Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

UFAFANUZI WA DINI NO.2

0 Voti 00.0 / 5

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

UFAFANUZI WA DINI NO.2

Ufafanuzi wa dini:-

Dini ni udadisi na utafutaji wa mwanaadamu kwa ajili ya kumfikia na kumtambua Mola wake, siku zote, hatima ya udadisi na utafutaji huo humalizikia kwa Mola Mtakatifu, kwa hiyo udadisi na utafutaji huo ni lazima ufanywe kwa mujibu wa mapendekezo ya mwanaadamu mwenyewe.

Ufafanuzi huo wa dini ulioelezewa hapo juu hautoshelezi, kwa sababu, (ingawa) Mwenyeezi Mungu anayekusudiwa ni yule Mwenyeezi Mungu aliye katika nyoyo za wanaadamu, na hii inaonyesha nafasi ya mwanaadamu katika dini, hali ya kwamba maudhui ya dini ni mwanaadamu, na nafasi ya dini kwa mwanaadamu sio Mwenyeezi Mungu tu, bali kuna mambo mbali mbali yaliyo muhimu kwa mwanaadamu.

Katika makala iliyopita tulielezea kuhusu ufafanuzi wa dini , na tukaashiria baadhi ya vidokezo ambavyo vinahusiana na mada hiyo ya dini katika makala hii vile vile tutaendelea kuelezea vidokezo hivyo vinavyohusiana na umuhimu wa dini katika jamii ya wanaadamu. Ili kutambua umuhimu wa dini ni vyema tukaashiria baadhi ya vidokezo vinavyohusiana na ufafanuzi na umuhimu wa dini kwa walimwengu na jamii kwa ujumla.

Vidokezo kuhusiana na ufafanuzi wa dini.

Vidokezo vya mwisho:

Kidokezo ni habari au jambo linalosaidia kutoa fununu au njia ya kufumbua tatizo fulani.

 Kidokezo cha nane:

Mfumo wa dini unaonyesha fungamano maalumu liliopo baina ya dini na Uislamu, Fungamano ambalo ndio kiini na chanzo cha dini, kwa upande mmoja, mfumo huo unaonyesha uhusiano ulipo baina ya mwanaadamu na Mwenyeezi Mungu, baina ya mwanaadamu mwenyewe na nafsi yake, baina ya mwanaadamu na wanaadamu, na baina ya mwanaadamu na hali halisi nyengine zilizomo ndani ya dini, na kwa upande mwengine mfumo huo unaonyesha upeo uliopo ndani ya dini Kwa hiyo, dini sio mwenendo wa maisha tu, bali ni mwenendo wa maisha yaliyopita uliokusanya na kufungamana na akida, tabia, fikra, mitazamo, nadharia, na mazingatio tofauti yanayomuelekea mwanaadamu. Ni jambo lililowazi kabisa kuwa, fungamano hilo:-

A: Ni natija ya hukumu, na mabainisho ya dini ya Mwenyeezi Mungu, na sio natija ya kila dini, (dini nyenginezo, dini ya makafiri, washirikina, n.k.). kwa sababu fungamano hilo ni natija na mapato ya wenye dini.

B: Fungamano hilo, ambalo ndio chanzo cha dini, ni lazima limalizikie kwa Mwenyeezi Mungu Mtukufu. Mola ambaye daraja ya utukufu wake itatambuliwa na wanaadamu pindi wakiiamini Mitume ya Mwenyeezi Mungu, na Ahlulbayt (a.s).

Tukijaalia kuwa fungamano hilo linaweza kupatikana, (ambapo ni jambo lisilowezekana) hata bila ya kuyatekeleza maamrisho ya Mwenyeezi Mungu katika hukumu na elimu zake, basi hapana shaka fungamano hilo halitakuwa na thamani hata chembe moja, hata kama fungamano hilo litajenga uhusiano fulani na Mola Mtakatifu.

Kwa kuzingatia maelezo hayo, natutupilie macho nadharia ya William Jams kuhusiana na dini, yeye anasema:-“Maana na madhumuni ya dini ni ile hali (mawazo) inayomfanya mwanaadamu, (asiweze kujizuia) kuchukua hatua za kujifikisha katika daraja ya juu, na kikawaida hali hiyo inaendana na dini[1].

Ufafanuzi huo aliouelezea William Jamz haukubaliki na sio sahihi, kwa sababu hizi zifuatazo:-

Moja: Kikawaida, kikwazo au kizuizi (kifungo fulani) ni alama au ishara inayoonyesha uwezekano wa kubagua (kutenganisha) baina ya hali halisi ya hisia hiyo na dini.

Mbili: hali kama hiyo inayomtokezea mwanaadamu ni tofauti na hali nyengine zinazomtokezea mwanaadamu, kwa mfano, hali inayomfanya mtu kujenga uhusiano, au kupata mshangao, au hali ya upendo, hivyo, hali hiyo inayomjia mwanaadamu kuhusiana na dini ni tofauti na hali kama hizo, kwani hali hiyo humfanya mwanaadamu awe na dini, dini ambayo inampa mahitajio yake kulingana na fungamano hilo alilonalo, na uhusiano ulipo baina ya dini, na hali hiyo, ni fungamano ambalo linaweza kujengeka.(hata katika masuala ya mapenzi baina ya wapendanao), lakini ni lazima tuzingatie kuwa kuna tofauti kubwa baina ya mafungamano hayo mawili.

Tatu: Kutokana na ufafanuzi huo alioutoa William Jams kuhusiana na dini, tunapata natija ya kuwa, hali kama hiyo humfanya mwanaadamu ajenge uhusiano na Mwenyeezi Mungu tu, hali ya kwamba mwanaadamu kwa kuwa na hali kama hiyo (ambayo ni dini) mbali ya Mwenyeezi Mungu anahitajia mambo mengine mbali mbali yatakayomdhamini katika mahitajio yake na kwa mujibu wa dini yake,Kwa ufafanuzi zaidi, Mwanaadamu kuwa na dini, sio tu kunamfanya yeye ajenge uhusiano na Mwenyeezi Mungu, bali mbali ya uhusiano huo vile vile anahitajia kuwa na uhusiano baina yake mwenyewe, na kuwa na uhusiano baina yake na jamii.(hali ya kwamba William ameufunga uhusiano huo mahasusi kwa Mwenyeezi Mungu tu, na sio jamii na wanaadamu, hali ya kwamba kila mwanaadamu mbali na uhusiano na Mwenyeezi Mungu, vile vile anahitajia uhusiano na wanaadamu na jamii).

Nne:Ufafanuzi huo wa dini alioutoa William Jams unapinga kazi za utendaji na utekelezaji wa mahitajio ya wanaadamu katika jamii, hali ya kwamba kazi ya dini ni kutekeleza mahitaji na matakwa ya wanaadamu katika nyanja mbali mbali, kwa sababu mwanaadamu ana uhusiano na jamii, na jamii ina uhusiano na mwanaadamu, na wadhifa wa dini ni kuitekelezea jamii hiyo, (ambayo ndani yake mna wanaadamu) mahitajio na matakwa yake. Kwani malengo makuu ya dini ni kumuongoza mwanaadamu na kumfikisha katika saada ya duniani na Akhera.

[1] Kitabu Seyr Hikmat dar Uropa, (njia za hekima ndani ya nchi za kimagharibi), Muhamad Ali furughi, juzuu ya 3, uk 238.

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini