Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

MALENGO YA MITUME YA ALLAH NO.2

0 Voti 00.0 / 5

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

MALENGO YA MITUME YA MWENYEEZI MUNGU NO.2

* Mitume Mitukufu ya Mwenyeezi Mungu imekuja kuwalingania wanaadamu katika kitu gani?.katika makala iliyopita tulielezea kuhusu malengo ya Mitume ya Mwenyeezi Mungu, katika makala hii tutabainisha malengo hayo muhimu moja baada ya mengine.

MITUME (A.S) IMESHIRIKIANA KATIKA MALENGO YAO.

Tukitupilia macho elimu ya Tarekhe tutafahamu kuwa katika kipindi chote kilichopita elimu ya Tarekhe inathibitisha kuwa Mitume yote imekuja ikiwa na malengo mamoja, nayo ni kuwalingania wanaadamu kwa kuwataka wamuabudu Mola mmoja. Miongoni mwa malengo ya Mitume ya Mwenyeezi Mungu ni haya yafuatayo:-

1. KUTUMIA AKILI NA KUPINGANA NA KUKALIDI

Mitume yote ya Mwenyeezi Mungu imewalingania watu kutumia akili na kupigana na kukalidi mambo ya wengine bila ya kuwa na dalili nayo,Kuwalingania watu kutumia akili na dalili na kujikinga na dhana ni miongoni mwa malengo waliyoshirikiana Mitume katika kuwalingania wanaadamu, kwa sababu akili ni nyenzo ya kukubali wahyi, Mitume imekuja kwa ajili ya kuwaongoza watu katika njia iliyonyooka. kwa hiyo, njia ya Mitume ndio njia bora inayopambanua maarifa ya Mwenyeezi Mungu, kama anavyosema Mtume Muhammad (s.a.w.w) yeye binafsi na wafuasi wake:-

قُلْ هَـذِهِ سَبِيلِى اَدْعُو إِلَي اللهِ عَلـٰي بَصِيرَةٍ اَنَاْ وَمَنِ اتَّبَعَنِى وَسُبْحَانَ اللهِ وَمَا اَنَاْ مِنَ الْمُشْرِكِينَ[1]

Sema: Hii ndiyo Njia yangu - ninalingania kwa Mwenyezi Mungu kwa kujua - mimi na wanao nifuata. Na ametakasika Mwenyezi Mungu! Wala mimi si katika washirikina.

*Hapa anaambiwa Mtume awaambie viumbe kuwa yeye na kila wanaomfuata yeye kuwalingania watu maneno ya dini ya Uislamu, kwa ujuzi wa kweli kweli, kwa hoja na dalili. Sio kusema kuwa.

“Mwendo wetu sisi kuitakidi tu” (ikiwa iko hoja na dalili na ujuzi au hapana).” Sio huu mwendo uliosemwa katika Qur-ani wala katika hadithi za Mitume, wala katika maneno ya wanavyuoni wote wa mbele huko.

Hana ruhusa Muislamu kujifuatia tu pasi na hakika ya jambo hilo. Hana ruhusa kabisa Muislamu kufanya hivi, na Qur-ani inasema dhahir shahir: usijifuatie tu jambo usilokuwa na ujuzi nalo maadamu hakulisema Mwenyeezi Mungu au Mtume wake, hata likiwa linafuatwa na wazee au Maraisi. Si hoja hiyo kuwa linafuatwa na Wazee na Maraisi. Qur-ani yote nzima inasema kuwa si hoja hiyo kufuatwa na Wazee na Maraisi. Dini hiyo ya kufuata Wazee na Maraisi sio dini iliyoletwa na Uislamu.

Mitume ya Mwenyeezi Mungu ili kuthibitisha kuwa njia ya washirikina na Makafiri ni njia iliyo batili, waliwataka na kuwalingania wanaadamu kuleta dalili zao, na watumie akili kufikiri au kudabiri katika mambo. Kama tunavyosoma Qur-ani katika kauli yake Mtume Muhammad (s.a.w.w):-

امِ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ آلِهَةً قُلْ هَاتُوا بُرْهَانَكُمْ هَذَا ذِكْرُ مَن مَّعِيَ وَذِكْرُ مَن قَبْلِى بَلْ اَكْثَرُهُمْ لاَ يَعْلَمُونَ الْحَقَّ فَهُم مُّعْرِضُونَ[2]

Au wanawaabudu miungu mingine badala yake? Sema: Leteni ushahidi wenu! Haya ni ukumbusho wa hawa walio nami, na ukumbusho wa walio kabla yangu. Lakini wengi wao hawaijui kweli, na kwa hivyo wanapuuza.

Ama kwa wale waliowakhalifu Mitume, na wakaziwafiki sunna za kijahili zilziopita, au wakaiga tamaduni za wale wanaofuata njia za batili, basi hao hawana jawabu ya kumjibu Mola wao ila tu watasema:-

“Sisi tuliwafuata wazee wetu”, kama inavyosema Qur-ani kuwaambia watu hao:-

وَإِذَا قِيلَ لَهُمُ اتَّبِعُوا مَا اَنزَلَ اللّهُ قَالُواْ بَلْ نَتَّبِعُ مَا اَلْفَيْنَا عَلَيْهِ آبَاءنَا اَوَلَوْ كَانَ آبَاؤُهُمْ لاَ يَعْقِلُونَ شَيْئاً وَلاَ يَهْتَدُونَ[3]

Na wanapo ambiwa: Fuateni aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu; wao husema: Bali tutafuata tuliyo wakuta nayo baba zetu. Je, hata ikiwa baba zao walikuwa hawaelewi kitu, wala hawakuongoka?

*Yaani wamepewa akili na viungo vyengine vya kujulia jema na baya, lakini hawavitumii, wanajifuatia tu waliyowakuta nayo wazee wao, - hawatazami kuwa ni mazuri hayo au mabaya, na hata wakizinduliwa hawakubali kuzinduka.

[1] Surat Yussuf Aya ya 108

[2] Surat Al Anbiyaa Aya ya 24

[3] Suratul Baqarah Aya ya 170

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini