UTAKASO WA MAIMAMU NO.2
BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
UTAKASO WA MAIMAMU (A.S) NO.2
ISMA YA IMAMU.
Moja katika sifa na sharti muhimu zinazomuwajibikia Imam kuwa nazo ni ismati, (ismati yaani kuepukana na maovu na kutofanya madhambi).
Imamu anatakiwa kuwa ni mwenye elimu ya hali ya juu ili aweze kuwaongoza wengine, na kwa sababu mbili hizi (yaani kutokufanya madhambi na kuwa na elimu ya hali ya juu) Imamu hujizuia na kuitakasa nafsi yake na maovu, na kujiepusha kufanya madhambi, basi kwa vile Imamu ni mwenye kuelewa na kufafanua masuala ya dini, yeye ndie anayefahamu vipi tunatakiwa kuyafanyia kazi masuala hayo, na huyapambanuwa yale yenye kuleta maslahi na yenye kuleta ufisadi na upotovu katika jamii ya kiislamu.
Kuna dalili tofauti za kuthibitisha kwamba Imamu ameepukana na maovu na wala sio mwenye kufanya madhambi, na dalili hizo tunazishudia katika Qur-ani tukufu au katika hadithi tofauti zilizonakiliwa kutoka kwa Mtume Wetu Muhamad (s.a.w.w).
UONGOZI WA IMAM KATIKA JAMII (KUSHIKA HATAMU IMAM)
Kwa vile Binaadamu ni kiumbe ambacho kinaishi katika jamii, na katika jamii kuna watu tofauti wenye kutafautiana katika masuala mbali mbali, hiyo inampelekea mwanaadamu huyo kupata athari tofauti katika maisha yake, basi ili mwanaadamu aishi katika muongozo ulio sahihi na ili awe karibu na Mola wake, hakuna budi ni lazima awepo mtu ambaye atamuongoza mwanaadamu huyo ili aweze kuongoka, basi Imamu ni lazima awe kiongozi na awaongoze wanaadamu katika dasturi ambazo Allah (s.w) amewaamrisha waja wake kuzifuata desturi hizo. Na Imamu humuongoza mwanaadamu huyo kwa kutumia elimu ambayo Mola wake amempa, na hutumia Qur-ani na sunna za Mtume wetu Muhammad (s.a.w.w) na sheria ambazo zimo katika uislamu ili kuwaongoza watu.
IMAM NI LAZIMA AWE NA TABIA NJEMA
Kwa vile Imamu ni kiongozi katika jamii basi ni lazima aepukane na tabia mbaya, na anatakiwa awe na tabia njema na nzuri kupita kiasi kwa sababu yeye ni kigezo kwa wengine, basi ili watu wamuamini na kufuata anayowaamrisha ni lazima yeye mwenyewe awe ni mwenye kuyafanyia amali (kuyatekeleza) yale anayowaamrisha watu.
Imamu ni lazima awe na elimu, shujaa, na mwenye kumcha Mola wake[1].
Baada ya kufariki Mtume Muhammad (s.a.w.w) kiongozi anaefuata ni Imamu, ambae anatakiwa kuwaongoza wanaadamu, kwa hiyo ni lazima yeye mwenyewe awe na tabia njema na kumtukuza Mola wake kupita wengine.
Imam Aliy (a.s) anasema:- "Mtu mbaye amechaguliwa kuwa Imamu na Mola wake, Kwanza ni lazima yeye mwenyewe ajitakase na awe na tabia njema ,ili wale anowaongoza wasiwe na shaka ya yale ambayo Imam wao amewataka wayatekeleze[2],
IMAMU NI LAZIMA ATEULIWE NA ALLAH (S.W)
Kutokana na madhehebu ya Shia kabla ya kufariki Mtume Muhammd (s.a.w.w) Imam ni lazima achaguliwe na Allah (s.w) na baadae Mtume ndie anaewajulisha watu kwamba baada ya kufariki mimi nani atakuwa kiongozi wenu, kwa hiyo hakuna haki ya mtu, watu, kundi au kabila kumchaguwa mtu kuwa ndio kiongozi wao baada ya kufariki mtume (s.a.w.w).
[1] (Rejea kitabu Maani l-ah-bari, juzuu ya 4, ukurasa wa 102)
[2] (Rejea kitabu Miyzani l-hik-ma mlango wa 147,ukurasa wa 85).
MWISHO