Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

UUMBAJI WA MWENYEEZI MUNGU

0 Voti 00.0 / 5

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

UUMBAJI WA MWENYEEZI MUNGU
NI VYA MWENYEZI MUNGU VILIVYOMO MBINGUNI NA VILIVYOMO ARDHINI
Mwenyeezi Mungu Mtukufu anasema:-
  1]وَللّهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الأَرْضِ وَلَقَدْ وَصَّيْنَا الَّذِينَ أُوتُواْ الْكِتَابَ مِن قَبْلِكُمْ وَإِيَّاكُمْ أَنِ اتَّقُواْ اللّهَ وَإِن تَكْفُرُواْ فَإِنَّ لِلّهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الأَرْضِ وَكَانَ اللّهُ غَنِيًّا حَمِيدً
Ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini. Na hakika tuliwaamrisha waliopewa Kitabu kabla yenu na nyinyi kwamba,mcheni Mwenyezi Mungu. Na kama mkikufuru, basi ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na ardhini. Na Mwenyezi Mungu ni mkwasi mwenye kusifiwa.

 وَلِلّهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الأَرْضِ وَكَفَى بِاللّهِ وَكِيلاً[2]
Na ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyo ardhini, na Mwenyezi Mungu atosha kuwa mlinzi.
[3]إِن يَشَأْ يُذْهِبْكُمْ أَيُّهَا النَّاسُ وَيَأْتِ بِآخَرِينَ وَكَانَ اللّهُ عَلَى ذَلِكَ قَدِيرًا
Akitaka atawaondolea mbali, enyi watu alete wengine. Na Mwenyezi Mungu ni muweza wa hilo.
 مَّن كَانَ يُرِيدُ ثَوَابَ الدُّنْيَا فَعِندَ اللّهِ ثَوَابُ الدُّنْيَا وَالآخِرَةِ وَكَانَ اللّهُ سَمِيعًا بَصِيرًا[4]

Anayetaka malipo ya duniani, basi yako kwa Mwenyezi Mungu malipo ya duniani na akhera na Mwenyezi Mungu ni mwenye kusikia mwenye kuona.
Ufafanuzi wa Aya 131 – 134 Suratun-Nisaa
Katika juzuu ya kwanza na juzuu hii, tumezungumzia kuhusu kukaririka katika Qur'an. Sasa tutazungumzia kukaririka kwenye Aya hasa hii,kwa sababu ni Aya iliyotajwa na kurudiwa zaidi katika Qur'an . Kisha tutadokeza kukaririka kwa namna maalum ambayo imetajwa kwa kunakiliwa mara mbili katika Aya moja na kurudiwa mara ya tatu katika Aya inayoifuatia moja kwa moja bila ya kuweko kati kitu kingine.
 Ama sababu za kukaririka kwake kwa ujumla ni kwamba maudhui yake ni ulimwengu ambao pamoja na vilivyomo ndani yake unatolea dalili kuwapo Mwenyezi Mungu na sifa zake; kama elimu, uweza, matakwa na hekima. Ni dalili inayokusanya aina za dalili zote na vyenye kutolewa dalili. Kwa hiyo kukumbuka Aya hii ni kukumbuka kuwapo Mwenyezi Mungu na utukufu wake.
 Ama kutajwa kwake hapa mara tatu, ni ishara ya faida tatu: Kwanza: Mwenyezi Mungu katika Aya iliyotangulia amesema: "… Atamtosheleza kila mmoja kwa wasaa wake" Kwa hiyo dalili hii imenasibiana na wasaa huu kuwa ni vyake vilivyomo mbinguni na ardhini.
 Pili: Amesema: Kama mkikufuru basi ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini.
Yaani yeye hamhitaji mwenye kukufuru kwa sababu vilivyomo mbinguni na ardhini ni vyake.

Tatu: Amesema Mwenyezi Mungu: Ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini, na Mwenyezi Mungu atosha kuwa mlinzi.

Akitaka atawaondelea mbali, enyi watu na alete wengine.
Makusudio ni kwamba Yeye ni muweza wa kuwamaliza waasi na kuwaleta watiifu; kwa sababu ni vyake vilivyomo mbinguni na ardhini. Kwa hiyo kila moja katika mara hizo tatu ina sababu yake na kukutanishwa na faida mpya.

Anayetaka malipo ya duniani, basi yako kwa Mwenyezi Mungu malipo ya duniani na akhera.
Yaani malipo ya duniani na akhera yanawezekana kupatikana pamoja na imani na takua. Mwenye kudhani kuwa malipo ya duniani hayawi pamoja na takua, basi huyo amekosea. Kwa sababu hakuna kitu chochote kinachotengeneza vizuri maisha ya hapa duniani ila kitakuwa kinakubaliwa na dini bali kinaamrishwa na kuhimizwa na hiyo dini, lakini kwa sharti moja tu; kuwa kufanikiwa kwake kusiwe ni uovu kwa mwingine na utukufu wake usiwe ni utwevu wa mwingine.
Kwa hivyo malipo ya duniani na akhera hayagongani; isipokuwa kugongana kunatokea baina ya dhulma na malipo ya akhera - baina ya ghushi,hadaa na unyang'anyi na vilevile radhi za Mwenyezi Mungu, neema zake na pepo yake.
 يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ كُونُواْ قَوَّامِينَ بِالْقِسْطِ شُهَدَاء لِلّهِ وَلَوْ عَلَى أَنفُسِكُمْ أَوِ الْوَالِدَيْنِ وَالأَقْرَبِينَ إِن يَكُنْ غَنِيًّا أَوْ فَقَيرًا فَاللّهُ أَوْلَى بِهِمَا فَلاَ تَتَّبِعُواْ الْهَوَى أَن تَعْدِلُواْ وَإِن تَلْوُواْ أَوْ تُعْرِضُواْ فَإِنَّ اللّهَ كَانَ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرًا[5]
Enyi mlioamini! Kuweni imara na uadilifu mtoao ushahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ijapokuwa ni juu ya nafsi zenu au wazazi wawili na jamaa wa karibu. Akiwa ni tajiri au fukara basi Mwenyezi Mungu anawastahiki zaidi. Basi msifuate hawaa ili mfanye uadilifu. Na mkiupotoa au mkaachana nao basi Mwenyezi Mungu ana habari ya myatendayo.
Maelezo kuhusiana na Aya ya 131
Hapana jambo bora kabisa kuliko kumcha Mwenyeezi Mungu:-
a) Kujiepusha na kila alichokukataza, kwani ni salama yako mwenyewe duniani na Akhera;.
b) kufanya kila unachokiweza katika alichokuamrisha, kwani ni nafuu yako duniani na Akhera, Uma zote zimeusiwa haya.
Maelezo kuhusiana na Aya ya 132:
Mwenyeezi Mungu anabainisha kila wakati kuwa hakuna mwenye amri mbele ya Mwenyeezi Mungu, la mbinguni wala ardhini, na natosha kuwalinda mwenyewe waja wake wasifikwe na lolote, lakini viumbe hawasikii tu. Watatafuta pepo wa fulani awalinde au mzimu, au makaburi, au pango na kama haya, uko wapi Uislamu wao watu kama hao?.
Maelezo kuhusiana na Aya ya 134
Tunahimizwa tutafute yole mawili – dunia na Akhera.
Maelezo kuhusiana na Aya ya 135
Hapana cha kuleta raha kubwa na masikilizano duniani kama insafu – kutimiziana haki. Basi hapa inahimizwa kweli kweli kusimamia haki vilivyo kweli kweli, ijapokuwa kusimamia huko kutawadhuru wako na kutakudhuru wewe mwenyewe nafsi yako. Isaidie haki itande, na itapakae kila upande.

[1]Suratun Nisaa Aya ya 131

[2] Suratun Nisaa Aya ya 132

[3] Suratun Nisaa Aya ya 133

[4] Suratun Nisaa Aya ya 134

[5] Suratun-nisaa Aya ya 135

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini