VIZUIZI NA CHANGAMOTO ZA UMOJA
BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM
VIZUIZI NA CHANGAMOTO ZA UMOJA
Umoja wa umma wa Kiislamu ni lengo muhimu na aali ambalo wanafikra na maulamaa wa Kiislamu wamekuwa wakifanya jitihada kubwa tangu zama za awali za Uilslamu kwa ajili ya kufikia lengo hilo. Hivi sasa tumo katika Wiki ya Umoja kati ya Waislamu ambayo ilitangazwa na hayati Imam Khomeini kutokana na hitilafu za mapokezi kuhusu siku aliyozaliwa Mtume Muhammad (saw). Wiki hiyo inaanzia tarehe 12 hadi 17 Rabiul Awwal. Makala hii inazungumzia Umoja wa Umma wa Kiislamu, Vizuizi na Changamoto.
Umoja wa umma wa Kiislamu ni lengo muhimu na aali ambalo wanafikra na maulamaa wa Kiislamu wamekuwa wakifanya jitihada kubwa tangu zama za awali za Uilslamu kwa ajili ya kufikia lengo hilo. Hadi sasa kumetolewa fikra nyingi na kuitishwa vikao na mikutano chungu nzima kujadili kadhia ya udharura wa kuwepo umoja na mshikamano kati ya Waislamu wote.
Udharura wa umoja na mshikamano wa Kiislamu umesisitizwa mno katika maandiko ya kidini na dalili za kimantiki na kiakili. Hata hivyo inasikitisha kwamba Waislamu wanapokaribia kuungana na kuimarisha umoja na mshikamano wao hujitokeza vizuizi chungu nzima ambavyo kunahitajika juhudi kubwa, tadbiri na mwamko wa Waislamu ili kuweza kuviondoa na kukabiliana navyo. Baadhi ya vizuizi na vikwazo vya umoja wa Waislamu vinatokana na hitilafu za ndani ya umma wa Kiislamu japokuwa hapana shaka kwamba wakoloni na madola ya kibeberu daima yamekuwa yakifanya njama za kuzusha hitilafu na mifarakano katika umma wa Kiislamu.
Umoja na mshikamano wa umma wa Kiislamu ndio nguvu kubwa isiyoshindika ya umma huu ambayo inaweza kutumiwa na Waislamu kukabiliana na madola yanayoingilia masuala yao na kutaka kupora utajiri na maliasili zao. Pamoja na hao yote tunapaswa kuelewa kwamba lengo kuu la wakoloni na madola ya kibeberu ni kuuondoa Uislamu katika maisha ya kawaida na kuidhoofisha dini hiyo inayopambana na dhulma na uonevu ambayo daima imekuwa kizuizi kikubwa dhidi ya siasa za kibeberu na tamaa za madola kikoloni.
Maadui wa Uislamu wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali katika kuzuia umoja na mshikamano wa Kiislamu. Maadui hao hufanya jitihada za kutia chumvi na kukuza hitilafu ndogondogo za kimitazamo zinazotokea kati ya Waislamu na baadaye kuzitumia kwa ajili ya kuzusha mifarakano kati yao. Maadui hao hutumia hitilafu au tofauti za kimadhehebu, kilugha, kikaumu na kikabila na kadhalika kama nyenzo za kuzusha fitina na kuwatenganisha Waislamu. Ni wazi kuwa jiografia ya ulimwengu mkubwa wa Kiislamu inajumuisha makabila, kaumu, lugha, madhehebu na mataifa tofauti. Hata hivyo tofauti hizo za kimaumbile au hitilafu ndogondogo hazipaswi kuwa tatizo kubwa au kizuizi cha umoja na mshikamano.
Katika upande mwingine nchi za Magharibi zinaanzisha au kuhamasisha makundi yenye misimamo ya kupindukia na bandia katika ulimwengu wa Kiislamu kwa lengo la kuzuia umoja na mshikamano wa Waislamu. Kwa mfano sisi sote tunaelewa ni kwa kiwango gani makundi mawili ya Kiwahabi na Kibahai yalivyowasababishia Waislamu matatizo na mashaka makubwa mno katika kipindi cha karne mbili zilizopita.
Historia ya sasa ya dunia ya Kiislamu inaonesha kwamba madola ya kikoloni mara nyingi huwatumia watu ambao kidhahiri ni Waislamu lakini hakika yao ni watu waliopotoka na wanaotumiwa kuzusha mifarakano na hitilafu katika umma wa Kiislamu. Watu wa aina hii wamekuwa wakijitokeza wakiwa na anwani na sura mbalimbali, lakini sifa inayowakutanisha pamoja wote ni kuzua itikadi zinazokwenda kinyume na misingi ya awali ya Uislamu ambazo lengo lake kuu ni kuzusha mfarakano na hitilafu. Watu hawa wenye mitazamo potofu na isiyokuwa sahihi wanapatikana katika nchi mbalimbali.
Baada ya kukithiri mitandao ya intaneti katika miaka ya hivi karibuni mwenendo wa kuzusha mijadala na kueneza itikadi zisizokuwa sahihi dhidi ya Uislamu na kukuza maudhui zinazozusha mfarakano na hitilafu, imeongeza zaidi. Hii ni moja ya mbinu zinazotumiwa na wakoloni kwa ajili ya kueneza hitilafu na kuzuia umoja na mshikamano kati ya Waislamu.
Wataalamu wa masuala ya ulimwengu wa Kiislamu wanaamini kuwa vizuizi vya umoja ndani ya ulimwengu wa Kiislamu vinaweza kuwa na madhara na hatari kubwa hasa pale zinapotumiwa vibaya na madola ambayo daima yananyemelea fursa kama hiyo kutoa pigo na dharba kali kwa umma wa Kiislamu. Wataalamu hawa wanasema kuwa njama hizo zinaweza kuzimwa kirahisi hasa kwa kutilia maanani kwamba Waislamu wa madhehebu zote wanashirikiana katika mambo mengi ya Kimsingi kama itikadi ya Mungu Mmoja, Mtume Mmoja, kitabu kitakatifu kimoja cha Qur'ani, kibla kimoja na masuala mengi ya kisheria na kiibada. Si hayo tu, bali wanafikra wengi wa masuala ya Kiislamu wanasisitiza kuwa hata tofauti za kimadhehebu haziwezi kuwazuia Waislamu kuwa na umoja na mshikamano kwa kuzingatia nguvu kubwa na mambo mengi ya kimsigi yanayowakutanisha pamoja kama itikadi tulizozitaja punde kidogo.
Nini maana ya umoja na mshikamano wa Kiislamu
Kimsingi maana ya umoja na mshikamano kati ya Waislamu si kuwataka wafuasi wa madhehebu mbalimbali za Kiislamu kutupilia mbali itikadi zao, bali lengo kuu ni kujenga maelewano na mshikamano mbele ya adui wao wa pamoja. Naam, tofauti hizo za kimadhehebu zinaweza kujadiliwa kwa njia za kimantiki na busara katika vikao vya mijadala ya kielimu vya wanazuoni na maulamaa wa Kiislamu na kufikia nukta za wazi. Hapana shaka kuwa makelele na malumbano yasiyokuwa ya kielimu katika vikao vya umma kuhusu masuala ya kitaalamu hayawezi kuwa na matunda ya kuridhisha. Tunaweza kusema hapa kuwa moja ya vizuizi vya umoja na mshikamano katika umma ni kutolewa mijadala kama hiyo ya kielimu na kitaalamu kuhusu masuala ambao Waislamu wanatofautiana juu yake katika vikao vya umma na kwa njia ya kichochezi.
Dini tukufu ya Kiislamu inawalingania wafuasi wake wote kutumia akili na kutafakari na kuzidisha maarifa na elimu yao kadiri inavyowezekana. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kuwa na maarifa na elimu huzuia mifarakano na ukosefu wa maelewano. Inasikitisha kwamba katika zama za sasa Waislamu wa madhehebu moja hawajui kabisa au wana maarifa finyu kuhusu itikadi za ndugu zao wa madhehebu nyingine ya Kiislamu. Upungufu huu wa maarifa kuhusu itikadi za madhehebu tofauti za Kiislamu umekuwa moja ya vizuizi vya umoja na mshikamano wa Kiislamu na umekuwa ukisababisha mambo mengi ya kusikitisha katika ulimwengu wa Kiislamu.
Mwanafikra mashuhuri wa Kiislamu Ustadh Murtadha Mutahhari anasema: "Tishio linalowakabili Waislamu kutokana na hali ya kutofahamiana na kudhaniana vibaya ni kubwa zaidi kuliko lile linalotokana na tofauti zao za kimadhehebu." Ustadh Shahid Mutahhari anasema kuhusu taathira mbaya za kutofahamiana kati ya Waislamu na mchango wake katika kukuza hitilafu kwamba: "Tofauti za kimadhehebu na kiitikadi ni jambo ambalo limekuwepo katika zama zote lakini jambo linalobadilika kila wakati na katika kila zama ni ukosefu wa maelewano na kutofahamiana kwa pande husika. Kwa sababu hiyo, moto wa ugomvi, malumbano na mifarakano huchochewa zaidi na zaidi."
Kutofahamiana na ukosefu wa maelewano kati ya wafuasi wa madhehebu tofauti hufuatiwa na tuhuma zisizokuwa na msingi kati ya pande husika. Tuhuma hizo hujibiwa kwa tuhuma mfano wake, suala ambalo huchochea zaidi moto wa hitilafu na ukosefu wa maelewano. Ni jambo lililowazi kwamba maadui wa dini ya Kiislamu hutumia hali hiyo na kufanya jitihada za kushadidisha zaidi anga ya ukosefu wa maelewa
no na hitilafu kati ya Waislamu. Hali hiyo inapoambatana na taasubi na fikra finyu huwa na maafa makubwa zaidi. Sheikh Muhammad Abu Zahra ambaye alikuwa miongoni mwa maulamaa wa chuo cha al Azhar cha Misri amesema: "Tofauti na hitilafu zilizoko kati ya Waislamu zimepenya na kuingia zaidi katika fikra, hisia na nyoyo zao kutokana na taasubi na chuki za kikaumu na kimadhehebu kwa kadiri kwamba Muislamu mmoja humuangalia Muislamu mwenzake anayehitilafiana naye kifikra kama adui aliyeko mafichoni dhidi yake na si kama mtu mwenye mitazamo tofauti kama yeye anayefanya jitihada za kujua hakika ya sheria za Mwenyezi Mungu."
Mawahabi na Masalafi wanawakufurisha Waislamu
Kuna watu au makundi mengine yenye fikra zisizokuwa sahihi na potofu ambayo hayatosheki na kutoa tuhuma tu, bali yanachukua hatua za kutoa dharba na kuuangamiza upande wa pili; hali ambayo ni ya kusikitisha zaidi. Mfano wa wazi wa hali hiyo ni mwenendo wa maulamaa wa Kiwahabi wa kuwakufurisha Waislamu wa madhehebu ya Shia. Licha ya kwamba mashekhe hawa wa Kiwahabi na Kisalafi wanaelewa vyema kwamba Waislamu wa madhehebu ya Shia wanakubali na kuamini misingi na nguzo zote za Uislamu na hawatofautiani na Waislamu wenzao katika masuala mengi mno ya kisheria na kifiqhi, lakini bado wanawaita kuwa ni makafiri na wanahalalisha kumwaga damu ya watoto, wanawake na wafuasi wote wa madhehebu ya Shia. Fatuwa kama hizo zinazotokana na chuki za kimadhehebu na mitazamo finyu zimesababisha mauaji ya maelfu ya wafuasi wa madhehebu ya Shia katika nchi za Iraq, Afghanistan na Pakistan.
Mchango wa siasa katika kuzusha hitilafu kati ya Waislamu
Hitilafu za kidini na kimadhehebu zinapochukua sura ya kisiasa hutishia zaidi na zaidi umoja na mshikamano wa Kiislamu. Baadhi ya serikali na nchi katika ulimwengu wa Kiislamu ambazo aghlabu yao ziko chini ya satua na ushawishi wa madola ya kikoloni ya Magharibi, huzipa tofauti za kifikra za madhehebu tofauti sura ya kisiasa na kuzidisha chumvi katika hitilafu hizo. Serikali na nchi kama hizo hudhamini na kutimiza matakwa ya nchi za kibeberu na hudhania kuwa zinaimarisha misingi ya tawala zao kwa kutumia mbinu chafu kama hizo. Kwa maneno mengine ni kuwa, baadhi ya tawala na serikali zilizoko katika ulimwengu wa Kiislamu huliona suala la kuwepo mifarakano na hitilafu katika umma wa Kiislamu kuwa ni sehemu ya sababu ya kubakia kwazo. Hivi sasa fedha nyingi zinazotolewa na nchi na tawala kama hizo katika maeneo mbalimbali ya ulimwengu wa Kiislamu kama Iraq, Pakistan na Afghanistan zinatumiwa katika vitendo vya kigaidi vya kulipua misikiti na maeneo ya ibada ya madhehebu za Kiislamu kwa shabaha ya kuzidisha hitilafu na mifarakano.
Mpango eti wa 'Hilali ya Kishia' ambao umetajwa kuwa ni hatari kubwa kwa eneo la Mashariki ya Kati pia umetolewa na baadhi ya nchi za Kiarabu kwa lengo hilo hilo. La kusikitisha zaidi ni kuwa baadhi ya maulamaa na wanazuoni wa Kiislamu wameathirika na siasa hizo za kuwatenganisha wafuasi wa dini hiyo zinazobuniwa na serikali vibaraka zinazoungwa mkono na nchi za Magharibi na kuanza kutoa mihadhara na hotuba za kichochezi na fatuwa za kukufurisha na kuhalalisha damu za Waislamu wenzao. Wakati mwingine mshikamano na umoja wa Kiislamu umekuwa ukiathiriwa na hitilafu za kimbari, kikabila na hata kilugha na misimamo mikali ya kitaifa. Uzoefu wa miaka mingi umethibitisha kuwa madola ya kikoloni yamekuwa na nafasi kubwa katika kueneza hitilafu za aina hii. Hi ni pamoja na kuwa Qur'ani Tukufu inasisitiza kwamba wanadamu wameumbwa katika kaumu na makabila yenye lugha na rangi tofauti kwa ajili ya kuelewana na kutambuana na kwamba kigezo pekee cha ubora mbele ya Mwenyezi Mungu ni takwa na uchamungu.
Japokuwa kuna baadhi ya mambo yanayozuia umoja na mshikamano wa kivitendo katika ulimwengu wa Kiislamu, lakini vikwazo na viizingiti hivyo vinaonekana dhaifu mbele ya azma na irada halisi ya umma wa Kiislamu. Hususan ikitiliwa maanani kwamba hii leo mwamko wa Waislamu kote duniani umeshika kasi zaidi na kutayarisha uwanja nzuri wa kuimarishwa umoja, mshikamano na ushirikiano kati ya Waislamu wote duniani. Tunakamilisha makala hii kwa aya ya 105 ya Suratu Tauba inayosema: Na waambie: Tendeni, Mwenyezi Mungu, na Mtume wake, na waumini wataviona vitendo vyenu.
MWISHO