Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

FALSAFA YA DINI NO.3

0 Voti 00.0 / 5

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

FALSAFA YA DINI NO 3

Katika makala iliyopita (makala no 2) tuliashiria na kuelezea baadhi ya miongozo ya dini ambayo inaweza kumuongoza mwanaadamu katika saada, katika makala hii pia tutaendelea kuashiria miongozo hiyo.

6.Utangazaji na usambazaji wa dini ni lazima uwe chini ya mikono ya wajumbe maalumu (makhalifa wa Mwenyeezi Mungu) juu ya ardhi, na hiyo ndio sharti na mzizi mkuu wa dini unaoifanya dini iwe dini, kwani nguzo kuu inayowapelekea kuwafunga watu na Mwenyeezi Mungu katika kuyafikia matalaba yao pamoja na matalaba ya viumbe wengine ni kule kuwa na yakini juu ya ukweli na ujumbe uliotumwa kwao, pamoja na kuwa na uwezo wa kuyafanyia kazi yale yote yaliyotoka kwa Mwenyeezi Mungu, na kuwafikia wao kupitia posta ya Mitume, na kwa kutokana na kuwa, imani na yakini juu ya lile robota la ujumbe wa Mwenyeezi Mungu lililokuja kupitia njia ya Utume, haliwezi kuthibitika ukweli wake mbele yao bila ya kuweko na fungamano maalumu lenye kuwaunganisha wao (wanajamii) na yule aliyewatumia ujumbe huo, na fungamano hilo ni lazima kabla ya kufungamana (halijawaunganisha wao na Mwenyeezi Mungu moja kwa moja), kwanza liwafungamanishe na yule mjumbe wa kwanza (posta kuu), iliyoteremka ndani yake robota hilo la ujumbe kwa ajili yao, tukielewa kuwa sio rahisi kwa mtu wa kawaida ambaye ataishi katika zama za baada ya Mtume, kuweza kuwa na fungamano la moja kwa moja na Mtume (s.a.w.w), ambaye ndiye posta ya ujumbe wa Mwenyeezi Mungu, kwa hiyo ili yeye aweze kuwa na aina fulani ya fungamano na posta hiyo, kunatakiwa kuwa na kiungo kitakachoweza kuunganisha na ule ulimwengu anaoishi ndani yake mwanaadamu, na ule ulimwengu wa ghaibu wenye kufungamana moja kwa moja na mjumbe wa Mwenyeezi Mungu. Basi ni nani mbora wa kufanya hivyo kuliko watu wa nyumba yake (s.a.w.w)?.

Kwa hiyo, Maimamu (a.s) ndio viungo wa kila zama wanaoweza kuunganisha watu na chanzo cha mwanzo kilichokuwa kinaitangaza dini yao?.

7. Dini huthibitika kuwa ni dini pale inapomletea mwanaadamu saada na mafanikio ya duniani na Akhera, dini inamdhamini mwanaadamu katika hali tofauti, kuanzia katika maisha yake ya duniani, maisha yake baada ya kufa, na maisha yake ya siku ya Kiyama.

Dini huthibitika kuwa dini pale inapomuarifisha na kumfafanulia mwanaadamu kuhusiana na saada yake katika maisha ya duniani na Akhera kiamali na kimatendo, dini ya haki ni ile dini inayomdhamini na kumpa mwanaadamu hadhi na mahitajio yake, na kwa sababu saada ya mwanaadamu katika maisha yake ya duniani ni kuwa mahitajio yake yote anayohitajia katika nyanja tofauti yanahitajia mazingatio ya desturi ya dini, kwa hiyo kupatikana kwa saada ndani ya dini ni kutokana na akili, malengo, madhumuni, matendo, mwenendo n.k. ikiwa mwanaadamu atayazingatia hayo, hapana shaka atadhaminiwa saada yake katika maisha yake ya duniani na Akhera.

Basi huo ndio uhakika na ufafanuzi sahihi wa dini.

    قال الباقر علیه السلام: اما انه لیس عند احد من الناس حق ولاصواب الاشیئ اخذوه منا اهل البیت ولا احد من الناس یقضی بحق وعدلا الا ومفتاح ذالک القضاء وبابه واوله سنة امیر المؤمنین علی بن ابیطالب علیه السلام[1]

Katika bayana za hadithi za Imamu Baaqiri (a.s), yeye amesema:-

Ama ule usemi usemao kuwa; hakuna mtu hata mmoja miongoni mwa wanajamii Mwenye kudai kwamba ana haki ya kuwa yeye labda amejibu jambo fulani katika fatuwa zake, isipokuwa yeye atakuwa ukweli na uhakika huo ameupata kwetu, (Mitume ya Mwenyeezi Mungu na Ahlulbayt (a.s)). Na hakuna hata mmoja aliyehukumu kwa uadilifu, isipokuwa funguo za hukumu hizo na mlango wake, na mwanzo wake zinatokana na nyenendo za Imamu Aliy (a.s).
8. Dini sio tu inaelezea maamrisho na hali halisi ya mfumo wa maisha ya binaadamu kulingana na mahitajio yake, bali mbali ya hayo inaelezea taaluma nyengine nyingi zinazohusiana na maisha ya mwanaadamu. Kikawaida, mwanaadamu ni mtu jeuri, muasi, mkanushaji, mvivu na mwenye kupenda starehe na anasa za dunia, hivyo mwanaadamu sio mtekelezaji mzuri wa maamrisho hayo ya dini. Tukiachana na hayo, kimsingi, uelezaji na utekelezaji wa maamrisho ya dini umegawika katika daraja (nafasi) mbili, (nyadhifa mbili) ambazo kila moja ina sehemu yake maalumu katika kuyatekeleza maamrisho hayo.

[1] Amaliy Mufiyd, uk57

 

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini