UTAKASO WA MAIMAMU NO.1
BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
UTAKASO WA MAIMAMU (A.S) NO.1
ISMAT IMAMU.
Moja katika sifa na sharti muhimu zinazomuwajibikia Imam kuwa nazo ni ismati, (ismati yaani kuepukana na maovu na kutofanya madhambi).
Imamu anatakiwa kuwa ni mwenye elimu ya hali ya juu ili aweze kuwaongoza wengine, na kwa sababu mbili hizi (yaani kutokufanya madhambi na kuwa na elimu ya hali ya juu) Imamu hujizuia na kuitakasa nafsi yake na maovu, na kujiepusha kufanya madhambi, basi kwa vile Imamu ni mwenye kuelewa na kufafanua masuala ya dini, yeye ndie anayefahamu vipi tunatakiwa kuyafanyia kazi masuala hayo, na huyapambanuwa yale yenye kuleta maslahi na yenye kuleta ufisadi na upotovu katika jamii ya kiislamu.
Kuna dalili tofauti za kuthibitisha kwamba Imamu ameepukana na maovu na wala sio mwenye kufanya madhambi, na dalili hizo tunazishudia katika Qur-ani tukufu au katika hadithi tofauti zilizonakiliwa kutoka kwa Mtume Wetu Muhamad (s.a.w.w). Zinazofuata ni dalili za kiakili:-
1. Kuihifadhi dini tukufu ya kiislamu.
Moja katika wadhifa wa Imamu ni kuihifadhi dini na utamaduni wa kiislamu, na kuwaongowa watu, kwa hiyo na lazima katika vitendo vyake na katika mazungumzo yake awe mkweli ili watu waweze kumuamini na kuyafuata yale ambayo anawaongoza, kwa hiyo Imamu ni lazima aielewe dini kwa undani ili aweze kuwaongoza watu katika njia iliyo sahihi.
2.Wanaadamu ni wenye kufanya makosa na maovu.
Wanaadamu wanahitaji kiongozi ambaye anaweza kuwaongoza ili kuifahamu dini yao, sasa kama ikiwa kiongozi pia ni mwenye kufanya maovu au mwenye kukosea vipi watakuwa na matumaini ya yale ambayo Imam amewaamrisha? Kwa hiyo ni lazima Imam aepukane na kufanya madhambi ili binaadamu wasiwe na shaka ya yale ambayo Imam amewaamrisha kufanya au kuyafuata.
Kuna aya nyingi pia katika Qur-ani ambazo zinathibitisha ulazima wa kuwepo Imam, moja katika aya hizo ni katika Suratul baqara aya ya 124, aya hii inaelezea kwamba baada ya Allah (s.w) kumpa Unabii hadharati Ibrahim (a.s) pia amempa Uimamu, na ndipo hadharati Ibrahim alipomuomba Allah (s.w) ya kuwa katika nasli yake (ukoo wake) awape neema hiyo (yaani Uimamu).
وَإِذِ ابْتَلَي إِبْرَاهِيمَ رَبُّهُ بِكَلِمَاتٍ فَاَتَمَّهُنَّ قَالَ إِنِّى جَاعِلُكَ لِلنَّاسِ إِمَاماً قَالَ وَمِن ذُرِّيَّتِى قَالَ لاَ يَنَالُ عَهْدِى الظَّالِمِينَ[1]
Ndipo Allah (s.w) aliposema Imam hawezi kubarikiwa mtu aliyekuwa dhalimu, Allah (s.w) alikuwa akibainisha kwamba atawabarikia Uimamu ukoo wa hadharati Ibrahim (a.s) lakini sio kwa watu madhalimu.
Qur-ani kariym imethibitisha kwamba kumshirikisha Allah (s.w) ni dhulumu kubwa isiyo kiasi, na kupinga dasturi ambazo Mola ameziamrisha (yaani kufanya dhambi na maovu) pia zimehisabiwa kuwa ni dhulumu, kwa hiyo kila mtu ambaye katika maisha yake atakuwa kafanya maovu na madhambi mtu huyo atakuwa ni dhalimu, na hakutokuwa na hekima yoyote ya kumchagua mtu huyo kuwa Imamu.
Kwa maelezo mengine, hakuna shaka yoyote kwamba hadharati Ibrahim (a.s) hakuwa ni mwenye kumuasi Mola wake, na kama tukiangalia katika makundi haya yafuatayo tunaweza kufahamu kwa undani kabisa. Makundi ya watu yamegawika katika sehemu nne kuu, nazo ni hizi zifuatazo:-
1. Watu ambao katika umri wao wote walikuwa ni waovu wenye kufanya madhambi.
2. Watu ambao mwanzo wa umri wao walikuwa ni wenye kufanya mema, (yaani walikuwa ni watu wema) lakini baadae wakabadilika kuwa waovu na kumuasi Mola wao kwa kufanya madhambi.
3. Watu ambao mwanzo wa umri wao walikuwa waovu wenye kumuasi Mola wao, Lakini baadae wakatubu na kurejea kwa Mola wao na wakawa watu wema.
4. Watu ambao toka mwanzo mpaka mwisho wa umri wao hawakumuasi Mola wao na wala hawakufanya madhambi. Basi hakuna shaka kwamba Allah (s.w) amemchagua Nabii Ibrahim kuwa Imam kwa sababu toka mwanzo mpaka mwisho wa umri wake hakuwa akifanya madhambi wala hakumuasi Mola wake.
[1] Suratul Baqara aya ya 124
MWISHO