Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

BIBI ZAINAB (A.S)

0 Voti 00.0 / 5

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

BIBI ZAINAB (A.S)

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelipongeza taifa la Iran kwa mnasaba wa kuadhimisha siku ya kuzaliwa Bibi Zainab bint Ali (sa) ambayo inaadhimishwa hapa nchini kama Siku ya Wauguzi. Huku akiashiria taathira za harakati ya kihistoria ya mtukufu huyo katika Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na mchango wa imani na masuala ya kiroho katika uwezo na adhama ya mapinduzi hayo, amesema: "Jambo lililolifanya taifa la Iran liwe kigezo na kutoa ilhamu katika dunia ya Kiislamu kwenye kipindi cha miaka 30 iliyopita ni kufuata shakhsia adhimu wa kidini akiwemo Bibi Zainab (as). Ameongeza kwamba uwezo wa taifa la Iran unatokana na kuathirika na masuala hayo ya kimaanawi.

Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa uwezo wa taifa la Iran hautokani na zana za kijeshi na kuongeza kuwa japokuwa taifa hili limepiga hatua kubwa za maendeleo katika nyanja za zana za kujilinda, lakini sababu kuu ya uwezo na adhama ya nchi na taifa la Kiislamu ni imani yake.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, ni kwa sababu hiyo ndiyo maana taifa la Iran likapiga hatua kubwa za ustawi na maendeleo na kusonga mbele kwa kasi kubwa zaidi licha ya miaka 30 ya vikwazo, vitisho, mashambulizi ya kijeshi na usaliti wa kisiasa na kiusalama.

Ayatullah Khamenei ameongeza kwamba tishio lisilokuwa la moja kwa moja la kuishambulia Iran kwa silaha za atomiki halitakuwa na taathira yoyote kwa taifa la Iran, lakini tishio hilo ni fedheha kubwa katika historia ya kisiasa ya Marekani na doa jeusi katika utendaji wa serikali ya sasa ya nchi hiyo.

Amesisitiza kuwa vitisho hivyo vimedhihirisha kikamilifu sura ya nyuma ya pazia ya mchezo wa kuigiza wa eti kutaka suluhu na amani, madai ya Marekani ya kuheshimu makubaliano yanayohusiana na silaha za nyuklia na kiini macho cha kunyoosha mkono eti wa urafiki kwa taifa la Iran.

Ameongeza kuwa vitisho vya Marekani vya kuishambulia Iran kwa silaha za nyuklia kwa hakika ni kubadili tabia za kimbweha za serikali ya Marekani na kuwa na tabia za mbwa mwitu.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa nchi zinazomiliki silaha za nyuklia hususan Marekani, zinataka kutumia uwezo huo kuidhibiti dunia na kuongeza kuwa nchi hizo haziheshimu makubaliano ya kimataifa kuhusu silaha za nyuklia wala hazitekelezi makubaliano hayo. Amesema nchi hizo zinasema orongo waziwazi na wakati nchi nyingine zinapotaka kutumia teknolojia ya nyuklia kwa matumizi ya kiraia, zinatuhumiwa kwamba haziheshimu makubaliano ya kimataifa; hii ni kwa sababu nchi hizo zinazomiliki silaha za nyuklia hazitaki kuwa na mshindani.

Amesisitiza tena juu ya siasa za nyuklia za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na akasema: "Iran imetangaza mara kwa mara kwamba haina nia ya kutumia silaha za mauaji ya halaiki lakini wakati huo huo taifa hili halitasalimu amri mbele ya vitisho kama hivyo na litawapigisha magoti wanaotoa vitisho hivyo.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amezitaka jumuiya za kimataifa kutopuuza vitisho vya Rais wa Marekani vya kulishambulia taifa la Iran kwa silaha za atomiki na akahoji kwamba "ni kwa kutumia haki gani Rais wa Marekani akatoa vitisho vya kulishambulia taifa la Iran kwa silaha za nyuklia? Vitisho hivyo vinatishia pia amani na usalama wa kimataifa na wanadamu wote na mtu yeyote duniani hapaswi kuthubutu kutoa vitisho kama hivyo japokuwa kwa maneno tu."

Ayatullah Khamenei amesema kuwa taifa la Iran litasimama ngangari mbele ya vitisho kama hivyo na akaongeza kuwa taifa hilo halitaruhusu tena Wamarekani kurejesha udhibiti wao wa kijahannamu nchini Iran kwa kutumia vitisho na nyezo nyingine.

Amesisitiza kuwa taifa la Iran litapiga hatua za maendeleo na ustawi katika nyanja zote licha ya njama za maadui na kwamba imani na mwamko wa kila leo wa vijana na taifa la Iran vitashinda vitisho na njama kama zile za mwaka jana.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia shakhsia ya Bibi Zainab (as) na mchango wake mkubwa katika kubakisha hai tukio la Ashura na ujumbe wake wa kihistoria. Amesema sababu kuu ya ushindi wa damu dhidi ya upanga katika tukio la Ashura ni Bibi Zainab amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake ambaye alionesha kwa mchango wake mkubwa kwamba mwanamke anashiriki katika matukio muhimu ya kihistoria.

Amesema kuwa Bibi Zainab aliifanya hijabu na stara ya mwanamke kuwa fahari na jihadi kubwa. Ameongeza kuwa mfano wa wazi wa ukweli huo ni hotuba ambayo haitasahaulika ya mjukuu huyo wa Mtume katika soko la mji wa Kufa (Iraq) na katika mazingira magumu ya zama hizo. Amongeza kuwa mtukufu huyo alitoa uchambuzi wa kina na mkubwa wa hali ya mambo ya wakati huo ya jamii ya Kiislamu kwa ufasaha mkubwa na kubainisha changamoto zinazoyakabili mapinduzi yaliyofanywa na Mtume Muhammad (saw) na wasii wake Imam Ali bin Abi Twalib (as).

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amefafanua baadhi ya vipengee vya hotuba ya Bibi Zainab huko Kufa na akasema: "Mtukufu huyo alisema kuwa tatizo kubwa la jamii ya Kiislamu ya wakati huo lilikuwa wananchi kutokuwa na maarifa ya kutambua fitina za wale waliodai kuwa wanamapinduzi na kutoweza kupambanua baina ya haki na batili; suala ambalo matokeo yake yalikuwa kutundikwa kicha cha mjukuu wa Mtume (saw) juu ya mishale ya maadui.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa nafasi na mchango wa Bibi Zainab (sa) katika tukio la Ashura na baada yake ni kigezo cha wanadamu wote hususan wanawake Waislamu. Ameongeza kuwa mtukufu huyo alidhihirisha nafasi na adhama halisi ya mwanamke kwa kuchanganya hijabu, haya na staha ya mwanamke na izza ya mwanamke Muislamu na muumini.

Ameashiria pia mbinu zisizokuwa sahihi na opotofu wa dunia iliyojaa ufisadi na ufuska ya Magharibi katika kuarifisha shakhsia na hadhi ya mwanamke na akasisitiza kuwa, ulimwengu wa Magharibi unafanya jitihada za kuonesha kwamba adhama na utukufu wa mwanamke umo katika kutupilia mbali hijabu na stara na kudhihirisha urembo wake mbele ya wanaune na mafisiki; suala ambalo ni kudhalilisha na kumdunisha mwanamke.

Amesema kuwa harakati ya wanawake katika Mapinduzi ya Kiislamu ilikuwa harakati inayoshabihiana na ile ya Bibi Zainab na kwamba wanawake daima wamekuwa na mchango mkubwa katika Mapinduzi ya Kiislamu na kujitetea kutakatifu.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kazi nzito ya wauguzi katika kulinda uzima na afya za watu na akasema kuwa sambamba na kazi hiyo nzito, majukumu ya wauguzi ikiwa ni pamoja na suala la kulinda maadili ya uuguzi pia lina umuhimu mkubwa.

Amezungumzia pia mashaka ya kazi za wauguzi katika kutuliza machungu ya kimwili na kiroho ya wagonjwa wao na akasema, kwa kutilia maanani umuhimu wa kazi ya wauguzi, ni vyema kukatayarishwa hati ya maadili ya wauguzi na kutolewa elimu ya hati hiyo kwa wauguzi wote.

Kabla ya hotuba ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Waziri wa Afya, Tiba na Mafunzo ya Udaktati Dakta Mardhiye Vahid Dastjerdi alihutubia hadhara hiyo akizungumzia kazi nzito ya wauguzi katika medani ya afya na akasema: "Serikali ya Bunge zimechukua hatua nzuri za kuboresha hali ya kikazi ya wauguzi. Bibi Dastjerdi ameashiria duru zaidi ya 300 za mafunzo kwa wauguzi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita na akaongeza kwamba katika miaka ya hivi karibuni kumeanzishwa masomo ya elimu ya juu na kubuniwa viwango vya fani ya uuguzi.

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini