Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

NAFASI YA UANAADAMU WA MWANAMKE

0 Voti 00.0 / 5

NAFASI YA UANAADAMU WA MWANAMKE

UTANGULIZI

Kwa jina la Muumba Mkamilifu ninaishika kalamu kwa dhamira ya kuielezea nafasi ya uwanaadamu wa mwanamke. Katika kurasa za makal hii, nitajaribu kuzifafanua baadhi ya fikra zinazoungalia Uislamu kuwa ni dini inayowakandamiza wanawake.

Tuhuma mabali mbali ambazo kwa mara nyingi huwa ni zenye kuelekezwa katika dini mbali mbali, zinaweza kuwa ni zenye kusema kweli, na mara nyengine zikawa ni zenye kulenga malengo ya kuleta uadui fulani. Lakini watu wenye akili huwa hawayachukulii madai hayo kuwa ni madai ya uwongo, bali huyachukulia kuwa ni kama changamoto ya kuwatumbukiza wao katika uwanja wa utafiti kuhusiana na masuala hayo. Nami nimeamua kuwaiga wenye akili katika kulipekuwa suala la Uwanaadamu wa mwanamke, ili kuweza kuthisha au kukanusha tuhuma za unyanyasaji wa wanawake unaodaiwa kuwepo ndani ya dini ya Kiislamu.

Kuwepo kwa unyanyasaji wa wanawake katika jamii mbali mbali, huwa kunategemea hali ya utamaduni wa jamii hizo ulivyo muweka mwanamke, hivyo basi unyanyasaji wa wanawake hauwezi tu kuegemezwa katika jamii za Kiisalmu, bali unaweza kuegemezwa juu ya migogo ya Waislamu na wasiokuwa Waislamu, kwa kutokana na tamaduni na fikra zao zilivyo. Kutovutia upande mmoja katika suala la utafiti huu, kunaweza kumvutia kila mtu apendaye ukweli na mwenye busara. Ninamtaraji Mola aniongoze katika utafiti huu, ili nisije kuwatetea Waislamu kwa Uslamu wao, au Wakristo kwa Ukristo wao. Kwani kufanya hivyo kutaitoa thamani makala hii, na hakutompa msomaji shauku ya kuendelea na usomaji wake. Ninatarajia malengo yangu yatafanikiwa kwa uwezo wa Muumba Mkamilifu.
Aamin.

MWANAMKE KATIKA JAMII MBALI MBALI

Mwanamke katika jamii mbali mbali huwa ana nafasi yake maalumu, na nafasi yake huwa inaendana na namna ya jamii yake inavyompa thamani kiumbe huyu. Kila jamii hua inamuhesabu mwanamke kuwa ni mmoja kati ya viungo vya jamii, lakini tofauti huwa inapatikana kwa namna ya kila jamii inavyo muangalia mwanamke.

Jicho la Uislamu linamuangaliaje mwanamke? Je Uislamu katika suala la Ubinaadamu, huwa unamuhesabu mwanamke kuwa sawa na mwanamume katika suala hilo, au huwa unamuona mwanamke kuwa ni mwenye daraja ya chini kuliko mwanamme? Haya ni masuala ambayo tutajaribu kuyajibu katika kurasa hizi.

FALSAFA YA UISLAMU KUHUSU HAKI ZA KIFAMILIA

Uislamu katika suala la haki za mwanamke na mwanamme ndani ya familia, huwa una falsafa yake maalumu, falsafa ambayo mitazamo yake huwa inatofautiana na ile mitazamo ya karne kumi na nne ziliyopita, pamoja na kutofautiana na mitazamo ya zama zetu hizi za ulumwengu wa kileo.

Katika suala la nyadhifa, sheria pamoja na haki mbali mbali, Uislamu haukuwahesabu wanawake na wanaume kuwa ni wenye aina moja ya masuala hayo. Uislamu umezipanga baadhi ya sheria ambazo huwa zinawalazimu wanawake na nyengine ambazo zinawalazimu wanaume, pamoja na kuzipanga baadhi ya sheria nyengine ambazo huwa zinawagusa wote wawili kwa usawa. Uislamu huwa una zihesabu baadhi ya nyadhifa kuwa ni nyadhifa ambazo zinawiana zaidi na hali ya wanaume walivyo, pamoja na kuziona baadhi ya nyadhifa kuwa ni zenye kulingana zaidi na hali ya wanawake walivyo. Na hivyo ndivyo Uislamu unavyo zigawa nyadhifa mbali mbali za kijamii. hivyo basi katika baadhi ya masula fulani, mwanamke na mwanamme huwa ni wenye kutofautinana na katika baadhi ya masuala mengine huwa ni wenye kulingana kinyadhifa, kisheria pamoja na kimatendo.

Bila shaka kila mtu atakuwa ana haki ya kuuliza kuwa, ni vipimo gani vilivyo tumika katika kumbagua mwamke kinyadhi, kisheria pamoja na kimatendo? Je Uislamu nao una mtazamo wa kunyanyasa mwanamke na kumbagua kama zilivyofanya tamaduni na dini mbali mbali? Je Uislamu unamuona mwanamke kuwa ni mwenye daraja ya chini kuliko mwanamme? Au Uislamu una falsafa nyengine inayotofautiana na falsafa mbali mbali kuhusina na masuala hayo?

Katika semi tofauti pamoja na maandiko au mihadhara mbali mbali, Watu huusikia Uislamu ukituhumiwa kwa masuala mbali mbali, kama vile: suala la mahari, chejio, talaka, uke wenza na mengineyo. katika masuala kama hayo Uislamu umekuwa ukituhumiwa kumkandamiza mwanamke, huku kukifikiriwa kuwa, hakuna dalili iliyo ufanya Uislamu kuzipanga sheria katika mtindo huu unaotuhumiwa nao, bali kunafikiriwa kuwa msingi mkuu uliyo zingatiwa katika sheria za Uislamu ni kumtukuza mwanamme na kumuweka yeye katika hali ya ubwana.

Kuna usemi usemao kuwa: sheria na kanuni zote zilizokuwako katika karne ishirini zilozopita, zilisimama juu ya msingi umtukuzao mwanamme na kumuona yeye kuwa ni mbora zaidi kushinda mwanamke, huku sheria na kanuni hizo zikimuona mwanamke kuwa yeye ameumbwa akiwa ni chombo maalumu cha kumtumikia mwanamme, chombo ambacho kinatakiwa kuzitekeleza amri zote zitokazo kwa wanaume bila ya kuwa na haki ya udadisi wa aina yeyote juu ya amri hizo. Uislamu nao huwa hauna namna nyengine ya sheria, bali nao umekuja na mtindo ule ule uliyokuwepo katika zama zilizopita, mtindo ambao huwa una kawaida ya kuyashangiria manufaa ya mwamme na kuyapiga teke yale yote yanayomtukuza na kumpa utu wake mwanamke.

Usemi huu umezizaa kauli zisemazo kuwa: Uislamu ni dini ya wanaume, na mwanamke katika dini hii, huwa hapewi thamani kamili ya Uwanaadamu kama alivyo mwanamme, na wala dini hii haikumpa mwanamke haki zake za Kibinaadamu anazopaswa kupewa akiwa ni kama Mwanaadamu kamili.

Uislamu ungalikuwa unamuhesabu mwanamke kuwa ni Mwanaadamu kamili, basi kusingekuwa na haja ya dini hii kujuzisha kuowa zaidi ya mwanamke mmoja, na vile vile kusingehesabiwa ushahidi wa wanawake wawili kuwa ni sawa na ushahidi wa mwanamme mmoja, na wala uongozi wa nyumba usingewekwa juu ya mikono ya wanaume, na urithi nao ungaligawiwa kwa usawa baina ya mwanamke na mwamme, na mwanamke katika suala la ndoa asingekua na thamani maalumu ya mahari kama kinunuliwavyo kitu dukani.

Yote hayo ni yenye kuonyesha kuwa, Uislamu ni wenye jicho la kumdhalilisha mwanamke, na unamuhesabu yeye kuwa ndiye uwanja anaotakiwa mwanamme kuupita juu yake, katika kuyafikia malengo yake. Chonza hizi zimeweza kuleta usemi usemao kuwa: haidhuru tunaweza kusema kuwa Uislamu ni dini ya haki na usawa, tukizingatia kuwa, Uislamu katika sehemu mbali mbali umeweza kuweka haki sawa, lakini kuhusiana na mwanamke dini hii haikuweka haki sawa, na wala haikuzilinda haki za Kibinaadamu za mwanamke kama zilivyolindwa na kupendelewa haki za wanaume ndani ya dini hii.

Usemi huu unasema kuwa mwanamme amekadiriwa haki za hali ya juu na dini hii, pamoja na kupewa fadhila zaidi kuliko mwanamke. Na kama mwanamme hana thamani zaidi ya mwanamke katika dini hii basi kusingekuwa na haja ya kumpandisha daraja katika haki mbali mbali za kijamii na kifamilia.

USAWA NA MALINGANO

Dalili zilizotumika hapo juu katika suala la kuutuhumu Uislamu, zimeegemea na kusimama juu ya msingi wa hoja isemayo kuwa: jambo pekee linaloweza kuuonyesha usawa wa Kibinaadamu walionao watu mbali mbali, ni kule kuwiana kwa haki mbali mbali za watu hao, ili kuuona ukweli au udhaifu wa msingi wa hoja hii, ni lazima kwanza tuulize suala moja muhimu la kifalsafa lisemalo kuwa: ni jambo gani linaloweza kutufahamisha kuwa mwanamke na mwanamme ni wenye usawa wa Kibinaadamu katika Ubinaadamu waliyo nao?

Hapa basi Inatubidi sisi tuelewe kuwa: je kuzifanya haki za wawili hawa kua ni sawa ndiko kutako mtukuza mwanamke, au sisi tunatakiwa kuwapa haki sawa pamoja na kuwawekea nyadhifa za hali moja zisizotofautiana, na huko ndiko kutakomfanya mwanamke kuwa ni mwenye utukufu sawa na mwanamme? Sisi hatuna woga wa kusema kuwa mwanamke na mwanamme ni wenye usawa katika suala la Ubinaadamu waliyo nao, jambo ambalo huwa linatulazimisha sisi kuwapa wao haki sawa za Kibinaadamu, lakini je iwapo sisi tutakubaliana katika suala la usawa wa haki za Kibinaadamu wanazopaswa kupewa wanawake na wanaume, itatubidi vile vile tukubaliane na usawa wa haki za kikazi na mingineyo?

Msingi wetu ukiwa ni kuto fuata falsafa za Kimagharibi kiupofu, bali ni kuzichunguza falsafa hizo pamoja na kuzitafakari, hapo basi cha kwanza kabisa tunachotakiwa sisis kukifanya, ni kuangalia kuwa: Je neno usawa katika haki huwa linalazimisha kuwa na maana ya kuwiana kwa haki hizo? Neno usawa katika haki huwa halimaanishi kushabihiana au kufanana katika haki na wala halina maana sawa na neno hilo. Ili lifahamike vizuri suala hili inabidi tuunagalie mfano wa mzazi mwenye mali. Mzazi huyu anaweza kuigawa mali yake kwa usawa miongoni mwa wanawe, hali ya kuwa yeye hakuigawa mali hiyo kwa katika uwiano mmoja, tujaalie kuwa yeye ni mwenye viwanda, mashamba, na maduka mbali mbali.

Mzazi huyu basi anaweza kuzigawa mali zake kwa kulingana na hali za wanawe walivyo, kwani miongoni mwa watoto wake kukiwa kuna yule aliyesomea biashara, itambidi yeye kupewa maduka, kwani yeye ndiyo muhusika zaidi wa mali hiyo, na aliyesomea kilimo naye atastahiki kupewa mashamba, na hali ndiyo kama hiyo katika utowaji wa mali na upangaji wa kazi za watoto hao kibusara. Iwapo kutatokea mtu mwenye mali za aina kama hiyo, huku akiwa na watoto wenye fani mbali mbali, hapo basi busara na haki itakuwa ni kumpa kila mmoja kazi iyendayo sawa na elimu yake aliyokuwa nayo. Kumpa mtu kazi asiyo kuwa na ujuzi nayo, huwa ni kumtia yeye mashakani, na wala kufanya hivyo hakuto hesabiwa kuwa ni kusaidia yeye.

Wingi sio ubora na wala usawa katika haki haumaanishi kuwa watu wote wanatakiwa kuwa na aina moja ya haki. Ukweli ni kwamba Uislamu haukumuwekea haki za aina moja mwanamke na mwanamme, na vile vile Uislamu haukumpa mwanamme haki zaidi kuliko mwanammke, bali Uislamu umezingatia vya kutosha msingi wa usawa kwa Wanaadamu wanawake pamoja na wanaume. Uislamu unakubaliana na kuwepo kwa haki baina ya wanawake na wanaume, lakini haukubaliani kuwepo kwa haki za aina moja baina yao, na hicho ndicho kinachopingwa na Uislamu kwa kutegemea misingi maalumu.

Neno usawa au kutokuwa na mapunjo, ni neno lililobeba utukufu maalumu ndani yake, na ni lenye kumvutia kila mwenye kulisikia neno hili, hii ni kwa kutokana na kwamba, usawa ndiyo mpezi wa kila mwenye akili timamu katika ulimwengu huu, pamoja na ulimwengu mwengine wowote ule wa watu wenye akili, hasa hasa pale neno hili linapofungamana na neno haki na kushikamana pamoja nalo. Haiwezekani kutokea mtu mwenye moyo msafi na mkunjufu aendaye sawa na maumbile ya Mola wake, akawa si mwenye kuliheshimu neno hili pamoja na kuuthamini uhakika wake.

Leo mimi ninapigwa na butwaa sana, pale ninapouona uma ulikuwa ukiiongoza dunia kitamaduni na kielimu, ukiyumbishwa na baadhi ya wale wanaojivika vilemba visivyokuwa vyao katika suala la kuzitetea haki za wanawake duniani, walikuwepo wapi watu hawa, wakati Uislamu ulipo inyanyua bendera ya falsafa na mantiki katika utetezi wa sheria mbali mbali, zama ambazo bado kulikuwa kuna wengi waliokuwa wakiwakandamiza wanawake na watoto katika jamii tofauti. Kama leo kuna makundi yanayojaribu kuzipigia upatu haki za wanawake kwa kuutegemea mtazamo wa Kimagharibi, basi watu hawa watakuwa wanafanana na wale wanaozitangaza biashara zao kwa kupitia majina ya watu wengine. Je kuna mtu anaye uza juice ya mabungo kwa jina la coka kola?. Bila shaka hayo huwa ni maradhi ya kuto jiamini au kuto iamini silaha ya kimaarifa uliyokuwa nayo, au kuto ufahamu uzito wa silaha hiyo.

Uislamu hauna khofu katika kuitangaza sheria yake juu ya kuto wawekea wanawake na wanaume sheria za aina moja, katika masuala ya utendaji au ushikaji wa nyadhifa mbali mbali. Lakini kufanya kwake hivyo hakuonyeshi hata kidogo ubora wa wanaume juu ya wanawake Kiubinaadamu. Wala jambo hilo halimaanishi kuwa nyadhifa walizopewa wanawake katika Uislamu, ni nyadhifa duni zisizokuwa na thamani kama zile za wanaume zilivyokuwa na thamani. Jukumu letu sisi, ni kuithibitishia jamii yetu ya kileo uadilifu wa Kiislamu, kwani jamii yetu ya leo iko hatarini na kukumbawa na mawimbi mbali mbali, huku utandawazi wa Kimaghari ukijaribu kuzimeza jamii mbali mbali, na kuzivisha joho la kishetani na kinyama.

Busara, hekima, ukweli na huruma vimeanza kubadilika vikionekana kua ni ujinga, huku ujinga na ubeberu ukifahamika kuwa ndio ujanja wa kileo katika kujipatia maisha rahisi kwa jasho la wanyonge. Ni utamu ulioje kula bure kwa kupitia mifuko ya wengine, lakini je huo ndiyo Ubinaadamu? Jawabu iko akilini mwako, sifikirii kuwa kuna mtu anayeweza kukubaliana na mambao kama hayo, na iwapo kutatokea mtu mwenye kuyapigia vigeregere mambo hayo, basi huyo atakuwa akiwatakia wengine tu kutendewa uhalifu huo, lakini pale atendewapo yeye au jamaa zake, hapo basi huwa ni mkali wa kuyaripia matendo hayo. Wahenga wanasema "Mkuki kwa nguruwe, kwa Binaadamu uchungu". Na huo ni ukweli usio fichikana.

Wanajamii mbali mbali Waislamu na wasio Waislamu, wanaweza kuwa ni wadadisi wa kutaka kujua kuwa, ni sababu gani iliyo ufanya Uislamu kuzibagua nyadhifa za wanawake katika baadhi ya masuala? Kwa nini Uislamu haukuzifanya nyadhifa au kazi mbali mbali za kijamii kuwa sawa kwa wote? Je kuzifanya haki kuwa sawa kwa wote si ndiyo uadilifu zaidi?

Ili tuweze kuwanufaisha wasomaji kwa vizuri zaidi, inatubidi kuugawa utafiiti wetu katika sehemu tatu:
1- Mtazamo wa Kiislamu juu ya hali halisi ya daraja ya kimaumbile aliyo nayo mwanamke.
2- Kuna malengo gani katika tofauti za kimaumbile zinazopatikana baina ya mwanamke na mwanamme? Je tofauti hizi ndizo zinazowatofautisha wawili hawa katika ugawikaji au ugawaji wa haki mbali mbali ziendazo na maumbile yao?
3- Kuna falsafa gani katika kuwatenganisha wawili hawa kihaki? Au kuna falsafa gani ya kuwafanya wao wasiwe na aina moja ya nyadhifa? Na je hadi leo Uislamu ungali unashikilia kamba ile ile ya mwanzo katika suala hilo, au kuna haja ya kufanya marekebisho?

MTAZAMO WA KIISLAMU JUU YA MWANAMKE

Katika kukichambua kipengele namba moja, na kukifanya kijibike vya kutosha kabisa, itatubidi tuwafahamishe watu kuwa, Qurani si kitabu cha kanuni na sheria tu, bali ni kitabu kilicho kusanya ndani yake mambo mbali mbali yanayo weza kumlea na kumuongoa Mwanaadamu, kama vile tarehe, ambayo huwa ni mawaidha mazuri kwa wale wenye fikra za kuitafakari Qurani, na ndani yake mnapatikana ufafanuzi kamili juu ya hali halisi ya uumbaji, na ndani yake mtu anaweza akaelewa siri ya kuwepo kwake katika ulimwengu huu au hata kuelewa siri ya kuwepo vitu vyote vilivyo mzunguka yeye katika dunia hii, na kuna mengi ndani yake yanayo weza kumpa ufunuo wa kutosha juu ya suala la uhai wake pamoja na mauti yake, au uhai na mauti ya vitu mbali mbali, na kwa upande mwengine Qurani ni yenye kutoa taaluma tosha kuhusiana na lipi linaloweza kumpandisha daraja Mwanaadamu na lipi linaloweza kuporomosha, lipi linaloweza kumpa mali na lipi linaloweza kumfukarisha. Yote hayo bayana zake zinaweza kupatikana ndani ya Qurani tukufu bila ya mapunjo yeyote.

Qurani sio kitabu cha falsafa, lakini kitabu hichi hakikuacha kutoa mtazamo wake kuhusiana na masuala ya ulimwengu, Binadamu pamoja na jamii, kwani vitu vitatu hivi ndivyo vinavyo jenga misingi mikuu ya falsafa mbali mbali. Qurani haiwafundishi wafuasi wake kanuni peke yake, wala haiwatumbuizi wafuasi wake kwa kuwapa mawaidha tu, bali Qurani inachukuwa jukumu la kuifasiri hali nzima ya kimaumbile ya ulimwengu na vilivyomo ndani yake.

Kufanya kwake hivyo, huwa kuna malengo ya kumpa Mwanaadamu mtazamo maalumu juu ya ulumwengu huu, jambo ambalo huwa linamjenga yeye kifikra na kitamaduni. Misingi mikuu ya sheria mbali mbali inayo husiana na masuala ya jamii, milki, serikali, haki za kifamilia pamoja na mambo mbali mbali, huwa inategemea namna ya Wanaadamu walivyoifahamu dunia na mambo yake, hivyo basi kuifasiri dunia na ulimwengu ulivyo, ndiko kunakompa Mwanaadamu muelekeo mzuri wa kujipangia sheria na kanuni za mipango mbali mbali ya leo na kesho.

Moja kati ya masuala yaliyo fasiriwa na kuchambuliwa vizuri na Qurani, pale Qurani ilipokuwa ikiifasiri hali nzima ya kilimwengu, ni suala la maumbile ya mwanamke na mwanamme. Qurani haikulinyamazia kimya suala hili na kulifungia mikono, na wala Qurani haikuwapa Wana falsafa fursa ya kuzinowa falsafa zao kwa ajili ya upangaji wa sheria zinazowahusu wanawake na wanaume. Ingawaje Qurani imebainisha vya kutosha kuhusiana na sheria za wake na waume, lakini bado kulionekana kutokea baadhi ya watu waliozipinga sheria hizo, na kuzua sheria nyengine ziendazo kinyume na hali halisi ya mambo yalivyo.

Kwa mara ya kwanza kabisa tunapotaka kuupekuwa na kuutambua mtazamo wa Kiislamu juu ya suala la uumbaji wa mwanamke na mwanamme, inatubidi kwanza kabisa tuuelewe uhakika wa mwanamke na mwanamme ulivyo. Uhakika ambao umeelezewa vya kutosha ndani ya vitabu tofauti vya dini mbali mbali. Waislamu nao wanapata maelezo ya kutosha kuhusiana na suala hilo, kutoka katika Qurani yao kwa ajili ya kuuongoza ulimwengu huu, ninapenda kukumbusha tena kuwa, Qurani haikulinyamazia kimya suala la uhakika wa mwanamke na mwanamme.

Hebu basi tuiangaliye Qurani na tuichunguze kwa makini, huku tukijiuliza kuwa: je uhakika wa mwanamke ndani ya Qurani ni sawa na uhakika wa mwanamme kimaumbile, Au viumbe hawa wawili ni wenye uhakika wa aina mbili tofauti?

Qurani katika Aya tofauti inatufahamisha kuwa: mwanamke ametokana na mwanamme, vile vile ianatuambia kuwa: mwanamke ameumbwa kwa kupitia uhakika ule ule aliyoumbiwa mwanamme. Uhakika huu unaweza kupatiakana katika Qurani katika Sura na Aya tofauti, kama vile Suratu Ruum, Nahl na Suratu Nisaa. Katika Suratu Nisaa Mwenye Ezi Mungu Mtukufu anasema: {Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni kutokana na nafsi moja, na akamuumba mkewe kutokana na nafsi ile ile. Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi. Na tahadharini na Mwenyezi Mungu ambaye kwaye mnaombana, na jamaa zenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kukuangalieni.} 1

Qurani iko kinyume kabisa na zile fikra za Madhehebu na dini mbali mbali, zisemazo kuwa: mwanamke ameumbwa akiwa ni kama msindikizaji wa mwanamme katka dunia hii, au ameumbwa kwa kupitia ubavu wa kushoto wa mwanamme. Kwa kweli yote hayo yaliomo katika dini mbali mbali ni yenye kwenda kinyume na mtazamo wa Qurani juu ya mwanammke.

Moja kati ya mambo mbali mbali yaliyo letwa na fikra potofu za baadhi ya watu katika zama zilizopita, ni kumuhesabu mwanamke kuwa yeye ni kiungo cha shetani katika upotoshaji, fikra hizi huwa zinamuona mwanamke kuwa yeye ni shari kwa mwanamme, na ni mwenye kuleta wasi wasi wa aina mbali mbali ndani maisha ya mwanamme, fikra hizi zinasema kua: kila pale mwanamme alipo onekana kufanya dhambi, basi mwanamke alikuwa ndiye msukumaji na mchochezi wa matendo hayo, vile vile husemwa kuwa, mwanamme ametakasika na dhambi, bali mwanamke huwa ni kishawishi cha matendo ya ufisadi, na hata Adamu (a.s) alipofukuzwa kutoka Peponi, basi Hawa (a.s) ndiye aliyekuwa ni chombo cha Shetani katika kumpotosha Adamu.

Qurani ilipo kizungumzia kisa cha Adamu (a.s), haikumtumbukiza makosani Hawa (a.s) peke yake wala haikumvua yeye katika makosa hayo, bali Qurani iliwanadi wote wawili Adamu na Hawa (a.s) na kuwahesabu kuwa ni wenye hatia ya aina moja, bila ya ubaguzi wa aina yeyote. Kwa ajili ya kupata ufafanuzi kamili juu ya hilo, hebu tuitafakari Qurani katika Aya zifuatazo: {Na wewe, Adam! Kaa wewe na mkeo katika Bustani hii, na kuleni humo mpendapo. Wala msiukaribie mti huu, mkawa katika wale walio dhulumu.}

{Basi Shet'ani aliwatia wasiwasi ili kuwafichulia tupu zao walizo fichiwa, na akasema: Mola Mlezi wenu hakukukatazeni mti huu ila msije mkawa Malaika, au msije mkawa katika wanao ishi milele.} {Naye akawaapia: Kwa yakini mimi ni miongoni wa wanao kunasihini. } {Basi akawateka kwa khadaa. Walipo uonja ule mti, tupu zao zilifichuka na wakaingia kujibandika majani ya Bustanini. Mola wao Mlezi akawaita: Je, sikukukatazeni mti huo, na kukwambieni ya kwamba Shet'ani ni adui yenu wa dhaahiri?} {Wakasema: Mola wetu Mlezi! tumejidhulumu nafsi zetu, na kama hutusamehe na kuturehemu, hakika tutakuwa katika wenye kukhasirika.} {Akasema: Teremkeni! Mtakuwa nyinyi kwa nyinyi maadui. Na kwenye ardhi itakuwa ndio makao yenu na starehe yenu mpaka ufike muda.} {Akasema: Humo mtaishi, na humo mtakufa, na kutoka humo mtatolewa}{Enyi Wanaadamu! Tumekuteremshieni nguo za kuficha tupu zenu, na nguo za pambo. Na nguo za uchamngu ndio bora. Hayo ni katika Ishara za Mwenyezi Mungu mpate kukumbuka.}

{Enyi Wanaadamu! Asije Shet'ani kukufitinini kama alivyo watoa wazazi wenu Peponi, akawavua nguo zao kuwaonyesha tupu zao. Hakika yeye na kabila yake wanakuoneni, na nyinyi hamuwaoni. Hakika Sisi tumewafanya Mashet'ani kuwa ni marafiki wa wasio amini.} 2 Katika kisa hichi unadhihirika wazi usawa wa mwanamke na mwanamme katika Ubinaadamu na ukamilifu wao, kwani Qurani haimuusii tu mwanamke kujihadhari na Shetani, bali inawausia Wanaadamu wote kwa ujumla, wake kwa waume. Wala jambo hilo halionekani kupewa masisitizo zaidi kwa upande wa wanawake kuliko mwanmme, jambo ambalo labda lingeliweza kutoa ushuhuda juu ya upungufu wa mwanamke. Hivyo ndivyo Qurani inavyotoa jawabu kwa wale wenye uoni mbaya juu ya kiumbe huyu aliye fadhiliwa na Mola wetu. Qurani haikuanza leo kupigana vita kwa ajili ya utetezi wa haki za wanawake duniani, kwani fikra kama hizi zilikuwepo katika zama tofauti, na zilidhihirika ndani ya dini na tamaduni mbali mbali zilizopita, jambo ambalo liliifanya Qurani izisimamie kidete haki za kiumbe huyu kwa kutumia hoja zisizo pingika.

Moja kati ya ile mitazamo pofu iliyokuwa ikitumika kwa ajili ya kumdhalilisha mwanmke, ni ule mtazamo uliyokuwa ukisema kuwa: mwanamke ni kiumbe asiyekuwa na uwezo wa kujitakasa kiroho, na ni jambo lisilowezekana kwake yeye kuingia Peponi, naye ni vigumu kuweza kijikaribisha mbele ya Mola wake. Qurani imechukuwa hatua mbali mbali, katika juhudi zake za kuzifuta fikra kama hizi zilizokuwa zimeshaota mizizi katika jamii mbali mbali. Moja kati kati ya njia iliyoweza kutumika katika harakati za kuzitokomeza dhana hizo, ni kule kuzitangaza sera za wanawake wema ambao walipiga hatua kubwa hata kuliko baadhi ya wanaume wa zama hizo, juu ya kazi mbali mbali zilizoweza kuzikuza jamii zao kimaendeleo.

Katika kila zama huwa hakukosekani kupatikana mwanamke aliyesifika kibusara na kitabia ambao baadhi yao wametajwa ndani ya Qurani. Kuwataja baadhi ya wanawake wakorofi walio watimba waume zao katika Qurani, hakumaanishi udhalili wa wanawake wengine, kwani Qurani haikutoa tu mifano mbali mbali ya wanawake waovu, bali kwa upande mwengine iliwataja wanawake mbali mbali waliotakasika kiimani na kitabia, kama vile bibi Asia, ambaye alikuwa ni mke wa Farao (firauna), au Mariamu ambaye ni Mtawa aliye jitakasa, naye ni mama wa Yesu mtakatifu.

Bibi Mariamu (a.s) alipata cheo kikubwa kutoka kwa Mola wake, kiasi ya kwamba alikuwa akiletewa chakula kutoka mbinguni, na cheo kama hicho si rahisi kupatikana na wanaume mbali mbali. Majigambo tofauti ya wanaume wanao jaribu kuwadhalilisha wanawake huwa yanagonga mwamba pale yanapo kutana na majabali makubwa ya nuru yaliyo mzunguka bibi Mariamu. Katika masuala ya utendaji, Muumba Mkamilifu huwa haziangalii nyuso za watendaji, bali huwa ana angalia uzito wa lile lililotendwa na thamani ya tendo hilo. Hivyo basi kutoa madai yasemayo kuwa: mwanamke ni kiumbe asiyeweza kuingia Peponi, au ni kiumbe dhalili ambaye hastahiki kuwa karibu na Mola wake, ni maneno yasiyo kuwa na msingi wowote. Mwenye Ezi Mungu katika Qurani anasema: {Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa ni Muumini, tutamhuisha maisha mema; na tutawapa ujira wao kwa bora ya waliyo kuwa wakiyatenda.} 3

Si jambo la udanganyifu kusema kuwa: wanawake ni wenye cheo sawa na wanaume katika suala la Ubinaadamu, kwani kuna nyota ngapi za kike zilizong'aa katika anga la Uislamu, na jee yuko anaye dai kuwa yeye ni mwenye cheo zaidi kuliko Faatima Zahzaa (a.s) pamoja na bibi Khadija ambaye ni mama wa Faatima (a.s)? Hakuna mtu awezaye kumpindukia fadhila Faatima (a.s) isipokua baba yake tu, ambaye ni Mjumbe wa Mola Mtakatifu. Cheni ya watukufu wa kike bado itaendelea kung'ara katika zama mbali mbali. Kwani wanawake kuwa na utukufu maalamu ni neema ya Muumba Mtakatifu, na ni zawadi maalumu kwa wale wanawake walio watiifu kwa Mola wao, na hakuna zama zikosazo wanawake wema, na hiyo ni moja kati ya fadhila za Mwenye Ezi Mungu.

MITAZAMO YA BAADHI YA DINI JUU YA MWANAMKE Katika baadhi ya dini huwa kuna mtazamo unao liangalia suala la kijinsia, kuwa ni tendo chafu lenye kumzuwia mtu katika maendeleo yake ya Kiucha Mungu. Kwa mtindo huo basi, mwanamke huonekana kuwa, ni kama chombo kinachotumika katika suala hilo la kumzuwia Mja asizifikie zile daraja za juu za Kiucha Mungu, na huko ndiko kumdhalilisha mwanamke. Katika dini zenye mitazamo kama hiyo, Utawa huwa ndio unaopewa kipau mbele zaidi, kwa ajili ya kuikuza roho ya Mwanaadamu. Na mja bora kwao ni yule aliyejizuwia kutenda tendo la ndoa.

Uislamu haukubaliani na masuala kama hayo, na dilili tosha kuhusiana na hilo, ni kule kuonekana Mitume mbali mbali, wakiwa ni wenye kulitukuza tendo la ndoa, na wengi miongoni mwa Mitume (a.s) walionekana wakiwa na wake zaidi ya mmoja, yawezekana kuwa, kufanya kwao hivyo kulikuwa na malengo ya kuzibomoa fikra potofu zilizokuwa zikitawala katika zama zao. Na kufanya kwao hivyo hakukuonyesha aina yeyote ile ya unyanyasaji au dhulma fulani kwa wanawake waliyokuwa wakiwamiliki, kwani upendo, busara, na heshima walizowafanyia wake zao kiuadilifu, zilikuwa zikionyesha wazi kuwa wao hawakuwa wakiwaona wanawake hao kuwa ni kama njia za kuyafikia matamanio ya nafsi zao, bali hilo lilikuwa likilenga upendo juu ya kiumbe huyu mnyanyaswa.

Wengi miongoni mwa wale wasio fahamu, huwa wanamuangalia mwanamke kuwa yeye ni msindikizaji wa mwanamme katika dunia hii, huku wakifikiria kuwa mwanamke ameumbwa kwa ajili ya mwanamme. Kwa kweli hiyo ni dhulma juu ya mwanamke, Qurani nayo haikubaliani na maneno hayo. Qurani inaeleza kuwa: mwanamke ameumbwa kwa ajili ya mwanamme, na mwanamme naye ameumbwa kwa ajili ya mwanammke, hii inamaanisha kuwa: watu walili hawa ni wenye kukamilishana kimaumbile na kimatendo. Mwenye Ezi Mungu katika Qurani anasema: {Wao wanawake ni nguo zenu, na nyiyi wanaume ni nguo za wanawake} 4 .

Katika Qurani Mwenye Ezi Mungu kwa mara nyengine amesema kuwa: Yeye ameviumba vilivyomo katika dunia hii kwa ajili ya Mwanaadamu, na wala hakumbagua mwanamke katika suala la Ubinaadamu, au kumzuwiya asinufaike na neema za ulimwengu huu. Na hakuna Aya inayoonyesah kuwa mwanamke ameumbwa kwa ajili ya mwanamme tu, huku akiwa yeye ni kama mtumwa wa mwanamme.

Uislamu hamtaki mume kumtumia mke atakavyo, bali katika suala la kazi za ndani mwanamke huwa halazimiki kuzifanya kazi hizo, isipokuwa huwa ni makubaliano ya ndani ya jamii, kuwa manamme afanye kazi za nje, na mwanamke afanye kazi za ndani, na hayo ni makubaliano ya pande mbili tu, na ni mawafikiano wanayo kubaliana mke na mume, na wala siyo amri itokayo kwa Muumba wa ulimwengu.

Mwanamke ni kiungo muhimu katika jamii, na kama tunavyo elewa kuwa, kila mmoja katika jamii huwa anakabiliwa na majukumu maalumu yaendayo sawa na hali yake ilivyo. Mwanamke kwa kutokana na hali yake na ujuzi wake katika suala la ulezi wa watoto, basi yeye huwa ndiye muhusika zaidi katika suala la malezi ya watoto. Lakini hilo halitazuwia harakati nyengine zinazoweza kufanywa na wanawake katika sekta mabi mbali, kwa mazingatio ya ujuzi na uwezo wa kila mmoja ndani ya jamii. Lakini bado katika suala la kumtumia mwanamke katika kazi mbali mbali za jamii litahitajia uchunguzi zaidi juu ya hali halisi ya kazi hizo pamoja na hali halisi ya uwezo wake wa kimaumbile, pamoja na uwezo wake wa kielimu, jambo ambalo litakuwa ni kama ngao ya kumlida mwanamke.

Mwanamke katika jamii tofauti huonekana ni kama balaa kwa mwanamme, na katika zama za kale, mwanamke alikuwa akihesabiwa kuwa ni kama chombo tu au mashine ya kuzalishia watoto, na hakuwa mwanamke akipewa aina yeyote ile ya ushauri juu ya kizazi chake, kwani yeye alikuwa akionekana si chochote si lolote katika suala hilo. Uislamu umejaribu kuzifahamisha jamii mbali mbali kuwa: mwanamke ni utulivu kwa mwanamme na wala sio shari kwake.

NDOA Katika mila zetu za Kiafrika, wakati mwengine huwa kunaonekana baadhi ya aina za ukandamizaji wa mwanamke, kwani huwa kunatokea baadhi ya wazazi wanao walazimisha watoto wao wa kike kuolewa kwa lazima, bila ya watoto hao kuridhika na waume wanaotaka kuwaowa. Hapa sitaki nifahamike vibaya, lakini hili ni suala ambalo limo ndani ya jamii zetu. Vile vile mara nyingi hasa katika sehemu za mashamba, mwanamke huwa hapewi mahari yake pale anapo olewa, bali mahari hayo huwa yanachukuliwa na wazee. Kwa kweli hiyo sio haki, kwani kumlazimisha bint wa kike aolewe na mtu asiye mtaka ni makosa, na vile vile kuyala mahari ya mabinti zetu ni makosa yasio kubaliwa na Uislamu.

Maslahi ya mtoto wa kike ni lazima yazingatiwe. Kumshauri mtoto katika suala la ndoa ndio jambo linalotakiwa, na sio kumlazimisha. Hakuna mtu anaye kataa kuwa mara nyingi watoto wetu huwa wanashindwa kumuelewa ni nani anaye wafaa zaidi kuwa ni mume au ni mke kwao, hivyo basi kukaa nao na kuwapa ushauri watoto wetu ni jambo la muhimu kwa ajili ya maisha yao ya baadae.

Watoto nao ni lazima wajaribu kuwafikiana na wazee wao kimantiki zaidi kuliko kimapenzi, na wazee vile vile wanatakiwa kuwa na mantiki katika kumkubali mposaji au kumkataa mposaji huyo anaye leta posa kwao. Sura, mali, na uluwa vinaweza kuwa ni hatari iwapo havito ambatana na tabia njema. Mtoto wa kike anaweza kumtetea mposaji kwa kuwa tu tayari ameshakuwa na mapenzi naye, lakini Waswahili wanasema: "Akipenda chongo huita kengeza". Ndiyo maana mara nyingi sana watoto wetu huwa ni wenye kujuta baadae, hivyo basi ni vizuri na ni lazima tutumie akili zetu katika suala la kuchagua mume au mke mwenye manufaa kwetu pamoja na jamii yetu.

KUOWANA WAISLAMU KWA WAISLAMU

Kuowana Waislamu wao kwa wao ni moja kati ya misingi ya Itikadi ya Kiislamu, hivyo basi kuwalaumu Waislamu, au kuwaita wao kuwa ni wabaguzi na wenye udini, ni suala lisilokuwa na mazingatio ya kiakili, kwani kila mmoja yuko huru katika masuala ya Imani za dini mbali mbali. Usemi unaowataka Waislamu kuchanganyika na wengine katika ndoa ni suala lisilokuwa la kiadilifu, kwani huko ni kuwataka wao waiache sehemu fulani ya Imani yao. Kwa hiyo iwapo mtoto wa Kiislamu ataposwa na asiyekuwa Muislamu, hapo wazee wanatakiwa kuwa na mazingatio ya Imani zao za Kiislamu au Kikristo zinavyo waamuru.

Uislamu huwa unazingatia mambo tofauti katika suala la ndoa. Tabia, hisani, Imani na ujasiri ni moja kati ya mambo yanayo zingatiwa katika ndoa. Kumkataa mposa kwa sababu za msingi, huwa si kumdhulumu mtu huyo, bali ni kumsaidia ili aweze kuyafikia malengo yake ipaswavyo. Watoto wa kike nao ni wenye mapenzi ya haraka, kitu ambacho hua kinasababisha upofu wa kuufahamu ukweli, hasa pale mabinti zetu wanapokuwa katika umri wa chini.

Iwapo mtoto mwenye tabia njema ataozeshwa mtu asiye na tabia nzuri, hilo linaweza kumuathiri binti huyo na kumpotezea hali ya tabia nzuri alizokuwa nazo hapo mwanzo. Hali nzima ya mfumo kamili wa jamii huwa imelala juu ya mgongo wa masuala ya ndoa, kwa hiyo ndoa kitu muhimu kinachotaka kutiliwa maanani na kila familia, na kila mmoja anatakiwa kulisoma vizuri suala hili ili kuleta mafanikio ya kijamii, kwani kuowana kiholela bila ya kuzingatia masuala mbali mbali, kama vile elimu ya wanao owana au hali ya afya za wawili hao, huwa ni kuisaidia jamii katika kuitokomeza kwenye majangwa mbali mbali. Hadi kufikia hapa tutakuwa tumeshaifahamu falsafa na mtazamo wa Kiislamu juu ya mwanamke, na kila mmoja atakuwa ameelewa kuwa: Uislamu huwa haumkandamizi mwanamke bali ni wenye kumtetea na kumpa heshima apaswayo kupewa kiumbe huyu.

KUTO FANANA KWA HAKI ZA WANAWAKE NA WANAUME

Hapo mwanzo tulisema kuwa: Uisalamu una falsafa maalumu juu ya haki za kifamilia, falsafa ambayo ni yenye kwenda kinyume na mitazamo mbali mbali ya karne kumi na nne zilizopita au katika zama zetu hizi za leo, kuhusiana na suala hilo, vile vile tulisema kuwa: Uislamu hauzingatii suala lisemalo kuwa mwanmke na mwanamme ni viumbe wawili wenye kutofautiana Kiubinaadamu, bali Uislamu unawangalia wote wawili kuwa ni wenye haki sawa katika masuala ya Kibinaadamu, kwa kutokana na Ubinaadamu wao.

Uislamu pale ulipomzingatia mwanamke kuwa ni mwanamke pamoja na kumzinagatia mwanamme kuwa ni mwanamme, hapo basi haukuweza kuwawekea wao haki sawa zinazo lingana katika kila kitu, bali kila mmoja baina yao huwa ana haki sawa na mwengine katika yale masuala tu wanayo shirikiana kuwa nayo kwa pamoja bila ya kutofautiana. Lakini kwa upande wa yale masuala amabayo wao huwa ni wenye kutofautiana kwa kutokana na kila mmoja kuwa na hali maalumu ya kimaumbile, kila mmoja huwa ana haki isiyo fanana na mwengine, na hilo si kwa wanawake na wanaume tu, bali ni kwa kila kiumbe anaye ishi katika dunia hii, kwani mbuzi huwa hastahiki kubeba soji la nazi, bali punda ndiye anayestahiki kufanya hivyo, hapa basi utaona kuwa: mwanamke kwa kutokana na hali maalumu ya kimaumbile aliyo nayo, huwa ana aina maalumu ya haki ziendazo na hali halisi ya maumbile yake yalivyo. Hivyo basi mwanamke kuwa ni muhisika zaidi wa jambo fulani, au kuto husika na jambo fulani, huwa si kumdharau mwanamke, bali ni kumpa nafasi yake anayostahiki kupewa kiuadilifu.

MWANAMKE KATIKA AKILI YA KIMAGHARIBI

Nchi za Kimagharibi zinafanya juhudi mbali mbali, ili kumfanya mwanamke awe na haki sawa na mwanamme katika kila kitu, juhudi hizi hazikuanza leo bali ni juhudi za muda mrefu, na bidhaa hii ya fikra za Kimagharibi tayari imeshaingia katika nchi tofauti. Kila nchi leo hua ina aina mbili za makundi ndani ya jamii yake, ndani ya nchi tofauti huwa kuna kundi ambalo hufikiria kuwa: kila bidhaa itokayo katika nchi za Kimagharibi, ni bidhaa safi isiyo na matatizo. Na kwa upande mwengine huwa kuna kundi linalokwenda kinyume na fikra hizo.

Kinachotakiwa na Wamagharibi, si kumpa mwanamke haki yake, bali ni kumgeuza mwanamke kuwa ni mwanamme, au baadhi ya wakati huonekana mwanamme kupewa haki za mwanamke, jambo ambalo huwa ni lenye kuzisambaratisha familia za Kimagharibi. Haidhuru madai yao huwa yanadai kumtukuza mwanamke, lakini uchunguzi wa kiakili hauonyeshi hilo, bali linalo onekana ni kumdhalilisha mwanamke, kwa kumbebesha majukumu yaendayo kinyume na uwezo wa maumbile yake yalivyo.

Kumpa mtoto mdogo mali nyingi kisha ukamuamuru atembee peke yake barabarani, ni kumhatarishia maisha yake, na sio kumpa uhuru wake. Na kumtandaza mwanamke uchi katika hadhara mbali mbali, ni kumuweka panya katika kinyang'anyiro cha paka.

Mavurugiko ya ndoa yaliopo katika nchi mbali mbali huwa yanasababisha na kuto aminiana kwa mke na mume, na iwapo mtu ataamua kumtandaza mkewe mbele ya wanaume, basi ni nani wa kulaumiwa? Huu ndiyo uhuru wa Kimagharibi, haidhuru tabia za nchi zao pamoja na tamaduni zao huwa haziko mbali na aina ya uhuru waliyo nao, lakini si kila bidhaa hua ni neema kwa mataifa mengine.

DOZI MOJA KWA WALIMWENGU WOTE

Kila dokta hua anatowa aina maalumu ya dozi na aina maalumu ya dawa, na linalozingatiwa katika suala hilo, ni jinsi ya hali halisi ya mgonjwa na magonjwa yalivyo, na si busara kwa dokta kutoa aina moja ya dawa na dozi kwa watu wote.

Wamagharibi kila siku huwa wanazitaka nchi nyengine kuuiga mfumo wao wa Kidemokrasia, lakini wao wenyewe ni wenye matatizo mbali mbali katika mifumo yao hiyo ya Kidemokrasia. Si ujinga wa wanasiasa kuzikubali aina mbali mbali za siasa za Kimaghari na kuzitumia katika nchi zetu, lakini tatizo liko kwetu sisi wenyewe, kwani bado sisi hatujawa na uwezo wa kuzalisha fikra zetu wenyewe ziendazo na hali halisi ya jamii zetu na tamaduni zetu zilivyo.

Acha basi sote tuwe na aina moja ya dawa na aina moja ya dozi. Nchi fulani kutumia siasa zilizofahamika na kueleweka vizuri ndani ya jamii yake, ndiyo busara isiyo pingika. Lakini mimi nina uhakika wa kwamba asilimia kubwa ya wananchi wa nchi mbali mbali, huwa hawazitambui kiundani sera za kisiasa zinazotumika ndani ya nchi zao, au huwa hawakubaliani na sera za siasa hizo. Lakini wao huwa wametumbukizwa kwa nguvu ndani ya siasa hizo. Na mara nyingi mataifa mbali mbali huwa yanatumia siasa zisizo kubaliwa na wana jamii wa jamii zao, Hii ni kwa kutokana na kuwa aina hizo za siasa ni zenye kwenda kinyume na tamaduni mbali mbali za nchi hizo.

KAZI NA MAJUKUMU YA SIASA

Siasa huwa hazilengi tu maendeleo ya upande mmoja wa jamii, bali huwa zinalenga sehemu mbali mbali za jamii, kama vile kivazi, dini, michezo na mambo mengine tofauti ya kitamaduni waliyo fungika nayo watu wa taifa fulani. Hivyo basi ni vizuri kwa wananchi kuielewa vizuri aina ya siasa ya nchi yao inavyo waongoza, na hilo ni kwa manufaa ya maendeleo yao ya kidini, kitamaduni na kiuchumi.

Siasa za Kimagharibi hazitokuwa na malengo ya kuzikuza tamaduni za mataifa mbali mbali, bali malengo yake hulenga zaidi ule upande ubomowaji wa damaduni za wengine, jambo ambalo hutekelezwa kwa ajili ya kuziimarisha tamadduni zao, kwa ajili ya manufaa na maslahi yao wenyewe.

Madai ya Kimagharibi yanayo tutaka sisi kuisawazisha dini ya Kiislamu katika sula zima la haki za wanawake, ni madai pocho, kwani ni kitu kisichoingia akilini kuwa mwanamke afanane na mwaname katika kazi mbali mbali za kijamii. Je wao wanatutaka tawatwise wanawake magunia ya mbatata kama wanaume? Au wanatutaka sisi tuwe ni wenye kuzaa kama wanawake?

Wanawake wengi nao wamekuwa ni wenye kulishangiria suala hilo la haki sawa, lakini hawafahamu madhara ya neno hilo, kwani kukandamizwa kwao kwa muda mrefu, kumewasababishia wao kuivamia kauli hiyo yenye madai ya kuwatetea, bila ya kuwa na mazingatio kamili juu ya kauli hiyo. Mimi nikiwa ni kama mtafiti wa masuala haya, ninawataka wao wajielewe kwanza kwa undani kabisa, kabla ya kuivamia kauli hiyo. Kuwa na jazba katika masuala mbali mbali, kunaweza kuihatarisha hali ya afya ya Mwanaadamu kiroho pamoja na kimwili, hivyo basi hala hala mti na macho.

Njia pekee iwezayo kuzilinda haki za wanawake, ni kule kuwatofautisha wanawake na wanaume kinyadhifa, kikazi, kifikra na kimatendo, na kama hatuto fanya hivyo, basi tutakuwa bado tumo katika njia ya kuwanyanyasa wanawake. Iwapo mwanamke atautumia uwezo wake wa kimaumbile aliyo nao, hapo ndipo awezapo kuufikia usawa wa haki zake, na hapo ndipo atakapokuwa ni kiumbe aliye na daraja ya juu, na hata kumzidi mwanamme.

Mwanamme anaweza kumzidi mwanamke kinyadhifa katika baadhi ya masuala fulani, lakini mwanamme kupewa kazi nyingi zaidi kuliko mwanmmke, huwa hakumaanishi kuwa yeye ni mtukufu zaidi, bali lenye kumpa mtu utukufu ni kule kuitekeleza kazi aliyopewa kuifanya kwa ufanisi zaidi na bila ya kuwa na upungufu wowote. Kwa hiyo basi, iwapo mwanamke atayatekeleza majumu yake ipaswavyo kuliko mwanamme hapo basi yeye atakuwa na utukufu zaidi, kwani ubora wa kila mtu, huwa unaangalia namna ya utiifu wa mtu yule alivyo katika utendaji wa majukumu yake ya kijamii na kibinafsi. La muhimu basi ni kule kila mmoja kuielewa hali yake ya kimaumbile ilivyo, pamoja na kuyaelewa majukumu yake, ili tuweze kuvitumia vitu viwili hivi, vikiwa ni kama ngazi ya kuifikia daraja ya utu wa kila mmoja wetu.

MWANAMKE KATIKA DUNIA YA LEO

Jambo la muhimu ambalo Waislamu wanatakiwa kulifahamu ni kwamba: dunia ya kileo inatofautiana kabisa na ulimwengu wa zama za zamani, hivyo basi ni lazima Waislamu wakae kitako na kuzitafakari haki za wanawake kwa jinsi ya hali halisi ya ulimwengu wa leo ulivyo. Katika usemi huu sitaki kusema kuwa haki za wanawake zilizowekwa na Uislamu zibadilishe, bali ninataka kusema kuwa: kuna mambo mengi amabayo yanawalazimisha wanawake kushirikiana na wanaume katika kazi mbali mbali za jamii, hivyo basi si busara kumungalia mwanamke wa zama za hivi sasa, kuwa ni sawa na mwanamke wa zama za zamani. Mwanamke wa kileo katika jamii mbali mbali, analazimika kuungana na jamii katika utendaji wa kazi mbali mbali za jamii kiupana zaidi, kuliko mwanamke wa zama zilizotangulia, sasa je bado sisi tunatakiwa kugombana na dunia kwa kumtenga mwanamke, au tunatakiwa kuzipanga sheria na kanuni maalumu zimlindazo mwanamke, huku akiwa yeye ni mmoja kati ya wafanyakazi wa ndani ya jamii fulani, bila ya kubughudhiwa?

Mashule na vyuo vikuu imekuwa ndiyo sababu kuu za kuharibiwa watoto wa kike kamaadili, hatimae jamii yetu leo imekuwa haijali malezi mema yaendayo sawa na tamaduni zetu za Kiafrika. Kuwa sisi ni wenye tamaduni za Kiafrika kumekuwa leo ni matusi, na hakuna mtu anayeufurahia Uafrika wake, bali kila mmoja anatamani awe mzungu au kwa lugha nyengine, anatamani awe ni mtu mweupe. Yote hayo yamekuja kwa kutokana na baadhi ya watu kuuondoa wivu wa Kiafrika ulikuwa ndani ya vifua vya Waafrika. Hali hii inaonekana zaidi katika upande wa Afrika mashariki, kwani sehemu hii ndiyo sehemu ya mwambao inayokumbwa zaidi na mawimbi ya wageni wenye fikra mbali mbali.

Hadi kufikia miaka ya thamanini na moja thamanini na mbili, bado umalaya na uzinzi ulikuwa ukihesabiwa kuwa ni kero katika jamii zetu, na wala haukuonekana kuwa ni msaada ndani ya jamii hizi, lakini fikra mbali mbali zilizopandikiwa kwa njia moja au nyengine, zikionekana kuwa ni teteo za kumtetea mwanamke, zimeweza kuchukua nafasi kubwa ndani ya jamii zetu, na hadi kufikia leo, mwanamke anaonekana kuwa ni kama chombo cha kuwastarehesha wanaume na kuwatumbuiza kwa njia mbali mbali.

Kwa kila mtu mwenye macho kamili anaweza leo akazifahamu siasa mbali mbali za Kimagharibi zikiwa katika mipango ya kuulea umalaya ndani ya jamii za wengine. Kila sehemu leo katika mikoa mbali mbali kuna mamia ya watoto wasio kuwa na wazee wa kuwalea, hii inatokana na maadili ya zinaa na mimba zisizo dhaminiwa na waume. Jambo ambalo mara nyigi huwa linasababisha utowaji wa mimba kiholela na hatimae kusababisha vifo au magonjwa mbali mbali kwa wasichana wetu wa Kiafrika.

Kuzuka kwa magonjwa mbali mbali kwa upande wa kinamama, kunahatarisha hali nzima ya kijamii, kwani akina mama ndiyo walezi wa jamii zetu, hivyo basi katika kuwatetea wao, kunatakiwa kutumike akili zilizo pevuka kielimu na sio kuifuata mitazamo ya Kimagharibi kiholela.

Kuna tofauti kubwa baina ya Wamagharibi na watu wa mataifa mengine, watu wa mataifa ya Kimagharibu huwa ni wenye kujali zaidi suala la haki kuliku masuala ya kitabia, lakini watu wa mataifa mengine kama vile Waafrika, huwa wana jali zaidi suala la tabia kuliko wanavyo yajali masuala ya haki na sheria. Hivyo basi kwa waafrika utu kwao huwa ni jambo lenye kipau mbele zaidi hata kushinda haki na sheria, ndiyo maana mara nyingi Waafrika huwa si wenye kushtakiana kiholela.

Kwa upande wa Wamagharibi, wao mara nyingi huwa ni wenye kupindukia mika katika suala la kuzilinda haki zao au haki za wana nchi wao, jambo ambalo mara kwa mara huwa lina sababisha vifo vya maelfu ya watoto wadogo na kina mama, kwani si mara moja wala mbili Wamagharibi wamekua wakizivamia nchi mbali mbali kwa kisingizio cha utetezi wa haki fulani. Kila mmoja natakiwa kuelewa kuwa: kuwafuata Wamagharibi kifikra ni kuutokomeza utu wetu na urithi wetu wa jadi tuliyo rithishwa na wazee wetu.

Kuilida jamii kutokaa na maradi au maafa mbili mbali ni moja kati ya kazi muhimu za serikali. serikali zetu leo zimeweza kufaulu kwa kiasi fulani, katika kuyapiga vita maradhi mbali mbali, kama vile polio, malaria, na mengineyo, na sasa umefika wakati wa kuupiga vita umalaya, kwani umalaya ni maradhi mabaya ndani ya jamii yetu, na ni wenye kusambaza maradhi hatari ya AIDS, maradhi ambayo yamekuwa yakisonga mbele kwa nguvu zaidi humu barani Afrika.

NATIJA

Uislamu haukumkandamiza mwanamke kwa kumpangia sheria maalumu katika suala la ndoa, bali umeilinda jamii pamoja na mwanamke kiujumla. Uislamu vile vile umelizingatia suala la kuaminiana kwa mke na mume, na ukampa hiari mwanamme kumuacha mkewe iwapo itathibiti kuwa yeye hakuwa ni mtawa kabla ya kupita suala la ndoa, na yote hayo hayakuzingatia kumkandamiza mwanamke au mwanamme, bali kilichozingatiwa ni usalama wa jamii kiujumla. Kwa hiyo haki na uadilifu hua si hisia za mtu fulani zinavyo muelekeza, bali hua ni kanuni au sheria maalumu ziendazo na hali halisi ya kimaumbile ya kila mmoja wetu. Ili uadilifu usimame ni lazima kila mmoja wetu aizingatie hali halisi ya kimaumbile iliyomo ndani ya ulimwengu huu, kisha akiheshimu kila kimoja kwa hali yake kilivyo. Na hayo ndiyo mafunzo ya dini ya Kiislamu.

Wamagharibi pamoja na wafuasi wao wamemdhalilisha Mwanaadamu kwa kule kumfanya yeye awe ni mtumwa wa mwili wake, na wamemdalilisha mwanamke kwa kumfanya yeye awe ni mtumwa wa mwili wa mwanamme. Wao wanamuhesabu Mwanaadamu kuwa ni kiwiliwili tu, kwa hiyo wao huwa wanafanya kila namna ya hila kwa ajili ya kuutumikia mwili wao, huku wakiwataka wengine kua ni wafuasi wao. Wamesahau kuwa Mwanaadamu ni roho na wala si kiwiliwili tu, wao wamezitupa nyuma huduma za kiroro huku wakishikamana na huduma za kimwili. Jambo ambalo limemgeuza Mwanaadamu kuwa ni myama asiye fikiria maisha yake ya baadae, na yeyeto yule miongoni mwao anapogutuka na kufahamu kuwa mbele yake kuna giza, kwa kule kutoyafahamu maisha yake ya baadae yatakavyokua, baada ya kuondoka katika ulimwengu huu, hapo basi huamua kujiuwa, na hiyo ndiyo hatima ya wengi leo katika ulimwengu wa Kimagharibi.

REJEO

1- Suratu Nisaa Aya ya 1.
2- Suratu Aa'raaf kuanzia Aya ya 19 hadi Aya ya 27.
3-Suratu Nahli Aya ya 97.
4- Suratul Baqara Aya ya 187.

MWISHO 

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini