Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

KUZALIWA KWA NABII YAHYA (A.S)

0 Voti 00.0 / 5

BISMILLAAHI RAHMANI RAHIM

KUZALIWA KWA NABII YAHYA (A.S)

Kuzaliwa kwa Nabii Yahya ni kutokana na dua ya Baba yake Nabii Zakaria wakati alipomuona Sayyida Mariam akiruzukiwa na Mola wake vyakula na matunda wakati ambao ilikuwa si musimu wake. Nabii Zakaria akapata matumaini makubwa ya kumuomba Mola wake ili naye amruzuku mtoto ambaye atashika mahali pake baada ya kifo chake. Baada ya Nabii Zakaria kumuomba Mola wake kwa siri, Mwenyezi Mungu S.W.T. alimuahidi kwamba atazaa mtoto atakayemwita Yahya. Mwenyezi Mungu S.W.T. amemsifu sana Mtume Wake Yahya ndani ya Qur-ani Tukufu kwamba alikuwa Nabii mchaMungu sana na hata inasemekana siku moja watoto wenzake walimwendea wakamwambiya:

“Ewe Yahya! Twende tukacheze.” Akawajibu: “Mimi sikuumbwa kucheza.” Kwa ile khofu aliyokuwa nayo Yahya A.S., Nabii Zakaria alikuwa akitaka kuwatolea mawaidha Ma-Bani Israil, basi kwanza hugeuka kushoto na kulia kumwangalia Yahya, ikiwa yupo nao, basi alikuwa hazungumzii kuhusu “Moto na Pepo.” Kwani siku moja Nabii Zakaria alizungumzia kuhusu “Moto na Pepo” na Yahya A.S. alikuwa nao lakini kajificha mahali, mara tu aliposikia kuhusu khabari za Moto na adhabu zake Yahya A.S. alikimbia mbio kisha wakaanza kumtafuta mpaka wakampata. Yahya A.S. alimuomba mama yake amshonee nguo za sufi ili naye akashiriki katika ibada katika Msikiti wa Baitil Muqaddas, lakini mama yake alimwambia kwamba mpaka akubali baba yake, Nabii Zakaria alipoelezewa akamjibu Yahya A.S.

“Ewe mwanangu! Wewe bado ungali mtoto mdogo.” Yahya A.S. akamjibu Baba yake: “Jee, hukuona mdogo kuliko mimi na yamemjia mauti?” Yahya alijaaliwa na hekima naye angali mtoto. Kwa kauli ya Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat Maryam Aya ya 12 na ya 13,

[يَايَحْيَى خُذْ الْكِتَابَ بِقُوَّةٍ وَآتَيْنَاهُ الْحُكْمَ صَبِيًّا * وَحَنَانًا مِنْ لَدُنَّا وَزَكَاةً وَكَانَ تَقِيًّا)

Maana yake, “Ewe Yahya! Kishike Kitabu kwa nguvu! Nasi tulimpa hekima angali mtoto. Na tukampa huruma itokayo Kwetu, na utakaso, na akawa mchaMungu.” Mwenyezi Mungu S.W.T. pia alimjaalia usalama na amani iwe juu yake siku aliyozaliwa na siku aliyokufa na siku atakapofufuliwa hai, kama alivyomjaalia Nabii Issa A.S.. Kwa kauli ya Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat Maryam Aya ya 15,

 [وَسَلامٌ عَلَيْهِ يَوْمَ وُلِدَ وَيَوْمَ يَمُوتُ وَيَوْمَ يُبْعَثُ حَيًّا)

Maana yake, “Na amani iwe juu yake (Nabii Yahya) siku ya kuzaliwa, na siku ya kufa, na siku ya kufufuliwa hai.” Nabii Yahya hakuoa kabisa katika uhai wake. Na alikuja kusadikisha kuzaliwa kwa Nabii Issa A.S. kama ilivyothibitika katika Surat Aali-`Imraani Aya ya 39,

 […أَنَّ اللَّهَ يُبَشِّرُكَ بِيَحْيَى مُصَدِّقًا بِكَلِمَةٍ مِنْ اللَّهِ وَسَيِّدًا وَحَصُورًا وَنَبِيًّا مِنْ الصَّالِحِينَ)

Maana yake, “…Hakika Mwenyezi Mungu anakubashiria (kupata mtoto; umwite) Yahya, atakayekuwa mwenye kumsadikisha (Mtume atakayezaliwa) kwa neno litokalo kwa Mwenyezi Mungu (naye ni Nabii Issa). Na (Yahya) atakayekuwa bwana na mtawa na Nabii kwa watu wema.” KUFA KWA NABII YAHYA A.S.. Inasemekana wakati wa zama za Nabii Yahya alikuwapo mfalme akitawala aliyejulikana kwa jina la Hirodaut. Huyu mfalme alipatwa na tamaa ya kutaka kumuoa binti wa ndugu yake. Siku moja yule binti alitoka akenda mbele ya mfalme kucheza. Mfalme akavutiwa sana na uzuri wa mwanamke huyo. Mfalme akataka kumuoa lakini yeye alikataa kuolewa na alimuahidi mfalme “Ikiwa kweli unanitaka, basi kwanza kilete kichwa cha Nabii Yahya.” Kwani Nabii Yahya aliikataza ndoa ya namna hiyo kufuatana na sheria iliyokuwemo ndani ya Taurati. Kwa hivyo yule mfalme akawatuma askari wake wakakate kichwa cha Nabii Yahya kisha wakilete kwa mfalme. Walipokileta mbele ya yule mwanamke akakiona halafu akakubali kuolewa.

 
MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini