MALENGO YA MITUME YA ALLAH NO.3
BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
MALENGO YA MITUME YA MWENYEEZI MUNGU NO.3
* Mitume Mitukufu ya Mwenyeezi Mungu imekuja kuwalingania wanaadamu katika kitu gani?.
katika makala iliyopita tulielezea kuhusu malengo ya Mitume ya Mwenyeezi Mungu, katika makala iliyopita tulielezea lengo moja miongoni mwa malengo ya Mitume, nalo lilikuwa ni kutumia akili na kupinga kukalidi bila ya kuwa na dalili au elimu yoyote. katika makala hii tunaendelea na lengo jengine nalo ni kuwalingania watu kumuabudu Mola mmoja na kupingana na wafanyao shirki.
MITUME (A.S) IMESHIRIKIANA KATIKA MALENGO YAO.
Tukitupilia macho elimu ya Tarekhe tutafahamu kuwa katika kipindi chote kilichopita elimu ya Tarekhe inathibitisha kuwa Mitume yote imekuja ikiwa na malengo mamoja, nayo ni kuwalingania wanaadamu kwa kuwataka wamuabudu Mola mmoja. Miongoni mwa malengo mengine ya Mitume ya Mwenyeezi Mungu ni haya yafuatayo:-
2. KUWALINGANIA TAWHIYD NA KUPINGANA NA WAFANYAO SHIRKI SHIRKI
Mitume yote imekuja kuwalingania watu kumuabudu na kumuamini Mola mmoja, na kujiepusha na shirki.
Kwa hiyo baada ya kuwalingania watu kutumia akili na kudabiri, akili ambayo ndio chanzo cha kufahamu na kukubali haki, malengo muhimu ya Mitume katika kuwalingania watu na kuwaongoza ni kumuabudu Mola mmoja na kujiepusha na kumshirikisha, na vile vile kujiepusha na kutii amri yza kitaluti,Ufafanuzi wa neno Tawhiyd:-
Tukielezea maana ya neno Tawhid – kwa upana zaidi – yaani ni kumuabudu Mola mmoja tu, Mola wa mbingu na ardhi, na wala hana mshirika. Kama anavyosema Mwenyeezi Mungu kumuambia Nabii Mussa (a.s):-
إِنَّنِى اَنَا اللهُ لاَ إِلَهَ إِلاَّ اَنَا فَاعْبُدْنِى وَاَقِمِ الصَّلاَةَ لِذِكْرِي[1]
Hakika Mimi ndiye Mwenyezi Mungu. Hapana mungu ila Mimi tu. Basi niabudu Mimi, na ushike Sala kwa ajili ya kunikumbuka Mimi.
Maana nyengine ya neno tawhiyd, ni kutii na kufanya amali kwa amri zake Mwenyeezi Mungu tu. Kama alivyosema Nabii Yussuf (a.s) kuwaambia wenziwe waliokuwa gerezani pamoja naye:-
مَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِهِ إِلاَّ اَسْمَاء سَمَّيْتُمُوهَا اَنتُمْ وَآبَآؤُكُم مَّا اَنزَلَ اللّهُ بِهَا مِن سُلْطَانٍ إِنِ الْحُكْمُ إِلاَّ لِلّهِ اَمَرَ اَلاَّ تَعْبُدُواْ إِلاَّ إِيَّاهُ ذٰلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ وَلَـكِنَّ اَكْثَرَ النَّاسِ لاَ يَعْلَمُونَ[2]
Hamuabudu badala yake ila majina tu mliyo yapanga nyinyi na baba zenu. Mwenyezi Mungu hakuyateremshia hayo uthibitisho wowote. Hapana hukumu ila ya Mwenyezi Mungu tu. Yeye ameamrisha msimuabudu yeyote isipo kuwa Yeye tu. Hiyo ndiyo Dini Iliyo Nyooka. Lakini watu wengi hawajui.
*Hapa anawabainishia baadhi ya Tawhiyd ya Mwenyeezi Mungu, mtu huchukua fursa ya kufundisha popote pale anapopatia wasaa, usiitupe fursa ukiipata, usije ukajuta.
[1] Surat taha Aya ya 14
[2] Surat Yussuf Aya ya 40
MWISHO