TOFAUTI KUU ZA SHERIA 3
BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM
TOFAUTI KUU ZA SHERIA 3
SHERIA ZA KIISLAMU ZINAENDA NA WAKATI
Dalili zinaonesha kuwa sheria za Kiislamu ni za milele na hazihitaji marekebisho na wala marekebisho hayahitajiki kwa sheria za kiislamu. Sheria za Kiislamu zimewekwa kurekebisha tabia na matatizo ya jamii ya binaadamu kwa muda wote ambao atajaaliwa kuishi ndani ya dunia hii. Ingawa Sheria za Kiislamu msingi wake ni Qur-aan na isiyohitaji mabadiliko, lakini sheria hizi za Kiislamu zinaweza kuendelezwa na kupatiwa ufumbuzi wa mambo ambayo yana khitilafu ndogo ndogo. Hii ni kwa kutumia vipengele vya Fiqhi kama Qiyaas (ufumbuzi), kauli za Maswahabah, Sadd al-dharai (kuharamisha halali inayopelekea kwenye haramu) na nyenginezo.
Kwa mfano asili ya kuharamishwa ulevi ni kuwa na athari mbaya kwa jamii, lakini Qur-aan imezungumzia kinywaji cha ulevi na sio kuhusu madawa ya kulevya kama kokeni na bangi. Hapa tunatumia Qiyaas ili kupata hukmu yake na kuona kuwa nayo pia yana athari mbaya kwa jamii, hivyo kila chenye madhara ni haramu. Na kupata hukmu ya madawa ya kulevya kuwa ni haramu pia.
Itambulike kuwa vipengele hivi (mfano Qiyaas, Sadd al-dharai, kauli za Maswahabah na kadhalika) vyote vya Fiqhi vinapitia msingi wa sheria ya Qur-aan ama Sunnah. Ikiwa Qur-aan au Sunnah imetoa hukmu, hamna sheria nyengine itakayotolewa ufafanuzi. Na wala isiwe sheria itokanayo na fiqhi haramu inayohalalisha au halali inayoharamishwa. Kwa mfano kuhalalisha kutovaa Hijabu kwa mwanamke au kuharamisha Zakaah.
Mfano mzuri ni kuhusu mjadala wa Hijaab. Kwani Hijaab ina nafasi kubwa katika hukmu za Kiislamu. Lakini Dkt. Zaki Badawi (mwanazuoni wa Kiislamu kutoka Uingereza) ameruhusu wanawake kutovaa hijaabu kwa kuwa hijabu inamfanya adhuriwe kama vile kutukanwa, kusumbuliwa na hata kuvamiwa. Dr. Badawi ameghafilika na kusahau Quran (Suratu An-Nur:31 na Suratul Ahzab:59) kuwa hijabu ni lazima na wala sio Sunnah. Kisingizio cha kukejeliwa wanaovaa hijab sio sahihi kwani Waislamu waliopita walikashifiwa zaidi ya haya lakini sheria zilibaki kama zilivyo.
Hivyo, sheria za Kiislamu ni zenye kwenda na wakati, kwani sheria kuu za Kiislamu zipo kamili na mawazo ya kisheria (Fiqhi) yapo wazi kutumika.
Sheria za Kiislamu zinatofautiana baina ya mwanazuoni mmoja na mwengine tu. Tunaposema Qur-aan na Sunnah ni vyanzo vya sheria, tunakusudia kusema kuwa hivi ndivyo vyanzo na dalili kuu zinazofuatwa na kupatiwa ufumbuzi ikizingatiwa kufuata kanuni zinazohusika katika kutoa ufumbuzi kwa suala la Kiislamu.
Kanuni hizi za Kiislamu hazipatikani isipokuwa kwenye vyanzo vikuu. Hii ndio tofauti kubwa na sheria zenginezo. Kwani sheria za mwanaadamu zinatokana na akili yake mwenyewe, akija mmoja ataweka sheria hii na akiingia mwengine madarakani atazibadilisha. Anavyoamka ndivyo anavyotunga sheria. Sheria za Kiislamu zimeshushwa zaidi ya miaka 1400 iliyopita. Tokea muda huo, binaadamu anajulikana kubadilika kiakili, muundo na maendeleo. Watu wa kale hawakuweza hata kuota uvumbuzi usioingia akilini kutoka katika sheria za Kiislamu. Adabu za binaadamu zimeelezwa humo na matawi mengi tu ya elimu yametokana na hiyo Sheria kuu ya dunia.
Ama kwa binaadamu, huweka sheria kwa ajili ya kutawala muda mchache unaomzunguka akiangalia matakwa yake na jamii kuwa ujumla. Juu ya kubadilishwa na kutiwa viraka sheria hii, haijawa mfano hata chembe, mbele ya sheria za Kiislamu ilhali sheria hizi zinatungwa mpya. Lakini ile kongwe (Sheria ya Kiislamu) ipo imara na katu haihitaji viraka na wala haitohitaji viraka. Ukiangalia na kuisoma Sheria ya Kiislamu utakutia bado binaadamu hajafikia mambo yote yaliyotajwa, hivyo kuifanya kwenda na wakati. Kwa mfano ujio wa Nabii Issa (Alayhis Salaatu wa Salaam) kabla ya Qiyama, ni nani ajuaye lini atafika duniani? Ni Qurani tu iliyoeleza haya! Bado wakati wake tu kufika. Ni hivi karibuni tu imegundulika kuwa ni dunia inayozunguka jua na sio jua kulizunguka dunia. Qur-aan imetaja hili miaka 1400 iliyopita. Mfano mwengine ni kugundulika upulizwaji wa roho kwa kiumbe kilicho ndani ya tumbo la mama kabla ya kuzaliwa, wanasayansi wasiokuwa na ujuzi wa Qur-aan bado wanashikilia kusema kuwa kiumbe kinakuwa hai tokea pale yanapotoka manii. Hii sivyo kwa elimu sahihi ya Uislamu kwani tunafundishwa kuwa linakuwa ni pande la nyama tu (sio kiumbe hai), na hupuliziwa roho baada ya miezi minne tokea mimba inapotungwa.
Imepokewa kutoka kwa Bukhari na Muslim, kutoka kwa Abdillahi bin Masuud (Radhiya Allahu Anhu), kutokana na Mtume (Swalla Allahu Alayhi Wasalam) amesema: ((Hakika mmoja wenu linakusanywa umbile lake ndani ya tumbo la mama yake kwa siku arobaini kuwa ni tone (nutfaa), kisha linageuzwa kuwa pande la nyama (‘alaqatah) mfano wa hizo (siku), kisha linakuwa mifupa mfano wa hizo (siku), kisha anateremshwa juu yake malaika, anampulizia ndani yake roho…)) [Amesema kweli Mtume (Swalla Allahu Alayhi Wasalam)]
Sheria za Kiislamu sio zenye kubadilika ukilinganisha na za binaadamu ambazo zinabadilishwa kuanzia sheria ndogo mpaka Katiba. Kwa mfano ili kuingiza siasa za sasa (demokrasia) inabidi Katiba ibadilishwe kuruhusu vyama vingi. Historia ya Uislamu umeruhusu changamoto inayoanza kutoka Kwake Allah (Subhanahu Wataala) dhidi ya Ibilisi. Kisha kumuachia ibilisi akawa na sifa ya kuishi, kutembea ndani ya mishipa ya damu ya mwanaadamu. Akimuachia mwanaadamu aamue mwenyewe pa kufuata (ama Allah (Subhanahu Wataala) au Ibilisi). Siasa ya Uislamu iliendelea hata kwa Maswahaba baada ya kufa Nabii Muhammad (Swalla Allahu Alayhi Wasalam).
Historia ya Kiislamu inaonesha kuwa baada ya kufa Mtume (Swalla Allahu Alayhi Wasalam) Waislamu walichagua Khalifa (kiongozi) wa mwanzo msikitini, walitumia haki yao kwa kwenda kumpa mkono (kura) Sayyidna Abubakar (Radhiya Allahu Anhu) na kuonesha kuridhika naye kuwa ni Khalifa wao. Hakuingia madarakani Sayyidna Abubakar (Radhiya Allahu Anhu) kwa nguvu au kujipigia kampeni na propaganda. Hataaa! Njia ya Baya’h (kupiga kura) ilitumika.
MWISHO