TOFAUTI KUU ZA SHERIA 2
BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM
TOFAUTI KUU ZA SHERIA (2
Hapana shaka kuwa binaadamu mmoja anatofautiana na mwengine, ni sababu hii imesababisha kuwepo mipaka ya nchi, tofauti ya lugha, kutofautiana kwa makabila na rangi. Ndivyo sheria za mwanaadamu zinavyotafautiana baina ya sheria moja na nyengine. Pia sheria hizi za leo ni tofauti na zile za miaka hamsini tu iliyopita.
Sheria za Kiislamu zinajulikana na zitaendelea kuwa hazina mpaka (boundary) wowote wa tofauti ya wakati, taifa au sehemu anayoishi. Tuelewe kuwa mwananchi yeyote aliyekuwa chini ya Taifa la Kiislamu awe mweupe au mweusi, wa nchi yoyote, basi sheria ya mwizi (pindi ushahidi wa kweli ukithibitishwa) ni kukatwa kiganja cha mkono wa kulia, mlevi bakora 80 na mengineyo. Tofauti na sheria za binaadamu ambapo akibadili taifa na sheria zake zitabadilika.
Kwa mfano, twaelewa sote namna ya gonjwa hatari la ukimwi linavyoangamiza dunia nzima. Lakini Tanzania ipo kimya kuhusu muathirika anayetambuwa kuwa ameathirika kujamiiana na asokuwa muathirika kwa lengo la kumuambukiza gonjwa la ukimwi kwa makusudi. Hali sio hiyo kwa Afrika ya Kusini kwani sheria zao zinaruhusu muathirika wa namna hiyo kufikishwa Mahakamani. Kwa upande wa silaha za nyuklia, Marekani na Israel zimejipa ruhusa ya kutengeneza na kuhifadhi silaha hizo ilhali nchi nyengine zote yawa ni haramu kwao sio tu kutengeneza, hata kuhifadhi mali asili zinazotumika kutengenezea nyuklia kama zebaki “mercury”. Pia vitendo vya liwaati vimezuiwa Zanzibar (kifungu namba 150 cha Sheria ya Jinai namba 6 ya mwaka 2004). Wakati sheria za Magharibi sio tu zinaruhusu maingiliano haya machafu, hata ndoa zafungwa baina ya watu wa jinsia moja.
Hivyo, ni kusema Tanzania inaruhusu kuambukizana ukimwi wakati Afrika Kusini inazuia. Israel na Marekani wanaruhusa ya kutengeneza nyuklia ilhali nchi nyengine ni kosa. Liwaati ni kosa ndani ya Zanzibar wakati nchi za Magharibi zinaruhusu.
Tofauti na Uislamu, Sheria ipo wazi kuhusu muathirika kumuambukiza mwengine kwa lengo la kupata maradhi ateseke na mwisho kufariki kifo kibaya. Uislamu unasema anayeua nafsi moja ni sawa na kuua nafsi zote. Pia ipo Hadithi ya Mtume (SwallaAllahu Alayhi Wasalam) inayosema “Aliye na maradhi asimuambukize asiyekuwa nayo.” Kwa upande wa nyuklia, ni sawa tunasema mtu ajihami na kumruhusu kukaa nazo lakini nyuklia zina hatma mbaya. Sadd adh-dharai ni sheria inayozuia halali ambayo inaweza kuleta athari ya haramu. Sheria inayofafanua mwenendo wa maisha ya Muislamu (Majallah al-ahkaam adaliyah) Kifungu 30 pia chaeleza Sadd al-dharai. Haramu hii ni mfano wa ile tuipatayo juu ya ulevi, kwani ina manufaa lakini ni finyu ukilinganisha na athari zake. Allah (Subhanahu Wataala) anasema na tutajaribu kutafsiri kama ifuatavyo:
{Wanakuuliza juu ya ulevi na kamari. Sema: “Katika hivyo mna madhara makuu na (baadhi ya) manufaa kwa (baadhi ya) watu. Lakini madhara yake ni makubwa zaidi kuliko manufaa yake.”} [Suratul Al-Baqarah: 2)
Hivyo nyuklia inafanana na kesi ya ulevi na hivyo kuwa ni haramu. Ama kuhusu liwati, hamna mjadala kuwa ni haraam na itafika Qiyama, liwaat itabaki kuwa ni haraam. Liwaat ni katika dhambi kubwa ndani ya Uislamu na katu haikubaliki kwa jamii. Sheria zote hizi hazitakuwa na mabadiliko ndani ya Uislamu kwa sababu Mungu ni Mmoja na Sheria Zake ni hizo hizo. Allah Anasema na tutajaribu kutafsiri kama ifuatavyo:
{“Je mnawaendea wanaume, na mnawakatia njia (watu kwa kuwaua na kuwanyan’ganya njiani) na mnafanya maovu katika mikusanyiko yenu?” Basi halikuwa jawabu ya watu wake ila kusema: “Tuletee adhabu ya Mwenyezi Mungu ikiwa miongoni mwa wasemao kweli!”} [Suratul Al-Ankabuut: 29]
Je, hamna mtu asiyejua nini kiliwafika watu wa Nabii Luut (Alayhi Salaatu Wasalaam)?.
Sheria kuu za Kiislamu ambazo zinapatikana ndani ya Qur-aan imechukua sifa Yake Muumba, imehifadhiwa tokea mwanzo wa kushushwa hadi leo na mpaka siku ya Qiyama. Allah (Subhanahu Wataala) Anasema na tutajaribu kutafsiri kama ifuatavyo:
{Hakika Sisi ndio Tulioiteremsha mawaidha haya (hii Qur-aan), na hakika Sisi ndio Tutakayoilinda} [Suratu Al-Hijr: 9]
Hapana shaka kuwa Qur-aan tuliyonayo leo ni kitabu hichi hichi alichoshushiwa Nabii wetu (Swalla Allahu Alayhi Wasalam) kwa Ummah wake wote. Sheria hizi zilizowekwa kutoka Kwake Allah (Subhanahu Wataala) zinadhihirisha sifa Zake Mola ambazo hazina doa, Mwenye kuishi daima, Hakimu wa Mahakimu, Mfalme wa Wafalme na sifa zengine nzuri nzuri. Sifa hizi Allah (Subhanahu Wataala) anazo kabla, leo na mpaka Qiyama. Ni sifa hizi tuzipatazo kwa Qur-aan isobadilika na kwa sheria za Kiislamu zisotaka mabadiliko yoyote!
Kwa hiyo sheria za binaadamu ni kanuni zinazotungwa kwa ajili ya kuitengeneza vizuri jamii ili kutimiza matakwa ya hiyo jamii husika. Sheria za binaadamu zinatungwa kutokana na matatizo yanayojitokeza ndani ya jamii. Mahitaji ya jamii yenye kubadilika kutokana na yeye binaadamu kuwa na mabadiliko ndio sababu ya sheria za binaadamu. Jamii inaendelea, ndivyo sheria zinavyobadilika. Hivyo, sheria za binaadamu haziishi maisha ya milele, bali zinazaliwa na kufa. Kutokana na sababu ya wakati, sheria za mwanaadamu zinakwisha muda (expire). Hapa tunaona kuwa sheria za mwanaadamu zinatengenezwa kutokana na mahitaji ya jamii na kwa ajili ya muda fulani na baada ya muda huo kupita na jamii kubadilika kutokana na sheria hizo basi sheria hizo huwa sawa na takataka zitakiwazo kutupwa jalalani.
Kwa mfano sheria ya makosa ya Jinai ya Zanzibar namba 13 ya mwaka 1934 inaruhusu adhabu ya viboko. Adhabu hii imefutwa mwaka 2004 (Kifungu namba 26 ya sheria namba 6 ya mwaka 2004 – Sheria ya Makosa ya Jinai ya Zanzibar) Hivyo ni kusema sheria hii imezaliwa 1934, imeishi na kufa mwaka 2004. Adhabu zinazokubaliwa kwa sasa ni kama faini, kifungo cha jela na nyenginezo.
Tofauti na Uislamu, kwa mfano sheria ya mzinifu asoowa/kuolewa atatumikia mijeledi mia moja. Haitobadilika sheria hii mpaka Qiyama kisimame hata ikiwa Waislamu poa hawaitaki hata kuisikia. Ile dhana za zinaa kamwe hazijabadilika ila huongezeka. Uislamu umeliona hilo ndiyo maana sheria hiyo inadumu. Mwanadamu ana kasoro zake na huona yale madhara ndiyo faida. Mwanaadamu anaivamia zinaa akidhani ina manufaa ila haina hiyo zinaa ila madhara matupu tena ya kuangamiza. Matokeo ya kukataa kufuata Sheria za Kiislamu ni kujiangamiza. Sheria za Kiislamu zinamzuia mwanaadamu asijiangamize. Ni dhambi kubwa mtu kujiingiza katika hilaki yeye mwenyewe kwa mwenyewe.
MWISHO