UTHIBITISHO NA USHAHIDI
UTHIBITISHO NA USHAHIDI KWAMBA IMAM ALI (A.S) NI KHALIFA WA KWANZA
Ni ukweli unaoeleweka wazi duniani kote kwamba kama unataka kumshawishi mtu kuuendea ukweli wa imani yako, na ikiwa mtu mwenyewe hakubaliani na imani yako, inabidi utumie mantiki (busara) na umtolee dalili kwa kupitia vitabu vyake yeye mwenyewe anavyovikubali. Kwa mfano kama unataka kumshawishi Mkristo juu ya Utume wa Nabii Muhammad (s.a.w.w) inabidi umshawishi kwa kutumia ushahidi ulio katika kitabu chake anachokiamini : Biblia Takatifu. Halikadhalika tutatoa ushahidi kuthibitisha kuwa Mtume Muhammad (s.a.w.w) alimteua Imam Ali (a.s) kwa amri ya Allah (s.w.t) kuwa wasii wake, kutoka katika Qur'an Tukufu na vitabu vya Tafsiir, vitabu vya Siirah, vitabu vya Tarikh (Historia), na vitabu vya Hadithi vilivyoandikwa na Maulamaa wa Kisunni wao wenyewe.
USHAHIDI JUU YA UIMAMU WA ALI (A.S)
1- Hadithul Indhaar au Da'wat Dhul Ashirah.
Katika miaka ya mwanzo ya kuutangaza Uislamu, ndipo iliposhuka aya hii: "WA ANDHIR ASHIIRATAKAL AQRABIIN" - "Na waonye jamaa zako wa karibu (As-Shu'araa 26:214), Mtume Muhammad (s.a.w.w) alimwita Imam Ali (a.s.) na akamwambia: "Ewe Ali, Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameniamrisha kuwaita jamaa (ndugu) zangu wa karibu, hivyo niitie watoto wa Abdul Muttalib na tuandalie chakula kutokana na nyama ya kondoo na maziwa".
Imam Ali (a.s) anasimulia kuwa: "Niliwaita kama nilivyoamrishwa na Mtume na walihudhuria takriban watu 40 ikiwa ni pamoja na ami zake Mtume : Abu Talib, Hamza, Abbas na Abuulahab. Walipokusanyika, Mtume aliwaletea chakula. Ingawa chakula kilikuwa kichache, lakini kiliwatosha na kuwashibisha wote waliokuwepo na bado chakula kingine kikabakia.
Baada ya kula chakula, Mtume alipotaka kuzungumza, Abulahab aliingilia kati na kusema: "Huyu mwenzenu (Muhammad (s.a.w.w) amewaroga", hivyo watu wakasambaa bila kumsikiliza Mtume. Mtume aliniita tena na kusema: "Ewe Ali, huyu mtu ameingilia kati na kuzungumza kabla sijazungumza, hivyo waite tena kesho na utuandalie chakula kama leo".
Siku ya pili walipokuja, Mtume (s.a.w.w) aliwaletea chakula na walikula wakashiba kama jana yake. Walipomaliza kula Mtume alisimama juu na kuwahutubia akisema: "Enyi wana wa Abdul Muttalib, kwa hakika Mwenyezi Mungu amenituma kwa watu wote kwa ujumla na kwenu nyinyi pia nukulinganieni Uislamu. Mwenyezi Mungu ameniamrisha kuwa niwaonye ndugu (jamaa) zangu wa karibu, hivyo ninakulinganieni mambo mawili ambayo ni mepesi sana katika ulimi lakini ni mazito sana katika mizani (siku ya Kiyama). Mambo hayo ni Shahada ya Laa Ilaaha illa llah na kwamba mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu.
Yeyote atakayeukubali (atakayeitikia) wito huu na kunisaidia atakuwa ndugu yangu, msaidizi (Waziri) wangu, Wasii wangu, Mrithi wangu na Khalifa baada yangu". Hakuna aliyejibu isipokuwa mimi (Ali bin AbiiTaalib) nilisimama na kusema: "Mimi Ewe Mtume wa Allah niko tayari". Mtume aliniambia nikae chini na akarudia tena maneno yale. Hakuna aliyejibu isipokuwa mimi. "Mimi, Ewe Mtume wa Allah".
Mtume aliniambia nikae chini na akamrudia maneno yale kwa mara ya tatu, kwa vile hakukuwepo aliyesimama isipokuwa mimi, Mtume aliweka mkono wake katika bega langu na kutangaza: "HUYU (ALI) NI NDUGU YANGU, WASII WANGU, WAZIRI (MSAIDIZI) WANGU, MRITHI WANGU NA KHALIFA BAADA YANGU KWENU, HIVYO MSIKILIZENI NA MTIINI".
Wale waliohudhuria waliposikia maneno haya, walisimama juu wakicheka na kumwambia AbuuTalib: "(Mtume) amekuamrisha umsikilize na umtii mtoto uliyemzaa mwenyewe!" Huu ni ushahidi na uthibitisho wa kwanza na kuan nyingi ziliopo, zenye kuonyesha kua Imam Ali bin AbiiTaalib aliteuliwa kuwa wasiy na Khalifa baada ya Mtume.
Hadithi tulioitaja hapo juu inapatikana katika vitabu vya Kisinni vifuatavyo:
- Taarikh Tabari - Juz. 3, uk. 560. - Sharh Nahjul Balagha cha Ibn Abil Hadiid, Juz. 3, uk. 263. - Al -Kaamil cha Ibn Al-Athiir - Uk. 24. - Taariikh Jawami cha Suyuti. - Musnad cha Imam Ahmad bin Hambal; na vitabu vingine vingi vya Kissuni.
Kwa sababu hadithi hii ni ushahidi uliodhahiri juu ya Uimamu na Ukhalifa wa Imam Ali bin Abitalib, ndio maana baadhi ya Maulamaa na waandishi wa vitabu wa Kisunni, wameanza kujaribu kuificha hadithi hii. Mmoja ya watu waliojaribu kuificha hadithi hii ni Muhammad Husayn Haykal wa Misri, Katika toleo la kwanza la kitabu chake "Hayaat Muhammad" (Maisha ya Muhammad (s.a.w.w) aliitaja hadithi hii kwa urefu wake kama ilivyo Hadithi ya Indhaar, lakini aliiondoa katika toleo lake pili na la tatu la kitabu hicho hicho kimoja.
Kwanini anaamua kuuficha ukweli na kujipendelea upande wake? Inashangaza. Qur'an tukufu inasema: "Na msiufiche ukweli kwa uongo na wala msiufiche ukweli na hali ya kua mnajua". (Baqara 2:42).