Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini

MALINGANIO YA MITUME NO.5

0 Voti 00.0 / 5

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

MALINGANIO YA MITUME YA ALLAH (S.W) NO.5

Katika makala iliyopita (makala namba nne) tulielezea njia walizotumia Mitume na malinganio yao katika kufikisha ujumbe wa Mwenyeezi Mungu kwa walimwengu. katika makala hii vile vile tutaendelea kuelezea njia nyengine walizotumia Mitume katika kutimiza wadhifa wao huo wa kufikisha ujumbe waliopewa na Mola wao Mtakatifu.

*Namna ya kuwalingania watu, ni maneno mazuri yenye hekima yanayoweza kumtoa nyoka pangoni, seuze yawe ni ya akili pia.

Mitume ya Mwenyeezi Mungu ilitumia njia mbali mbali katika kufikisha ujumbe wa Mola wao. miongoni mwa hizo ni:-

2-2. KUWABASHIRIA WATU PEPO NA KUWA WATASAMEHEWA MAKOSA YAO.

Mwenyeezi Mungu Mtukufu amewaahidi waja wake kuwa atawasamehe kutokana na makosa waliyoyafanya, na hii ni dalili muhimu inayowapa watu matumaini na kuwa na shauku ya kufanya matendo mema, kwa hiyo Mitume ya Mwenyeezi Mungu ilitumia njia hii katika kuufikisha ujumbe wa Mwenyeezi Mungu, na ilileta athari kubwa kwa watu. Katika Qur-ani tunasoma hivi:-

قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ اَسْرَفُوا عَلـٰي اَنفُسِهِمْ لاَ تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللهِ إِنَّ اللهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعاً إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ[1]

Sema, “Enyi waja wangu mliojidhulumu nafsi zenu! Msikate tamaa na rehema za Mwenyeezi Mungu, bila ya shaka Mwenyeezi Mungu husamehe dhambi zote, hakika Yeye ni Mwingi wa kusamehe na Mwingi wa kurehemu.”

Vile vile Mwenyeezi Mungu amewaahidi waja wake kuwalipa Pepo pindi watakapofanya yale aambayo wameamrishwa na Mola wao, na hii ni katika dalili muhimu na thabiti inayowapa watu matumaini, na kuwa na imani ya kufanya matendo mema, na Mitume vile vile katika kufikisha ujumbe wao kwa watu waliitumia njia hii. Kama anavyosema Allah (s.w):-

وَبَشِّرِ الَّذِين آمَنُواْ وَعَمِلُواْ الصَّالِحَاتِ اَنَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِى مِن تَحْتِهَا الاَنْهَارُ كُلَّمَا رُزِقُواْ مِنْهَا مِن ثَمَرَةٍ رِّزْقاً قَالُواْ هَـذَا الَّذِى رُزِقْنَا مِن قَبْلُ وَاُتُواْ بِهِ مُتَشَابِهاً وَلَهُمْ فِيهَا اَزْوَاجٌ مُّطَهَّرَةٌ وَهُمْ فِيهَا خَالِدُونَ[2]

Na wabashirie walio amini na wakatenda mema kwamba watapata mabustani yapitayo mito kati yake; kila watapo pewa matunda humo, watasema: Haya ndiyo kama tuliyo pewa mbele. Na wataletewa matunda yaliyo fanana; na humo watakuwa na wake walio takasika; na wao humo watadumu.

B.) HEKIMA, MAWAIDHA, NA MAJADILIANO MAZURI

Mwenyeezi Mungu amemtaka Mtume wake Muhammad (s.a.w.w) kuufikisha ujumbe wake kwa kutumia njia tatu zifuatazo:-

Hekima, mawaidha na majadiliano mazuri. Kama anavyosema Allah (s.w):-

ادْعُ إِلِى سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ وَجَادِلْهُم بِالَّتِى هِيَ اَحْسَنُ إِنَّ رَبَّكَ هُوَ اَعْلَمُ بِمَن ضَلَّ عَن سَبِيلِهِ وَهُوَ اَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ[3]

Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa hikima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. Hakika Mola wako Mlezi ndiye anaye mjua zaidi aliye ipotea Njia yake, na Yeye ndiye anaye wajua zaidi walio ongoka.

Maelezo kuhusiana na Aya

Hii ndio namna ya kulingania, maneno matamu humtoa nyoka pangoni, seuze yawe ni ya akili pia, imebainishwa katika Suraul-Baqarah, Aya ya 253, na katika aya ya 90 ya surat Al-An-aam,namna gani Mwenyeezi Mungu alivyowafadhilisha hao Mitume waliokuwa kabla ya Nabii Muhammad (s.a.w.w). Katika jamii kuna makundi tofauti, kuna kundi lililo na uwezo wa kudiriki mambo kwa kutumia akili zao, na hawakubali jambo lolote isipokuwa kwa dalili, na kuna kundi ambalo miongoni mwao mna watu wengi ambao nyoyo zao ziko safi na zimetakasika, watu hao huongoka na kufuata njia ya Mwenyeezi Mungu kwa kuonywa au kupewa nasaha tu. Na kuna kundi la watu ambao ni kidogo, miongoni mwao wamewakhalifu Mitume na kupinga kile walichokuja kuwalingania watu, basi kundi hili ni lazima kupitishwe majadiliano baina yao, ili kupunguza shari zao, kukiwa na matumaini ya kuwa pengine wanaweza kuongoka na kufuata njia ya Mwenyeezi Mungu.

Vile vile ni lazima tuzingatie kuwa mwanaadamu ana nafsi tofauti, kiasi ya kwamba kama hatakuwa madhubuti katika akida na itikadi yake kwa kile anachokiamini, au kwa yale masuala yanayomsumbua yaliyomo akilini mwake ambayo hajayapatia jawabu zake, mtu huyo anaweza kubabaika katika kufanya amali ya yale aliyo na itikadi nayo, mtu kama huyo basi baada ya kuwa na imani na hekima za Mwenyeezi Mungu ni lazima aonywe na kupewa nasaha, kwa sababu mtu hawezi kufanya jambo isipokuwa awe na mapenzi ya kufanya jambo hilo, na afanye jambo kwa hiari yake na sio kulazimishwa, ama itakapokuwa kwa kuonywa au kupewa nasaha hakutaleta athari yoyote, basi inawezekana kutumia njia nyengine itakayomfanya mtu kama huyo akubali yale anayousiwa, nayo ni kufanya majadiliano naye kwa uzuri, kwa kutumia njia hii anaweza akakinai na kuamini yale anayoambiwa, au anaweza kubakia kimya, pengine anaweza kuongoka na kufuata njia ya Mwenyeezi Mungu, na kunufaika na rehema zake Allah (s.w),

[1] Surat Zumar Aya ya 53

[2] Suratul Baqarah Aya ya 25

[3] Suratun Nahli-Aya ya 125

MWISHO

Toa maoni yako

Maoni ya watumiaji

Hakuna maoni
*
*

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini (A.S) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini