KUCHOMOZA KWA WAHYI
BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KUCHOMOZA KWA WAHYI
Utafiti katika suala la Wahyi ni moja kati ya mambo yaliyo muhimu, na kutokana na kwamba suala hili ndio msingi wa kuyaelewa maneno ya Mwenyeezi Mungu, basi tunaweza kusema kua utafiti juu ya suala hili ndio msingi wa mwanzo katika masuala ya Qur-ani, na katika utafiti huu mtu hua anajiuliza, Wahyi ni nini? Na vipi linatimia fungamano baina ya Mteremshaji Wahyi na Mpokeaji wa Wahyi huo, jawabu za masuali kama haya, hua yanampa mtu njia ya kuelewa ukweli wa Qur-ani.
WAHYI KATIKA MAANA ZA KILUGHA
Neno Wahyi katika lugha lina maana tofauti, miongoni mwa maana hizo ni:Kuonesha ishara (kuashiria), maandishi, ujumbe, mazungumzo ya kiundani yaliyofichwa maana yake, kufahamisha kitu kwa kificho, haraka na spidi (speed), na aina yeyote ile ya matamshi, iwe ni kwa njia ya kimaandishi,ujumbe, au kumfahamisha mtu kwa kutumia ishara bila ya kuelewa watu wengine, huitwa wahyiMtafiti mkuu wa kilugha (Raaghib Isfahaniy) anasema: (Wahyi ni ujumbe unaofikishwa kwa njia ya kificho ambao hutimia kwa kupitia ishara na kwa haraka))
Abu Ishaaq vilevile amesema: (asili ya neno wahyi katika lugha limekuja kwa maana ya (ujumbe ulio wa siri), ndio maana Ilhaam ikapewa jina la wahyi.
WAHYI KATIKA QUR-ANI
Neno Wahyi katika Qur-ani limekuja katika maana nne zifuatazo :
1. ISHARA KWA NJIA YA SIRI
Maana hii ni sawa na ile maana ya kilugha, kama vile ilivyokuja katika Qur-ani kuhusiana kisa cha Nabii Zakariya (a.s) pale alipofunga funga ya kutozungumza. Allah (s.w) katika (Suratul Maryam aya ya 11) anasema
فَخَرَجَ عَلـٰي قَوْمِهِ مِنَ الْمِحْرَابِ فَاَوْحَي إِلَيْهِمْ اَن سَبِّحُوا بُكْرَةً وَعَشِيّاً
Maana ya aya hiyo ni kama ifuatavyo:
(Basi (Zakariya) akawatokea watu wake kutoka kwenye mihrabu akawaashiria kua mtukuzeni Mwenyeezi Mungu asubuhi na jioni)
2. MUONGOZO WA KIMAUMBILE
yaani muongozo wa kitabia, muongozo ambao umewekwa katika vitu vyote vilivyomo ulimwenguni, na vitu vyote vilivyomo ulimwenguni visivyo na uhai pamoja na vyenye uhai, kama vile mimea wanyama pamoja na watu, vyote hivi kimaumbile, vinaelewa njia ya kufanya ili kuweza kubakia katika ulimwengu huu, na muongozo huu wa kitabia na kimaumbile, ndani ya Qur-ani umepewa jina la wahyi Allah (s.w) katika Suratul Nahl aya ya (68-69) anasema:
وَاَوْحَي رَبُّكَ إِلَي النَّحْلِ اَنِ اتَّخِذِى مِنَ الْجِبَالِ بُيُوتاً وَمِنَ الشَّجَرِ وَمِمَّا يَعْرِشُونَ
ثُمَّ كُلِى مِن كُلِّ الثَّمَرَاتِ فَاسْلُكِى سُبُلَ رَبِّكِ ذُلُلاً يَخْرُجُ مِن بُطُونِهَا شَرَابٌ مُّخْتَلِفٌ اَلْوَانُهُ فِيهِ شِفَاء لِلنَّاسِ إِنَّ فِى ذٰلِكَ لآيَةً لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ
Maana ya aya hizo ni kama ifuatavyoNa Mola wako akamfahamisha nyuki ya kwamba:- "jitengenezee majumba (yako) katika milima na katika miti na katika yale (majumba) wanayojenga (watu
Kisha "Kula katika kila matunda, na upite katika njia za Mola wako zilizofanywa nyepesi (kuzipita)" Kinatoka katika matumbo yao kinywaji (asali) chenye rangi mbali mbali; ndani yake kina ponyo (poza) kwa wanaadamu. Hakika katika hayo muna mazingatio kwa watu wenye fikra.
3 . UJUMBE WA NDANI YA MOYO
Baadhi ya wakati mwanaadamu hupokea ujumbe (kutoka kwa Mola wake) hali ya kuwa haelewi chanzo cha ujumbe huo, (katika hali ambayo mwanaadamu anakutwa na matatizo na hajui afanye nini ili kuyatatua matatizo hayo), ghafla mtu huyo hupata njia ya kulitatua tatizo hilo na hufurahika moyoni mwake, na huondokewa na kile kite cha roho alichokuwa nacho, hali hiyo basi ni ule ujumbe uliomo ndani ya nyoyo za wanaadamu, ambapo Allah (s.w) huwaongoza na kuwasaidia waja wake kwa njia kama hiyo, ujumbe kama huo katika Qur-ani umeitwa Wahyi, Allah (s.w) katika Qur-ani (Surat-Taha aya ya 37-40) akimuelezea Mama wa Nabii Mussa (a.s) anasema:
وَلَقَدْ مَنَنَّا عَلَيْكَ مَرَّةً اُخْرَي إِذْ اَوْحَيْنَا إِلَي اُمِّكَ مَا يُوحَي اَنِ اقْذِفِيهِ فِى التَّابُوتِ فَاقْذِفِيهِ فِى الْيَمِّ فَلْيُلْقِهِ الْيَمُّ بِالسَّاحِلِ يَاْخُذْهُ عَدُوٌّ لِّى وَعَدُوٌّ لَّهُ وَاَلْقَيْتُ عَلَيْكَ مَحَبَّةً مِّنِّى وَلِتُصْنَعَ عَلـٰي عَيْنِي إِذْ تَمْشِى اُخْتُكَ فَتَقُولُ هَلْ اَدُلُّكُمْ عَلـٰي مَن يَكْفُلُهُ فَرَجَعْنَاكَ إِلَي اُمِّكَ كَيْ تَقَرَّ عَيْنُهَا وَلاَ تَحْزَنَ وَقَتَلْتَ نَفْساً فَنَجَّيْنَاكَ مِنَ الْغَمِّ وَفَتَنَّاكَ فُتُوناً فَلَبِثْتَ سِنِينَ فِى اَهْلِ مَدْيَنَ ثُمَّ جِئْتَ عَلـٰي قَدَرٍ يَا مُوسَي
Maana ya aya hizo ni kama ifuatavyo
"Na hakika Tulikufanyia ihsani mara nyengine (nyingi; kama vile)
Tulipomfunulia Mama yako Yaliyofunuliwa (kwake. Tulimfahamisha kufanya haya)
Ya kwamba mtie (mwanzo, ambaye ndiye wewe Mussa) sandukuni, kisha litie mtoni, na mto utamtupa ufukoni ili amchukue adui Yangu na adui yake (amlee kwa uzuri. Naye ni Firauni). Na nimekutilia mapenzi yanayotokana kwangu (ili upendwe na watu wote), na ili ulelewe machoni mwangu (nimekurejesha kwa mama yako)
(Kumbuka) dada yako alipokwenda (kwa watu wake Firauni) na akasema: "Je! Nikujulisheni mtu wa kuweza kumlea?" Na tukakurudisha kwa mama yako ili macho yake yaburudike wala asihuzunike. Na ulimuuwa mtu na Tukakuokoa katika huzuni na Tukakujaribu kwa majaribio mengi. Na ukakaa myaka mingi pamoja na watu wa Madina; kisha umekuja (hapa) kama ilivyokadiriwa, ewe Mussa.
Kutokana na maelezo ya aya hizo imefahamika kuwa wakati Nabii Mussa (a.s) alipozaliwa, mama yake alikuwa na huzuni pamoja na wasi wasi juu ya mtoto huyo. Kwa sababu,
Nabii Mussa alizaliwa katika zama za Firauni, na Firauni kwa sababu alikuwa na hofu asije akazaliwa mtoto atakayeweza kumuondoa katika sehemu yake hiyo ya ufalme, aliamua kila anapozaliwa mtoto wa kiume amuuwe ili asitokee mtu atakayeweza kuchukua ufalme wake huo)
Mama wa Nabii Mussa ghafla ilimjia ndani ya moyo wake kuwa kwa kutegemea msaada wa Mwenyeezi Mungu amnyonyeshe mwanawe na baadae amtie katika sanduku la mbao, na kumtia mtoni, akiwa na matumaini kuwa mtoto huyo atarudia mikononi mwake, kwa hiyo hakuna haja ya kuhuzunika wala kusikitika, hayo yalikuwa ni matumaini aliyokuwa nayo mama yake Nabii Mussa. Fikra kama hizo ambazo zina muokozi ndani yake ni katika rehema zake Allah (s.w) ambapo huwapa waja wake wema muongozo pale wanapokutwa na matatizo
Vile vile Qur-ani imeielezea aina hiyo ya Wahyi baadhi ya wakati inawezekana ikawa ni wasi wasi wa shetani, Kwa mfano katika (Suratul-Al-Anaam aya ya 121) Allah (s.w) anasema:
وَلاَ تَاْكُلُواْ مِمَّا لَمْ يُذْكَرِ اسْمُ اللهِ عَلَيْهِ وَإِنَّهُ لَفِسْقٌ وَإِنَّ الشَّيَاطِينَ لَيُوحُونَ إِلَي اَوْلِيَآئِهِمْ لِيُجَادِلُوكُمْ وَإِنْ اَطَعْتُمُوهُمْ إِنَّكُمْ لَمُشْرِكُونَ
Maana ya aya hiyo ni hii ifuatayo:
Wala msile katika wale waliosomewa jina la Mwenyeezi Mungu (yaani vilivyokufa wenyewe), maana (kula) huko ni uasi. Na kwa yakini mashetani wanawafunulia marafiki zao kubishana nanyi (katika mambo namna haya yasiyokuwa na maana). Na kama mkiwatii, mtakuwa washirikina.
MWISHO