DINI YA KIISLAMU NI DINI YA HAKI
BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
DINI YA KIISLAMU NI DINI YA HAKI NO 1
UFAFANUZI WA NENO DINI KILUGHA NA KISHERIA
Ufafanuzi wa neno “dini” kilugha na kisheria ndani ya historia ya mwanaadamu.
Chanzo na asili ya neno dini, kwa mtazamo wa wana lugha; wao wamesema kuwa, dini ni neno wanalotumia waajemi wa kizamani (persian) linalotokana na neno – Daena – likiwa na maana ya johari, hisia na dhati ya mwanaadamu, na baadhi ya watu wamesema kuwa asili ya neno –Daena – lina maana ya kutafakari na kutambua, na wanaamini kuwa neno hilo ni miongoni mwa maandishi maalumu ya sanskrit dehi, Sanskrit ni lugha ya zamani ya india na nchi za mashariki ya kati kwa ujumla, kwa mfano,Irani, Palestina n.k.
Wafuasi wa dini ya Zartushti walijiita “Behdiyn” wakiwa na maana ya watu waumini, na katika kitabu cha Zartushti neno “dini” limekuja likiwa na maana ya kishi, akida, dhati ya mwanaadamu,tabia za kiroho, haiba ya kibinaadamu na hisia za ndani za mwanaadamu. Katika Mizdisna “dini” ni jina la malaika, kutokana na maelezo hayo, katika lugha ya persian, neno dini lina maana ya madhehebu, akida, utiifu na jazaa au malipo. Vilevile baadhi ya wakati neno “dini” katika lugha ya persian ni jina maalumu
kwa ajili ya tarehe ishirini na nne ya kila mwezi kwa miezi ya jua, au ni jina maalumu la Malaika .
Katika lugha ya kiarabu asili ya neno “dini” limepatikana kutokana na neno “daan, daina, diyanatan” na neno “daan” lina maana ya kunyenyekea,utiifu, heshima, hudhui na hushui.
Kwa hiyo asili ya neno “dini” kilugha lina maana ya kunyenyekea au hudhui, kusalimu amri, na kutii .
Baina ya kaumu “Akad” neno “Denu” na “Dinu” lina maana ya kanuni, haki, na hukumu. Na baina ya kaumu ya “Aramiy na Ibriy” neno “Din na Dina” yana maana hiyo hiyo.
Katika lugha ya nchi za kimagharibi, asili ya neno “Din” – Religion – ni asili ya kilatini, Religio au Religar likiwa na maana ya itikadi.
Maana nyengine ya neno “ Religio” ni hofu ya mwanzo inayomjia mtu kutokana na vitu asivyoviona au visivyoonekana .
Dini kwa mtazamo wa kitaalamu (kiistilaha).
Kuna umuhimu mkubwa katika kufahamu maana ya kitaalamu ya neno din, kwa sababu kama pataongezwa au kupunguzwa kitu katika kulifafanua neno hilo katika maana yake ya kitaalamu,kunaweza kusababisha kuleta maana nyengine katika mafunzo ya dini au hukumu za dini, hii itawafanya wale wasiotambua maana ya neno hilo, au wale wasio na itikadi yoyote kuhusiana na dini, kubakia katika ujahili bila ya kupata taaluma yoyote kuhusiana na neno hilo. Kwa hiyo, ili kufahamu maana sahihi ya neno din,ni lazima kulitafuta neno hilo katika matini za dini au turejee katika habari za dini, kwa sababu yale yaliyoandikwa na baadhi ya watu kuhusiana na dini, wameyaandika kulingana na ufahamu wa akida au itikadi zao, hali ya kwamba neno “Din” linapatikana
maana yake kulingana na “ Kupatikana misingi ya lazima ya kuifahamu dini ndani ya matini ya dini yenyewe” katika kitabu kitukufu cha mwisho cha Mwenyeezi Mungu alichoteremshiwa Nabii Muhammad (s.a.w.w) “Qur-ani”.
Kwa hiyo, matini za dini ndizo zinazobainisha maana asili ya neno dini, basi kwa yeyote yule asiyejua maana ya neno hilo na arejee katika vitabu vya dini ili kufahamu matumizi ya neno hilo. Kwa kuzingatia tafsiri ya uwalii wa dini – Ahlulbayt Alayhimu salamu – kuthusiana na neno Dini, tunaweza kufahamu maana asili ya neno hilo kwa mtazamo wa kitaalamu. Basi vipi tunaweza kufahamu maana asili ya neno dini bila ya kurejea katika vitabu vya dini? Hali ya kwamba neno hilo ndani ya Qur-ani limekuja katika Aya na sentensi tofauti likiwa limetumiwa katika maana tofauti.
MWISHO