Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

KUPENDA DUNIA

0 Voti 00.0 / 5

 BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

KUPENDA DUNIA

Kila binadamu afahamu kuwa sababu kubwa ya udanganyifu wa mambo yote na kusahau Akhera ambayo ni nchi ya kudumu ni kupenda maisha ya dunia. Kwani mtu anapopenda maisha ya dunia na kusahau Akhera humtamanisha mtu huyo arefushe umri wake ili apate kuishi daima milele, na kumghafilisha mauti, na kumsahaulisha amsahau Mola wake na kumpunguzia mambo ya dini. Kama alivyomkataza Mwenyezi Mungu S.W.T. Mtume Wake S.A.W. ajiepushe na watu hao katika Suratin Najm aya ya 29,

فَأَعْرِضْ عَنْ مَنْ تَوَلَّى عَنْ ذِكْرِنَا وَلَمْ يُرِدْ إِلاَّ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا

Maana yake, “Basi jiepushe na wale waupao kisogo ukumbusho Wetu huu, (Qurani) na wala hawataki ila maisha (ya starehe) ya dunia.”

Pia alimkataza katika Surat Taha aya ya 131,

وَلاَ تَمُدَّنَّ عَيْنَيْكَ إِلَى مَا مَتَّعْنَا بِهِ أَزْوَاجًا  مِنْهُمْ زَهْرَةَ الْحَيَاةِ الدُّنيَا لِنَفْتِنَهُمْ فِيهِ وَرِزْقُ رَبِّكَ خَيْرٌ وَأَبْقَى

Maana yake, “Wala usivikodolee macho yako tulivyowastareheshea baadhi ya watu miongoni mwao (hao wabaya). Hivyo ni mapambo ya maisha ya dunia tu, ili tuwafanyie mtihani kwavyo.”

Na kuna Hadithi nyingi ambazo zinatukumbusha ubaya wa kupenda dunia na kusahau Akhera. Mtume S.A.W. kasema,

حب الدنيا رأس كل خطيئة

Maana yake, “Kupenda dunia ni sababu ya kila kosa.
Pia Mtume S.A.W. kasema,

‘‘ما من شئ أبْغَضُ إلى الله تعالى بعد الشرك بالله من حب الدنيا’’

Maana yake, “Hakuna kitu cha kuchukiza mbele ya Mwenyezi Mungu baada ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu kama kupenda dunia.”

Pia katika Hadithi iliyopokelewa na Abu Huraira R.A.A. na iliyotolewa na Muslim, Mtume S.A.W. kasema,

الدُّنْيَا سِجْنُ الْمُؤْمِنِ وَجَنَّةُ الْكَافِرِ

Maana yake, “Dunia ni jela ya Mwislamu na Pepo ya kafiri.”
Ibn Abbas R.A.A. kasema: “Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu amefanya dunia iwe na sehemu tatu: Sehemu moja ya Waislamu, na sehemu ya pili ya wanaafiki na sehemu ya tatu ya makafiri.” Mwislamu anajiandaa tayari, na munaafiki anajipamba na kafiri anajifurahisha kwa matamanio.”

Mambo sita ambayo humsababishia mja kuepukana na Moto na kuingia Peponi: Anaemjua Mola akamtii, na anaemjua Shetani akamuasi, na anaeijua haki akaifuata, na anaeijua batili akaiacha na kuiepuka, na anaeijua dunia akaikataa na anaeijua Akhera akaitaka.

HASARA ZA KUPENDA MAISHA YA DUNIA NA KUSAHAU AKHERA.

1) Hasara ilioje ya mtu kupenda maisha ya dunia na kusahau maisha ya Akhera kwa kuacha kumuamini Mola wake na kutenda mema ni kumuangamiza mja mwenyewe na kumsababishia kuadhibiwa adhabu kali bila huruma. Kwa kauli ya Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratil Baqarah aya ya 86,

أُوْلَئِكَ الَّذِينَ اشْتَرَوْا الْحَيَاةَ الدُّنْيَا بِالآخِرَةِ فَلا يُخَفَّفُ عَنْهُمْ الْعَذَابُ وَلا هُمْ يُنصَرُونَ

Maana yake, “Hao ndio waliokhiari (starehe za) uhai wa dunia badala ya (starehe za) Akhera; kwa hivyo hawatapunguziwa adhabu wala hawatanusuriwa.”

2) Mwenyezi Mungu S.W.T. ameyafananisha maisha ya dunia na mfano wa mchezo hayana thamani yoyote ile, kwa sababu maisha yake ni mafupi na binaadamu hakukusudiwa kuishi duniani milele na dunia ina mwisho wake. Kama alivyopiga mfano, kasema katika Suratil An`aam aya ya 32,

وَمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلاَّ لَعِبٌ وَلَهْوٌ وَلَلدَّارُ الآخِرَةُ خَيْرٌ لِلَّذِينَ يَتَّقُونَ أَفَلَلا تَعْقِلُونَ

Maana yake, “Na maisha ya dunia (hii) si kitu ila mchezo tu na upuuzi. Na bila shaka nyumba ya Akhera ni bora zaidi (bila kiasi kuliko hii dunia) kwa wale wamchao (Mwenyezi Mungu). Basi hamtii akilini (haya mnayoambiwa)?”

3) Mola S.W.T. katuhadharisha kuifanyia mchezo dini Yake, na wale ambao wanaoifanyia mchezo wakadanganyika na maisha ya dunia wakasahau ya Akhera basi watapata adhabu ya kinywaji cha moto na adhabu iumizayo. Kama alivyowaonya wale watu wa aina hiyo katika Suratil An`aam aya ya 70,

وَذَرِ الَّذِينَ اتَّخَذُوا دِينَهُمْ لَعِبًا وَلَهْوًا وَغَرَّتْهُمْ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا وَذَكِّرْ بِهِ أَنْ تُبْسَلَ نَفْسٌ بِمَا كَسَبَتْ لَيْسَ لَهَا مِنْ دُونِ اللَّهِ وَلِيٌّ وَلا شَفِيعٌ وَإِنْ تَعْدِلْ كُلَّ عَدْلٍ لا يُؤْخَذْ مِنْهَا أُوْلَئِكَ الَّذِينَ أُبْسِلُوا بِمَا كَسَبُوا لَهُمْ شَرَابٌ مِنْ حَمِيمٍ وَعَذَابٌ أَلِيمٌ بِمَا كَانُوا يَكْفُرُونَ

Maana yake, “Na waache wale walioifanya mchezo na upuuzi dini yao (hii aliyowaletea Mwenyezi Mungu), na yamewadanganya maisha ya dunia. Basi wakumbushe (kwa hiyo Qurani, watahadhari) isije (kila) nafsi (katika nafsi zao) ikaangamizwa kwa sababu ya yale iliyoyachuma. Haitakuwa na mlinzi (nafsi hiyo) wala mwombezi yo yote mbele ya Mwenyezi Mungu. Na hata ikitoa fidia ya kila namna haitapokelewa. Wao watapata kinywaji cha maji ya moto kabisa na adhabu iumizayo, kwa sababu ya kukanusha (kwao).”

4) Allah S.W.T. atayauliza makundi ya Binaadamu na Majini siku ya Kiyama zile sababu ambazo ziliwasababisha hata wakamuasi Mola wao na kwa nini hayakufuata amri Zake. Jee! Hawakujiwa na Mitume wa kuwaonya kabla kwamba watahukumiwa siku hiyo? Lakini Mwenyezi Mungu S.W.T. katoa sababu kubwa ya kuasi na kutokufuata amri za Mola wao walidanganyika na maisha ya dunia. Kama alivyotueleza katika Suratil An`aam aya ya 130,

يَا مَعْشَرَ الْجِنِّ وَالإنسِ أَلَمْ يَأْتِكُمْ رُسُلٌ مِنْكُمْ يَقُصُّونَ عَلَيْكُمْ آيَاتِي وَيُنذِرُونَكُمْ لِقَاءَ يَوْمِكُمْ هَذَا قَالُوا شَهِدْنَا عَلَى أَنفُسِنَا وَغَرَّتْهُمْ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا…

Maana yake, “(Siku ya Kiyama wataambiwa): “Enyi makundi ya Majini na wanadamu! Jee, hawakukufikieni Mitume miongoni mwenu kukubainishieni aya Zangu na kukuonyeni mkusanyo wa siku yenu hii ya leo?” Watasema: “Tumeshuhudia juu ya nafsi zetu (kuwa sisi wabaya).” Na yaliwadanganya maisha ya dunia…”

5) Mola katuhadharisha sana kuhusu mali na watoto kwa sababu Yeye ameweka mitihani Yake katika mambo haya. Kwa hali hiyo mambo haya wakati mwingine huweza kumtelezesha mtu yawe ndio adhabu yake hapa duniani badala ya kustarehe nayo, na ili pia yamshughulishe na asifanye ibada na baadaye afe hali ya kuwa ni kafiri.” Kama alivyotuhadharisha katika Surat Tawba aya ya 55,

فَلا تُعْجِبْكَ أَمْوَالُهُمْ وَلا أَوْلادُهُمْ إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّهُ لِيُعَذِّبَهُمْ بِهَا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَتَزْهَقَ أَنفُسُهُمْ وَهُمْ كَافِرُونَ

Maana yake, “Yasikufurahishe mali yao wala watoto wao. Anataka Mwenyezi Mungu awaadhibu kwa hayo katika maisha ya dunia, na zitoke roho zao, na hali ya kuwa ni makafiri.”

6) Nabii Musa aliomba dua kwa Mwenyezi Alllah S.W.T. ili iangamizwe mali ya Firauni na watu wake, kwa sababu Firauni alikuwa na mali nyingi kupita kiasi ndio ambayo ilimsababishia Firauni na watu wake kuringa na kuwapoteza wao wenyewe katika maisha ya dunia, na pia iliwasababishia kutomuamini Mola wao na kufa makafiri. Kama alivyotufahamisha Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat Yuunus aya ya 55,

أَلا إِنَّ لِلَّهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ أَلا إِنَّ وَعْدَ اللَّهِ حَقٌّ وَلَكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لا يَعْلَمُونَ

Maana yake, “Na Musa (akaomba dua kwa Mola wake) akasema: “Mola wetu! Wewe umempa Firauni na watu wake wakubwa mapambo na mali (nyingi) katika maisha ya dunia. Mola wetu! Hivyo wanapoteza watu katika njia yako. Mola wetu! Ziangamize mali zao na uzishambulie nyonyo zao, hawataamini mpaka waione adhabu inayoumiza.”

7) Kutaka maisha ya dunia tu peke yake humsababishia mja akose maisha ya Akhera. Kwa kauli ya Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat Huud aya ya 15,

مَنْ كَانَ يُرِيدُ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا وَزِينَتَهَا نُوَفِّ إِلَيْهِمْ أَعْمَالَهُمْ فِيهَا وَهُمْ فِيهَا لا يُبْخَسُونَ

Maana yake, “Wanaotaka maisha ya dunia na mapambo yake, tutawapa humu duniani (ujira wa) vitendo vyao kamili; humu wao hawatapunjwa (lakini Akhera hawatapata kitu).”

8) Mwenyezi Mungu S.W.T. katuhadharisha kwamba starehe za maisha ya dunia kulinganisha na starehe za maisha ya Akhera ni ndogo kabisa kwa sababu maisha yake ni mafupi na yana mwisho. Lakini maisha ya Akhera ni ya milele na starehe zake ni za kila aina na hazifananishwi na za duniani za taabu na mitihani na misiba. Kama alivyotuhadharisha katika Suratir Ra`ad aya ya 26,

وَمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا فِي الآخِرَةِ إِلاَّ مَتَاعٌ

Maana yake, “…Na uhai wa dunia kwa kulinganisha na wa Akhera si kitu ila starehe ndogo.”
Na kwa kuilinganisha starehe ya dunia na ya Akhera Mtume S.A.W. ametupigia mfano mzuri na mwepesi wa kufahamika. Kasema kuwa starehe ya dunia ni kama mfano wa mtu kachovya kidole chake kwenye bahari, na starehe ya Akhera ni kama bahari. Basi kitie kidole kwenye bahari kisha kitoe ukiangalie ikiwa kimechukua maji. Ukweli ni kwamba hakikuchukua maji ila labda tone moja katika bahari. Kwa hali hiyo starehe ya dunia ni ndogo kabisa kuilinganisha na ya Akhera kama ilivyoelezewa katika Hadithi iliyotolewa na Muslim, Mtume S.A.W. kasema,

وَاللَّهِ مَا الدُّنْيَا فِي الْآخِرَةِ إِلا مِثْلُ مَا يَجْعَلُ أَحَدُكُمْ إِصْبَعَهُ هَذِهِ (وَأَشَارَ بِالسَّبَّابَةِ) فِي الْيَمِّ فَلْيَنْظُرْ بِومَ تَرْجِعُ

Maana yake, “Naapa kwa Mwenyezi Mungu, (kwamba ukiilinganisha) dunia na Akhera (inakuwa) ni mfano wa mmoja wenu ameweka kidole chake hiki (na akaonesha kidole cha pili) katika bahari kisha aangalie nini kinachorudi.”

9) Mola S.W.T. katupigia mfano wa maisha ya dunia ni kama mfano wa mvua iliyonyesha duniani kisha ikastawisha mimea ya ardhini. Baadaye mimea ile ikawa majani makavu yanayopeperushwa na upepo. Kama alivyotuelezea katika Suratil Kahaf aya ya 45,

وَاضْرِبْ لَهُمْ مَثَلَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا كَمَاءٍ أَنزَلْنَاهُ مِنْ] السَّمَاءِ فَاخْتَلَطَ بِهِ نَبَاتُ الأَرْضِ فَأَصْبَحَ هَشِيمًا [تَذْرُوهُ الرِّيَاحُ وَكَانَ اللَّهُ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ مُقْتَدِرًا

Maana yake, “Na wapigie mfano wa maisha ya dunia ni kama maji tunayoyateremsha kutoka mawinguni; kisha huchanganyika nayo (maji hayo) mimea ya ardhi (ikastawi); kisha (baadaye) ikawa (mimea hiyo) majani makavu yaliyokatika katika ambayo upepo huyarusha huku na huko. Na Mwenyezi Mungu ana uwezo juu ya kila kitu.”

10) Allah S.W.T. katuambia kwamba siku moja Qaruun aliwatokea watu wake kwa mavazi mazuri sana ya ufakhari. Na wale watu waliokuwa na nyoyo dhaifu na kutaka maisha ya dunia walipomuona hivyo wakasema: “Laiti tungelikuwa tunayo kama aliyopewa Qaruun! Hakika yeye ni mwenye bahati kubwa.” Lakini Mwenyezi Mungu S.W.T. alipomdidimiza yeye na mali yake kwa sababu ya kujitakabari, wale ambao walitamani maisha ya dunia wakajuta na kusikitika, wakabadili maneno yao wakasema: “Tunamshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa katufanyia ihsani hakutujaalia kama Qaruun, bila shaka angetudidimiza pamoja naye.” Kama alivyosema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratil Qasas tokeya aya ya 79 hadi ya 82,

فَخَرَجَ عَلَى قَوْمِهِ فِي زِينَتِهِ قَالَ الَّذِينَ يُرِيدُونَ الْحَيَاةَ الدُّنيَا يَالَيْتَ لَنَا مِثْلَ مَا أُوتِيَ قَارُونُ إِنَّهُ لَذُو حَظٍّ عَظِيمٍ… لَوْلا أَنْ مَنَّ اللَّهُ عَلَيْنَا لَخَسَفَ بِنَا

Maana yake, “Basi akawatokea watu wake katika pambo lake. Wakasema wale wanaotaka maisha ya dunia “Laiti tungalipata kama aliyopewa Qaruun; hakika yeye ni mwenye bahati kubwa…Asingetufanyia hisani Mwenyezi Mungu bila shaka angetudidimiza (kama alivyomdidimiza kwani sisi tuliitamani hali yake)…”

11) Mwenyezi Mungu S.W.T. katuhadharisha tusidanganyike na maisha ya dunia kwa sababu maisha yake ni mafupi na pia tusikubali kudanganywa na adui yetu Iblisi kwani yeye anataka kuzidisha kundi lake la watu wa Motoni liwe kubwa. Kama alivyosema katika Surat Luqmaan aya ya 33,

…فَلا تَغُرَّنَّكُمْ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا وَلا يَغُرَّنَّكُمْ] [بِاللَّهِ الْغَرُورُ

Maana yake, “…Basi yasikudanganyeni maisha ya dunia (hii), wala asikudanganyeni yule mdanganyifu mkubwa, (Iblisi) katika (mambo ya) Mwenyezi Mungu.”

12) Mola S.W.T. kutuonya kwamba maisha ya dunia si chochote ila ni starehe ipitayo haraka bila ya mtu kuhisi. Na ukichunguza utaona maneno ya Mola Mtukufu ni ya kweli kabisa, kwani miaka yote uliyoishi duniani hujui imepitaje na kama ndio kwanzaa unaanza kuishi maisha mapya. Lakini mtu anapokufa na kuyaendea maisha ya Akhera, basi maisha yake ya huko ni ya kudumu. Kama alivyosema katika Suratil Muumin aya ya 39,

يَا قَوْمِ إِنَّمَا هَذِهِ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا مَتَاعٌ وَإِنَّ الآخِرَةَ هِيَ دَارُ الْقَرَارِ

Maana yake, “Enyi watu wangu! Kwa hakika maisha ya dunia hii ni starehe (ipitayo tu), na bila shaka Akhera ndiyo nyumba ya kukaa daima.”

13) Allah S.W.T. amerudia rudia kusema mara kwa mara kwa katuonya kuwa maisha haya ya dunia si chochote ila ni mchezo na upuuzi na kufakharishana baina ya maskini na matajiri, na kufakharishana baina yetu kwa mali na watoto. Lakini yule ambaye atachukulia kwamba ndio maisha ya raha na akasahau maisha ya Akhera basi Mola wake kawaahidi wale wabaya waliofuata dunia tu adhabu kali. Na kwa wale watu wema ambao waliikumbuka Akhera na kufanya amali nzuri atawasamehe na kuwalipa malipo mema. Kama alivyotuhadharisha Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratil Hadyd aya ya 20,

اعْلَمُوا أَنَّمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا لَعِبٌ وَلَهْوٌ وَزِينَةٌ] وَتَفَاخُرٌ بَيْنَكُمْ وَتَكَاثُرٌ فِي الأَمْوَالِ وَالأَوْلادِ كَمَثَلِ غَيْثٍ أَعْجَبَ الْكُفَّارَ نَبَاتُهُ ثُمَّ يَهِيجُ فَتَرَاهُ مُصْفَرًّا ثُمَّ يَكُونُ حُطَامًا وَفِي الآخِرَةِ عَذَابٌ شَدِيدٌ وَمَغْفِرَةٌ مِنْ اللَّهِ وَرِضْوَانٌ وَمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلاَّ مَتَاعُ الْغُرُورِ

Maana yake, “Jueni ya kwamba maisha ya dunia ni mchezo na upuuzi na pambo na kufaharishana baina yenu (kwa nasaba), na kufaharishana kwa mali na watoto. (Na hali ya kuwa vyote hivi hamdumu navyo. Mfano wake) ni kama mvua ambayo huwafurahisha (wakulima) mazao yake, kisha yanakauka ukayaona yamepiga umanjano (badala ya kupiga uchanikiwiti), kisha yanakuwa mabuwa (hayana chochote). Na Akhera kuna adhabu kali (kwa wabaya); na (pia) msamaha wa Mwenyezi Mungu na radhi (Yake kwa wema). Na hayakuwa maisha ya dunia ila ni starehe idanganyayo; (mara huondoka).”

14) Mwishoni Mtume S.A.W. aliwanasihi Masahaba zake na kuwaonya kwamba wasiichukulie dunia kwa pupa. Lakini wachukue yenye kheri na maslaha kwao na waache mabaya. Kwa sababu Mwenyezi Mungu S.W.T. kaidharau dunia na hakuithamini hata sawa na bawa la mbu. Kama ilivyokuja katika Hadithi iliyopokelewa na Sa`ad bin Sahil R.A.A. na kutolewa na Ttirmidhi, Mtume S.A.W. kasema,

"لَوْ كَانَتِ الدُّنْيَا تَعْدِلُ عِنْدَ اللَّهِ جَنَاحَ بَعُوضَةٍ مَا سَقَى كَافِرًا مِنْهَا شَرْبَةَ مَاءٍ"

Maana yake, “Ingelikuwa dunia mbele ya Mwenyezi Mungu ina usawa na bawa la mbu asingelimnywesha humo maji kafiri.”

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini