidi katika kuipekua Haki na kuifafanua kwa upana zaidi. Jambo ambalo linaweza kuzibadilisha nadharia zetu na kuziongoza katika malengo yaliyo bobea fikra sahihi kwa ajili usalama wa jamii zetu, na vizazi vyetu.

HAKI

Neno Haki kilugha huwa lina maana ya uhakika wa jambo fulani lilivyo, au kuthibika kwa kitu fulani katika picha halisi ya kitu hicho kilivyo. Wakati mwengine neno Haki huwa lina maana ya kuwajibika kihalali ipaswavyo, na mara nyingi watu hulitumia neno hilo katika maana hiyo, kwa mfano pale anapoambiwa mmoja wetu, ni Haki yako kutenda jambo fulani, yaani ni wajibu wako kutenda jambo hilo, na hilo linamaanisha kuwa kutenda kwako huko kwa jambo hilo ndiko kunakoonyesha nafasi halisi uliyoishika katika jamii yako.1

Mwanazuoni maarufu ajulikanaye kwa jina la "Tabarsiy" anasema: "Neno Haki huwa lina maana ya kila kitu kukaa katika sehemu yake ipaswayo kukaa, hivyo basi wakati wowote ule mtu atapokuwa na itikadi ya kitu fulani kwa kupitia dalili iimara katika kuisimamisha itikadi hiyo, hapo basi itikadi hiyo itasadikika kuwa ni itikadi ya Haki, kwani kuthibitika itikadi fulani kwa kupitia misingi imara na dalili madhubuti ni Haki, na kinyume chake huwa ni Batili". 2

Neno Haki katika Mahakama mbali mbali, huwa lina maana muowano unaoweza kupatikana baina hali dhahiri ya mambo fulani na ukweli halisi wa mambo hayo yalivyo, hivyo basi neno Haki Kimahakama huwa lina maana ya ambatano la ukweli wa jambo fulani linaloshikamana na udhahiri wa shuhuda zilizotolewa au kupatikana na Mahakama fulani katika kumsimamishia mtu kesi au kumhukumu mtu huyo kwa mujibu wa sheria za mahakama hiyo zisemavyo.

Utendaji wa mambo Kihekima ndiko kunakoweza kuifanya Haki ithibiti katika kila kitu, mara nyingi iwapo mtu atakuwa ni mwenye kushikamana na sifa fulani, mwisho wake sifa hiyo hugeuka kuwa ndiyo umaarufu wa mtu huyo. Kwa kutokana na kuwa Muumba Mkamilifu Ndiye Mbora wa kutenda Haki, hivyo basi neno Haki limegeuka kuwa ndiyo sifa maarufu ya Mola wetu, na sifa hii hakupewa na mtu, bali Yeye mwenyewe Ndiye aliyejipa sifa hiyo, Mwenye Ezi Mungu katika Qurani anasema: {Kisha watarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, Mola wao wa Haki. hakika, hukumu ni yake. Naye ni Mwepesi kuliko wote wanao hisabu.} 3

Muumba Mkamilifu ni Mola wa Haki asiyepingika, na dalili ya kuwa Yeye ni Mola wa Haki, kule kuthibitika kwake katika zama zote bila ya kuwa na mabadiliko yeyote katika Dhati yake. Na kwa kutokana na kuwa Yeye ni Mola wa Haki, hivyo basi Mahakama yake nayo huwa ni Mahakama ya Haki.

MIZANI YA HAKI MBALI MBALI ZA JAMII

Wanaadamu kwa kutokana na hali mbali mbali walizo nazo, huwa hawawezi kuwa na Haki zilizo sawa, na Mahakama ya Kidunia pamoja na Mahakama ya Muumba Mkamilifu huwa haziwezi kutoa huku ziendazo sawa kwa watu wote bila ya kuzingatia uwezo wa watu hao unavyo tofautiana.

Kuna aina mbli kuu za mambo yanayoweza kuwatofautisha Wanaadamu, nazo ni kama ifuatavyo:
1- Maumbile:
Tofauti za kimaumbile kutoka mtu hadi mtu, huwa ni zenye kujitokeza katika hali mbali mbali, kama vile hali ya utendaji au hali ya upangaji wa mambo tofauti. Mtu asiyesoma kwa kutokana na udhaifu fulani aliyo nao hatoweza kuwa ni mpangaji mzuri wa mambo fulani ya Kisiasa au Kiuchumi, na Mja mzito naye hatoweza kuwa na jukumu la kubebeshwa vitu vizito hali akiwa katika hali kama hiyo.

2- Cheo au sifa maalumu:
Bila shaka mtu anaposifika kwa sifa fulani, mtu huyo huwa anatofautiana na watu wengine wasiokuwa na sifa hiyo, kama vile mtu kupata sifa ya kuitwa "mume" baada ya kuowa, au mtu kupewa sifa ya "Udereva" kwa kutokana na kazi yake, sifa zote ambazo watu huwa ni wenye kusifika nazo kwa kupitia ukweli wa mabo yalivyo, huwa zinawatofautisha watu hao na watu wengine waliomo ndani ya jamii zao.

Kwa kutokana na vigao hivyo viwili tulivyovitaja hapo juu, kuku tukizingatia kuwa, sifa anazoweza kusifika nazo Mwanaadamu, zinawe kua ni sifa za mpito au ni sifa za daima, kwa msingi huu basi, hapa tunaweza kuigawa Haki katika vipengele viwili, navyo ni kama ifuatavyo:
1-Haki iliyo thabiti
2-Haki inayokubali kuhama (Haki ya mpito)
Haki thabiti: ni ile Haki isiyokubali kuhama, kutokubali kuhama kwa Haki hii kumesababisha na hali ya sifa hiyo ilivyo, kama vile mtu kuwa ana sifa ya Uwalimu, mtu mwenye sifa hii atakuwa na Haki ya uwalimu isyokubali kuhama katika hali yeyote, na hata kama mtu huyo atakuwa ameshashindwa kusomesha, lakini bado mtu huyo atakuwa ni mwenye kupewa sifa hiyo ya uwalimu, au sifa ya ujenzi, iwapo mtu atakuwa na sifa hiyo, mtu huyo hata kama atakuwa amesha acha kujenga, bado mtu huyo ataitwa ni mjenzi, sina haja ya kutoa dalili zilizosababisha sifa za watu hao kubakia katika hali mbali mbali, kwani kufanya hivyo kutarefusha maneno na kutatuchelewesha kuifikia natija tuliyo ikusudia kuifikia.

Mfano mzuri zaidi wa aina hii ya Haki, ni Haki ya ubaba au umama kwa mtoto, Haki hii haitaweza kufutika katika hali ya aina yeyote ile, hata kama baba au mama wa mtoto huyo wataukataa wadhifa wao, bado hilo halitokuwa ni dawa ya kuwafanya wao wasiwe wazee wa mtoto huyo.

Haki inayokubali kuhama ni ile Haki yenye kufuatana na sifa za mpito au sifa za hiyari, sifa ambazo mtu huwa ana uwezo kujivika au kujivua sifa hizo, kama vile "sifa ya mtu kuwa ni mume wa bibi fulani" sifa hii humfanya kila mmoja kati ya mume na mke kuwa na Haki maalumu, lakini sifa hii yawezekana kuwa ni sifa ya mpito, hivyo basi wakati wowote ule ambao mtu ataamua kujivua sifa ya kuwa yeye ni mume, hapo basi ataondokewa na Haki zate alizokuwa nazo mwazo wakati alipokuwa akisifika na sifa hiyo.

UCHAMBUZI

Katika Ulimwengu tuliyo nao kila kitu huwa kina Haki yake maalumu kwa kutokana hali ya kitu hicho kilivyo, kwa mfano Jaa (jalala) halitakiwi kuwepo karibu na maisha ya Wanaadamu, na Haki ya Jaa ni kukaa kando ya mji. na viwanda mbali mbali huwa havina Haki ya kujengwa karibu na maisha ya Wanaadamu, bali vinatakiwa kujengwa nje ya miji ili kuepusha madhara yanayoweza kusababishwa na viwanda hivyo Kikemia, hii ni kwa upande wa vitu visivyo na uhai.

Vitu vyenye uhai navyo huwa vina Haki zake maalumu, na Haki ya kwanza ya vitu hivyo, ni Haki ya kuishi. Haki ya kuishi ni Haki ya kila chenye uhai, hii ni Haki ya kiujumla, na Haki hii huwa haibagui kitu wala kukivua kitu fulani chenye uhai katika Haki hiyo ya kuishi. Lakini Haki hii inaweza kutumiwa zaidi na kiumbe fulani kuliko viumbe wengine, jambo ambalo linatokana na umuhimu wa kiumbe huyo aliyo nao.

Tukiangalia maisha ya wanyama tutakutia kuwa maisha yao ni yenye umuhimu zaidi kuliko maisha ya baadhi ya mimea au mimea yote, jambo ambalo linatokana na hisia walizonazo wanyama hao. Wanyama kwa kutokana na nafasi waliyo nayo huitumia mimea kuwa ni kama njia ya kudumisha maisha yao, wanyama mbali mbali wanaokula mimea, huwa wanafanya hivyo kwa kutokana na hisia za kimaumbile walizonazo, hisia ambazo huwa zinawafahamisha kua mimea ilioko katika ardhi hii ni Haki yao kuitumia bila ya kubughudhiwa, na kwa upande wa wanyama wenye kuwinda wenzao, nao pia huwa wana hisia za kimaumbile zinazowaongoza katika kuendeleza maisha yao, na kuwinda kwao kwa ajili ya maisha yao huwa ndiyo Haki kwao kwa ajili ya maisha yao, kwa lugha nzuri zaidi maisha haya ya Kidunia ambayo tumo ndani yake, tunaweza kuyaita kuwa ni "maisha ya kula nikule".

Wanaadamu nao kwa kutokana na ubora wao, huwa wanatumia njia mbali mbali za kuwawezesha kuishi katika maisha yaliyo bora, nao basi kwa ajili ya kudumisha maisha yao huwa wana Haki ya kuvitumia vitu vilivyomo katika ardhi hii au Ulimwengu. Lakini Wanaadamu huwa wana tofauti na wanyama katika kizijenga Nafsi zao, kwani wanyama huwa hawana hiyari wala uhuru wa chaguo katika ukamilikaji wa maumbile yao, na si kitu rahisi kuweza kumkuta kuku mwenye sifa za mbwa, au za mnyama mwengine, bali siku zote kuku huwa na sifa za kuku.

MJENGEKO WA MWANAADAMU KIMAADILI

Mwanaadamu ni kiumbe asiyetabirika kimatendo, na kila mmoja kati ya Wanaadamu huwa anatofautiana na wengine katika kukabiliana kwake na mambo mbali mbali, kwa mfano: Iwapo iwapo wewe utakuwa na shida fulani, na ukaamua kuomba msaada kutoka kwa watu tofauti, hapo basi kila mmoja utamuona anakabiliana na wewe katika hali tofauti na wengine, au iwapo katika jamii kutatokea msiba au neema maalumu, kila mmoja kati ya wana jamii wa jamii hiyo huwa anatofautiana na mwengine kimtazamo na kimatendo kuhusiana na msiba au neema hiyo ilioko katika jamii hiyo. Tofauti hizo tulizozizungumza hapa huwa zinasababishwa na hali mbali mbali walizokuwa nazo watu wenye kuishi katika jamii moja.

Mwanaadamu katika kujengeka kwake, anaweza kuathiriwa na mambo mbali mbali, kama vile jamii pamoja na wazazi walio mlea Mwanaadamu huyo. Lakini bado jamii pamoja na malezi ya wazee hayatokuwa ni sababu tosha za kumjenga Mwanaadamu katika sifa maalumu, bali ujengekaji wa Mwanaadamu huwa unategemea zaidi matakwa na uhuru wa Mwanaadamu huyo unavyotumika katika kuyachagua malengo anayoyataka kuyafikia.

Si jambo linalokubalika katika jamii ya Wanaadamu mtu kudai kuwa yeye mwenyewe hakuwa na hiyari wala uhuru wa kujiainishia malengo yake ya baadae, hivyo basi nafasi mbali mbali za jamii huwa ni zenye kuainishwa na wana jamii wenyewe, na kila mmoja kati yao huwa ana uhuru kamili wa kuijenga Nafsi yake na kuipa sifa maalumu Nafsi hiyo, lakini vile vile kwa upande mwengine, kunaweza kukapatikana vizuizi mbali mbali ambavyo vinaweza kumfanya mtu ashindwe kuyafikia malengo yake aliyo jiwekea.

Vizuwizi mbali mbali vinavyoweza kutokea katika kumnyima mtu maendeleo mbali mbali, vinaweza kuapatikana katika hali mbali mbali. Wakati mengine mhusika wa vizuwizi hivyo huwa ni Mwanaadamu mwenyewe, na wakati mwengine vizuwizi hivyo husbabisha na matokeo mbali mbali. Hivyo basi iwapo mtu atahusika kwa namna moja au nyengine katika kujitokeza vizuwizi vya maendeleo yake, hapo basi itampasa azikubali gharama zote na maafa yote yatakayomkumba bila ya kuwalaumu wengine. Wakati mwengine mtu anaweza kukabiliwa na vizuwizi, lakini vizuwizi hivyo vikawa vimesababishwa na mtu fulani, katika hali kama hiyo lawama zote huelekezwa kwa yule aliyesababisha kuwepo kwa vizuwizi hivyo, na yeye ndiye atakyewajibika kubeba gharama zote zilizosababishwa na vizuwizi hivyo.

HAKI KATIKA HALI MBALI MBALI

Neno Haki kama tulivyoona hapo mwanzo kuwa, neno hili ni lenye maana ya kuthibitika kwa kitu fulani, kama ukweli wa kitu hicho kilivyo. Hii ndiyo maana halisi ya neno Haki, lakini kinachotakiwa kufahamika hapa ni kwamba, si kila mahala mtu anaweza kusema Haki au kuisimamisha Haki, bali Haki inaweza kuepukwa katika hali fulani ili kuweza kuyafikia malengo makubwa zaidi yanayo tarajiwa kufikiwa. Ninaposema kuwa Haki yaweza kuepukwa katika hali fulani, huwa simaanishi kuwa iepukwa Haki na itawalishe dhuluma na batili, bali ninakusudia kuwa, kunawezakana kukatokea mtu fulani ambaye ana Haki ya kuzuiliwa kufanya jambo fulani, lakini kwa kuzingatia faida maalumu inayoweza kupatikana baada ya mtu huyo kuendelea na jambo hilo, hapo basi Akili huwa zinakubali kumruhusu mtu huyo aendelee na jambo hilo.

HAKI NA HISANI

Kumfadhili mtu kuliko vile anavyostahi kupewa huwa ni kumfanyia hisani, na wala kumfadhili huko huwa hakumaanishi kuwa yeye amepewa Haki yake itakikavyo, Muumba Mkamilifu katika Qurani anasema: {Hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha kufanya uadilifu, na hisani, na kuwapa jamaa; na anakataza uchafu, na uovu, na dhulma. Anakuwaidhini ili mpate kukumbuka.} 4 Viongozi wa jamii ni lazima wafahamu kuwa, si kila mahala kunatakiwa kutendwa mambo kwa Haki bila ya kupunjwa au kuzidishiwa mtu Haki yake, bali wakati mwengine kumpunja mtu kitu fulani huwa ndiyo kumtendea Haki, nikitowa mfano: kwa mtu mwenye maradhi ya sukari kumpunja mtu huyo sukari huwa ndiyo Haki ya mtu huyo, ingawaje mara nyingi watu wa aina hii huwa ni wakaidi na ni wenye kujihisi kuwa wanadhulumiwa, hasa hasa iwapo mtu mwenye magonjwa hayo atakuwa ni mtu mwenye umri mkubwa, lakini kutowatii watu kama hao katika kuwapa Haki sawa na wengine katika masuala ya utumiaji wa sukari, huwa ni manufaa yao pamoja na familia zao, pia kuwafanyia hivyo huwa ndiyo Haki yao. Vile vile wakati mwengine huwa kunahitajia mtu kumpa nyongeza zaidi kuliko Haki yake ilivyo, na huko huwa ndiko kunakoitwa "kumfanyia mtu hisani".

UADILIFU, HAKI NA HISANI

Siku zote kila jamii huwa ina sheria maalumu zilizopangwa na viongozi wa jamii hiyo, au kupangwa na Muumba Mkamilifu. Katika suala la upangaji wa sheria na kanuni mbali mbali, huwa kunazingatiwa masuala mbali mbali, miongoni mwa masuala yanayozingatiwa katika upangaji wa sheria, ni faida za kijamii pamoja na faida za reja reja zinazoweza kuwafaidisha wanajamii hao kiujumla na kireja reja.

Sheria zinaweza kugawika katika vipengele tofauti, na katika ugawikaji huo wa sheria, huwa kuna zile sheria ambazo zinaweza kutiliwa mkazo zaidi kuliko nyengine. Utiliwaji mkazo wa sheria fulani huwa unazingatia uzito wa faida za sheria hizo.

Jamii kuwa na sheria fulani huwa hakumaanishi kuwakandamiza wanajamii wa jamii hiyo, bali huwa kunaitaka jamii hiyo iishi katika utaratibu maalumu uwezao kuiweka salama jamii hiyo. Mwana sheria wa jamii fulani huwa halazimiki kuitumia fimbo ya sheria katika jamii bila ya kuzingatia hali ya wanajamii wa jamii hiyo walivyo. Wanajamii nao wanatakiwa kufahamu kuwa, ni Haki ya kila mmoja kuzijua sheria za nchi anayoishi ndani yake. Viongozi nao wanatakiwa kuhakikisha kuwa sheria zilizopangwa na viongozi wa nchi, ni zenye kwenda sawa na hali ya wananchi wa nchi hiyo. Kumhukumu mtu mwenye njaa kwa tuhuma ya wizi huwa hakukubaliki iwapo mtu huyo atakuwa ni mwenye njaa ya kifo, na Uislamu nao katika hali ngumu inayoweza kumkuta Mwanaadamu, huwa umetoa ruhusa hata ya kula mfu, hii ni kwa kuzingatia hali ya mambo yalivyo.

Haki na Uadilifu huwa kunamaanisha maana ya kukiweka kila kitu katika sehemu yake, hivyo basi sheria huwa hazimlazimishi mwana sheria kuzitumia sheria hizo kiholela, bali mwana sheria hulazimika kutumia uadilifu katika kutoa sheria kwa ajili ya mtu fulani kwa jinsi ya hali ya mtu huyo ilivyo. Makusudio hasa ya ukurasa huu ni kutaka kusema kuwa, hivi leo katika jamii mbali mbali huwa kunatungwa sheria mbali mbali, lakini iwapo sisi tutakaa na kuzizingatia sheria hizo, tutazikutia sheria hizo kuwa ni zenye kuwahusu wachache tu miongoni mwa wanajamiii waliyotungiwa sheria hizo. Na sheria hizo huwa ni zenye kuwakandamiza wengi waliohusishwa ndani ya sheria hizo.

Upangaji wa sheria hautakiwi kuliangalia jopo fulani la wanachi na kulipuuza jopo jengine, kwa mfano leo sisi tunaweza kuwambia watu waanze kulipia ada ya maji, lakini je sheria hii inatakiwa kuwahusu wote miongoni mwa wanajamii yetu, bila hata kuwavua mafukara na wasiojiweza? hii ni kwa upande mmoja, kwa upande mwengine serikali ni lazima iwatambue mafukara wa jamii yake pamoja na kuwawekea mchango maalumu utakaowawezesha kuishi kwa salama ndani ya jamii zilizo jaaa msokotano wa kula nikule, lakini leo mara nyingi wapangaji wa sheria huwa wanaangalia tu, ni kiwango gani cha fedha kinachoweza kukusanywa kutoka katika kodi mbali mbali, bila ya kuzingatia hali za watowaji wa kodi hizo. Kweli kabisa kuwa ni Haki ya kila mmoja wetu kuisaidia nchi yetu kimaendeleo, lakini si Haki kuwa watu wote waamrishe kuwa na malipo ya hali moja katika kutowa kodi mbali mbali.

Kusifika kiongozi wa nchi au kiongozi wa jamii fulani kuwa ni muadilifu, huwa kunamaanisha kuwa, kiongozi huyo huwa ni mtendaji wa kazi zake kwa kuuangalia haili ya jimii yake ilivyo, na mtu muadilifu huwa si mwenye kujivutia upande wake, bali huwa ni mwenye kuwatakia wengine kheri hata kuliko anavyojitakia yeye mwenyewe, na hapo ndipo mtu huyo anapoweza kulipa hisani za wale waliyomchunuka kwa kumpa kura zao.

Hisani ni sifa kubwa zaidi kuliko uadilifu kwani hisani huwa haiangalii hali ya mtu alivyo, bali wakati mwengine hali halisi huwa inaonyesha kutostahiki mtu kukirimiwa, lakini kwa kutokana na mtu kuwa na hisani utamuona mtu huyo kumkirimu asiyestahiki kukirimiwa.

TAKRIMA MBALI MBALI

kumkirimu mtu huwa ni moja kati ya njia zinazotumika katika kumlainisha mtu kitabia na kimwenendo, hivyo basi ni jambo la kuingia akilini kua kila mmoja kati yetu awe ni mwenye kuzingatia pale anapopata takrima kutoka upande fulani. Sio kila takrima yaweza kuhesabika kuwa ni takrima, bali wakati mwengine takrima hua ni hadaa ya kumhadaa mwengine ili kuweza kuyafikia matakwa maalumu.

Mwenye Ezi Mungu katika Qurani katika kisa cha Nabii Suleimani (a.s) anasema: {Basi (Hud-hud) akakaa si mbali na akasema: Nimegundua usilo gundua wewe, na ninakujia hivi kutoka nchi ya Sabai, na nakuletea khabari za yakini.} {Hakika mimi nimemkuta mwanamke anawatawala, naye amepewa kila kitu, na anacho kiti cha enzi kikubwa.} {Nimemkuta yeye na watu wake wanalisujudia jua badala ya Mwenyezi Mungu; na Shet'ani amewapambia vitendo vyao na akawazuilia Njia. Kwa hivyo hawakuongoka.} {Na hawamsujudii Mwenyezi Mungu ambaye huyatoa yaliyo fichikana katika mbingu na ardhi, na anayajua mnayo yaficha na mnayo yatangaza.}

{Mwenyezi Mungu - hapana mungu ila Yeye, Mola Mlezi wa A'rshi tukufu..} {Akasema (Sulaiman): Tutatazama umesema kweli au wewe ni miongoni mwa waongo.} {Nenda na barua yangu hii na uwafikishie, kisha waache na utazame watarejesha nini.} {(Malkia) akasema: Enyi wahishimiwa!Hakika nimeletewa barua tukufu.}

{Imetoka kwa Sulaiman nayo ni: Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.} {Msinifanyie jeuri, na fikeni kwangu nanyi mmekwisha kuwa wenye kusalimu amri.} {Akasema: Enyi wahishimiwa! Nipeni shauri katika jambo langu hili, kwani mimi sikati shauri yoyote mpaka mhudhurie.} {Wakasema: Sisi ni wenye nguvu na wakali kwa vita; na amri iko kwako, basi tazama ni nini unaamrisha.} {Akasema: Hakika wafalme wanapo uingia mji wanauharibu, na wanawafanya wale watukufu wake kuwa wanyonge. Na hivyo ndivyo watendavyo.}

{Lakini mimi nitawapelekea zawadi, nami nitangoja watakayo rudi nayo wajumbe.} {Basi alipo fika (mjumbe) kwa Sulaiman, alisema (Sulaiman): Hivyo ndio nyinyi mnanisaidia kwa mali? Aliyo nipa Mwenyezi Mungu ni bora zaidi kuliko aliyo kupeni nyinyi. Lakini nyinyi mnafurahia hii zawadi yenu.} {Rejea kwao! Kwa yakini sisi tutawajia kwa majeshi wasio yaweza kuyakabili. NaHakika tutawatoa humo na hali wao wamekuwa madhalili na wanyonge.} 5 Kukisimulia kisa hichi cha Nabii Suleiman (a.s), hakukuwa ndiyo lengo hasa la mazungumzo haya, lakini nilikuwa nikitaka tu kuonyesha kuwa, sio kila zawadi mtu huwa ni mwenye kutunikiwa bila ya kuwepo malengo maalumu, na kwa lugha nyengine ni kwamba, siku zote mtu huwa hatoi kitu bila ya kuwepo malengo fulani, lakini la muhimu kwa mtunukiwa ni kule kuyafahamu malengo ya takrima aliyo kirimiwa. Mara nyingi takrima ya mara moja mbili huwa ndiyo isababishayo maudhi ya daima, au maumivu yasiyoweza kusahaulika. Shauku ya kutaka kutunukiwa au kupigwa na bumbuwazi kwa kupata tunuko mbali mbali, kunaweza kukaleta maafa ya kibinafsi pamoja na maafa ya kijamii.

Ngao bora ya kuepukana na madhara kama hayo ni kuifahamu Haki kabla ya kupendezwa na sura ya mdai Haki, au mwenye kudai kuwa yeye ndiye mtetezi wa Haki. Fadhila, Takrima pamoja na kujichekesha ovyo hakutoweza kua ndiyo vipimo na vigezo vya kuwatambua wakweli au watetezi wa Haki.

Haki, Uadili, na Hisani haviwezi kupatikana kirahisi katika kila Nafsi ya Mwanaadamu asiye Mcha Mola wake, bali ni nadri kweza kumkuta mtu akashikamana na hayo bila ya kuwa na Ucha Mungu. Ninapolisema neno Ucha Mungu, huwa sikusudii tu Wacha Mungu wa Kiislamu, bali yawezekana kukapatikana Mcha Mungu wa Dini nyengine ambaye anaweza kuwa na sifa kama hizo, hii ni kwa kutokana na kuwa yeye ni mwenye kufungamana na imani maalumu inayomsukuma na kumlazimisha kuwa na uadilifu. Nikitoa mfano kuhusiana na hilo, hebu tuiangalie safari ya kwanza ya Masahaba wa Mtume (a.s.w.w). Baaya ya madhila kuwa ni yenye kupamba moto zaidi, Mtume (s.a.w.w) aliwaamrisha Waislamu kuukimbia mji wa Makka na kuelekea Uhabeshia (Ithiopia), huku Yeye akiwambia Waislamu hao kuwa huko Uhabeshia kuna mfalme asiyedhulumu watu, hii ni kwa sababu tu mfalme huyu alikua ni mfalme mwenye Imani thabiti ya Dini ya Kikristo.

Kwa haya tulioyatoa hapa itakuwa inapatikana natija isemayo kuwa Haki na Uadilifu ni vyenye kunamaanisha ile hali ya kukiweka kila kitu katika mahala pake kinapostahiki kuwekwa, ama Hisani huwa inamaanaisha kule kupewa mtu fadhila zaidi hata ya vile yeye apaswavyo kupewa, au kule kumlipa mtu kheri juu ya wema aliyokutendea. Na maana nyengine ya Hisani, ni kule kuwafadhili wengine bila ya kuwa na tamaa ya kitu fulani kutoka kwao, na katika maana ya kiujumla jamala neno hili huwa lina maana ya kutenda wema katika hali tofauti.

Mwenye Enzi Mungu katika Qurani anaposema : {Hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha kufanya uadilifu, na hisani,na kuwapa jamaa; na anakataza uchafu, na uovu, na dhulma. Anakuwaidhini ili mpate kukumbuka.} 6 Mola wetu natutaka kuwa waadilifu pamoja na kuwa na Hisani, na iwapo mtu atashikamana na hayo hapo ndipo atakapokuwa ni mtu apasaye kuiendesha jamii. Yawezekana mtu akawa ni Haki yake kutenda kitu fulani kwa mujibu wa sheria, lakini iwapo mwana sheria atakuwa ni mtu mwenye Hisani anaweza kumpunguzia uzito wa kazi aliyolazimika kuifanya kwa mujibu wa sheria. Kumlipa mtu ajira yake huwa ni Haki ya kila mtu, lakini kumharakishia mtu ujira huo huwa ni kumfanyia Hisani mtu huyo, hivyo basi jamii yaweza kuwa na maendeleo mazuri, iwapo wanajamii pamoja na viongozi wa jamii hiyo watakuwa ni wenye kushikamana na Haki, Uadilifu pamoja na Hisani.

Haki, Uadilifu pamojana na Hisani vinapaswa kutekelezwa katika hali tatu muhimu, nazo ni:
1-Haki, Uadilifu na Hisani katika Akili na Dhana mbali mbali.
2-Haki, Uadilifu na Hisani katika matendo.
3-Haki, Uadilifu na Hisani katika matamko mbali mbali.
Hisani Kidhana: huwa ni kule kuwadhania wengine mambo mema, hata kama wao hawastahiki kudhaniwa hivyo, na siyo kumfikiria kila asiyekuwa wewe kuwa ni mtu muovu, au ni mwenye kuwa na nia mbaya juu yako, hapa simaanishi kuwa watu wasiwe na tahadhari juu ya maadui zao, bali ninakusudia kusema kuwa, sio kila dhana huwa ni halali kwa wengine, kwani mara nyingi dhana huwa hazina misingi madhubuti ya dalili katika kuzithibitisha dhana hizo. Mwenye Ezi Mungu katika Qurani anasema: {Enyi mlio amini! Jiepusheni na dhana nyingi, kwani baadhi ya dhana ni dhambi. Wala msipelelezane, wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi. Je! Yupo katika nyinyi anaye penda kuila nyama ya nduguye aliye kufa? Mnalichukia hilo! Na mcheni Mwenyezi Mungu.Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupokea toba, Mwenye kurehemu.}7

Na katika suala la Haki na Uadilifu Kidhana na Kiakili ni kwamba, kwa kutona na kuwa siku zote Haki na Uadilifu huwa ni vyeny kutegemea uoni pamoja na dalili thabiti katika kusimamishwa kwake, hivyo basi Dhana zote zinatakiwa kuwa na uthibitisho kamili katika kudhaniwa kwake, na hiyo ndiyo maana ya Haki na Uadilifu Kidhana na Kiakili, kwani bila ya kuwa na dalili tosha, huwa ni vigumu kukiweka kila kitu katika sehemu yake ipaswayo kuwekwa kitu hicho, hali ya kwamba Haki na Uadilifu huwa kuleta maana ya kukiweka kitu katika hali yake ipaswayo kuwekwa, kama tulivyokwisha sema hapo mwanzo. Hali halisi ya mambo kidhahiri yaweza tu kumuweka mtu katika hali ya tahadhari na kumjenga katika dhana ya kutarajia kutokea matokeo fulani, lakini hali kama hiyo haiwezi kuwa ni sababu tosha ya kumhukumu mtu au kumchukulia hatua za kisheria mtu huyo, bila ya kuwa na dalili tosha ya kuthibitisha uhakika uliopo juu ya dhana iliyodhaniwa kutokea.

Haki, Uadilifu na Hisani kimatendo tayari kumeshapita ufafanuzi wake hapo mwanzo, na wala hakuna haja tena ya kuyakariri tena maelezo yaliopita hapo mwazo. Hisani kimatamko: huwa ni kule kuwazungumza wengine kwa mazungumzo ya kheri, na siyo kuwapaka matope wengine bila ya msingi wowote wa dalili. Ama Haki na Uadilifu kimatamko: huwa kunamaanisha kule kuuzungumza ukweli wa mambo yalivyo kwa jinsi hali na mahali pa mazungumzo hayo palivyo, wakati mwengine kuuzungumza ukweli kunaweza kukasababisha maafa mbali mbali, hivyo basi siyo kila mahala au mbele ya kila mtu huwa ni sawa kuuzungumza ukweli wa mambo mbali mbali, na huwa ni ujinga ulioje mtu kulizungumza kila alijualo bila ya kuzingatia faida na madhara ya hilo alinenalo, wanahekima wanatuambia kua "kila neno huwa lina pahala pake pa kuzungumzwa, na kila pahala huwa kuna namna yake ya mazungumzo".

HITIMISHO

Kwa kutokana na uchunguzi huu uliyoweza kuihusisha Haki katika uchunguzi wake, tunaweza kuibuka na natija isemayo kuwa: Mwana Haki pekee anayeweza kuitekeleza Haki ipaswavyo ni Mola Mtakatifu, hii ni kwa kutokana na kuwa, Haki ni yenye kwenda sawa na hali halisi ya mambo yalivyo, na hakuna mtu anayeweza kuyatambua kiundani mambo mbali mbali ya ulimwengu huu pamoja na hali halisi ya mambo hayo, isipokuwa Yeye tu Mola wa ulimwengu wote, hivyo basi yeyote yule atakaye taka kushikamana na Haki, basi na ashikamane na Mola wake Mtukufu. Natija nyengine tunayoweza kuipata kutokana na utafiti huu ni kwamba, kila mtu aliye karibu na Mola wake, huyo basi ndiye awezaye kuitambua Haki kwa makini zaidi, kwani yeye ndiye awezaye kujichotea elimu yenye uhakika zaidi kutoka kwa Mola wake, na si lolote linaloweza kumpatia mtu elimu ya ukweli na ya uwazi wa mambo mbali mbali, zaidi ya mtu kumcha Mola wake Mtakatifu. Mwenye Ezi Mungu Mtukufu anasema:

{Enyi mlio amini! Mnapo kopeshana deni kwa muda ulio wekwa, basi andikeni. Na mwandishi aandike baina yenu kwa uadilifu, wala mwandishi asikatae kuandika. Aandike kama alivyo mfunza Mwenyezi Mungu. Na mwenye deni juu yake aandikishe; naye amche Mwenyezi Mungu, Mola wake Mlezi. Wala asipunguze chochote ndani yake. Na akiwa mwenye kudaiwa ni mtu aliye pumbaa au mnyonge au hawezi kuandikisha mwenyewe, basi aandikishe mlinzi wake kwa uadilifu. Na mshuhudishe mashahidi wawili katika wanaume wenu. Ikiwa hapana wanaume wawili, basi mwanamume mmoja na wanawake wawili katika mnao waridhia kuwa mashahidi. Ili ikiwa mmoja wao akipotea, mmoja wao amkumbushe mwengine. Na mashahidi wasikatae waitwapo.

Wala msipuuze kuliandika deni likiwa dogo au kubwa mpaka muda wake. Hayo ndiyoHaki zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu, na ndiyo sawa zaidi kwa ushahidi, na vyema zaidi ili msiwe na shaka. Ila ikiwa ni biashara ya mkono-kwa-mkono baina yenu, basi hapo si vibaya kwenu msipo iandika. Lakini mnapo uziana wekeni mashahidi. Wala asitiwe matatani mwandishi wala shahidi. Na mkifanya hivyo basiHakika hilo ni kosa kwenu. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.} 8

Katika Aya hii Mwenye Ezi Mungu ameielezea misingi mbali mbali ya sheria za kijamii, misingi ambayo iwapo itazingatiwa, basi itaipa afueni jamii ya Wanaadamu, na kuifanya iishi katika hali ya kimaendeleo na Kibinaadamu, na mwishoni mwa Aya hii, Mola wetu anatutaka tuwe ni Wacha Mungu wazuri ili tuweze kufaidika kielimu. Ninamuomba mola wetu atusalimu salama na misukosuko mbali mbali ya Kidunia pamoja na misukosuko ya Akhera, na la mwisho kabisa ninamuomba Mola Mtukufu azijaaliye Thawabu za makala hii ziwaendee wazazi wangu pamoja na jamaa zangu wote walionifadhili kwa kunilea na kunipa fadhila mbai mbali. Aamina yaa Rabbal-aalamiin.

MAREJEO YA VITABU

1- Rejea kiitabu Dairatul-Maaarifi cha Faridi Wajdiy juzu ya 3 ukurasa wa 465.
2 -Rejea Tafsiri Majmaul-Bayaan kwenye tafsiri ya Aya 7 na ya 8 ya Suratul-Anfaal.
3 -Suratul-An-a'am Aya ya 62
4 -Suratu Nahli Aya ya 90
5 -Aya ya 22 hadi Aya ya 37 ya za Surati Naml
6 -Suratu Nahli Aya ya 90.
7 -Suratul Hujurati Aya ya 12.
8-Suratul Baqara Aya ya 282.

MWISHO WA MAKALA

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini