Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

FALSAFA YA DINI NO.2

0 Voti 00.0 / 5

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

FALSAFA YA DINI NO 2.

Katika makala iliyopita tuliashiria umuhimu wa dini na umuhimu wa kuitambua falsafa ya dini, vile vile tulielezea baadhi ya miongozo ambayo inaweza kumuongoza mwanaadamu katika njia sahihi, katika makala hii pia tutaendelea kuelezea miongozo hiyo ya dini ambayo inaweza kumsaidia mwanaadamu na kumuongoza katika njia iliyo sahihi.

4. Dini ya haki ni ile dini iliyothibitishwa na Mwenyeezi Mungu na Mitume yake, na Ahlulbayt (a.s). Ikiwa Mtume Muhammad (s.a.w.w) amesema:-

قال رسول الله صلی الله علیه وسلام:"علی مع الحق و القران والحق والقران مع علی ولن یفترقا حتی یردا علی الحوض[1]"

Mtume Muhammad (s.a.w.w) amesema:-

Imam Ali (a.s) yuko pamoja na haki, na Qur-ani iko pamoja na haki, na Qur-ani iko pamoja na Ali (a.s), vitu hivyo viwili (Qur-ani na Ali (a.s) havitengani hadi siku ambayo vitarudi kwangu mimi.

Na vile vile, Mtume Muhammad (s.a.w.w) amesema:-

قال رسول الله صلی الله علیه وسلام: "یا علی بنا ختم الله الدین کما بنا فتحه"  "

Mtume Muhammad (s.a.w.w) amesema:-

Ewe Ali, Mwenyeezi Mungu kwetu sisi kaifungua dini, na kwetu sisi akaifunga.

قال الرضا علیه السلام:" و امر الامامة من تمام الدین  "

Imamu Ridhaa (a.s) amesema:-

Suala la Uimamu (ukhalifa) limo ndani ya hitimisho la dini, wala haliko nje. (Dini haikutimia bila ya kuwepo Uimamu). (Uimamu ni chanzo endelezo cha kubakia dini iendelee).

قال الصادق علیه السلام: " بنی الاسلام عتی خمس علی الصلوة والزکاةوالصوم والحج والولایة و لم یناد بشیء کما نودی بالولایة "

Imam Sadiq (a.s) amesema:-

Uislamu umejengeka kwa nguzo tano, sala, zaka, funga, hija, na uwalii, na wala halikulinganiwa suala la ukhalifa na Uimamu miongoni mwa matano hayo.

قال رسول الله صلی الله علیه وسلام: والذی بعثنی بالحق نبیا لو ان رجلا لقی الله بعمل سبعین نبیا ثم لم یآت بالولایة ولی الامر من اهل بیت علیهم السلام ما قبل الله منه صرفا ولا عدلا

Mtume Muhammad (s.a.w.w) amesema:-

Naapa kwa yule aliyenituma mimi kwa haki kuwa Nabii, iwapo mtu atakwenda mbele ya Mola, huku akiwa amebeba amali zenye kulingana na matendo ya Mitume sabiini, bila ya yeye kuwa na imani na Uimamu wa ukhalifa wa watu wa nyumba yangu, basi Mwenyeezi Mungu hatokikubali chochote kile kutoka kwake.

Kwa hakika dini ya haki ni ile dini ambayo imekubalika kwa kufuata miongozo ya Mitume na Ahlulbayt (a.s) kiamali na kimatendo, kwa hiyo mtu yoyote atakayeibainisha dini bila ya kuzingatia maamrisho ya Mitume na Ahlulbayt (a.s) mtu huyo atakuwa hajaibainisha dini ya haki kama inavyotakiwa, na mtu yoyote yule anayejua uhakika wa dini na akaikubali hiyo dini lakini bila ya kuwa na imani na Mitume ya Mwenyeezi Mungu na Ahlulbayt wake basi mtu huyo hatakuwa na dini, dini ya haki ni ile dini ambayo miongozo yake ni kutoka kwa Mitume na Ahlulbayt (a.s) katika hali zote, kuanzia kuifahamu dini, kuwa na imani nayo, na kuifanyia amali na matendo dini hiyo.

Ikiwa uhakika na desturi zote za dini zilizobainishwa na Mwenyeezi Mungu hazikubainishwa kupitia Mitume na Ahlulbayt (a.s), na tujaalie kuwa desturi hizo zilifahamika na kufanyiwa amali lakini bila ya miongozo ya watu hao watukufu, basi dini hiyo haitakuwa dini, na mtu mwenye itikadi na dini kama hiyo  hatakuwa katika njia sahihi.

Maelezo hayo hayana maana ya kuwa Mitume ya Mwenyeezi Mungu na nyumati zilizopita hazikuwa na dini, kwa sababu Mitume hiyo na nyumati zao zilikuwa na dini, dini ambayo katika zama hizo hawakuwepo Maimamu wa Ahlulbayt (a.s), kwa kweli fikra hiyo sio sahihi, kwa sababu akida za Mitume zilijengwa kwa bishara za Maimamu (a.s), na katika zama zile kabla ya kuja Maimamu vitabu vitukufu vya Mwenyeezi Mungu (Taurati, Zaburi, Injili), vilikwisha elezea kuja kwa watu hao watukufu, na Mitume yote ilikuwa tayari imeshajenga uhusiano kiakida na kiimani na watukufu hao, kwa hiyo katika zama hizo Ahlulbayt (a.s) walikwishaanza huduma za kutoa miongozo yao kutokana na maamrisho na hekima zake Allah (s.w).

5. Dini ya haki ni ile dini ya Wahyi aliyoiteremsha Mwenyeezi Mungu Mtukufu kwa ajili ya waja wake, kwa hiyo, ikiwa tutajaalia kuwa, elimu, taaluma na hukumu zote za dini zililetwa na kuwekewa nidhamu na asiyekuwa binaadamu, au mtu mwengine yoyote yule, na mtu huyo asiwe na uhusiano wowote na wahyi wa Mwenyeezi Mungu, hiyo haitakuwa dini, kwa sababu dini ni lazima iwe na fungamano na mfumo mzima wa maisha ya binaadamu, na dini ya Mwenyeezi Mungu peke yake ndiyo iliyo na sifa hiyo.

Dini ya haki ni lazima idhamini mahitajio ya kila mwanaadamu, na mwanaadamu anaweza kuyapata mahitajio hayo kupitia mabainisho ya mtu ambaye ana elimu na anajua uhakika wa kila kitu, na huyo sio mwengine isipokuwa Yeye Mola Mtakatifu (s.w). Kwa hiyo, dini ya haki ni ile dini iliyoletwa kutoka kwake Allah (s.w).

Maelezo hayo tuliyoyaelezea hapo juu yana maana ya kuwa, dini imeletwa na kuteremshwa kutoka kwake Allah (s.w), ikiwa tayari imejengwa na kupangwa katika nidhamu maalumu kwa mujibu wa mahitajio ya wanaadamu na matakwa yao. Kwa hiyo dini haiwezwi kutengenezwa au kufichiliwa na mwanaadamu, ijapokuwa inawezekana mwanaadamu atakayetengeneza au kufichua dini awe ni mwenye akili pevu na fikra iliyo salama, awe ni mjuzi na mwenye tajiriba ya juu kabisa, hivyo ni lazima tuzingatie kuwa, kufikia katika haki ya mambo matatu katika maisha ya mwanaadamu, elimu, dini, na tajiriba, haiendani sambamba na uteremshwaji wa dini, na kutovumbuliwa dini.

[1]Tarehe Baghdadi, juzuu ya 14, uk, 321.

 

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini