Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

MBAA MWEZI YA MWEZI WA DHAHABU

0 Voti 00.0 / 5

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

MBAA MWEZI YA MWEZI WA DHAHABU

UTANGULIZI
Asalamu alaikum wasomaji wetu wapenzi Ninamshukuru Muumba Mkamilifu kwa kuniwezesha kuandika Makala hii inayomhusu mmoja kati ya watu watukufu wa uma wetu huu. Nitajaribu kutoa ufafanuzi kuhusiana na mtukufu huyu kwa kadri ya uwezo wangu wa kielimu utakavyoniruhusu, kwani kuwazungumzia watukufu mbali mbali huwa kunahitajia kalamu iliyobobea wino wa kielimu, wino ambao utaweza kufafanua kwa upeo uliyo wa wazi kabisa, kuhusiana na sifa za watukufu hao, na kwa upande mwengine sisi tunapotaka kuzielezea sifa mbali mbali za watukufu wa uma huu huwa tunahitajia mimeremeto mbali mbali ya wino wenye kupendeza katika rangi nzuri za kielimu, na mimi mwenyewe sijihisi kuwa nina uwezo wa kuziakisi sifa za watukufu hao ipaswavyo, hii ni kwa kutokana na uchanga wa nuru ya kielimu niliyo nao. Ninatarajia kuwa jitihada zangu zitaweza kutoa angalau picha ya kivuli tu cha sifa za Mtukufu huyu ninaye mkusudia kumuelezea katika makala hii, na hata kama nitashindwa kutoa picha halisi ya Mtukufu huyu, pia sitaacha kumshuru Mola wangu kwa kunionyesha angalau kivuli tu cha picha halisi ya sifa zake. Ninamuomba Mola Mtukufu atuwafikishe katika mema na atuepushe na yale yote yasiyompendeza Mola wetu. Aamin.

VIDOKEZO
Kumsifu bibi Faatima (a.s) kunahitajia ufafanuzi wa kitaalamu, kwani jamii yetu bado haina uoni wa kutosha juu ya umuhimu aliyonao bibi huyu. Hivyo basi ninalazimika kabla ya kushika kalamu na kuanza kumzungumzia binti wa Mtume ajulikanaye kwa jina la Faatimatu Zahraa (a.s), kwaza kabisa kuuelezea umuhimu wa mwanamke katika ulimwengu wa Kiislamu. Ingawaje uwanja wa Makala Hii ni mdogo mno, kiasi ya kwamba sitokuwa na uwezo wa kuuelezea umuhimu wa mwanamke katika ulimwengu wa Kiislamu kwa urefu na mapana. Lakini jambo hili nitajaribu kulizungumzia katika Makala zangu nyengine zijazo. Lakini kufanya hivyo pia kwanza kabisa huwa kunahitajia taufiki itokayo kwa Mola wetu Mtukufu, nami sina budi kumuomba Yeye aniwafikishe katika uandishi wa Makala hiyo.

Jitihada zangu za kutoa maoni ya Uislamu juu ya mwanamke, zinatokana na kuyaona mataifa mengi pamoja na Dini mbali mbali zikijaribu kuelekeza tuhuma mbali mbali kwenye Dini ya Kiislamu, huku mataifa hayo yakidai kuwa Uislamu unampuuza mwanamke na haumpi haki zake ipaswavyo.

Hatuwa ya kumuhesabu mwanamke kuwa ni kiungu muhimu katika ulimwengu wa Kiislamu, ni moja kati ya hatuwa muhimu za kumtukuza mwanamke na kumrudishia cheo chake cha Kibinaadamu kama walivyo wanaume. Ni jambo la wazi kabisa kuwa mwanamke kabla ya Uislamu alikuwa akihesabika kuwa ni kiumbe nuhusi katika jamii ya Wanaadamu. Baada tu ya Uislamu kuweka mguu wake katika ardhi hii, Uislamu huo ulitumia kila njia ili kumrudishia mwanamke hadhi yake ya asili, huku ukimuhesabu kuwa yeye ni kiumbe anayepaswa kuheshimiwa na kupewa heshima kamili, kama vile wanaume wapewavyo heshima hiyo. Hivyo basi tuhuma zote zinazoelekezwa kwenye Dini ya Kiislamu haziwezi kuwa ni sahihi, kwani kila mmoja wetu anazitambua wazi juhudi zilizofanywa na Uislamu bila ya ubaguzi wa aina yeyote, katika harakati za kuzijenga jamii za Wanaadamu kifira, kielimu na kitamadini.

UMUHIMU WA MWANKE KATIKA UISLAMU
Mawingu ya ujinga na ngiza la ukafiri lilikua limetanda katika eneo zima la Makka, huku nchi nyengine nazo zikiwa zimo katika aina mbali mbali za ujinga wa kuabudu asiyekuwa Mwenye Ezi Mungu. Jua la utume lilichomoza na kung'aa dunia nzima, baada ya kipindi kichacche tu, sifu za Mtume (s.a.w.w) zikawa zimeenea kila mahala, na kwa juhudi mbali mbali zilizofanya na wafuasi wa Mjumbe huyu, Uislamu akaenea na kutambulikana kwa haraka mno.

Bila shaka Uislamu ulihitajia himaya mbali mbali, ili kuupa nguvu Uislamu huo pamoja na kuidumisha nuru yake njema kwa ajili ya kizazi kijacho. Kuuhifadhi Uislamu na kuuweka katika hali ya uslama, huwa kunahitajia mali, elimu ya kutosha pamoja na himaya itokayo kwa Mola Mkamilifu.

Katika Dini ya Uislamu mwanamke ni mwenye nafasi ya hali ya juu katika kuleta maendeleo ya Kidini na Kijamii, na kama tutazitupia macho baadhi ya kurasa za tarehe ya Kiislamu, tutamkutia mwanamke kua ndiye mtu wa mwanzo aliyetoa msukumo wa hali ya juu katika kuusogeza mbele Uislamu, kwani Mtume wetu (s.a.w.w) aliweza kupata msukumo wa hali ya juu kutoka kwa bibi Khadija kabla ya kuutangaza Uislamu aliyoamrishwa kuutangaza, na vile vile baada kuutangaza Uislamu huo. Kufariki kwa bibi Khadija kulimpa huzuni kubwa bwana Mtume (s.a.w.w), na jambo hilo linaonyesha wazi nafasi aliyokuwa ameishika bibi huyu katika Uislamu. Hii ni hatua moja ya mwanzo ya kudhihiri picha nzuri ya mwanamke katika kuuokoa na kuuendeleza Uislamu kwa njia moja au nyengine, jambo ambalo lilionekana hata kabla ya Uilsamu kutangazwa na kunea kwake.

FAATIMATU ZAHRAA (A.S)
Bibi Khadija hakuwa tu ni mwanamke aliyeutetea Uislamu, kisha akamuacha Mjumbe wa Mwenye Ezi Mungu auendeleze peke yake, bali alimzalia Mtume wetu (s.a.w.w) binti pekee aliyependwa na Mtume (s.a.w.w) kuliko watu wote wa umaa huu.

Kama tulivyosema hapo mwanzo kua, kuuendeleza na kuutetea Uislamu, kunahitajia elimu ya kutosha ili kulifanikisha jambo hilo. Hivyo basi kuzaliwa kwa bibi Faatimatu Zahraa (a.s) kulikuwa ni bishara njema kwa Waislamu, kwani kulelewa kwake bibi huyu katika nyumba ya Mtume yeye pamoja na mumewe ambaye ni Ali bin Abi Taalib, kuliweza kuwawivisha na kuwakomaza vizuri kielimu kuliko wengine wote wanaodaiwa kuwa na uwezo huo, katika zama za Mtume (s.a.w.w) na hata katika zama zilizokuja baadae.

NAFASI YA NASABA KWA WAARABU
Waarabu katika zama zilizopita walikuwa wana tabia ya kujinasibu kwa kabila zao walizo nazo, na kila mmoja alikuwa akijaribu kuisifia kabila yake kwa sifa mbali mbali, na kama wengi wanavyotambua kuwa katika jamii ya Kiarabu, huwa kuna suala la utabaka wa kikabila, kiasi ya kwamba ndani ya jamii hii ya Kiarabu, huwa kuna makabila yanayoheshimika na kupewa daraja ya juu, na kuna yale makabila yenye daraja za chini. Wengi katika zama za zamani walijihesabu kuwa ndiyo mabwana huku kuwaona wengine kuwa ni watu duni kwa kutokana na kabila zao. Mashairi mbali mbali yalikuwa yakitungwa kwa ajili ya kuzikweza kabila fulani, au nasaba fufali. Zawadi mbali mbali nazo watu walikuwa wakijipatia kwa ajili ya kutunga mashairi yenye kuwasifu viongozi wa makabila mbali mbali, ima kwa kuwaveka vilemba vya ukoka, au kuwasifu kwa sifa za ukweli ziendazo na ukweli wa tabia zao zilivyo, ilimradi tu kuwaridhisha viongozi hao, ili kuweze kunyofoa fungu lililo nono kutoka katika mifuko ya viongozi hao.

NASABA YA FAATIMATU ZAHRAA (A.S)
Si mara nyingi kuweza kuwakuta viongozi wa jamii kuukubali ukweli, au kuukubali udhaifu walio nao, ima kwa kutokana na uroho wa mali au kwa kutokana na uroho wa madaraka. Hivyo basi kila panapotokea mtu anayetaka kuikoa jamii fulani kutokiana na matatizo mbali mbali, kwanza kabisa hukabiliwa na mashambulizi yatokayo kwa viongozi wa jamii hiyo. Silaha kubwa iliyokuwa ikitumika katika kuzuvunja kasi za watetezi mbali mbali wa jamii, ilikuwa ni kuwapaka matope kwa kutokana na hali zao za kijamii walizokuwa nazo. Lakini ilikuwa si jambo rahisi kwa viongozi wa zama za Mtume (s.a.w.w) kweza kupata sababu ya kumpaka matope Mtume huyu, hii inatokana na kuwa Yeye ni mwenye kabila kubwa inayoheshimika mbele ya Waarabu, na wazee wake walikuwa ni wenye kusifika kwa mali pamoja na nasaba. Na kizazi chake nacho hakikuweza kubughudhiwa katika masuala kama hayo, kwa kutokana na ukamilifu wa kila hali waliokuwa nao, na hii ilikuwa ni himaya maalumu waliyokuwa nayo watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.w).

Bibi Faatiama (a.s) alitukuka kinasaba na kikabila, na vile vile alisifika kwa sifa njema ya upendo, naye ndiye kilele cha tabia na upendo. Yeye kwa upande wa nasaba ni mwenye umashuhuri wa kilimwengu, kwani baba yake ndiye Mtume wa uma huu, na mama yake ni miongoni mwa wanawake bora wa ulimwengu huu, na vile vile mumewe ni Ali (a.s) mtu ambaye amepewa sifa mbali mbali na Mtume (s.a.w.w), na kizazi cha Faatimatu Zahraa (a.s) kilikuwa ni Hasan na Husein pamoja na Zainabu Kubraa na Zainabu Sughraa. Watoto ambao walipikika vya kutosha kielimu na kiimani, basi wapi unaweza kukipata kizazi bora kama kilivyo kizazi cha Faatimatu Zahraa (a.s). Nani katika uma huu ambaye baba yake ni mtume, mumewe ni Imamu wa Waumini, na wanawe ni Maimamu wa uma huu? Si mwengine bali ni Faatimatu Zahraa (a.s), basi wapi unaweza kuipata nyumba iliyo wakusanya watu wema na watukufu, kama ilivyowakusanya nyumba ya Faatimatu Zahraa (a.s).

UTUKUFU WA BIBI FAATIMATU ZAHRAA (A.S)
Si kila mtu anaweza kuutambua utukufu wa bibi Huyu, na ni wachache tu ambao wanaweza kuutambua utukufu wake. Uchahe wa watu wanaoweza kumtabua mwanamke Huyu unasababisha na kule kule kulipa mgongo suala la kuwafanyia mapenzi watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.w). Lakini si haba leo kuwaona baadhi ya wanachoni mbali mbali wakilitilia uzito suala la kumtangaza bibi Fatimatu Zahraa (a.s). Kwa kule kuzielezea baadhi ya sifa za bibi Huyu.

Maelezo yaliyopita hapo juu ni maelezo ya baadhi tu ya sifa za bibi Huyu, na kama tulivyosema kuwa, si kila mtu anaweza kuzitambua sifa za Faatimatu Zahraa (a.s), kwani sifa zake ni kama bahari isiyoweza kuogeleka. Na kulifahamu hilo kunahitajia kuitupia macho vya kutosha historia ya Kiislamu, mimi sitaki kuvutia upande wa Mahehebu fulani, bali ninataka tu kupata radhi za Mola wetu, kwani kumsifu mmoja kati ya Mawalii wa Mungu, ni moja kati ya matendo ya ibada. Na kuthibitisha hilo hebu basi tuziangalie Aya zifuatazo :
{Na mtaje Maryamu katika Kitabu, pale alipo jitenga na jamaa zake mahali upande wa mashariki.} 1
{Na mtaje katika Kitabu Ibrahim. Hakika yeye alikuwa mkweli, Nabii.} 2
{Na mtaje Musa katika Kitabu. Hakika yeye alikuwa ni mwenye kuchaguliwa, na alikuwa Mtume, Nabii.} 2
{Na mtaje katika Kitabu Ismail. Bila ya shaka yeye alikuwa ni mkweli wa ahadi, na alikuwa Mtume, Nabii.} 4
Hizi ni baadhi tu ya Aya zinazotuhimiza kuwataja Mitume (a.s) pamoja na Mawalii wa Mwenye Ezi Mungu, na mahimizo haya yanayotutaka sisi kuwataja watu kama hawa, huwa yanadhamiria kutoa picha halisi ya maisha pamoja na Ucha Mungu waliyo nao watu hao, ili kuwapa wengine changa moto ya kushikamana na Dini ya Mwenye Ezi Mungu, au wakati mwengine huwa kunakusudiwa kuonyesha hali ya subira waliyokuwa nayo watu hao, ili kutoa somo kwa wengine pamoja na kuwafanya wao waweze kushikamana na subira hiyo, na hilo ni kwa ajili ya manufaa ya Duniani na Akhera. Nami katika Makala hii sitaacha kumsifu binti wa Mtume wetu (s.a.w.w) kwa sifa zake zilizojaza nuru Duniani humu, na sitarajii kuufanya mdomo wangu kuwa ndiyo kurasa kuu za marejeo ya sifa hizo, bali nitatoa sifa hizo kwa jinsi ya tarehe ilivyomzungumza mtukufu Huyo.

Mtume wetu (s.a.w.w) anasema: {Ingelikuwa wema na uzuri vinaweza kuja kwa umbile la kibinaadamu, basi umbile Faatima (a.s) ndilo lingalikuwa umbile la wema huo, bali daraja ya Faatima (a.s) bado ni ya juu zaidi kuliko wema huo. Kwa hakika binti wangu Faatima ni mbora wa Wanaadamu waliyokuwamo juu ya ardhi hii kwa umbile lake na kwa dhati yake takatikatifu, na Yeye ni mwenye utukufu wa hali ya juu kabisa.} 5

Kuna wengi waliomsifu Faatima (a.s) kwa kutokana na utukufu aliyo nao na kusifiwa kwake hakuzingatii tu kuwa Yeye ni binti wa Mtume (s.aw.w), bali kunazingatia sifa za Ucha Mungu alizonazo, pamoja na jitihada zake za kuutetea Uislamu. Ibnu Sibaagh Al-Maalikiy anasema: {Faatimatu Zahraa (a.s) kuwa Yeye ni binti wa Mtume (s.a.w.w), huwa kunamtosha kumpa Yeye ufakhari, Faatima ni mwenye utakaso wa uzawa na ni bibi mwenye utukufu, na hilo ni jambo lililokubaliwa na Wanazuoni wote wa Kiislamu.} 6

Kumsifu Faatima (a.s) huwa ni changa moto ya kila Muislamu asiye na kasumba za Kimadhehebu, na Mwanachuoni huyu aliyemsifu Faatima (a.s) ni Mwanachuoni wa Madhehebu ya Imam Maalikiy (r.a). Lakini leo huwa kuna kasumba za kuonekana kila yule amsifuye mmoja kati ya watu wa nyumba ya Mtume, kuwa yeye ni mfuasi wa Madhehebu fulani, jambo ambalo limewafanya wengi kuwa na khofu ya kuwasifu watu hao, na hilo halionekani tu katika zama zetu za leo, bali katika zama zilizopita hali ilikuwa ni mbaya zaidi hata kuishinda hali ilioko leo. Lakini Muumini hatakiwi kuwaogopa watu, au kuipiga teke Haki kwa kuliogopa kundi fulani, isipokuwa iwapo mtu atakhofia kufikwa na madhara ya kupoteza roho yake au mali yake, hapo basi Dini itaweza kumpa ruhusa ya kutoidhihirisha imani yake.

Mtu kuitanguliza nafsi yake katika manufaa mbali mbali, huwa kunategemea hali halisi ya mambo yalivyo, kwani wakati mwengine mambo huwa magumu, kiasi ya kwamba mtu huwajibika kuitoa nafsi yake muhanga kwa ajili ya Dini yake, na Dini ndiyo inayo chukuwa jukumu la kutoa ufafanuzi kuhusiana na mambo hayo, pamoja na kumfahamisha Mwanaadamu wadhifa wake katika hali tofauti ambazo zinaweza kumsibu Mwanaadamu huyo. Mwenye Ezi Mungu akiwazungumzia wale watu wenye kuwakhofu Wanaadamu wenzao zaidi, kuliko hata wanavyomkhofu Mola wao anasema: {Je, huwaoni wale walio ambiwa: Izuieni mikono yenu, na mshike Sala na mtoe Zaka. Na walipo amrishwa kupigana, mara kundi moja kati yao liliwaogopa watu kama kumwogopa Mwenyezi Mungu, au kwa khofu kubwa zaidi. Na wakasema: Mola Mlezi wetu! Kwa nini umetuamrisha kupigana? Laiti unge tuakhirishia kiasi ya muda kidogo hivi! Sema: Starehe ya dunia ni ndogo, na Akhera ni bora zaidi kwa mwenye kuchamngu. Wala hamtadhulumiwa hata uzi wa kokwa ya tende.} 7

Mwanachuoni mwengine anayemsifu Faatima (a.s), ni Muhammad bin Talha Shaafiy, mwanachuoni huyu katika kauli yake anasema: {Kuwa makini na uizingatie kwa vizuri Aya ya (Mubaahala) 8 jinsi ilivyo pangika, na jinsi inavyoashiria utukufu wa daraja ya Faatimatu Zahraa (a.s), na jinsi gani bibi Huyu alivyokamata nafasi ya kati na kati katika Aya hii, hali akiwa yeye anatembea baina ya Mtume (s.a.w.w) na Ali (a.s), ili jambo hilo liwe ni ishara tosha kwa Wanaadamu juu ya kuuashiria utukufu aliyo nao bibi Huyu.} 9 Abbas Mahmuud Al-Aqqaad Al-Misriy anasema: {Katika kila Dini huwa kunapatikana mwanamke mkamilifu anayeheshimiwa na watu wote, kiasi ya kwamba mwanamke huyo huwa ni Aya na dalili waliodhihirishiwa Wanaadamu, wake kwa waume kutoka kwa Mola wao. Katika Dini ya Kikristo Mariamu ndiye mwanamke aliyeshika nafasi hiyo, na katika Uislamu nafasi hiyo imeshikwa na bibi Faatimatu Zahraa (a.s).} 10

MTAZAMO WA MUANDISHI
Hawa ni baadhi tu ya wanazuoni walio jaribu kuzizungumzia sifa za Faatimatu Zahraa, na kuna wengine wengi ambao hatukuwataja katika makala hii. Kuwataja watu mbali mbali waliothibitisha fadhila mbali mbali za Fatima Zahraa, hakumaanishi kuwa sisi ni wenye kuziegemea nadharia za watu hao tu, bali iwapo mtu atarudi katika vitabu mbali mbali, ataweza kuzikuta Hadithi chungu nzima kutoka kwa bwana Mtume mwenyewe (s.a.w.w) zinazomsifu bint wake.

Bila shaka Mtume hakuwa na jicho la upendeleo katika kuwasifu watu mbali mbali, wala yeye hakuwa akiwapenda watu wa nyumba yake kwa kutokana na upendeleo fulani, kwani Yeye ni muadilifu mwenye kukiweka kila kitu katika sehemu yake bila ya kudhulumu kitu. Tunachotakiwa sisi kukitambua ni kwamba, kuzaliwa kwa bint wa Mtume (s.aw.w) kulibashiriwa na Mwenye Enzi Mungu Mtukufu, kwa ajili ya Kumpoza moyo Mtume wake, pamoja kumfanya bint huyu kuwa ndiyo njia pekee ya kuudumisha Uislamu. Wengi huwa wanakejeli pale wanapowasikia wapenzi wa bint huyu wanapomsifia kwa sifa mbali mbali, hii huwa inatokana na kuto kuwa na ufahamu wa kutosha kuhusiana na utukufu aliyonao mtukufu huyu, kama nilivyoelezea hapo mwanzo. Lakini iwapo mtu atalifumbua jicho la akili yake juu ya Hadithi iliyopokewa katika vitabu mbali mbali vya Madhehebu tofauti isemayo: {Fatima ni kipande cha mwili wangu, basi atakaye muudhi yeye atakuwa ameniudhi mimi…}, hapo ataweza kufungukiwa na masuali mbali mbali yatakayomuongoza katika kumfahamu Bint Huyu mtukufu.

Wengine hujaribu kusema kuwa Yeye alikuwa ni kama walivyo wanawake wengine kitabia, lakini ukweli sio huo kwani kutofautishwa kwake na Mtume (s.a.w.w) huwa ni dalili tosha ya kuuonyesha ubora aliyo nao. Chuki na mafundo ya moyo waliokuwa nayo baadhi ya wale wenye maradhi ya Kimadhehebu hakutoweza kuzitia gizani Nyota zilizopambazukiwa na kila sifa isiyostahiki kusifiwa nazo, Nyota ambazo ziling'aa katika kila zama, na kila kulipochomoza wingu la dhulma mnga'ro wa nyota hizo uliweza kuliunguza wingu hilo la dhulma na kuliyayusha kwa ushupavu wake. Kuwanoa kitabia makhalifa dhalimu, hakutoweza kuzizima nuru za nyota hizo. Katika zama za baadhi ya viongozi kulitokea dhulma juu ya kizazi cha mtume, na ujinga wa kuto yafahamu hayo, hakotukuwa ndiyo sababu tosha ya kuyafuta matokeo hayo katika ukurasa wa taerehe. Kuwahesabu Ahlu-Bait kuwa ni kama watu wengine kielimu, kifadhila na kitabia, ni jambo lisilokubalika, hasa pale tunapozingatia kauli mbali mbali za viongozi mbali mbali waliouegemea mgongo wa Ahlul-Bayt kielimu, wanapoeleza ukweli wa mambo yalivyo. Mimi mwenye sioni sababu za kukiwekwa nyuma Kizazi cha Mtume (s.a.w.w) katika masula ya uongazi, na wala sioni sababu tosha ya kumuhesabu Muaawia kuwa ni Sahaba muadilifu.

Wengi huwa wanasema kuwa mambo yameshapita na maji yakimwagika hayazoleki, basi kuna haja gani ya kuyataja yaliyopita? Mimi kwa mtazamo wangu ninaona kuwa, ipo haja ya kuyatambua yaliopita, na kuyarithisha kwa wengine, ili iwe ni changa moto kwa kizazi chetu katika muelekeo wao wa kupambana na dhulma mbali mbali za madhalimu. La pili ni kwamba, kila mmoja kati ya Masahaba walikuwa ni wapokezi wa Hadithi mbali mbali, hivyo basi ni vizuri kuwatambua tabia zao pamoja na utiifu wao, jambo ambalo huwa ndilo linaloweza kuzipa riwaya zao thamani ya kuthaniwa au kuto thaminiwa kwa riwaya hizo. Si mara nyingi kuweza kumkuta mtu akazipuuza Hadithi zilizopokelewa na kizazi cha Mtume (s.a.w.w), hii inatokana na kuwa kizazi hicho ni chenye kuamainika kitabia na kimatendo, haidhuru mimi bado ningali katika hali ya mshangao pale ninapofungua vitabu mbali mbali, kwani si mara nyingi kuweza kupata Hadithi zilizopokelewa na kizazi cha Mtume (s.a.w.w) katika vitabu mbali mbali, mimi sitaki kuutia hatiani upande wowote ule wa Kimadhehebu kuhusiana na suala hilo, bali sitaacha kujilaumu mwenyewe kwa kutoweza kupata natija ya suala hilo ipaswavyo. Elimu busara hekima na tabia njema zimeweza kurikodiwa kutoka katika kizazi cha Mtume (s.aw.w), lakini yote hayo hayakuwa ni sababu tosha ya kuwatukuza watu hao, kwani hadi leo bado huwa kunapatikana aina mbali mbali za tuhuma kutoka katika sehemu mbali mbali.

Bado pingamizi zitaendelea kuyafunika mawimbi ya bahari za fadhila za watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.w), kwa kutokana na kupiga mbwizi kwetu na kuto vitowa vichwa vyetu nje ya bahari za wale tunaowadhania kuwa ni waadilifu wasiokubali kuingia dosari. Kuwatukana Masahaba nako, kutabakia kuwa ni ujinga wa wale wadhaniao kuwa ni wenye kuitengeneza jamii kwa kupitia matusi yao. Wengi wameusahau usemi wa Maimamu wao usemao:
{کونوا دعاه لنا بغير ألسنتكم }
Maana yake ni kwamba: {Kuweni walinganiaji wetu bila ya kuzitumia ndimi zenu}. Usemi huu unawataka watu wawe ni wenye matendo mema yawezayo kuwavutia wengine na kuwaingiza katika Uislamu, pasi na kua na haja ya kuwaita kwa midomo yetu. Kwani mara nyingi watu katika huwa hawaangalii nini unacho kisema, bali hua wanayaangalia matendo yako unayo yatenda, ndiyo maana leo ukawaona Wakristo kuwa ni wenye kufaulu zaidi katika kazi zao za kuilingania dini yao.

Watu wa nyumba ya mtume walikuwa wakizingatia mno suala la kushikamana na tabia njema, huku wakiwa wao ndiyo kilele katika utekelezaji wa mambo ya kheri, na suala hili haliwahusu tu wanaume katika jamii yetu, bali wanawake nao wanatakiwa kuwa katika mstari wa mbele juu ya kushikamana na tabia njema, kwani Fatimatu Zahraa (a.s), kwao ndio kigezo bora katika masuala ya utendaji mbali mbali wa kazi za jamii, hebu basi tujaribu kumsoma bint Huyu kwa makini zaidi ili tuweze kujipatia taaluma zaidi zitakazoweza kutupa ufundi wa kuwalea watoto wetu katika misingi ya Kibinaadamu, na hilo ndilo litakaloweza kutunufaisha na kutuongoza katika njia yenye maendelea na manufaa kwa wote.

Kurasa hizi chake hazikuweza kuhimili utukufu wa bint wa Mtume (s.a.w.w) ipaswavyo. Na iwapo sisi tuta taka kuzizungumzia sifa kamili za Faatima (a.s), basi hatutaweza kuzizungumzia kwa masiku mawili au matutu, bali kazi hii yaweza kuchukuwa miaka mingi sana bila kukamilika.

Ndugu wasomaji ninatarajia kuwa mumefaidika vya kutosha na makala hii, na vile vile mumeweza kupata ufunuo wa kiasi fulani kuhusiana na Mtukufu Huyu, hivyo basi iwapo mtagundua upungufu wowote katika makala, basi tambueni kuu jambo hilo limesababishwa upungufu wa wino wa marifa yangu. Ninamuomba Muumba Mtukufu awarehemu wazazi wetu kwa utukufu na baraka za Mtume na Aali zake (s.a.w.w). Aamin.
REJEO
1 - Suratu Maryam Aya ya 16.
2- Suratu Maryam Aya ya 41.
3- Suratu Maryam Aya ya 51.
4- Suratu Maryam Aya ya 54.
5- Faraaidi Simtaini juzu ya 2 kurasa wa 68
6- Al-Fusulil-Muhimma chapa ya Lebanon ukurasa wa 143.
7- Suratu Nisaa Aya ya 77.
8- Aya ya 61 ya Suratu Aali Imraan
9- Mataalibu Sauul chapa ya Iran ukurasa wa 6 hadi wa 7.
10- Kitabu Ahlul-Bait cha Taufiiq Abuu Aalam ukurasa wa 128

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini