Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

FALSAFA YA DINI NO.4

0 Voti 00.0 / 5

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

FALSAFA YA DINI NO 4

Katika makala iliyopita tulielezea baadhi ya miongozo ya dini inayoweza kumuongoza mwanaadamu na kumpa taaluma itakayomuwezesha kutafakari na kutambua umuhimu wa dini na falsafa yake, katika makala hii tutaendelea kuelezea mada hiyo hiyo.

Dini ya haki, ni ile dini inayoelezea uhakika na hali halisi ya mahitajio ya mwanaadamu, katika kumtafutia njia bora ambazo zitamfikisha yeye katika njia njema ya saada, na kumdhamini kwa kumtekelezea mahitajio yake kutokana na matakwa yaliyomo katika nafsi yake.

Dini ambayo hukumu na mabainisho yake hayamkidhii mwanaadamu mahitajio yake, wala haina uwezo wa kumdhamini mwanaadamu huyo katika maisha yake, basi dini hiyo haina thamani yoyote kwa wanaadamu na kwa viumbe vyote kwa ujumla, hii ni kwa sababu haimletei mwanaadamu manufaa wala saada yoyote katika maisha yake. Ni kwa sababu hiyo basi, katika dini pia mna mambo ya kiserikali na kitawala.

Katika daraja ya utangazaji, na usambazaji wa dini, Mwenyeezi Mungu ameiteremsha dini kupitia wajumbe maalumu (Mitume yake na Ahlulbayt (a.s)) kwa ajili ya kuwalingania na kuwataka watu wayatekeleze maamrisho ya dini, na akawadhamini wanaadamu kwa mujibu wa utekelezaji wa maamrisho hayo kulingana na undani wa nafsi zao, (yaani wanaadamu huyatekeleza maamrisho hayo kutokana na fitra na matakwa ya nafsi zao).

Baada ya Mwenyeezi Mungu kuiteremshwa dini duniani, na kujenga mazingatio na uhusiano baina ya ulimwengu huu na ulimwengu wa Akhera, aliwadhamini wanaadamu kupata athari nzuri pindi wakiyatekeleza maamrisho ya dini yake, na akawadhamini katika mienendo na matendo yao, na madhara watakayoyapata pindi watakapokuwa hawakutekeleza maamrisho yake.

Ndio, mwanaadamu huyatekeleza maamrisho ya dini ya Mwenyeezi Mungu kwa mujibu wa fitra ya nafsi yake na mahitajio yake, nafsi ya mwanaadamu ni yenye kupenda dini ya Mola wake, kwa sababu matakwa ya dini ndio matakwa ya binaadamu, dini ambayo haimdhamini mwanaadamu na kumtekelezea mahitajio yake hiyo sio dini, kwa sababu tukijaalia kuwa dini hiyo ina mabainisho yake, lakini kusiwe na mtu atakayeitangaza au kuibainisha vipi dini hiyo inaweza kujitangaza au kujitekeleza wenyewe?, kila sheria na kila kanuni ni lazima iwe na mtekelezaji. Na dini nayo imebeba kanuni hiyo. Kwa hiyo dini ni serikali, utawala, na siasa inayotambulika na inayowiana na mahitajio ya mwanaadamu, wanyama, mimea, na vitu vyote duniani, dini ya Mwenyeezi Mungu ni dini yenye kudhamini katika mambo mbali mbali, mbali ya hayo, dini haitengani na amali alizozifanya  mwanaadamu ulimwenguni, na athari ya amali zake alizozifanya ulimwenguni, baadhi ataziona hapa hapa ulimwenguni, na baadhi atazikuta Siku ya Kiama.

9. Ikiwa mpaka wa maisha ya mwanaadamu sio duniani tu, (bali baada ya kufa pia atakuwa na maisha yake huko Akhera), basi dini nayo pia haiko duniani tu (bali itaendelea hadi siku ya kiama),mbali ya kuwa Mwenyeezi Mungu ameiteremsha dini kwa maamrisho mbali mbali kulingana na mahitajio ya mwanaadamu duniani, vile vile ametoa mabainisho yake yanayohusiana na hukumu mbali mbali za siku ya Kiama, Mwenyeezi Mungu pia alizingatia sana katika kubainisha hali halisi ya siku ya kiama. Kwa hiyo, dini ya Mwenyeezi Mungu imezingatia ulimwengu wa duniani na Akhera, kiasi ya kwamba kuna uhusiano baina ya dunia hizo mbili na hukumu zake Allah (s.w), na uhusiano huo ndio unaomfanya mwanaadamu afikie katika saada na kudhaminiwa katika maisha yake.

10. Dini ya haki ni ile dini ambayo ina uwezo wa kumletea mwanaadamu mafanikio, yaani, dini ni lazima im-bainishie mwanaadamu hali halisi ya maisha ya duniani na Akhera na vilivyomo humo,na namna ya uhusiano uliopo baina ya dunia hizo mbili na mwanaadamu mwenyewe.Na vipi anaweza kuifikia saada na mafanikio yake. Na kwa sababu hiyo basi Qur-ani takatifu inajiarifisha kuwa ni kitabu kinachobainisha kila kitu. Kama anavyosema Allah (s.w):-

وَعِندَهُ مَفَاتِحُ الْغَيْبِ لاَ يَعْلَمُهَا إِلاَّ هُوَ وَيَعْلَمُ مَا فِى الْبَرِّ وَالْبَحْرِ وَمَا تَسْقُطُ مِن وَرَقَةٍ إِلاَّ يَعْلَمُهَا وَلاَ حَبَّةٍ فِى ظُلُمَاتِ الاَرْضِ وَلاَ رَطْبٍ وَلاَ يَابِسٍ إِلاَّ فِى كِتَابٍ مُّبِينٍ

Na ziko kwake funguo za ghaibu; hakuna azijuaye ila Yeye tu. Na Yeye anajua kilioko nchi kavu na baharini. Na halidondoki jani ila analijua. Wala punje katika giza la ardhi, wala kinyevu, wala kikavu ila kimo katika Kitabu kinachobainisha.

Na madai hayo, ni yenye kuthibitisha hali halisi ya mabainisho hayo, kwa mujibu wa Aya hii ifuatayo:-

لَقَدْ كَانَ فِى قَصَصِهِمْ عِبْرَةٌ لِّاُوْلِى الاَلْبَابِ مَا كَانَ حَدِيثاً يُفْتَرَي وَلَـكِن تَصْدِيقَ الَّذِى بَيْنَ يَدَيْهِ وَتَفْصِيلَ كُلَّ شَيْءٍ وَهُدًى وَرَحْمَةً لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ[1]

Kwa hakika katika hadithi zao limo zingatio kwa wenye akili. Si maneno yaliyo zuliwa, bali ni ya kusadikisha yaliyo kabla yake, na ufafanuzi wa kila kitu, (kinachohitajiwa katika dini) na ni uwongofu na rehema kwa kaumu yenye kuamini.

[1] Surat yussuf Aya ya 111

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini