DINI YA KIISLAMU NI DINI YA HAKI No.5
BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
DINI YA KIISLAMU NI DINI YA HAKI NO.5
Katika makala iliyopita, (makala ya nne inayohusiana na dini ya haki ya Kiislamu) tulielezea kuwa dini ya haki ni dini ya Kiislamu pekee, lakini baadhi ya wafuasi wa dini nyengine kama Mayahudi na Manasara walidai kuwa dini zote ni haki, na mfuasi wa dini yoyote ile atapata saada na ujira mwema kutoka kwa Mola wake, na watu hao wamethibitisha madai yao hayo kupitia dalili za Qur-ani takatifu, hivyo katika makala hii tutaelezea baadhi ya madai ya watu hao na kuyapatia majibu yake inshaallah. suala liko hapa hivi kweli dini za Mayahudi na Manasara ni dini za haki ? kwani dini za Mayahudi na Manasara zote hazikuteremshwa na Mola Mtakatifu? basi hivi kweli madai hayo ni sahihi?
Madai ya watu hao ni haya yafuatayo:-
Katika Aya ya 62 ya Suratul Baqarah Allah (s.w) anasema:
إِنَّ الَّذِينَ آمَنُواْ وَالَّذِينَ هَادُواْ وَالنَّصَارَي وَالصَّابِئِينَ مَنْ آمَنَ بِاللهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ وَعَمِلَ صَالِحاً فَلَهُمْ اَجْرُهُمْ عِندَ رَبِّهِمْ وَلاَ خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلاَ هُمْ يَحْزَنُونَ
Kupitia Aya hiyo wamethibitisha kuwa:-
1. Aya hiyo inatoa himaya kwa dini tofauti na watu tofauti, na sio Dini ya Kiislamu tu, au kwa wafuasi wa dini ya Kiislamu.
2. Aya hiyo inawapa himaya na kuwalingania watu wa dini tofauti, kumuamini Mwenyeezi Mungu, kuamini siku ya Kiyama, na kufanya amali njema.
3. Aya hiyo inaunga mkono dini tofauti. Na sio dini ya Kiislamu tu. Bali watu wa dini zote watapata saada na ujira mzuri kutoka kwa Mola wao.
4. aya hiyo imeelezea sifa tatu zitakazowafanya watu wa dini tofauti kupata saada, sifa hizo ni hizi zifuatazo:-
- Kumuamini Mwenyeezi Mungu (s.w).
- Kuamini siku ya Kiyama.
- Kufanya amali njema.
Sifa hizo ndizo zitakazomfanya mwanaadamu wa dini au madhehebu yoyote yale kuongoka na kupata saada. Basi kwa nini Waislamu wanadai kuwa ni Waislamu na wafuasi wa dini ya Kiislamu tu ndio watakaopata saada hiyo?
Hali ya kwamba Aya hiyo inasema kuwa wafuasi wa dini ya Yahudi na Nasara na Sabiina watapata saada.
Kwa kweli madai hayo sio sahihi, na hiyo ni tata finyu iliyotolewa na baadhi ya watu wa nchi za kimagharibi.
Tunayajibu madai hayo kwa kusema hivi:-
Moja: Kumuamini Mwenyeezi Mungu yaani ni kumuamini Mtume Muhammad (s.a.w.w) na kuamini Mitume yote ya Mwenyeezi Mungu na Ahlulbayt (a.s), na kuamini Malaika wake, na vile vile kuamini hukumu zote alizoteremsha Mola Muumba, miongoni mwa hizo ni sala, funga, hijja, jihadi, desturi na maamrisho yote aliyoyaamrisha Allah (s.w). Kwa hiyo vipi inakubalika mtu kuwa na imani na Mwenyeezi Mungu lakini asiwe na imani na Mitume yake na Ahlulbayt (a.s), na hukumu zake zote kijumla?
Mbili: Kwa mujibu wa itikadi hiyo, (yaani kuwa sahihi dini tofauti) basi hakuna faida yoyote ya kupewa Utume Nabii Muhammad (s.a.w.w). kwa sababu dini ya Mayahudi na Manasara
zingelitosheleza. Hilo sio jambo linalokubalika kuwa Mtume Mtukufu ameteremshwa bila ya malengo au faida yoyote, kwa sababu huyo ni Mtume aliyetumwa na Allah (s.w) kwa ajili ya kuwalingania watu dini hiyo takatifu, na kwa sababu Mwenyeezi Mungu ni Hakiym, na hufanya mambo yake kutokana na hekima alizonazo, basi hafanyi jambo lisilokuwa na faida yoyote kwa waja wake na kwa wajumbe wake.
Tatu: Ni natija gani hiyo mliyoipata kutokana na Aya hiyo mliyoitumia katika kuthibitisha madai yenu?. Hali ya kwamba kuna Aya nyengine nyingi zinazothibitisha kuwa Mwenyeezi Mungu anaikubali dini ya Kiislamu peke yake, na wafuasi wa dini hiyo ndio watakaopata saada?. Pale Allah (s.w) aliposema:-
وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الإِسْلاَمِ دِيناً فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِى الآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ[1]
Na anaye tafuta dini isiyo kuwa Uislamu haitakubaliwa kwake. Naye Akhera atakuwa katika wenye kukhasiri.
Kwa hiyo ni dini ya Kiislamu tu ndiyo dini ya haki inayokubaliwa na Mwenyeezi Mungu (sw).
[1] Surat Al-Imrani Aya ya 85
MWISHO