DA'AWA KWA WATU WA THAMUUD
BISMILLAAHI RAHMANI RAHIM
DA'AWA KWA WATU WA THAMUUD
Nabii Swaalih عليه السلام alikuwa ni Mtume katika kabila maarufu ambalo jina lake linatokana na jina la Babu yao Thamuud ambaye ni katika ukoo wa Nabii Nuuh عليه السلام
Kwa hivyo jina lake ni Swaalih ibn 'Ubayd ibn Maasih ibn 'Ubayd ibn Haajir ibn Thamuud, ibn 'Aabir ibn Iram, ibn Saam, ibn Nuuh. Naye Swaalih na watu wake wa Thamuud ni waarabu waliokuwa wakiishi Hijr ambayo iko baina ya Hijaaz na Tabuuk (Kaskazini magharibi ya Madiynah) ambako siku moja Mtume
صلى الله عليه وآله وسلم
alipita wakati wanaelekea kwenda kwenya vita vya Tabuuk kama tutakavyoelezea mwisho wa kisa hiki.
Hiki ndio kisa chake Nabii Swaalih عليه السلم na watu wake kama tulivyoelezewa katika aya mbali mbali za Qur'aan Watu wa Thamuud walikuwa ni watu baada ya Nabii Huud عليه السلام ambao walikuwa wakiabudu masanamu na baada ya kuletewa Nabii Huud عليه السلام na kumkanusha Allaahسبحانه وتعالى Aliwaangamiza. Na baada ya miaka, watu wa Thamuud wakaibuka na kuwa na nguvu na ufahari. Nao pia waliabudu masanamu, kwa hivyo Allaah
سبحانه وتعالى Akawatumia mjumbe miongoni mwao naye ni Nabii Swaalih عليه السلام ambaye naye kama kawaida ya Mitume alikuja na wito uleule wa kuwaita watu katika Tawhiiyd ya Allaahسبحانه وتعالى yaani kumuabudu Yeye pekee bila ya kumshirikisha na kitu, na kuwanasihi waache ibada ya masanamu na pia kuwataka watubu kwa Mola wao kwa kufuru wanayoifanya.
(وَإِلَى ثَمودَ أَخَاهمْ صَالِحًا قَالَ يَا قَوْمِ اعْبدواْ اللّهَ مَا لَكم مِّنْ إِلَهٍ غَيْره هوَ أَنشَأَكم مِّنَ الأَرْضِ وَاسْتَعْمَرَكمْ فِيهَا فَاسْتَغْفِروه ثمَّ توبواْ إِلَيْهِ إِنَّ رَبِّي قَرِيبٌ مّجِيبٌ )
{{Na kina Thamud tuliwapelekea ndugu yao Swaalih. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye. Yeye ndiye aliyekuumbeni katika ardhi, na akakuwekeni humo. Basi mwombeni msamaha, kisha mtubu kwake. Hakika Mola wangu Mlezi yupo karibu, anaitikia maombi}Huud: 61
Kwa maana kwamba: Amekujaalieni kuwa makhalifa baada ya watu wengine (kina 'Aad na wa nyuma yao) ili mfikiri na mtambue ubaya wao waliotenda, na nyinyi msiwe kama wao, na Akakujaalieni katika hii ardhi na kukuneemesheni neema mbali mbali kama za mashamba na matunda na majumba ya fahari mkastarehe, basi Yeye Pekee ndiye anayestahiki kuabudiwa bila ya kumshirikisha, vile vile mkabilini Mola wenu kwa kumshukuru na kufanya amali njema wala msjije kumkhalifu amri Zake na kutoka nje ya mipaka kwa kutokumtii, basi rudini kwake kwa kutubia na Yeye Allaahسبحانه وتعالى yuko tayari kupokea tawbah zenu. Aya ifuatayo inaeleza zaidi neema hizo walizojaaliwa na pia kuonesha ukumbusho wa Swaalih عليه السلام kwa hao watu wa Thamuud kwa kuwaita kwao kwenye dini ya haki.
وَإِلَى ثَمودَ أَخَاهمْ صَالِحًا قَالَ يَا قَوْمِ اعْبدواْ اللّهَ مَا لَكم مِّنْ إِلَهٍ غَيْره قَدْ جَاءتْكم بَيِّنَةٌ مِّن رَّبِّكمْ هَذِهِ نَاقَة اللّهِ لَكمْ آيَةً فَذَروهَا تَأْكلْ فِي أَرْضِ اللّهِ وَلاَ تَمَسّوهَا بِسوَءٍ) فَيَأْخذَكمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ)
{{Na kwa Thamuud tulimpeleka ndugu yao, Swaalih. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye. Hakika imekwisha kukufikieni Ishara iliyo wazi kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Huyu ni ngamia jike wa Mwenyezi Mungu aliye ni Ishara kwenu. Basi mwachieni ale kwenye ardhi ya Mwenyezi Mungu, wala msimdhuru, isije kukushukieni adhabu chungu}} Al-A'araaf: 73
(وَاذْكرواْ إِذْ جَعَلَكمْ خلَفَاء مِن بَعْدِ عَادٍ وَبَوَّأَكمْ فِي الأَرْضِ تَتَّخِذونَ مِن سهولِهَا قصورًا وَتَنْحِتونَ الْجِبَالَ بيوتًا فَاذْكرواْ آلاء اللّهِ وَلاَ تَعْثَوْا فِي الأَرْضِ مفْسِدِينَ)
{{Na kumbukeni alivyokufanyeni wa kushika pahala pa 'Aadi na akakuwekeni vizuri katika nchi, mnajenga majumba ya fakhari katika nyanda zake, na mnachonga majumba katika milima. Basi zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu wala msitende uovu katika nchi kwa ufisadi}} Al-A'araaf: 74
Kama zilivyo umma zilizopita zilipojiwa na Mitume, wakaamini wachache miongoni mwao na wengi wakamkanusha.
(وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا إِلَى ثَمودَ أَخَاهمْ صَالِحًا أَنِ اعْبدوا اللَّهَ فَإِذَا همْ فَرِيقَانِ يَخْتَصِمونَ)
{{Na kwa kina Thamuud tulimtuma ndugu yao Swaalih kuwaambia: Muabuduni Mwenyezi Mungu. Basi wakawa makundi mawili yanayogombana}} An-Naml :45 Waliomkanusha walimhutumu kuwa anawaletea shari, na kwamba labda akili yake haiko sawa kwani hawakumtegemea yeye Swaalih عليه السلام ambaye kwao alikuwa ni mtu mwema kabisa, aje kuwakataza kuacha waliyokuja nayo mababu zao na kutaka wamfuate hayo anayotaka yeye Swaalih عليه السلام? Wakamwambia;
( قَالواْ يَا صَالِح قَدْ كنتَ فِينَا مَرْجوًّا قَبْلَ هَذَا أَتَنْهَانَا أَن نَّعْبدَ مَا يَعْبد آبَاؤنَا وَإِنَّنَا لَفِي شَكٍّ مِّمَّا تَدْعونَا إِلَيْهِ مرِيبٍ)
{{ Wakasema: Ewe Swaalih! Hakika kabla ya haya ulikuwa unatarajiwa kheri kwetu. Je, unatukataza tusiwaabudu waliyokuwa wakiwaabudu baba zetu? Na hakika sisi tuna shaka na wasiwasi kwa hayo unayotuitia}} Huud: 62
Walikuwa na shaka kubwa juu ya yale Swaalih aliyowalingania nayo na kuyaona ni mapya! Swaalihعليه السلام akawajibu:
(قَالَ يَا قَوْمِ أَرَأَيْتمْ إِن كنت عَلَى بَيِّنَةً مِّن رَّبِّي وَآتَانِي مِنْه رَحْمَةً فَمَن يَنصرنِي مِنَ اللّهِ إِنْ عَصَيْته فَمَا تَزِيدونَنِي غَيْرَ تَخْسِيرٍ)
{{Akasema: Enyi watu wangu! Mwaonaje ikiwa ninazo dalili zilizo wazi kutokana na Mola wangu Mlezi, naye akawa kanipa rehema kutoka kwake - je, ni nani atakaye ninusuru kwa Mwenyezi Mungu nikimuasi? Basi nyinyi hamtanizidishia ila khasara tu}} Huud:63
(قَالَ يَا قَوْمِ أَرَأَيْتمْ إِن كنت عَلَى بَيِّنَةً مِّن رَّبِّي)
{{Akasema: Enyi watu wangu! Mwaonaje ikiwa ninazo dalili zilizo wazi kutokana na Mola wangu Mlezi}} Dalili za dhahiri zenye uhakika kabisa kwa yale anayowaitia kumuabudu kwamba Yeye ndiye Mola wa Viumbe wote na Mola wa mbingu na Ardhi na mwenye kupasa kuabudiwa kwa haki.
(وَآتَانِي مِنْه رَحْمَةً)
{{naye akawa kanipa rehema kutoka kwake}} Rahma kutoka kwa Allaah سبحانه وتعالى kumchagua yeye na kumpa uongofu na kumfanya Mjumbe Wake Allaah
سبحانه وتعالى
Aliyemtuma kwao kuwatoa katika upotofu.
(فَمَن يَنصرنِي مِنَ اللّهِ إِنْ عَصَيْته فَمَا تَزِيدونَنِي غَيْرَ تَخْسِيرٍ)
{{je, ni nani atakaye ninusuru kwa Mwenyezi Mungu nikimuasi?}}
Nikiacha kukuiteni katika hakki ya kumuabudu Allaah سبحانه وتعالى Pekee basi nyinyi hamtoweza kunifaa wala kuninusuru na adhabu yake Allaah سبحانه وتعالى atakaponiadhibu, bali itakuwa ni hasara tu na kuangamia kwangu. Vile vile wakamwambia:
(قَالوا إِنَّمَا أَنتَ مِنَ الْمسَحَّرِينَ)
{{Wakasema: Hakika wewe ni miongoni mwa waliorogwa}}
Ashura: 153 Mujaahid kasema; Wamemaanisha kuwa kaathirika na uchawi. Wafasiri wengi wamefasiri kwamba ina maana; Hujui unachokisema kutuita katika ibada ya mungu mmoja na kuacha miungu mingine! Hiyo ndio ilikuwa kawaida ya watu wa umma za nyuma, walipojiwa na Mitume yakawa majibu yao ni kuwaambia hao Mitume kuwa ni wachawi! kama alivyoambiwa vile vile Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na makafiri wa ki-Quraysh. Vile vile ni kawaida yao nyingine kuwadharau hao Wajumbe wa Allaah سبحانه وتعالى kwa vile wao ni binaadamu tu kama wao. Na wakisema:
(مَا أَنتَ إِلَّا بَشَرٌ مِّثْلنَا)
{{Wewe si chochote ila ni mtu kama sisi}} Ashura: 154
(كَذَّبَتْ ثَمود بِالنّذرِ) ( فَقَالوا أَبَشَرًا مِّنَّا وَاحِدًا نَّتَّبِعه إِنَّا إِذًا لَّفِي ضَلَالٍ وَسعرٍ) (أَؤلْقِيَ الذِّكْر عَلَيْهِ مِن بَيْنِنَا بَلْ هوَ كَذَّابٌ أَشِرٌ) ( سَيَعْلَمونَ غَدًا مَّنِ الْكَذَّاب الْأَشِر)
23. Thamudi waliwakanusha Waonyaji
24. Wakasema: Ati tumfuate binaadamu mmoja katika sisi? Basi hivyo sisi tutakuwa katika upotofu na kichaa!
25. Ni yeye tu aliyeteremshiwa huo ukumbusho kati yetu sote? Bali huyu ni mwongo mwenye kiburi!
26. Kesho watajua ni nani huyo mwongo mwenye kiburi.
Al-Qamar : 23-26
Kama kweli yeye ni Mtume basi wametaka miujiza ndio waweze kumuamini.
(مَا أَنتَ إِلَّا بَشَرٌ مِّثْلنَا فَأْتِ بِآيَةٍ إِن كنتَ مِنَ الصَّادِقِينَ)
{{Wewe si chochote ila ni mtu kama sisi. Basi lete Ishara ukiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli}} Ashu'araa: 154 Nabii Swalih عليه السلام akajitenda nao kwani alikwishakata tamaa nao:
(فَتَوَلَّى عَنْهمْ وَقَالَ يَا قَوْمِ لَقَدْ أَبْلَغْتكمْ رِسَالَةَ رَبِّي وَنَصَحْت لَكمْ وَلَكِن لاَّ تحِبّونَ النَّاصِحِين)
{{Basi Swaalih akwaacha na akasema: Enyi watu wangu! Nilikufikishieni Ujumbe wa Mola wangu Mlezi, na nikakunasihini, lakini nyinyi hamwapendi wenye kunasihi}} Al-A'araaf: 79
Ishara au Miujiza waliyotaka kutoka kwa Nabii Swaalih عليه السلام ni ngamia kama tutakavyoona:
MIUJIZA YA NGAMIA
Wafasiri wamesema kwamba siku moja watu wa Thamuud walikusanyika katika baraza yao akaja Nabii Swaalihعليه السلام kuwanasihi kwa kuwaita katika Tawhiiyd, na akawapa mawaidha na kuwaonya. Wakataka alama au uhakikisho kuwa huo ujumbe aliokuja nao, ulitoka kweli kwa Mungu. Wakamwambia, "ewe Swaalih ikiwa utatutolea katika jabali lile (wakaashiria jabali lililokuwepo) ngamia wa kike, ambaye ana mimba ya miezi kumi, na wakataja sifa nyingine kadha na kadha.
Nabii Swaalihعليه السلام akawauliza; "je, mkiletewa hiyo miujiza mliyoomba na mliyotaka iwe vile vile, mtaniamini na kuamini ujumbe niliotumwa nao kwenu?" Wakajibu: "Ndio tutakuamini na kukusadiki yote utakayotuambia" Nabii Swaalihعليه السلام akachukua ahadi hiyo kwa watu wake kisha akamuelekea Allaahسبحانه وتعالى kumuomba awaletee miujiza hiyo waliyotaka. Kama tunavyojua na kuamini kuwa kwa Allaahسبحانه وتعالى hakuna jambo lolote linalomshinda kulifanya kama Anavyosema mwenyewe:
(إِنَّمَا أَمْره إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَنْ يَقولَ لَه كنْ فَيَكون)
{{Hakika amri yake anapo taka kitu ni kukiambia tu: Kuwa! Na kikawa}} Yasiyn: 82
Basi watu wa Nabii Swaalih عليه السلام wakakusanyika mbele ya jabali hilo na wakaona muujiza huo wa ngamia mbele ya macho yao. Allaahسبحانه وتعالى Aliamrisha jabali lipasuke na akatoka ngamia mwenye sifa zile zile walizozitaka; ngamia mwanamke, mwenye mimba ya miezi kumi, mweupe na sifa zote walizozitaka. Akatokeza huyo ngamia kutoka kwenye hilo jabali akipita mbele yao. Ni jambo tukufu, miujiza mikubwa, ya pekee, ya kustaajabisha kabisa, yenye dalili za dhahiri ya uwezo mkubwa wa Allaahسبحانه وتعالى na bila ya shaka msomaji atawaza hapa "Je, waliamini?" mwengine atawaza "bila ya shaka wataamini". Lakini jambo la kushangaza ni kwamba juu ya kwamba wameoneshwa muujiza mkubwa mbele ya macho yao, si wote walioamini. Wako walioamini lakini wengi wao hawakuamini! Subhanah Allaah! Hii inatuonyesha jinsi watu wa zamani walivyokuwa wakaidi sana katika kufuata haki. Hata makafikiri wa ki-Quraysh pia walikuwa hivyo hivyo, wakaidi. Miujiza mingapi imewafikia mbele ya macho yao na hawakukubali?. AlhamduliLLaah sisi Umma Wa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم tumepewa Rahma na Allaahسبحانه وتعالى ya kuamini haki, kuamini Qur'aan ingawa wakati zilipokuwa zinateremshwa aya hatukuwepo, lakini tumeziamini aya hizo na zaidi kumpenda Mtume
صلى الله عليه وآله وسلم
bila ya kumuona. Hivyo tunapaswa kushukuru neema hii tuliyojaaliwa na Allaahسبحانه وتعالى kuwa ni umma bora kabisa kuliko umma zote zilizopita.
Na tunaona katika aya zinazofuata kuwa wale wasioamini ambao zaidi ni wakubwa kwa cheo wakawa wanawashawishi walio dhaifu kutuokumuamini Nabii Swaalihعليه السلام
(قَالَ الْمَل الَّذِينَ اسْتَكْبَرواْ مِن قَوْمِهِ لِلَّذِينَ اسْتضْعِفواْ لِمَنْ آمَنَ مِنْهمْ أَتَعْلَمونَ أَنَّ صَالِحًا مّرْسَلٌ مِّن رَّبِّهِ قَالواْ إِنَّا بِمَا رْسِلَ بِهِ مؤْمِنونَ)
{{Waheshimiwa wa kaumu yake wanao jivuna waliwaambia wanao onewa wenye kuamini miongoni mwao: Je, mnaitakidi ya kwamba Saleh ametumwa na Mola Mlezi wake? Wakasema: Hakika sisi tunayaamini yale aliyo tumwa}} Al-A'araaf :75
( قَالَ الَّذِينَ اسْتَكْبَرواْ إِنَّا بِالَّذِيَ آمَنتمْ بِهِ كَافِرونَ )
{{ Wakasema wale wanao jivuna: Sisi tunayakataa hayo mnayo yaamini}} Al-A'araaf: 76
Ngamia huyo wa Allaah سبحانه وتعالى aliletwa na shuruti zake walizoombwa wazitimize kama vile wamwache huru wasimdhuru, wala wasimuuwe.
(وَإِلَى ثَمودَ أَخَاهمْ صَالِحًا قَالَ يَا قَوْمِ اعْبدواْ اللّهَ مَا لَكم مِّنْ إِلَهٍ غَيْره قَدْ جَاءتْكم بَيِّنَةٌ مِّن رَّبِّكمْ هَذِهِ نَاقَة اللّهِ لَكمْ آيَةً فَذَروهَا تَأْكلْ فِي أَرْضِ اللّهِ وَلاَ تَمَسّوهَا بِسوَءٍ فَيَأْخذَكمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ )
{{Na kwa Thamud tulimpeleka ndugu yao, Saleh. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye. Hakika imekwisha kukufikieni Ishara iliyo wazi kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Huyu ni ngamia jike wa Mwenyezi Mungu aliye ni Ishara kwenu. Basi mwachieni ale kwenye ardhi ya Mwenyezi Mungu, wala msimdhuru, isije kukushukieni adhabu chungu}}. Al-A'araaf:73
Pia katika Suratul-Qamar Allaahسبحانه وتعالى Kamuamrisha Nabii Swaalih عليه السلام asubiri na kuwatazama watafanya nini juu ya mtihani huu watakaopewa wa muujiza walioutaka, je wataamini kweli? Au wataendelea na kufru yao?
(إِنَّا مرْسِلو النَّاقَةِ فِتْنَةً لَّهمْ فَارْتَقِبْهمْ وَاصْطَبِرْ )
{{Hakika Sisi tutawapelekea ngamia jike ili kuwajaribu, basi watazame tu na ustahamili}} Al Qamar: 27 Shuruti nyingine ni kwamba ilikuwa waweke zamu ya kunywa maji katika mji huo, siku moja wamwachie anywe ngamia huyo na siku nyingine wanywe wao kina Thaamuud.
( وَنَبِّئْهمْ أَنَّ الْمَاء قِسْمَةٌ بَيْنَهمْ كلّ شِرْبٍ مّحْتَضَرٌ )
{{Na waambie kwamba maji yatagawanywa baina yao; kila sehemu ya maji itahudhuriwa na aliye khusika}} Al-Qamar: 28
Basi mwanzo wakawafikiana kwamba abakie huyo ngamia kwani alikuwa ni ngamia mwenye baraka nyingi, maziwa yake yaliyokamuliwa siku moja yaliwatosheleza watu wa mji mzima. Alikuwa akilala mahali ambapo wanyama wengine walikuwa hawapakaribii pahali hapo kulala naye, kwa hiyo walijua kuwa huyu hakuwa ngamia wa kawaida bali ni dalili na ishara kutoka kwa Allaah سبحانه وتعالى. Kwa hivyo wakamwacha atembee anapotaka katika mji huo, ale anavyotaka, na zamu iwe siku moja anywe maji yeye na siku ya pili wanywe wao. Na siku ya zamu yao kunywa maji walijichotea maji ya kutosha na kuyaweka ili kuyatumia kwa haja zao ya siku ya pili. Na ile siku ya kunywa ngamia maji, wao Wathamudu walikuwa wakinywa maziwa yake huyo ngamia. Na hii ndio kauli ya Allaahسبحانه وتعالى
(قَالَ هَذِهِ نَاقَةٌ لَّهَا شِرْبٌ وَلَكمْ شِرْب يَوْمٍ مَّعْلومٍ)
{{ Akasema: Huyu ngamia jike; awe na zamu yake ya kunywa, na nyinyi muwe na zamu yenu ya kunywa katika siku maalumu}} Ash-Shu'araa :155
Tena wakaonywa kuwa wasimdhuru wasije kupata adhabu.
(وَلَا تَمَسّوهَا بِسوءٍ فَيَأْخذَكمْ عَذَاب يَوْمٍ عَظِيمٍ )
{{Wala msimguse kwa uwovu, isije ikakushikeni adhabu ya Siku Kubwa}} Ash-Shua'raa : 156 Lakini wapi! Hawakutaka kufuata amri ya mwanzo ya kuacha ibada yao ya masanamu wala amri hii ya kumtunza huyo ngamia kama walivyoambiwa, bali walimuua na kutaka kumuua pia Nabii Swaalihعليه السلام Kasema Allaah سبحانه وتعالى
(وَآتَيْنَا ثَمودَ النَّاقَةَ مبْصِرَةً فَظَلَمواْ بِها)
{{Na tuliwapa Wathamudi ngamia jike kuwa ni Ishara iliyo dhaahiri, lakini walidhulumu kwaye}} Israa: 59 Maana yake ni kwamba walikanusha na wakamdhuru. Basi haukupita muda, wakaona hawawezi kustahmili hali hiyo ya ngamia na masharti waliyopewa. Na chuki zao walizokuwa nazo kwa Swaalihعليه السلام wakazigeuza kumchukia ngamia, wakakutana wakubwa wao Wathamudi wakapanga kumuua ngamia ili wapate uhuru wa maji yao, na shetani akawapambia njama zao hizo kama alivyosema: Allaahسبحانه وتعالى
(فَعَقَرواْ النَّاقَةَ وَعَتَوْاْ عَنْ أَمْرِ رَبِّهِمْ وَقَالواْ يَا صَالِح ائْتِنَا بِمَا تَعِدنَا إِن كنتَ مِنَ الْمرْسَلِينَ)
{{ Na wakamuuwa yule ngamia, na wakaasi amri ya Mola Mlezi wao, na wakasema: Ewe Swaalih! Tuletee unayo tuahidi ikiwa wewe ni miongoni mwa Mitume}} A'araaf :77 Juu ya hivyo wakamhimiza Nabii Swaalih عليه السلام awaletee hiyo adhabu aliyowaonya nayo mwanzo ikiwa hawatofuata masharti ya kumhifadhi ngamia wa Allaahسبحانه وتعالى Kwa usemi wao huo yakajumuika maasi haya yafuatayo: " Wamekhalifu amri ya Allaah سبحانه وتعالى na Mtume wake kwa kumuua ngamia huyo. " Kufanya istihizai na kuhimiza adhabu ya Allaah سبحانه وتعالى iwateremkie.
Wakastahiki adhabu ya Allaah سبحانه وتعالى kama alivyowaonya kabla:
(وَلاَ تَمَسّوهَا بِسوءٍ فَيَأْخذَكمْ عَذَابٌ قَرِيبٌ)
{{wala msimguse kwa ubaya, isije ikakuangamizeni adhabu iliyo karibu}} Huud: 64 Katika aya nyingine Allaah سبحانه وتعالى
Ametaja aina za adhabu hizo:
(وَلَا تَمَسّوهَا بِسوءٍ فَيَأْخذَكمْ عَذَاب يَوْمٍ عَظِيمٍ)
{{wala msimdhuru adhabu ya Siku Kubwa}} Ash-Shu'araa :156
(وَلاَ تَمَسّوهَا بِسوَءٍ فَيَأْخذَكمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ)
{{wala msimdhuru isije kukushukieni adhabu chungu}}. Al-A'araaf: 73
MPANGO WA KUMUUA NGAMIA
Wakapanga kumuua ngamia na wakatafuta usaidizi kutoka kwa mwanamke kutoka kabila la heshima na aliye tajiri kabisa akiitwa Saduq Bint Mahya. Akajitolea kujiuza kwa kijana aliyeitwa Masra'i ibn Mahraj kwa sharti amkate miguu ngamia. Mwanamke mwengine mtu mzima akiitwa Aniza, alijitolea kumuuza mtoto wake wa kike kwa kijana aliyeitwa Qudaar ibn Saluf kwa sharti amuue ngamia. Vijana hao wawili walipata tamaa na hayo waliyoahidiwa ya kupata wasichana, wakatoka kutafuta watu wengine saba kuwasaidia kufanya kazi hiyo. Vijana hao wawili wakaungana na wengine saba wakawa ni jumla ya watu tisa.
Amesema Allaah سبحانه وتعالى kuhusu hao watu tisa na mipango yao ya kumuua ngamia katika Suratun-Naml:
(وَكَانَ فِي الْمَدِينَةِ تِسْعَة رَهْطٍ يفْسِدونَ فِي الْأَرْضِ وَلَا يصْلِحونَ )
{{Na walikuwamo mjini watu tisa wakifanya ufisadi katika nchi wala hawafanyi la maslaha}} An-Naml: 48 Wakawa wanamfuatilia ngamia na kumvizia, wakitazama nyendo zake zote. Alipokuja ngamia kunywa maji katika kisima, Masra'i akamdunga katika mguu wake kwa mshale. Ngamia aljaribu kukimbia lakini alishindwa kwani mshale ulishamwingia katika mguu na kumjeruhi. Qudaar akamfuata ngamia na kumdunga mshale katika mguu mwengine. Ngamia akaanguka chini, na kisha akamchoma na upanga.
( فَنَادَوْا صَاحِبَهمْ فَتَعَاطَى فَعَقَرَ) ( فَكَيْفَ كَانَ عَذَابِي وَنذرِ )
29. {{Basi wakamwita mtu wao akaja akamchinja}}
30. {{Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu!}}
Al-Qamar: 29-30
Maelezo zaidi yaliyopo katika Suratus-Shams yanaeleza:
(كَذَّبَتْ ثَمود بِطَغْوَاهَا) ( إِذِ انبَعَثَ أَشْقَاهَا) ( فَقَالَ لَهمْ رَسول اللَّهِ نَاقَةَ اللَّهِ وَسقْيَاهَا ) (فَكَذَّبوه فَعَقَروهَا فَدَمْدَمَ عَلَيْهِمْ رَبّهم بِذَنبِهِمْ فَسَوَّاهَا ) ( وَلَا يَخَاف عقْبَاهَا )
11. {{Kina Thamudi walikadhibisha kwa sababu ya upotofu wao}}
12. {{Alipo simama mwovu wao mkubwa,}}
13. {{Hapo Mtume wa Mwenyezi Mungu alipo waambia: Huyu ni ngamia wa Mwenyezi Mungu, mwacheni anywe maji fungu lake}}
14. {{Lakini walimkadhibisha na wakamchinja ngamia, kwa hivyo Mola wao Mlezi aliwaangamiza kwa sababu ya dhambi zao na akawafuta kabisa}}
15. {{Wala Yeye haogopi matokeo yake.}} Ash-Shams 11-15
Na hii ni hadithi ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kuhusu mtu muovu kabisa:
عن عمار بن ياسر، قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم لعلي: "ألا أحدثك بأشقى الناس"؟ قال: بلى، قال: "رجلان: أحدهما أحيمر ثمود الذي عقر الناقة، والذي يضربك يا علي على هذا ـ يعني قرنه ـ حتى تبتل منه هذه ـ يعني لحيته. رواه ابن أبي حاتم
((Kutoka kwa 'Ammaar bin Yaasir ambaye kasema: Alisema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kumwambia 'Aliy, "Je, nikujulishe ni yupi mtu muovu kabisa?" Akasema ndio; kasema, "watu wawili; mmoja ni mpiga chuku wa Thamuud aliyemuua ngamia na mwengine ni yule atakayekupiga ewe 'Aliy hapa juu (yaani kichwani kwake) mpaka hizi (ndevu) zirowe damu")) Imesimuliwa na ibn Haatim
Aya nyingine katika suratul A'araaf inazidi kutuelezea tukio la uovu wao kwa ngamia:
(فَعَقَرواْ النَّاقَةَ وَعَتَوْاْ عَنْ أَمْرِ رَبِّهِمْ وَقَالواْ يَا صَالِح ائْتِنَا بِمَا تَعِدنَا إِن كنتَ مِنَ الْمرْسَلِينَ)
{{Na wakamuuwa yule ngamia, na wakaasi amri ya Mola Mlezi wao, na wakasema: Ewe Swaalih! Tuletee unayo tuahidi ikiwa wewe ni miongoni mwa Mitume}} Al-A'araaf: 77
Wauaji hao wakashangiliwa na kupongezwa kwa uhodari wao huo, walifurahikiwa kwa nyimbo na mashairi ya kuwasifu uhodari wao. Na kwa ujeuri wao wakamkejeli Swaalih عليه السلام Nabii Swaalih عليه السلام akawapa onyo kuwa waendelee kustarehe kwa muda wa siku tatu tu na wataona.
(فَعَقَروهَا فَقَالَ تَمَتَّعواْ فِي دَارِكمْ ثَلاَثَةَ أَيَّامٍ ذَلِكَ وَعْدٌ غَيْر مَكْذوبٍ )
{{ Wakamchinja. Basi (Saleh) akasema: Stareheni katika mji wenu muda wa siku tatu. Hiyo ni ahadi isiyo kuwa ya uwongo}} Huud:65 Wapi! Hawakumuamini tena Swaalih عليه السلام kwa onyo hilo alilowapa, wakamuuliza Swalih عليه السلام na kuihimiza kwa istihzai adhabu "kwa nini siku tatu?" Naye akawajibu kwa masikitiko na huku kuwanasihi kuwa ni bora kwao watubie kuliko kuhimiza hiyo adhabu.
(قَالَ يَا قَوْمِ لِمَ تَسْتَعْجِلونَ بِالسَّيِّئَةِ قَبْلَ الْحَسَنَةِ لَوْلَا تَسْتَغْفِرونَ اللَّهَ لَعَلَّكمْ ترْحَمونَ)
{{Akasema: Enyi watu wangu! Kwa nini mnauhimiza uwovu kabla ya wema? Kwa nini hamuombi msamaha kwa Mwenyezi Mungu ili mrehemewe?}} An-Naml: 46
Walimjibu tena kwa ujeuri:
(قَالوا اطَّيَّرْنَا بِكَ وَبِمَن مَّعَكَ قَالَ طَائِركمْ عِندَ اللَّهِ بَلْ أَنتمْ قَوْمٌ تفْتَنونَ )
{{Wakasema: Tuna kisirani nawe na wale walio pamoja nawe. Yeye akasema: Uaguzi wa ukorofi wenu uko kwa Mwenyezi Mungu; lakini nyinyi ni watu mnao jaribiwa}}. An-Naml: 47 Walisema "Swaalih anasema kuwa atatumaliza baada ya siku tatu, lakini sisi tutammaliza yeye na aila yake kabla ya hizo siku tatu hazikufika."
NJAMA ZA KUMUUA NABII SWAALIH
Kisha wakafanya njama za kumuua Nabii Swaalih عليه السلام kama inavyoelezwa katika Suratun-Naml Allaah سبحانه وتعالى katika aya hizo Ametuelezea kuhusu watu hao waovu ambo ni viongozi wa wa Thaamuud waliokua wakiwapotoa watu wao kutokumuamini Nabii Swaalih na kumkanusha na ujumbe aliokuja nao. Na baada ya kumuua ngamia sasa wamepanga kumuua Swaalih عليه السلام
(وَكَانَ فِي الْمَدِينَةِ تِسْعَة رَهْطٍ يفْسِدونَ فِي الْأَرْضِ وَلَا يصْلِحونَ)
{{Na walikuwamo mjini watu tisa wakifanya ufisadi katika nchi wala hawafanyi la maslaha}}. An-Naml: 48
(يفْسِدونَ فِي الْأَرْضِ وَلَا يصْلِحونَ)
{{wakifanya ufisadi katika nchi wala hawafanyi la maslaha}} Ni kwamba walikuwa wakilazimishia watu wa Thamuud rai zao kwa sababu wao walikuwa ni viongozi na vigogo. Al-Awfi kasema kwamba Ibn 'Abbaas رضي الله عنهما kasema "hawa ni watu waliomuuwa ngamia" (At-Twabariy 19:477) Wamepanga njama kuwa Nabii Swaalih عليه السلام atakapolala usiku na aila yake waende kumuua kisha wawaambie jamaa zake Swaalih عليه السلام kuwa wao hawajui lolote kuhusu kuuliwa kwake na yaliyotokea usiku huo na kwamba wao wanasema kweli kwa sababu hakuna wala mmoja wao aliyeona kitu. Kila mmoja wao kaapa na kuchukua ahadi kwamba usiku ule yeyote atakayeonana na Swaalih amuue. Lakini Allaah سبحانه وتعالى Alimuokoa Nabii Swaalih عليه السلام na aila yake pamoja na walioamini kutokana na njama za ukatili wa jamaa hao kwa kuwaondosha kwenda sehemu nyingine usiku ule.
(قَالوا تَقَاسَموا بِاللَّهِ لَنبَيِّتَنَّه وَأَهْلَه ثمَّ لَنَقولَنَّ لِوَلِيِّهِ مَا شَهِدْنَا مَهْلِكَ أَهْلِهِ وَإِنَّا لَصَادِقونَ )
{{Wakasema: Apishaneni kwa Mwenyezi Mungu tutamshambulia usiku yeye na ahali zake; kisha tutamwambia mrithi wake: Sisi hatukuona maangamizo ya watu wake, na sisi bila ya shaka tunasema kweli}} An-Naml : 49 Lakini Allaah سبحانه وتعالى akapanga mipango yake adhimu na kuifanya mipango yao iwarudie wenyewe. Mujaahid kasema: "Wameapa kiapo na kuchukua ahadi ya kumuua lakini kabla ya hawajamfikia, wao na watu wao wakaangamizwa".
KUANGAMIA KWA WATU WA THAMUUD
Nabii Swaalih عليه السلام
alikuwa ana sehemu ya kufanya ibada yake katika bonde lenye mawe. Wakasema "akija kuswali tutamuua kisha tutarudi, na tukimmaliza tutakwenda kwa aila yake na kuwamaliza nao pia, "Allaah سبحانه وتعالى akawateremshia jiwe kubwa kutoka mlimani, wakaogopa kuwa jiwe lile litawasaga, wakakimbia katika pango na lile jiwe likaziba upenyo wa pango lile na hali wakiwa ndani. Watu wao hawakujua wenzao wamekwenda wapi wala hawakujua yaliyowafika! Kwa hiyo Allaah سبحانه وتعالى Kawaadhibu baadhi yao hivyo na wengineo kawaadhibu kwa adhabu ya aina nyingine kama tutakavyoona katika maelezo yajayo. Allaah سبحانه وتعالى Akamuokoa Mtume wake Swaalih عليه السلام na wale walioamini, ndipo Aliposema katika aya hii:
(وَمَكَروا مَكْرًا وَمَكَرْنَا مَكْرًا وَهمْ لَا يَشْعرونَ)
{{Basi wakapanga mipango yao, na Sisi tukapanga mipango yetu, na wao hawatambui}} An-Naml:50
(فَلَمَّا جَاء أَمْرنَا نَجَّيْنَا صَالِحًا وَالَّذِينَ آمَنواْ مَعَه بِرَحْمَةٍ مِّنَّا وَمِنْ خِزْيِ يَوْمِئِذٍ إِنَّ رَبَّكَ هوَ الْقَوِيّ الْعَزِيز )
{{Basi ilipo kuja amri yetu tulimwokoa Swaalih na wale walio amini pamoja naye kwa rehema yetu kutokana na hizaya ya siku ile. Hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kushinda}}Huud:66
Baada ya siku tatu ikaanza adhabu sasa kuwadhihirikia kama walivyoonywa na Nabii Swaalih عليه السلامnayo ilianza siku ya Alkhamisi, nyuso zao zikaanza kubadilika rangi kuwa manjano. Kisha siku ya Ijumaa zikawa nyekundu. Kisha siku ya Jumamosi nyuso zao zikageuka kuwa nyeusi kabisa. Baada ya kuchomoza jua siku ya Jumapili wakakaa kusubiri na kutaka kujua adhabu gani hiyo aliyosema Swalih
عليه السلام.
Mara kukanza mvua ya umeme iliyokuja kwa nguvu kisha ikafuatia mtetemeko wa ardhi mkali ambao uliharibu mji mzima na kuwaangamiza watu wake. Mji ulitingishwa na viumbe vyote vilivyokuwemo humo vilikufa.
(فَأَخَذَتْهم الرَّجْفَة فَأَصْبَحواْ فِي دَارِهِمْ جَاثِمِينَ)
{{Basi tetemeko la ardhi likawanyakua, na kulipo kucha wakawa majumbani mwao kifudifudi wamekwisha kufa}} Al-A'araaf: 78 Athari za Adhabu za Allaah
سبحانه وتعالى
zipo bado duniani sehemu mbali mbali kwa mfano 'bahari iliyokufa' (the dead sea) katika kisa cha Luut عليه السلام ndio maana Allaahسبحانه وتعالى anasema katika Qur'aan katika aya mbali mbali:
(قلْ سِيرواْ فِي الأَرْضِ ثمَّ انظرواْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَة الْمكَذِّبِين)
{{Sema: Tembeeni ulimwenguni, kisha mtazame ulikuwaje mwisho wa wanao kanusha}} Al-An'aam:11
Hivyo kuhusu athari za Wathamudu, Allaahسبحانه وتعالى Anasema:
(فَانظرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَة مَكْرِهِمْ أَنَّا دَمَّرْنَاهمْ وَقَوْمَهمْ أَجْمَعِين)
{{Basi angalia ulivyo kuwa mwisho wa mipango yao, ya kwamba tuliwaangamiza wao pamoja na watu wao wote}} An-Naml: 51
(فَتِلْكَ بيوتهمْ خَاوِيَةً بِمَا ظَلَموا إِنَّ فِي ذَلِكَ لَآيَةً لِّقَوْمٍ يَعْلَمون)
{{Basi hizo nyumba zao ni tupu kwa sababu ya walivyo dhulumu. Hakika bila ya shaka katika hayo ipo Ishara kwa watu wanao jua}}An-Naml: 52
Na alama hizo za adhabu ya watu Wathamudu zipo kama tutakavyoelezea mwisho wa kisa hiki alipopita Mtume صلى الله عليه وآله وسلم katika mji wa Wathamudu. Vile vile Allaah سبحانه وتعالى Kataja adhabu yao nyingine ya ukelele mkali ambao kabla ya kumalizika kwake ukelele huo, makafiri wote wa Thamuud walikufa pamoja wote kwa wakati mmoja. Hakuna chochote kilichoweza kuwahifadhi, wala majumba yao ya fahari ya mawe hayakuweza kuwalinda na adhabu hizo.
(وَأَخَذَ الَّذِينَ ظَلَمواْ الصَّيْحَة فَأَصْبَحواْ فِي دِيَارِهِمْ جَاثِمِينَ )
{{Na ukelele uliwaangamiza wale walio dhulumu, wakapambazukiwa nao ni maiti majumbani mwao}} Huud: 67
(كَأَن لَّمْ يَغْنَوْاْ فِيهَا أَلاَ إِنَّ ثَمودَ كَفرواْ رَبَّهمْ أَلاَ بعْدًا لِّثَمودَ )
{{Kama kwamba hawakuwako huko. Hebu zingatieni! Hakika kina Thamud walimkufuru Mola wao Mlezi. Hebu zingatieni! Thamud wamepotelea mbali}} Huud: 68 Maelezo zaidi kuhusu adhabu hiyo:
(فَكَيْفَ كَانَ عَذَابِي وَنذر)
( إِنَّا أَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ صَيْحَةً وَاحِدَةً فَكَانوا كَهَشِيمِ الْمحْتَظِرِ )
30. {{Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu}} 31. {{Hakika Sisi tuliwapelekea ukelele mmoja tu, wakawa kama mabuwa ya kujengea uwa}} Al-Qamar: 30-31
As-Sudi kasema walikuwa kama nyasi kavu za kichaka katika jangwa zinapoungua na kupeperushwa na upepo. Ibn Zayd kasema "Waarabu walikuwa wakisimamisha 'Hizar' (kutokana na neno 'almuhtazir') ambayo ni kichaka kikavu, (walichowazungushia) wakiwawekea ngamia na ngo'mbe. Ndipo Allaah
سبحانه وتعالى
Aliposema: ( فَكَانوا كَهَشِيمِ الْمحْتَظِر)
{{wakawa kama mabuwa ya kujengea uwa}} Al-Qamar: 31
MTUME ALIPOPITA MJI WA THAMUUD
Ibn 'Umar amesimulia kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم
alipokuwa akipita nyumba za watu wa Thamuud wakati akielekea na jeshi lake la Maswahaba kwenda katika vita vya Taabuuk alisimama hapo na Maswahaba wakachota maji katika visima ambavyo watu wa Thamuud walikuwa wakichota maji ya kunywa. Wakatumia maji kukandia unga wao wa kupikia mikate, na wakajaza maji ya kunywa katika mifuko yao ya ngozi (viriba), lakini Mtume صلى الله عليه وآله وسلم aliwaamrisha wayamwage maji na unga waliokanda walishe ngamia wao. Kisha akaondoka nao mpaka wakafika katika kisima ambacho ngamia wa Thamuud alikuwa akinywa maji, akawaonya wasiingie kwa watu walioangamizwa kwa kuwaambia: "Nakhofu msije kupatwa yale yaliyowapata wao, kwa hiyo msiingie kwao"
Riwaya nyingine imesema hivi:
عن عبد الله بن عمر قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم وهو بالحجر: ((لا تدخلوا على هؤلاء المعذبين، إلا أن تكونوا باكين، فإن لم تكونوا باكين فلا تدخلوا عليهم، أن يصيبكم مثل ما أصابهم)).
أخرجاه في (الصحيحين) من غير وجه.
((Imetoka kwa Abdullah Bin 'Amr ambaye alisema: Kasema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alipokuwa Hijr "Msiingie kwao hawa walioadhibiwa, isipokuwa muingie na huku mnalia, na kama hamlii basi msiingie kwao msije kufikwa na masaibu kama yaliyowafikia wao)) Al-Bukhari Na Muslim Wa Allaahu A'alam
MWISHO