Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

MALINGANIO YA MITUME NO.3

0 Voti 00.0 / 5

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

MALINGANIO YA MITUME YA ALLAH (S.W) NO.3

Katika makala iliyopita (makala namba mbili) tulielezea njia walizotumia Mitume na malinganio yao katika kufikisha ujumbe wa Mwenyeezi Mungu kwa walimwengu. katika makala hii vile vile tutaendelea kuelezea njia nyengine walizotumia Mitume katika kutimiza wadhifa wao huo wa kufikisha ujumbe waliopewa na Mola wao Mtakatifu.

*Namna ya kuwalingania watu ni maneno mazuri yenye hekima yanayoweza kumtoa nyoka pangoni, seuze yawe ni ya akili pia.

Mitume ya Mwenyeezi Mungu ilitumia njia mbali mbali katika kufikisha ujumbe wa Mola wao. miongoni mwa hizo ni:-

1-1. KUONYA KUTOKANA NA TABU NA ADHABU ZA DUNIA
Mitume Mitukufu baada ya kuwalingania watu katika dini ya Mwenyeezi Mungu, waliwatahadharisha watu kutoipinga dini ya Mwenyeezi Mungu, kwani kwa kufanya hivyo kutawasababishia wao kuteremshiwa adhabu, hivyo waliwalingania watu na kuwatahadharisha kutokana na adhabu hiyo, kama tunavyosoma ndani ya Qur-ani:-

فَإِنْ اَعْرَضُوا فَقُلْ اَنذَرْتُكُمْ صَاعِقَةً مِّثْلَ صَاعِقَةِ عَادٍ وَثَمُودَ[1]

Basi wakipuuza wewe sema: Nakuhadharisheni adhabu mfano wa adhabu ya A'di na Thamudi.

*Mtume (s.a.w.w) alimsomea mkubwa wa Makureishi – Utba bin Rabia – mwanzo wa sura hii, hata alipofika hapa, Utba akamziba Mtume kinywa kwa hofu iliyompanda. Akenda zake mbio, na Uislamu umekwishaanza kumuingia moyoni mwake, akawazungumzia wakubwa wenzake, lakini Abujahli na  wenziwe walimpandisha mori wa kijahili mpaka akaitoa azma ile, akafa ukafirini katika vita vya Badri kama alivyokufa Abujahli na wafujaji wenzake.

Vile vile Mitume iliwatahadharisha wale ambao wanaghafilika katika kumkumbuka Mwenyeezi Mungu na kutii amri zake kuwa watapata mashaka na tabu katika maisha yao ya duniani. Hata kama atakuwa na kila anachohitajia katika maisha yake ya duniani, kuhusu kauli hiyo Allah (s.w) anasema:-

وَمَنْ اَعْرَضَ عَن ذِكْرِى فَإِنَّ لَهُ مَعِيشَةً ضَنكاً وَنَحْشُرُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ اَعْمَي[2]

Na atakaye jiepusha na mawaidha yangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na Siku ya Kiyama tutamfufua hali ya kuwa kipofu.

Pale Mitume ilipoeleza kuwa Makafiri watapata adhabu katika dunia, na wakawahofisha watu na kuwatahadharisha kutokana na adhabu ya Mwenyeezi Mungu, kutawasababishia wao kupata ibra na kusahihisha amali na matendo yao, kama anavyosema Allah (s.w) baada ya kuteremsha adhabu zake katikaa Kaumu ya Luti:-

وَتَرَكْنَا فِيهَا آيَةً لِّلَّذِينَ يَخَافُونَ الْعَذَابَ الاَلِيمَ[3]

Na tukaacha humo Ishara kwa ajili ya wanao iogopa adhabu chungu.

1-2. KUWAHOFISHA WATU KUTOKANA NA TABU NA ADHABU YA SIKU YA KIAMA

Mitume ya Mwenyeezi Mungu ilipokuwa ikifikisha ujumbe wa Mwenyeezi Mungu kwa watu, iliwatahadharisha watu kutokana na tabu ya siku ya Kiama, na iliwaelezea watu hali watakayokuwa watu wa motoni, kama tunavyoshuhudia ndani ya Qur-ani:-

وَسِيقَ الَّذِينَ كَفَرُوا إِلَي جَهَنَّمَ زُمَراً حَتَّي إِذَا جَاؤُوهَا فُتِحَتْ اَبْوَابُهَا وَقَالَ لَهُمْ خَزَنَتُهَا اَلَمْ يَاْتِكُمْ رُسُلٌ مِّنكُمْ يَتْلُونَ عَلَيْكُمْ آيَاتِ رَبِّكُمْ وَيُنذِرُونَكُمْ لِقَاء يَوْمِكُمْ هَذَا قَالُوا بَلَي وَلَكِنْ حَقَّتْ كَلِمَةُ الْعَذَابِ عَلـٰي الْكَافِرِينَ[4]

Na waliokufuru watapelekwa katika Jahannamu makundi makundi, mpaka watapoifikia itafunguliwa milango yake, na walinzi wake watawaambia: “ je! Hawakukujieni Mitume miongoni mwenu wakikusomeeni Aya za Mola wenu, na kukuonyeni makutano ya siku yenu hii?” watasema : “kwa nini? (wametujia)! Lakini limethubuti neno la adhabu juu ya wale waliowakanusha. (nao ndio sisi).”

*Basi natutengenee kabla ya kusimangwa kwa Aya hii na nyenginezo, Aliyeonya, Hana Lawama Akitesa. Na Mwenyeezi Mungu ametuonya kweli kweli.

Katika Aya nyingi za Qur-ani kumelezewa mateso na mashaka ya moto wa jahannamu, kama anavyosema Allah (s.w):-

فَاَنذَرْتُكُمْ نَاراً تَلَظَّي[5]

Basi nakuonyeni na Moto unao waka!

Mwenyeezi Mungu katika Aya zake nyingi anawatahadharisha watu na adhabu ya Siku ya Kiama kwa sababu kuwa na hofu na adhabu ya siku ya Kiama, ni miongoni mwa dalili muhimu zitakazowafanya waja wa Mwenyeezi Mungu kutii amri za Mola wao na kufanya yale ambayo Mola wao amewaamrisha, kama anavyosema Allah (s.w) kuhusiana na watu hao:-

رِجَالٌ لاَّ تُلْهِيهِمْ تِجَارَةٌ وَلاَ بَيْعٌ عَن ذِكْرِ اللهِ وَإِقَامِ الصَّلاَةِ وَإِيتَاء الزَّكَاةِ يَخَافُونَ يَوْماً تَتَقَلَّبُ فِيهِ الْقُلُوبُ وَالاَبْصَارُ[6]

Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na kumdhukuru Mwenyezi Mungu, na kushika Sala, na kutoa Zaka. Wanaikhofu Siku ambayo nyoyo na macho yatageuka.

[1] Surat Fussilat Aya ya 13

[2] Surat Taha Aya ya 124

[3] Surat Dhaariyati Aya ya 37

[4] Surat Zumar Aya ya 71

[5] Surat Layl Aya ya 14

[6] Surat Nuur Aya ya 37

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini