Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

KUMUELEWA NA KUMTAMBUA IMAM

0 Voti 00.0 / 5

MLANGO WA PILI

KUMUELEWA NA KUMTAMBUA IMAM

SEHEMU YA KWANZA.
MTIZAMO KUHUSU IMAM MAHDI (A.S).

Imam Mahdiy ni Imamu wa kumi na mbili na ni Imamu wa mwisho katika madhehebu ya mashia, Imam Mahdiy amezaliwa siku ya Ijumaa mwezi wa shabani katika mwaka 255 hijria Qamaria, (868 miyladiy) katika mmoja wa mitaa ya nchi ya Irak unaojulikana kwa jina la Samarraa.
baba yake Imam Mahdiy anaitwa Imam Hassan Askariy, na yeye ni Imam wa kumi na Moja katika madhehebu ya mashia, mama yake Imam Mahdiy ambae ni mwanamke mtukufu katika historia ya kiislamu anaitwa bibi Nargis, ama kuhusu historia ya mwanamke huyo kuna hadithi mbali mbali zilizonakiliwa kuhusu mama huyo, kuna hadithi isemayo kwamba bibi Nargis ni mtoto wa (Yushuw), Yushuw ni mtoto wa mtawala wa Roma (yaani ni mtoto wa Mtawala wa nchi ya Urumi). Ama kuhusu mama yake inasemekana kwamba mama yake ni kutoka katika ukoo wa (Sham-uun) Sham-uun ni mrithi wa Nabii Issa (a.s)

Kutokana na hadithi zilizonakiliwa imethibitishwa kwamba mama Nar-gis aliingia katika dini ya kiislamu, na Imam Askari (a.s) alimuongoa mwanamke huyo katika watekwa ambao walitekwa na Waislamu katika vita vilivyotokea baina ya jeshi la Roma na Waislamu, Imam Askari (a.s) alimtuma mtu ili kumnunua mwanamke huyo na baadae mtu huyo akampeleka bibi Nar-gis katika mtaa wa Samarraa. (rejea kitabu Kamalud Din juzuu ya 2, mlango wa 41, ukurasa wa 132). Na hadithi hiyo pia imenukuliwa katika kitabu cha (Biharul-an-war, juzuu ya 5. ukurasa wa 11 hadi ukurasa wa 22).
Jambo lililo muhimu na linalofaa kuzingatiwa ni kwamba bibi Nar-gis amelelewa katika nyumba ya bibi (Hakima Khatun) bibi Khatuwn ni dada wa Imam Haadi(a.s) na mama huyo ni mwenye kuheshimiwa sana na Imam Haadi (a.s).
Bibi Nar-gis ni mwanamke ambaye historia yake imenukuliwa katika miaka iliyopita tangu zama za Mtume Muhammad (s.a.w) na imesikika kutoka kwa Mtume(s.a.w), Imam Ali (a.s) na Imam Sadiq (a.s) kuwa mwanamke huyo ni mwanamke bora katika uma wa kiislamu.
Bibi Nargis mbali ya jina hilo ana majina mengine ambayo anaitwa mfano wa majina hayo ni kama vile Malika, Ray-hana, Saykal, na Susan.

JINA, KUNIA NA LAKABU.

Jina na kunia Imam Mahdiy, ni kama jina na kunia ya Mtume Muhammad (s.a.w), ama katika baadhi ya hadithi imekatazwa kutajwa jina hilo mpaka pale ambapo Imam atadhihiri.
Lakabu mashuhuri aliopewa Imam Mahdi ni kama vile Qaa-imu, Mun-tadhari, Baqiyatu-llahi, Hujjat, Khalfu salih, Mansuwr, Saa-hibul-amri, Saahibuzamaan, Waliyi-Asri. Ama jina lililo maarufu ni Mahdi, kila moja kati lakabu hizo zina maana yake.
Ameitwa Imam Mahdi kwa sababu amekwishaongoka, na atawaongoza watu katika njia ya haki, na ameitwa Qaaimu kwa sababu atasimama ili kulingania haki, na ameitwa Mun-tadhari kwa sababu watu wote ni wenye kumsubiri yeye, na ameitwa Baqiyatu-llahi kwa sababu yeye ndie Imamu wa mwisho aliyebakia hadi leo akiwa ni mtimizaji hoja kwa walimwengu, nae ni dhihiriko la mwisho la Mwenyeezi Mungu.

Neno Hujat lina maana ya dhihiriko kutoka kwa Mola kwa ajili ya viumbe, na ameitwa khalafu Saalih kwa sababu yeye ni mmoja katika wafuasi bora wa Mtume Muhammad (s.a.w), na ameitwa Mansuri kwa sababu ni mwenye nusura ya Mola wake,na ameitwa Saahibul-amri kwa sababu yeye ndie atakaesimama kupigania uadilifu kwa ajili ya Mola wake, na ameitwa Saahibu Zamani na Waliyi Asri kwa sababu yeye ni hakimu katika zama ambazo atadhihiru.
Kuzaliwa kwa Imam Zamani (Mahdi)
Kuna hadithi nyingi zilizonakiliwa kutoka kwa Mtume Muhammad (s.a.w) zinazohusiana na Imam Zamani (Mahdi) (a.s).

Kuna hadithi isemayo kwamba kuna mtu atakaetoka katika ukoo wa Mtume aitwae Mahdiy, ambaye atasimama ili kupinga udhalimu, katika zama za kale kulikuwa na kabila lijulikanalo kwa jina la Bani Abass, kabila hilo lilikuwa ni kabila la kidhalimu katika zama hizo na ndipo baada ya kuisikia hadithi hiyo waliamua atakapozaliwa Imam Mahdi wamuuwe, na kwa sababu hii kuanzia zama za Imam Jawad maisha ya maimamu yalikuwa katika hatari sana, na yalizidi zaidi katika zama za Imam Askari (a.s) ambapo watu walikuwa karibu na Imamu walizuiliwa hata kumtembelea kiongozi wao, na siku hadi siku jeshi la Abasi lilikuwa likienda katika nyumba ya Imam Askariy ili kuchunguza habari, na ni sababu hizo basi zilizofanya kuzaliwa kwa Imamu Mahdi kusidhihirishwe, hata ikabidi watu katika famili ya Imamu pia wasielewe kuzaliwa kwa Imam Mahdiy, na mama yake Imam Mahdi hakuwa na dalili zozote za kuonesha kuwa alikuwa na mimba (yaani hata karibu ya kumzaa mtoto huyo hakuonekana na tumbo wakati alipokuwa na mimba ya Imam (Mahdi).

Bibi Hakima Khatun mtoto wa Imam Jawad (a.s) kuhusu kuzaliwa kwa Imam Mahdi anasema:-
"Imam Hassan Askari (a.s) alimfata dada yake Bibi Khatun na akamwambia ewe shangazi karibu nyumbani kwetu usiku wa leyo kwa ajili ya chakula cha usiku, kwa sababu leyo ni usiku wa mwezi wa shaabani, na Mwenyeezi Mungu anataka kunibarikia mtoto ambaye ni hoja kwa walimwengu, bibi Khatun akamuuliza Imam mama yake ni nani? Imam akamjibu kwamba mama yake ni Nar-gis, bibi Khatun akamuambia Imam kwamba bibi Nargis hana dalili zozote zinazoonesha kuwa ana mimba, Imam akamwambia bibi Khatun kwamba ni rehema zake Mwenyeezi Mungu.

Bibi khatun akaenda nyumbani kwa Imamu na kumsalimia bibi Nargis na baadae akakaa kitako, bibi Nargis akaenda karibu yake ili kumvuwa viatu, na baadae akamsalimia na kumwambia mama yangu hali yako, lakini bibi Khatun akamwambia hali yako na hali ya mjukuu wangu ikoje, bibi Nargis hakuamini yaani hakuwa na uhakika kwamba alikuwa na mimba na ndipo bibi Khatun akamwabia usiku wa leo Mola atakubarikia mtoto wa kiume ambae ni hoja kwa walimwengu wote, bibi Nargisi akainamisha kichwa chini kwa haya alizokuwa nazo.

Bibi Khatun anaendelea kwa kusema kwamba "baada ya kusali sala ya Ishaa na kula chakula cha usiku akaenda kulala, ulipofika usiku wa manane akaamka kwa ajili ya kusali sala ya usiku, lakini wakati huo Nargis alikuwa amelala, na hakuwa na dalili yoyote inayoonesha kuwa anataka kuzaa, baada ya kwisha kusali Bibi Khatun akarejea kulala, baada ya dakika chache akaamka na kumuona bibi Nargis anasali sala ya usiku naye baada ya kumaliza akarejea kulala". Bibi Khatun anaendelea kwa kusema "ilipofika alfajiri ya mwanzo alitoka nje na akamuona Bibi Nargis bado amelala, akaingiwa na shaka, baada ya muda mchache Imam Askari akamuita dada yake na kumwambia ewe dada wakati wa kuzaliwa mtoto uko karibu.

Bibi Khatun anasema akakaa kitako na kuanza kusoma suratul Sajidah na suratul Yaasin, hapo hapo bibi Nargis akaamka hali ya kuwa yuko na simanzi, bibi Khatun akamsogelea karibu na kusema unajisikia unataka kuzaa, akasema ndio bibi Khatun akamwambia jikaze na utulie moyo wako, Mola wako sasa hivi atakubarikia mtoto, wote wawili wakiwa wameghumiwa na ndipo baada ya muda mchache wakasikia sauti ya mtoto analia, Bibi khatun alipoondowa nguo akamuona mtoto akiwa amesujudu, akamchukuwa na kumuweka mikononi mwake hali akiwa ni msafi.

Wakati huo huo Imam Askari akamuita dada yake ili ampelekee mtoto, na yeye akampeleka mtoto huyo mbele ya Imamu, Imamu akamchukua mtoto huyo na kumuweka mikononi mwake na kusema, mwanangu sema basi, hapo hapo Mtoto akafumbuwa mdomo na kusema Ash-hadu an- lailaha il-la llah,wahadahu la sharika lahu, wa a-sh-hadu anna Muhammada Rasulu-llah.

Kisha akaanza kumsalia Imamu Ali a.s akaendelea mmoja baada ya mwengine mpaka akafikia baba yake akasimama ili kuonesha heshima na hapo Imamu akamuambia bibi Khatun amchukuwe mtoto huyo na kumpeleka kwa mama yake ili amsalimie. Bibi Khatun anasema siku ya pili yake alikwenda nyumbani kwa Imam Askariy ili kumsalimia lakini alipofungua pazia Imam Mahdi hakumuona ndipo alipomuuliza Imam kumetokea nini kwa walii wangu mbona simuoni, Imam akamjibu kwamba nimemkabidhi Mola wangu kama ambavyo mama wa Mussa amemkabidhi Mussa mbele ya Mola wake.

Bibi Khatun anaendelea kusema kwamba ilipofika siku ya saba alikwenda tena kwa Imam na kumsalimia, lakini mara hii alimkuta mtoto (Mahdi) yupo. Imam akawambia nileteeni mwanangu karibu yangu, na bibi Khatun akampeleka Imam akamwambia tena mwanawe, ewe mwanangu sema basi, mtoto akafumbuwa mdomo na kuanza kumsalia Mtume na Maimamu wote, alipokwishamaliza akasoma aya hii:-
Na tukataka kuwafanyia ihsani wale waliodhoofishwa katika ardhi hiyo,na kuwafanya viongozi,na kuwafanya warithi wa (neema hizo). Na kuwapa nguvu ardhini, na kumuonesha Firauni na Hamana na majeshi yao yale waliyokuwa wakiyaogopa. (Suratul Qasas aya ya 5 hadi ya 6).

SIFA ALAMA NA VIGEZO VYA IMAM MAHDI (A.S)

Kuna hadithi nyingi zilizonakiliwa kutoka kwa Mtume Muhammad (s.a.w) zinazoelezea sifa za Imam Mahdi (a.s), tutazielezea sifa hizo kwa ufupi.
Imam Mahdi ni mwenye sura iliyojaa nuru na yenye kupendeza, nyusi zake ni mfano wa mwezi, macho yake ni makubwa na meusi,pua yake ni ndefu na nzuri, meno yake ni yenye mwanya, na ni mrefu wa kiasi.

kuna hadithi nyengine pia zilizonakiliwa zinazobainisha sifa za Imamu Mahdi, yeye alikuwa ni mwenye kufanya ibada, na wakati wa usiku alikuwa halali kwa kufanya ibada, alikuwa akiishi kikawaida, mwenye subira, ni muadilifu na mwenye tabia nzuri, ni mwenye elimu ya hali ya juu, ni mwenye kupigania jihadi, ni kiongozi mkubwa wa mapinduzi ya kiislamu katika ulimwengu, yeye ametokana na ukoo wa Mtume Muhammad (s.a.w) na ni mtoto alietokana na watoto wa bibi Fatima binti Rasuli, ni mtoto wa tisa katika ukoo wa mashahidi wa Ahlul bayt, Imam Mahdi wakati atakapodhihiru ataegemea kaaba akiwa na bendera ya Mtume (s.a.w) mkononi, na atasimama ili kupinga udhalimu na kuiimarisha dini ya Allah (s.w) na atazitangaza hukumu za kiislamu katika ulimwengu mzima, na watu watakuwa ni wenye mapenzi ya dini yao.

MAISHA YA IMAMU YAMEGAWIKA KATIKA SEHEMU TATU

1. Maisha ya mwanzo ya Imamu yalikuwa ni ya siri, yaani hakuna mtu aliekuwa anajuwa kuzaliwa kwake ila watu wachache tu, na aliendelea kuishi katika maisha hayo ya siri mpaka alipofariki baba yake Imam Askari (a.s).
2. Maisha ya pili ya Imamu ni kutoweka kwa Imamu ,yaani baada ya kufariki Imamu wa kumi na moja, Imam Mahdiy alitoweka kwa rehma za Allah, na mpaka pale ambapo Mola atataka kumdhihirisha basi atadhihiri.
3.Sehemu ya tatu ya maisha ya Imamu ni wakati ambao Imamu atadhiihiri, na kudhuhuru kwake Mola tu ndie anayejuwa ni siku gani atadhuhuru, na wakati huo dunia itakuwa ni yenye usalama na uadilifu kwani Imamu atapigana na watu wote ambao walifanya dhulma katika dunia, basi kwa hiyo watu ambao wanadai wanaelewa ni siku gani Imamu atadhuhuru ni waongo.

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini