Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

UFAFANUZI WA DINI NO.5

0 Voti 00.0 / 5

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

UFAFANUZI WA DINI NO.5

Ufafanuzi wa dini:-

Dini ni udadisi na utafutaji wa mwanaadamu kwa ajili ya kumfikia na kumtambua Mola wake, siku zote, hatima ya udadisi na utafutaji huo humalizikia kwa Mola Mtakatifu, kwa hiyo udadisi na utafutaji huo ni lazima ufanywe kwa mujibu wa mapendekezo ya mwanaadamu mwenyewe.

Ufafanuzi huo wa dini ulioelezewa hapo juu hautoshelezi, kwa sababu, (ingawa) Mwenyeezi Mungu anayekusudiwa ni yule Mwenyeezi Mungu aliye katika nyoyo za wanaadamu, na hii inaonyesha nafasi ya mwanaadamu katika dini, hali ya kwamba maudhui ya dini ni mwanaadamu, na nafasi ya dini kwa mwanaadamu sio Mwenyeezi Mungu tu, bali kuna mambo mbali mbali yaliyo muhimu kwa mwanaadamu.

Katika makala iliyopita tulielezea kuhusu ufafanuzi wa dini , na tukaashiria baadhi ya vidokezo ambavyo vinahusiana na mada hiyo ya dini katika makala hii vile vile tutaendelea kuelezea vidokezo hivyo vinavyohusiana na umuhimu wa dini katika jamii ya wanaadamu.

Ili kutambua umuhimu wa dini ni vyema tukaashiria baadhi ya vidokezo vinavyohusiana na ufafanuzi na umuhimu wa dini kwa walimwengu na jamii kwa ujumla.

Vidokezo kuhusiana na ufafanuzi wa dini.

Vidokezo vya mwisho:

Kidokezo ni habari au jambo linalosaidia kutoa fununu au njia ya kufumbua tatizo fulani.

 Kidokezo cha kumi na mbili:

Dini sio kifungo, wala dini haijajifunga, na hakuna mtu yoyote yule anayeweza kuifunga dini katika hali moja tu, hali ya kwamba dini imekusanya mambo tofauti, maamrisho, makatazo, misingi mbali mbali ya kielimu, maendeleo mbali mbali ya kijamii, kiutamaduni,n.k. hivyo tukijaalia kuwa dini ni hali moja tu tutasababisha kuzifunga na kuziondoa njia nyengine ambazo zinahitajiwa na kila mwanaadamu, kwa maelezo mengine; kuifunga dini katika hali moja ni kuibagua dini na wahyi wa Mwenyeezi Mungu, kuitenga dini na akili, na kuitenga dini na tajiriba tofauti, kuifunga dini katika hali moja kuna maana ya kutokuwa na uhakika wa dini katika milango miwili:-

1. Mlango wa kielimu.

2. Mlango wa kisheria.

Dini ambayo haiendani sawa na akili na wahyi wa Mwenyeezi Mungu kwa hakika hiyo sio dini, na wala hatuwezi Kuibagua akili na wahyi, Wahyi umekusanya bahari iliyotandaa kila upande wa ulimwengu, bahari ambayo haina upeo na imefufurika kwa mambo ya uhakika. Mambo ambayo mwanaadamu kutokana na wingi wake hawezi kuyapatia ufahamu wake, hata kama atautumia umri wake wote katika kuyatafutia ufumbuzi,(hii haimaanishi kuwa mwanaadamu hawezi kufahamu chochote kuhusiana na dini au elimu ya dini), bali kuna baadhi ya mambo ya elimu, ni Mola peke yake ndiye anayejua uhakika wa mambo hayo. Mwenyeezi Mungu Mtukufu anasema:-

وَيَسْاَلُونَكَ عَنِ الرُّوحِ قُلِ الرُّوحُ مِنْ اَمْرِ رَبِّى وَمَا اُوتِيتُم مِّن الْعِلْمِ إِلاَّ قَلِيلاً[1]

Na wanakuuliza khabari za Roho. Sema: Roho ni katika mambo ya Mola wangu Mlezi. Nanyi hamkupewa katika ilimu ila kidogo tu.

Kwa hiyo kauli ya Lord Wirk kuhusiana na ufafanuzi wa dini sio sahihi na wala haukubalili. Lord kuhusiana na ufafanuzi wa dini anasema hivi:-

“Asili ya “Dini” ni kifungo maalumu. (fungamano maalumu). Kwa hiyo, fungamano lolote liliopo biana ya watu wawili ni aina ya dini fulani, kwa hiyo ufafanuzi kuhusu mapenzi ya kijinsia yanayotokea baina ya watu wawili hubadilika na kuwa dini.

Kauli hiyo haikubaliki, kwa sababu; sio kila fungamano ni dini, fungamano la dini, ni lile fungamano ambalo ni lenye kufuata njia na malengo maalumu ya dini, kwa hiyo kama itakuwa kila fungamano ni dini, basi vipi tunaweza kulibagua fungamano la dini na fungamano lisilo la dini? Tuachane na hayo, kwa kuzingatia tofauti ziliopo baina ya mafungamano mbali mbali, na kwa kuzingatia hali halisi ya haki na uhakika wa mambo ulivyo, basi ni lazima dini iwepo, kwa sababu dini ni mfumo maalumu unaoendana na mahitajio ya maisha ya wanaadamu. Kunaweza kuulizwa suala ya kuwa; kuna tofauti gani baina ya dini na njia zinazofuatwa zisizokuwa za dini? Hivi kuwepo mafungamano mbali mbali, na kuwepo wafuasi mbali mbali wa dini tofauti, hii haiwezi kuwa ni dalili tosha inayowapelekea watu kupinga kuwepo kwa dini moja tu?. Jawabu ya suala hilo tayari tumeshalielezea katika maelezo yaliyopita, huko nyuma tumefafanua kwa uwazi kabisa kuwa dini ya haki ni ipi, na dini ya haki inatakiwa kuwa na sifa gani, hivyo hakuna ulazima wa kurejea tena jawabu ya suala hilo.

[1] Surat Al-Israa aya ya 85

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini